Riwaya: Mkoloni Mzawa

Riwaya: Mkoloni Mzawa

MNYONGA TAI—08
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
MAWASILIANO: 0673056571

Mjimile na wale askari waliwasilishwa jijini Dar es salaam kwa haraka sana. Fadhy aliwapokea. Akaenda kuwahifadhi kwenye moja ya majengo ya siri yaliyopo chini ya kitengo chake maeneo ya Mbweni. Safe house, ndivyo zilivyotambulishwa kwa urahisi.

Kila mmoja alihifadhiwa chumba chake. Na kwa mazingira yalivyo ulikosekana upenyo wa kuwashinikiza washirikiane kwa jambo lolote lile. Walikuwa zaidi ya wafungwa. Ijapokuwa waliwekewa maji ya kunywa ya chupa nyenye ujazo wa nusu lita, na kasha moja la biskuti.

“Huo ndiyo mlo wenu kwa siku zote mtakazokuwa humu. Ukimaliza kabla ya wakati, utajua mwenyewe utakakopata chakula,” Fadhy aliwaasa kwa wema. Ili wawe na matumizi mazuri ya vile vitu.

Zilipita siku tatu, pasi na kutokea mtu yeyote kwenye lile jengo walilohifadhiwa. Siku ya nne, ndipo Fadhy alipotembelea, tena kwa lengo la kumhoji mtu mmoja tu. Wakati huo, wengi wao walishamaliza vile vitu walivyopatiwa kwa ajili ya kuchangamsha tumbo. Hivyo njaa ikawa inawasumbua mbaya.

Wa kwanza kuhojiwa alikuwa Mjimile. Alitolewa chumbani kwake, akapelekwa kwenye ukumbi husika.

“Tajiri,” Fadhy aliita. Mjimile akamtumbilia mboni kali.

“Pole kwa matatizo. Lakini ukiuhitaji uhuru wako ni wewe tu, namna tutakavyoshirikiana katika hili. Upo tayari?”

Mjimile hakujibu.

“Kama haupo tayari sema, niamuru urudishwe chumbani kwako.”

Badala ya kujibu kwa kauli, Mjimile alionyesha ishara. Ya uhitaji wa chakula. Fadhy akamsaili. Mjimile akaonyesha ile ishara kwa mara nyingine kwa msisitizo zaidi.

“Upo tayari kwa ushirikiano?”

Mjimile akatingisha kichwa; juu-chini. Ishara ya kuridhia.

Kwa msisito huo, Fadhy aliondoka mle ofisini na kurejea baada ya dakika kadhaa. Alibeba kibakuli kilicho na chakula, akamkabidhi Mjimile. Kutokana na njaa, Mjimile alikifakamia kile chakula na kumaliza ndani ya muda mfupi sana. Akapewa na maji kishuke vyema.

“Upo sawa?”

“Ndiyo,” Mjimile alijibu.

“Sihitaji uongofu katika hili.” Akamtumbulia mboni kali za usaili. Mjimile hakujibu.

“Okay, unawafahamu hawa?” Fadhy akamsogezea picha mnato ziwaonyeshazo Cheyaya na Kasembe.

Mjimile alishtuka kidogo alivyozibaini. Mshituko uliobainika na Fadhy.

“Unawafahamuje hao?”

“Ni wafanyabiashara wenzangu.”

“Zaidi ya hivyo?”

Mjimile hakujibu kwa uharaka. Jambo lililotengeneza ukimya kwa muda, karibu na kushika hatamu, Fadhy akaufukuza, “Unafahamu sababu ya matatizo wapitiayo hivi sasa?”

“Aaah, sina ukaribu nao kiasi hicho. Hivyo ni ngumu...”

Fadhy akadakia, “Lakini unashirikiana na wasababishi wa tatizo.”

Mjimile izara ikamjaa.

“Nilikutahadharisha mwanzo, sihitaji uongofu. Au nitumie nguvu ya ziada?” akavuta saraka, akatoa mjeledi, bisibisi na nyundo.

Mjimile akabaki kumstaajabu.

“Nakuuliza kwa mara ya mwisho kabla hivi vitu havijagusa mwilini mwako. Nini sababu ya hao wafanyabiashara kupitia matatizo waliyonayo?”

Kwa hofu ya mwili wake kupata maumivu, Mjimile ikambidi afunguke anachokifahamu. “Nalimuka ndiyo sababu,” alisema na kutulia. Sauti ikiwa nyongefu. Hofu ikimtukuta nafsini. Anasaliti wenzie. “Nalimuka anahitaji hela za wale watu.”

“Kwa nini anahitaji hela zao? Na kwa nini anatumia mgongo wa serikali kufanya kitu kama hicho?”

“Ndiyo njia rahisi ya kujihalalishia. Hata ungelikuwa wewe ungelifanya hivyo. Wanyonga tai wote wana kawaida hiyo.”

“Okay, nitakurudia siku nyingine kwa mahojiano zaidi.” Fadhy akainuka.

“Kwa hiyo narudishwa kwenye kilekile chumba?” akamtumbulia mboni za huruma.

“Utapelekwa sehemu nyingine.” Akaondoka.

Siku zilizofuatia aliwahoji wale askari. Mbinu ya kuwashindisha njaa ilimsaidia sana, akapata ushirikiano mzuri uliompa mwangaza baada ya kuunganisha doti. Alijihakikishia kile alichotaarifiwa hapo awali.

Awamu zote za mahojiano, alikuwa na tepurekoda iliyomsaidia kuhifadhi yale mazungumzo.

“Na vipi kama Nalimuka anatekeleza haya kwa amri ya Rais? Na hata kama ni amri yake, kwa nini iwe kwa uonevu?” Fadhy alijiuliza, baada ya kuyatafakari kwa kina mahojiano ya watu wote. Alikuwa amesimama hatua chache kutoka dirishani ndani ya ofisi yake akiyasaili mandhari ya jiji.

Akili ilivyoduwazwa na mwonekano wa jiji kwa usawa aliouchukulia umakini, wazo jipya likamwingia. Nini anapaswa kufanya kwa wakati huo.

“Meneja mamlaka ya mapato Mtwara,” alijisemeza. “Yeah, huyu mtu anahitajika upenuni mwangu,” alijihakikishia kwa utingishaji wa kichwa.

***

Baada ya mafikirio ya muda wa dakika kadhaa Jovin alikata shauri na hatimaye kumruhusu Stella kuingia ndani. Yeye ndiyo alitangulia, alipofika usawa alipoiacha bunduki, aliisukumizia uvunguni mwa sofa kwa mguu pasi na Stella kuona.

“Tumekuwa adimu kwa hizi siku kadhaa, tunashindwa kutafutana,” Jovin alisema, pindi wakichukua mkao sofani.

“Nilisafiri kidogo. Si unajua hili tatizo lililomkumba mzee linahitaji mihangaiko?”

“Ulienda na mama?”

“Ndiyo.”

“Wapi?”

“Mmmh! Kwenye miji ya watu. Huko mbelembele.”

Jovin akavuta pumzi na kuzitua kwa nguvu. Alionekana kuguswa, kana kwamba ndiyo mtendewa. Stella akampimia tu.

“Kwa hiyo mama bado yupo huko?”

“Ndiyo, anaendelea kushughulikia mambo yakae sawa.”

Mtiririko huu wa maswali ulimhakikishia Stella, Jovin sio mtu mzuri katika ustawi wa familia yao.

Mwito wa simu ya Jovin ndiyo ilisitisha kwa muda mazungumzo yao. Alimsaili mpigaji kwa sekunde chache kisha aliipokea. Ilikuwa simu kutoka kwa Nalimuka.

“Jiandae kwa ugeni wangu.” Ikakatwa pasi na Jovin kujibu ameridhia kwa mapokeo ama lah.

Akaiondoa kwa unyonge sikioni.

“Kuna tatizo?” Stella aliuliza, muda wote hakubandukua mboni zake kumsaili Jovin.

“Hapana.”

“Sasa mbona umebadilika ghafla?”

“Amenichanganya tu huyu niliyewasiliana naye pasi na kunipatia wasaa wa kuchangia mazungumzo.” Ikambidi aongope. Maana kilichomtatiza ni namna gani watazungumza na Nalimuka Stella akiwepo mazingira yale. Ilimtatizisha.

“Sasa si umpigie ili mwelewane?” Stella akamwondoa mawazoni.

“Haina salio.”

“Chukua hii.” Stella akatoa simu yake, akamkabidhi.

Pindi Jovin yu'mbioni kuiopokea, sauti ya kugongwa mlango ishara ya hodi ikasikika. Akasitisha uchukuaji simu, akaenda kufungua mlango. Akakumbana na Nalimuka.

“Nimetoka...” Nalimuka alisema, mwili ukiwa umefura, lakini kabla hajahitimisha kauli yake akaoneshwa ishara fulani ya kuzibwa mdomo-ina maana asiendelee kuzungumza na Jovin.

Jovin akamnong'oneza, “Mazingira ya ndani sio mazuri, twende tukaongelee huku hivi.” Akamsukumiza kidogo Nalimuka, kisha alimwaga Stella, “Dakika tano kipenzi.” Akatoka nje, akafuatia kufunga mlango.

“Kuna nini ndani?” Nalimuka uvumilivu ulimshinda.

“Nipo na mtoto wa Cheyaya mle ndani. Yule bintiye.”

Nalimuka akasitisha mwendo na kumgeukia Jovin. “Amefuata nini?” aliuliza.

“Mambo ya wanaume. Na ni sehemu ya chanzo cha taarifa katika ufanikishaji wa mambo yangu.”

“Asije kuwa naye anakufanyia ushushushu?”

“Hajabaini hilo.”

Wakarejelea mwendo.

Walipoweka tuo hapakuwa mbali sana na nyumba. Wakafungua uwanja wa mazungumzo kwa mara nyingine. Awamu hii, ilikuwa kwa unong'ozi.

“Nimekutana na Cheyaya leo tukafukuzana kama mbwa. Sijui wapi amenichenga yule mjinga, tulikuwa tunamaliza kazi kabisa.”

“Acha bhana!” Jovin alistaajabu.

“Ndiyo hivyo. Ilinibidi nifanye. Tambua siku zimesalia chache za Waziri Mkuu kuwasili halafu yule mjinga bado anadunda. Hiyo inanipa mashaka sana. Inanifanya nikose amani.”

“Ukiwa hivyo unaweza kuharibu mpango mzima. Ulinikabidhi kazi, ya nini uingiwe mashaka wakati siku tuliyoahidiana bado haijawadia?”

“Ndugu. Akijificha, kama alivyofanya siku zilizopita unadhani tutampatia wapi?”

“Haijalishi. Ni lazima tu, alambe mchanga.”

“Utafanyaje fanyaje?”

Jovin alikaa kimya kwa muda akifikiri jambo, alivyoridhishwa na alilolipata, aliliweka wazi, “Nitachoma moto nyumba yao. Kama atakuwa papa hapa mjini, atatokeza tu katika mazingira hayo. Hapo ndipo nitakapomfumua.”

“Basi na iwe hivyo,” Nalimuka aliafikiana naye.

Kitu pekee ambacho hawakukifahamu, Stella alikuwa jirani nao na alifanikiwa kunyaka kwa ufasaha mipango hiyo. Ilimbidi tu ajikaze, lakini hali iliyomkumba haikuwa ya kawaida. Mapigo ya moyo yalimbadilika mara kwa mara na kumfanya azidi kuwa mwenye hasira dhidi ya Jovin.

Hasira hizo zilipelekea ashindwe hata kupata ufafanuzi sahihi kumhusu Jovin. Amkamatishe muda huohuo? Au ajipe subira?

Akabaki kugugumia.

***

Cheyaya aliwasili kwa mwenyeji wake akiwa mwenye mihemo juujuu. Hakusita kumhadithia mwenzie mkasa mzima, mara baada ya hapo walimalizia ngwe ya kasi iliyosalia na kufuatia usakaji wa usingizi.

Sauti ya mwito ya mwenyeji wake aliyetoka mazoezini asubuhi hiyo ndiyo ilimwamsha Cheyaya. Alilala usingizi mzito hasa, kutokana na uchovu wa mabio aliyoyafanya.

“Nimechoka sana. Maana jinsi ninayoisikia hiyo miguu, sitamani hata kutoka hapa kitandani,” Cheyaya alisema, huku akiamka.

“Kuna taarifa mbaya.” Cheyaya akapotezea hali ajisikiayo na kushawishika asikie hicho chenye ubaya. “Nyumba yako inaungua moto muda huu,” mwenyeji alizidi kumpasha.

Moyo ulipiga kite kwa mshituko. Kile alichokisikia kilishindwa kujituliza, hivyo kilifukunyua kila sehemu iliyohusika na chimbuko la furaha.

“Ina ukweli hiyo taarifa?” Cheyaya aliuliza, akiwa ameshainuka. Akili haikutuliana kabisa.

“Hakika.”

Cheyaya alianza kwa kuguna, kisha akatingisha kichwa kuonyesha masikitiko yake, “Yaani.” Akaguna tena. “Mbona matatizo hayaniishi?”

“Mungu ndiyo anajua.”

“Nataka nikaisaidie familia yangu iweze kuokokana na hili. Sipati picha namna wanavyoteseka huko,” Cheyaya alisema, akiwa ameshaanza kuvaa tayari kwa kuondoka.

“Huisi...” kabla mwenye nyumba hajamaliza kauli yake, Cheyaya alikwishaanza mwendo. Naye akaona isiwe tabu, akaungana naye.

***

Stella naye asubuhi hiyo alikuwa kwenye mizunguko iliyomshinikiza aifikie nyumba yao. Kile alichokisikia kutoka kwa Jovin hakikubanduka akilini. Alikesha kukijengea picha jinsi kitakavyotokea. Alivyohitimisha, machozi yalishatengeneza njia mashavuni.

Alivyokaribia nyumbani kwao, akaanza kuushuhudia moshi angani. Akaingiwa mashaka; Jovin ameshatekeleza kile alichokiahidi, ama lah. Moyo ukabaki njia panda, huku akijitahidi kuomba kile akionacho kisitokee nyumbani kwao.

Akajitengenezea hali ya ukosefu wa amani nafsini.

Nusuru adondoke, pale aliposhuhudia nyumba yao ndiyo iteketeayo. Kabla hajajua afanye nini, aliduwaa kwa muda na kuruhusu kumbukizi ya maongezi ya kina Jovin.

“Ina maana amefanya kweli!” Stella alijisemeza chozi likimtiririka. Wakati huo mpwito wa mapigo ya moyo si ya kawaida. “Kweli anataka kwenda kumuua baba'ngu?” Kumbukizi ya baba'ke kuhitajika kuuwawa katika tukio hilo likamwondolea mduwao na kutimua mbio. Alikimbia mboni zikihangaika huku na kule kusaili halaiki iliyopo.

Wakati huo Jovin alikuwa kwenye paa ya moja ya nyumba, umbali wa mita kadhaa akikazana kuwasaili watu waliopo katika lile tukio kupitia darubini iliyofungwa juu ya bunduki. Azma ampate Cheyaya.

Hangaiko hilo lilichukua dakika chache tu, akafanikiwa kumwona Cheyaya akiwa mbio kuifikia nyumba yake. Ndiyo alikuwa anawasili kutoka mafichoni na yule mwenyeji wake. Zilisalia takribani mita kumi na saba, Cheyaya ajiunge na halaiki iliyokuja kushuhudia na kutoa msaada pia, Jovin akafanikiwa kumweka kilengeoni kwa usahihi. Tena shabaha ilisoma pajini.

Mungu ampe nini.

Jovin akabana pumzi. Akajihakikishia mkito wa bunduki kwenye nyama ya bega, kisha akakisereresha kidole cha shahada taratibu kuelekea kilipo kifyatulio. Hakukawiza, akaruhusu mtupo wa risasi.

Kitendo cha kushangaza, kilengeoni akasomeka Stella.

***

Askofu Ponera ndiyo alikuwa wa kwanza kufikwa na taarifa ya lile tukio kupitia vijiweni. Hakuwa mroho, aliwataarifu wenzie, kisha na Fadhy pia. Fadhy alipatiwa kwa njia ya video call wakiwa kwenye makazi yao waliyofikia-Meswaki.

“Hilo tukio linahusiana na tatizo tunalokumbana nalo?” Fadhy aliuliza.

“Haina uhakika chifu.”

“Awali, hili tukio nilihisi halitofikia ukubwa huu.”
“Tupe mwongozo sasa.”

“Uhitaji wa taarifa bado ni mkubwa sana. Askofu lishughulikie hilo. Wakati Luteni Ringo na wenzio, kuna kazi ya kufanya Mtwara mjini.”

“Ipi?”

“Namhitaji Meneja mamlaka ya mapato mkoa.”

“Sawa chifu.”

Maongezi yakahitimika.

Fadhy naye hakuwa mchoyo, aliwafikishia ile taarifa kina Dorice. Kwa sababu ya wepesi wa uhimilivu, wakaangua vilio na kumpa Fadhy zoezi la kuwatuliza. Walitulia walipojisikia wenyewe, baada ya kuamini wameondoa kiasi fulani cha uchungu.

“Tumtaarifu Stella?” Dorice aliuliza.

“Aaah, sio vibaya naye akafahamu. Ukizingatia hatujapata uthibitisho wa moja kwa moja kuwa hili la moto linahusiana na kadhia ya waume zenu katika biashara zao.”

Dorice akapiga simu. Isivyo bahati, hakupatikana hewani.

“Sio kesi, unaweza kumweleza hata baadaye,” Fadhy akamtuliza. Maana kichwa kilishaanza kupata moto na alikwishaanza kulengwa na machozi.

“Shem, toka nifahamu Stella anamiliki simu, sijawahi kimsikia akilalamikia bahari za kuisha chaji.”

“Sasa...,” Fadhy alidakia. Kabla hajahitimisha akapata simu kutoka kwa Askofu Ponera. Hakuchelea kuipokea.

“Ndiyo,” Fadhy alisema.

“Imeshabainika nani amepigwa risasi.”

“Nani?” Fadhy aliuliza kwa shauku.

“Mtoto wa Cheyaya.”

Moyo ukapiga kite kwa mshituko. Wajihi ukambadilika, kiasi cha kuwashtua kina Dorice na kuwajaza hamu wafahamishwe apatiwacho.

“Ina ukweli wowote?” Fadhy aliuliza na kutulia kwa sekunde kadhaa. Bado alikuwa anaichakata ile taarifa. “Nikiwa na maana umeifanyia utafiti ukajihakikishia.”

“Pasi na shaka. Sambamba na hilo, mkusudiwa wetu mbaroni. Cheyaya amekamatwa na askari polisi. Alikuwa hapa hospitalini.”

Fadhy akazidi kunyong'onyea.

“Kuna jambo lolote ninaloweza kufanya kwa idhini yako?” Askofu Ponera akamzindua.

“Askofu, hii vita sio ya kuichukulia poa. Kama wapinzani wetu wanafanya vitendo vya kikatili zaidi ili wafanikishe walifikirialo, basi tuna kazi nzito sana.” Fadhy akainuka, na kupiga hatua ndogondogo akipotelea ushorobani.

Akawaacha kina Dorice mzuka umewapanda.

Fadhy akaendelea, “Nafikiria nini tufanye ili tuwashinde kwa haraka. Maana hiki walichozidi kukifanya hakivumiliki.”

“Kwa hiyo tuwaache tu wakiondoka na huyu?”

“Stella. Tafuta taarifa za kina kumhusu Stella. Nini matokeo ya risasi aliyopigwa.”

“Sawa chifu.”

“Fanya hima ujitahidi.” Fadhy akakata simu. Akarejea sebuleni.

“Kuna tatizo?” Dorice kimuhemuhe akafanya kazi yake. Hakumpooza.

“Halihusiani na hili tunalolishughulikia,” Fadhy akawaongopea.

“Mmh! Shem...”

“Kuna jambo lingine tu linalohusiana na majukumu ya kazi yangu. Kukiwa na utofauti wa hili letu siwezi kuwanyima taarifa zake. Kuweni na amani.”

“Unanifanya nianze kukuogopa. Kwani sura yako inaficha kilichopo moyoni ambacho umetoka kutaarifiwa.”

Wakati wote wa maongezi Fadhy alikuwa amesimama. Baadaye ikambidi ajibweteke sofani, kisha kuwasaili ma-shemeji zake tuo kwa tuo, huku akijipa fikra, aanzaje kuwataarifu ile taarifa ya Stella kupigwa risasi na Cheyaya kukamatwa?

Alichokuwa anakikwepa, ni kuona wanawake hao wanaondoka jijini na kurudi Mangaka. Aliamini, kwa namna yoyote ile, akiwaambia watakuwa na uhitaji huo. Jambo litakalochangia ugumu wa ufanikishaji wa kuwaweka hatiani washukiwa wao.

“Sasa umeamini kuwa lipo unalotuficha?” Dorice akamgutusha.

“Kwa nini umekuwa hivyo shem?”

“Nina uchungu namna uhuru wetu unavyozidi kupotea kila uchao pasi na kosa lolote tulilolifanya. Jitihada zote za upambanaji tulizozifanya hadi kuutwaa ubilionea leo hii tumegeuka wahujumu uchumi kwa sababu tumekataa matakwa yao.

“Nina uchungu na huu uonevu unaozidi kuendelea shem. Kwa nini tunaonewa? Wanatuoneaje? Wanatuoneaje hawa?” alilalama hadi machozi yakaanza kumlenga. Uvumilivu ulipomshinda kilio kikawa nafuu yake.

“Ni lini hao tunaowaamini wataacha uonevu? Wataendelea kuongoza kwa kudhulumu? Au ndiyo miiko ya uongozi inavyotaka eeh?” Dorice aliendelea kulalama.

“Ndiyo maana nimechukua maamuzi ya kushughulikia ili kufutilia mbali dhana hii iliyokita mizizi kila nyanja. Nitaitokomeza, na kujenga nidhamu kwa watumishi wengine. Kupitia hili, litakuwa fundisho kwao,” Fadhy alimtuliza.

Dorice akafuta machozi, kisha akamsaili Fadhy.

“Nakuhakikishia tena, niaminini. Tunaenda kushinda huu mchezo,” alimsisitizia.

TUKUTANE TOLEO LIJALO.
 
MNYONGA TAI—09
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
MAWASILIANO: 0673056571

Alistaajabu kuona vitu vimetua kwa nguvu mezani asubuhi hiyo ofisini kwake. Kabla hajavisaili kuvifahamu, akamsaili mrushaji. Alikuwa Dorice, akiambatana na Pendo. Wajihi umefura kama mtu mwenye fangasi ya mdomo aliyelishwa pilipili. Baadaye alisaili kile kilichorushwa-gazeti.

Alienda mbali zaidi kwa kusoma vichwa vya habari-kimoja baada ya kingine. Kabla hajahitimisha, akasitishwa na ulizo kutoka kwa Dorice.

“Hiki ndicho ulitaarifiwa ukatuficha siyo?” lilikuwa ulizo lililoambatana na hasira kali, kiasi cha kutiririkwa na machozi. Machungu aliyokuwa nayo si ya kawaida.

Fadhy badala ya kujibu, alirejea kumsaili Dorice baadaye Pendo. Akajisikia mwenye fadhaa, alipokumbuka namna alivyowaongopea.

“Sasa unajisikiaje kwa kutuficha?” Dorice aliuliza kwa mara nyingine.

Awamu hii Fadhy akagandisha mboni zake kwenye moja ya kichwa cha habari picha ielezeayo Cheyaya amekamtwa na jeshi la polisi. Akafuatia kuvuta pumzi na kuzitua kwa nguvu.

Alipoinua awasaili wageni wake, Dorice akamwongoza Pendo wajiondoe mahali hapo. Tena waliondoka kwa mwendo wanguwangu, ijapokuwa Pendo alionekana kufuata mkumbo. Aliburuzwa buruzwa tu. Hakuwa na maamuzi yaliyonyooka kama yake binafsi.

Kwa namna walivyoondoka Fadhy akaumba jambo akilini. Kwamba hakuna wema baina yao. Hivyo hata hamu ya kuendeleza uwepo wake ofisini ikatamatika hapo. Aliondoka kuwafuata.

Alipowasili nyumbani, aliteremka garini kwa haraka na kukimbilia ndani. Hata hakuhakiki usawia wa uegeshaji wa gari. Alivyonuia kufungua mlango ili aingie ndani, mlango ukafunguliwa kutoka ndani. Akakumbana na kina Dorice wakikokota mabegi.

“Safari ya wapi?” Fadhy aliuliza, akiwa amesimama pale mlangoni kwa nia ya kuwazuia.

Swali hili halikujibiwa kwa haraka. Na kufanya ukimya uchukue nafasi kwa muda, kabla Fadhy hajaendeleza kujichukulia hatamu. “Ilinibidi nifanye vile, nipate kutuliza nyoyo zenu. Kwani sio hilo tu lililojitokeza, lipo lingine.”

Dorice na Pendo wakamkodolea mboni kali zilizoashiria kutaka kujua zaidi.

Fadhy aliendelea kuwaeleza, “Kama mtakumba nilikwishawahi kuwaambia, kuna mengi yatakayojitokeza. Haya ni miongoni mwa hayo mengi. Kikubwa ni uvumilivu na imani.”

“Hilo lingine ni lipi?” Dorice alishindwa kuvumilia.

Fadhy aliwasaili kwanza ndipo alijibu, “Stella.”

“Amefanyaje?” haraka ya ufahamu ikawajaa wote kwa pamoja.

“Alishambuliwa kwa risasi kwenye lile tukio la moto.”

Dorice akahamaki. Pendo akazidi kuwa mwenye staajabiko.

“Kwa sasa yupo hospitalini, anapatiwa matibabu,” Fadhy alizidi kuwadadavulia.

Dorice akaangua kilio.

Lakini kwa jitihada zao wakafanikiwa kumtuliza.

“Shem,” Fadhy aliita, Dorice alipotulia. Awamu hii walijibweteka sofani-sebuleni.

“Sijui nifanyaje niwaokoe. Naumia sana shem. Nini wema wa jitihada zao kwa jamii yetu?” Dorice alilalama.

“Shem, hatuhitaji uharaka katika ushindi wa hili. Hatupaswi kuwa na haraka kwa sababu aliyopo nyuma ya mipango ni mtu mzito serikalini.”

“Kwa hiyo tuache nduguzo wakiumia? Wacha sisi tukawasaidie.”

“Nilitaka mbaki hapa kwa lengo la kuondoa mazingira ya kuwalazimisha waume zenu kupitia ninyi. Sio salama, wanaweza wakawateka. Hata hivyo, timu yangu bado ipo macho kwa mapambano.”

“Mpaka lini? Mimi nadhani unafurahia nduguzo wanavyozidi kusota.”

“Hapana. Tukifanya kwa papara, tutashindwa kupata vidhibiti sahihi vya kuwaweka hatiani.”

“Kwa hiyo tuvumilie mpaka lini?” Dorice alipaniki.

Fadhy hakujibu. Aliishia kuwatazama huku akifikiria awapatie ahadi gani itakayowaaminisha kufikia siku hiyo kila kitu kitakuwa sawa.

***

Cheyaya aliwasilishwa mahabusu ileile aliyohifadhiwa Kasembe. Gereza la Lilungu. Lililopo umbali wa takribani kilomita tatu kutoka katikati ya mji. Mapokeo ya mazingira yakampa unyonge. Unyonge huo ulianzia akilini hadi viungoni pia.

Akahifadhiwa kwenye moja ya chumba. Kwa mtazamo tu wa haraka akabaini ni chumba cha mateso. Alipofungwa kitini, hisia zikamthibitishia.

Kweli.

Kwani dakika kadhaa baadaye waliingia maafisa wawili wa magereza mle alipohifadhiwa. Maafisa walio na maumbo ya unene wastani, warefu, rangi iliyopamba ngozi ni nyeusi.

Wakasimama mbele ya meza wakiangaliana na Cheyaya. Ambaye jasho lilimtoka chapachapa kutokana na mazingira ya mle chumbani. Hakikuruhusu kuingiza mwanga wa kutosha. Madirisha yalikuwa madogo na yalijengwa karibu na paa.

“Tajiri karibu mahali salama,” mmoja wa wale askari alisema kwa dhihaka. Wakati huo akichukua rungu pale mezani. Alivyolikamatia vyema, akaanza kumsondoa sondoa Cheyaya kwa kumsukumiza kichwani.

“Tajiri jeuri,” yule askari mwingine alidakia. “Mwamba, asiyetaka kutii, kwa kujiona bingwa pekee hapa nchini.” Akachukua rungu na kujipigiza pigiza kwenye moja ya kiganja. Wakati huo akimzunguka Cheyaya.

Cheyaya hakuwa na la kushirikiana nao, zaidi ya kuiandaa akili na mwili kwa masubirio ya wanachotaka kukifanya. Na haikuchukua muda, yule wa kwanza kumsemesha akalitua kwa nguvu lile rungu tumboni kwake. Akagugumia kwa maumivu, huku akijaribu kulirudisha tumbo kwa ndani-kupooza.

“Upo tayari kushirikiana na serikali yako kuanzia sasa hivi?” yule aliyekuwa anamzukunga aliuliza.

“Hujasikia ulichoulizwa wewe?” Rungu likatua shingoni.

Kabla umivu la pigo hilo halijapoa, akapokea pigo lingine lililotua shavuni. Mara zote hizo, alijikaza kusikilizia maumivu, yalipomshinda, akaanza kuangua kilio. Udume haukufua dafu kwa nguvu walizotumia zile njemba.

Na wala hawakuguswa kwa kilio chake. Ndiyo kwanza waliendeleza kichapo, tena kwa mtungo. Maswali hayakusahaulika, kumuuliza kama yu'radhi kupunguza misimamo yake aendane na itakiwayo na yule aliyewatuma. Nalimuka.

Baada ya mvua ya kipigo cha muda mrefu kilichowaridhisha wale watesi. Cheyaya akiwa hoi bin taabani kwa kutojiweza kwa lolote, walimfungua pale kitini wakamkokota kokota hadi chumba alichohifadhiwa Kasembe.

“Hakuna mpigania haki aliyefanikiwa. Mkijitia wajuaji mtazidi kuozea humu ndani, acheni upumbavu,” mmoja wa wale askari alisema pindi wakiondoka. Kasembe akabaki kustaajabia alichotendewa mwenzie. Sio staajabiko tu, alizidi kuingiwa na hasira dhidi ya mhusika mkuu wa yale yote.

“Pole sana kaka. Haya yana mwisho, yataisha tu,” Kasembe alimtuliza.

“E... Da...p, endapo nitakufa naku...mba usikate tamaa,” Cheyaya alisema kwa kitetemeshi. “Endelea kupambana hadi tone la mwisho kuhakikisha haki yetu inapatikana.”

“Hapana kaka. Hili pambano ni letu sote.”

“Siuoni unafuu wa kuendelea kuwa hai, Kasembe. Hali yangu ni mbaya sana.” Akacheua damu mezani. “Usiwasamehe. Vilevile hakikisha unaipatia ulinzi familia yangu.”

“Nooo!” Kasembe aliunguruma akiwa ameinuka. “We are champ all the time. Hapaswi kusema hivyo kaka. Haijalishi tutapitia magumu mangapi, ipo siku moja, siku moja tutafikia tukitakacho na kuondokana na kadhia hii. Jasho letu sio la dhambi. Lile sio jasho la dhambi, Cheyaya, hivyo tusi...”

Akakatishwa na ufunguzi wa mlango. Taratibu akainua kichwa kumwangalia aliyefungua. Waliingia watu watatu ambao alimfahamu mmoja tu kati yao. Nalimuka. Waliingia kwa hatua za madaha, zilizomchukulia muda na umakini kuwafuatilia.

Walipowafikia walipo wakaweka tuo. Walivuta viti wakaketi. Nao mboni zao zikikesha kuwasaili Kasembe na Cheyaya. Wakasailiana. Ijapokuwa kwa Kasembe alijaa chuki. Vivyo hivyo Cheyaya, kwa mwono wa tabu alionao.

Walioongozana na Nalimuka walikuwa; meneja mamlaka ya mapato Mtwara na Mkurugenzi wa mashtaka ya jinai. Mkurugenzi akatupia faili mezani kisha kulifunua.

“Tumekuja kwa makubaliano, baina yenu nasi tuwakilishao serikali. Sehemu yetu tumeshaijaza, iliyosalia ni yenu.” Nalimuka akaweka kalamu juu ya karatasi ionekayo ndani ya faili.

Kasembe akawaangalia kwa unyali akiwa vilevile alivyosimama. Hakukielewa kile anachotaarifiwa.

“Hili ni kwa uhuru wenu,” Mkurugenzi mashtaka ya jinai alidakia. “Mtailipa serikali kiasi kadhaa cha fedha ili mambo yakae sawa. Nikiwa na maana muurejee uhuru wenu.”

Kasembe akaketi kitini, na kuzidi kuwasaili. Cheyaya pia.

“Lakini kama mtaleta ukaidi, hatutoona dhambi kutaifisha mali zenu,” Meneja mamlaka ya mapato alichangia.

“You dammit, umesahau nilikuambia nini mara ya mwisho?” Kasembe alifoka na kumwinamia Nalimuka. Alimwelekezea kichwa kama ugomvi wa kondoo. Kifua kikipwita pwita kwa hasira.

“Oooh, unataka malumbano? Sisi tumekuja kwa wema. Lakini kama unahitaji hivyo hatuna budi kuwatendea. Si unaona hali aliyonayo mwenzio?”

Kasembe akajirudisha.

“Mko tayari kwa tulichowataarifu?” Mkurugenzi alihoji.

“Ondokeni. Ondokeni mbele yetu,” Kasembe alikoroma na kugonga mbeza kwa nguvu.

Cheyaya akadakia, “Na usifanye lolote Kasembe. Wasikutishe kwa lolote hao mbwa.”

“Hatujaja hapa kuwabembeleza.” Nalimuka akainuka, akapiga hatua taratibu hadi nyuma ya alipoketi Kasembe.

Sekunde mbili mbali, akamkamata mikono yake huku Mkurugenzi mashtaka ya jinai akimshikiza kalamu. Kasembe akaleta ngumu, kwa kujitingisha tingisha ili kupoteza lengo. Ukatokea msuguano mkali uliotulizwa na Meneja mamlaka ya mapato kwa kumlamba makofi kadhaa.

Kabla hajapoa, akavutwa dole gumba na kuchovywa kwenye kikopo cha rangi kisha kugandamiziwa pale karatasini. Akaachiwa, lakini sio bure, mtupo wa ngumi kutoka kwa Nalimuka ukampata shingoni na kumyumbisha hadi chini.

Hawakuhangaika naye, wakahamishia majeshi kwa Cheyaya. Kwake hawakupata shida, walitumia nguvu ndogo sana kwa sababu hakuwa na uhimili wa kupimana ubavu.

“Sasa tutaongea lugha moja,” Nalimuka alisema kwa bashasha pindi akichukua nafasi ya kuketi. “But kuna sharti lazima niwapatie ili tuende sawa.” Akawasaili.

Kasembe alikwishajiinua na kuwatolea jicho zongo. Hakutaka kuwasogelea walipo, lakini viwambo vilikuwa makini kunasa kizungumziwacho.

“Mtafunga mabakuli yenu,” Nalimuka aliendelea kuwaamuru. “Mkiwa wakaidi, mtaona matokeo yake, maana sisi ndiyo wenye mamlaka wenyewe.”

“Na hiki kilichofanyika leo ni njia ya ninyi kurudi uraiani. Mkakae kwa kutulia huko,” Mkurugenzi mashtaka ya jinai alichangia hoja.

“Yeah, mtatoka. Lakini kwa sababu ya kibri na usumbufu wenu nitachukua vitu vyenu vyote vya thamani mlivyokuwa mnavimiliki.” Nalimuka akainuka. Wenzie pia. Wakapiga hatua ndogondogo kuondoka mle chumbani kwa madaha. Kwa nini wanyongeke wakati wameshinda?

Maumivu yaliibuka kwa Kasembe na Cheyaya. Waliumia kwa jitihada zao kuangukia pua.

Wakati wa kuliacha eneo la gereza, Nalimuka aliambatana na Jovin, wakati meneja wa mamlaka ya mapato na Mkurugenzi mashtaka ya jinai kila mmoja alikuwa na uelekeo wake. Ikiwa na maana walikuwa na usafiri tofauti.

“Tumefanikisha tulichokifuata, ijapokuwa sio katika mazingira ya makubaliano,” Nalimuka alimtaarifu Jovin. Wakiutafuta uelekeo wa Mtwara mjini. Jovin ndiyo aliketi nyuma ya usukani.

“Lini?”

“Siku yoyote.”

“Kwa hiyo kazi ya…”

Nalimuka akadakia, “Kazi yako iko palepale. Tena awamu hii ni wote wawili- kwani sitaki wawe vinong'ona. Isitoshe nataka nimiliki vyote vyenye thamani wanavyovimiliki-hadi wanawake wao.”

Jovin akatabasamu. “Gharama…”

“Usiwaze kuhusu hilo,” akamkatisha tena. “Ewe ni mkono wangu wa kuume, hivyo siwezi kukutupa.”

Jovin akazidi kukanyaga mafuta kuutafuta mji. Akilini, akiumba namna ya ufanikishaji wa vifo vya Kasembe na Cheyaya kwa pamoja.

“Watatoka kabla ya mkutano wa Waziri Mkuu?” Jovin alihoji mara baada ya kuhitimisha uumbaji wa tukio.

“Nitakuwa mjinga nikifanya hivyo. Watatoka siku kadhaa mbele kutoka ile ya mkutano wa Waziri Mkuu.”

“Siku watakayotoka ndiyo siku ya kifo chao.”

“Hiyo ni ngwe yako, siwezi kuiingilia.”

***

Gari walilopanda Luteni Ringo, Pte Bayo na Pte Pemba, Volvo xc90 lilikuwa mita kadhaa nyuma kutoka gari alilopo Meneja mamlaka ya mapato mkoani Mtwara. Hawakuwa na mwendo mkali. Ulikuwa wa wastani, wasishtukiwe. Ukomo wa safari ukawa hoteli ya Tiffany Diamond. Kwani ndipo alipoingia yule Meneja. Luteni Ringo akateremka, akapotelea ndani ya hoteli. Aliishia mapokezi.

“Habari binti?” alimsabahi binti aliyemkuta.

“Salama. Karibu kwa kukusaidia.”

“Naitwa Natenda, mfanyabiashara kutoka Tandahimba, nina shida na Meneja wa mamlaka ya mapato. Nimetaarifiwa makazi yake yapo hapa.”

Na kweli, meneja wa mamlaka ya mapato pale ndipo yalikuwa makazi yake. Kwani toka ateuliwe kushika wadhifa huo ni wiki mbili tu zimepita. Mtangulizi wake hajamaliza kuhamisha vyombo vyake kwenye nyumba anayopaswa kuishi.

“Naomba dakika moja, nitarudi kwako kwa mrejesho,” binti alijibu kikarimu hasa, akaondoka na kuweka tuo umbali wa mita nne kutoka ilipo meza ya kaunta. Hapo akahangaika na simu ya mezani.

Kama alivyoahidi, kabla dakika haijatamatika yule mhudumu alimrejea Luteni Ringo. “Amesema msubiri.”

Luteni Ringo akachukua mapumziko kwenye sofa zilizopo kwa masubirio.

Haikuchukua muda mrefu meneja kuwasili. Luteni Ringo akamwonyesha ishara fulani na kumfanya afuatwe alipoketi. Kwani tofauti naye, walikuwepo watu wengine.

Kwa bashasha, Luteni Ringo akajitambulisha-kwa utambulisho ule ongofu aliompatia mhudumu.

“Nipo na wenzangu wawili hapo nje, ukipendezwa, nakuomba tuongozane tukatete. Ama la, niwaite, kisha utuongoze sehemu nzuri tunayoweza kuteta kwa uhuru,” Luteni Ringo alisema. Sauti ikishamiri unyenyekevu ulio na woga. Kama walivyo wafanyabiashara mbele ya afisa wa mamlaka ya mapato nchini.

“Twende walipo wenzio,” meneja alishauri.

Pasi na kuchelea, Luteni Ringo akaongoza safari hadi eneo la maegesho.

Walipoifikia gari, Pte Bayo aliteremka na kumsukumizia meneja ndani ya gari. Kilikuwa kitendo kilichochukua sekunde chache sana, kuja kutahamaki, meneja akatazamana na bastola.

“Kwa usalama wako, tunahitaji kufanya upekuzi chumbani kwako,” Luteni Ringo alimwamuru. Awamu hii ile hofu ya ufanyabiashara ilishatoweka.

“Ninyi ni kina nani?”

“Wasamaria wema, tunaohakikisha haki ya mtu haidhulumiwi.”

“Kwa hiyo…”

Akakatishwa na Pte Pemba kwa kofi la nguvu lililotua shavu la kushoto, “Acha kuuliza maswali yasiyo na msingi. Unatupotezea muda. Au tupekeche hizi bastola mbavuni mwako?”

Ladha ya maumivu aliyoisikia hapo, ikamfahamisha waliopo mbele yake hawana matani.

“Sawa, nipo tayari.” Meneja akaafikiana nao.

“Sasa usitoe ishara ya aina yoyote ile. Nakusisitizia, aina yoyote ile kwa mtu, yenye kuashiria upo matatizoni,” Luteni Ringo alimwasa.

Meneja mamlaka ya mapato akatingisha kichwa kukubaliana naye. Wajihi ulijaa hofu tele.

Hawakupoteza muda, walimteremsha wakaongozana; meneja mbele, Luteni Ringo nyuma, kushoto mwa meneja Pte Bayo. Pte Pemba alisalia garini. Kwa mwendo usiotia shaka, walikata hatua kupotelea ndani.

Walipofika chumba husika, walimwamuru afungue kila sehemu waliyoamini hawawezi kuifikia pasi na kufanya hivyo. Naye alitii. Baada ya hapo walimfunga pingu miguuni na mikononi, pasi na kusahau kumbandika utepe mdomoni ili asiwaletee bughuza itakayofichua dhamira yao. Wakamketisha kwenye moja ya kona, kisha wakafanya upekuzi makini.

Ndani ya dakika nne, walipekua kila sehemu mle chumbani lakini hawakupata chochote chenye manufaa. Wakamzoa zoa tena mtu wao akiwa huru, wakarudi naye garini.

“Safari maalumu,” Luteni Ringo aliamuru. Kauli iliyoeleweka kwa haraka kwa Pte Pemba uelekeo wa safari wanaopaswa kwenda. Aliungurumisha gari, wakajiondoa taratibu.

“Mnanipeleka wapi?” meneja mamlaka ya mapato aliuliza.

“Utakapoenda kuungama dhambi zako.”

Meneja akapigwa na butwaa. Hakuelewa. Kiasi cha kuwatumbulia jicho kali kwa zamu.

“Dhambi unayoshiriki, ya kudhulumu jasho la wenye jitihada zao ndiyo inayokupeleka usikokujua,” Luteni Ringo ikambidi amweleshe.

***

Saa tisa alasiri, meneja mamlaka ya mapato mkoani Mtwara-aitwaye Chuma Nyumba alikuwa mbele ya Fadhy kwenye ukumbi wa kikao wakitenganishwa na meza. Kila kitu kwake alikiona cha ajabu, hasa kwa kuwekwa kizuizini na watu asiowafahamu.

“Bw. Chuma, nataka nikuondolee staajabiko lako, naitwa afisa haki,” Fadhy alijitambulisha huku akimsaili.

“Mna shida gani na mimi?”

Badala ya kujibu, Fadhy alivuta saraka akatoa faili na kumsukumizia Chuma. Akalifunua. Akakumbana na picha za Cheyaya na Kasembe.

“Nadhani sasa utakuwa umeelewa kwa nini naitwa afisa haki?”

Chuma akamsaili Fadhy kwa tuo, kisha akamjibu, “Bado.”

“Usitake yawe mahojiano ya kutumia nguvu kubwa, nielezee kwa undani, dhuluma wanayoenda kufanyiwa hao wafanyabiashara.”

Matumizi ya nguvu yakamtetemesha kwa kiasi fulani Chuma. Ukizingatia alipopelekwa hakuna mtu wa karibu anayefahamu, akashawishika kueleza ukweli wa alichoulizwa.

“Nilipelekwa kwenye ule mkoa kwa kazi hiyo mahsusi. Mhe. Waziri anahitaji fedha zao kwa gharama yoyote ile.”

Fadhy akamkatisha, “Kiasi gani?”

“Bilioni moja.”

“Nawe…”

“Natii maelekezo ya mkubwa wangu, sina namna.”

“Hiyo pesa itatolewa vipi hadi imfikie?”

“Tayari leo wamelazimishwa kujaza fomu ya makubaliano. Na muda huu, Mkurugenzi mashtaka ya jinai atakuwa ofisi ya meneja wa benki ya wananchi tawi la Mtwara mjini akikamilisha taratibu za muamala.”

Fadhy akapigwa na butwaa. Mapigo ya moyo yakamwenda kasi na kumpotezea umakini kwa muda. Aliwazua namna ya kusitisha zoezi hilo.

“Ukweli ndiyo huo,” Chuma alisisitizia maelezo yake. “Kama mna mpango wa kuwasaidia, mumeshachelewa.”

TUKUTANE TOLEO LIJALO.
 
MNYONGA TAI—10
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
MAWASILIANO: 0673056571

Wasia wa Fadhy kwa kina Dorice ulikuwa kazi bure. Hisia za kuondoka ziliwatekenya haswa na mwishowe kuzifuata. Walifunga safari ya kurejea Mangaka pasi na kumtaarifu mwenyeji wao. Kwanza waanzaje kumtaarifu wakati ni utorokaji?

Lengo la uondokaji huo waliona jitihada za Fadhy zitachukua muda mrefu ilhali mahasimu wanazidi kudunda. Wakapanga wakakiwakilishe kile kilichodhamiriwa na waume zao mkutanoni kwa Waziri Mkuu, kwa sababu siku zilishakaribia. Waliamini huo ndiyo utakuwa msaada utakaowapigisha hatua ya mafanikio kwa haraka kuliko hatua mnyato zifanywazo na Fadhy.

Walipowasili Mangaka walifikia nyumbani kwa Pendo. Kwa sababu mazingira hayakuwa vyema, waliyasafisha, baada ya hapo walifunga safari kuelekea hospitalini-wakamwangalie Stella. Hiki nacho ndicho kiliwatekenyesha wajawe na kimuhemuhe cha kuelekea Mangaka. Kutoka nyumbani kwa kina Pendo hadi hospitali, iliyopo mtaa wa Saiti ni mwendo wa dakika chache tu, hivyo hawakutumia muda mrefu kuifikia.

Kwa sababu ulikuwa muda mahsusi kuwaangalia wagonjwa, waliongoza moja kwa moja wodi ya wanawake. Wakapita taratibu macho kwa kila kitanda kilicho na mgonjwa. Isivyobahati hawakufanikiwa kumwona Stella. Wakajawa upoozi uliosumbua kwa muda akili zao kwa mafikirio.

“Itakuwa yuko wapi?” Dorice alijisemeza, lakini sauti ilimtoka kwa nguvu tofauti na matarajio yake.

“Labda tuulizie,” Pendo alishauri.

Dorice alisonya kwanza, kisha akakubaliana na Pendo.

Wakamfuata mmoja wa wagonjwa, walimsabahi na kumpa utambulisho wao, mara baada ya hapo walieleza hitajio.

“Alikuwepo hapa. Hicho kitanda mnachokiona,” Akawaonyesha kidole kuelekezea kitanda amaanichasho, kisha aliendelea kuwaeleza, “Ameruhusiwa dakika chache zilizopita.”

Wakazidi kunyong'onyea.

Wapi waelekee kumtafuta?

Ulikuwa mtihani mkubwa kwao. Ambao jibu la kwanza walilolipata wamtafute hewani. Lakini namba yake haikupatikana.

Wakakumbuka maneno ya Fadhy. Namna alivyowahabarisha tukio lilivyotokea na uratibu ufanywao na watu wake.

“Tumpigie simu tumuulize?” Pendo aliuliza, wakiwa wameshaliacha jengo la hospitali kwa hatua kadhaa.

“Hapana. Kumbuka kwake tumetoroka.”

“Sasa unadhani tutafanyaje? Au tutampatia wapi?”

“Dah, sijui hata nifanyaje.”

“Tumeyavulia nguo, hivyo ni wajibu wetu kuyaoga haya maji pasi na kujalisha yapo katika hali gani.”

“Ishu tunayaoga kwa namna ipi?”

“Tujiandae kwa utekelezaji wa hatua inayofuata.”

“Itaniondolea ari pasi na kufahamu mwanangu yupo wapi na yuko katika hali gani.”

***

Risasi iliyoruhusiwa na Jovin ilimpata Stella begani. Kwani katika hangaikahaingaika za kumtafuta baba'ke alipomwona alimkimbilia na kumrukia. Urukaji alioufanya ukamuumba kuwa mrefu zaidi ya umbo la baba'ke. Chiku akawa mwangalizi wake wa kujiiba. Hilo liliratibiwa na Askofu Ponera.

Aliporuhusiwa, Chiku na Askofu Ponera wakasaidizana kumchukua. Wakamhifadhi Meswaki.

Kiu ya kufahamu mkasa ulivyokuwa ikawalazimisha timu nzima watake kuhadithiwa. Walihitaji wafahamu chochote kutoka kwake anachokihisi. Stella naye hakuwa mchoyo. Alifunguka kila kitu kumhusu Jovin na Nalimuka. Aliuelezea mpango wao wa kuchoma nyumba moto na dhamirio la shambulizi.

Kwa kiasi kikubwa wote waliguswa na simulizi yake. Mioyo ilisinyaa. Furaha ikafungwa kibindoni. Udhalimu uratibiwao na Nalimuka ulikinaisha.

“Sasa wamezidi. Wamefikia kutaka kuondoa uhai wa watu!” Chiku alisikitika.

“Kwa hiyo umefikiria kufanya nini?” Askofu Ponera alihoji.

“Nataka hawa ma-mbwa wakamatwe,” Stella alijibu.

“Upo ridhaa kurudi tena kwa Jovin ili utusomee mienendo yake itakayoturahisishia tumweke himayani?” Luteni Ringo aliuliza.

“He! Hata kupona…” Chiku akaingilia kati.

“Yafaa aende sasa. Na aendelee kujionyesha kama alivyofanya mwanzo-kwamba hafahamu matendo ya Jovin.”

“Hilo kwangu halina shida.”

“Basi utarejea jioni ya leo. Kikubwa kuwa makini, Jovin asinuse uhusika wa namna yoyote utakaonyesha unamchunguza. Na kwa taarifa yenye shaka, utaiwasilisha kwangu.” Askofu Ponera akamkabidhi karatasi iliyoandikwa namba yake ya simu.

“Hamna shida.”

Jioni ya siku hii ndipo Stella alirejea nyumbani kwa Jovin. Katu, hakuonesha ishara zozote zilizoashiria anaufahamu uovu wake. Aliigiza, kama ilivyokuwa awali. Jovin naye aliigiza kama hafahamu chochote kuhusu shambulizi alilolifanya.

“Ulikuwa wapi siku zote hizo?” Jovin alihoji, wajihi ukiwa umefura kwa hasira.

“Nilipata ajali mpenzi'ngu. Kwani nilivyopata taarifa nyumba yetu nilikimbilia kuona kiendeleacho. Matokeo yakawa haya-kushambuliwa na kitu chenye ncha kali. Ijapokuwa wauguzi wanasema ni risasi.” Stella akamwonyesha jeraha alilofungwa bandeji.

“Oooh, pole sana. Ina maana siku zote ulikuwa hospitalini?”

“Ndiyo.”

“Mbona hukunitaarifu hata kwa njia ya simu?”

“Sifahamu simu yangu nilipotezea wapi. Hivyo naomba uniwie radhi. Sijapotea kwako kwa makusudi,” Stella alinyenyekea.

“Jitahidi siku nyingine unitaarifu. Huwezi kupata shida na jambo kubwa hivi, halafu nishindwe kuwa na taarifa.”

“Sawa mpenzi'ngu.” Stella akainuka na kupotelea chumbani.

Kilichopo moyoni, alikidhibiti vyema kutokitoa mbele ya Jovin lakini kilimjaza kifua kadri sekunde zilivyozidi kusonga mbele. Alikuja kukitua alipofika chumbani-kugugumia kilio cha kimyakimya.

***

Mkurugenzi mashtaka ya jinai alikuwa ofisini kwa meneja wa benki ya wananchi tawi la Mtwara mjini-iliyopo mtaa wa Rahaleo. Mengi waliyateta na kuyafanya, sasa walikuwa na zoezi moja la masubirio ya kuwasili kwa Teller wamkabidhi nyaraka walizokuwa wanazishughulikia. Lengo, akaidhinishe uhamishaji fedha kutoka akaunti ya kampuni ya Cheka, kwenda iliyopo kwenye nyaraka, ambayo ilisadifu kuwa ni ya wizara ya fedha.

Ukimya ndiyo ulitawala ndani ya chumba cha ofisi hiyo. Watete nini kwenye kuhujumu? Hivyo kila mmoja alikesha kusaili mazingira ya ofisi-jinsi samani zilivyopamba.

Aghalabu, ni mvumo wa kiyoyozi ndiyo ulisikika kwa mbali na kufanya ofisi itawaliwe na baridi kiasi.

Luteni Ringo, Pte Bayo na Pte Pemba karibu na muda wa huduma kuhitimika, wakafanikiwa kuingia. Kwa uharaka wawili kati yao, walichukua mapumziko eneo la masubirio wakati Luteni Ringo akipanga foleni ya kwenda kupata huduma. Si kama ilikuwa huduma ya dhati, la.

Bali alipanga foleni kwa kumzuga mlinzi wa kampuni aliyekuwa anahangaika kuwaondoa baadhi ya watu wasiokuwa na sababu za msingi kuwepo mle ndani. Hivyo alisimama kwenye foleni kwa dakika chache, kisha alielekea walipo wenzie.

Hapo, wakawa makini kuzihimiza mboni kusaili chumba cha Meneja. Sio kama walikuwa wenye mapepe, hasha. Waliuvaa utulivu usiotoa chembe ya shaka kumfahamisha mtu wana zoezi maalum mahali hapo. Zoezi la kuhakikisha muamala wa Mkurugenzi mashtaka ya jinai hautekelezeki.

Dakika kadhaa baadaye walimwona binti wa makamo aliyevaa kinadhifu sare za wahudumu wa benki hiyo akipotelea ofisini kwa meneja. Hakuchelea, akatoka akiwa amebeba makaratasi yaliyowafahamisha kina Luteni Ringo ndiyo yamebeba uidhinisho wa muamala.

Wakazidi kumfuatilia.

Kwa kusaili dirisha la ma-teller atakalotokezea.

Wakamwona ameingia kwenye dirisha la kioo cha wazi kilichotambulishwa na bandiko la Teller 5.

Watauzuiaje muamala huo? Ikawabidi wafanye tukio la uvamizi baridi kwa muda.

“Mboni zote kwangu na hapa mlangoni,” Luteni Ringo aliwapanga vijana wake.

“Hamna shida kamanda,” Pte Bayo na Pte Pemba wakaitikia kwa pamoja.

Mara baada ya makubaliano hayo Luteni Ringo aliinuka na kupiga hatua makini kuelekea ofisini kwa meneja. Kwa kuanzia hapo, aliamini wakitakacho kitafanikiwa. Ukizingatia waliingia mle ndani na bastola zao. Walipozificha ilikuwa ngumu kubainika kwa urahisi.

Mwendo wa dakika chache tu, ukamfikisha ofisini kwa meneja wa ile benki. Akapokelewa na macho kodo kutoka kwa aliowakuta. Naye akajifanyisha mjinga zaidi, kwa kuumba wajihi huruma akiwa amesimama kuangaza mazingira ya mle ndani.

“Karibu,” meneja akamkaribisha.

Luteni Ringo akaketi kwenye moja ya viti vilivyopo wazi.

“Mnh! Nikusaidie nini?” meneja aliuliza. Wakati huo Luteni Ringo alikuwa anapambanua namna itakayompa ushindi kwa urahisi. Kwani alifahamu fika, uzembe mdogo tu, utagharimu misheni kwa ukubwa.

Atarukaje vihunzi vitakavyotoa ishara ya hatari kwenye vyombo vya ulinzi kutoka kwa meneja wa benki?

Ndicho kilichomtatizisha.

“Aaaah, kuna tatizo fulani katika akaunti yangu bosi,” Luteni Ringo alisema, pindi akihangaika kutoa kadi ya benki kwenye kibeti. Akaitupa juu ya meza iliyopo mbele ya meneja.

Isivyobahati, kadi ilidondokea chini-uvunguni mwa meza. Meneja akafanya bidii ya kuiokota.

Likawa kosa, na fursa kwa Luteni Ringo.

Alitumia wasaa huo kujiinua kwa haraka, akakisukumiza kiti kilichokaliwa na meneja, akampa zoezi lingine lisilo na madhamirio. Meneja alianguka.

Mkurugenzi mashtaka ya jinai akapigwa na butwaa. Alipotaka kujichomoa kwenye zahama hiyo, akakumbana na mdomo wa bastola.

“Kaa hapo kabla sijamwaga ubongo wako,” Luteni Ringo alimwamuru. Mkono aliokamatia bastola ukimwelekezea anakopaswa aketi.

Mwendesha mashtaka akatii. Naye akaketi kwenye kiti cha meneja.

“Kwa usalama wenu nyote, mpigieni simu yule binti haraka iwezekanavyo kabla hajafanya muamala kupitia makabrasha mliyomkabidhi,” Luteni Ringo alisema. Bastola ikihamahama uelekeo kila baada ya sekunde kadhaa; awamu hii anaoneshwa meneja wa benki, awamu nyingine Mkurugenzi mashtaka ya jinai.

Hofu ya risasi ikamfanya meneja wa benki ajiinue na kwenda kuungana na Mkurugenzi mashtaka ya jinai alipoketi.

“Mumenielewa nilichowaamuru?” Awamu hii alikichukua kiwambo na kukirushia kwa meneja wa benki. “Mpigie simu haraka iwezekanavyo.” Akakazia.

Cha kufia nini?

Meneja wa benki alikamata kiwambo, akabonyeza vitufe kadhaa, akafuatia kukiweka sikioni. Haikumchukua muda mrefu kuzungumza na mtu wa upande wa pili. Alipokitua kiwambo, Luteni Ringo akawafuata walipoketi.

Jicho kali walilowaonyesha likawapa picha namna gani wanapaswa kuwa, pindi yule binti atakavyoingia mle ndani.

Binti alivyoingia hawakuonesha mazingira yoyote yakumfanya afahamu wapo hatarini.

“Weka hapo mezani kwanza,” Meneja alimweleza.

“Kuna tatizo bosi?” binti aliuliza pindi akiweka yale makaratasi alipoelekezwa.

“Hapana. Tutakuita tena baada ya muda kidogo.”

Binti akaondoka.

Luteni Ringo akayakusanya yale makaratasi, akayakunja kunja na kuyahifadhi mfukoni.

“Haya, kwa utulivu, nyoosheni mlangoni kuelekea nje,” Luteni Ringo akawaamuru, nao kutii pasi na majadiliano.

Walivyoufikia ukumbi wa huduma kwa wateja, Luteni Ringo akiwa nyuma yao, Pte Pemba akawahi garini, wakati Pte Bayo akidumisha ulinzi kwa kusaili uono wa watu kumtafuta atiliaye shaka.

Lakini hakubahatika kumwona. Wateja wengi walitekwa na umakini wa kufikia zamu zao za kuhudumiwa.

Kwa sababu mlango ulishafungwa-kuashiria muda wa huduma umehitimika, mlinzi ashughulikaye na usalama kutoka moja ya kampuni ya ulinzi, aliwafungulia, nao kwa hatua zilezile walilifikia eneo la nje ya jengo. Pte Bayo ndiyo alifunga msafara.

Kule nje Luteni Ringo alimwamuru Mkurugenzi mashtaka ya jinai aingie garini. Alivyotekeleza, walifuatia wenyewe. Pte Pemba akaungurumisha injini, ilivyoitika, waliondoka eneo hilo kwa mwendo wanguwangu wakimwacha meneja wa benki na staajabiko.

***

Kutowakuta kina Dorice na Pendo nyumabni kulimpagawisha kwa dakika kadhaa Fadhy. Kila jitihada ya mawasiliano aliyoifanya haikumpa jibu tarajiwa. Mwisho, alimshukuru Mungu. Na kumwomba popote walipo watu hao wawe wenye usalama.

Fikra ya kutorokea Mangaka ikakumbata kuta za ubongo wake. Kwamba kwa namna yoyote ile, wamekimbilia huko, kutokana kitendo walichokifanya mara ya mwisho.

Baadaye akajilaumu sana kwa uzembe.

Kabla hali hiyo haijakoma, simu yake ikaanza kuita. Aliitoa alipoihifadhi, alimfahamu mpigaji, hakuchelea kupokea.

“Ndiyo Luteni,” Fadhy alisema kiunyonge sana. Kiasi kwamba Luteni Ringo aligundua hilo kwa haraka.

“Unaonekana kutokuwa sawa chifu.”

“Nijuze kwanza dhamirio la simu yako.”

“Mkurugenzi mashtaka ya jinai tunduni. Hivyo tunaomba maelekezo yako.”

“Himahima upepuni mwangu. Sambamba na hilo…”

Luteni Ringo akadakia, “Ndiyo chifu.”

“Wake wa ndugu wametoroka hapa nyumbani,” Fadhy akatulia kwa muda. Kama alikuwa anasikilizia mapokeo ya Luteni Ringo. Akaendelea, “Nina wasiwasi watakuwa huko.”

“Itakuwa vyema ukitupatia picha zao.”

“Nipe dakika moja.”

Luteni Ringo akakata simu.

***

Baada ya kumkosa Stella hospitalini, wakiwa mita kadhaa kutoka uzio uzungukao majengo ya hospitali, Dorice aliita boda, wakampatia uelekeo wanaohitaji kufika, walivyoelewana nauli, walipanda-mshikaki kisha dereva aliachia mchuma.

Ukomo wa safari ulikuwa katikati ya mji. Maeneo ya ghala la Mangaka Amcos-pembezoni tu mwa barabara ielekeayo Mtambaswala. Waliteremka, Dorice akafanya malipo. Dereva boda alivyoondoka, wakaichakatisha akili wapi waelekee.

Zoezi hilo liliwachukua takribani dakika moja, ndipo wakakubaliana uelekeo wanaopaswa kwenda. Wavuke barabara, waingie maeneo ya Kilimanihewa. Kwa hatua fupifupi zenye uharaka; hatua-mbio wakajitoma barabarani.

Wakiwa wamepiga hatua mbili tu, akili imezuzukwa na umalizaji wa kuvuka, baada ya kujihakikishia kwa kuangaza huku na kule hakuna gari inayokuja, hamadi bin vuu! Ikajitokeza gari upande wa kulia kwao ikiwa moto mbaya. Kwa uono wa harakaharaka wakabaini hakuna uwezekano wa wao kuvuka kabla ile gari haijawafikia. Wafanye nini?

Wakasitisha mwendo na kubaki kuduwaa.

Pindi wao wanasimama, na mhusika wa gari akafunga breki ya nguvu. Gari ikasimama hatua chache toka walipo. Hofu ikawajaa. Dorice akashindwa kuihimili na hatimaye alidondoka pasi na fahamu.

Mashuhuda wakalipuka kwa ukunga uliojaa masikitiko.

“Dada, dada. Mama Stella…” Pendo aliita huku akimtingisha.

Mashuhuda wakaacha shughuli zao wakasogelea wajionee kwa ukaribu.

Mwenye gari naye aliteremka akaungana na Pendo kufanya bidii ya kumrejeshea fahamu zake.

“Tumuwahishe hospitali,” mwenye gari alipendekeza. Ushauri ulioafikiwa kwa urahisi na Pendo. Hata baadhi ya mashuhuda nao.

Hivyo walimtwaa juu kwa haraka na kumpakiza garini. Walimlaza siti za kati. Gari ilikuwa aina ya Toyota land cruiser Prado. Dereva akaketi na Pendo kule siti za mbele. Pasi na kukawia safari ya kuelekea hospitali ikaanza. Ukimya ukiwa umechukua hatamu.

Baadaye Pendo uvumilivu ulimshinda. Ukiachilia mbali ukimya, asimfahamu hata aliyenaye? Akathubutu kugeuka kwa kujiiba amwangalie. Moyo ukapiga kite kwa nguvu na kusinyaa kwa haraka. Hakuamini, aliyemwona ndiye. Nalimuka.

***

Akiwa amejaa mihangaiko ya kutembea huku na kule kwenye ushoroba wa kuingia vyumbani kwa madaktari, Nalimuka alipata simu na kumfanya asitishe lile zoezi. Hakuchelea, alitoa simu mfukoni, alimsaili mpigaji kwanza ndipo akafuatia kuipokea.

“Ndiyo meneja,” Nalimuka aliita.

“Mambo hayapo sawa kiongozi,” sauti ya upande wa pili ilisikika. Sauti ya meneja wa benki ya wananchi tawi la Mtwara mjini.

“Nini shida?”

“Mpango haujafanikiwa.”

“Inawezekanaje?” Nalimuka alifoka, kiasi kwamba hadi mapigo ya moyo yalimbadilika. Kwani ile taarifa ilimpa mshituko kwa kiasi fulani.

“Pindi tunasubiri taratibu za muamala kukamilika, walikuja wavamizi waliotushurutisha kusitisha zoezi. Kwa namna tulivyobanwa, hatukuwa na ujanja wowote zaidi ya kutii matakwa yao.”

Nalimuka akadakia kwa unyonge, “Ooooh.”

“Tuwie radhi bosi. Na tunaweza tukafanya taratibu za kiusalama kuwakamata hao wahalifu kama utahitaji.”

“Nitakuja kuwaona. Walikuwa wangapi?”

“Watatu bosi.”

“Sawa. Wewe kuwa na amani, nitashughulikia kila kitu mwenyewe.”

“Hamna shida bosi, mimi nitakuwa nyuma kwa msaada wowote.”

“Vipi kuhusu DPP?”

“Waliondoka naye bosi.”

“Hee!”

“Ndiyo hivyo bosi.”

“Okay…okay.” Nalimuka akajawa na kitetemeshi. Fikra zikamwenda mbali kiasi cha kutengeneza ukimya uliomshinikiza meneja wa benki akate simu.

Nalimuka akabaki mwenye kusawijika.

Zilipita dakika mbili toka simu ilivyokatwa, ndipo Nalimuka alikaa sawa ki-akili kwa kiasi fulani. Hasa baada ya kumbikizi ya kiapo chake. Kwamba atamiliki vitu vyote vya thamani vya wabaya wake. Akaona huo ndiyo muda wa kufanya hivyo.

Na kwa utekelezaji, alimfuata Pendo alipoketi.

“Nakuomba mara moja,” Nalimuka alisema.

Pendo hakutii kwa haraka. Alimsaili kwanza, kwani wasiwasi wa uovu dhidi ya mtu huyo ulifanya asitamani hata awepo mbele yake.

“Kuna jambo nahitaji tujadiliane.” Kauli hii ikamlainisha Pendo na kumwinua pale alipoketi.

Wakaongozana na Nalimuka, wajihi ukiwa umesawijika. Wakati huo Dorice alikuwa chumba cha daktari akipatiwa matibabu.

Mwisho wa mwendo wao ulikuwa eneo la maegesho ya vyombo vya usafiri. Moja kwa moja waliifikia gari walilokuja nalo. Nalimuka akamfungulia mlango Pendo, akapanda. Naye akafuatia.

Ukimya ukachukua nafasi kwa muda kabla Nalimuka hajaufukuza, “Kwanza naomba usahau yote yaliyopita. Nataka nitumie nafasi hii kwa masahihisho kwenu kama hautojali.”

“Masahihisho yapi?”

“Kuwasaidia.”

Pendo akamgeukia na kumtolea mboni za mshangao.

“Ndiyo. Nimeamua hilo. Lakini kwa kuanza na mtu mojammoja. Nataka nianze nawe.”

Wakashangaana.

Upole wa Pendo ukamfanya ashindwe kuihimili hali hiyo. Akakwepesha macho.

“Mimi nawe tunaweza kufanya jambo tukamsaidia mumeo. Halafu mwenzio akishazinduka, niongee naye pia namna ya kumsaidia mwenza wake.”

Pendo akazidi kumshangaa. Huku akikumbwa na hali fulani mtimani.

Kujirudi kwa Nalimuka kulimlainisha zaidi Pendo. Hasira alizonazo dhidi ya mtu aliyeketi naye hapo ziliyeyuka taratibu kadri sekunde zilivyozidi kusonga mbele.

“Kwa hiyo mimi nahusikaje kama unataka kutusaidia?” Pendo aliuliza, mboni zimelala kwa Nalimuka akizidi kumsaili.

Nalimuka badala ya kujibu, akamsaili Pendo kwa mboni zilizojaa uchu wa matamanio. Kwani alikesha kumsaili usoni, kifuani na nyongani. Haukuwa usaili wa mara moja, alirudia zaidi na zaidi kiasi cha kumchipuzia Pendo aibu ya kike.

Baadaye akamshika sehemu ya tumbo kwa usawa mbavu. Pendo akashtuka.

“Natamka haya kwa dhati ya moyo wangu. Sisi sote ni wa hapahapa, hivyo ni heri tumalize ki-utu uzima,” Nalimuka alimsisitizia. Wajihi ukionyesha uhalisia wa kile atamkacho.

Kupitia msaada alioutoa, ikiwemo kugharamia matibabu ya Dorice, Nalimuka aliteka akili ya Pendo na kumsahaulisha kabisa machungu yote aliyonayo. Akajenga imani, akisikiacho ni kweli. Na kwa sababu ndiyo lilikuwa hitajio lao, hakuwa na budi kuonyesha ushirikiano.

“Kwa hiyo…” Pendo alisema, akakatishwa kabla hajahitimisha.

“Wewe ni mtu mzima. Nina imani kila nimaanichasho umekielewa.”

“Hapana.”

Nalimuka akamshika shingo na kumgeuzia aliko, waangaliane. Pendo akazidi kushindwa kuihimili aibu. Akakwepesha macho.

“Siku hizi usipojisaidia huwezi ukasaidika. Wewe ndiyo unapaswa kumsaidia mwenzio.”

“Ni sahihi. Lakini kwa namna ipi?”

Nalimuka akajisogeza kwenye siti aliyoketi Pendo ndipo akanuia kujibu. “Nadhani mpaka sasa utakuwa umeelewa nini nitakacho.”

Na hakika Pendo alishanusa harufu hiyo. Kule kukaribiwa na kuguswa guswa mwili kulimvumbua.

“Lakini…” Pendo akakatishwa kwa mara nyingine. Alikatishwa na mkono wa Nalimuka uliogusa nyama ya paja.

“Usiwe na wasiwasi. Lakini kama unahitaji mumeo azidi kusota kule ndani sio kesi,” Nalimuka akatoa ule mkono na kujirudisha kwenye siti yake. Alijifanya kuzira.

Kitendo kilichompa wakati mgumu Pendo. Kwani hakubanduka kupiga jicho zongo huku mapigo ya moyo na akili vikiwa na kazi ya kumshinikiza achukue maamuzi gani. Akafikiria mazingira aliyonayo mumewe-Kasembe kule mahabusu na kile kitendo atakachofanya ambacho kilimpa imani thabiti ya msaada.

Kwa nini amtese wakati anaweza kumsaidia kwa urahisi kwa kitendo cha mara moja?

“Sasa, tuta…”

Nalimuka akadakia, “Hata hapa panatufaa.” Akamsogelea kwa mara nyingine, kisha akalaza siti.

Abahatike mara ngapi mzee wa watu?

Akakesha kupiga vigelegele mtimani. Alichokuwa amekidhamiria ndicho kilichopo mbele yake. Alimvaa binti wa watu. Akamsasambua, na kumfanya ndani ya muda mfupi awe kama alivyozaliwa.

“Tufanye haraka basi,” Pendo alisema kwa sauti dhoofu. Alishatekwa kila kitu.

“Usiwaze,” Nalimuka alijibu akiwa anateremsha suruali aianze shughuli.

Dakika kadhaa baadaye, katika hatua ya maandalizi ya kuianza safari, Nalimuka akawa anamchombeza Pendo kwa kumtaka aelezee jitihada walizozifanya kipindi cha nyuma. Naye bila hiyana, huba lilimfumba, akatoa ushirikiano pasi na kuacha jambo lolote. Alielezea jitihada zote zifanywazo na Fadhy. Baada ya hapo, ndipo akatumikia hitajio la Nalimuka. Hitajio la kumwonyesha undani na kumwachia akitumie atakavyo kile kimpacho jinsia.

ITAENDELEA.
 
NYAYO ZA JASUSI
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

Jioni, yapata saa kumi na moja, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Cosmas Luambano, aliongoza kikao kilichojumuisha maafisa wa Idara maalum intellijensia ofisi ya Rais (IMI). Jumla ya wahudhuriaji walikuwa saba; Benson Lau-Mkurugenzi idara ya usalama wa Taifa (Tanzania security service-TSS) Fadhy Njau-mkuu wa idara, Askofu Ponera (Luteni Kanali John Chiwa), Luteni Enos Ringo, Pte Shaban Bayo na Pte Mussa Pemba. Kilifanyika katika ukumbi wa kikao ofisi ya IMI iliyopo chini ya Fadhy Njau.

Nyuso zilijaa umakini. Mavazi waliyovaa-suti zikawafanya kuwa nadhifu. Na kuakisi kilichopo ubongoni mwao.

Makutano yao mahali hapo yalichangiwa na wito wa Fadhy, kupitia simu aliyoipata kutoka nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo siku kadhaa zilizopita. Sio hilo tu, mhusika aliyepiga simu hiyo ndiyo alimpa msukumo wa nguvu-kiasi cha kuwakutanisha viongozi wakubwa wa nchi. Koplo Frederka Tarimo, afisa idara maalumu intellijensia ofisi ya Rais. Aliyesadikika kuuwawa nchini Burundi.

Hivyo kama ilivyo jadi ya wanaintellijensia, kutilia mashaka na kuifanyia kazi taarifa yoyote kwa usalama wa nchi, Fadhy, ambaye ni jasusi mwandamizi, alilazimika kuifanyia kazi taarifa hiyo haraka iwezekanavyo.

“Huisi hili jambo linaweza kuwa mtego kwetu?” Rais Luambano alihoji, mara baada ya Fadhy kuelezea mazingira ya taarifa ilivyomfikia.

“Nina uhakika na ile sauti kuwa ni ya mtu wetu,” Fadhy akawahakikishia.

“Kwa hiyo umeshafikiria nini cha kufanya ili tujihakikishie? Maana tunaenda kufanya ujasusi katika nchi ambayo haijatukosea kwa lolote.” Mkurugenzi usalama wa Taifa, Benson Lau akaingilia kati.

“Yeah, nimeshafikiria. Lazima tufute nyayo za jasusi wetu, hivyo naipeleka timu huko.” Fadhy akawasaili wajumbe wote wa kikao, kisha aliendelea, “Nilishawadokeza vijana wangu awali, awe mzima, ama amefariki, Koplo Frederka lazima arejeshwe nyumbani. Ni afisa wetu, hivyo ni lazima tumpe heshima yake, ijapokuwa miiko ya kazi yetu inatuonya katika hili.”

“Nami hofu yangu tusiingize nchi katika hatari. Sihitaji wananchi waishi kwa hofu, kama wamekopeshwa makazi ilhali ni nchi yao,” Rais Luambano alionyesha wasiwasi wake.

SC (Spy Chief) au DGIS kama inavyofahamika na wengi (Director General of Intelligence Service) Benson akadakia, “Sahihi mheshimiwa Rais. Ukizingatia haifahamiki uelekeo wa mhusika alipo. Tutafanyiaje kazi kitu ambacho hakifahamiki kipo uelekeo gani? Kigezo cha kutumika namba ya kidemokrasia ya Kongo hakikidhi. Tusije kutoa vijana wetu hapa wakishawasili demokrasia ya Kongo...”

Fadhy akamkatisha, “Tayari nimeshachora ramani ya ufanikishaji wa hili.”

“Haya tueleze,” Rais Luambano alishikwa na shauku ya kufahamu zaidi.

“Fadhy,” Benson aliita. Wajumbe wote wa kikao wakamwangazia, “Mimi sikubaliani nawe katika hili. Hebu pata kwanza uhakika wa mahali ndipo...”

Rais Luambano akaingilia, “Mwache atueleze. Mara baada ya hapo ndipo tuchangie mawazo.”

Fadhy akaendelea kushika hatamu ya kuwafafanulia mipango aliyoiratibu. “Kwa mazingira ya mawasiliano tuliyoyafanya yalinipa picha Koplo Frederka yupo hatarini. Hii nilijithibitishia kupitia mirindimo ya risasi niliyoisikia na sauti ilivyomtoka. Hivyo nikaamua kwa dhati, niwatume vijana wangu; Askofu Ponera, Luteni Ringo na Pte Pemba wakalishughulikie hili. Wanaanzaje
“Nimedhamiria kumtanguliza Askofu Ponera akaifanyie kazi namba iliyotumika kuwasiliana nami. Wanaosalia, watasafiri...”

Benson akamkatisha, “Haiwezekani hilo kushughlikiwa papahapa?”

“Itakuwa vyema tukifanyia kule. Afisa, anayehudumu usalama ubalozi wa DRC atasaidia ufanikishaji.”

“Umehisi nani wanaweza kuwa wahusika?” Rais Luambano aliuliza.

Ulizo hili lilitengeneza ukimya wa muda, uliotoa picha muulizwa-Fadhy yupo tafakurini. Karibu na kushika hatamu, akajibu, “Waasi.”

“Kwa nini umewahisi wao moja kwa moja? Hata makamanda wa kiserikali wanaweza...” Benson alihoji.

Fadhy akamkatisha, “Wao ndiyo wanaovuma kwa matendo maovu asilimia zote kule DRC.”

“Nilitaka tutumie njia ya ki-diplomasia kulitatua hili,” Benson alishauri.

Rais Luambano akadakia, “Swadakta. Nami nilikuwa na mawazo hayohayo. Tuketi chini na serikali ya DRC tuone tutakavyolitatua.”

“Tambueni yule ni kamanda wa jeshi. Tukiitaarifu serikali ya DRC watashikwa na butwaa, imekuaje mtu wetu ameingia kwao, hivyo itawalazimu waingie kazini kupeleleza. Na kama wahusika ni waasi, tukiiambia serikali, mlolongo utakuwa mkubwa wa kufanikisha tukitakacho.

“Hamna namna, zaidi ya kuruhusu vijana kwenda ili liwe zoezi la haraka na muda mfupi.” Akawasaili wajumbe wapokeavyo.

Kama walimwelewa.

Kwani wote walizama tafakurini kuchakata walichotaarifiwa. Ukimya ukachukua nafasi kwa mara nyingine.

Rais Luambano akaufukuza, “Nimekuelewa Fadhy. Upo sahihi. Na itakuwa vyema utekelezaji ukafuatia haraka iwezekanavyo.” Benson akamgeukia. “Yeah, tulibebe hili kwa mikono yote. Simu aliyopiga Frederka inahitaji msaada wetu, hivyo hayo mengine tuyaache pembeni.” Rais Luambano alikazia.

“Hivyo basi,” Fadhy akawashtua. Wote wakageuka kumwangalia, “Kama nilivyoanza kutoa dokezo, Askofu Ponera atatangulia na atatumia usafiri utakaomfikisha kwa uharaka-ndege. Wakati Luteni Ringo na Pte Pemba watasafiri kwa basi.”

“Huyu mwingine?” Benson akamwelekezea kidole Pte Bayo.

“Afya yake haiko vyema. Alipata madhara yaliyopelekea mwili wake kutokuwa sawa katika operesheni ya mwisho waliyoitekeleza,” Fadhy alijibu.

“Sina pingamizi na hiyo ramani. Nawatakia kila heri katika ufanikishaji. Mwenyezi mungu apate kuwatangulia,” Rais Luambano aliwatia moyo.

“Amina.” Askofu Ponera, Luteni Ringo na Pte Pemba wakaitikia kwa pamoja.

Kikao kikahitimishwa.

***

Mruko uliosababishwa na shambulizi lilimtua Koplo Fredreka kwenye tawi la mti mkubwa pasi na fahamu. Akakwama hapo na kuwa kama kuku aliyebanikwa. Wakati huo jeraha la kukitwakitwa kwa vyuma vidogovidogo vilivyotokana na shambulizi vikimpa majeraha kadhaa yaliyochangia kutokwa na damu.

wa-mama wawili wenye rika la miaka arobaini na tisa, waliowahi kwenye poromoko hilo kukusanya kuni asubuhi ya siku iliyofuata, ndiyo walikuwa wa kwanza kumbaini Koplo Frederka baada ya mmoja wapo kudondokewa na matone ya damu.

“He!” yule aliyedondokewa na damu alipigwa na butwaa, huku akiruka hatua moja ndefu mbele, kisha akaangazia matone yalipotokea.

“Nini tena?” mwenzie aliuuliza.

Badala ya kujibu, alimvuta na kumkumbatia, kisha akamhimiza mboni zake zielekee alipoelekeza kidole. Juu ya mti.

“Mama!” yule aliyevutwa naye akastaajabu.

Walistaajabu kuuona mwili wa Koplo Frederka kule juu. Staajabiko lililowapa hofu na kupoteza hamu ya kilichowaleta porini.

Wasichokijua, yowe walilopiga liliwafikia m-baba mmoja akadiriaye miaka hamsini na ushee pamoja na mtoto-apataye rika la miaka kumi na nne aliyambatana naye ndani ya poromoko hilo wakihangaika kutafuta kitu.

Kwa mwonekano wa mavazi, dhahiri yaliwaonyesha wao si watu wema. Yule m-baba alivaa suruali ya jeans rangi nyeusi, buti ya kijeshi, fulana mchinjo, koti rangi nyeusi lililoshuka hadi magotini, pasi na kusahau kapelo rangi ya hudhurungi. Mtoto naye alivaa namna hii. Tofauti ni rangi tu-yeye ilishamiri rangi ya samawati. Wote, walisundika bastola na ala yenye kisu kimoja kiunoni.

Uchangamfu wajihini kwao kilikuwa kitendo cha nadra mno. Mashavu yaliwatuna muda wote kama watu waliolishwa pilipili. Hali hiyo ilichangiwa na ukosefu wa kile wakitafutacho.

Kusikia sauti ya kike iliyoshamiri hofu iliwafanya wasitishe kwa muda zoezi lao. Walisimama, na kutega viwambo vyema kwa lengo la kusikilizia tena, lakini hakuna sauti iliyoendelea kusikika. Wakaingiwa na hofu kiasi, iliyosinyaisha mioyo yao na kujenga picha mbaya akilini kwa mtoa ukunga huo.

“Twende kwanza tukawaangalie hao,” yule m-baba alishauri. Mtoto kwake ni utii tu.

Wakabadili uelekeo wa safari. Mwendo nao ukiongezeka.

Baada ya kukata kichaka kwa takribani dakika nne, walifikia kwenye ule mti mkubwa uliokuwa na mwili wa Koplo Frederka. Wakasitisha mwendo, na kuangaza huku na kule. Macho zaidi ya mita mia moja. Walifanya kazi ya ziada kuushinda msitu.

Malalo ya nyasi ndiyo yaliyopelekea mwendo wao uishie mahali hapo. Wakahisi, wale waliopiga ukunga walikuwa hapo. Lakini isivyo bahati, hawakufanikiwa kuwakuta. Katika jitihada ya kuangazia huku na kule kwa uzungukiaji, yule mtoto akabaini lundo la damu umbali wa mita tatu toka kwenye shina la mti.

“Kuna damu hapa,” akamtaarifu yule baba. Kauli iliyomhimiza auache uelekeo aliopo na kukimbilia pale kwa mtoto.

Akajihakikishia. Na kwa uthibitisho zaidi, alikihimiza kidole chake cha shahada kuigusa na kuisigina sigina kwa vidole viwili. Aliporidhishwa na kitendo hicho, akainua mboni kuangazia mbele yao. Umbali wa mita moja toka walipo kulikuwa na lundo lingine la damu. Wakashawishika kulisogelea.

Napo alifanya kama pale pa awali. Huku mlalo wa nyasi ukizidi kuumba jambo akili mwao.

“Itakuwa wameelekea huku,” yule mtoto alieleza wasiwasi wake.

“Kwa hiyo unashaurije; Tuendelee na zoezi letu, au tulifanyie kazi hili tulilolibaini?” yule m-baba aliuliza.

Wakati huo mtoto amezielekezea mboni zake kwenye ule mti. Akabaini jambo lililompa dukuduku maradufu.

Akavuta koti la yule mzee na kumtaarifu jambo, “Hebu ona kile pale mtini.” Akamwelekezea kwa kidole sehemu ya kutazama.

Lahaula!

Walishuhudia michirizi ya damu.

Wakaparudia chap kupachunguza kwa umakini.

Naam, ile damu ilitiririka kutoka kwenye moja ya tawi. Wakazihimiza mboni kuangalia juu-chanzo cha ile damu.

Hawakuona kitu.

“Itakuwa ni yule tumtafutaye,” mtoto alitoa wazo.

“Hakika. Hata nami nimehisi hilo,” yule m-baba aliafikiana naye.

Dakika moja baadaye walitii takwa la mioyo yao, kuufuatilia ule mlalo wa nyasi wenye damu. Mwendo ukawa changamano; nusu kukimbia, nusu kutembea. Muda wote wakiwa na ombi la kumkuta wamhisiye-Koplo Frederka.

Ndiyo waliyokuwa wanahangaika kumtafuta. Lengo wajihakikishie ameshafariki. Kama bado, wammalizie. Kwani yule mtoto ndiyo aliyefanya shambulizi la kuishambulia gari waliyopo kina Brigedia Jenerali Buyoya kule Buyenzi. Yule m-baba ni ndugu na Brigedia Jenerali Buyoya.

Hivyo walikuwa kwenye kiu ya kuiadhibu serikali ya Tanzania ki-sawasawa.

Baada ya mwendo uliowachukua takribani dakika kumi na sita, mihemo ikiwa juujuu, jasho likiwatiririka kama wanariadha wa mbio ndefu, uchovu ukiwakumbata kwa kiasi, karibu na kuumaliza ukuta utengenezao poromoko, wakafanikiwa kuwaona wale wa-mama waliopiga ukunga. Mmoja wao alimbeba Koplo Frederka begani.

Morali ya kuwakaribia ikazidi kuwa juu. Vyote vya kuwanyong'onyeza wakavipotezea. Kasi ya utembeaji ikachukua nafasi. Hadi wanamalizia kuupanda ule ukuta na kuingia tarambare kuelekea makazi ya watu, wakawashuhudia wale wa-mama wakipotelea kwenye uchochoro kuingia zaidi kwenye makazi.

Wakafungua riadha, ambayo iliwahakikishia wawaonao hawatohisi jambo baya dhidi yao. Walipoufikia uchochoro ambao wale wa-mama walipotelea, mboni pima mbele, hawakuona mtu yeyote. Wakajihamasisha kusonga mbele zaidi lakini matokeo hayakubadilika.

“Hawawezi kufika mbali hivi bila kuwaona,” yule mtoto alitoa dukuduku lake.

“Kwa hiyo unahisi?”

“Watakuwa wameingia kwenye moja ya nyumba kati zile za nyuma.” Yule mtoto akageuka na kurejea kwenye nyumba azimaanishazo.

M-baba naye hakuwa na budi, alimfuata. Walipojumuika pamoja, wakayahimiza macho na masikio yanase yaendeleayo kwenye nyumba husika, lakini hawakuambulia cha maana zaidi ya ukimya. Jambo lililowakerehesha na kuwajaza kifua kwa sababu ya hasira.

TUKUTANE TOLEO LIJALO
 
NYAYO ZA JASUSI
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

Jioni, yapata saa kumi na moja, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Cosmas Luambano, aliongoza kikao kilichojumuisha maafisa wa Idara maalum intellijensia ofisi ya Rais (IMI). Jumla ya wahudhuriaji walikuwa saba; Benson Lau-Mkurugenzi idara ya usalama wa Taifa (Tanzania security service-TSS) Fadhy Njau-mkuu wa idara, Askofu Ponera (Luteni Kanali John Chiwa), Luteni Enos Ringo, Pte Shaban Bayo na Pte Mussa Pemba. Kilifanyika katika ukumbi wa kikao ofisi ya IMI iliyopo chini ya Fadhy Njau.

Nyuso zilijaa umakini. Mavazi waliyovaa-suti zikawafanya kuwa nadhifu. Na kuakisi kilichopo ubongoni mwao.

Makutano yao mahali hapo yalichangiwa na wito wa Fadhy, kupitia simu aliyoipata kutoka nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo siku kadhaa zilizopita. Sio hilo tu, mhusika aliyepiga simu hiyo ndiyo alimpa msukumo wa nguvu-kiasi cha kuwakutanisha viongozi wakubwa wa nchi. Koplo Frederka Tarimo, afisa idara maalumu intellijensia ofisi ya Rais. Aliyesadikika kuuwawa nchini Burundi.

Hivyo kama ilivyo jadi ya wanaintellijensia, kutilia mashaka na kuifanyia kazi taarifa yoyote kwa usalama wa nchi, Fadhy, ambaye ni jasusi mwandamizi, alilazimika kuifanyia kazi taarifa hiyo haraka iwezekanavyo.

“Huisi hili jambo linaweza kuwa mtego kwetu?” Rais Luambano alihoji, mara baada ya Fadhy kuelezea mazingira ya taarifa ilivyomfikia.

“Nina uhakika na ile sauti kuwa ni ya mtu wetu,” Fadhy akawahakikishia.

“Kwa hiyo umeshafikiria nini cha kufanya ili tujihakikishie? Maana tunaenda kufanya ujasusi katika nchi ambayo haijatukosea kwa lolote.” Mkurugenzi usalama wa Taifa, Benson Lau akaingilia kati.

“Yeah, nimeshafikiria. Lazima tufute nyayo za jasusi wetu, hivyo naipeleka timu huko.” Fadhy akawasaili wajumbe wote wa kikao, kisha aliendelea, “Nilishawadokeza vijana wangu awali, awe mzima, ama amefariki, Koplo Frederka lazima arejeshwe nyumbani. Ni afisa wetu, hivyo ni lazima tumpe heshima yake, ijapokuwa miiko ya kazi yetu inatuonya katika hili.”

“Nami hofu yangu tusiingize nchi katika hatari. Sihitaji wananchi waishi kwa hofu, kama wamekopeshwa makazi ilhali ni nchi yao,” Rais Luambano alionyesha wasiwasi wake.

SC (Spy Chief) au DGIS kama inavyofahamika na wengi (Director General of Intelligence Service) Benson akadakia, “Sahihi mheshimiwa Rais. Ukizingatia haifahamiki uelekeo wa mhusika alipo. Tutafanyiaje kazi kitu ambacho hakifahamiki kipo uelekeo gani? Kigezo cha kutumika namba ya kidemokrasia ya Kongo hakikidhi. Tusije kutoa vijana wetu hapa wakishawasili demokrasia ya Kongo...”

Fadhy akamkatisha, “Tayari nimeshachora ramani ya ufanikishaji wa hili.”

“Haya tueleze,” Rais Luambano alishikwa na shauku ya kufahamu zaidi.

“Fadhy,” Benson aliita. Wajumbe wote wa kikao wakamwangazia, “Mimi sikubaliani nawe katika hili. Hebu pata kwanza uhakika wa mahali ndipo...”

Rais Luambano akaingilia, “Mwache atueleze. Mara baada ya hapo ndipo tuchangie mawazo.”

Fadhy akaendelea kushika hatamu ya kuwafafanulia mipango aliyoiratibu. “Kwa mazingira ya mawasiliano tuliyoyafanya yalinipa picha Koplo Frederka yupo hatarini. Hii nilijithibitishia kupitia mirindimo ya risasi niliyoisikia na sauti ilivyomtoka. Hivyo nikaamua kwa dhati, niwatume vijana wangu; Askofu Ponera, Luteni Ringo na Pte Pemba wakalishughulikie hili. Wanaanzaje
“Nimedhamiria kumtanguliza Askofu Ponera akaifanyie kazi namba iliyotumika kuwasiliana nami. Wanaosalia, watasafiri...”

Benson akamkatisha, “Haiwezekani hilo kushughlikiwa papahapa?”

“Itakuwa vyema tukifanyia kule. Afisa, anayehudumu usalama ubalozi wa DRC atasaidia ufanikishaji.”

“Umehisi nani wanaweza kuwa wahusika?” Rais Luambano aliuliza.

Ulizo hili lilitengeneza ukimya wa muda, uliotoa picha muulizwa-Fadhy yupo tafakurini. Karibu na kushika hatamu, akajibu, “Waasi.”

“Kwa nini umewahisi wao moja kwa moja? Hata makamanda wa kiserikali wanaweza...” Benson alihoji.

Fadhy akamkatisha, “Wao ndiyo wanaovuma kwa matendo maovu asilimia zote kule DRC.”

“Nilitaka tutumie njia ya ki-diplomasia kulitatua hili,” Benson alishauri.

Rais Luambano akadakia, “Swadakta. Nami nilikuwa na mawazo hayohayo. Tuketi chini na serikali ya DRC tuone tutakavyolitatua.”

“Tambueni yule ni kamanda wa jeshi. Tukiitaarifu serikali ya DRC watashikwa na butwaa, imekuaje mtu wetu ameingia kwao, hivyo itawalazimu waingie kazini kupeleleza. Na kama wahusika ni waasi, tukiiambia serikali, mlolongo utakuwa mkubwa wa kufanikisha tukitakacho.

“Hamna namna, zaidi ya kuruhusu vijana kwenda ili liwe zoezi la haraka na muda mfupi.” Akawasaili wajumbe wapokeavyo.

Kama walimwelewa.

Kwani wote walizama tafakurini kuchakata walichotaarifiwa. Ukimya ukachukua nafasi kwa mara nyingine.

Rais Luambano akaufukuza, “Nimekuelewa Fadhy. Upo sahihi. Na itakuwa vyema utekelezaji ukafuatia haraka iwezekanavyo.” Benson akamgeukia. “Yeah, tulibebe hili kwa mikono yote. Simu aliyopiga Frederka inahitaji msaada wetu, hivyo hayo mengine tuyaache pembeni.” Rais Luambano alikazia.

“Hivyo basi,” Fadhy akawashtua. Wote wakageuka kumwangalia, “Kama nilivyoanza kutoa dokezo, Askofu Ponera atatangulia na atatumia usafiri utakaomfikisha kwa uharaka-ndege. Wakati Luteni Ringo na Pte Pemba watasafiri kwa basi.”

“Huyu mwingine?” Benson akamwelekezea kidole Pte Bayo.

“Afya yake haiko vyema. Alipata madhara yaliyopelekea mwili wake kutokuwa sawa katika operesheni ya mwisho waliyoitekeleza,” Fadhy alijibu.

“Sina pingamizi na hiyo ramani. Nawatakia kila heri katika ufanikishaji. Mwenyezi mungu apate kuwatangulia,” Rais Luambano aliwatia moyo.

“Amina.” Askofu Ponera, Luteni Ringo na Pte Pemba wakaitikia kwa pamoja.

Kikao kikahitimishwa.

***

Mruko uliosababishwa na shambulizi lilimtua Koplo Fredreka kwenye tawi la mti mkubwa pasi na fahamu. Akakwama hapo na kuwa kama kuku aliyebanikwa. Wakati huo jeraha la kukitwakitwa kwa vyuma vidogovidogo vilivyotokana na shambulizi vikimpa majeraha kadhaa yaliyochangia kutokwa na damu.

wa-mama wawili wenye rika la miaka arobaini na tisa, waliowahi kwenye poromoko hilo kukusanya kuni asubuhi ya siku iliyofuata, ndiyo walikuwa wa kwanza kumbaini Koplo Frederka baada ya mmoja wapo kudondokewa na matone ya damu.

“He!” yule aliyedondokewa na damu alipigwa na butwaa, huku akiruka hatua moja ndefu mbele, kisha akaangazia matone yalipotokea.

“Nini tena?” mwenzie aliuuliza.

Badala ya kujibu, alimvuta na kumkumbatia, kisha akamhimiza mboni zake zielekee alipoelekeza kidole. Juu ya mti.

“Mama!” yule aliyevutwa naye akastaajabu.

Walistaajabu kuuona mwili wa Koplo Frederka kule juu. Staajabiko lililowapa hofu na kupoteza hamu ya kilichowaleta porini.

Wasichokijua, yowe walilopiga liliwafikia m-baba mmoja akadiriaye miaka hamsini na ushee pamoja na mtoto-apataye rika la miaka kumi na nne aliyambatana naye ndani ya poromoko hilo wakihangaika kutafuta kitu.

Kwa mwonekano wa mavazi, dhahiri yaliwaonyesha wao si watu wema. Yule m-baba alivaa suruali ya jeans rangi nyeusi, buti ya kijeshi, fulana mchinjo, koti rangi nyeusi lililoshuka hadi magotini, pasi na kusahau kapelo rangi ya hudhurungi. Mtoto naye alivaa namna hii. Tofauti ni rangi tu-yeye ilishamiri rangi ya samawati. Wote, walisundika bastola na ala yenye kisu kimoja kiunoni.

Uchangamfu wajihini kwao kilikuwa kitendo cha nadra mno. Mashavu yaliwatuna muda wote kama watu waliolishwa pilipili. Hali hiyo ilichangiwa na ukosefu wa kile wakitafutacho.

Kusikia sauti ya kike iliyoshamiri hofu iliwafanya wasitishe kwa muda zoezi lao. Walisimama, na kutega viwambo vyema kwa lengo la kusikilizia tena, lakini hakuna sauti iliyoendelea kusikika. Wakaingiwa na hofu kiasi, iliyosinyaisha mioyo yao na kujenga picha mbaya akilini kwa mtoa ukunga huo.

“Twende kwanza tukawaangalie hao,” yule m-baba alishauri. Mtoto kwake ni utii tu.

Wakabadili uelekeo wa safari. Mwendo nao ukiongezeka.

Baada ya kukata kichaka kwa takribani dakika nne, walifikia kwenye ule mti mkubwa uliokuwa na mwili wa Koplo Frederka. Wakasitisha mwendo, na kuangaza huku na kule. Macho zaidi ya mita mia moja. Walifanya kazi ya ziada kuushinda msitu.

Malalo ya nyasi ndiyo yaliyopelekea mwendo wao uishie mahali hapo. Wakahisi, wale waliopiga ukunga walikuwa hapo. Lakini isivyo bahati, hawakufanikiwa kuwakuta. Katika jitihada ya kuangazia huku na kule kwa uzungukiaji, yule mtoto akabaini lundo la damu umbali wa mita tatu toka kwenye shina la mti.

“Kuna damu hapa,” akamtaarifu yule baba. Kauli iliyomhimiza auache uelekeo aliopo na kukimbilia pale kwa mtoto.

Akajihakikishia. Na kwa uthibitisho zaidi, alikihimiza kidole chake cha shahada kuigusa na kuisigina sigina kwa vidole viwili. Aliporidhishwa na kitendo hicho, akainua mboni kuangazia mbele yao. Umbali wa mita moja toka walipo kulikuwa na lundo lingine la damu. Wakashawishika kulisogelea.

Napo alifanya kama pale pa awali. Huku mlalo wa nyasi ukizidi kuumba jambo akili mwao.

“Itakuwa wameelekea huku,” yule mtoto alieleza wasiwasi wake.

“Kwa hiyo unashaurije; Tuendelee na zoezi letu, au tulifanyie kazi hili tulilolibaini?” yule m-baba aliuliza.

Wakati huo mtoto amezielekezea mboni zake kwenye ule mti. Akabaini jambo lililompa dukuduku maradufu.

Akavuta koti la yule mzee na kumtaarifu jambo, “Hebu ona kile pale mtini.” Akamwelekezea kwa kidole sehemu ya kutazama.

Lahaula!

Walishuhudia michirizi ya damu.

Wakaparudia chap kupachunguza kwa umakini.

Naam, ile damu ilitiririka kutoka kwenye moja ya tawi. Wakazihimiza mboni kuangalia juu-chanzo cha ile damu.

Hawakuona kitu.

“Itakuwa ni yule tumtafutaye,” mtoto alitoa wazo.

“Hakika. Hata nami nimehisi hilo,” yule m-baba aliafikiana naye.

Dakika moja baadaye walitii takwa la mioyo yao, kuufuatilia ule mlalo wa nyasi wenye damu. Mwendo ukawa changamano; nusu kukimbia, nusu kutembea. Muda wote wakiwa na ombi la kumkuta wamhisiye-Koplo Frederka.

Ndiyo waliyokuwa wanahangaika kumtafuta. Lengo wajihakikishie ameshafariki. Kama bado, wammalizie. Kwani yule mtoto ndiyo aliyefanya shambulizi la kuishambulia gari waliyopo kina Brigedia Jenerali Buyoya kule Buyenzi. Yule m-baba ni ndugu na Brigedia Jenerali Buyoya.

Hivyo walikuwa kwenye kiu ya kuiadhibu serikali ya Tanzania ki-sawasawa.

Baada ya mwendo uliowachukua takribani dakika kumi na sita, mihemo ikiwa juujuu, jasho likiwatiririka kama wanariadha wa mbio ndefu, uchovu ukiwakumbata kwa kiasi, karibu na kuumaliza ukuta utengenezao poromoko, wakafanikiwa kuwaona wale wa-mama waliopiga ukunga. Mmoja wao alimbeba Koplo Frederka begani.

Morali ya kuwakaribia ikazidi kuwa juu. Vyote vya kuwanyong'onyeza wakavipotezea. Kasi ya utembeaji ikachukua nafasi. Hadi wanamalizia kuupanda ule ukuta na kuingia tarambare kuelekea makazi ya watu, wakawashuhudia wale wa-mama wakipotelea kwenye uchochoro kuingia zaidi kwenye makazi.

Wakafungua riadha, ambayo iliwahakikishia wawaonao hawatohisi jambo baya dhidi yao. Walipoufikia uchochoro ambao wale wa-mama walipotelea, mboni pima mbele, hawakuona mtu yeyote. Wakajihamasisha kusonga mbele zaidi lakini matokeo hayakubadilika.

“Hawawezi kufika mbali hivi bila kuwaona,” yule mtoto alitoa dukuduku lake.

“Kwa hiyo unahisi?”

“Watakuwa wameingia kwenye moja ya nyumba kati zile za nyuma.” Yule mtoto akageuka na kurejea kwenye nyumba azimaanishazo.

M-baba naye hakuwa na budi, alimfuata. Walipojumuika pamoja, wakayahimiza macho na masikio yanase yaendeleayo kwenye nyumba husika, lakini hawakuambulia cha maana zaidi ya ukimya. Jambo lililowakerehesha na kuwajaza kifua kwa sababu ya hasira.

TUKUTANE TOLEO LIJALO
Good start
 
NYAYO ZA JASUSI—02
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

M-baba naye hakuwa na budi, alimfuata. Walipojumuika pamoja, wakayahimiza macho na masikio yanase yaendeleayo kwenye nyumba husika, lakini hawakuambulia cha maana zaidi ya ukimya. Jambo lililowakerehesha na kuwajaza kifua kwa sababu ya hasira.

***

Wale wa-mama walimfikisha Koplo Frederka kwenye nyumba ya mmoja wapo. Nyumba ya hadhi ya kawaida iliyoakisi hali ya maisha ya mhusika. Ilipauliwa kwa bati mchanganyiko wa rangi, chini; pande mbili tope, nyingine tofali. Walimtua kitandani, kisha wenyewe wakajitupia sakafuni mihemo ikiwa juujuu-kutokana na wingi wa nguvu walizozitumia katika ubebaji.

Wakatua pumzi kwa nguvu kuutuliza mwili. Muda wote mboni kitandani walipomlaza Koplo Frederka.

Miili ilivyopoa walijiinua kisha kumsaili Koplo Frederka kwa kumgusa hapa na pale. Bado alikuwa yu’hai.

“Kalete maji-chumba kinachofuata hapo,” mwenye nyumba alimwomba mwenzie. Wakati huo akimvua baadhi ya nguo Koplo Frederka ili aingiwe na hewa ya kutosha mwilini.

Mwagizwa alifanya kitendo kile kwa haraka sana. Alirejea akiwa na ndoo ya lita kumi yenye maji kiasi.

“Sasa wewe mmwagie mwagie hayo maji, kuna kitu naenda kuchukua mara moja chumbani.” Mwenye nyumba akamwachia mwenzie nafasi na kupotelea alikokusudia.

Aliporejea, alikuwa na fuko dogo lililo na utuno kiasi. Akalitua kitandani, kisha kulifungua. Madawa mbalimbali ya asili na kitaalamu yakajibainisha. Wakati huo Koplo Frederka alishaanza kuweweseka kitendo kilichoinua matumaini kwao na kuongeza morali ya wakifanyacho.

“Futa damu hizo sehemu za majeraha.” Mwenye nyumba akamtupia mwenzie kitambaa, pindi mwenyewe akijihangaisha kuchanganya changanya baadhi ya dawa.

Zoezi hilo lilichukua muda mfupi tu, baada ya hapo walimpaka ile dawa sehemu zenye majeraha na mauvimbe, kisha wakajipa subira kumtazamia.

Tofauti na matarajio yao, kadri sekunde zilivyozidi kusonga mbele ahueni haikupatikana kwa Koplo Frederka. Tiba haikufua dafu. Hali ilizidi kuwa mbaya. Alianza kutetemeka. Kijasho kikamtoka kwa wingi. Macho yakamtutumuka kama mgonjwa kifafa kiasi cha kuwafarakanisha wale wa-mama.

Wakavutana nje ya chumba, mboni wamezielekeza kumwangalia Koplo Frederka ahangaikavyo.

“Una uhakika na tiba yako? Hili ni balaa ndugu, ooooho!” Yule mama mwingine alielezea mashaka yake. Kiroho kilikuwa juujuu. “Au mfumo wake wa uponyaji ndivyo ulivyo?”

“Hapana. Hiki nikionacho kwa huyu ni kigeni. Nimewatibu watu wengi kwa mchanganyiko wa hizi dawa kwa matatizo ya namna hii na wamepona.”

“Asije kutufia bure, kama vipi tumpeleke kituo cha polisi wakamhangaikie?”

“Polisi!” mwenye nyumba akashtuka. “Una wazimu? Tukimpeleka polisi si ndiyo tutakuwa matatizoni?”

“Fikiria kuhusu kutufia mikononi, hapo si ndiyo tutakuwa hatari zaidi.”

“Aaah, huwezi kunishawishi kirahisi hivyo kuhusu mambo ya polisi. Ni heri tumrejeshe kulekule porini.” Mwenye nyumba akapotelea nje. Mwenzie akamfuatia.

Ile hali haikumchukua Koplo Frederka kwa muda mrefu. Akatulia. Uangavu wa kuona ukajiimarisha kwa kiwango cha wastani. Akili ikapambanua kwa shida kile kilichoongelewa na wale wa-mama pindi yupo kwenye utete.

Hitajio la kuwa salama likakumbata kingo ya ubongo wake na kumjaza matamanio yaliyomsukuma kwa kiasi kikubwa ayatekeleze. Alijiinua, kisha kwa msaada wa kujishikiza ukutani, akaondoka mle chumbani. Mwendo ni mchechemeo, ulioupa meno kazi ya ziada kuyaumanisha kwa nguvu kama tiba ya upoozaji wa maumivu.

Ijapokuwa kwa shida, lakini alifanikiwa kutoka chumbani na kuufikia ushoroba uliotenganisha vyumba. Viwambo akavisimamisha kidete ajaribu kunasa ya wenyeji wake kule nje, hofu nayo haikumwacha, asije kushtukiwa kisha nia yake ikaangukia pua. Nia ya kumfikisha nchini Tanzania.

Hakukata tamaa, alijikaza hadi akaufikia mlango wa nyuma wa ile nyumba. Ambao ulifungwa na komeo iliyomchukulia sekunde chache kuifungua kisha kuendelea na ondoko.
Wale wa-mama waligundua mgonjwa wao hayupo mle ndani kwa kuchelea. Jakamoyo likawapanda. Wakazunguka vyumba vyote kumtafuta, walipomkosa, waliyazungukia maeneo jirani lakini hawakufanikiwa.

“Itakuwa si mwema. Maana kuumia kote kule, ingelikuwa ni mwema angeliendelea kusalia pale ili ahudumiwe,” rafiki wa mwenye nyumba alieleza hisia zake baada mihangaiko iliyowachukua zaidi ya dakika kumi kumtafuta Koplo Frederka.

“Kwa hiyo kama sio mtu mwema...” mwenye nyumba alisema na kutulia kwa sekunde chache, akamsaili mwenzie kwa tuo kisha akaendelea, “Tusimruhusu afurahie uwepo wake mtaani.”

“Unamaanisha?”

“Tukatoe taarifa kituo cha polisi.” Wakasimama ghafla na kusailiana.

Mwenye nyumba akaendelea kufafanua, “Tufanye hivyo, kama ni mwema apatiwe haki yake.”

“Mimi sina shida,ni wewe tu.”

Dakika kadhaa baadaye wakaianza safari ya kuelekea kituo cha polisi. Walipowasili, wakapokelewa na yule m-baba aliyekuwa ameambatana na mtoto mshambuliaji. Alikuwa ni afisa wa polisi-mwenye cheo cha Sajini. Anafahamika kwa jina la Bunyoni. Umbo lake ni jembamba mrefu wastani.

Kuwazuga wale wa-mama, aliiandika ile taarifa kwenye daftari husika-OB (occurrence book) kisha akawaahidi litafanyiwa kazi dakika chache zijazo.

Na hakika ilikuwa hivyo.

Alilivalia njuga binafsi. Kwani aliondoka pale kituoni na gari yake wanguwangu hadi nyumbani kwake. Akabadili yunifomu akavaa nguo za kiraia, baada ya hapo alielekea aishipo yule mtoto. Afahamikaye kwa jina la Alain.

“Tuondoke,” Sajini Bunyoni alimwamuru Alain akiwa hajateremka garini.

Alain akampachika ulizo pindi akiketi sitini. “Kuna tatizo?”

“Nimefuatwa na wa-mama waliyombeba tumdhaniaye mkusudiwa wetu,” Sajini Bunyoni alijibu huku akiingiza gari kwenye uelekeo autakao.

Aliegesha gari umbali mfupi toka nyumbani kwa wale wa-mama. Wakateremka na kuingia mtaani kwa haraka mboni wakizizungusha kila sehemu.

***

Maumivu yaliendelea kumtafuna Koplo Frederka na kumfanya mwendo wake uwe wa shida sana. Mara kwa mara hakuacha kupumzika, mapumziko ya muda mfupi kisha kuendelea na safari. Safari iliyojaa hadhari, kwa kutojipitisha pitisha maeneo yenye mkusanyiko wa watu wengi.

Akiwa ameshatembea umbali mrefu, maeneo ya nje ya mji, uvumilivu ulimshinda akaamua kujipumzisha kwa muda mrefu. Pumziko lililomsafirisha namna atakavyopata mawasiliano yatakayomwezesha kufikika ofisini ili asaidike kurejea Tanzania.

Alikinaishwa na lile pumziko pindi jua limeshamezwa, na kiza kuchukua hatamu. Akajiinua, na kuendeleza safari kwa mara nyingine. Awamu hii alirejea katikati ya mji. Kwani huko ndipo alijihakikishia atapata akitakacho kwa haraka. Akazidi kusota kwa mchechemeo. Alipobaini mwendo huo pia huchangia maumivu kuongezeka, akavunja mti mdogo akautumia kwa kupata uwiano.

Akiwa ameshatembea takribani mita arobaini na ushee, wakati huo ameshayafikia makazi akapishana nao Sajini Bunyoni na Alain kwenye uchochoro. Wao wakiwa himahima kuelekea atokako. Kwa sababu hakuwa na mashaka nao akawachukulia kawaida. Lakini ghafla, akasikia mvumo wa vishindo vya nguvu vikimsogelea. Akasimama, akageuka nyuma na kusaili vinasababishwa na nini. Akawashuhudia wale aliopishana nao wakirejea.

Kwa sababu hakuwa na mashaka nao, akili ikamtupa haina haja ya kujihangaisha kwa lolote, zaidi ya kusogea pembeni awapishe. Na alianza kufanya hivyo, kwa kujisota sota hadi ukutani.

Wazo hilo liliyeyekua alivyopatwa na msisimko wa ghafla mwilini, kiasi cha kuona nywele zinamcheza.

“Yumkini wamekutana na jambo baya waelekeako ndiyo maana wanarudi kwa namna hiyo,” alijisemeza, na kuchukua maamuzi ya kujificha kwa haraka mno, kwenye kona chochoro nyingine mbele ya aliposimama awali. Chochoro ya mkono wake wa kuume.

Sala ikaanza, apitwe pasi na kuonekana.

Lakini haikuwa hivyo. Vishindo viliishia usawa uleule aliopo. Na kabla hajafahamu cha kufanya, aliishuhudia mikono ikisafiri kwa kasi kutoka kwa sajini Bunyoni iliyodhamiriwa kumpiga kabari ya shingo na kumgandamizia ukutani. Kwa ustadi wa mapigano aliyonayo, aliinamisha kichwa na mgongo kupitia katikati ya ile mikono na kumfanya aepukane na hila ya kwanza.

Mikono ya sajini Bunyoni ikapita kapa na kwenda kujipigiza ukutani. Kwa kuwa hakujiandaa na matokeo hayo, alipoteza uhimili na kuparamia kichwa cha Koplo Frederka. Alipotaka kujirudi ili apange mashambulizi upya, Koplo Frederka alivuta ule mti akaushindilia milikini kwa sajini Bunyoni na kuuchezesha chezesha.

Maumivu aliyoyasikia, hayakuelezeka. Kupooza, aliruka nyuma hatua kadhaa, akaisafirisha mikono kutuliza. Alain akachukua nafasi yake huku akichomoa kitu kiunoni. Kabla hajakimiliki vyema mkononi, Koplo Frederka aliusafirisha ule mti mfululizo na kumchabanga Alain usoni mapigo yasiyo na idadi.

Alijidhatiti kufanya hivyo ili wasitumie udhaifu wake. Baadaye akauelekezea ule mti shingoni. Akalisukumiza koo kiasi cha Alain kukosa uwezo mzuri wa upumuaji. Alipomwachia, Alain alianguka chini.

Akahamishia majeshi kwa sajini Bunyoni, alimchabanga mara kadhaa usoni na ule mti kisha akatokomea.

Kwa mwendo uleule, lakini alijitahidi kuongeza kasi kidogo, maumivu hakuyajali tena. Kikubwa uzima kwanza.

Baada ya matembezi ya dakika kadhaa, aliifikia barabara ya Av. De I'oua kisha akazidi kukaza msuli huku asielewe uelekeo vyema. Alipofika barabara ya Av. Du marais aliikuta semi trailer imeegeshwa kando ya barabara wahusika wake; dereva na utingo wakihangaika kujaza maji kwenye rejeta.

Akashawishika kuitumia. Hasa baada ya kuona sahani ya namba ya ile gari. Namba ya ki-Tanzania.

Akajawa matumaini ya kuwasili nyumbani kupitia gari hiyo.

Akawasaili kwa chati, alipojihakikishia uwepo wake mahali hapo haujabainika, alinyatia kuelekea usawa wa tela. Akabana uvunguni kwa sekunde kadhaa, baadaye, alijivuta taratibu kwa msaada wa matairi kupanda. Haikumchukua muda, kuwa juu ya mzigo uliofunikwa turubai.

Bahati, alipata sehemu ya turubai iliyowazi, akaitumia kujificha.

Dakika kadhaa baadaye safari ikaanza. Koplo Frederka akamshukuru Mungu, kisha akahangaika aupate mlalo utakaompatia usingizi murua.

ITAENDELEA...
 
NYAYO ZA JASUSI—03
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

Soga zilichukua nafasi kubwa baina ya dereva na utingo wake kule mbele. Soga zilizojaa vicheko na kila aina ya hisia aipatayo binadamu ukiachilia mbali kulia. Walikuwa vijana halisi wa ki-Tanzania. Safari haikuwa fupi. Ni safari ndefu iliyowachukua saa nyingi huku wasijue waelekeako watawasili baada ya muda gani.

Alivyohisi Koplo Frederka kuwa safari ile itamfikisha nchini ambako atairejelea amani yake ya nafsi, haikuwa hivyo. Kwani walivyoiacha Bujumbura waliuchukua uelekeo wa nchini Rwanda hadi Butare. Hapo wakauchukua uelekeo wa Bukavu nchini DRC. Muda mwingi Koplo Frederka alikuwa mlalaji, ijapokuwa kuna muda aliamka, akajinyoosha nyoosha kidogo kisha kuendelea kuuchapa.

Naam, ilikuwa safari yenye mzunguko mrefu, na wakiwa mbioni kuumaliza mlima ili waingie Kashero, kiza kimefunga kisawasawa, mvua ikawalaki, maongezi yao yakakata ghafla baada ya kubaini mawe makubwa yamepangwa barabarani. Mapigo ya moyo yakawaenda mbio. Hofu ikawakumbata, mwendo ukapunguzwa huku wakiwazua watajikwamuaje kwenye kihunzi hicho. Kwani walifahamu fika, waliofanya hivyo si watu wenye nia njema.

Gari iliposimama wakatazamana kwa muda. Ishara tosha ya kuulizana wanatatuaje?

“Tujaribu bahati yetu, nenda kayaondoe ya upande mmoja tupate nafasi ya kupita,” dereva alimwamuru utingo.

Utingo hakutii kwa haraka, alizidi kumsaili dereva wake huku akipambanua amri aliyoambiwa. Mashaka yake yakajibainisha wajihini.

Dereva akatoa jambia pembeni ya siti yake, akamkabidhi.

Utingo hakuwa na budi, alifungua mlango, akateremka.

Kwa hatua fupifupi zilizojaa hadhari, kwani hakuacha kuangalia huku na kule kila muda kujihakikishia usalama wake, aliyafikia yale mawe. Hofu ikazidi kumpanda. Kiasi cha mwili kuchemka. Pasi na mvua, jasho lingejidhihirisha.

Hata dereva naye, muda wote kiroho kilikuwa juujuu, kwa hofu ya kumwona mwenzie akifanikiwa. Lakini isivyo bahati, pindi utingo akimalizia kulisukuma jiwe la mwisho upande wa gari lilipo, jambia amelilaza barabarani, akavamiwa na vijana wanne waliobeba bunduki za kivita. Utingo alipokumbuka jambia kwa nia ya kulichukua akabiliane nao, buti kubwa likatua juu ya jambia.

Utingo akashindwa kulichukua. Na kabla hajang'amua mbinu mbadala ya kujikwamua, pigo la buti likatua usoni na kumsukumizia nyuma. Akakosa uhimili, kitendo kilichomshinikiza ajipigize chini kwa utangulizi wa makalio.

Cha kufia nini?

Dereva akajihimiza kutafuta ustaarabu utakaomweka huru dhidi ya mabaradhuli hao. Akafungua mlango. Akiwa mbioni kuteremka baada ya kuushusha mguu wa kwanza kwenye kanyagio, alivutwa ule mguu na kumfanya ajipigize lamini kama hana akili timamu.

Kuna wavamizi wengine waliizingira ile gari. Na ndiyo waliofanya kitendo hicho. Wakapiga ukunga kushangilia, baadhi yao wakiruhusu mitupo kadhaa ya risasi hewani.
Makelele hayo yakamwamsha Koplo Frederka kule nyuma. Alivyofunua turubai ili ajionee kwa uzuri nini kisababishacho, miali ya tochi ikamwangazia. Alivyojaribu kukinga kwa mikono isimmulike machoni, alikishwachelewa. Kwani alichoropolewa kwa nguvu na kurushwa chini. Uzuri, alifikia vyema-kwa kutanguliza moja ya mkono kugusa chini na mguu kuundia umbo la goti.

“Aaah, walikuwa wanambaka dada yetu hawa ma-mbwa. Yaani wamembaka hadi wamemuumiza hivi?” mmoja wa wavamizi alisema. Walikuwa wavamizi sita; watano wa kiume, mmoja wa kike. Rika, walikadirika kuwa na miaka ishirini na ushee, kutoka kikundi cha waasi kifahamikacho NPF (National Patriots Front).

Wakamzingira Koplo Frederka kumsaili kwa uzuri.

Mwonekano wa maumivu waliyonayo wakafahamu utingo na dereva wake ndiyo wasababishaji.

Baadaye walifolenishwa pamoja huku wakiamriwa kupiga goti na kuita mvua. Kitendo walichokitekeleza kwa haraka mno ili wasiangukie kwenye kipigo zaidi. Wakati, maswali lukuki yakiwarindima dereva na utingo mwanamke huyo ameingiaje garini mwao na katokea wapi.

Hawakupata jibu la haraka. Wakabaki kumtumbulia pima, huku kijiba cha maulizo kumhusu kikijishindilia.

Dakika kadhaa baadaye waasi watatu walipanda garini na kufanya upekuzi. Vitu vyote vya thamani walivyokutana navyo wakavichukua. Walipoteremka, walitoa upepo kwenye matairi kwa mitupo ya risasi.

Mwisho wa safari yao ulikuwa hapo. Kama sio kuona mwisho wa maisha yao.

“Anga na dereva aje haraka sana,” aliyeonekana kuwa kiongozi wa wale waasi alimwamuru mmoja wao.

Aliyeamriwa alitii kwa kuvuta redio ya upepo aliyoipachika kwenye mkanda aliofunga kiunoni, akabonyeza moja ya kitufe kisha kutokwa na kauli. “Fanya hima, uwepo wako unahitajika eneo tulilopo, ova.”

“Aaah, romeo. Mike-mike kwenu, ova.” Mtu wa upande wa pili alijibu.

Haikuchukua muda mrefu, ikawasili gari dogo aina ya Toyota pick up double cabin pale walipo. Dereva, utingo na Koplo Frederka wakatwaliwa juujuu na kupakizwa garini. Wakafuatiwa waasi wenyewe kisha gari ikapotelea katikati ya msitu.

***

Nderemo zilitamalaki. Shangwe lilikosa kipimo; kwani makelele ya milio ya risasi, na vifijo vilihanikiza eneo zima la kambi ya waasi punde walivyowateremsha Koplo Frederka, dereva na utingo garini. Mitupo ya risasi ilisikika pasi na mpangilio. Ilitupiliwa hewani nyingine pande ambazo hakukuwa na watu. Walijitahidi kukwepesha madhara.

“Walete, walete, walete haooo...,” wengi wao walishangilia.

Shamrashamra hizo zilikoma, Koplo Frederka na wenzie walivyoingizwa kwenye moja ya jengo lililo na sifa toshelevu la gereza. Kwa mwonekano wa haraka lilionekana kujengwa kwa mawe kuanzia msingi hadi juu. Madirisha madogo, milango ya mbao nzito, yenye upana zaidi ya inchi nne.

Ndani, wakapokelewa na ushoroba uliotenganisha vyumba. Giza na harufu kali ikawakaribisha. Harufu iliyowachachafya nafsini lakini hawakuwa na uwezo wa kuikwepa zaidi ya kuvumilia. Wakasukumiziwa kwenye moja ya chumba, kisha mlango ukafungwa kwa kufuli kubwa.

Ukimya ukachukua nafasi kwa muda. Ukimya uliojenga fikra za matamanio kwa kila mmoja kufahamu la mwenzie. Dereva na utingo ndiyo walikuwa na uhitaji zaidi wa hilo. Kwani hawakuchukua muda mrefu, walipojihakikishia wabaya wao wamefika umbali wastani walisota hadi alipo Koplo Frederka.

Juu ya kiza kilichopo, lakini Koplo Frederka aliwaona wale watu wamsogeleavyo. Hakuwa na papara nao, ukamanda ulimsaidia. Hivyo hakuwa na hofu yoyote dhidi yao.

“Taratibu jamani,” Koplo Frederka aliwatuliza.

“Tuambie umeingiaje ingiaje kwenye gari letu,” utingo aliweka bayana hitajio lao.

Koplo Frederka hakuwajibu kwa haraka. Alijipa muda kutafakari, mihemko ya walio mbele yake ni ya namna gani. Lengo, wawe watu wanaozungumza lugha moja katika sakata hilo.

“Si tunakuuliza wewe malaya?” awamu hii utingo alifoka.

“Niliingia kule Buyenzi mlipoegesha gari.”

Dereva na utingo wakastaajabu. Kabla staajabiko lao halijajikitisha mizizi, Koplo Frederka akaendelea kuwaeleza, “Nataka nifike Tanzania.”

“Sisi safari yetu haikuwa ya kuelekea huko, ni heri ungetuomba usingeingia kwenye hii dhahma,” dereva alimhurumia.

“Kwani hapa ni wapi?”

“Tupo Kivu kaskazini-uwanda wa Goma.”

“Kwa hiyo wewe ni mtanzania?” utingo alihoji.

“Ndiyo.”

“Ilikuaje ukawa kule?”

“Ni habari ndefu.” Koplo Frederka akajinyongesha.

Na aliweza kuwahadaa.

“Mwombe Mungu kwa sana hawa jamaa wasiwe wajinga.”

“Unamaanisha nini?”

“Kwani hufahamu desturi ya waasi? Ndiyo hawa sasa. Tumeingia mikononi mwao,” utingo alizidi kuonyesha wasiwasi alionao. Akarejea alipoketi awali. Dereva akafuatia.

Ile hasira dhidi yake ikawatoka. Wakapatwa na fikra namna hatma yao itakavyokuwa kutoka mikononi mwa waasi hao. Fikra zilizofifisha kope na kuruhusu ulegevu wa mboni. Wakati nafsi ikitapakaa hofu.

Baadaye walipitiwa na usingizi.

Pindi wao wakiusaka usingizi uliotawaliwa mang'amung'amu, wale waasi waliowateka walifunga safari kurejea eneo walipoiacha ile semi. Awamu hii walioondoka katika magari sita aina ya Toyota landcruiser double cabin. Walipowasili eneo kusudiwa, walichumpa chini kwa haraka wakavamia sehemu ya tela kwa kulichana chana turubai. Mzigo uliopakizwa ukajibainisha. Magunia ya mahandi.

Wakajigawa; baadhi kuteremsha magunia na kupakiza kwenye gari walizokuja nazo, wengine walikesha kurekodi tukio hilo kwa simu janja zao.

Shamrashamra ikawa sehemu ya tukio hilo. Walivyotosheleza kwenye magari yao, walilichoma moto lile semi na magunia yaliyosalia kisha walichukua uelekeo wa kambini kwao.

Kabla hawajawasili kambini kwao, viherehere miongoni mwao wakapandisha video mtandaoni. Ikatapakaa kwa haraka. Sio DRC tu, ukanda mwingi wa nchi za kiafrika. Kwa watanzania, mapokeo yakawa tofauti. Kwani huruma na taharuki vilikumbata mioyo ya waliofikiwa na ile video na kuiona. Roho zilikuwa juujuu. Roho ya kisasi. Roho ya kuona waasi waliotenda tukio lile wanalipa kwa walichokitenda.

***

Mchana wa siku iliyofuata, Koplo Frederka alitolewa mle chumbani walipohifadhiwa akaamriwa amfuate mwasi aliyopo mbele. Nyuma, kulikuwa na mwasi mwingine; vijana tu, rika la miaka ishirini na mbili, kwa pamoja walibeba bunduki za kivita-aina ya AK 47.

Pingu zikaminya uhuru wa matembezi kwa Koplo Frederka; alifungwa miguuni, akafungwa mikononi. Hatua zikawa ndogondogo, udhoofu wa hali uliochangiwa kwa mawazo na ukosefu wa mlo sahihi ukamyumbisha huku na kule. Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, waliifikia gari dogo aina ya LX Toyota Land Cruiser iliyoegeshwa mita chache kutoka langoni mwa ngome, wakamsukumiza Koplo Frederka ndanimwe, walipomalizikia wenyewe, safari ikashika hatamu.

“Controller kwa escort two,” kijana aliyeketi siti jirani na dereva, alivuta kiwambo cha redio ya upepo akaita.

Ukiachilia mbali wale vijana wawili walioongozana na Koplo Fredeka kulikuwa na vijana wengine wawili garini; dereva, na aliyeonekana kuwa kiongozi wa msafara.

“Escort two ujumbe kwangu.”

“Aah, basi escort one ajiandae kwa mapokeo yetu, ova.”

“Roger. Roger.”

Akarejesha kiwambo mahali pake.

Wakiwa wameshaliacha eneo la kambi kwa mita kadhaa, yule kijana aliyeonekana kiongozi wa msafara, alifungua sehemu fulani ya dashibodi, akatoa mfuko wa kitambaa rangi nyeusi akaurushia siti za nyuma.
“Mvalisheni.” Akawasisitizia wenzie.

Koplo Frederka aliwekwa kati; baina ya wale vijana waliomsindikiza. Hivyo ilikuwa safari ya watu tano.

Mmoja wa wale vijana waliopo siti za nyuma aliuchukua ule mfuko akafanya alivyoamriwa. Utambuzi wa uelekeo kwa Koplo Frederka ukaishia hapo.

ITAENDELEA...
 
NYAYO ZA JASUSI—04
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

Wakiwa wameshaliacha eneo la kambi kwa mita kadhaa, yule kijana aliyeonekana kiongozi wa msafara, alifungua sehemu fulani ya dashibodi, akatoa mfuko wa kitambaa rangi nyeusi akaurushia siti za nyuma.
“Mvalisheni.” Akawasisitizia wenzie.

Koplo Frederka aliwekwa kati; baina ya wale vijana waliomsindikiza. Hivyo ilikuwa safari ya watu tano.

Mmoja wa wale vijana waliopo siti za nyuma aliuchukua ule mfuko akafanya alivyoamriwa. Utambuzi wa uelekeo kwa Koplo Frederka ukaishia hapo.

Ilikuwa safari iliyowapitisha kwenye kila aina ya msitu.

Baada ya matembezi ya kilomita kadhaa, wakiwa katikati ya msitu mnene, miti imefunga pande zote za barabara, dereva alipunguza mwendo kisha kuigesha gari kando. Pindi walioketi siti za nyuma wakishikwa hamu ya kufahamu sababu iliyopelekea kitendo hicho, dereva na yule kiongozi wa msafara waliteremka na kupotelea hatua kadhaa toka gari ilipoegeshwa.

Wakajihangaisha kumwaga maji machafu.

Vijana waliosalia garini wakajihangaisha kwa kuinuka inuka kujionea wakifanyacho wenzao. Mmoja kati ya wale wa nyuma naye akajikuta amekabwa na haja. Akateremka, akapotelea wenzie walipo.

Kwa upande wa Koplo Frederka akili yake ilisafiri maili kadhaa kwa kuwazua hila itakayomwezesha kujiweka mbali na watu hao. Mungu amwezeshe mara ngapi? Kusalia kwa mtu mmoja mle garini ni nafasi tosha ya yeye kuwa huru, ukizingatia hakufahamu uelekeo wala dhamira ya safari. Akafunua kidogo mfuko, akapata mwanya wa kuona. Yule kijana aliyesalia garini hakuonekana kuwa makini naye.

Naam.

Naye aliitumia vyema nafasi hiyo. Akamalizia kuuvua kwa haraka ule mfuko akautupia pembeni yake. Mwasi alivyohamaki kwa kutaka kumkabili mfuko uendelee kuwa kichwani mwake, alimkaba kooni kwa kumsogeza karibu yake. Viganja vya mikono akaziba mdomo.

Mwasi alijitahidi kujinasua lakini kadri alivyofanya pilikapilika hizo ndivyo alivyozidi kujiumiza. Kwani chuma ya pingu ilimfukunyua fukunyua vilivyo shingoni kiasi cha kumpatia maumivu yasiyosimulika. Sambamba na hilo aliishiwa pumzi taratibu hadi akatulia. Koplo Frederka akaiondoa mikono yake, kisha alimpapasa kwa haraka akabahatika kukuta funguo na kiswaswadu-akavichukua. Miongonimwe, zilikuwepo za pingu.

Hakuchelea, alijifungua, baada ya hapo aliteremka kwa hadhari na kupotelea upande wa pili wa msitu.

Wale waasi wengine waliporejea ili waiendeleze safari, walistaajabu kumkuta mwenzao yupo mbali na uhai na mateka wao hayupo. Mapigo ya moyo yakawabadilika. Yalienda kasi huku kifua kikijaa kwa namna wahemavyo. Mwonekano wa sura nao ukawabadilika, walidhihirisha unyama uliowagubika.

Kwa sekunde kadhaa akili yao ilibadilika pia. Sehemu kubwa ilitawaliwa na kuchanganyikiwa, hasa ukizingatia wamefanya uzembe. Ilivyojirudi, walivuta chuma walipozihifadhi wakazama msituni walikoamini Koplo Frederka ameelekea. Gari waliiacha palepale.

Mwendo ukawa wanguwangu, muda mwingine waliruhusu mitupo kadhaa ya risasi kwa kufuata uelekeo wa kati, kimo cha mtu atembeapo. Ilikuwa mitupo ya ubahatishaji, kwamba yumkini zitampata. Ama kule aliko, asikiapo milio asiwe mwenye amani tena na mwendo wake.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, jasho limewatoka chapachapa, kwa mbali miguu ikiingiwa na unyong'onyo, wakafanikiwa kumwona Koplo Frederka amejituliza chini ya mti mkubwa akiwasiliana na mtu kwa njia ya simu. Wakapunguza hatua wamvizie. Lakini hila hiyo haikufua dafu, kwani tayari walikwishaonekana. Hivyo Koplo Frederka alijiinua na kukimbia. Ijapokuwa si mbio yenye kasi. Mbio mchechemeo.

Wapoteze tena?

Wale waasi hawakukubaliana na hilo. Waliruhusu mitupo ya risasi kumwelekezea nao wakiwa himahima kwa mbio kumkimbiza. Namna wamkimbizavyo na ile mirindimo ya risasi utadhani wanashambuliana na kundi pinzani. Mirindimo ilishamiri huku wakipangiana majukumu yatakayosaidia kuushinda mchezo huo kwa haraka.

Lakini ikawa tofauti na matarajio yao. Koplo Frdereka aliwachezesha kama watoto wadogo mle msituni. Hawakubahatika kumsogelea, na shabaha zao zilienda mrama. Ni chache, zilizobahatika kupita karibu na Koplo Frederka. Nazo zikaishia kukita kwenye miti.

Uhitajika wa nguvu kuongezeka ukaonekana.

Na ulitekelezwa kwa haraka na yule kiongozi wa msafara kwa kuvuta redio aliyoipachika kiunoni. Akabonyeza moja ya kitufe, akaanga na mtu wa upande wa pili. Wakati huo amepunguza hatua, wenzie ndiyo walionekana kuvalia njuga kwa ufasaha zoezi lililopo.

“Controller kwa escort two.” Akaachia kile kitufe kumpa nafasi mtu wa upande wa pili kusikika.

“Ujumbe kwangu.”

“Aaah, safari imeingia doa...” redio ikakoroma kidogo kuashiria kuna shida ya kimtandao. Iliporejea, aliendeleza taarifa. “...mamluki amefanya jinai kwa kuondoa uhai wa mpiganaji wetu na kutokomea. Hapa tulipo, ni himahima kufuata nyayo zake, ova.” Akaachia tena kile kitufe.

“Aah, roger. Umesomeka kwa nguvu ya tano. Taarifa, mezani kwa kamanda hivi punde, ova.”

“Aaah, roger. Roger.” Akairejesha redio kiunoni. Aliipachika usawa wa mbavu. Kisha akaunga kushirikiana na wenzie.

Aliyepokea ile taarifa upande wa pili, kijana mwenye rika la miaka kumi na tisa-mrefu-mweusi, mara baada ya kukitua kiwambo cha redio mezani, akiwa kwenye chumba cha ukubwa wastani kilichotawala mitambo kadhaa ya kimawasiliano, aliondoka wajihi ukiwa umesawijika kiasi.

Akapotelea chumba cha tatu toka alichopata kuwepo.

Akapokelewa na m-baba mwenye mwonekano wa miraba minne, mfupi-mweusi. Rika miaka hamsini na ushee. Alikuwa anazunguka kitini nyuma ya meza, mdomo ukihangaika hangaika kuututumua moshi auvutao kutoka kwenye sigara kubwa.

“Kuna tatizo?” yule m-baba aliuliza, wajihi umefura, macho mekundu kama amevilia pilipili. Akasitisha na zoezi la kuzunguka.

“Ndi...yo kamanda,” yule kijana alijibu, sauti ikiwa na kitetemeshi kiasi. Akatingisha kichwa juu-chini kukazia. Wakati huohuo harufu na moshi vikimshinikiza kukohoa.

M-baba wa miraba minne akanyoosha mkono kumwelekeza kijana mahali pa kukaa.

Mandhari ya kile chumba hayakuwa nadhifu. Hakukuwa na mpangilio mzuri wa vitu. Kwani ukiachilia mbali meza na kiti alichokalia mhusika, kulikuwa na sofa lililofubaa pasi na kusahau kabati ndogo lililopangwa mafaili.

Yule kijana akaketi sofani. M-baba akapigiza mikono juu ya meza, na kuufanya mwili upunguze umbo kidogo kwa kwa kumsaili kwa umakini yule kijana.

“Nimepokea taarifa kutoka kwa escort two...”

Yule m-baba akadakia, “Nimewahimiza wawahi hapa haraka iwezekanavyo, nimwone huyo mlimbwende.”

“Sasa matokeo hayapo kama utarajiavyo.”

“Unamaanisha nini?”

“Mkusudiwa amefanya mauaji ya mmoja kati ya vijana wa usindikizaji na ku...”
Yule m-baba akainuka wajihi umezidi kufura, kwani taarifa haikuwa ridhisho. Akamtolea mboni kali mtaarifu mithili ndiye mtenda kosa. Jambo lililozalisha ukimya kwa muda, karibu na kushika hatamu, akaufukuza.

“Waamuru vijana waongezwe msituni ili huyo mwanaharamu apatikane kwa haraka.” Yule m-baba akaondoka hadi dirishani, alisogeza pazia pembeni kidogo, akapata taswira ya nje. Mandhari ya mji.

Jengo walilopo lilikuwa la ghorofa moja.

Kijana mwambiwa hakusubiri, naye akajiondoa kwa hatua fupifupi zenye uharaka. Alipoufikia mlango, akasitishwa hatua kwa mwito wa yule m-baba-aliyepambika kwa kaptura ya jeans rangi ya samawati, na fulana mchinjo yenye mchanganyiko wa rangi ya kombati ya kijeshi.

“Sikia...” akageuka kumwangalia yule kijana. Kijana naye aligeuka, utii kwa bosi yake. “...si alikamatwa na wenzie yule?”

“Ndiyo kamanda.”

“Wawasilishwe kwangu haraka.”

“Hamna shida bosi.” Kijana akaondoka.

Utekelezwaji wa kilichoamriwa kilifanyika dakika chache baadaye. Vijana kadhaa walielekea msituni, kule Koplo Frederka alipopotolea, na wengine waliwawasilisha dereva na utingo wa semi mbele ya yule m-baba wa miraba minne.

Wakafungwa vitini kwa kamba ngumu na kuhifadhiwa moja ya chumba kwenye lilelile jengo lililopo mkabala na hospitali ya General Goma. M-baba wa miraba minne aliingia dakika nne baadaye toka walivyowasilishwa. Akavuta kiti, akaketi mbele yao. Meza ikawatenganisha.
Muda wote hofu imewakumbata.

Mazingira ya chumba; ukubwa haukutofautiana na ofisi ya yule m-baba. Unadhifu pia ulikuwa haba, kwani vumbi lilitamalaki kiasi cha kutotamanisha kwa makazi ya aina yoyote.

“Nimewaita ili tufahamiane kidogo,” yule m-baba aliwataarifu. Na kufanya mioyo ya dereva na utingo itulie kiasi.

“Yule dada mliyompakiza kwenye gari yenu ni nani?” m-baba aliendelea kuwauliza. Akawatumbulia mboni kali za umakini.

“Hatumfahamu,” utingo alijibu.

Yule m-baba akaghafirika kwa muda. Jibu alilopatiwa si tarajiwa, alilojiandaa nalo kulipokea. Hivyo ukimya ulichukua nafasi kwa muda.

“Nawauliza kwa mara nyingine, yule dada ni nani?”

Dereva akadakia, “Hakika hatumfahamu...” Hakuhitimisha kauli yake, akakatishwa na yule m-baba baada ya kupigiza viganja vya mikono yake mezani kwa nguvu. Wajihi ukambadilika, matuta ya hasira yakatutumuka. Mboni akazitoa kama mtu aliyebanwa korodani. “...kweli kamanda, sisi hatumfahamu, tumemwonea pale tulipokamatiwa.” Dereva alikazia.

Yule m-baba akazidi kuwasaili kwa mboni ogofya.

“Hii mara ya mwisho, yule dada ni nani?”

Namna swali hili lilivyoulizwa kwa msisitizo ubaridi wa hofu ukaanza kuwatapakaa dereva na utingo wake. Mwendelezo wa maisha yao waliamini unaenda kuishia hapo. Waliposailiana, kila mmoja akabahatika kuiona hali ya mwenzie. Wafanyaje kujinusuru?

Machozi yakaanza kuwatiririka. Harufu ya kifo iliwakurubia.

“Kilio sio suluhisho kwenu. Nielezeni yule dada ni nani? Maama hawezi kumuua kijana wangu halafu...” yule m-baba akawafungukia kilichowafanya wawe mahali pale. Taarifa iliyozidi kupigilia msumari wa kutourejea uhuru wao mpaka atakapopatika Koplo Frederka. Ama la, wanaweza kujumuishwa kwamba walikula njama pamoja.

Yule m-baba akavuta saraka, akatoa rungu lenye urefu wa nusu mita akalipigiza kwa nguvu mezani. Mboni, akazidi kuwakodolea dereva na utingo.

Hakuonekana mwenye matani. Na ndivyo alivyo toka ajihusishe na shughuli hiyo sasa.

Naam, ni Kanali mstaafu wa jeshi la DRC-FARDC (Forces armées de la république démocratique du congo) kamandi ya ardhi. Kifwa Kabarebe.

ITAENDELEA...
 
NYAYO ZA JASUSI—05
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

Machea Hassan; mwanaume mwenye umbo nene wastani, mfupi-mweusi, akadiriaye miaka hamsini, mmoja kati ya wafanyabiashara wakubwa nchini Tanzania, makazi yake ya biashara yakiwa jijini Dar es salaam, ndiyo mmiliki wa ile semi iliyochomwa moto na waasi chini ya umiliki wa kampuni ya Machea Logistic. Taarifa ya tukio hilo ilimfikia asubuhi akiwa ofisini, baada ya kuperuzi peruzi yaliyojiri mitandaoni.

Kwa ughafla wa taarifa hiyo, moyo ulishindwa kuhimili na hatimaye kuruhusu upotevu wa fahamu. Bahati, pindi anadondoka, mshindo ulisikika kwa mmoja wa wafanyakazi aliyepita karibu na ofisi hiyo. Hivyo mapema tu, aliingia ofisini kujionea kilichosababisha.

Alivyomkuta Machea pale chini pasi na fahamu akawataarifu wenzie kisha walishirikiana kumwahisha hospitalini. Akazinduka saa nne baadaye.

Alipopata ahueni kwa mapumziko ya dakika kadhaa, watu mbalimbali anaofahamiana nao wakamiminika kumjulia hali. Hasa wafanyabiashara wenzie.

“Mnh! Unaamuaje kuhusu hili?” mmoja wa wafanyabiashara alimdadisi alipomtembelea.

“Nashindwa kuelewa, hao waasi hupendezewa na magari yangu tu?” Machea alitoa uchungu uliomsibu.

“Jaribu kuiomba msaada serikali ikusaidie. Ule upuuzi hauvumiliki, umefikia wakati wa kuukataa.”

Machea akasonya kwanza, “Yaani...” hakumalizia, kilio kikamkamata.

“Vumilia ndugu, kwa hili tuko pamoja hadi tone la mwisho litakalotuhakikishia ushindi wako,” yule mfanyabiashara alimliwaza huku akimpapasa papasa begani.

Hali yake ilipotengemaa aliruhusiwa kurejea nyumbani. Kabla hajapoa, Fadhy akamtembelea. Akajitambulisha kama afisa mwandamizi kutoka wizara ya mambo ya nje. Lengo la ujio wake ni kumtuliza Machea asihangaike hangaike kwenye vyombo vya kisheria kufuatilia suala hilo, kwa sababu linaweza kugharimu sehemu ya misheni iliyopo mkononi mwake.

“Kwa hiyo safari ilianzia wapi?” Fadhy aliuliza, viwambo amevisimamisha chechemaa.

“Nina tenda ya kupeleka mahindi Bujumbura na Goma. Hivyo lile gari lilikuwa linatokea Bujumbura. Inauma sana afisa, ukizingatia sio gari la kwanza kufanyiwa vile?”

“Kuna mengine?” Fadhy akabadili mkao, akakunja mzungu wa nne.

“Kuna magari matatu hapo nyuma yamefanyiwa kitu cha namna ile. Na ni uwanda huohuo. Sijui niwafanyaje hao wajinga wanaofanya unyama huo? Maana wanaendelea kudunda.”

“Nimekuja hapa kama wizara, tuko pamoja nawe. Hili jambo hatutolifumbia macho. Kikubwa, ziba mdomo ili tupate nafasi ya kulitendea kazi kwa ufasaha na manufaa makubwa.”

“Msaada wenu ni wa muhimu. Fanyeni jambo kunirejeshea amani yangu.”

“Hamna shida. Hii ni kadi yangu ya mawasiliano, kwa lolote lenye wasiwasi usisite kunitaarifu.” Fadhy akatoa kadi kwenye kibeti, akamkabidhi. Baada ya hapo aliaga na kuondoka. Ukomo wa safari yake ukawa ofisini, akakutana na Bayo, wakajenga himaya ya mazungumzo.

Kusikika sikika kwa lile tukio la gari kuchomwa moto ingelikuwa ni jambo baya kwa IMI. Kwani waasi wangelitumia taarifa hizo kuzidi kujipanga, hivyo kina Askofu Ponera, Luteni Ringo na Pte Pemba wangelikuwa na mzigo mkubwa wa majukumu ya kumpata Koplo Frederka. Fadhy alihitaji waasi wasiwe kwenye umakini wa namna yoyote ile, ili vijana wake watimize majukumu haraka. Hakuhitaji waasi watengeneze umakini utakaodhibiti njia za usafiri katika kujilinda, ndiyo maana alimwahi Machea.

“Machea amekubaliana nami, sasa ni wajibu kuwahimiza wenzio wawe watulivu katika utekelezaji,” Fadhy alifungua mazungumzo.

“Kuhusu vijana wake; dereva na utingo?”

“Nimemhakikishia kumsaidia. Hivyo tutaona namna kwa baadaye pindi hili letu tumelitimiliza.”

“Sio tufanye yote kwa wakati mmoja?”

“Haitowezekana. Kuna sehemu tutazidiwa na kuwapa nguvu wapinzani wetu.”

Bayo akatingisha kichwa ishara ya kuelewa ufafanuzi aliopatiwa.

***

Askofu Ponera aliwasili jijini Kinshasa usiku. Aliwasili na ndege ya shirika la Ethiopia. Baada ya kukamilisha taratibu za kiusalama aliondoka uwanja wa ndege kwa teksi hadi hoteli aliyoifanyia booking iliyopo katikati ya mtaa wa Nguma. Alivyomlipa dereva teksi, alipotelea ndani ya hoteli. Ifahamikayo Mukina.

Hakutumia muda mrefu mapokezi, alivyojitambulisha tu, alihudumiwa kwa haraka kisha aliongoza chumba husika. Huko, baada ya kutua begi dogo mezani akakisaili chumba kilivyopambika. Kilikuwa chumba kilichopo sakafu ya kwanza, upande wa mbele ya jengo.

Zoezi la usaili halikumchukua muda mrefu. Na aliridhishwa na mazingira ya chumba kilivyo; kilipambwa kwa kitanda chenye ukubwa wa futi tano kwa sita, kabati mbili-ndogo, meza, kioo ukutani na picha za urembo zilizobandikwa ukutani pia. Alipohitimisha aliweka tuo dirishani, akafunua pazia, kisha kuangazia mandhari ya nje ya jengo yalivyopambika.

Usiku ule jiji lilinawirishwa kwa mataa.

Alipokinaishwa alijitupia kitandani. Akatua mhemo wa nguvu wa pumzi, baada ya hapo alivuta begi lake karibu naye. Aliliacha, alipopata alichokihitaji, kikaratasi kidogo kilichoandikwa namba.

Juu ya moja ya kabati lilipo karibu na kitanda kulikuwa na simu ya mezani, akaziandika zile namba, kisha kukisogeza kiwambo sikioni. Iliita kwa sekunde chache, baada ya hapo ikasikika sauti iliyojaa ngurumo kutoka upande wa pili. Sauti ya kiume.

“Askofu kwenye laini,” Askofu Ponera alijitambulisha.

“Ndiyo chifu.”

“Nimeshawasili. Tuonane kesho asubuhi hoteli ya Mukina. Nitakuwa mgahawani.”

“Copy and out.”

Askofu Ponera akakirejesha kiwambo mahali pake. Akakoga kuondoa uchovu, baada ya hapo akapiga mianguko kuusaka usingizi.

Kulipopambazuka, alijiswafi, akavaa mavazi yake nadhifu; suruali ya kadeti rangi ya kahawia, raba nyeusi kampuni ya Adidas, fulana-form six, akashushia kapelo kichwani rangi nyeusi. Alipojihakikishia mwonekano huo upo vyema kwenye kioo, aliondoka hadi eneo la mgahawa. Akachukua ukazi moja ya kona mwisho mwa ule mgahawa. Mhudumu alipomfikia kusikiliza uhitaji wake, akaagiza kahawa.

Dakika chache baadaye alitekelezewa uhitaji wake, kisha akaanza kujinoofisha taratibu kwa funda fupifupi. Muda mwingi mboni alizitupa langoni kusaili waingiao.

Zilipita takribani dakika nane toka alivyoletewa ile kahawa, akaingia kijana fulani aliyepambika kwa umbo jembamba, mrefu-mweusi. Kadirio la rika, ni miaka thelathini na ushee. Alikuwa amevaa suruali ya jeans rangi ya samawati, fulana rangi nyeupe, raba chini. Alivyoimaizi sura yake vyema akamfahamu. Akamnyoonyeshea mkono wa wito, na yule kijana kutii.

Yule kijana alivyochukua ukaazi, mhudumu akawatembelea.

“Naomba kahawa,” yule kijana akamwamuru mhudumu. Alipopotolea kutii agizo, wakachukua nafasi ya mazungumzo.

“Karibu sana Kinshasa.”

“Nimeshakaribia. Lakini sijaja kwa ajili ya starehe ndani ya jiji hili.”

“Mmnh!”

“Kuna asset yetu, inapaswa ipatikane.”

“Kwa hiyo mimi...” yule kijana akakatishwa kabla hajahitimisha kauli yake, kwa Askofu Ponera kukitoa kile kipande cha karatasi chenye namba na kukitua mezani.

Yule kijana akakisogeza karibu yake. Pindi anasaili kilichoandikwa, mhudumu aliyemwagiza akawasilisha hitaji na kuondoka.

“Nataka nipate taarifa za hiyo namba,” Askofu Ponera akamgutusha.

Yule kijana akamsaili Askofu Ponera kwa sekunde kadhaa. Usaili uliompa picha Askofu Ponera anafikiria hitajio lake.

Ukimya ukachukua nafasi. Karibu na kushika hatamu, yule kijana akatoa simu ndogo kwenye mfuko wa suruali aliyoivaa, akaitupia juu ya meza.

“Kwa mawasiliano yenye usalama, hii simu ni nzuri kwa matumizi.” Askofu Ponera akaichukua.

“Itakuwa vyema nikipata mrejesho wa kazi...”

Yule kijana akadakia, “ Haitovuka leo hii-hasa usiku.”

Askofu Ponera akatingisha kichwa kuafikiana naye. Baada ya hapo waliagana kisha kila mmoja kuchukua uelekeo wake.
Usiku ulipowadia walikutana kwa mara nyingine. Awamu hii ilikuwa umbali wa mita kadhaa kutoka pale hotelini alipofikia Askofu Ponera. Makutano yalikuwa ndani ya gari ndogo aina ya Mercedes-Benz c 300 4 matic sedan aliyofika nayo yule kijana-afahamikaye kwa jina la Jalana.

“Nimefanikiwa kupata detail husika,” Jalana alimtaarifu, kisha akatoa karatasi kutoka kwenye mfuko wa shati akamkabidhi Askofu Ponera.

Askofu Ponera kwa shauku aliyonayo alizihimiza mboni zake kwa haraka ubongo ufahamu kilichoandikwa. Akili ikapotelea huko.
“Mara ya mwisho kuwa hewani ni saa kumi na tano zilizopita. Ilisomeka mtaa wa du 20 Mai moja ya mtaa mjini Goma,” Jalana akamtoa Askofu Ponera kwenye umakini wa usaili wa ufafanuzi karatasini, akahamishia wajihini kwa Jalana. Kitendo kilichotengeneza ukimya kwa muda.

Jalana aliufukuza baadaye, “Vilevile ofisi imekuachia huu usafiri kwa ajili ya ufanikishaji wa zoezi lililopo mikononi mwako.”

Askofu Ponera akatingisha kichwa, wajihi ukapambika kwa tabasamu ishara ya kufurahishwa na uamuzi huo.

ITAENDELEA...
 
NYAYO ZA JASUSI—06
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

“Mara ya mwisho kuwa hewani ni saa kumi na tano zilizopita. Ilisomeka mtaa wa du 20 Mai moja ya mtaa mjini Goma,” Jalana akamtoa Askofu Ponera kwenye umakini wa usaili wa ufafanuzi karatasini, akahamishia wajihini kwa Jalana. Kitendo kilichotengeneza ukimya kwa muda.

Jalana aliufukuza baadaye, “Vilevile ofisi imekuachia huu usafiri kwa ajili ya ufanikishaji wa zoezi lililopo mikononi mwako.”

Askofu Ponera akatingisha kichwa, wajihi ukapambika kwa tabasamu ishara ya kufurahishwa na uamuzi huo.

***

Ilikuwa asubuhi siku iliyofuata, Askofu Ponera akiwa ndani ya gari, mwendo hahehahe akiutafuta uelekeo wa Goma. Safari aliyoianza saa 12 asubuhi, taarifa akiiacha kwa Jalana na Fadhy pia, kwamba kile alichotumwa kinaenda kutimilika. Muziki ulinogesha safari yake; kwa kusikiliza ladha mbalimbali zilizohifadhiwa kwenye diski mweko. Muda mwingi miziki ya wasanii wa Kongo ndiyo ilisikika. Kwani hata mavazi aliyovaa hayakumtofautisha sana na wanaKongo; alivaa kofia ya Yombe rangi ya kahawia, koti la jeans rangi ya samawati, shati la drafti rangi nyeusi-kwa kahawia. Suruali ya jeans pia. Iliyo na utambulisho wa bwanga.

Pia miwani ilikuwa sehemu ya upambaji wa mtoko wake siku hiyo. Miwani ya kijasusi, aina ya Mccoy ambayo mara kwa mara aliitumia kupiga picha maeneo apitayo. Haikuwa safari fupi. Ilikuwa ndefu, na ilimchukulia saa nyingi kuufikia mji husika. Ili asipate uchosho, muziki wa ki-lingala ukakonga ubongo na kufanya ajawe msisimko.

Aliwasili Goma usiku. Kabla ya kujihangaisha na kilichompeleka, akaenda mahali kupata chakula, shibe ilivyomchukua, alipumzika kwa muda garini baada ya hapo ndipo alielekea kwenye pointi husika iliposomeka simu aliyoitumia Koplo Frederka kwa mara ya mwisho. Alipoweka tuo alitazamana na kibanda kidogo cha fundi simu, takribani umbali wa mita arobaini, alipochukua ramani kujihakikishia, akajithibitishia yupo sehemu sahihi anayotakiwa. Akazihimiza mboni kusaili yaendeleayo.

Kwa muda mchache alioangazia mwenendo wa pale bandani, aliwashuhudia wataka huduma wakujavyo na kuondoka. Akanuia, wakishaisha, au kupungua, ndipo aende akafanye alichokidhamiria. Wakati huo akajipa zoezi jipya la kuwazua namna Koplo Frederka alivyohitaji huduma ya mhusika. Hakupata jibu dhirisho. Akaamua kufungua mlango ili akapate uhakika.

Alipoteremka garini, alijiweka sawa na kuondoka kwa hatua fupifupi. Alipopiga hatua kadhaa, akiwa ameshaziacha mita takribani nane toka alipoegesha gari, Landrover Tdi rangi ya kijani ikaegeshwa kwa kasi mbele ya lile banda la fundi simu. Kabla haijasimama vyema, vijana wanne walio na bunduki za kivita walichumpa na kuvamia pale bandani.

Wateja watatu waliopo hofu ikawatamalaki na kuondoka mahali hapo wanguwangu pasi na utimilizaji wa huduma zao. Ya nini waziuze roho zao kirahisi?

Wale wavamizi hawakuanza kwa usemi, kwanza waliuvaa wajihi uliopangika kwa matuta pajini, mtuno wa mashavu ulioonekana umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ubananishwaji wa meno ya pembeni. Hawako kwa masihara mahali hapo. Baadaye walijigawa kuyakabili majukumu yaliyowaleta. Wawili walimtwaa juujuu mhusika wa pale bandani, wengine walivunja vunja baadhi ya vitu vya wateja na viteleavyo huduma kwa nia ya kukomoa.

Askofu Ponera akasitisha mwendo na kujirudisha garini ajionee kitendo kile kwa uhuru zaidi. Ndani ya dakika moja, wale wavamizi-ambao ni waasi walikwishamtua yule fundi simu garini na kutokomea kwa mwendo waliokuja nao.

“Kazi imeshaanza,” Askofu Ponera alijisemeza, huku akiwapimia wale waasi waondokavyo.

Walivyofika umbali wa mita kadhaa, ushawishi wa kuwafuatilia ili afahamu hatma ya fundi simu ikamtamalaki. Akatekenya gari auanze mwendo. Pindi anaauachia mguu kwenye eksileta alishtuka kuona anagongewa mlangoni. Kutokana na giza, alishindwa kuiona vyema sura ya mtenda hilo. Na kwa mazingira yaliyojitokeza akaona asijenge taharuki itakayoshawishi atiliwe mashaka mapema.

Hivyo alifungua kioo na kumsaili mtenda tukio.

Alikuwa Kanali mstaafu Kifwa Kabarebe.

“Ndugu za masiku?” Kifwa alimsalimu, wajihi ukipambika kwa bashasha.

Askofu Ponera naye ikabidi aonyeshe ushirikiano kwa uchangamfu, ijapokuwa mtimani alijaa ghadhibiko.

“Ooooh, Kifwa.” Askofu Ponera aliita, huku akiteremka garini.

“Ndiyo mimi John Chiwa. Kifwa-wa kubeba.”

Wakakumbatiana. Kwa sekunde chache tu, kisha wakaachiana. Vicheko vya furaha vikitawala.

Askofu Ponera, au John Chiwa kama jina lake halisi linavyotambulika na Kifwa Kabarebe walifahamiana. Ni marafiki. Urafiki wao ulianzia walipokutana kwa mara ya kwanza kwenye mafunzo ya kijeshi nchini Jordan. Mafunzo ya Luteni usu (second commander).

“Kulikoni tena huku kwetu? Huogopi haya machafuko?” Kifwa alihoji.

“Nimekuja kwenye mapumziko kidogo. Si unajua siku hizi nimekuwa...”

Kifwa akadakia, “Askofu.” Akaangua kicheko kwa sekunde chache mboni zote ameziangazia kwa umakini kwa Askofu Ponera.

“Nawe una taarifa hizo?”

“Yeah, kazi ya Mungu haijifichi,” Kifwa alisema na kusita kwa muda. Kuna jambo lilimwingia akilini ghafla, alitamani kumwambia Askofu Ponera lakini akapotezea. Matumizi ya jina bandia. Iweje anatumia jina bandia katika kueneza neno la Mungu?

Alama ya hatari ikajijenga akilini.

“Huwezi kufika hapa ushindwe kupafahamu ninapoishi, naomba ukapaone, ikibidi upate japo ja-supu ndipo uendelee na ratiba zako,” Kifwa akabadili mada, ilihali nafsini alijawa fukuto tele la ufahamu wa Askofu Ponera ndani ya mji wao. Akilinganisha na kile kitendo cha kundi lake kuwashikilia wale madereva wa ki-Tanzania na kuchoma gari lao, mashaka yakamwongezeka kama ilivyo jadi ya wanausalama wote makini ulimwenguni.

Askofu Ponera hakuwa na pingamizi, akaafikiana naye. Sekunde chache baadaye wakaingia garini na kuianza safari. Kifwa aliketi nyuma ya usukani.

Kwa mwendo walioenda nao, ilikuwachukua takribani dakika nne kuwasili nyumbani kwa Kifwa, mtaa wa Uélé. Mandhari tu, yakamshangaza Askofu Ponera. Ilikuwa nyumba yenye hadhi zote za kuitwa kasri. Nyumba kubwa yenye ghorofa moja, iliyozungukwa na wigo wenye ulinzi wa nyaya za umeme, vijana waliobeba bunduki, kamera baadhi ya kona na mbwa wakubwa aina ya Labrador retriever.

Vilevile kulikuwa na bwawa la kuogelea, viwanja vya michezo; vya kikapu na pete.

“Karibu sana,” Kifwa alimkaribisha Askofu Ponera kwa bashasha pindi wakipotelea ndani.

“Hamna shida kaka, tuko pamoja,” Askofu Ponera akamwondolea hofu, lakini ile hali ya kughadhibika ikiendelea kumea. Amepoteza shabaha yake iliyomleta ndani ya mji huo.

Wakaweka ukomo sebuleni-sofani.

Baada ya kushusha pumzi za uchosho, waliandaliwa maakuli, wakayafakamia taratibu, huku mazungumzo yakitawala. Walikumbushiana mengi yaliyotokea pindi wako pamoja mafunzoni, sambamba na marafiki zao wengine waliopata kuwa nao.

Kilikuwa kitendo kilichochukua zaidi ya saa moja, kisha Askofu Ponera akaona ni vyema akaendelea na ratiba zake. Aliaga.

“Kwa hiyo utakuwa hapa mjini kwa muda gani?” Kifwa aliuliza.

Askofu Ponera alibana kingo za mdomo kwa sekunde kadhaa akitafakari cha kujibu, alipojiridhisha, alimjibu, “Niponipo. Maana nimekuja kuichangamsha akili kidogo. Sio izoee mazingira yaleyale kila siku.”

“Basi tutazidi kuwasiliana. Hii hapa kadi yangu ya mawasiliano,” Kifwa akamkabidhi ki-kadi Askofu Ponera.

Wakainuka na kupotelea nje.

Kifwa akaishia barazani, Askofu Ponera hadi alipoegesha gari yake. Alipofungua mlango tayari kwa kuingia, alishtuka vyuma vya baridi vikigusa shingo yake. Akaisitisha zoezi afanyalo, akageuka kujionea; alitazamana na mitutu ya bunduki. Vijana watatu waliochafukwa sura hadi roho walikamatia vyema Ak 47, ishara ya onyo kwake asithubutu kufanya jambo lolote.

Kabla hajang'amua sababu ya kufanyiwa vile, mmoja wao aliteremsha bunduki akaanza kumpekua. Akaviondoa vitu vyote alivyohisi ni hatari kwao; hasa bastola.

Askofu Ponera akazidi kustaajabu. Kulikoni? Ijapokuwa alipatwa na chipuo la kuhisiwa hila yake. Akageuka kumwangalia Kifwa.

Kifwa akakenua domo kwa dhihaka, kisha akatokwa na kauli, “John Chiwa, hebu njoo uniambie ukweli, nini kimekuleta ndani ya mji wetu?” Akaondoka pale barazani na kupotelea ndani.

Askofu Ponera akazidi kuduwaa. Huku asiamini kama kuna baya atakalofanyiwa na Kifwa kutokana na ukaribu waliopata kuwa nao. Alipokumbuka kuhusu kuchelewa kwa utimizaji wa malengo yake, akapatwa na hasira.

ITAENDELEA...
 
Mkuu tukumbuke kidogo wakati huu ambao tunawaza Gwajima yupi wa kumfuata.
 
NYAYO ZA JASUSI—07
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

Toyota hiace, iliyopambwa kwa rangi nyeusi ilichanja mbuga kuutafuta mji wa Goma. Luteni Ringo na Pte Pemba ni miongoni mwa abiria kumi na tano waliopo ndani ya gari hiyo. Kama walivyoamriwa na Fadhy, ndivyo walivyotekeleza. Walisafiri kwa basi kutoka jijini Dar es salaam hadi Kagera. Hapo wakaingia Rwanda kisha kuchukua uelekeo wa DRC.

Ilikuwa mchana, karibu na kuufikia mji wa Goma wakitokea Rukoko, gari ikasimama ghafla katikati ya msitu. Abiria waliopo wakaingiwa shauku ya kufahamu sababu, wakafungua vioo, kisha kuchungulia.

Hamadi!

Wakarudisha vichwa ndani kwa haraka na kufunga vioo.

“Wapiganaji wa msituni,” wakawahabarisha wenzao. Kitendo kilichotapakaza hofu kwa abiria wengine.

Luteni Ringo na Pte Pemba waliketi siti na upande tofautitofauti. Lakini wote, walikuwa usawa wa dirisha. Hivyo baada ya kusikia uwepo wa waasi wakafungua vioo kujihakikishia. Walipomaliza, walikonyezana. Ishara ya kufanya jambo litakalowaweka huru.

Kweli. Sekunde chache baadaye Pte Pemba aliondoka kwenye siti yake akahamia alipo Luteni Ringo. Wakanong'onezana jambo, kisha Luteni Ringo alifungua kioo wakachumpia nje.

Pindi mtu wa mwisho anamalizikia, Pte Pemba, waasi watatu wakaingia garini. Walikuwa wamebeba Ak 47. Mmoja wao ndiyo aliona kitendo kile. Akarudi nje kwa haraka wakati waliosalia wakijipa zoezi la usaili wa abiria waliopo.

Kwa namna walivyojawa sura ngumu, abiria walikesha kuwa na hofu muda wote.

“Waliokuwa wameketi hapa wako wapi?” mwasi mmoja wapo aliuliza alipofikia pale walipokuwa wameketi Luteni Ringo na Pte Pemba.

Akajibu abiria siti za nyuma kwa kitetemeshi, “Wame...wamekimbia kupitia hapo.” Akaelekezea mkono pale dirishani. Yule mwasi akachungulia. Hakujionea mtu.

Alijirudisha ndani, akamtaka mwenzie awe makini na wale abiria kisha akapotelea nje.

Luteni Ringo na Pte Pemba walivyochumpa hawakwenda mbali, walichukua maficho nyuma ya gari. Wakajipa utulivu na kuruhusu viwambo vinase hata vilivyo na mshindo mdogo. Wasikia zile purkashini za waasi wakujavyo. Wakajigawa; mmoja kona ya ubavu wa kulia, mwingine kushoto.

Jumla ya waasi walikuwa sita. Ukiachana na yule aliyesalia garini, tano wakajigawa kuwazungukia kina Luteni Ringo. Upande huu wawili, upande mwingine watatu. Na kutokana na ghadhibiko lililowapanda, hawakuwafuata kwa hadhari yoyote. Wataogopaje, wakati wao ndiyo wafalme wa mwituni?

Mwasi wa kwanza alivyokurubia aikamate kona upande aliopo Luteni Ringo, bunduki ikiwa usawa wa ushambuliaji, akiwa mbioni kukisogeza kidole cha shahada karibu na kifyatulio, Luteni Ringo aliukamata mtutu wa bunduki akauvuta kwa nguvu. Kwa sababu mwasi hakuwa na maandalizi yoyote ya kujikinga, ule mvuto ulimpelekesha akadondoka chini, bunduki ikasalia mikononi mwa Luteni Ringo.

Waliosalia wakajaa wenge lililowalazimisha wazidishe hatua kumfuata Luteni Ringo, naye kwa umaridadi wa hali ya juu, kabla waasi hawajajipanga kwa kushambulia, aliirusha ile bunduki ikatua usoni kwa aliyetangulia. Maumivu yaliyompata yakamsitishia mwendo, akadondosha bunduki ili ajipooze. Mwenzie akamsogeza pembeni apate nafasi ya kupita. Alivyofikia, akaruhusu mitupo kadhaa ya risasi iliyokosa shabaha. Kwani Luteni Ringo alizama uvunguni mwa gari na kutambaa kwa haraka akatokezea upande wa kulia wa gari.

Yule mwasi akaendeleza mitupo ya risasi, lakini isivyo bahati, ilitua sehemu ambayo Luteni Ringo alikwishaachia nyoya. Alivyotokezea upande wa pili, akawavaa vaa wale waasi wawili waliokuwa wanaugulia maumivu. Aliwatumia kama kinga dhidi ya yule aliyekuwa anamshambulia kwa risasi. Hivyo akampotezea umakini, nafasi iliyotumiwa vyema na Pte Pemba, ambaye alijitokeza kutoka upande wa pili, waasi aliokuwa anapigana nao hawakuweza mziki wake, wakaachia nyoya. Alimchapa teke la shingo yule mwasi akaenda kujipigiza garini. Bunduki ikamdondoka, sehemu ya kichwa ikampasuka, damu ikatafuta njia.

Yule aliyopo ndani ya gari, akatoka mkukumkuku kuongeza nguvu, lakini kabla hajawafikia, Pte Pemba aliokota bunduki akaruhusu mitupo kadhaa ya risasi kumfuata.

“Wasitupotezee muda,” Pte Pemba alishauri na kuwachapa chuma risasi kadhaa wale waasi.
Muda wote abiria walikuwa wenye kufumba macho kuepuka ushahidi. Mioyo ikiwa juujuu kwa hofu-watakuwa kwenye hali gani wakija waasi wengine? Ikabidi wamshinikize dereva aondoe gari.

Wale waasi wawili mwisho wa mbio zao ulikuwa kwenye gari waliyokuja nayo, ambayo waliiegesha katikati ya barabara mita kadhaa kutoka iliposimama hiace. Wakaingia kwa haraka na kutokomea. Kuona vile, kina Luteni Ringo hawakuangaika nao, walijitoma msituni na kupotelea huko.

Abiria wenzao walipowapigia makelele warejee garini, waendeleze safari, wala hawakuwatilia maanani.

Waasi waliokimbia na gari, walipofika umbali wa mita kadhaa, dereva akafunga breki ya nguvu kisha mmoja wao alivuta kiwambo cha redio aka-anga na wenzao.

“Wazalendo sita kwa wazalendo kwanza,” aliita. Neno wazalendo ni call sign watumiayo kama uwakilishi wa jina la kundi lao.

“Ujumbe kwangu,” yule wa upande wa pili alijibu.

“Aaah, hali ya usalama wetu sio mzuri. Kuna wavamizi himayani hivyo tunaomba back up.”

“Roger. Mnahitaji nguvu ya kiasi gani?”

“Itakuwa vyema mkija pointi nzima.”

“Tupe dakika tatu, tutakuwa hapo.”

Kweli. Ndani ya dakika zilizoahidiwa timu ya back up iliwasili walipo wale waasi watoa taarifa. Wakateta kwa muda, kisha wakaongozana kuirejea ile hiace.

Waliikuta palepale. Kitendo hicho kilichangiwa na ubishani wa abiria waelekee uelekeo upi utakaowaweka salama.

Hofu ikawarejelea zaidi ya mwanzo.

Kwani waasi waliwaamuru wateremke garini na kuketi katikati ya barabara kama fungu la nyanya. Kisha waasi walijigawa; wachache walisaili mazingira yazungukayo gari, wengine wakawalinda wale abiria. Kwa kuwaelekezea mitutu ya bunduki kama onyo wasithubutu kufanya hila ya aina yoyote.

Wale waliojipa zoezi la usaili waliungana na wenzao baada ya dakika kadhaa. Waliungana wakiwa wamechafukwa roho baada ya kukuta miili ya wenzao haina uhai. Kuchafukwa huko kulitambulika vyema na wale abiria, wakaona moto utawawakia. Uhakika wa kuwa salama ulikuwa ndoto moyoni mwao. Walitamani mbingu iwameze, ili wasichezee kichapo kutoka kwa watu hao.

“Wapo timilifu?” aliyeonekana kuwa kiongozi wa timu ya back up aliuliza.

“Hapana. Kuna watu wawili hawapo hapa.” Mwasi mmoja wapo wa timu ya mwanzo alijibu.

Yule aliyeuliza akauma meno na kutingisha kichwa huku akiwasaili wale abiria. Wote walijawa nyuso zenye huruma. Nyuso za kuomba wasamehewe.

“Wenzenu wako wapi?” yule kiongozi aliuliza. Swali lililotengeneza ukimya kwa muda kutokana na kukosekana kwa mjibuji. Wale abiria walitegeana.

“Si nawauliza ninyi?” yule kiongozi aliuliza kwa mara nyingine, awamu hii sauti ikimtoka kwa ukali zaidi. Kabla hajajibiwa, alitoa bastola aliyoisunduka kiunoni na kuruhusu mitupo kadhaa ya risasi kwa mmoja wa abiria. Ikampasua kichwa.

Abiria wengine wakapiga ukunga huku wakifunika uso kwa viganja vyao, damu isiwapate usoni. Hawakutarajia kuuona ukatili huo mbele yao.

Wengi wao abiria hao walikuwa raia wa Rwanda. Ni dereva tu ndiyo alikuwa m-Kongo.

“Ni nani na nani hao wenzenu?” yule kiongozi aliuliza kwa mara nyingine.

“Hatuwafahamu mkuu,” abiria walijibu kwa pamoja.

“Dereva kalete chati ya abiria.”

Dereva akainuka na kukimbilia garini. Alirejea baada ya dakika mbili baada ya pekuapekua za hapa na pale. Akamkabidhi yule kiongozi, naye aliita jina moja baada ya lingine.

Kama alivyotaarifiwa awali, kwamba watu wawili ndiyo hawamo, ndivyo matokeo aliyokutana nayo. Haikumsumbua kichwa. Kikubwa alichokihitaji ni majina ya wahusika tajwa.

“Isidor Kulyamo na Rajab Machemba-watanzania.” Luteni Ringo na Pte Pemba waliingia nchini humo kwa utambulisho bandia. Akaitupa ile karatasi kisha kuisundika bastola kiunoni. “Sam, hawa wafike kambini. Na huu usafiri wao haupaswi kuendelea na safari-uteketezeni,” yule kiongozi aliwaamuru wenzie. “ Peter na Davi mnifuate.”

Amri yake ilitekelezwa kwa haraka mno. Ile hiace ilichomwa moto. Kisha wale abiria walisagwa kuelekea kambini kwao. Kiongozi na wale vijana aliowaita wakazama mwituni uelekeo waliouchukua kina Luteni Ringo.

***

Luteni Ringo na Pte Pemba walikata pori kwa kila aina ya mwendo; kuna sehemu walikimbia, nyingine walitembea-kwa haraka na taratibu. Hofu hawakuwanayo kabisa. Bali walijawa furaha moyoni mwao kuwa wamewashikisha adabu wale waasi. Kwa nini wasijivunie?

Baada ya mwendo uliowachukua zaidi ya saa mbili wakaamua kupumzika. Kwani haukuwa mwendo mdogo. Walitembea sehemu ndefu sana kiasi cha kuwapa uchovu. Waliendelelea na safari uchosho ulipowapungua. Walikaza mikanda kwa mara nyingine, kisha kwa hatua asteaste zilizosindikizwa na soga za hapa na pale walizidi kuusogelea uelekeo wa mbele yao.

Kama mwendo wa dakika hamsini kutoka pale walipopumzikia, viwambo vikaruhusu kusikika kwa purkushani fulani zilizowatambulisha wapo karibu na makazi ya watu. Wakasitisha mwendo, kisha kujipa utulivu wa kusikia vyema. Zilisikika sauti za mifugo mbalimbali; ng'ombe, mbuzi, kuku n.k.

Wakasaili mienendo ya watu, walipojiridhisha ushwari umetamalaki, wakasonga mbele. Waliingia pale kijijini, hadhari wameikumbata ili wasifanye kosa litakalowagharimu.

Walipojichanganya mitaa ya katikati yenye uchangamfu kiasi, waliingia mgahawani wakapata chakula. Uzuri, hakuna mtu aliyewatilia mashaka. Na walijitahidi kujenga mazoea kwa haraka na mhudumu.

“Tunahitaji tufike Goma, wapi tutakapopata usafiri utakaotufikisha huko?” Luteni Ringo aliuliza, wakati huo walikuwa wanafanya malipo. Kwani hawakuchukua muda mrefu kumaliza chakula walichoagiza; wali maharage.

“Ninyi ni wageni hapa?” mhudumu aliwahoji. M-mama wa makamo.

Luteni Ringo alitingisha kichwa juu-chini, akafuatia kutokwa na kauli, “Ni wenyeji wa Kin...” hakuhitimisha, akakatishwa na milio ya magari matatu ya waasi yaliyowasili maeneo yale kwa mwendo wanguwangu. Moja ya gari hizo ilikuwa wmik.

Wote wakatekwa na tukio hilo.

Kabla magari hayajasimama vyema, waasi waliobeba bunduki za kivita walichumpa na kuzagaa sehemu mbalimbali huku wakiruhusu mitupo ya risasi hewani na kwa baadhi ya wananchi waliokuwa na mihangaiko yao.

Wakaijenga hofu ndani ya sekunde chache tu. Iliyopelekea mtafutano wa hali ya juu kutoka kwa wananchi kusalimisha uhai wao. Luteni Ringo na Pte Pemba nao hawakuwa nyuma katika hili. Walivutwa na yule mama muuza mgahawa wakaenda kujificha nyuma ya banda kulikokuwa na mzigo mkubwa wa magunia ya mkaa.

Kwa upenyo mdogo, wakawashuhudia wale waasi namna wamwagavyo damu za watu wasio na hatia. Iliwauma sana. Kiasi kwamba kuna muda walitamani wajitokeze wakamatwe ili wananchi wasiendelee kuteswa. Kwani walifahamu, kuwasili kule kumechangiwa na wao. Wanatafutwa.

Baadaye walishuhudia wanakijiji kadhaa wamekusanywa sehemu ya wazi wanahojiwa. Mahojiano yaliyojaa unyanyasaji. Kwani hawakuachwa kupigwa na vitako vya bunduki na wengine wenye kibri walipigwa chuma.

“Ili mbaki, elezeni hao watu tunaowatafuta wameelekea wapi. Hatupo hapo kuwabembeleza,” mmoja wa waasi alifoka. Kauli iliyofanya isikike na kina Luteni Ringo pale walipo. Hata yule mhudumu aliinyaka vyema, na kumpa ushawishi wa kuwageukia kina Luteni Ringo kama mtu anayeomba kuthibitishiwa alichokisikia.

“Shiiii, tulia,” Luteni Ringo akamsihi yule mhudumu. Akawa kama haelewi, kwani alizidi kuwashangaa.

“Tunakuomba, ututekelezee ombi letu la mwanzo. Tunahitaji tufike Goma,” Luteni Ringo aliendelea kumsihi yule mhudumu.

“Nifuateni,” mhudumu akakubaliana nao.

Walijiondoa pale mafichoni kwa unyapio wa kuzungukia upande mwingine wa banda ambao uliwaficha dhidi ya mboni za watu. Walipofika umbali fulani, banda wameliacha mita za kutosha, wakafungua riadha wakiongozwa na yule mhudumu. Ukomo ulikuwa mtaa wa tatu, ambako walikuta baadhi ya gari-hiace zikinadiwa kwa uhitaji wa abiria waelekeao miji mbalimbali.

Kwenye mtaa ule kulipoa kidogo, hakukuwa na kashikashi zozote za waasi.

Wakajitoma kwenye moja ya gari.

Ilikuwa kama wanasubiriwa wao, kwani walivyoingia tu, utingo alifunga mlango. Dereva akashika hatamu ya safari kwa kuuanza mwendo.

Wakiwa wamealiacha eneo la kituo cha hiace umbali wa mita kadhaa, mioyo ya Luteni Ringo, Pte Pemba na yule mama imejaa ahueni ya mafanikio, dereva akalishuhudia gari la waasi-wmik likija nyuma yao kwa kasi.

“Jamani, wafalme wa mwitu wapo nyuma yetu hapo wanakuja kwa kasi mbaya,” akawataarifu abiria. Nao wakageuka nyuma kuthibitisha.

Kabla hawajageuka kurejea awali yao, mitupo ya risasi ikamiminika kama mvua kwenye ile hiace.

ITAENDELEA...
 
NYAYO ZA JASUSI—08
MTUNZI: HASSAN MBONECHE

Wakiwa wamealiacha eneo la kituo cha hiace umbali wa mita kadhaa, mioyo ya Luteni Ringo, Pte Pemba na yule mama imejaa ahueni ya mafanikio, dereva akalishuhudia gari la waasi-wmik likija nyuma yao kwa kasi.

“Jamani, wafalme wa mwitu wapo nyuma yetu hapo wanakuja kwa kasi mbaya,” akawataarifu abiria. Nao wakageuka nyuma kuthibitisha.

Kabla hawajageuka kurejea awali yao, mitupo ya risasi ikamiminika kama mvua kwenye ile hiace.

***

Yale mashambulizi yalimpata Koplo Frederka sehemu ambazo sio hatarishi. Hivyo alimudu kupiga hatua na kusonga mbele. Sehemu zenye majeraha, alifunga kwa vitambaa alivyochana kwenye shati. Lakini maumivu hayakumwacha.

Alifika Goma mjini akiwa hoi. Maumivu ya majeraha yalimfukunyua ki-sawasawa. Kiasi kwamba aliona kama nyayo zinaungua moto. Uvumilivu ulipomshinda, alitafuta sehemu akachukua mapumziko.

Miungurumo iliyojikakamua tumboni ikamkumbusha uhitaji wa chakula. Ukijumlisha na hali ya maumivu ya majeraha ikamtaka kupata tiba itakayomfanya ajisikie mwenye unafuu kidogo. Atatimizaje matakwa hayo?

Tafakuri ikashika hatamu.

Kupambanua mbinu itakayomwezesha kupata kipato kidogo kitakachomwezesha kukimu mahitaji ayatakayo. Hakupata suluhisho kwa haraka. Ugeni wa mazingira ndiyo uliompelekea kuona ugumu wa ufanikishaji wa azma. Mwisho moyo wa matumaini ukapotea, fikra za hali aliyonayo kudumu muda mrefu taratibu ikajishikiza kwenye kuta za ubongo.

Kabla haijawa komavu, mboni akizihangaisha huku na kule kusaili mazingira, mbele yake, umbali wa mita takribani kumi na tisa, akakiona kibanda cha fundi simu. Akajikuta mwili ukitua pumzi la sisimko. Aliikumbuka ile simu ya mwasi aliyonayo. Aliitoa alipoihifadhi, akaisaili kwa chati.

“Inaweza kunipatia ninachokihitaji,” Koplo Frederka alijisemeza, huku akiitoa laini. Akaivunja vunja, kisha alijiinua kuelekea pale bandani.

Akalakiwa kwa bashasha na mhusika wa lile banda.

“ Naiuza hii simu yangu,” Koplo Frederka alijieleza. Akaitoa simu alipoihifadhi akaitua juu ya meza.

“Faranga ngapi?”

“Elfu nane mia tano,” Koplo Frederka alijibu na kumsaili fundi simu. Amepokeaje hitajio lake.

“Nakupa elfu saba. Simu yenye imeshaanza kupoteza ubora wake.”

Koplo Frederka akasita kwa muda kufikiria pendekezo alilotajiwa. Ushawishi wa mahitaji ayatakayo ukamfanya akubaliane naye.

Alivyokabidhiwa, alijiondoa mazingira yale kwa haraka na kupotelea mtaa wa pili. Aliishia kwenye moja ya mgahawa. Akaagiza chakula, na kukifakamia kwa haraka. Alipohitimisha, alifanya malipo na kuendeleza safari.

Sasa alihitaji kulifikia duka la madawa anunue dawa itakayompunguzia maumivu.

Akiwa ameshatembea mita kadhaa kutoka pale mgahawani, mwendo wake ukizidi kuwa wa mchechemeo na unaopungua kasi, akaparamiana na m-mama mmoja aliyeonekana kuwa mwingi wa mambo akilini. Kutokana na maumivu, akashindwa kuuhimili mparamio huo, akadondoka chini. Ikawa shida kuinuka.

Wakati huo yule aliyeparamiana naye aliendelea na safari yake. Hakutaka kujali kilichompata mwenzie huku nyuma. Lakini alipofika hatua kadhaa, akapatwa na msukumo uliomshinikiza asitishe mwendo na kugeuka nyuma. Alimshuhudia Koplo Frederka akaihangaika kujiinua.

Huruma ikamvaa. Akamrejea kumsaidia.

“Nashukuru sana,” Koplo Frederka alisema baada ya kuinuliwa.

“Unaonekana kutokuwa sawa...”

Koplo Frederka akadakia, “Nahitaji nifike duka la dawa. Unaweza kunielekeza lilipo?”

Kwa namna Koplo Frederka alivyojieleza mbele ya mama huyo ndivyo alivyopenyeza hila ya ushawishi. Baadaye akafanikiwa kuziteka kabisa hisia za yule mama kiasi kwamba alimsitishia safari yake.

“Unaishi wapi?”

“Ni mgeni hapa mjini. Nataka nipate kwanza tiba ya majeraha yangu yakishaleta unafuu, ndipo nifanye taratibu za malazi.”

“Naweza nikakusaidia. Mimi ni bingwa wa tiba asili-kama hautojali tunaweza kuongozana hadi nyumbani nishughulikie tatizo lako.”

“Utakuwa umeniokoa sana.”

Kweli. Dakika kadhaa baadaye Koplo Frederka aliongozana na yule mama; aliyepambwa kwa umbo fupi, mnene-mweupe hadi nyumbani kwake. Hakukuwa mbali sana. Ni maeneo ya mtaa huohuo.

Pasi na kuchelea, yule mama akaandaa vifaa tiba; asili vilivyochangamana na taaluma ya kidaktari, baada ya hapo alianza kumganga Koplo Frederka. Halikuwa zoezi la muda mrefu. Alitumia dakika chache tu kuhitimisha, kisha alielekea duka la dawa akanunua dawa ya kutuliza maumivu, alivyompatia, akajipumzisha kwa masubirio ya matokeo.

***

Fundi simu aliyetekwa na waasi alifikishwa kambini kwao akiwa mwenye hali tete iliyojengwa kwa hofu. Hofu ilimfanya mwili uwe na mabadiliko lukuki kwa kufikiria hatma ya maisha yake mikononi mwa mabaradhuli hao. Alivyoteremshwa garini, aliburuzwa hadi kwenye uwazi ulio na nguzo zilizosimikwa kwa mtindo wa goli la mpira wa miguu.

Wakamfunga kwa kudu kwenywe mtalimbo wa juu. Akabaki kuning'inia kama kuku aliyebanikwa. Hatua kadhaa mbele yake, kuliwashwa moto uliojikoleza haswa kadri sekunde ziongezekanavyo. Akaishia kuhangaika asipatwe na ule ukali wa moto lakini haikumsaidia.

Aliondolewa mahali pale robo saa baadaye. Mwili wote ukiwa umeiva, kiasi cha kutotamani kuguswa mahali popote, lakini waasi hawakujali hilo. Walimshika shika wajisikiavyo ili wamwongezee hasira itakayomshawishi aeleze ukweli wautakao.

Wakamketisha kitini. Upande wa pili tu, toka alipopatia mateso awali.

“Kuna jambo tunahitaji utusaidie,” aliyeonekana kuwa kiongozi wa lile kundi la waasi waliofanya utekaji alisema. Fundi simu akamtolea mboni kali ishara ya kumsikiliza.

“Kuna simu ipo dukani kwako, nataka utueleze aliyekuuzia ameelekea wapi,” yule kiongozi aliendeleza hatamu ya uzungumzaji.

“Nauziwa simu na watu wen...” fundi simu alijieleza, kabla hajahitimisha, akala teke lililotua shavuni na kumsukumizia nyuma. Akaanguka.

“Kuna mwanamke ameekuuzia simu,” yule kiongozi alimfafanulia pindi akimwinua. Akampatia na mwonekano wa Koplo Frederka ulivyo.

“Sikumtilia maanani. Hivyo sifahamu uelekeo wake baada ya kutoka ofisini kwangu.”

Jibu la awamu hii likawapa ushawishi kidogo. Waliingiwa na matumaini, kwamba wakiongeza bidii, hawatokawia kumpata mlengwa wao.

“Tulishatoa onyo hapo awali, huu mji upo chini ya himaya yetu. Akitokea amewasili mtu asiyefahamika, tuwasilishiwe taarifa haraka uwezekanavyo, kwa nini ewe hujafanya hivyo?”

Yule kijana akajibu kwa kitetemeshi, “Mi...mim...mimi nilimhi...si ni mmm...” hakuhitimisha kauli yake, kiongozi wa lile kundi la waasi alitoa bastola aliyoisundika kiunoni na kuruhusu mitupo kadhaa pajini mwa yule kijana. Akakata moto.

“Nord,” yule kiongozi wa kundi aliita pindi akiirejesha bastola alipoihifadhi awali.

“Yes, kamanda,” aliyeitwa akaitika.

“Mkusudiwa wetu atakuwa hayupo mbali na yale maeneo. Na kwa hali aliyonayo, lazima atapita maeneo yatakayombainisha pasi na usumbufu. Hivyo ingia mtaani kafuatilie taarifa zake,” kiongozi aliamuru na kuondoka eneo hilo.

Mpatiwa amri naye hakukawia, haraka sana, alidaka chuma-pikipiki na kupotelea mitaa ya jiji la Goma. Hasa du 20 mai. Akaegesha pikipiki nje ya duka la madawa, kisha alipiga hatua taratibu kuelekea ndani. Alimkuta mhudumu; kijana akadiriaye miaka thelathini na ushee, mrefu, mwembamba-mweusi.

“Oooh, kiongozi. Karibu sana,” mhudumu akamlaki kwa bashasha yule mwasi aliyeingia.

“Sijaja kuchelewa. Nipe jipya la hapa mtaani.”

Yule mhudumu ni mmoja miongoni mwa infomer wa waasi.

“Kuna moja lenye shaka.”

Yule mwasi akatekenywa na habari hii. Ilifungua msisimko nafsini mwake.

Mhudumu akaendelea kumweleza, “Kuna mama mmoja hivi nahisi ana mgeni nyumbani kwake.”

“Kwa nini?”

“Ninavyomfahamu huishi pekee. Lakini siku hizi amekuwa mteja wangu wa mara kwa mara wa ununuzi wa dawa. Sijui humpelekea nani hizo dawa.”

“Dawa gani?”

“Za kutuliza maumivu na kukausha majeraha.”

“Nipe uelekeo wa sehemu apatikanapo.”

Yule mhudumu akavuta daftari na kalamu kutoka sarakani, kisha alipotelewa na sekunde kadhaa za kuandika jambo. Alipohitimisha, alichana ile karatasi aliyoandika, akamkabidhi yule mwasi. Naye alisaili kwa muda kilichoandikwa kisha alihifadhi mfukoni.
Uwepo wa yule mwasi ukaishia hapo. Akaaga na kuondoka.

Dakika kadhaa baadaye alijumuika na waasi wenzie waliomteka fundi simu kule kambini. Akawapatia mrejesho wa matokeo yake. Hawakupoteza muda, wakaingia garini kuufuata uelekeo walioelekezwa.

Ukomo wa safari yao ulikuwa nyumbani kwa yule mama amsaidiaye Koplo Frederka matibabu. Kila mmoja alikuwa na bunduki ya kivita na silaha nyingine ya ki-jadi kama silaha ya msaada. Kabla gari haijaegeshwa vyema, wakachumpa mithili ya makomando wenye hali ya juu ya mazoezi wakaizingira ile nyumba. Wajihi, ukawatambulisha hali waliyonayo mtimani; walichafukwa haswa.

ITAENDELEA...
 
Back
Top Bottom