Riwaya:Mtuhumiwa

Riwaya:Mtuhumiwa

RIWAYA; MTUHUMIWA

MTUNZI; HUSSEIN TUWA

SEHEMU YA ARUBAINI NA TANO

Wale askari walionekana kuwa walikuwa wakimuuliza maswali fulani mama yake, ambaye alikuwa akitikisa kichwa chake kutoafikiana na yale waliyokuwa wakimueleza huku machozi yakimtiririka. Aliwatazama wale askari kwa makini, lakini hakuwa amepata kuwaona kabla na hakuwa na njia yoyote ya kuweza kujua iwapo walikuwa ni askari wa kweli au ni miongoni mwa wale wa bandia wanaotaka kumuua.
Alijiondoa pale dirishani na kuanza kukimbia kwa kasi kutoka pale nyumbani kwao bila ya kujua ni wapi hasa alikuwa akielekea. Ilimfunukia kuwa hakuwa na mahala pa kukimbilia. Mvua iliongezeka na radi zilikuwa zikipiga kwa nguvu na kutisha. Bila shaka watu waliomuona waliamini kuwa alikuwa akiikimbia ile mvua, ingawa yeye haikumshughulisha hata kidogo. Alikimbia na kukimbia. Hatimae alishindwa kukimbia zaidi. Pumzi zilimwishia na alisimama akitweta, akabaki akiangaza huku na huko. Kiza kilikuwa kimetanda na bado mvua ilikuwa ikipiga kwa nguvu sana. Mbio zake zilimfikisha ufukweni mwa bahari. Bila shaka ilikuwa ni pwani ya msasani, hakuwa na hakika.
Alijivuta kwa uchovu kukiendea kichaka cha miti iliyokuwa kando ya bahari ile na kujibwaga kama mzigo. Akiwa amejilaza pale mchangani alihisi unyevu uliotokana na maji ya bahari na mvua, lakini kwa uchovu aliokuwa nao hilo lilikuwa ni jambo dogo sana. Usingizi ulimpitia. Hakujua alilala kwa muda gani, ila usingizi ule ulikuwa mzito na mrefu.
Alipozinduka, mvua ilikuwa ikinyesha kwa rasha rasha tu. Alijiinua kwa taabu na kuanza kutembea kuelekea barabarani. Kibegi chake bado kikiwa kinaning’inia mgongoni, alianza kuelekea tena nyumbani kwa mama yake akiwa na uhakika kabisa kuwa kwa muda ule wale askari watakuwa wameshaondoka. Ulikuwa ni umbali mrefu kidogo, na kabla hajafika kwao, mvua ilianza kunyesha tena kwa nguvu.
Hakujali.
Hatua chache kutoka mlango wa mbele wa nyumba yao alishtuka ule mlango ukifunguliwa ghafla na mmoja kati ya wale askari aliowaona sebuleni kwao hapo mwanzo akitoka nje.
Walionana uso kwa uso.
“Huyu hapa!” Yule askari alibwaka huku akitoa bastola yake iliyokuwa ikining’inia kiunoni mwake na kumfyatulia risasi.
Jaka alijitupa chini upesi sana na kujibiringisha pale chini ili kuongeza umbali baina yake na yule askari, ile risasi ikamkosa. Risasi nyingine mbili zilifyatuliwa haraka haraka wakati akijibiiringisha pale chini, nazo zilimkosa na kuchimba ardhi huku zikirusha tope.
Alijitupa wima kutimua mbio, nyuma yake akisikia vishindo vya wale askari na sauti ya mama yake akipiga kelele kutokea kule nyumbani kwao. Alikata kona kwa kasi na kutokea mtaa mwingine. Wale askari walimkimbiza huku bastola zikiwa wazi mikononi mwao. Akakata kona nyingine kwa kasi na kuibukia mtaa mwingine hali wale askari wakiwa hatua kadhaa nyuma yake. Mlio mwingine wa bastola ulisikika na risasi ikachimba ukuta wa nyumba iliyokuwa kwenye kona aliyopotelea. Aliendelea kutimua mbio kwa kasi zaidi.
Alipotokeza kwenye ule mtaa wa pili alijikuta akimulikwa na mwanga mkali wa taa za gari. Gari aina ya Toyota lililokuwa katika muundo wa pick-up lilikuwa likipita kwa kasi kwenye ule mtaa aliokuwa ameuingia. Na hata pale taa zile zilipommulika alikuwa ameshafika katikati ya barabara. Dereva alipiga honi kwa nguvu huku akikanyaga breki ghafla. Gari lilisota mbele na Jaka akaturusha mbele kwa nguvu na kuangukia upande wa pili wa ile barabara, akinusurika kugongwa. Sasa lile gari likawa katikati yake na wale askari waliokuwa upande wa pili wa ile barabara.
Na mara hiyo hiyo risasi nyingine ilivuma na kupasua moja ya taa za mbele za ile gari. Dereva kakanyaga tena mafuta kwa nguvu na lile gari likairuka mbele na kuondoka kwa kasi kutoka eneo lile.
Kwa mara ya pili katika siku ile Jaka alijikuta akifanya jambo lisilotarajiwa.
Alikamata upande wa sehemu ya mizigo ya lile gari kwa nguvu na kujaribu kulidandia wakati lilipoondoka kwa kasi kutoka eneo lile. Alirusha mguu wake kuuingiza kwenye ile sehemu ya kubebea mizigo, mguu ukateleza naye akabaki akining’inia ubavuni mwa lile gari kwa mikono yake huku miguu yake ikiburuzwa.
Wale askari waliona taa za nyuma za lile gari zikitokomea kizani kwa kasi. Waliangaza huku na kule katika eneo ambalo walitarajia Jaka angekuwepo bila mafanikio. Hawaelewa kabisa Jaka aliwatokaje pale na hawakutaka kabisa kuamini kuwa angekuwa amedandia lile gari kutokana na ile kasi iliyokuwa nalo. Kwa kasi iliyoondoka nalo kutoka eneo lile, mtu yeyote mwenye akili timamu asingeweza kudiriki hata kufikiria kulidandia lile gari.
Dereva wa lile gari alikata kona kwa kasi kuingia mtaa wa tatu kutoka ule zilipotokea risasi, na msukumo wa kasi ya kukata kona ile ulimtupa Jaka hewani na kumbwaga kwa kishindo kando ya barabara na kumgaragaza vibaya kwenye matope na majani. Alijiinua kutoka kando ya barabara na kuanza kukimbia kwa kuchechemea kuelekea kule lile gari lilipokuwa limepotelea. Wakati huu mvua ilikuwa inanyesha kwa nguvu zaidi na mji ulikuwa kimya na kiza kinene kilitawala. Jaka alihisi kuwa umeme ulikuwa umekatika, kama kawaida ya jiji la Dar katika kipindi cha mvua kubwa.
Aliacha kukimbia na kuanza kuifuata ile barabara iliyompeleka hadi akatokea kwenye barabara ya Old Bagamoyo road. Aliifuata barabara ile hadi kwenye eneo la maduka mengi ya Namanga. Bila ya kujali aliendelea na safari yake ambayo kwa kweli hakujua ingeishia wapi. Alitokea kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Akaivuka na kuingia mitaa ya maeneo ya Block 41. Kwa namna ya ajabu begi lake dogo bado lilikuwa likining’inia mgongoni kwake pamoja na misukosuko yote ile iliyotokea.
Alikuwa akitembea katika ile mitaa ya Block 41 bila ya uelekeo maalum katika usiku ule wa kiza kizito na mvua kubwa bila ya kujua kuwa mtaa wa pili kutoka pale alipokuwa, kulikuwa kuna msichana mmoja ambaye naye pia alikuwa matatani usiku ule. Msichana aliyekuwa akijitahidi kuwakimbia watu wanne waliokuwa na dhamira mbaya dhidi yake.
Ni katika usiku huu wa kiza kinene na mvua kubwa ndipo Jaka alipokutana na msichana yule, na pamoja wakajikuta wakikabiliana na wale watu wanne wenye dhamira mbaya.
Mmoja alikuwa ameshika rungu refu na zito.
Mwingine alikuwa ameviringisha mnyororo mnene kwenye ngumi yake.
Wa tatu alikuwa mikono mitupu, lakini mikono yake ilikuwa mikubwa yenye misuli minene.
Na yule wa nne alikuwa ameshika kisu kilichotoa mng’ao katika kiza kile cha usiku.
Na huo ndio ukawa mwanzo wa matukio mengine mengi katika maisha yake…

______________________

Saa ya ukutani iliyokuwa ikining’inia kwenye moja ya kuta za pale sebuleni ilionesha kuwa muda ulikuwa ni saa moja na nusu za jioni. Jaka alikuwa amekaa kwenye kochi kubwa la pale sebuleni huku akiwa amejishika tama na uso wake umekunjamana kwa mawazo mazito.
Alikuwa akitafakari matukio yaliyotokea siku ile.
Baada ya mlipuko wa lile bomu asubuhi ile pale sokoni, walichukuliwa na gari la polisi hadi kituo cha polisi cha mkoa ambako walimkuta mzee Januari Mwakaja akiwasubiri ofisini kwake. Baada ya kuwauliza juu ya hali zao na wao kumthibitishia kuwa walikuwa salama aliwatupia maswali mengi ambayo hawakuwa na majibu ya moja kwa moja.
Waliulizwa iwapo kuna mtu yeyote waliyekuwa wakimhisi kuhusika na tukio lile la kuogopesha.
Hawakuwa na mtu yeyote waliyekuwa wakimhisi kuhusika na tukio lile.
Januari Mwakaja alisisitiza sana juu ya uwezekano wa kuhusika kwa yule mtu ambaye Jaka na Clara walimjua kama John Doe na tukio lile. Kwa hilo Jaka alisema kuwa ingawa naye alikuwa akihisi hivyo, hakuwa na hakika. Alikumbuka onyo alilopewa na yule mtu mwenye koti refu na kofia pana kuwa pindi akihojiwa na polisi, asiseme lolote kuhusu kuonana kwao.
Muda wote huo Clara alikuwa ametulia kimya.
Walitolewa pale kituoni na kupelekwa hospitali ya mkoa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi iwapo walikuwa wamepata madhara yoyote kutokana na mlipuko ule. Uchunguzi ulionesha kuwa hawakuwa na madhara yoyote ya kutisha hivyo wakarudishwa nyumbani.
Muda mfupi baada ya kufika pale nyumbani, Mzee Wilfred Masahuri Zaza, baba yake Clara, alifika akiwa amejaa wahka mkubwa baada ya kupata taarifa ya mlipuko uliotaka kuondoa maisha ya mwanaye kipenzi na pekee hapa duniani.
Baba na mwana walikumbatiana kwa upendo na kufarijiana huku wakitokwa na machozi. Jaka waliwatazama wakiwa katika hali ile na moyo ulimuuma sana. Wazo kuwa yeye ndiye chanzo cha mashaka yale kwa baba na mwanye lilimuumiza roho sana.
Mzee Zaza alimgeukia na kumtazama kwa huzuni.
“Jaka…unajua kuwa sina chuki yoyote juu yako, lakini sasa ni dhahiri kuwa kuendelea kwako kuwa pamoja na binti yangu ni hatari kubwa kwa maisha yake.” Alimwambia huku akijifuta machozi. Jaka alimtazama tu yule mzee bila ya kumjibu, moyoni mwake akikubaliana naye moja kwa moja. Yule mzee alimgeikua binti yake.
“Clara mwanangu, nikiwa kama baba yako, kwa usalama wako nakuomba sana uhamie nyumbani kwangu mara moja. Huko utakuwa salama zaidi…lakini hutakuwa tena na huyu …mwenzio…hali halisi imejionesha kuwa si salama kwako.” Alimwambia.
Clara hakukubaliana kabisa na baba yake. Pamoja na Jaka kuingilia kati na kumsihi akubaliane na ushauri wa baba yake kuwa ndio wa busara zaidi kwake kwa wakati ule, bado Clara alishikilia msimamo wake.
“Hivi mnataka mimi niwe mtu wa aina gani?” Clara aliuliza kwa hasira baada ya kuona kuwa Jaka na Mzee Zaza wanazidi kumshawishi awe mbali na Jaka japo kwa muda tu mpaka hali itakapokuwa shwari.
Wote wawili walibaki wakimtazama.
“Tumekaa na Jaka kwa heshima na furaha kwa siku zote hizi, muda wote tukijua kuwa Jaka alikuwa anakabiliwa na tuhuma nzito…kabla ya hapo yeye alijitolea maisha yake kunisaidia wakati nilipokuwa nakiona kifo waziwazi machoni mwangu, sasa leo hii yeye afikwe na tatizo mimi niondoke niende kwa baba, naye nimwache peke yake? Hapana jamani. Siwezi kabisa kufanya kitu kama hicho!”
“Lakini mimi niko radhi Clara…ni bora iwe hivi!” Jaka alidakia.
“Na mimi pia nina maamuzi na maisha yangu Jaka, na uamuzi wangu kwenye hili ndio huo!” Clara alimjia juu, na akaondoka kwa hasira akiwaacha pale sebuleni.
“Clara!” Jaka na Mzee Zaza waliita kwa pamoja, lakini Clara alipitiliza na kujifungia chumbani kwake. Jaka na Mzee Zaza walitazamana, kisha wakainamisha nyuso zao. Baada ya muda mfupi Jaka aliinua uso wake na kumtazama yule mzee.
“Nimekuelewa sana mzee na wala sikulaumu kwa uamuzi wako…mimi nitaondoka leo hii hii hapa nyumbani, lakini naomba sana uendelee kumshawishi Clara ahamie kule kwako kwa usalama zaidi. Wema ambao wewe na yeye mmenifanyia ni mkubwa sana na mimi sina haki kabisa ya kutaka chochote zaidi kutoka kwenu…” Alimwambia.
 
RIWAYA; MTUHUMIWA

MTUNZI; HUSSEIN TUWA

SEHEMU YA ARUBAINI NA SITA

“Nimekuelewa sana mzee na wala sikulaumu kwa uamuzi wako…mimi nitaondoka leo hii hii hapa nyumbani, lakini naomba sana uendelee kumshawishi Clara ahamie kule kwako kwa usalama zaidi. Wema ambao wewe na yeye mmenifanyia ni mkubwa sana na mimi sina haki kabisa ya kutaka chochote zaidi kutoka kwenu…” Alimwambia.
“Hapana Jaka…” Mzee Zaza alimjibu, “…mimi namjua sana mwanangu. Akiamua jambo huwa haamui kipumbavu, huwa amelifikiria…na akishaamua, ni vigumu sana kumshawishi vinginevyo...ni tabia aliyoirithi kutoka kwa mama yake…marehemu mke wangu.” Alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu. Jaka alitaka kusema kitu lakini mzee Zaza akamuashiria anyamaze.
“Mama yake Clara alijua kuwa iwapo atapata ujauzito na kujifungua, basi maisha yake yangekuwa hatarini na angeweza kupoteza maisha kutokana na afya yake kuwa dhaifu. Lakini alipopata ujauzito alikataa katakata ushauri wa daktari kuwa ile mimba itolewe ili aokoe maisha yake…kwa sababu alikuwa anataka sana kupata mtoto. Na kweli…baada ya kuzaliwa Clara mke wangu mpenzi akaaga dunia…na tangu siku hiyo Clara amekuwa ndiye amekuwa familia yangu…” Aliongea yule mzee kwa huzuni, na Jaka alibaki akimtazama yule mzee tajiri bila ya kujua aseme nini.
“Wacha nikaongee naye tena.” Yule mzee alisema huku akielekea chumbani kwa Clara.
Nusu saa baadaye, mzee Wilfred Mashauri Zaza alirejea pale sebuleni na kusimama kwa muda mrefu kabla ya kuanza kuongea.
“Najua kuwa binti yangu anakupenda sana Jaka, lakini sijui kama amefanya uamuzi wa busara au wa kipuuzi kwa kukupenda. Ninachojua ni kuwa hivyo ndivyo mapenzi yalivyo. Wakati mimi naanza mapenzi na marehemu mama yake, sikuwa tofauti sana na wewe…kwamba Joanna, mama yake Clara alikuwa tajiri sana wakati mimi nilikuwa mfanyabiashara wa kawaida tu, sikuwa na ndugu wala jamaa na sikuwa tajiri kama yeye. Lakini Joanna hakufanya jambo la kipuuzi alipoamua kupendana nami…mimi sikuwa na nia mbaya juu yake.”
Jaka alitulia kimya akimsikiliza.
“Nadhani usalama wa mwanangu unategemea sana na nia yako kwake, Jaka. Kwa sababu yule ni msichana tu aliyetokea kukupenda, I can understand that …sasa wewe ukija kumfanya yeye bwege kwa hilo sitakuelewa kabisa. Usije ukamfanya ajutie uamuzi wake Jaka. Kwa sababu ukimfikisha katika hatua hiyo hutakuwa umemuumiza yeye tu bali na mimi vilevile…”
Jaka aliendelea kumsikiliza kwa makini huku yale maneno yakimwingia vizuri mno.
“Clara ameamua kuendelea kukaa na wewe hapa hapa…hivyo ndivyo mwanangu anavyokupenda Jaka. Yuko tayari kuhatarisha maisha yake kwa ajili yako…sio jambo la mchezo hata kidogo hilo. Mimi nimemkubalia kwa sharti kwamba nitaweka askari wa kuhakikisha usalama hapa nyumbani saa ishirini na nne…na kila atakapokwenda, atasindikizwa na askari. Namna hiyo nadhani kidogo kutakuwa kuna amani japo kidogo, moyoni mwangu.”
“Nashukuru mzee…na sitamfanya ajute hata kidogo.” Jaka alisema, na yule mzee alimtikisia kichwa tu kuafikiana naye, kisha akaiendea simu na kuanza kufanya taratibu za ulinzi kwa kuwasiliana na mkuu wa polisi wa mkoa. Baada ya kufanya hivyo walikaa kimya pale sebuleni hadi dakika ishirini baadaye wakati askari wawili waliporipoti kuanza kazi ya kulinda usalama wa nyumba ya Clara pale Uhindini. Hapo Mzee Zaza alienda chumbani kuagana na mwanaye, kisha akarudi pale sebuleni na kuagana na Jaka.
“Zingatia maneno niliyokueleza kuhusu binti yangu kijana.” Mzee alimwambia.
“Bila shaka mzee…” Jaka alijibu.
Yule mzee akaondoka, akimuacha akiwa amekaa peke yake pale sebuleni.

_____________________

Sasa Jaka aliinuka kutoka pale kwenye kochi na kuchungulia dirishani. Askari mmoja alikuwa amesimama mbele ya nyumba ile. Bastola moja ilikuwa imening’inizwa kiunoni kwake na radio ya mawasiliano ya kipolisi ilionekana kuchungulia kutoka kwenye mfuko wa shati lake. Begani alikuwa amening’iniza bunduki aina ya SMG. Alienda kuchungulia dirisha la nyuma. Nako kulikuwa na hali kama ile ya kule mbele. Alirudi sebuleni na kurudia kujiinamia pale kwenye kochi, bado mawazo mazito yalikitawala kichwa chake.
Ina maana hawa jamaa wamenifuata mpaka huku Dodoma? Kule Dar wamenikosakosa mara mbili bloody fools…kule njia ya Segerea na pale darajani Manzese…sasa hii hali itakuwa hivi mpaka lini?
Alisonya.
Mwishowe wataniua kweli hawa, yaani walikuwa tayari hata kumuua na Clara ambaye hana makosa yoyote? Aaah mi’ naona sasa wakati wa wao kulipa kwa matendo yao umefika…na watajuta! Hivi lini John Doe atatokea? Nina hakika jamaa atakuwa na msaada fulani kwangu, kinyume na nilivyomdhania hapo mwanzo.
Muda huo Clara aliingia pale sebuleni kutokea chumbani kwake na kwenda kuketi naye kimya pale kochini. Jaka alimtazama na kukumbuka maneno ya mzee Wilfred Mashauri Zaza. Moyo wake wote ukamuendea yule binti na alijihisi kumpenda zaidi na zaid. Kitendo cha kuamua kuendelea kuwa naye hata katika kipindi kile kigumu na cha hatari kabisa kilimtia moyo sana Jaka. Alikumbuka jinsi Moze, mpenzi wake wa awali na aliyewahi kumpenda kwa moyo wake wote, alivyomkana na kumuacha katika kipindi ambacho ndio alikuwa akimhitaji sana kutokana na matatizo makubwa aliyokuwamo wakati huo…matatizo yaliyomkuta kutokana na kulitetea penzi lao wenyewe.
Sasa leo huyu binti aliyekaa pembeni yake amekuwa radhi kujitolea maisha yake kuliko kumuacha peke yake katika dimbwi la madhila yale yasiyosemeka…
Alibaki akimtazama tu yule binti kwa upendo uliojaa shukurani.
Clara alimgeukia na wakatazamana. Macho yao yaliongea na kuelewana vizuri sana. Walikumbatiana kwa upendo, na kubaki wakiwa wamekumbatiana pale kwenye kochi kwa muda mrefu.
“Asante sana Clara.” Hatimaye Jaka aliongea.
“Kwa nini…?”
“Kwa kutoniacha peke yangu katika matatizo haya…”
Clara aliinua kichwa chake na kumtazama usoni.
“Kwani kama ungekuwa wewe ungeniacha?”
“Hapana…hata kidogo.”
“Sasa kwa nini unadhani mi’ ningeweza hata kufikiria kukuacha?” Clara alimuuliza, na kuendelea, “Matatizo hayana mwenyewe Jaka, yanaweza kumpata mtu yeyote…na umuhimu wa rafiki…wa mpenzi…unaonekana zaidi pale ambapo mtu uko kwenye matatizo. Mi’ n’takuwa mpenzi wa aina gani kama nitakuacha mpenzi wangu katika kipindi kama hiki Jaka? Halafu matatizo yakiisha nitafanyaje..nitarudi tena kukwambia ‘haya mpenzi sasa tuanze kupendana tena’? Haiwezekani.”
Jaka aliafikiana naye kutikisa kichwa taratibu, akilini akijiuliza ilikuwaje hata Moze akashindwa kuelewa jambo kama lile. Waliendelea kukaa kimya huku wakiwa wamekumbatiana kwa muda mrefu zaidi.
“Ni mambo gani yaliyokutokea huko nyuma hata ukalazimika kuja kizuizini huku Dodoma, Jaka?” Hatimaye Clara alimuuliza.
“Mengi sana Clara…”
“Naomba leo unielezee juu ya mambo hayo mpenzi…ni nini kilitokea mpaka tukakutana siku ile ya mvua kubwa na kiza kizito kule Dar es Salaam, na pia ilikuwaje hata tukaja kukutana tena hapa Dodoma…na mara zote hizo tumekuwa tukikutana katika mazingira ya kutatanisha. Ni wazi kuwa tukio la leo linatokana na mambo yaliyokutokea huko nyuma…”
Jaka alitulia kimya kwa muda kabla ya kumjibu.
“Clara, mi’ naona ni salama zaidi kwako kutoyajua mambo yaliyotokea huko nyuma kuliko kuyajua…”
Clara alijiinua taratibu kutoka kifuani kwake na kuketi huku akimtazama usoni.
“Jaka, tangu tuanze kujuana kwa ukaribu, sijawahi hata siku moja kukuuliza kuhusu maisha yako ya huko nyuma, hasa kuhusiana na mambo yanayohusiana na matatizo haya uliyonayo. Ni kwa sababu nilijua kuwa yaliyotokea huko nyuma hayakunihusu, nami nikaamua kujihusisha na maisha yako niliyokukuta nayo na kuendelea mbele huku nikiamini kabisa kuwa wewe hukufanya hilo kosa linalosemekana kuwa umelifanya hadi ukapewa adhabu ya kufukuzwa jiji la Dar…”
“Clara…”
“Subiri nimalize…mi’ nilishawahi kukueleza kuwa huwezi kuukimbia ukweli Jaka, kwani kuukimbia ukweli ni sawa na kujikimbia mwenyewe. Sasa ukweli umeshadhihirika mpenzi wangu…nao ni kuwa kuazia sasa hauko peke yako kwenye jambo hili…tuko pamoja. Mimi na wewe. Na kama tuko pamoja, basi sasa na mimi nastahili kabisa kuelewa juu ya jambo ambalo saa kadhaa tu zilizopita lingesababisha wewe na mimi tuwe marehemu, kwa sababu lile bomu lisingechagua Jaka..tungekufa sote!”
Duh!
“Dah! Ni kweli Clara, lakini…”
“Lakini nini Jaka? We’ kama unaona kuwa hayo matatizo ni yako peke yako basi hali hiyo ilibadilishwa na ule mlipuko wa bomu asubuhi ya leo. Ule mlipuko umenipa haki ya kujua kila kitu kuhusu yaliyokutokea kule Dar, Jaka. Sasa matatizo haya ni yetu sote, na tunatakiwa tushirikiane katika kukabiliana nayo…na njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuanza kueleweshana hali halisi ilivyokuwa tangu mwanzo hadi hapa tulipo…halafu tuone tutaenda vipi huko mbele katika kukabiliana na hali hii.” Clara alimwambia kwa msisitizo.
Jaka hakuwa na hoja tena.
Akamueleza kisa chote cha maisha yake tangu mwanzo. Alimueleza kuhusu Moze, Joakim Mwaga na wenzake na mambo yote yaliyotokea hadi kuuawa kwa Joakim na yeye kutuhumiwa na hatimaye kuhukumiwa kwa mauaji yale. Alimalizia kwa kuelezea matukio yaliyotokea siku ile ambayo usiku wake ndio walikuja kukutana kwa mara ya kwanza kule Dar katika usiku ule wa mvua kubwa na kiza kinene…

_____________________

Clara alibaki mdomo wazi huku akimkodolea macho kwa huruma na mshangao.
“Aisee! Pole sana…dear…yaani, Ah! Hayo mambo huwa nayaona kwenye sinema tu, sikutegemea kabisa kuwa yanaweza kumtokea mtu kikweli kweli, na mtu mwenyewe awe ndiyo wewe…!”
“Yametokea dear…na yamenitokea mimi…nadhani sasa unaelewa ni kwa nini hao watu wataka kuniua.”
“Naelewa sasa…naelewa kabisa!”
Jaka alishusha pumzi ndefu na kutazama pembeni. Walibaki kimya kwa muda, kisha Clara aliuliza, “Kwa hiyo mtu aliyemuua Joakim hajajulikana mpaka sasa…?”
“Sijui kwa kweli…kwa sababu mtu pekee ambaye ningeweza kumhisi ni Tony, lakini Tony na Joakim walikuwa marafiki…” Jaka alijibu kwa mashaka.
Bado Clara alionekana kulitafakari kwa makini lile swala.
“Sasa…na zile glovu zilifikaje chumbani kwako…yaani inawezekanaje mtu aingie chumbani kwako na kupandikiza kitu kama kile bila ya wewe kujua?” Clara aliuliza kwa wasiwasi.
“Mmnh, Clara…! Hapo ndipo panaponishinda…kwa vyovyote vile yeyote aliyeingia na kupandikiza zile glovu chumbani kwangu siku ile, alifanya hivyo katika muda ule ambao mimi nilikuwa kule juu ya jengo nilipomkuta Joakim akiwa tayari ameuawa.” Jaka alijibu huku uso wake akiwa ameukunja kwa kutafakari.
“Kwani ulipotoka hukufunga mlango?”
“Mnh! Sikumbuki sawa sawa…”
“Mnh, Jaka! hebu rudia tena kunielezea kuanzia pale ulipoanza kujirekodi…” Clara alimwambia huku akijiweka vizuri pale kwenye kochi, uso wake ukionesha bashasha ya hali ya juu. Jaka alimtazama kwa mshangao kwani hakuelewa ingesaidia nini au Clara alikuwa na mawazo gani. Hata hivyo, alifanya kama alivyoombwa na kurudia kumuelezea ile sehemu.
Alipomaliza, Clara alibaki akiwa amekunja uso kwa mawazo huku akiangalia upande ule aliokuwapo Jaka ingawa Jaka aliona kabisa kuwa alikuwa hamuoni. Akili yake ilikuwa inafanya kazi kupita uwezo wake, na Jaka alizidi kushangaa ni nini kilikuwa kinapita kichwani mwa yule binti wakati ule.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom