AFRIKA YANGU—3
MTUNZI: HASSAN MBONECHE.
Yalishapita masaa mawili na dakika kadhaa, toka Ndinaa apitiwe na usingizi baada ya kitambo cha robo saa kilichomfanya aangushe kilio pale alipokaa. Kilio kwa ajili ya mama yake ambaye muda huo aliamini hayupo tena duniani.
Alikuja kuzinduka baada ya kusikia sauti mfululizo ya ukohozi na purkushani za hatua. Hatua zilizokuwa zinaelekea usawa ule aliopo. Hakusita kuwa mwenye hofu kwa muda, huku akisikilizia kwa makini mienendo ya hatua hizo, ambazo alifahamu fika, wasababishao hatua hizo ni watu.
Umakini aliouumba ukampa jibu kwa kuvuta mazungumzo ya wahusika.
“Huyu mbwa aombe tusimpate. Tukimpata, atajuta kwa nini alizaliwa mwanamke,” ilisikika sauti yenye ngurumo kidogo.
“Najaribu kuvuta picha namna nitakavyombambia,” sauti ya mtu mwingine ikachangia hoja.
Kikusidiwacho kikamvumbua. Kuwa aongelewaye hapo ni yeye na hao ni wale wavamizi wa kijijini kwao.
“Oooh! Ee Mola nisaidie mja wako,” Ndinaa alisema akijiinua pale alipoketi.
Alivyoinuka, alisikilizia kwa mara nyingine mienendo ya zile hatua, zilizidi kumsogelea. Kitendo kilichompa hadhari akiwa mzembe anaweza kufikiwa na kuwafanya wabaya wake wafurahie ushindi wa mezani.
Hakuta hilo.
Hivyo alianza kwa kuihakiki bahasha kama ipo mahali alipoihifadhi. Alipojihakikishia ipo, alipiga hatua ndogo ndogo zenye uharaka huku akipambanua namna atakavyokuwa huru dhidi ya mabaradhuli hao.
Alivyoona mwendo huo unamkawiza, alianza kukimbia. Lakini hakufika mbali, pale alipojikwaa kwenye kisiki na kutoa ukunga wa nguvu kutokana na anguko na maumivu aliyoyapata. Hamu ya kusonga mbele ikamwisha. Akaketi chini kwa muda kutathmini namna atakavyoyapunguza maumivu.
Pindi yeye anachukua majukumu ya kujiganga ili aendelee na safari, ule ukunga aliopiga na mshindo wa anguko uliwabainisha maadui kuwa lindo lao halipo mbali.
“Amepita huku,” kiongozi wa lile kundi alisema, huku akionyesha kwa mkono uelekeo wanaopaswa kuuchukua.
Lilikuwa kundi la watu wanne.
Pindi kundi la maharamia likiongoza kasi, Ndinaa alikuwa amemaliza kufuta damu kwa majani ya mti kisha kurudi upya kwenye mwendo. Awamu hii kasi ilipungua. Hakuwa na uwezo tena wa kukimbia kwa ustadi, badala yake alifanya mbio kwa mchechemeo.
Hata hivyo hazikumridhisha. Akaketi chini kwa mara nyingine na kuwazua afanyaje asiweze kufikiwa. Wakati anawazua mboni zake zililala kwenye kidole gumba cha mguu wa kuume. Kilikuwa kinavuja damu.
“Nisipoidhibiti hii damu haiwezi kukata,” Ndinaa alijisemeza, huku akiifuta futa ile damu inayozidi kutiririka kwa kijiti.
Alihisi kupatikana.
Ghafla, alikuwa kama mtu aliyepigwa shoti ya umeme, alivyoingiwa na wazo jipya akilini na kulitekeleza. Alichana sehemu ndogo ya khanga aliyovaa akajifunga pale kidoleni.
Kidogo, akahisi atapata ahueni katika utembeaji.
Alitumia takribani dakika tatu kuhitimisha zoezi hilo. Baada ya hapo ndipo alirudi kwa mara nyingine mwendoni kukimbia mawindo ya adui, ambayo yalikuwa zaidi ya hatari.
Kama alivyohisi awali, awamu hii ahueni ilikuwepo. Ijapokuwa kasi haikufanana na ile pindi yu'mzima wa afya.
***
Ndinaa alifanikiwa kuifikia barabara kuu ielekeayo Ruyigi, na kujichanganya kwenye halaiki ya watu wenye rika mbalimbali waliokuwa wameyakimbia makazi yao kwenda kutafuta sehemu ya kuishi.
Machafuko yaliyoshika kasi, familia yao ikiwa chanzo ilimfanya awaonee huruma wale wengine. Hasa wenye watoto wadogo, ambao muda huo walipaswa kuwa shule.
“Eeh, Mola, tupe mioyo yenye uvumilivu na subira kukipita kipindi hiki salama,” Ndinaa alijisemeza, akijitahidi kukatiza awe mbele zaidi.
Utulivu wa mioyo ya wanaburundi kwa wakati huo ulikuwa chini yake. Akabidhishe bahasha kwa mkusudiwa aliyoambiwa. Jambo ambalo kwa upande wake lilikuwa ngumu, kwa sababu hamfahamu huyo mtu. Kwani hakuwahi kubahatika kumuona japo kwa siku moja.
Zilipita dakika tano, toka Ndinaa ajichanganye kwenye ile halaiki vijana wamfukuzao nao walijichanganya. Walikuwa ni vijana wa makamo, wasiozidi hata umri wa miaka ishirini na miwili.
Asilimia kubwa wote walikuwa wembamba wenye vimo vya kati. Huku makoti makubwa yaliyoshuka hadi magotini yakizuia silaha; bunduki aina ya AK 47 waliyokata sehemu ya kitako ili iwe fupi na kufichika kwa urahisi. Pasi na kusahau mapanga waliyoyasundika kiunoni.
Ijapokuwa kiza kilishika hatamu wale vijana walikaza mboni zao juu juu kumwangalia Ndinaa. Lakini isivyo bahati, mboni zote nane, zilizokazwa kama watafuta shilingi ya malipo ya ada, hawakufua dafu.
“Tuhakikishe tunampata huyu kinyaragosi,” mmoja wa wale vijana, ambaye ndiye kiongozi alisema. Sauti ikiwa imesheheni ghadhibiko.
“Na atakuwa yuko humu humu,” kijana mwingine alikazia.
“Sasa sikilizeni...” yule kijana wa mwanzo alisema na kutulia kwa muda. Alivyojihakikishia wenzake wamevaa umakini kumsikiliza, aliendelea, “Tusitembee pamoja namna hii. Tujigawe; wengine waelekee mbele, na wengine tusalie uwanda huu huu.”
Kiongozi wao alivyohitimisha utekelezaji ulifuatia. Hakuna aliyepinga. Wawili kati yao walielekea mbele, waliobakia walisalia usawa uleule. Na kwa kutaka kufanya kazi yao kwa urahisi zaidi, yule kiongozi alipiga risasi kadhaa hewani na kuzua mshindo wenye taharuki iliyowafanya watu wakimbie ovyo ovyo.
Utulivu wa safari ukakosekana.
Kwani ile kimbia kimbia ilitengeneza utengano uliowasaidia wale vijana kufanya uchunguzi wao kwa urahisi. Kuendeleza urahisi, walichomoa tochi walipozisundika na kuziwasha.
Lahaula!
Ule mwanga pale ulipotua ulikuwa kwa mtu wamkusudiaye.
“Yule pale,” mmoja wa kijana aliyopo mbele alimtaarifu mwenzake.
Kweli, alikuwa Ndinaa.
Akapiga mbinja kuwajulisha waliopo nyuma kuwa windo lao limeshaonekana.
Wenzao walipowafikia waliunga nyuma yake huku wakiendelea kummulika asiwapotee. Lakini kitendo hicho kilimpa ishara fulani Ndinaa ya kumtaarifu yu'matatizoni zaidi, baada ya kuona ile miali haiendi sehemu nyingine tofauti na pale alipo.
Hatua ya kwanza aliyojiamini inaweza kuwa ya uokozi ni kuongeza mwendo. Akafanya hivyo. Akaongeza mwendo, na wale vijana pia waliongeza mwendo.
“Anataka kukimbia huyu mjinga,” kijana mdogo kuliko wote aliwavumbua wenzake. Nao kuafiki, baada ya kumuona Ndinaa akijitahidi kujipenyeza katikati ya kundi la wa-mama waliobeba vifurushi kichwani.
Ilikuwa anataka kumalizia mguu wake wa kulia apotelee kwenye lile kundi la wa-mama, pale kiongozi wa kundi la wale vijana alipochomoa bunduki yake na kutupa mitupo ya risasi kadhaa mwilini mwa Ndinaa.
Zilitua risasi mbili mwilini mwake, na kumtupa umbali wa mitaa kadhaa, huku akiharibu kwa mara nyingine utulivu wa safari. Kwani sio mlio wa risasi, wala mshindo wa anguko, ulioweza kuwazuia wasaka makazi purkushanini kwa mara nyingine.
Haraka sana, yule aliyepiga risasi baada ya kumaliza aliirejesha bunduki mahali alipokuwa ameihifadhi na kuwahimiza wenzake wakimbie wakamuangalie mtu wao. Cha kushangaza, walipofika eneo ambalo Ndinaa walimuona ameangukia hakukuwa na mtu.
Wakapigwa na butwaa.
Butwaa lililowashinikiza waanze kwa mara nyingine zoezi la kukodoa mboni zao kumtafuta. Walipatwa na hisio, baada ya lile anguko aliinuka na kujivuta vuta.
Walivyoangaza kwa makini walibaini mbururo walioutilia shaka. Wakaamua kuufuatilia, kwa kupiga hatua za wastani huku mwanga wa tochi ukiwaongoza. Hawakufika umbali mrefu, ule mburuzo ulikata na hawakufanikiwa kumuona Ndinaa.
“Inawezekanaje?” kiongozi wa lile kundi la vijana aliuliza, sauti ikiwa imesheheni mkoromo ulioonyesha kiwango cha chuki alichonacho.
Alichukia, kama ilivyo desturi ya wakosa mawindo.
***
Askofu Ponera ndivyo anavyofahamika na wengi. Lakini hilo sio jina halisi alilopatiwa na wazazi wake baada ya uzao. Jina alilopatiwa na wazazi ni John Chiwa. Isivyo bahati, jina hili lilipotea ghafla, pale alipoanza shule ya msingi. Kwa shinikizo kutoka serikalini, wazazi walilazimika kubadili jina masikioni mwa jamii na kupatiwa Ponera. Ilikuwa ni sehemu ya kazi kutoka kitengo nyeti serikalini.
Akiwa Ponera, hujulikana kama Askofu. Ilhali akiwa John Chiwa, hujulikana Luteni Kanali wa jeshi la wananchi Tanzania. Sifa moja wapo ilikuwa ya kutengenezwa na idara, kama walivyomtengenezea jina siku za nyuma.
Utawazwa wa kuwa Askofu ulitengenezwa na idara ya usalama wa Taifa baada ya kufukuzwa jeshi kwa geresha akiwa na cheo cha PTE (Private). Akatengenezewa nafasi mbalimbali za uongozi wa dini ndani ya dhehebu, mwisho akasimikwa rasmi kuwa Askofu Dayosisi ya Mtwara.
“Chiwa, hizi nafasi utazitumikia zote. Lakini moja ni kama kiremba kwa ajili ya kuficha nafasi nyingine,” ilikuwa kauli ya m-baba mmoja mwenye mvi nyingi ndani ya ofisi kubwa akiteta na Chiwa mara baada ya kuhitimu kidato cha sita.
“Utaenda jeshini. Na utakuwa Askofu. Lakini kazi yako kuu ni...” yule m-baba aliendelea kusema. Kabla hajahitimisha Chiwa akamkatisha.
“Spy.”
“Sahihi. Tunahitaji uwe jasusi tegemezi ndani ya taifa letu.”
“Sasa huoni kuwa upande wa dini utanizuia kufanya matendo hatarishi ya kijasusi?”
“Tunahitaji uwe kiongozi wa dini ili ukatulize mihemko ya waumini dhidi ya serikali pale watakapochochewa na watu hatarishi kwa taifa letu. Kama vile wanasiasa.”
Hivyo ndivyo ilikuwa.
Jasusi kuwa na kofia ya u-Askofu.
***
Luteni Bazombanza aliufungua mlango kwa uwazi, Koplo Rumera akiwa pembeni yake. Hakuwa na shaka yoyote kwamba anaweza kuwepo mtu ndani, hasa baada ya mhusika wa nyumba kutowepo duniani. Kabla hawajapiga hatua kuingia, Koplo Rumera aliwasha tochi na kufanya wajionee vyema mazingira ya mle chumbani.
Vumbi, lililoshika hatamu likawashinikiza wapige chafya. Huku mwanga wa tochi ukiwabainishia dama za buti sakafuni.
“Kuna mtu aliingia humu ndani,” alijisemeza Luteni Bazombanza. “Atakuwa nani?” akafuatia kujitupia ulizo. Wakati huo hofu ikimchonyota na hadhari ikimkwiva.
Vivyo hivyo kwa Koplo Rumera.
“Hili ni tatizo lingine. Tulikuwa tumekaa kwa kujiachia sana kwamba hakuna anayefuatilia nyendo zetu. Sasa huyu aliyeingia sio wa kumbeza,” Koplo Rumera alitoa wazo.
Hadhari ilivyokuwa komavu ndipo waliingia mle chumbani. Waliingia wakiwa wenye machale, kwani waliielekeza tochi huku na kule kwa uchunguzi. Wakati huo huo, wakiwezesha kurekodi video kupitia ile tochi. Kwani ilikuwa tochi ya kijasusi.
Juu ya kuangaza pande zote mle ndani lakini hawakumuona mtu. Wakahisi, yumkini ameshatoka. Au, mhusika wa zile dama hakuingia siku ile.
Wakarejea kwenye zoezi lililowaleta, upekuzi.
Kwa uharaka, wenye umakini wastani, walipekua kila pande ya chumba hicho. Hawakuacha kitu chochote ambacho waliamini kinahusika kwenye uhifadhi. Lakini juu ya jitihada zote hizo, hawakupata wala kuona kitakachowafutia hatua zao, au kufahamu mienendo ya Mugaza ndani ya Tanzania.
Muda wote huo Askofu Ponera alikuwa juu ya dari ameyatega masikio vyema asipitwe na neno. Hakujali hali ya huko, hasa joto, lililomshinikiza muda mwingine atamani kupata japo hewa, lakini ilishindikana. Kwani kupata habari kutoka kwa hao watu lilikuwa jambo la muhimu zaidi. Aliamini itamwezesha kusogea hatua nyingine zaidi katika misheni yake.
Juu ya muda wote waliotumia Luteni Bazombanza na Koplo Rumera kwenye lile zoezi hawakuambulia chochote. Mwisho, walighadhibika. Ghadhibiko lililowaamuru kusitisha na kuchukua maamuzi ya kuondoka.
Ilikuwa pindi wanaondoka, pale Luteni Bazombanza alipositisha hatua baada ya kuona kitu mbele yake.
“Kuna tatizo?” Koplo Rumera aliuliza.
Luteni Bazombanza badala ya kujibu, alichutuma na kukiokota kile kitu. Alivyoinuka, alianza kukisaili. Lilikuwa kacha livaliwalo mkononi. Kacha lililotungwa kwa shanga na kurembwa kwa berenda ya Tanzania.
“Limeingiaje humu ndani?” Luteni Bazombanza alijiuliza. Koplo Rumera akalisikia swali hilo kutokana na sauti iliyomtoka Luteni Bazombanza. Sauti ya wastani.
“Yumkini ndiyo mhusika wa hizi hatua,” Koplo Rumera alijibu.
“Nami nina wasiwasi huohuo.”
“Tunaweza kulitumia kumpata mhusika?”
“Mmmmh! Yeah, lakini tulifikishe kwanza mikononi mwa wakuu, yawezekana watakuwa na wazo bora zaidi yetu.”
“Hamna shida.”
Wakaondoka.
***
Yalikuwa makutano ya dharura usiku ule baina ya Wilhelmina, Kinigi na wale makamanda wa kijeshi wakiongozwa na Brigedia Jenerali Buyoya. Makutano yao yalichagizwa na hali waliyoikuta kina Luteni Bazombanza na Koplo Rumera kule nyumbani kwa hayati Jenerali Ndiyashena.
Makutano yao yalifanyika kwenye nyumba ya ghorofa moja katikati ya mtaa wa Buyenzi.
Kabla mazungumzo hayajaanza walipata nafasi ya kupitia video zilizorekodiwa, mara baada ya hapo ndipo utetaji ulianza. Utetaji uliojaa hasira kwa sababu ya ukosefu wa mafanikio.
“Nimeingiwa na mashaka dhidi ya hili jambo” Wilhelmina alisema.
“Tena ni makubwa sana,” Brigedia Jenerali Buyoya aliingilia kati. “Hii inatoa picha kwamba hatupo peke yetu. Kuna mtu, au watu wanaotafuta ukweli wa yanayojiri,” Brigedia Jenerali Buyoya alikazia.
“Hisio lenu la kwanza mnalipeleka wapi?” Wilhelmina aliuliza.
Kilipita kitambo kidogo cha ukimya kabla swali hili halijajibiwa. Kitambo kilichotoa picha makamanda wapo kwenye zoezi la ufikiriaji. Meja Uwizeye ndiye alikuja kuufukuza.
“Tanzania.”
“Why Tanzania? Kwani haiwezekani mtu wa hapa Burundi kuvaa kacha la taifa lingine?” Wilhelmina aliuliza kwa mara nyingine.
“Hakuna mzalendo wa kweli avaaye kacha la taifa lingine badala ya taifa lake,” Meja Uwizeye aliweka wazi jibu lake.
Brigedia Jenerali Buyoya akaingilia kati, “Ulichozungumza Uwizeye kipo sahihi. Huyu aliyetumwa kufuatilia hii ishu hawezi kuwa raia tu wa kawaida. Ni lazima awe mtu aliyepitia majeshini. Kama amepitia majeshini, mimi ndiye Kamanda wa operesheni ndani ya jeshi letu, hakuna operesheni yoyote iliyoanzishwa kuhusu hii mambo.
“Ingelianzishwa, ningelikuwa na taarifa. Hivyo basi...” Brigedia Jenerali akaachwa kauli yake ikielea baada ya kukatishwa na Wilhelmina.
“Ni lazima vyombo kama polisi na usalama wa Taifa wafanyapo operesheni zao wewe ufahamu?”
Brigedia Jenerali Buyoya akajibu, “Kimsingi ni hivyo. Kwani inasaidia uchangiaji wa mawazo katika ufanikishaji.”
“Kwa hiyo, Tanzania ni nani hadi aingilie mambo ya Taifa lenu?” Wilhelmina aliuliza, sauti ikibeba hali ya chukizo, wakati huo huo akimsaili mmoja baada ya mwingine.
Waulizwa walishindwa kulijibu hili swali. Kitendo kilichozalisha ukimya kwa sekunde kadhaa kabla Wilhelmina hajauondoa.
“Buyoya, wewe ni kamanda wa kijeshi, unafahamu miiko ya mtu wa majeshi kuingia nchi nyingine pasi na kibali,” akatulia kwa muda na kumsaili Brigedia Jenerali Buyoya apokeavyo kauli yake. “Fanya jitihada usiku na mchana kumsaka huyo aliyejiingiza kufuatilia nyendo.
“Fanya jambo, ukweli uzidi kubaki kwetu. Fanyeni jambo tusije kuhaibika. Na fanyeni jambo kuwaonyesha Tanzania si lolote, si chochote. Tumeelewana?”
“Hiyo ni sehemu ya kiapo chetu kwenye hii misheni,” Brigedia Jenerali Buyoya alijibu kikakamavu.
TUKUTANE TOLEO LIJALO