Riwaya:Mtuhumiwa

Riwaya:Mtuhumiwa

RIWAYA; MTUHUMIWA

MTUNZI; HUSSEIN TUWA

SEHEMU YA ARUBAINI NA SABA

“Mnh, Jaka! hebu rudia tena kunielezea kuanzia pale ulipoanza kujirekodi…” Clara alimwambia huku akijiweka vizuri pale kwenye kochi, uso wake ukionesha bashasha ya hali ya juu. Jaka alimtazama kwa mshangao kwani hakuelewa ingesaidia nini au Clara alikuwa na mawazo gani. Hata hivyo, alifanya kama alivyoombwa na kurudia kumuelezea ile sehemu.
Alipomaliza, Clara alibaki akiwa amekunja uso kwa mawazo huku akiangalia upande ule aliokuwapo Jaka ingawa Jaka aliona kabisa kuwa alikuwa hamuoni. Akili yake ilikuwa inafanya kazi kupita uwezo wake, na Jaka alizidi kushangaa ni nini kilikuwa kinapita kichwani mwa yule binti wakati ule.
“Jaka, ulipotoka kwenda kule juu ya jengo siku ile, ulitoka na ile simu yako uliyokuwa ukiitumia kujirekodi?” Clara alimuuliza baada ya kufikiri kwa muda mrefu. Jaka alimtazama Clara kwa mshangao huku akionesha wazi kuwa hakuona umuhimu wa swali lile.
“No, sikutoka nayo…niliiacha…” Alimjibu kw auhakika kabisa.
“Una hakika…?” Clara alizidi kumuuliza.
Bila ya kuelewa Clara alikuwa ana nia gani, Jaka alimjibu tena kuwa ana hakika kabisa na hilo.
“Mnh…haya…na sasa hili ninalokuuliza ni la msingi sana…uliizima ile sehemu ya kurekodia pale kwenye simu yako kabla hujatoka?” Clara alimuuliza tena, na Jaka akakunja uso.
“Aaa sasa ilikuwa ni muda mrefu sana Clara…sikumbuki iwapo…”
“Kumbuka Jaka…hebu fikiria kwa makini na urudishe kumbukumbu zako hadi siku ile ulipokuwa ukijirekodi…ulizima ile sehemu ya kurekodia ulipotoka…?” Clara alizidi kumhimiza, uso wake ukionesha umakini uliomfanya Jaka pia amakinike. Bila ya kuelewa Clara alikuwa anaelekea wapi na swali lile, alikunja uso na kufumba macho akijitahidi kukumbuka. Alikaa katika hali ile kwa muda mrefu huku Clara akimtazama kwa makini. Kichwani mwake, matukio ya siku ile ambayo alishajipiga marufuku kabisa kuyafikiria au kuyakumbuka, yalijirudia haraka haraka kichwani mwake, bila ya mpangilio maalum.
Na mara ikamjia.
Ilitokea tu kama kama kitu kilichoshushwa na mwenyezi Mungu kutoka mbinguni na kumuingia kichwani mwake.
Ghafla alifumbua macho huku akimgeukia Clara taratibu, akimtazama kwa mshangao na kutoamini.
“Umekumbuka!” Clara alimwambia kwa bashasha.
“Sikuizima ile simu, Clara!” Jaka alimwambia kwa sauti ya kunong’ona huku naye macho yake yakionesha bashasha kubwa.
Clara aliinuka kutoka kwenye kochi na kusimama mbele yake.
“Una hakika Jaka?”
“Ndio, aisee…ndio! Nina hakika kabisa sikuizima, Clara!”
“Oh, My God!” Clara alisema huku akimtazama kwa hamasa kubwa kabisa.
Siku zote amekuwa akitawaliwa na hisia kuwa kuna kitu fulani ambacho kingeweza kumpatia ufumbuzi wa kitendawili kikubwa kilichoizunguka ile kesi aliyoangushiwa na ambayo imemchafulia jina lake kwa kiasi kikubwa sana. Alikuwa akijua kabisa kuwa kuna kitu fulani lakini hakuweza kukigundua mara moja ni kitu gani…ni kitu kilichokuwa nyuma kabisa ya ubongo wake ambacho siku zote kilikuwapo, lakini hakuweza kukivuta kutoka nyuma ya ubongo wake na kukiona wazi katika fahamu zake.
Mpaka leo.
Leo kitu kile kimemjia wazi wazi akilini mwake. Fahamu ile ilimjia kama muujiza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hapo Jaka alikubali kabisa kuwa kumbe kweli Mungu yupo.
“Jaka! Unaelewa ni nini inamaanisha hiyo…?” Clara alimuuliza huku akiketi tena pale kochini kando yake.
Jaka alitikisa kichwa kwa mastaajabu.
“Kwa hakika kwanza nilikuwa sielewi kwa nini ulikazania kuulizia iwapo niliizima ile simu au la…lakini kama na wewe unafikiria lile ninalolifikiria hivi sasa, basi jibu ni kwamba ninaelewa ni nini inamaanisha…”
Walitazamana.
Alipopigiwa hodi chumbani mwake siku ile alipokuwa akijirekodi akiimba shairi kwa ajili ya Moze, yeye alikurupuka na kwenda kusikiliza ni nani aliyebisha hodi pale mlangoni na kuiacha ile simu ikiendelea kurekodi. Baada ya hapo alikurupuka kwenda kusubiri lifti baada ya kusoma ule ujumbe wa Joakim, na kuacha mlango wazi na ile simu ikiendelea kujirekodi pale mezani…
Mawazo yake hayo yalikatishwa na sauti ya Clara iliyojaa hamasa.
“Jaka! Hiyo inamaanisha kuwa ile simu itakuwa imerekodi sauti zote zilizotokea mle ndani muda mchache baada ya wewe kutoka, na mtu yeyote aliyeingia chumbani mwako siku ile na akatoa sauti yoyote ile, atakuwa amerekodiwa…”
“Sawa sawa kabisa!” Jaka alikubaliana na yule binti, kisha akiongezea, “kama atakuwa ametoa sauti, lakini kama aliingia na kutoka kimya kimya…”
“Hiyo itajulikana baadaye…lakini najua lazima watakuwa wamesema kitu Jaka…si umesema kundi lao wako watatu…?”
“Kama ni wao ndio waliohusika na kifo cha Joakim, na kunibambikia ule ushahidi, watakuwa watatu tu…Tony, Ng’ase na Muddy…na huwa hawaachani.”
“Jibu liko kwenye ile simu yako Jaka!” Clara alimwambia kwa wahka.
Jaka alimtazama yule binti kwa upendo na heshima kubwa.
“Clara you are a genious! Yaani sijaona msichana mwenye akili kama wewe! Bila ya wewe kufikiria juu ya simu niliyokuwa natumia kabla ya kutoka nje ya chumba changu sijui kama ningeweza kuigundua siri hii…!” Alimwambia kwa shukrani.
“Ndio uzuri wa kujadili matatizo pamoja dear…lazima kutapatikana ufumbuzi tu…” Clara alimjibu huku akimkumbatia.
“Oh, Clara…”
“Sasa swali kubwa zaidi mpenzi wangu ni je, ile simu bado ipo? Na tutaipataje?” Clara alimwambia huku akijichomoa kutoka kwenye kumbatio lake na kumtazama usoni.
Jaka aliafikiana naye kwa kichwa huku akikunja uso kwa kutafakari.
“Nakumbuka rafiki yangu niliyekuwa naishi naye pale chuoni aliniambia kuwa alikusanya vitu vyangu vyote na kuviweka kwenye boksi…ambalo alilipeleka nyumbani kwa mama yangu…sa’ sijui kama na ile simu itakuwa ni miongoni mwa hivyo vitu au hata kama bado inafanya kazi…ni muda mrefu sana unajua!” Alisema.
“Itabidi tulipate hilo boksi basi ili tujihakikishie…hatuwezi kumpigia simu mama’ako tumuombe aangalie kwenye hilo boksi?” Clara alisema. Jaka alisita.
“Mnh! Mimi sasa sina imani kabisa na hawa jamaa wanaoniwinda, vipi kama watakuwa wanafuatilia hadi mawasiliano yetu ya simu? Wanaweza kutuvurugia hata hili, unajua hiyo simu inaweza kubadili kabisa kila kitu kilichosemwa juu yangu kwenye kesi hii? Wale jamaa hawawezi kabisa kupenda hilo litokee.”
“Mnh, ila kweli aisee. Sasa itakuwaje? Maana we’ kwenda Dar kufuatilia huwezi…vipi tukimtumia mama ujumbe wa simu kumuagiza aatutizamie kwenye hilo boksi alilokabidhiwa na huyo rafikiyo?”
“Yote yale yale tu mi’ naona Clara…wanaweza kupata machapisho ya mawasiliano yetu ya meseji kutoka kwenye makampuni ya simu pia! Watu wameweza kujifanya maaskari wakasafiri nami gari moja bila kutiliwa mashaka, watashindwa hilo? Hapo ni mtu kwenda tu mpaka Dar…” Jaka alisema kwa kuchanganyikiwa.
Walikaa kimya kwa muda mrefu. Katika muda ule, Jaka alikuwa akifikiria ni jinsi gani watalitatua tatizo lile. Akilini mwake alikuwa akiikumbuka vizuri sana ile simu yake aliyokuwa akiitumia kujirekodia pale chumbani kwake siku ile. Ile simu ilikuwa imerekodi lile shairi kwa muda wa kama dakika mbili tu kabla yule mtoto hajabisha hodi mlangoni kwake siku ile. Ukitoa dakika zipatazo tano hivi alizotumia kuongea na yule mtoto pale mlangoni na kujishauri iwapo aende kule alipotakiwa kwenda kwa mujibu wa ujumbe wa Joakim, alibakiwa na dakika nyingine nyingi sana ambazo ile simu ingeweza kurekodi sauti nyingine yoyote ambayo ingesikika mle chumbani mwake. Katika dakika hizo zote, mtu aliweza kabisa kuingia mle ndani, akaweka zile glovu chini ya godoro, na kutoka.
Mara wazo lilimjia.
“Unajua…mimi siwezi kwenda Dar sasa hivi, lakini wewe unaweza…” Alimwambia mpenziwe. Clara alimtazama huku akiafikiana naye kwa kutikisa kichwa chake taratibu.
Hatimaye walikubaliana juu ya hilo. Jaka alimuelekeza nyumbani kwa mama yake na akaandika barua ambayo alimtaka ampe mama yake pindi akionana naye ili aweze kumpatia kile walichokuwa wakikihitaji.
Walipanga safari ya Clara iwe siku iliyofuata.
“Sasa naomba unihadithie mambo yote yaliyotokea baada ya mimi kuondoka kule Dar na kukuacha na wale askari pale kituo cha polisi cha OysterBay siku ile.” Clara alimwambia baada ya kukubaliana juu ya safari ile.
Usiku ule wakiwa wamelala kitandani Jaka alimsimulia mambo aliyokutana nayo tangu siku ile, miezi kadhaa iliyopita, alipomuacha pale kituo cha polisi cha Oyster Bay jijini Dar, hadi pale alipoamka na kujikuta chumbani kwa Clara pale Dodoma baada ya kupoteza fahamu kutokana na kipigo kwa kudhaniwa mwizi pale nje ya ukumbi wa Disko wa NK.

__________________

Wakati Jaka anamsimulia Clara mambo aliyopambana nayo tangu waachane jijini Dar miezi kadhaa iliyopita, Mzee Januari Mwakaja, mkuu wa Polisi wa mkoa wa Dodoma alikuwa akizungusha gari lake kwenye mzunguko wa Jamatini taratibu huku akipiga mwayo mrefu. Alikuwa amechoka na akilini mwake alikuwa anajaribu kuyatafakari matukio ya siku ile huku mara kwa mara mawazo yake hayo yakimfikiria mkewe huko nyumbani ambaye siku zote huwa hapendi kabisa mumewe achelewe kurudi kutoka kazini.
Huyu Jaka alifanya nini kule Dar? Hadi anategeshewa bomu!
Alipita ofisi ya mhandisi wa mkoa na kuzunguka mzunguko wa pili uliokuwa karibu na chuo cha biashara, akikata kushoto na kuchukua barabara ielekeayo Area C kupitia Makole.
Kitendo cha faili la kesi yake kutoweka katika mazingira yasiyoeleweka kinamaanisha kuwa jambo hili lilipangwa toka zamani…sasa leo angekufa katika mlipuko ule kusingekuwa na kumbukumbu yoyote ya mambo ambayo yeye alihusika nayo hapo mwanzo au uwezekano wa kugundua iwapo alisingiziwa mauaji ili kuficha ukweli fulani…ambao nadhani yeye Jaka atakuwa anaujua…
“Endelea kuendesha hivyo hivyo na utekeleze maelekezo yangu afande!” Sauti nzito ilimshitua kutokea kwenye kiti cha nyuma mle garini.
“AAAAARRGHH…!” Alipiga kelele kwa mshituko na kwa muda gari liliyumba kabla hajatulia na kuliweka sawa barabarani. Mara ile ile alihisi akiwekewa kitu cha baridi nyuma ya shingo yake naye akajua kuwa alikuwa amewekea mdomo wa bastola. Aliendelea kuendesha taratibu huku akili yake ikifanya kazi haraka haraka.
“Wewe ni nani bwana, na unataka nini? Unajua kuwa mimi ni nani?” Aliuliza huku akiendelea kuendesha kwa mwendo mdogo sana.
“Wewe ni RPC Januari Mwakaja, na kisogoni kwako kuna mdomo wa bastola aina ya
Graz-Burya. Ni silaha makini yenye uwezo wa kufanya uharibifu usiotengenezeka katika mwili wa binadamu, kwa hiyo ningekuomba utulie tu afande na unisikilize…” Ile sauti ilimkoromea kutokea kule nyuma. Mzee Januari Mwakaja alitulia huku akiendelea kuendesha, kisha akajaribu kutia jeuri huku akiongeza mwendo wa gari.
“Nadhani unaelewa kuwa ukiitumia hiyo silaha sasa hivi sote tutakufa, kwa sababu gari litapinduka na hutakuwa na uhakika kama wewe utatoka salama…” Alimwambia.
“Unataka tujaribu?” Ile sauti ilimuuliza, na Mzee Mwakaja akajua kuwa hakuwa na ujanja.

***DUH! NANI TENA?
 
RIWAYA; MTUHUMIWA

MTUNZI; HUSSEIN TUWA

SEHEMU YA ARUBAINI NA NANE

Mzee Januari Mwakaja alitulia huku akiendelea kuendesha, kisha akajaribu kutia jeuri huku akiongeza mwendo wa gari.
“Nadhani unaelewa kuwa ukiitumia hiyo silaha sasa hivi sote tutakufa, kwa sababu gari litapinduka na hutakuwa na uhakika kama wewe utatoka salama…” Alimwambia.
“Unataka tujaribu?” Ile sauti ilimuuliza, na Mzee Mwakaja akajua kuwa hakuwa na ujanja. Alibaki kimya huku akijaribu kumtazama yule mtu kwa kutumia kioo cha kutazamia magari yatokayo nyuma kilichokuwa mbele yake mle garini. Hakuweza kumuona vizuri kutokana na kiza, lakini aliweza kuona kofia pana iliyofunika sehemu kubwa ya uso wa yule mtu. Hapo hapo alikumbuka maelezo ya Jaka juu ya mtu aliyekuwa akimfuata fuata anayevaa koti refu na kofia ya pama.
Ndiye huyu…?
“Unataka nini?” Hatimaye alirudia swali lake la kwanza.
“Endelea kuendesha!”
Mzee Mwakaja alitii amri ile. Baada ya mwendo fulani, ile sauti ilimwamuru aegeshe gari kando ya barabara na atulize mikono yake kwenye usukani. Januari Mwakaja akatii amri ile huku akibaini kuwa yule mtu alimwamuru asimamishe gari sehemu ambayo ilikuwa mbali sana na nyuma za raia.
“Maongezi ninayotaka kuongea nawe ni ya siri sana ndio maana imenibidi nitumie njia hii ya kijasusi, bila shaka utaelewa.” Ile sauti ilimwambia kutokea kule nyuma huku muongeaji akimkabidhi kitambulisho kutokea kule nyuma. Mzee Mwakaja alikipokea na kuwasha taa ya ndani ya gari kukiangalia. Haikuwa mara yake ya kwanza kuona kitambulisho cha aina ile. Kilikuwa ni kitambulisho cha afisa wa usalama wa taifa.
“Sawa bwana Jeff Bijhajha…nimekiona kitambulisho chako, lakini sijui kuwa sura iliyoko huko nyuma ndiyo haswa ya huyu mtu anayeonekana kwenye hiki kitambulisho.” Alisema huku akirudisha kile kitambulisho bila ya kugeuka nyuma.
“Unaweza kugeuka nyuma taratibu sana kuniangalia.” Jamaa alimwambia huku akikipokea kile kitambulisho chake. Januari Mwakaja aligeuka na kumtazama. Walitazamana. Hakuwa amepata kumuona kabla ya wakati ule, lakini sura iliyokuwa kwenye kitambulisho kile ilikuwa ndiyo haswa aliyokuwa akitazamana nayo wakati ule.
“Umeridhika?” Jeff Bijhajha aliuliza, na mzee Mwakaja aliafiki kwa kichwa.
“Nadhani sasa unaweza kuzima taa ya gari ili tuongee.”
Mzee Mwakaja alizima taa ya ndani ya gari na yule afisa wa usalama wa taifa alianza kueleza.
“Sasa hivi kumetokea wimbi kubwa la biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini, na katika miaka miwili iliyopita serikali, ikivitumia vyombo vyake vya dola, imekuwa ikijitahidi bila ya mafanikio kukabiliana na wimbi hili…
“…tatizo kubwa limekuwa kwamba pamoja na kuwa inajulikana wazi kuwa biashara hiyo inafanyika humu nchini, kiini cha bidhaa hiyo haramu kimeendelea kuwa kitendawili…swala la nani hasa anayehusika na kuyaingiza hapa nchini na kwa kutumia njia gani ndilo limekuwa gumu mno kwa serikali na idara zake zote za kudhibiti madawa ya kulevya.”
“Ah, Lakini mbona kuna watu, hasa vijana, wengi tu wanaokamatwa na madawa hayo kila kukicha? Ina maana imeshindikana kuwabana wote hao hata wakataja ni wapi wanapata bidhaa hiyo?” Mzee Mwakaja alidakia.
“Hao unaowasema wewe ni wale wasambazaji wadogo wadogo tu ambao hawakuwa na msaada wowote wa maana mpaka sasa. Wengi wao wamekuwa wakitoa mtiririko wa habari zilizoishia hewani tu, hazifikii hasa pale kwenye shina kuu la biashara hii nchini…yaani hizi mbinu za kuendesha biashara hii ni za uficho sana kiasi kwamba ni vigumu kuwatia mkononi wale mapapa na manyangumi wa biashara hii. Tunaishia kukamata vijidagaa tu…wale watekelezaji wa mwisho kabisa ambao huwa hata hawaelewi hao mabosi wa biashara hii ni akina nani hasa…it’s very complicated…”
“Yote nayajua hayo…inahusu nini kuniinyatia garini mwangu usiku wote huu na kunieleza hayo?” Januari Mwakaja alitia hoja.
“Isitoshe, wengi wa hao wanaokamatwa ni watumiaji wadogo wadogo tu ambao huwa hawajali ni nani anayewaletea bidhaa hiyo, wanachojali wao ni kupata tu hiyo bidhaa, basi...” Jamaa aliendelea kama kwamba hakulisikia swali la yule mkuu wa polisi wa mkoa, na akaendelea, “…na wengine ni wale wanaokuja na bidhaa hiyo moja kwa moja kutoka nje ya nchi, kama vile Pakistan, Uturuki na nchi za Afrika ya Kusini na magharibi, wale wanaomeza paketi za unga huo na kukamatwa hapa uwanja wa ndege. Hawa mara nyingi huzitaja nchi walizotoka na unga huo kuwa ndio chanzo cha biashara hiyo. Wote hawa hawakuwa na msaada wa maana katika kuwafikia yale manyangumi ya biashara hii humu nchini.”
“Nimekuelewa. Lakini bado hujanielewesha ni jinsi gani swala lote hilo linahusika na mkoa wangu hadi ifikie hatua ya sisi kuongea katika mazingira kama haya.”
“Swali zuri…hapa ndipo utakapoelewa ni jinsi gani wewe unaingia…” Jeff Bijhajha alimjibu kisha akavuta pumzi na kutulia kidogo kabla ya kuendelea, “Kiasi cha kama mwaka mmoja uliopita, ujumbe maalum kutoka kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya cha marekani, kijulikanacho kama D.E.A…”
“Drug Enforcement Agency…” Januari Mwakaja alidakia.
“Yeah…Drug Enforcement Agency…ujumbe kutoka D.E.A. ukiongozwa na balozi wa Marekani hapa nchini ulimtembelea Rais Ikulu na kumkabidhi ripoti kuhusu biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini. Ripoti hiyo ilionesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kushiriki kwa viongozi wa ngazi za juu aidha serikalini au ndani ya jeshi la polisi katika uendeshaji wa biashara haramu ya madawa ya kulevya hapa nchini. Ingawa taarifa hii ilikuwa ngumu kukubalika mara moja, lakini ilileta maana kutokana na ukweli kwamba jitihada zote za serikali za kupambana na biashara hii zimekuwa zikigonga mwamba, na mara nyingi ilionekana kama kwamba hao wanaoendesha biashara hii, walikuwa wanapata taarifa zote za nini serikali ilikuwa inapanga na hivyo kuwawia rahisi kwao kukwepa mitego ya serikali.”
Mzee Januari Mwakaja alikaa vizuri huku akisikiliza kwa makini maelezo yale. Ile sauti nzito iliendelea kueleza kwenye kiza cha mle garini.
“Ni kutokana na ripoti hii ndipo rais alipounda tume maalum kuchunguza undani wa swala hili. Hii ni tume ya siri sana kiasi kwamba hata watu wa ngazi za juu kabisa serikalini hawajui juu ya uwepo wake. Mimi ni mmoja kati ya watendaji wa tume hii, na mpaka sasa tuna orodha ya baadhi ya askari wakubwa wanaoshukiwa kujihusisha na biashara hiyo, ingawa bado hatujafanikiwa kukitambua kiini cha uendeshaji wa biashara hiyo hapa nchini mpaka sasa.”
“Sasa bwana mdogo mbona unaniambia yote haya?” Januari alidakia tena.
“Hewaa! Nakueleza haya kwa sababu tume imenielekeza nije nikueleze habari hii, na nimetakiwa nikueleze habari hii ili uone umuhimu wa kunipa ushirikiano kwenye jambo lililonileta hapa Dodoma…”
“Mnh, okay. Ni jambo gani hasa lililokuleta hapa Dodoma bwana Bijhajha?” Januari Mwakaja aliuliza huku akiwa makini sana .
“Kijana aitwaye Jaka Brown Madega.”
“Whaat? Jaka…! Jaka si mhalifu aliyeletwa hapa kutumikia kifungo cha nje kwa kosa la mauaji!” Januari Mwakaja aliuliza kwa mshangao.
“Inaweza ikawa kweli amefanya hayo makosa…lakini pia inawezekana ikawa amepakaziwa tu kwa sababu ya kulinda maslahi ya watu fulani…” Jeff alimjibu.
“Kwa hiyo…?”
“Bila kutafuna maneno mzee kuna kila sababu za kuamini kuwa Jaka anaweza kuwa na taarifa nyeti zinazoweza kutusaidia kwenye kulifikia shina la biashara hii haramu hapa nchini.”
Mzee Januari Mwakaja aliduwaa.
“Kwa hiyo…?” Aliuliza tena, akili ikimzunguka, kile alichokuwa kikihisi kuhusu Jaka kikijidhihirisha katika zile taarifa alizokuwa anapokea wakati ule.
“Nimepewa kibali maalum cha kumtumia Jaka Brown Madega kwa namna yoyote ile nitakayoona inafaa katika kutekeleza uchunguzi wa tume niliyokuelezea,ili kuhakikisha kuwa tume inatimiza kazi iliyotumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.” Bijhajha alimalizia na kutulia.
Kwa mara nyingine Januari Mwakaja alilazimika kuwasha taa ya ndani ya gari ile na kusoma karatasi aliyokabidhiwa na yule mtu ambaye kitambulisho chake cha kazi kilimtambulisha kama Jeff Bijhajha. Ile karatasi ilikuwa inatoa kibali kwa Jeff Bijhajha kumtumia Jaka Brown Madega katika kutekeleza majukumu aliyokabidhiwa na tume ya siri ya kuchunguza uhusikaji wa maafisa wa polisi na viongozi wa juu serikalini katika uendeshaji wa biashara ya madawa ya kulevya nchini.
Kile kibali kilikuwa kina nembo ya rais na kusainiwa na waziri wa mambo ya ndani kwa niaba ya rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Januari Mwakaja alijikuta akipiga mbinja kwa mshangao na kustajaabia jambo lile.
“ Dduh! Imetoka moja kwa moja Ikulu hii!” Alisema kwa mastaajabu.
Jeff Bijhajha hakujibu. Aliichukua ile karatasi na kuihifadhi kwenye mfuko wa ndani wa koti lake refu.
“Kwa hiyo unadhani kuwa Jaka anaweza kuwa na msaada kwako?”
“Tukio la leo asubuhi pale sokoni linazidi kunihakikishia hivyo.”
“Kwa hiyo, wewe ndiye uliyekuwa ukimfuatilia nyendo zake yule kijana?” Mwakaja aliuliza, na kabla Bijhajha hajajibu, akaendelea, “Sasa kwa nini ulimtwanga mangumi kule uwanja wa sabasaba siku kadhaa huko nyuma?”
Badala ya kumjibu, Jeff akacheka kidogo, kasha akwamwambia, “Tuachane na hayo. Nadhani sasa umeshaelewa kuwa siko hapa kwa ubaya dhidi yake. Sasa, Mi’ nitahitaji kwenda Dar kwa siku mbili kabla ya kuja kuongea rasmi na Jaka. Katika siku mbili hizo, nakuomba sana mzee uhakikishe kuwa Jaka anaendelea kuishi hadi hapo nitakaporudi. Baada ya hapo atakuwa chini yangu.”
Alifungua mlango, akateremka na kuanza kutokomea kizani.
“ Hey! Jeff!” Januari Mwakaja alimwita, na Jeff akarudi na kuchungulia dirishani.
“Unasemaje?”
“Sasa tutaonana vipi tena? Huu utaratibu wa leo si mzuri bwana…”
“Nikikuhitaji nitakupata tu mzee…si unaona nilivyokupata leo?”
“Hii sio namna nzuri ya kukutana…”
“Lakini ndio salama zaidi…”
Akatoweka.
Januari Mwakaja alitia gari moto na kuondoka eneo lile huku akiwa na mawazo tele kichwani.
Siku iliyofuata, Clara alisafiri “kikazi” kuelekea Dar es Salaam kwa gari la kampuni. Dereva aliyekuwa akimuendesha na wafanyakazi wengine wote pale ofisini kwao, walijua kuwa ile ilikuwa ni moja kati ya safari zake nyingi za kikazi kuelekea Dar es Saalaam. Kama jinsi ambavyo wale askari waliowekewa kuwalinda pale nyumbani kwao walivyoelewa.
Ni wao pekee ndio walioijua dhima ya safari ile.

___________________

Akiwa ofisini kwake siku ile Jaka alikuwa akifanya kazi huku akili yake ikiwa kwa Clara tu aliyekuwa safarini wakati ule. Alikuwa na wahka mkubwa wa kujua iwapo atafanikiwa kuipata ile simu yake na iwapo ile simu itakuwa na ufumbuzi walioutarajia. Mawazo haya yalikuwa yakimjia na kuondoka huku akijitahidi kufanya zile kazi kadiri alivyoweza.
Hatimaye akili yake ikazama moja kwa moja kwenye zile kazi na kusahau kuhusu safari ya Clara kwa muda. Mlango wa ofisini kwake ulifunguliwa taratibu na kufungwa tena, naye akiwa na uhakika kuwa aliyefungua mlango ule alikuwa ni mhudumu wa ofisi akileta barua za kikazi au vocha za malipo ya madereva wa ile kampuni ya usafirishaji, aliendelea kushughulika na kazi zake kwa muda kabla hajainua uso wake kumsikiliza.
La Haula!
Moyo ulimlipuka na hapo hapo ukaanza kumwenda mbio huku akili ikikataa kabisa kuamini alichokuwa akikiona mbele ya uso wake.
Mbele yake mle ndani walikuwa wamesimama watu wawili ambao aliamini kuwa hatowaona tena maishani mwake.
Don Sibazosi, ambaye yeye alimtambua kama “mzee wa matabasamu”, alikuwa amesimama katikati ya ofisi ile hali akiwa amemuelekezea bastola ambayo alishawahi kuiona mikononi mwa muuaji yule hapo awali. Llama Automatic ilikuwa imemuelekea moja kwa moja usoni. Nyuma ya yule mtu mwenye tabasamu la kutisha kabisa alilopata kuliona, Puzo Vurumai, ambaye yeye alikuwa akimtambua kama “Claus Kinski” mwenye sura yenye alama za ndui, alikuwa amesimama akiwa ameegemea ukuta kando ya mlango hali mikono yake ikiwa imezama kwenye mifuko ya koti la suti nyeusi aliyovaa huku akimtazama kwa macho makali.
Jaka alibaki mdomo wazi.
Wale jamaa walikuwa amevalia suti ghali sana zilizowafanya waonekane kama aidha ni wafanyabiashara wenye mafanikio au ni maafisa wa maana sana kiasi kwamba Jaka hakuwalaumu walinzi waliowaruhusu kupita hadi pale ofisini kwake. Wakati Puzo alikuwa amepiga suti kali nyeusi, Don Sibazosi alikuwa amevaa suti safi sana ya kijivu iliyomkaa vyema sana.
Don Sibazosi alikuwa akimsogelea pale mezani huku akimlengeshea ile bastola iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti hali mdomo wake ukiwa umefanya tabasamu na wakati huo huo macho yake yakionesha chuki ya hali ya juu.
Heh!
“Unadhani unaweza kuwakimbia Don Sibazosi na Puzo Vurumai halafu uishi kwa raha mstarehe hapa duniani Jaka?” Don Sibazosi alimuuliza, na ndio kwa mara ya kwanza Jaka alipoyasikia majina ya wale wauaji, ingawa kwa pale alipokuwa hakuwa na namna ya kujua yupi ni yupi kati yao. Alibaki ameduwaa.

Weekend njema Chiefs
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom