Kilikuwa kijiwe chenye hekaheka sana cha mchezo wa drafti. Sio asubuhi, sio usiku, mahali hapo palikuwa hapabanduki watu. Huduma ya uuzaji wa kahawa na alkasusu kutoka kwa kijana mmoja mwenye rika kati ya miaka ishirini hadi ishirini na tatu ilinogesha kijiwe, ukiachilia mbali runinga ndogo yenye ukubwa wa inchi ishirini na moja aliyoifunga usawa wa mbele.
Kijiwe chake kilikuwa kibanda cha miti kilichopauliwa kwa makuti. Fomu kadhaa za mbao alizopigilia chini zikitumika kama vikalio. Jirani naye kulikuwa na mama n’tilie, halafu upande mwingine duka la jumla na rejareja la nafaka.
Kijiwe hicho kilikuwa eneo la mji wa Mwanga, hatua kadhaa kutoka barabara kuu. Upande wa pili na kituo cha mabasi. Jioni moja ya saa kumi na moja siku ya jumatano, kijiwe kilikuwa na watu watatu; wateja wawili, na muuzaji mwenyewe. Muuzaji alikuwa jikoni akihangaika kuchemsha mahitaji yake, wateja wamemakinika na mchezo wa drafti, pembeni yao kukiwa na bilauri za alkasusu.
“Huu mchezo ndugu hutoki. Hata kama unasema ukitoka kutumia mchicha mwiba unakuwa mkali wa mambo, lakini kwa huu, sahau!” Kijana mmoja wapo alitoa tambo zake kwa bashasha, uso ameliinamia lile drafti.
“Tutaona,” yule kijana mwingine alijibu huku akitafakari kuichagua kete ya kucheza.
Alipoipata alicheza. Ikawa zamu ya yule kijana aliyejigamba. Lakini kabla hajacheza, aliinua kichwa akachukua bilauri la alkasusu, akapiga funda mbili.
“Jamaa yako huyo, anakuja,” yule kijana wa majigambo alimnong’oneza mwenzie baada ya kumwona kijana fulani akija kule walipo mara baada ya kutua ile bilauri.
“Nani?” Mwenzie aliuliza kwa sauti ya wastani.
“Mzee wa kuparua.”
Yule kijana aliyetambiwa akageuka nyumaye kumwona huyo anayoelezewa, kisha alirejea mchezoni.
“Ndugu vipi?” Yule kijana aliyewasili aliwasalimia alipoingia mle bandani huku akiongoza kwenda jikoni.
“Tuko poa mwanangu. Niaje?” Alijibu yule kijana wa majigambo. Hakuacha kumwangalia yule kijana aliyeingia. Alisitisha hata kucheza.
“Oya, cheza basi,” mwenzie alimshitua.
“Tulia kwanza.” Kijana wa majigambo alimtuliza mwenzake. “oya, Mayunga ee!” Akamwita yule kijana aliyeingia.
Kijana aliyeingia akageuka na kuwaangalia wale vijana wawili.
“Oya, kashata mwanangu. Tufanyie mpango tupate hata kashata mbilimbili,” kijana wa majigambo alisema. Alikuwa mrefu, mwembamba, maji ya kunde.
“Sina hela mwanangu,” kijana aliyeingia, afahamikaye kwa jina la Mayunga alisema.
“Aaah, kaka, tufanyie. Tajiri kama wewe unakosaje?” Kijana wa majigambo alisema. Cheko la wastani lililoacha uso na tabasamu lilisindikiza kauli yake.
“Nina utajiri gani ndugu yangu?” Mayunga naye alijibu tabasamu la mshangao likipamba wajihi wake.
“Mwanangu we si mzee wa road. Kila siku upo road, unakosaje. Stori zako zimeenea kinoma kitaa.”
“Kwambaje?”
“Kwambaje!” Kijana wa majigambo alishangaa.
“Eeeh!”
“Hiyo shughuli unayoifanya sio siri tena. Watu wengi pale maeneo wanafahamu kuwa wewe ni paruwanja mbobevu.”
“Naona unaamua kunitusi, ndugu.” Mayunga akamgeukia muuzaji kuendelea na kilichomleta mahali pale.
“Kaka, tugawane wote hizo laana za wananchi.”
“Aisee, tuheshimiane basi,” Mayunga alichukia.
“Kwani hapa nakuvunjia heshima? Si ninakueleza yanayokuhusu. Kwani ukinipa mimi buku za huko barabarani si utakuwa umevunja mwiko wa viapo vya wananchi.”
“Nawe nenda kafanye hiyo kazi. Sio unaongea ongea utumbo. Umeshawahi kunikuta nikiparua?” Mayunga alizidi kuongea kwa kuchukia.
“Mkaushie basi, mwanangu,” yule kijana mwingine anayecheza drafti na yule kijana wa majigambo alimsihi mwenzie kwa sauti ya wastani.
“Acha woga. Kwani kuna ubaya gani hapo niliyomwambia?”
Mayunga akaondoka kule jikoni uso umefura. Alipofika usawa waliopo vijana wale wacheza drafti, akasimama. Akamwangalia kwa hasira yule aliyekuwa anazungumza naye.
“Sikia mwanangu, mimi na wewe tumekutana tu kazini. Hivyo acha shobo na mimi. Usinizoee kwa namna yoyote ile,” Mayunga alisema, bado akiwa mwenye hasira.
Hakusubiri jibu, akaanza kuondoka.
Akiwa jirani aliache lile banda, kijana wa majigambo akaongea, “Sema kuwa makini mwanangu. Maneno ya wananchi ni mabaya sana. Hiyo kazi sio nzuri. Ukiiendekeza itakuja kukuharibia kibarua chako.”
Mayunga hakujibu. Aliendelea na mwendo.
KAA TAYARI...