RIWAYA; MTUHUMIWA
MTUNZI; HUSSEIN TUWA
SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA
“Katika chumba ambamo Roze alifariki, ambamo na wewe ndimo unamoishi pale chuoni, kumepatikana kiasi kidogo cha unga wa madawa ya kulevya aina ya Cocaine ukiwa kwenye kifuko kidogo cha nailoni, na mwingine ukiwa umemwagika juu ya zulia la mle chumbani, wakati kiasi kingine cha unga huo kilionekana kutapakaa ukutani...sijui unafahamu nini juu ya hilo?”
Moze alionekana kushtushwa sana habari ile kiasi kwamba hasira zake zote ziliyeyuka mara moja na nafasi ya hasira zile ikachukuliwa na mashaka na mshituko.
“Niliona unga kidogo pale juu ya zulia, lakini sikijua ni unga gani na wala sikuutilia maanani kabisa...” Alisema kwa mashaka makubwa kabisa.
“Baada ya wale askari waliokuhoji mara ya kwanza kutoa ripoti ya kupatikana kwa unga huo, na baada ya unga huo kuthibitishwa kuwa ni Cocaine, uchunguzi wote wa kesi hii umehamishiwa moja kwa moja mikononi mwa idara inayohusika na udhibiti na ufuatiliaji wa madawa ya kulevya hapa nchini…na ndio maana mimi leo nimekuja tena kwako ili kuanza uchunguzi wa idara yangu katika kesi hii.” Alimalizia John Vata.
“Kwa hiyo wewe ndiyo umetoka kwenye hiyo idara ya...”
“Narcotics Department, ndiyo...na nipo hapa kuomba msaada wowote unaoweza kuutoa katika kutatua kesi hii. Kwani tuna imani kuwa tukiijua sababu ya kifo cha Rose, tutakuwa tumepata chanzo kizuri sana cha kutufikisha kwenye chimbuko la biashara hii ya madawa ya kulevya.”
“Dah! Sawa...sasa…unadhani mimi nitaweza kusaidia vipi Sajenti?”
“Mimi nadhani wewe unajua ni kwa nini Rose aliamua kujiua...kwa sababu hadi anakata roho alikuwa mikononi mwako...” Hapo Moze alifumba macho na mwili ulimsisimka kwa kumbukumbu zilizomjia. “...na bila shaka kuna maneno fulani ambayo Rose atakuwa amekuambia au ameyatamka katika dakika zake za mwisho, ambayo tunadhani yanaweza kutupatia mwanga juu ya swala hili.”
“Mimi sijui ni kwa nini Rose aliamua kujiua afande! Nami pia nakubali kuwa Rose alikuwa anataka kuniambia neno au kitu...ila tu kile alichokuwa akikisema kilikuwa hakileti maana yoyote...she was very delirius, man...!”Moze alimjibu, akimalizia kwa maneno ya kimombo yaliyomaanisha kuwa Rose alikuwa akibwabwaja vitu visivyoeleweka tu katika zile dakika zake za mwisho.
“Ni nini hasa alichokuwa akikueleza, au akijaribu kukueleza…? Hebu niambie namna ilivyokuwa, neno kwa neno…kadiri unavyoweza kukumbuka”
“Ah, afande! Yaani ni utata tu, kwani neno pekee alilokuwa akijaribu kunieleza ni...you know what I am saying...you know what I am saying...zaidi ya hapo hakusema neno lingine...mpaka leo hii sielewi ni kwa nini neno hilo lilikuwa na umuhimu sana kwake kwa wakati ule, au alitaka nielewe nini kwa maneno yale...it was very scary, Sajenti.” Moze alimjibu, akimalizia tena kwa kuchomekea maneno ya kimombo, akimaanisha kuwa hali aliyokuwa nayo Rose kabla ya kukata roho ilimtisha sana.
Vata alionekana kumakinika sana na maelezo yale. Alikunja nne, kisha hapo hapo akaikunjua na kuikunja tena kwa mguu mwingine.
“Aha! Yaani…kutokana na maneno hayo ni kwamba alikuwa akimaanisha kuwa wewe unajua ni nini Rose alikuwa anasema, sio?”
“Ndio. Hiyo ndio maana yake. Lakini kwangu hayakuleta, na wala hayaleti, maana yoyote...”
John Vata alimtazama Moze kwa muda bila ya kusema neno. Kisha aligeuka pembeni na kuendelea kukaa kimya, akifikiri juu ya yale maelezo ya Moze, akichezesha-chezesha ule mguu wake mmoja uliolazwa juu ya mwingine pale kochini. Hatimaye alimgeukia tena Moze.
“Rose aliandika barua kabla ya kifo chake...”
“Ambayo hakuwahi kuimalizia...” Moze alidakia.
John Vata aliafiki kwa kichwa huku akimkabidhi Moze kipande cha karatasi alichokitoa kwenye mfuko wake wa shati.
“Barua hiyo ndiyo hii?”
Moze aliipokea ile karatasi kwa mikono ya kutetemeka na kuitazama. Ilikuwa bado ina mikunjo- mikunjo, na ilikuwa imechanika kidogo.
Ilikuwa karatasi nyeupe, yenye urefu wa inchi zipatazo kumi hivi na upana wa inchi saba. Mwandiko ulioandika maneno machache yaliyokuwa juu ya karatasi ile ulikuwa dhaifu na wa kitetemeshi, ila Moze hakuwa na shaka kabisa kuwa ulikuwa ni mwandiko wa rafiki yake Rose.
“Ndiyo hii.” Alijibu huku akimrudishia Vata ile karatasi.
“Una uhakika huu ni mwandiko wa Rose?” Kama aliyekuwa akisoma mawazo yake, Vata alimuuliza. Moze aliafiki kwa kichwa na wote walibaki kimya kwa muda. Moze akijifuta machozi yaliyokuwa yakimchuruzika, ilhali Vata akisoma kwa mara nyingine kile kilichoandikwa kwenye ile karatasi.
Rafiki mpendwa Moze,
Samahani sana kwa uamuzi nilioamua kuuchukua, kwani najua utakuhuzunisha sana.
Naomba tu uelewe ya kuwa huu ni uamuzi wa busara zaidi kwangu hivi sasa na kwa maisha yako.
Moze, nimeamua kufanya hivi kwa sababu nimeshindwa kabisa kukusaliti kwa huyu mtu mbaya ambaye tayari ameyaharibu kabisa maisha yangu, nawe itabidi uwe makini san
Kilichofuatia baada ya hapo ni michoro isiyoeleweka, kama vile baada ya kufikia hapo tu kitu, au mtu alimshitua kiasi cha kufanya michoro ile isiyoeleweka kwenye ile karatasi, halafu hakuendelea tena kuandika.
“Inaelekea Rose alikuwa anataka kukuachia tahadhari fulani dhidi ya mtu fulani.” Vata alisema huku akimtazama Moze usoni. Moze aliuma mdomo na kuafiki kwa kichwa.
“Na wewe unadai kuwa ujumbe huu hauleti maana kwako.”
Halikuwa swali. Ilikuwa ni sentesi kamili iliyotolewa kama shutuma. Moze alimtazama yule askari kwa mshangao.
“Unadhani mimi nasema uongo nikisema hivyo?”
“Kwangu mimi huu ujumbe uko wazi kabisa...yaani wewe ungetakiwa uelewe ni nani Rose anayemzungumzia kwenye barua hii.”
“Sasa hilo ndilo ambalo halileti maana kwangu afande, kwa sababu sijui ni nini Moze anachozungumzia kwenye hiyo barua…na wala sijui ni nani huyo anayemtaja kwenye hiyo barua, na huo ndio ukweli.”
Vata alimtazama kwa muda bila ya kusema neno. Kama yule binti angekuwa anasema uongo kwa namna fulani angeweza kugundua, lakini aliona kuwa yule binti alikuwa akisema ukweli, na hii iliifanya kazi yake iwe ngumu kuliko alivyotarajia.
Ni nani huyu anayeongelewa kuwa ni mtu mbaya kwenye barua ya Rose?
Kwa nini uamuzi wa Rose kujiua uwe ndio salama ya Moze?
Rose alishindwa kumsaliti Moze katika lipi, hata akaona ajiue?
“Inaelekea Rose aliamua kujiua ili akuokoe wewe kutokana na hatari fulani Moze, halafu wewe unasema kuwa hujui lolote juu ya jambo lote hili?” Vata aliendelea kusaili.
“Sajenti, mimi ningekuwa naelewa kitu juu ya mambo haya nisingekuwa na sababu ya kuficha. Ukweli ni kwamba sielewi kitu chochote!” Moze alijibu kwa sauti iliyochanganyikiwa.
“Rose hakuwa na rafiki yeyote wa kiume, ambaye labda angeweza kumdhuru kwa namna yoyote ile ?”
“Hakuwa na rafiki yeyote wa kiume afande.”
“Je wewe?”
“Je mimi vipi?”
“Huna rafiki yeyote wa kiume?”
“Niliye naye hawezi kumdhuru Moze wala mimi. Ni mtu mzuri sana na wala hana tatizo lolote juu ya urafiki wangu na Rose.”
“Niandikie jina lake na mahala anapoweza kupatikana, ikiwezekana na namba yake ya simu.” Vata alimwambia huku akimsogezea kijitabu kidogo cha anuani na kalamu. Moze alitekeleza. John Vata aliutazama mwandiko wa yule binti wakati akiandika na kuufananisha kwa kichwa na ule aliouona kwenye barua iliyosemekana kuwa imeandikwa na Rose.
Ulikuwa ni mwandiko tofauti.
Kimya kilitawala kwa muda mrefu, kisha John Vata aliinuka ghafla.
“Bado kuna maswali mengi juu ya kifo cha rafiki yako Moze, hivyo nitarudi tena wakati wowote.” Alimwambia huku akimtazama moja kwa moja usoni. Moze aliafikiana naye kwa kichwa huku naye akiinuka kutoka pale kwenye kochi alilokuwa amekalia.
John Vata alitoka kuelekea mahala alipoegesha gari lake la polisi nje ya nyumba ile bila ya kuongeza neno zaidi.
Kikombe cha chai na biskuti alivyokaribishwa na mama Moze vilikuwa havijaguswa.
___________________
John Vata alikuwa amesimama kwenye chumba kidogo kilichokuwa ndani ya ofisi ya Dokta Felix Mgunda, mtafiti wa kitabibu wa polisi anayeshughulika na uchunguzi wa maiti zitokanazo na vifo vya jinai. Alipofika katika ofisi ile iliyopo ndani ya Hospitali maarufu ya serikali ya Muhimbili, alikaribishwa kwenye chumba kile na Dokta Mgunda mwenyewe, ambaye alimtaka asubiri kidogo pale ndani kwani alikuwa akimalizia kuichambua maiti nyingine kwenye chumba kingine, kikubwa zaidi, kilichokuwa upande wa pili wa ofisi ile.
Badala ya kuketi kitini, Vata alikuwa akiranda randa huku na huko mle ndani, akimsubiri tabibu yule makini. Dokta Mgunda hakuwa na muda wa kupoteza na alikuwa ana kumbukumbu ya hali ya juu, hivyo alipoingia tena mle ndani dakika kumi baadaye alianza kuongea moja kwa moja.
“Umekuja juu ya swala la Rose wa Chuo Kikuu, Sajenti Vata...ni nini hasa ulichokuwa unataka kujua juu ya kifo chake?”
John Vata alitabasamu kidogo kutokana na jinsi Dokta Mgunda alivyokuwa akiendesha ofisi yake. Alikuwa ni mtu mfupi, mnene na mwenye upara uliong’aa sehemu ya juu ya kichwa chake, ingawa alikuwa na nywele nyeusi mno kisogoni na pembeni ya kichwa kile kikubwa.
“Tuanze na sababu ya kifo chake.”
“Sababu halisi ya kifo chake...” Dokta Felix Mgunda alivuta droo ya meza iliyokuwa mbele yake na kutoa faili jembamba. Alifunua ukurasa mmoja wa faili lile na kulilaza mezani mbele ya macho yake, na kuendelea bila kusoma kutoka kwenye lile faili, “...ni kupasuka kwa mishipa midogo inayopeleka damu moyoni na kusababisha kusimama kwa mzunguko mzima wa damu na hivyo kuufanya moyo ulipuke ghafla na kusimama...”
“Kwa nini unasema sababu halisi...kuna sababu nyingine, au...”
“Hali hiyo ya kupasuka mishipa hiyo midogo ya damu imesababishwa na marehemu kumeza vidonge vingi vya Chloroquine kwa mkupuo...sasa Chloroquine in itself, if properly administered , haisababishi kifo, ndio maana nikasema kuwa sababu halisi ni kule kupasuka ile mishipa kulikotokana na marehemu kubwia vidonge vingi vya dawa hiyo.” Mgunda alifafanua kwa utaratibu kama anayemuelezea kitu mtoto mdogo huku akichanganya na lugha ya kiingereza, jambo ambalo Vata alilizoea.
“Kuna dalili yoyote katika mwili wa marehemu za kuonesha kuwa kulikuwa kumetumika nguvu dhidi yake kabla ya kumeza vidonge hivyo?”
Mgunda alimtazama Vata kwa muda, kisha alimjibu:
“Sajenti, mimi nitajibu kutokana na matokeo ya uchunguzi wangu, hayo mambo mengine ni juu yako mwenyewe. Swala la kwamba nguvu ilitumika lipo, lakini iwapo ilitumika kabla au baada ya kumeza vidonge hivyo haliko ndani ya taaluma yangu kujua. Sawa?”
“Sawa.”
“Kuna alama za mbali sana kwenye shavu la kulia la marehemu ambazo zinaashiria kuwa alipigwa kofi kali.”
Vata alimsikiliza Mgunda kwa makini.
“Pia kuna michubuko katika sehemu ya mbele ya shingo ya marehemu, ambayo inaweza kuwa imetokana na aidha kukabwa au kukandamizwa na kitu au mkono uliovikwa glovu au kitu kama hicho.”
“Hakukuwa na alama za vidole mwilini mwa marehemu?”
“Vijana wa alama za vidole waliupitia mwili wa marehemu hatua kwa hatua, Sajenti. Alama za vidole zipo lakini sio kwenye maeneo yaliyojeruhiwa au yaliyoshikwa kwa kupigwa....ripoti hiyo si unayo Vata?”
“Ninayo. Ni alama za wale wasichana wanafunzi wenzake waliokuwa wakijaribu kumsaidia baada ya kumkuta akiwa katika hatua za mwisho za kuaga dunia pale chumbani kwake. Kingine chochote?”
Sasa Dokta Mgunda alikuwa anasoma kutoka kwenye lile faili.
“Kulikuwa kuna majeraha mawili katika mwili wa marehemu ambayo yanaweza kuwa yamesababishwa na kitu chenye ncha kali...kama kisu chembamba au bisibisi..au kitu chochote chenye ncha kali...” Hapo Vata alionesha kumakinika zaidi na taarifa ile. “...jeraha moja lilikuwa upande wa kushoto wa uso wa marehemu, chini kidogo ya sikio la upande huo. Jeraha jingine kama hilo ilikuwa chini ya titi la kulia la marehemu.”
John Vata alikunja uso akitafakari habari zile. Dokta Mgunda alibaki kimya akimtazama, kama vile anayempa muda wa kuyaelewa vizuri mambo aliyomueleza.
“Nadhani alilazimishwa kumeza vile vidonge ili ionekane amejiua...” Vata alijisemea peke yake kwa sauti huku akimsahau kabisa Dokta Mgunda.
“Ningekuwa mimi nisingedhani hivyo.” Dokta Mgunda alimjibu taratibu. Vata aliinua uso wake na kumtazama kwa macho ya kuuliza. Mgunda aliendelea kumtazama bila ya kusema neno jingine. Vata akauliza.
“Kwa nini unasema hivyo Dokta...kuna kitu hujaniambia?”
Mgunda alishusha pumzi ndefu kabla ya kumuuliza.
“Unadhani alipata hayo majeraha wakati akilazimishwa kumeza hivyo vidonge?”
Vata aliafiki kwa kichwa. Mgunda aliendelea kumtazama kwa muda. Vata akashindwa kuendelea kucheza mchezo ule wa paka na panya.
“Una kitu cha kuniambia Dokta niambie, sio tena unanifanyia ana-ana-anado hapa! We’ unadhani kama hakukuwa na mtu mwingine hayo majeraha angeyapataje? Talk to me bwana, ni nini ambacho bado hujaniambia Dokta juu ya swala hili?”
Sasa Mgunda aliangua kicheko. Kwa hakika alikuwa akiifurahia sana sehemu hii ya kuwachezea askari kila wanapokuja kupata taarifa muhimu za kitaalamu kutoka kwake.
“Vata, Vata, Vata...Relax bwana, okay?” Mgunda alimwambia kwa mzaha huku akionekana wazi kuwa amefurahia sana hali ile, kisha kabla Vata hajajibu, akaendelea akiwa amemakinika, mzaha wote akiwa ameuweka pembeni, “ Uchunguzi umeonesha kuwa marehemu alikuwa ameingiliwa kimwili…au ameshiriki tendo la ndoa, muda mchache kabla ya kufariki...hivyo unaweza ukaanza kufikiria kuwa huenda hayo majeraha yalitokana na mtu kumlazimisha marehemu kufanya naye tendo la ndoa...”
“Alibakwa?”
“Manii yameonekana katika sehemu ya uke wake...manii ya kiume yaliyoganda. Huenda ikawa alibakwa, huenda ikawa alifanya tu mwenyewe kwa ridhaa yake, hiyo sasa ni juu yako kung’amua.”