RIWAYA; MTUHUMIWA
MTUNZI; HUSSEIN TUWA
SEHEMU YA THELATHINI NA NANE
Nini maana yake hii? Kama ule ujumbe ulikuwa ni mtego wa akina Tony, mbona hata wao hawapo huku juu?
Ilikuwa haileti maana.
Alisonya huku akigeuka kutoka pale kwenye ule ukuta aliokuwa ameuegemea kwa mbele na kuuegemea kwa mgongo. Alikuwa katika hatua ya kujisukuma kutoka pale ukutani kwa mgongo wake ili aondoke ndipo alipomuona.
Naam, alikuwa ni Joakim hasa.
Lakini hakuwa katika hali ambayo Jaka aliitarajia.
Kwenye kona baina ya ukuta wa kile chumba alichotoka kuchungulia punde tu, na ule ukuta uliozunguka ule ukumbi juu ya jengo lile, Joakim Mwaga alikuwa amejikunyata sakafuni, mgongo wake ukiwa umeegemea kwenye kona ile iliyofanya nyuzi tisini. Macho yake yalikuwa yamekodoka kwa mshangao wa kudumu, mdomo wake ulikuwa wazi hali ulimi wake ukining’inia nje. Eneo lote la kifua chake lilikuwa limetapakaa damu kutoka kwenye jeraha lililokuwa shingoni kwake.
Jaka alipiga yowe la mshituko huku miguu ikimwisha nguvu.
Joakima alikuwa ameegemeza kichwa chake kwenye bega lake la kushoto na sehemu ya kichwa kile ilikuwa imeegemea ukuta. Mpini wa kisu ulichomoza kutoka kwenye jeraha lililokuwa upande wa kulia wa shingo ile.
Jaka alipiga hatua tatu za haraka kumsogelea huku akimuita kwa wahka na woga mkubwa.
“Joakim! Joakim! Joakim...” Alizidi kumuita huku akiwa amechutama mbele yake, akimtikisa. Na hapo ndipo alipogundua kuwa ingawa macho yake yalikuwa yakitazama mbele kwa mshangao, Joakim alikuwa haoni, na alikuwa haoni kwa sababu sasa alikuwa marehemu. Joakim hakuwa hai tena. Alikuwa amekufa.
Ameuawa.
Ukelele wa woga ulimtoka Jaka na hapo hapo aliangukia mgongo alipojaribu kurudi nyuma ili awe mbali na ule mwili usio na uhai. Huku akipiga kelele Jaka alijaribu kuinuka huku akirudi nyuma, akadondoka tena. Akajaribu tena lakini kwa mara nyingine tena akadondokea matako. Akabaki akisotea makalio kurudi nyuma huku macho yamemtoka pima akimtazama Joakim kwa woga huku akipiga mayowe.
Hatimaye alifanikiwa kusimama na kujiegemeza kwenye ule ukuta na kubaki akitweta kutafuta pumzi ambazo zilimkaba kooni.
Ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kuona mtu aliyekufa, wachilia mbali aliyeuawa, hasa ikiwa mtu huyo ni ambaye alikuwa akimfahamu. Wazo la kwanza lililomjia kichwani mwake lilikuwa ni kwenda kutoa ripoti polisi juu ya tukio lile.
Alikurupuka mbio kutoka pale ukutani kuziendea ngazi za kuteremka kutoka eneo lile. Picha ya Joakim Mwaga, akiwa amejikunyata pale chini, mguu wake mmoja akiwa ameukunja kwa uchungu kiasi kwamba goti lake lilikuwa karibu sana kugusana na bega lake, wakati mguu wake mwingine akiwa ameunyoosha mbele pale sakafuni, mikono yake yote miwili ikiwa imeshikilia kwa nguvu sehemu chini kidogo ya shingo yake, karibu na pale mpini wa kisu ulipochomoza, bado ilikuwa kichwani mwake.
Mambo yote yaliyofuatia kuanzia muda ule yalitokea haraka sana.
Kabla hajaufikia ule mlango, alisikia vishindo vya viatu vikipanda zile ngazi kuelekea kule alipo kuwa. Havikuwa vishindo vya mtu mmoja. Ni watu wengi. Alitaka kugeuka arudi kule alipotokea, akagundua kuwa njia pekee ya kutokea eneo lile ni kupitia kwenye ule ule mlango, kuelekea kule kule vilipokuwa vikitokea vile vishindo. Kabla hajatanabahi, alipatwa na kihoro aliposhuhudia askari wa jeshi la polisi wanne wakiingia pale ju kupitia kwenye ule mlango, wakimlazimisha arudi nyuma bila kupenda, macho yakimtembea, mdomo ukimuanguka.
“Tulia kama ulivyo!” Mmoja wao alimfokea akiwa amemuelekezea bastola.
Jaka alibaki amepigwa na butwaa. Hakutaka kuyaamini macho yake alipoona wale askari wakimzingira huku wakimnyooshea mitutu ya bunduki aina ya SMG. Aliihisi akili ikimsinyaa na miguu ikimwisha nguvu.
“Sio mimi...I mean…sikufanya kitu...amekufa.
..nimemkuta ameuawa!” Aliropoka kwa hamaniko huku akipiga hatua kuwasogelea wale askari. Mara ile ile wale askari walikoki zile bunduki zao na yule aliyemuamuru atulie hapo mwanzo akamfokea.
“Tulia hapo hapo ulipo wewe! Hatua nyingine moja tu utakuwa kilema sasa hivi!”
Heh!
Jaka alikatisha hatua zake na kusimama huku akinyoosha juu mikono yakeiliyokuwa akimtetemeka vibaya sana.
“Kaa kimya!” Yule askari alimwamuru.
Jaka alijikuta akika chini, miguu ikishindwa kabisa kuendelea kumhimili. Macho makali ya yule askari yalimfuata pale pale chini na bila ya kutoa macho yake usoni kwa Jaka aliiita, “Koplo!”
“Afande!”
“Chunguza eneo hili haraka!”
Mmoja wa wale askari waliomzingira Jaka alichomoka na kuelekea kule alipotokea Jaka, mwisho wa ukumbi ule. Jaka alijua ni nini atakachokikuta kule alipoelekea, ila hakujua ni nini kingemkuta yeye baada ya hapo. Sauti ya mshituko ilisikika kutokea kule alipoelekea yule Koplo, na Jaka alifumba macho kama kwamba kufanya hivyo kungemsaidia asisikie maneno ambayo yangefuata.
“Kuna maiti hapa afande…kauawa…kama tulivyotaarifiw
a!” Yule koplo alijibu kwa sauti.
“Mlivyotaarifiwa? Nan…na nani?” Jala alijikuta akiropoka, na hapo hapo alizabwa kofi kali sana la uso, yowe kubwa likamtoka bila kupenda, maumivu makali yakimtawala usoni.
“Kimya wewe! Unaua mtu halafu unajitia kushangaa?” Yule askari alimkemea, kisha alienda kule alipoelekea yule Koplo, wale askari wengine walibaki vilevile wakiwa wamemuelekezea Jaka mitutu ya bunduki zao. Jaka alianza kulia kwa majuto na uchungu, akijua kuwa tayayi alikuwa amebebeshwa kesi ya mauaji. Baada ya muda yule askari kiongozi alirudi na kumuuliza jina lake. Jaka akamtajia.
“Jaka Brown Madega...uko chini ya ulinzi kwa tuhuma ya kuhusika na mauaji!” Yule askari kiongozi alimwambia kwa ghadhabu.
“Sio mimi afande...! Sio mimi...”
Mikono yenye nguvu ilimkamata na kumfunga pingu mikono yake kwa mbele.
“Maelezo yote utatoa kituoni!” Alikemewa.
Mambo yote yaliyofuata baada ya hapo yalikuwa kama ndoto tu kwa Jaka. Wale askari waliwasiliana na askari wengine ambao bila shaka walikuwa chini ya jengo lile kwa redio maalum za mawasiliano na dakika chache baadaye walikuja askari wengine wakiwa na machela ya kubebea maiti. Mwili wa Joakim Mwaga ulipigwa picha ukiwa umejikunyata pale chini kabla ya kubebwa kwenye machela na kuondolewa kutoka eneo lile.
Jaka aliteremshwa haraka haraka kutoka kule juu hali akiwa amefungwa pingu. Ilikuwa ni heka heka baada ya wanafunzi wenzake kumuona akiteremshwa ngazi na askari namna ile. Walikusanyika vikundi vikundi na kuanza kuulizana juu ya mkasa ule ambao wote hawakuuelewa.
Askari walimuamuru Jaka awapeleke chumbani kwake, naye alitii bila ubishi huku kichwa kikimzunguka. Alijitahidi kufikiri lakini hakuna fikra yoyote njema iliyomjia. Mlango wa chumba chake ulikuwa wazi na yule askari alimuuliza iwapo aliuacha wazi kabla ya kutoka nje ya chumba kile.
“Nakumbuka niliubamiza lakini sikuufunga kwa ufunguo...” Jaka alijibu.
“Okay, tuingie ndani humo…!” Askari aliamuru, nao wakaingia na kuacha askari mmoja nje ya mlango wa chumba kile kuwadhibiti wanafunzi waliojaa kwenye korido pale nje ya chumba chake wakitaka kujua kilikuwa kinaendelea.
“Tunapekua chumba chako kutafuta ushahidi wowote tutakaoweza kuutumia katika kuchunguza swala hili, sawa?” Yule askari mwenye bastola, ambayo sasa ilikuwa imehifadhiwa kwenye mkoba maalum ulioning’inia kiunoni mwake alimwambia. Kabla Jaka hajajibu wale askari walianza kupekua chumba kile kwa vurugu. Makabati yalifunguliwa na nguo zilitupwa huku na kule, vitabu vilichakuriwa na kutupwa hovyo sakafuni, kapeti liliinuliwa na kuvutwa bila mpangilio.
Jaka aliangalia mambo yake huku akili ikimzunguka.
“Afande!” Katikati ya upekuzi ule wa fujo, mmoja wa wale askari aliita, naye akapeleka macho yake kule ilipotokea ile sauti. Yule askari mwenye bastola alisogea pale kando ya kitanda cha Jaka alipokuwa amesimama yule askari aliyeita huku akiwa ameinua upande wa godoro la kitanda kile. Jaka naye alisogea taratibu huku akihisi moyo wake ukitaka kumchomoka kutoka kifuani kwake.
Chini ya godoro lile, juu ya chaga za mbao za kitanda chake, kulikuwa kuna glovu mbili za mpira mithili ya zile zinazotumiwa na madaktari wanapofanya upasuaji.
Zile glovu zilikuwa zimetapakaa damu mbichi!
E bwana we!
Jaka alitoa ukelele wa ghadhabu na kutoamini huku akizikodolea macho zile glovu, ukweli kuwa alikuwa ametegwa na amenasa ukimshukia dhahiri fahamuni. Alijirusha juu kwa nguvu akijaribu kugeuka ili atoke nje ya chumba kile.
“Haiwezekani...! Haiwezekani hii! Hii ni njama tu hii1 Nimepakaziwa...! Nimesingiziwa mimi...Hii ni njama kabbisa!” Alibwata kwa hasira. Mikono yenye nguvu ilimshika na kumbana, lakini alizidi kufurukuta.
“Niacheni, niacheni nasema, vibaraka wakubwa nyie!”
Alitwangwa ngumi nzito ya tumboni, na pumzi zikamkatika ghafla, maumivu makali yakimtawala. Alipiga yowe la maumivu huku akienda chini akiwa amejishika tumbo. Aliinua uso kwa ghadhabu kumtazama aliyempiga, akajikuta akiutumbulia macho mtutu wa bastola iliyoelekezwa katikati ya macho yake.
“Tulia kama ulivyo fisi wee! Uko chini ya ulinzi kwa tuhuma za amuaji na sitakukumbusha tena juu ya hilo...fanya tena upuuzi wako uone jinsi nitakavyotawanya bichwa lako kwa risasi, fala we! Unaleta vurugu wakati uko chini ya ulinzi, ebbo!” Yule askari kiongozi alimfokea kwa hasira.
“Lakini mimi sijaua, afande...huoni kama hii ni njama tu?” Jaka alisema kwa kuombeleza huku akiwa amepiga magoti pale chini, machozi yakimbubujika.
“Hakuna aliyekuambia kuwa umeua kijana...kuanzia sasa na kuendelea wewe ni mtuhumiwa tu wa mauaji haya...mpaka hapo mahakama itakapoamua kuwa uwe mshitakiwa namba moja au uachiwe huru, sawa bwana? Kwa sasa nataka ushirikiano wako wa kila hali.” Yule askari alimwambia na kukaa kimya kwa muda kabla ya kuanza kumtupia maswali huku askari mwingine akinukuu kwa maandishi mahojiano yale.
“Hizi glovu ni zako?”
“Hapana...”
“Umeshawahi kuziona kabla ya hapa?”
“Hapana...sijawahi.”
“Unaweza kujua zimefikaje hapa chini ya godoro ?”
“Sijui...”
Yule askari alimtazama kwa muda, na Jaka akajua kuwa alikuwa hamuamini.
“Sawa...” Hatimaye alisema yule askari na kutoa maelekezo kwa wale askari wengine waliokuwamo mle ndani. Zile glovu ziliwekwa ndani ya mfuko maalum wa nailoni na kuchukuliwa kama ushahidi. Jaka alitolewa mkiki-mkiki nje ya chumba kile kuelekea kwenye Land Rover ya polisi iliyokuwa imeegeshwa nje ya jengo lile. Wanafunzi wenzake walikuwa wamejaa pale nje kushuhudia tukio lile huku baadhi wa wanafunzi wa kike wakilia baada ya kuuona mwili wa Joakim Mwaga ulipotolewa hapo awali. Jaka alipitishwa akiwa amefungwa pingu kuelekea kwenye gari ile. Aliangaza huku na kule kwa uso uliohamanika akitarajia kumuona Raymond au Moze katika kundi lile la wanafunzi.
Wote hawakuwepo.
Huku akibubujikwa na machozi, Jaka aliingizwa ndani ya lile gari la polisi, ambalo liliondoka kwa kasi kutoka eneo lile.
12
Raymond Mloo alizipokea habari za kukamatwa kwa Jaka akihusishwa na kifo cha Joakim kwa mshangao na mshituko mkubwa sana. Kama angesikia kuwa Jaka amekutwa akiwa ameuawa, bila shaka asingeshangaa kama jinsi alivyoshangazwa na habari ile. Lakini pamoja na kushangazwa kwake, jambo ambalo alikuwa na uhakika nalo kabisa kichwani mwake ni kwamba zile zilikuwa ni hila za Tony na wenzake za kutaka kumkomoa Jaka na kuhakikisha kuwa anafungwa miaka mingi, au maisha...au kunyongwa kabisa, na hivyo kuwapa wao nafasi ya kuendelea na biashara zao haramu.
Lakini kwa nini Joakim?
Na kwa nini Jaka akutwe eneo la tukio?
Ni maswali ambayo hakuweza kuyapatia majibu mara moja mpaka alipoonana tena na rafiki yake siku mbili baada ya tukio. Na hapo aliweza kupata jibu la swali moja tu kati ya yale mawili: ilikuwaje hata Jaka akakutwa katika eneo la tukio.
Kesi ya mauji!
Ama kweli Tony ni mtoto mbaya...tena mtoto mbaya sana.
Masikini Jaka...nani atamuamini atakaposema kuwa hakumuua Joakim Mwaga? Wanafunzi wengi pale chuoni walijua juu ya uhasama uliojengeka baina yake na Joakim Mwaga. Kuna wanafunzi pale chuoni walioshuhudia kwa macho yao siku Jaka na Joakim walipoamua kurekebisha tofauti zao kwa kutupiana makonde. Na tangu siku ile ilijulikana wazi kuwa hawakuwa na uhusiano mzuri kabisa, jambo lililopelekea Jaka kupewa kipigo kikali kule Club Billicanas na kulamizika kulazwa hospitali kwa siku kadhaa.
Na tangu hapo baadhi ya wanafunzi walikuwa wanasubiri kuona Jaka atajibu vipi mapigo yale...
Na sasa Joakim ameuawa na Jaka amekutwa eneo la tukio.
Masikini Jaka...
___________________
Moze alikuwa akimsikiliza mhadhiri nusu nusu, kwani sehemu ya akili yake ilikuwa ikifikiria juu ya zawadi aliyoahidiwa na mpenzi wake siku ile. Aliangalia saa yake na kugundua kuwa ilikuwa ni saa tisa kasoro robo za alasiri. Ilikuwa imesalia robo saa tu kipindi kiishe, naye alikuwa ana ahadi ya kukutana na mpenzi wake baada ya kipindi kile na aliona kuwa yule mhadhiri alikuwa anamchelewesha tu.
Aliona askari wa jeshi la polisi akiingia mle darasani na kunong’ona na mhadhiri kwa muda. Kimya kilitanda darasani, kila kila mwanafunzi akiwa amemakinika na ujio wa yule askari mle darasani, na muda mfupi baadaye Moze alishangaa kusikia mhadhiri akiita jina lake na kumuomba aende kule mbele. Huku moyo ukimdunda kwa wasiwasi, Moze alienda kule alipokuwa amesimama mhadhiri na yule askari.
“Moze, huyu ni afisa wa polisi...alikuwa anahitaji kukuuliza maswali machache...” Mhadhiri alimwambia kwa upole. Moze alimtazama yule askari kwa mashaka halafu akamtazama mhadhiri, kisha akamtazama tena yule askari.
“Naomba tuongazane kituoni tafadhali.” Yule askari alimwambia. Moze alitaka kubisha, lakini akabadili mawazo. Akiwa haelewi ni nini kinachoendelea, alimfuata yule afisa wa polisi kuelekea kituo cha polisi cha Mlimani. Huko aliingizwa kwenye chumba kidogo na kuombwa asubiri. Alisubiri kwa muda wa nusu saa nzima huku akizidi kuchanganyikiwa juu ya sababu ya kuletwa pale kabla hajatokea mtu yeyote. Ndani ya muda huo mawazo mengi ya mashaka yalimuandama, yote yakiwa ni juu mpenzi wake kufanyiwa madhara na akina Tony.
Wamemfanya nini sasa Jaka wangu hawa watu yarabbi?
Wamemuua kama walivyomuua Rose? Oh Mungu wangu…isiwe hivyo jamani!
Alihamanika vilivyo.
ITAENDELEA