Riwaya: Mkoloni Mzawa

Jun 15, 2020
61
197
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 03.

ROMA, ITALY.

Ulikuwa ni usiku. Kamishna wa intellijensia Barabara Ndirimwe alivyokutana na vijana wa PSU, ambao kwa wakati huo walikuwa kama wahaini. Walikutana kwenye moja ya hoteli ya kifahari nje kidogo ya jiji la Roma.

“Hali si nzuri kule nchini. Nadhani mumewahi kupata taarifa juu ya hilo?” Kamishna Ndirimwe aliongea akiwa anamuangazia mmoja baada ya mwingine.

Walikuwa vijana watatu pekee; Luteni Mwaipeta, Konstebo Babaa na Jackson.
“Yeah! Taarifa tunazo,” walijibu kwa pamoja.

Kamishna Ndirimwe alijikohoza kidogo kisha akaendelea na maongezi, “Kwa sasa amani imekosekana nchini. Nafsi nyingi zimetawaliwa hofu juu ya viongozi wa serikali. Maana wakijaribu tu kukosoa, matokeo wanayokumbana nayo ni adha kubwa.”
“Hivyo lengo la ujio wako ni upi? Maana binafsi kuna tukio limenitokea kiasi kwamba linanipa wakati mgumu,” Luteni Mwaipeta alisema.
“Lipi?” Kamishna Ndirimwe aliuliza kwa shauku.
“Nimeshambuliwa usiku wa jana na mtu nisiyemfahamu. Lakini niliweza kutambua jinsia yake. Alikuwa mwanamke.”

Wengine nao wakachangia matukio yao. Lililowaacha katika sintofahamu ni lile la Konstebo Babaa.
“Ina maana kwamba mumeshashtukiwa? Oooh!...”
“Tueleweshe vyema kiongozi. Kwanza, bado tupo kwenye system?”

Kamishna Ndirimwe hakujibu kwa haraka. Alitulia kwa sekunde chache akionekana kufikiri jambo, alivyolipatia muafaka ndipo alijibu, “Yeah! Bado mupo. Lakini munahesabika kama watoro.”
“Mnh! Tupashe sasa lengo la ujio.”
“Kama ambavyo mumesikia yaendeleayo huko nchini, hali ni mbaya sana. Si wananchi, si viongozi ambao wanaaminiwa na wananchi wanaweza kuwa sehemu ya msaada; wote wapo sehemu moja kwa bwana mkubwa. Hawana amani na uhuru wao. Sasa binafsi nimeonelea kuiondoa hii hali.”

Ukapita ukimya mfupi.

Jackson akaufukuza, “Peke yako?”
“Hapana. Ndiyo maana nimekuja kwenu ili muwe sehemu ya msaada.”
“Unahitaji msaada gani?”
“Nahitaji kurejesha amani ya kila mmoja nchini. Ule uhuru wa kutoa maoni, kukosoa na kutoa ushauri urejee. Ki-ujumla, nahitaji kubadilisha mfumo wa serikali yetu.”
“Mzee, mpango kama huo unawezaje...”
“Mpango wowote huanza na mtu mmoja.”
“Sisi msaada wetu utakuwa wa namna gani?”
“Sasa hivi mzee wa nchi kakamata kila sehemu, lakini hatuwezi kuwakosa washiriki. Wapo wengi tu wenye nia kama yangu, wanashindwa kujitokeza kwa sababu ya woga wanaojazwa.”
“Fafanua basi, nini unataka kifanyike?”
“Nia yangu kama nilivyowaambia awali, kurejesha uhuru wa kila mmoja nchini. Nahitaji kuurejesha uhuru huu kwa msaada wenu na Ndalama Machicho.”
“Tupe full usituhadithie nusu nusu.”
“Rais Sharabu anataka kuwaondoa uraiani wanasiasa wote wenye nguvu mtaani. Ili wakati wa uchaguzi asipate ukinzani mkubwa. Kitendo cha kumweka Ndalama gerezani linadhihirisha hili. Sasa mimi nahitaji nimuondoe Ndalama kule gerezani tuje kushirikiana katika hili. Sifurahishwi na yale yafanywayo na Rais Sharabu. Anawakosea sana watangulizi wake. Hasa kwa kutofuata misingi ya katiba.

“Hivyo nimeandaa kampeni ya kumtoa kwa kumchangia kiasi cha faini alichoambiwa alipe...”
“Wewe ndiyo umeandaa ile harakati?” Luteni Mwaipeta aliuliza kwa mshangao.
“Yeah! Sasa ninyi wajibu wenu ni kurudi nchini ili mukawalinde wakusanyaji wa michango. Nina wasiwasi wanaweza wakawekwa kati na kunyang’anywa, kitendo ambacho kitaniweka katika wakati mgumu. Na ukizingatia sihitaji huu mpango ufeli.”
“Binafsi sitoweza. Nahitaji nimuuguze mke wangu,” Konstebo Babaa alisema.
“Najua. Lakini huu mpango upo kwa ajili ya ukombozi wa wanatuleane. Huna budi kushiriki kwa namna yoyote. Jipe muda ufikirie. Vipi wengine?”
“Binafsi sina pingamizi,” Luteni Mwaipeta alijibu.
“Mimi wajibu wangu utakuwa nini?” Jackson aliuliza.
“Utarudi na kubaki kwenye ujuzi wako. Kuna mahali nimekuandalia. Utaingia hapo ili uwape hamasa wananchi. Maana wengi wao wameshindwa kutambua umuhimu walionao juu ya uamuzi kwa kiongozi wa ki-serikali.”
“Okay!”
“Lazima turejeshe hili hitajio kwa gharama yoyote.”
“Hakika.”

***

Asubuhi ya siku iliyofuata walikutana hospitalini alikolazwa Dc/cpl Amina (Annastazia). Daktari amsimamiaye Dc/cpl Amina (Annastazia) akawaongoza kuingia wodini. Ilivyo bahati, walimkuta amerejewa na fahamu.
“Hongera sana dokta,” Kamishna Ndirimwe alishukuru.
“Ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye afaaye kushukuriwa katika hili.” Wakatabasamu.
“Yupo huru kufanya mazungumzo?”
“Yeah! Lakini jitahidini msimchoshe.”
“Hamna shida. Naomba utuachie nafasi.”

Daktari akaondoka.

Wakajipanga vyema kwa kuzunguka kitanda.
Awali, kwa pamoja walimpatia pole. Nyuso zao zikiwa zimetamalaki huzuni iliyoshindwa kuelezeka.
“Mwenyezi Mungu azidi kukujalia heri, upone haraka ili urudi majukumuni.”
“Hakika atajalia,” Dc/cpl Amina (Annastazia) alijibu.
“Tupo hapa kwa mambo mawili; moja, kukutakia hali. Pili, kukupasha yaendeleayo nchini. Naamini kuna machache unayoyafahamu.”
“Yeah!”
“Basi nimekuja kwa lengo la kuwafuata vijana wangu. Lakini nasikitika ewe hautokuwepo awamu hii kutokana na hali uliyonayo.”
Dc/cpl Amina (Annastazia) akatokwa na machozi.

Konstebo Babaa akafuta lile chozi kwa kitambaa chake. Nafsi ikitokota kwa uchungu.
“Natamani nami ningekuwa pamoja.”
“Labda kwa siku zijazo. Maana hali ya sasa haikuruhusu katika ushiriki wowote. Juu ya hilo, bwana mkubwa hataki.”
“Kwa nini?”
“Muulize?”
“Eti kwa nini hutaki mume wangu?”
“Nani atakuuguza nikiondoka?”
“Naamini Kamishna hajakosea hadi awafuate huku. Anajua nini anafanya. Kubaliana naye, sitokosa mtu wa kuniuguza.”

Ukapita ukimya mfupi.

Mwisho, Kamishna Ndirimwe alitoa bahasha mbili katika mfuko wa suruali aliyovaa. Moja alimkabidhi Luteni Mwaipeta, nyingine Konstebo Babaa.
“Babaa, naamini utafanyia kazi. Detective, ugua pole,” Kamishna Ndirimwe aliongea na kuwashtua Luteni Mwaipeta na Jackson waondoke.

Wakaondoka.

Konstebo Babaa akasalia na mkewe mule wodini, wakati wote akiisaili bahasha aliyokabidhiwa.

Muda mfupi baadaye Kamishna Ndirimwe alirejea tena mule wodini.
“Babaa, Mwaipeta anakuhitaji mara moja,” Kamishna Ndirimwe alizungumza.

Konstebo Babaa akatii.

Konstebo Babaa alivyoondoka, Kamishna Ndirimwe alipiga hatua hadi pale alipokuwa amesimama awali. Akaziangazia mboni zake kwa nguvu kumwelekezea Dc/cpl Amina (Annastazia).
“Don’t lose your target,” Kamishna Ndirimwe aliongea kwa msisitizo.
“Ondoa shaka, kila kitu kitakaa kwenye mstari namna kilivyopangwa.”

Kamishna Ndirimwe akaondoka. Konstebo Babaa akarejea wodini. Walipishana mlangoni. Kila mmoja akiwa makini na uelekeo wa mwendo wake.
“Inabidi ufanye ulivyoambiwa. Acha kuniangalia mimi. Kwa sababu nitapona tu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Waangalie wale waliopo nyumbani kwa jicho la tatu, nenda mukawarejeshee kile walichokipoteza kwa ukosefu wa usikivu wa viongozi wetu,” Dc/cpl Amina aliongea. Sauti ikiwa nyenyekevu, iliyojaa ushawishi.

Konstebo Babaa hakujibu. Aliishia kumwangalia mkewe kwa jicho lililoshesheni huruma, huku kwa mbali akilengwa lengwa na machozi.

***

Siku iliyofuata Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa walifunga safari kwa muda tofauti tofauti, kutokana na maelezo waliyoyakuta kwenye bahasha. Hayakuwa maelezo mengi. Yalikuwa machache tu, lakini yaliwapatia ukinzani mkubwa wa kutambua yanamaanisha nini.

Juu ya maelezo hayo, walikutana na tiketi walizotumia kusafiria. Jackson aliondoka na Kamishna Ndirimwe.
“5+4” Huu ndiyo ujumbe aliokutana nao Konstebo Babaa.

Luteni Mwaipeta alikutana na ujumbe uliosomeka, “5+5”

Ilikuwa changanyikeni. Kwani ilisumbua sana akili zao.

Luteni Mwaipeta ndiye alikuwa wa kwanza kuwasili jijini Nufaiko. Mara baada ya kuteremka ndani ya ndege na kukamilisha taratibu zote za ki-usalama alichanja mbuga kutafuta uelekeo. Alivyofika eneo la mapokezi ya wasafiri wanaowasili, aliangaza huku na kule, akamuona kijana mmoja amebeba bango lililoandikwa ile namba aliyokuta kwenye ujumbe aliopatiwa. 5+5.

Akasita kuendelea na safari. Akamwangalia yule kijana aliyebeba lile bango huku akiwazua nini afanye. Baadaye alikata shauri, akaamua kumfuata.
“Karibu sana,” yule kijana alimlaki. Wakati huo huo akipokea begi la Luteni Mwaipeta. Lilikuwa begi dogo la kuvaa mgongoni.

Hatimaye wakaongozana.

Walivyofikia eneo la maegesho waliingia kwenye gari fulani na kuondoka. Ilikuwa Range rover vogue, yenye rangi nyeusi, iliyopambwa kwa tinted zenye rangi nyeusi pia.

Hiyo ilikuwa alfajiri.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa waliripoti kwenye jengo moja katikati ya jiji. Maeneo ya Bondeni. Waliteremka, kisha wakaongozana kuingia ndani ya jengo hilo. Lililotoa picha ya wazi kuwa ni ofisi.
“Ingia mlango namba kumi,” yule mpokezi alimwambia Luteni Mwaipeta pindi akimkabidhi lile begi lake.

Luteni Mwaipeta akafanya kama alivyoamriwa. Cha kushangaza, kile chumba kilitawaliwa na kiza cha kuogofya. Akatamani awashe taa, lakini pindi akiwa kwenye harakati za kutafuta swichi sauti iliyojaa ngurumo ikamshtua.
“Hupaswi kufanya hivyo.” Akatulia.
“Naomba unikabidhi ujumbe uliopatiwa,” ile sauti ilijirudia kwa mara nyingine. Ilikuwa kama inatoka mtungini. Na muongeaji hakuwa ndani ya kile chumba.

Luteni Mwaipeta alifungua begi na kuitoa ile bahasha.
“Weka juu ya meza.”

Pale aliposimama, mbele yake kulikuwa na meza.

Kila alichoambiwa hakupinga. Alitii kwa haraka kwa sababu ya ukerehekaji uliojaa nafsini mwake kutokana na kile kiza. Hivyo alitamani mambo yaende haraka ili apate kuondoka.
“Kifuatacho?” Luteni Mwaipeta aliuliza.
“Upo tayari kwa kazi?”
“Yeah!”
“Okay! Chukua bahasha uionayo hapo mezani. Jitahidi, uhakikishe unampatia ulinzi huyo mtu. Ulinzi wa nguvu, lakini usibainike. Kwani ndiyo sehemu nyingine ya kuelekea ukombozi wa wanatuleane kuwarejeshea uhuru wao.”

Luteni Mwaipeta akaichukua ile bahasha na kuiweka ndani ya begi.
“Sasa unaweza kuondoka.”

Akaondoka.

Alipofika nje alipokelewa na yule kijana aliyempokea uwanja wa ndege. Akamuongoza aingie kwenye gari na kuondoka. Walihitimisha safari yao nje kidogo ya maeneo yale yale ya Bondeni, katika hoteli ya Nyangenyange.

Jambo la kwanza kufanya baada ya kuingia kwenye chumba chake katika ile hoteli, aliitoa begini ile bahasha aliyoambiwa aifanyie kazi. Aliisaili, na kukutana na maandishi machache pale juu. Yaliyoandikwa, ROAD TO LIBERATION. Akaifungua.

Ndani ya bahasha alikutana na picha ya mnato. Picha ya mtu anayemfahamu. Kidogo ilimshangaza.
“Inawezekanaje?” alijiuliza. Akiwa katumbua pima mboni zake kumsaili yule mtu amuonaye.

Ni picha imuonyeshayo Makamu Mwenyekiti wa chama cha Chautu, Ndg. Patrick Babigamba.

Alijiuliza maswali mengi kumuhusu, lakini hakuna hata moja alilolipatia ufumbuzi. Mwisho, alichukua simu na kumpigia Kamishna Ndirimwe.
“Naamini umeshafika,” sauti ya upande wa pili ilisikika. Mara baada ya simu kupokelewa. Sauti ya Kamishna Ndirimwe.
“Yap! Lakini...”

Akakatishwa kabla hajamalizia, “Huo ndiyo mpango mkakati. Kikubwa kuutekeleza. Ewe fuata kila utaratibu utaokapatiwa, ndiyo mafanikio yenyewe hayo.”
“Naweza kukuanimi?”
“Exactly!” Kamishna Ndirimwe aliongea na kukata simu.

Luteni Mwaipeta hakuitoa ile simu sikioni juu ya kuwa ilishakatwa. Usaili wa picha ulimpa butwaa asilolitarajia.

Baadaye alivyozinduka, aliirudisha picha begini akawasha runinga. Aliweka kwenye moja ya idhaa nchini, akakutana na taarifa ya dharura. Iliyobeba ujumbe, Makamu Mwenyekiti wa chama cha Chautu akimbizwa hospitali ya Litunu baada ya kuanguka ghafla ofisini kwake. Akatega sikio vyema kuisikiliza.
“...kwa maelezo ya awali, baadaya kufanyiwa uchunguzi, inasadikika kiongozi huyo amekutwa na sumu mwilini mwake, hivyo...” ilikuwa sehemu ya maelezo ya mtangazaji aliyekuwa anaripoti habari hiyo.

Luteni Mwaipeta alivuta pumzi na kuzitua kwa nguvu akiwa anaachia kiungambali na kuketi kitandani. Habari ilizidi kumtatanisha. Akavuta begi na kuitoa ile picha kwa mara nyingine. Taratibu, akaanza kuisaili upya.
“There is something which is not right,” alijisemeza. Akizidi kuichunguza ile picha.

Huyo ndiyo mtu aliyeambiwa ampatie ulinzi. Ana nini cha muhimu hadi apatiwe ulinzi? Hakujua.

ITAENDELEA...
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 04.

Konstebo Babaa alipokelewa kama ilivyokuwa kwa Luteni Mwaipeta. Jambo la kwanza alimtafuta Dc/cpl Amina kwa njia ya barua pepe na Whatsapp call lakini hakufanikiwa kumpata hewani. Mwisho alimtumia ujumbe wa sauti, uliomtaka endapo akiwa hewani asiache kumtafuta.

Akajilaza kitandani kwa mapumziko.

Muda mfupi baadaye ulisikika mlio ulioashiria kuingia ujumbe kwenye simu yake. Akaamka, akaichukua simu alipoihifadhi, na kuperuzi ujumbe husika. Ulitoka kwa Kamishna Ndirimwe.
“Kesho, saa 3 asubuhi. TU 921 ACW. End point Mkabala na Mahakama kuu,” ulisomeka ujumbe aliotumiwa. Ambaye aliuelewa unamaanisha nini kwa lugha za ki-intellijensia.
“Detective hapatikani. Kulikoni? Au ewe umejaribu kuwasiliana naye?”

Kamishna Ndirimwe hakujibu kwa haraka. Alitulia kwa sekunde chache, takribani tano, ndipo akamjibu, “Usichanganye maji na mafuta kwa wakati mmoja.”
“Ni mke wangu. Hivyo nina wajibu wa kufahamu maendeleo ya afya yake.”
“I know it. Lakini sio kwa wakati huu,” Kamishna Ndirimwe alijibu na kupotea hewani.

Konstebo Babaa akabaki kuwa mwenye ghafiriko.

Kama alivyotaarifiwa. Siku iliyofuata baada ya kukamilisha maandalizi yahusuyo usafi wa mwili na kifungua kinywa, Konstebo Babaa aliondoka pale hotelini. Alifikia hoteli iitwayo Rondo, iliyopo maeneo ya Ngowe.

Alifuata jinsi ujumbe ulivyomtaka. Pale nje ya hoteli, eneo la maegesho alikuta gari dogo aina ya Toyota Corolla, alipanda na kuondoka. Yeye akiwa mwendeshaji Kwani aliyeiacha, aliacha pamoja na funguo.

Mwisho wa safari ulikuwa karibu na Mahakama kuu. Akaegesha gari umbali mrefu kidogo toka mahakamani, kisha akawa anaangaza angaza huku na kule kwa masubirio.

Ikiwa imemchukua karibia dakika kumi kusubiri, kiasi cha kumfanya kuudhika, hadi akapata shinikizo la kumtafuta Kamishna Ndirimwe ili ikibidi aondoke, alipokea ujumbe kwenye simu yake. Uliotumwa na Kamishna Ndirimwe.
“Mtu yeyote atakayeingia garini ondoka naye kwa kasi.” Aliurudia kuusoma mara mbili mbili huu ujumbe.

Akaendelea na masubirio, huku akisinzia sinzia.

Alikuja kushtuliwa na kishindo cha nguvu kilichotokea nyuma yake ndani ya gari. Alivyogeuza macho, alimuona mtu fulani asiyemfahamu, wala hakufahamu alivyoingia ingia.

Kwa muonekano wa haraka haraka yule mtu alikuwa mwendawazimu. Hiyo ilimthibitishia kutokana na namna alivyovaa, na mazingira aliyonayo. Alivaa nguo chakavu, zilizochanika chanika na kutoa harufu ya uvundo. Hali ya nywele ndiyo kuzidi. Zilikuwa timtim na uchafu uliogandiana.

Konstebo Babaa alitamani amfukuze. Lakini alivyokumbuka ujumbe wa Kamishna Ndirimwe aliwasha gari na kuondoka.

Pindi anaondoka alikuwa anaangaza angaza pembeni, akawaona watu fulani waliokuwa wanamfuatilia yule mtu aliyeingia garini. Aliwaona kupitia side mirror, namna walivyokuwa wanahaha baada ya kukosa uelekeo wa mtu wanayemfuatilia.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa yule chizi aliomba kuteremka. Konstebo Babaa alisimamisha gari, naye kufanya alivyoomba. Aliteremka, na kupotelea uchochoroni. Lakini wakati anatoka, kuna kikaratasi alikiacha kwenye ile siti aliyokuwa amekaa. Pasipo Konstebo Babaa kufahamu.

Konstebo Babaa alimwangalia yule chizi hadi alivyopotea kwenye upeo wa mboni zake ndipo akaendelea na safari.

Alirudi hotelini. Moja kwa moja chumbani kwake, anaketi tu kitandani, akapigiwa simu na Kamishna Ndirimwe.
“Naomba unitumie ujumbe uliopatiwa na yule mtu,” ilikuwa kauli ya kwanza kutoka kwa Kamishna Ndirimwe pasi na salamu.

Konstebo Babaa alijibu akiwa na mshangao, “Mbona hajanikabidhi kitu chochote!”
“Una uhakika?”
“Yeah!”
“Rudi garini kaangalie.”

Alirudi, simu bado ikiwa hewani.

Alivyolifikia gari, alifungua mlango kule alipokuwa amekaa yule chizi na kuanza kutafuta. Isivyo bahati, hakukutana na kitu chochote.
“Hamna kitu afande.”
“Upo wapi umakini wako? Nini umefanya?” Kamishna Ndirimwe alimkoromea.
“Haa! Afande. Hajaniambia kama ameacha kitu.”
“Ulitakiwa uwe mtu mwenye mashaka muda wote.” Akakata simu.

Kiunyonge, Konstebo Babaa alipiga hatua kurudi chumbani. Alivyofika tu, akapata simu nyingine kwa namba ngeni. Hakuipokea kwa haraka, alianza kuijadili kwanza. Nafsi ilivyomuondolea utata, ndipo aliipokea.
“Hallo!” aliita.
“Sikutarajia utakuwa mzembe namna hiyo,” sauti ya upande wa pili ilisikika.
“Nani mwenzangu?”
“Mgeni wako ndani ya gari leo asubuhi.” Akakata simu.

Konstebo Babaa akahisi kudhalilishwa. Kwani baada ya utambulisho ule, alifahamu, aliyetoka kuwasiliana naye ni yule chizi aliyempakia ndani ya gari asubuhi. Atadhalilishwaje na chizi!

Akamrudia hewani Kamishna Ndirimwe.

“Ndiyo,” Kamishna Ndirimwe aliongea mara baada kupokea simu.
“Nahitaji kuonana na yule mtu uliyenikutanisha naye asubuhi.” Lengo amfahamu vyema. Ni nani? Na imekuaje akajiweka katika mazingira ya namna ile?
“Watu wengine ni kama Mwewe tu ndani ya hii misheni.” Kamishna Ndirimwe akakata simu.

Konstebo Babaa akabaki na maulizo. Nini maana ya kauli aliyoambiwa? Ikambidi aanze kuwazua tabia za Mwewe ni zipi.

***

Sintofahamu ilijengeka kwa watu wengi, hasa waliopata kusoma moja ya gazeti la kila siku litokalo nchini, liitwalo UHURU KWANZA. Litolewalo na kampuni ya FIKRA HURU. Kila aliyepata kusoma alizisambaza habari hizo kwa mwenzake, ikafikia hatua, ndiyo ikawa habari pekee zilizopewa kipaumbele kwa siku hiyo.

Habari zilizonena; Mheshimiwa Rais aamuru kufukuzwa kazi watumishi wa Mahakama kuu. Nyingine ilisema, Patrick Babigamba awekewa sumu na watu wasiojulikana.

Kazi iliyofanywa na Jackson. Ambaye alipewa ajira katika kampuni hiyo kama Kamishna Ndirimwe alivyomuahidi hapo awali. Kwenye habari zake hakujiweka wazi. Alitumia jina la uficho Mwandishi wetu.

Rais Sharabu alikuwa miongoni mwa watu waliofikwa na zile habari. Zikamkasirisha, kiasi cha kukereketa nafsini mwake, hadi koo likakabwa kwa uchungu.
“Nini hii? Nini hii?” alijisemeza. Akiyarusha rusha yale magazeti mezani.

Hakika, yeye ndiyo chanzo cha habari hizo zote. Lakini hakuhitaji ziwe publicity. Hasa imuhusuyo Babigamba.

Hakutaka tukio la Babigamba lifahamike na wengi. Ukizingatia yeye ndiyo alitoa amri kwa vijana wake, baada ya kukinzana katika kikao cha kamati kuu kuhusu adhabu ya Ndalama Machicho. Na matendo mengine aliyotendewa. Kumtuliza, aliamua awekewe sumu.

Kuhusu watumishi wa mahakama kuu kufukuzwa, kuna uhusika wake pia. Baada ya kubaini, wametoa namba ya malipo ya kesi ya Ndalama Machicho ili akalipiwe afaini atolewe gerezani. Hakupendezwa nalo. Tena ukizingatia hakutamani hata kusikia harufu ya mtu huyo.

Ukinzani kwa Rais Sharabu ulikuwa sawa na jahanamu.

“Nawahitaji nyote wawili ofisini kwangu muda huu,” Rais Sharabu aliongea kwa jazba, pindi akifanya mazungumzo na mtu wa upande wa pili kwa njia ya simu.

Waitwa hawakukawia. Walikuwa ni wale m-baba wa miraba minne na yule m-mama.
“Mumeona kilichotokea?” Rais Sharabu aliwafokea.
“Ndiyo. Tusamehe sisi mheshimiwa Rais,” yule m-baba, Killa Lauma alijibu. Ambaye ni Mkurugenzi wa usalama wa taifa. Wakati huo m-mama akitawaliwa na wajihi uliopambika kwa hofu. Alifahamika kwa jina la Maua Akwiti. Katibu wa itikadi, siasa na uenezi taifa ndani ya chama cha Chautu.
“Nini sasa kifanywacho na vijana wenu kama taarifa zinavuja hivi? Si muliniambia mumepeleka vijana wa usalama na wa-intellijensia ya chama?”
“Yeah! Kuna ulinzi wa kutosha mheshimiwa Rais. Sasa sijajua huyu mwanahabari kapataje nafasi ya kuhojiana na Babigamba na hiyo taarifa ya mahakamani,” Maua alijitetea. Mwili mzima ukiwa wenye kutetemeka kwa hofu. Jasho jembamba likimtiririka, ilhali kulikuwa na kiyoyozi.
“Ni uzembe huu. Hamfanyi kazi. Munahisi wananchi watanichukuliaje?”
“Usiohofu mkuu. Tutawasiliana na Kamanda wa kanda maalumu ashughulike na wahusika wa hili gazeti. Huku Waziri mwenye mamlaka tutamshawishi awapatie kashkash ya kulifungia.”
“Kufanya hivyo nitaonekana muhusika wa kweli.”
“Hapana. Waziri wa habari akanushe. Na kuwapachikia wameandika habari za uongo.”
Rais Sharabu aliongea kwa upole. Hasira zikiwa zimemuisha, “Juu ya vijana muliowaweka, kuna ulinzi mwingine?”
“Ndiyo. Tumetega kamera kwenye wodi aliyolazwa Babigamba.”
“Mumeangalia matukio ya leo?”
“Hapana.”
“Nataka kumuona mwandishi aliyeenda kumuhoji huyu mpuuzi.”
“Hamna shida.”

Wakaondoka hadi ofisi za usalama wa Taifa. Wakaiingia kwenye chumba husika, cha mapokeo ya matukio yote yarekodiwayo na kamera walizotega sehemu mbalimbali. Wao wakaiwekea umakini ichukuayo wodi ya Babigamba na mazingira jirani ya hospitali. Hasa langoni. Lango kuu; la kuingilia na kutokea.

Mboni zao zilikuwa makini kuangalia kila nukta. Lakini hadi wanafikia ukomo, hawakumuona mtu yeyote tofauti na daktari aliyeingia wodini. Tukio lingine walilolishuhudia walimuona Babigamba akichezea simu. Wakahamasika kuichunguza. Kufuatilia nyendo zake kwa ukaribu.
“Mwambie mmoja kati ya vijana wako unaowaamini watuletee ile simu. Halafu, vipi wale uliowatuma nje kwenda kufuatilia hawa wajinga walioua...” Rais Sharabu aliongea. Wakiwa ndani ya gari kurudi Ikulu. Lakini hakufanikiwa kuhitimisha kauli yake, muito wa simu ukamghairisha.
“Ndiyo,” Rais Sharabu aliita, mara baada ya kupokea simu.
“Kuna taarifa mbaya mheshimiwa Rais,” sauti ya upande wa pili ilisikika.

Wajihi, sambamba na mapigo ya moyo yakambadilika, akiwa mbioni kupokea taarifa. Kiasi cha Killa na Maua, nao kuanza kuingiwa na mashaka.
“Babigamba ametoroshwa hospitalini? Una uhakika?” Rais Sharabu aliuliza kwa ukali.
“Ndiyo mheshimiwa Rais. Tumeangaza kila kona hatujamuona.”
“Shiit!” alimaka na kuitupia simu kando ikiwa bado haijakatwa.
“Kulikoni mheshimiwa?” wakamvaa kwa ulizo la pamoja.
“Babigamba haonekani hospitalini.”

Wote wakachanganyikiwa. Inawezekanaje!
Kwa kasi isiyoelezeka, walipandwa na hasira huku kila mmoja akionekana kuwa mwenye mafikirio.

Roho halisi ya Rais Sharabu hapo ndipo ilijiimarisha kuonekana ni mtu wa namna gani.

“Harufu yao inazidi kuwa kali. Hivyo endapo mukifanikiwa kumpata, musisite kumfanyia chochote mutakachojisikia, ili mradi badaa ya muda fulani nisikie kifo chake. Maana hana umuhimu wowote katika ustawi wangu,” Rais Sharabu aliongea, hasira ikiwa imefura wajihini mithili ya matuta ya viazi.

ITAENDELEA...

BADO HUJACHELEWA, KITABU CHA RIWAYA YA NENDA KINAENDELEA KUPATIKANA. WASILIANA NAMI KWA 0693097151 KWA MAELEZO ZAIDI YA UPATIKANAJI WA KITABU HICHO.
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 05.

Luteni Mwaipeta ndiye aliyemtorosha Patrick Babigamba hospitalini. Baada ya kufanya hila, kama naye ni mmoja kati ya madaktari wa hospitali hiyo. Rais Sharabu na kamati yake ya roho mbaya walivyokuja kuangalia picha za video walimbaini.
“Mamamamaa!... Mamamaaa! Uuuuhu! Amekujaje huyu?” Rais Sharabu alipiga ukunga wa ghadhabu. Picha ya Luteni Mwaipeta akiwa amevaa koti la ki-daktari ikiwa imewekwa pozi kwenye skrini.

Killa Lauma na Maua wakahema kwa nguvu. Kuashiria mambo ni mazito.

Ukapita ukimya mfupi, uliofukuzwa na Rais Sharabu baada ya kupoa ile ghadhabu, “Wanafanya haya yote ili wamtoe Ndalama gerezani, halafu aje kufanya shughuli zake za kiasiasa huku nje.”
“Upo sahihi.”
“Sasa hicho kitu mimi sikihitaji. Kama mjuavyo, mwenzangu ni mkongwe kwenye ulingo wa ki-siasa. Ana ushawishi mkubwa. Akiwa huru atanisumbua.”
“Mheshimiwa Rais. Wewe ndiyo pekee mwenye mamlaka makubwa hapa nchini. Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vipo chini yako. Unasumbuliwa vipi na huyu kapuku? Acha wamtoe. Na watamtoaje ikiwa namba ya malipo waliyokabidhiwa tulishaichukua? Hata wakipata, hatutowapa nafasi ya kufanikisha hilo. Wakifanikiwa, una mamlaka, unaweza kumpachika kesi nyingine, akahangaikie harakati zake mahakamani,” Maua alichangia hoja.
“Nahisi kukuelewa!”
“Eeh! Ni hivyo tu.”
“Wananchi si wanaweza kunigundua?”
“Aaah! Wananchi wenyewe hawa wa kwetu? Wenye midomo ya mdondoo?”
“Nimekupata,” Rais Sharabu alisema akiwa anatingisha kichwa. Kukazia kauli yake. Baadaye aliendelea, “Lakini ni kweli. Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vipo himayani mwangu. Na mimi ndiyo final say wa kila idara hapa nchini... Aisee, akinisumbua sana nitamuondoa hapa duniani. Tena, muambie yule jamaa, awasiliane na mtu wake atupatie silaha za kisasa zaidi awamu hii.”

Wakatabasamu.

***

“Umezihifadhi wapi zile pesa? Na vipi kuhusu pesa za kujazilizia?” Kamishna Ndirimwe aliuliza. Wakiwa kwenye maongezi, baina yake, Luteni Mwaipeta na Babigamba. Nje kidogo ya jiji la Nufaiko. Maeneo ya Mara, Kilioni.
“Imeshakamilika. Na ipo sehemu salama. Mulishapata namba ya malipo?” Babigamba alijibu. Mzee; aliye na muonekano mfupi, mnene kiasi, amepambwa kwa rangi nyeusi, kunyanzi na mvi zikimkithiri kwa kiasi.
“Tumefanikiwa.”
“Vizuri sana. Tena sana. Lakini...”
“Ndiyo.”
“Vipi kuhusu ulinzi na usalama wetu?”
“Kuhusu hilo halina shida. Tutawalinda, mpaka pale Mwenyezi Mungu atakapoamua kuwachukua.”

Babigamba akawaomba Kamishna Ndirimwe na Luteni Mwaipeta wasogee karibu yake. Walifanya hivyo. Kisha aliwanong’oneza, huku akiwaonyesha kitu kwenye shajara, “Hapa ndipo nilipohifadhi zile pesa.”

***

Kiza kilikuwa kingi, pindi Kamishna Ndirimwe alivyokutana na washirika wenzake wa misheni nje kidogo ya jiji la Nufaiko. Kwenye moja ya nyumba za kulala wageni, iliyotamalaki uchakavu, kulingana na hadhi yao. Lakini hawakulijali hilo. Walichozingatia ni kupata mahali watakapoweza kuzungumza kwa uhuru.

Washirika wenzake walikuwa wawili; yule chizi, ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa idara ya usalama wa Taifa (DDGSS) afahamikaye kwa jina la Mabele Migomba. Na yule aliyekuwa anawasiliana na Luteni Mwaipeta kwenye kile chumba gizani. Mnadhimu Mkuu wa jeshi la Ulinzi, Luteni Jenerali Kipozi Hokororo.
“Kamishna, kuna lolote lenye dira?” Luteni Jenerali Kipozi aliuliza.

Walikuwa wanateta kwa sauti ya unong’ozi.
“Yeah! Tutamuondoa Mkoloni Mzawa. Na uhuru lazima urejee kwa kila mmoja. Mihimili yote mitatu, na mamlaka ya Rais lazima tuyapunguze.”
“Basi tuzidi kuongeza umakini.”
“Hilo si la kulijadili.”
DDGSS, Mabele Migomba akachangia hoja, “Binafsi nina moja.”
“Ndiyo.”
“Yafaa kuwaingiza wale vijana waliohusika kuzima mapinduzi utawala uliopita.”
“Hawapo upande wa pili?”
“Walipelekwaga mikoani. Hivyo nina hakika hawana upande kwa sasa.”

Ukapita ukimya mfupi.

Luteni Jenerali Kipozi akaufukuza, “Ni jambo zuri. Kamishna, lifanyie kazi hilo.”
“Hamna shida. Kwani kuna mtunzi na mwandishi mmoja wa riwaya nchini Tanzania alishawahi kunena, nanukuu, kama sitokosea, ‘Ukishindwa kumbadilisha mtu, badilisha mtu.’Anaitwa Abdallah Yahya Sufian. Lakini watu wengi wanamfahamu kama Abyas Mzigua. Mwanasayansi, mwenye utaalamu wa hali ya juu katika lugha ya Kiswahili.”
“Hakika, huu ni wakati wa kubadilisha. Kwa sababu Bw. Sharabu hayupo tayari kubadilika,” DDGSS (Deputy Director General of Security Service) Mabele Migomba alichangia hoja.
Mwisho wa maongezi, kila mmoja alielekea kwenye harakati zingine.

***

Saa 12 asubuhi Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa walikuwa ndani ya gari binafsi wakielekea mahali zilipohifadhiwa pesa na Babigamba. Lilido, mkoani Kondeni. Waliwasili asubuhi ya siku ya pili yake. Mchana walizuga zuga mjini, kwa kupata chakula na kujipumzisha, ili muda paswa wa shughuli wawe ngangari.

Usiku ulipowadia, walifunga safari kuelekea eneo husika. Nje ya Lilido, kwenye shamba la mzee mmoja hivi; aliyepata kuwa na nafasi mbalimbali kwenye chama cha Chautu kipindi cha nyuma. Pesa zilikuwa zimehifadhiwa sandukuni. Sanduku la chuma, na kufukiwa ardhini.

Walivyofika shambani hawakuhangaika sana, walifuata dira waliyopewa hadi sehemu kusudiwa. Walipopapata walianza uchimbaji. Vifaa vya uchimbaji walivibeba toka jijini Nufaiko.

Uchimbaji haukuchukua muda mrefu. Kwani walivyofikia funiko tu, hawakuendelea. Walifanya jitihada ya kulifungua lile funiko, kisha walizitoa pesa na kuziingiza kwenye mabegi. Hadi kukamilika, zoezi lilichukua takribani dakika arobaini na tano. Baada ya hapo waliingia ndani ya gari safari ya kurudi ikaanza.
“Moyo wangu umejaa wasiwasi sana juu ya hii misheni. Maana ina dalili zote za kutambulika waziwazi,” Konstebo Babaa aliongea. Wakati huo akiwa makini, ameketi nyuma ya usukani kupiga gia.

Soga za hapa na pale zilipamba safari.

“Nami ni vivyo hivyo. Lakini acha tufanye. Ikifanikiwa, tutakuwa sehemu ya maandishi yaliyobeba historia ya wakombozi,” Luteni Mwaipeta alichangia hoja.

Walivyouacha mji wa Lilido, na kuingia miji ya mkoani Ndwika, kwenye moja ya msitu, walimuona mtu fulani kalala barabarani. Walivyomtathmini zaidi, kila walivyokuwa wanamkaribia, wakamtambua ni mtu wa jinsia gani. Wa kike.

Konstebo Babaa akapunguza mwendo na kuegesha gari kando. Lilikuwa eneo lenye kalavati, lililo na kingo, hivyo hawakuweza kupita pembeni. Wangemgonga. Kwa wema, mmoja wao; Luteni Mwaipeta, aliteremka kwa lengo la kwenda kumchunguza zaidi na kumuweka vizuri wapate nafasi ya kupita.

Hakuwa na hofu wala mashaka ya jambo baya kutokea.

Katika hali ya kustaajabisha, Luteni Mwaipeta akiwa amemuinamia ili amgeuze, yule mtu aliinuka na kumtemea mate machoni. Akiwa anahangaika kuyafuta, alipokea ngumi mbili za uso, zilizomyumbisha na kwenda kupata muhimili kwenye zile kingo za kalavati.

Konstebo Babaa akatumbua mboni za hamaniko kule garini.

Kwa kasi ya ajabu, yule mwanamke alipiga hatua za haraka kumfuata Luteni Mwaipeta kule alipo huku akiwa amejiandaa kuachia pigo la ngumi. Luteni Mwaipeta alilitambua hilo. Lakini hakutaka kujionyesha mapema kama ameshafahamu dhamira yake.

Yule mwanamke alivyomfikia alitupa ile ngumi aliyoiandaa kuirusha, lakini Luteni Mwaipeta alihepa kidogo pembeni kwa upande wa mkono wake wa kushoto na kumzungukia yule mwanamke nyuma yake. Akamkwida shingoni na kumtupia ngumi za mbavuni.

Moto ulimwagiwa petroli.

Konstebo Babaa akaona wasipoteze muda. Aliteremka garini kwa lengo la kwenda kutoa msaada ili waendelee na safari. Wasipate kuchelewa.

Likawa kosa!

Kwani ile anajiandaa kupiga hatua, alivamiwa na mtu aliyetoka pembezoni mwa kingo wa lile kalavati upande aliopo. Alidakwa na kuangushwa chini mzima mzima. Waliviringishana kwa sekunde chache kisha wakaachiana baada ya kuhisi kizunguzungu.
Yule mvamizi akawa wa kwanza kuinuka na kumwahi Konstebo Babaa pale chini. Alivyomfikia, alimkita teke la mgongo lililomdidimiza Konstebo Babaa kwa maumivu makali. Akagugumia. Uchungu ukamjaa, na kumpa uharaka wa kufikiri nini afanye apate kujinusuru.

Kosa lingine ambalo Konstebo Babaa alilifanya ni kuto-lock milango. Na kuliacha gari likiwa linaunguruma.

Hivyo pindi wanahangaika na pambano, alijitokeza mvamizi mwingine akaingia ndani ya gari.

Konstebo Babaa akazinduka kwa kutambua hilo kosa. Akapandwa na mori ya kupambana kwa nguvu ili amfuate yule aliyopo garini. Ambaye ni Mauten Mpenyama. Wengine walikuwa Sharif Kinyonga na Shida Mdoka.

Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa hawakuacha kuonyesha umaridadi wao katika nyanja ya mapigano. Waliwakung’uta wale wavamizi mwishowe walikimbilia garini walivyoelemewa. Ile ya kina Konstebo Babaa. Aliyekalia siti ya dereva akakanyaga mafuta kwa nguvu.

Pindi wanaondoka eneo hilo, kwa mbali, ikasikika sauti ya ukokiji bunduki. Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa wakabaki wenye sintofahamu. Uzembe umewagharimu.

***

Koplo Namaya, ambaye kipindi cha nyuma alikuwa Konstebo wakati akishiriki jaribio la kuzima mapinduzi utawala wa Rais mstaafu Bi. Mwema Asononekaye, (riwaya ya Waraka wa Mstaafu) ndiye chanzo cha ile sauti. Alikuwa mita chache nyuma ya eneo lile la tukio. Hakuishia kukoki. Alipeleka mashambulizi huku akiendesha gari, lakini shabaha yake ilienda mrama.

Shambulizi lake liliiendea ile gari iliyotoroshwa na kina Mauten. Lakini umiliki mzuri wa bunduki mkononi ulimtoka, ndiyo maana akawa anakosa kosa, pindi akiwafuata Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa pale walipo.
“Tunajenga nyumba moja. Pandeni tuondoke,” Koplo Namaya aliongea akiwa ameteremka ndani ya gari.

Hawakujadili sana. Ukizingatia ni usiku, uhakika wa kupata usafiri haukuwepo, na wamepoteza msingi wa misheni kizembe. Ilibidi wakubaliane naye. Walipanda ndani ya gari wakaondoka.

Koplo Namaya akamkabidhi Konstebo Babaa ile bunduki, kisha yeye akawa makini kwenye uendeshaji. Luteni Mwaipeta alikuwa ameketi siti ya nyuma.

Kutokana na hasira, Konstebo Babaa alivyokabidhiwa tu ile bunduki alianza kuwashambulia kina Mauten. Hakujali, hata kama gari ni yao. Wavamizi nao hawakuwa nyuma. Kinyonga na Shida walijibu mashambulizi kwa kutumia bunduki za kina Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa walizokuwa wameziacha ndani ya gari.

Isivyo bahati, katika piga nikupige, Kinyonga alipeleka mashambulizi kwenye tairi. Tairi zote za mbele. Gari ikakita na kukuchochora kuelekea nje ya barabara. Ilipoteza uelekeo, mwisho, ilipinduka. Luteni Mwaipeta na wenzie wakiwa mule mule ndani ya gari.

***

Mikanda ya siti ndiyo iliwasaidia. Walinusurika. Lakini, walipata majeraha ya hapa na pale. Pasi na kusahau maumivu yaliyosababishwa na hayo majeraha. Walifanya jitihada za kujitoa, bunduki hawakuhisahau, baada ya hapo walikesha kupunga mikono kusimamisha vyombo vya usafiri vilivyokuwa vinapita muda huo. Hasa magari. Ili wapate lifti itakayowawezesha kuendelea na safari.

Walifanikiwa kupata semi-trailler. Wakapanda na kuondoka, huku kila mmoja akiwazua la kwake. Watajibu nini kwa Kamishna Ndirimwe? Lakini pindi wanaendelea na safari, Luteni Mwaipeta alimtaarifu Kamishna Ndirimwe kilichojiri kwa njia ya ujumbe.

Kamishna Ndirimwe alibaki kughadhibika.
Walivyowasili jijini Nufaiko Kamishna Ndirimwe aliwapokea mwanzo kabisa mwa jiji. Bondeni. Aliwapakiza ndani ya gari na kuelekea mahali fulani ambako wao hawakufahamu. Walivyowasili, jambo la kwanza kufanywa, walipatiwa matibabu na mtaalamu wa afya aliyoandaliwa na Kamishna Ndirimwe. Baada ya hapo walifungua uwanja wa mazungumzo.
“Mumeniangusha vijana wangu,” Kamishna Ndirimwe ndiye alifungua uwanja huo. Walikuwa nje ya jiji kabisa.
“Tunafahamu hilo afande. Tuwie radhi, katu halitokuja kujirudia ukitupatia nafasi kwa mara nyingine,” Luteni Mwaipeta alijibu.
“Mumeweza kutambua waliofanya hivyo?”
Wakatoa utambuzi kwa muonekano.
“Okay! Pumzikeni hapa kwa siku ya leo. Nitafikisha hili jambo kwa washirika wangu tuone namna ya kulitatua.” Kamishna Ndirimwe aliongea na kuanzia kupiga hatua za kuondoka.

Konstebo Babaa akadakia, “Tatizo lako hauko muwazi ndiyo maana tunafeli. Kazi ngumu, ukizingatia wengine tuna matatizo ya kisaikolojia kabla ya hii kazi.”
“Hivi...” Kamishna Ndirimwe aliongea na kutulia kwa sekunde chache. Baadaye aliendelea, “...nini utafanya endapo ukija kubaini mimi ni muhusika wa kushambuliwa kwa mkeo?”

Konstebo Babaa akashikwa na butwaa. Akamtumbulia mboni zake Kamishna Ndirimwe huku mapigo ya moyo yakiongezeka kadri sekunde zilivyozidi kusonga mbele.

ITAENDELEA...

KITABU CHA RIWAYA YA NENDA SASA KINAPATIKANA RENICS BOOKSHOP TAWI LA MOSHI. KWA MAHITAJI, WASILIANA NAO KWA 0767826134
received_2945314115533687.jpg


Sent from my CPH1609 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 07.

Wageni waalikwa wakakenua kingo za mdomo kwa tabasamu.

“Umeona?” Killa alimuuliza Rais Sharabu baada ya hafla kumalizika, na wageni kurejea makwao.
“Lakini bado nina hofu.”
“Ondoa hofu mheshimiwa. Ujue mambo ya intellijensia yanahitaji akili nyingi sana. Ukiwa mtu wa kukurupuka kurupuka, utaishia kufeli. Niamini mimi, ndege wetu lazima wapatikane.”
Rais Sharabu alivuta pumzi na kuzitua kwa nguvu. Moja ya mkono kakamata tama, “Ngoja tuone itakavyokuwa. Ikishindikana, sitokuwa na msamaha wala kusikiliza ushauri wa mtu.”

***

Siku iliyofuata ndiyo ilikuwa mahususi kwa kina Luteni Mwaipeta kwenda kuiba ule mzigo wa pesa kwenye ofisi za idara ya usalama wa taifa. Hivyo mapema sana, kabla muda paswa haujawadia wa tukio kufanyika, Kamishna Ndirimwe na DDGSS Mabele waliwasiliana kwa njia ya whatsapp call kuhitimisha hatua zilizosalia. Kila mmoja, alikuwa ofisini kwake.
“Wameshajiandaa?” Mabele aliuliza.
“Yeah! Nimetoka kuwasiliana nao muda mfupi uliopita. Wanasubiri amri tu kutoka kwetu.”
“Usiache kuwasisitizia, awamu hii wasituangushe.”
“Wameniahidi hilo. Hawatotuangusha.”
“Okay! Nikutakie kazi njema.”
“Nawe pia.”

Wakakata simu.

Haikuchukua muda mrefu, walijikuta kwenye mawasiliano kwa mara nyingine kutoka kwa Luteni Jenerali Kipozi. Aliyepiga kwa kuwaunganisha, wote pamoja kuwa hewani. Alitumia mtandao wa Zoom.
“Ndiyo afande,” Kamishna Ndirimwe alifungua mazungumzo.
“Ya leo ni tofauti hii. I think there is a problem,” DDGSS Mabele alichangia hoja.
“Tena kubwa sana,” Luteni Jenerali Kipozi alisisitizia.
“Kulikoni?” Kamishna Ndirimwe aliuliza akiwa ameanza kushikwa wahka nafsini.
“Munafahamu kuwa zawadi tulizokabidhiwa Ikulu zina vinasa sauti?”

Ukapita ukimya. Si mdogo, ulichukua dakika takribani nne. Wakati huo Kamishna Ndirimwe na DDGSS Mabele kule waliko wakikesha kujisaili mavazini. Walikuwa wamevaa zile zawadi walizokabidhiwa.

Luteni Jenerali Kipozi akaufukuza, “Ndugu?”
“Tumeumbuka,” Kamishna Ndirimwe aliongea huku akiviondoa vile vitu na kuvitupia umbali fulani. Vivyo hivyo kwa DDGSS Mabele.
“Fanyeni tuonane,” Luteni Jenerali Kipozi aliongea na kukata simu.

Baada ya robo saa walikutana nje ya jiji la Nufaiko. Wote, wakitawaliwa na hofu nafsini mwao, kwamba tayari Rais Sharabu na timu yake wameshawagundua ni watu wa namna gani. Wameshagundua uovu wanaoenda kuufanya.

Mwisho wa misheni waliuona unakuja kwa kasi.

“Aisee,” Kamishna Ndirimwe alilalama.
“Haina haja. Tukaze mioyo yetu,” Luteni Jenerali Kipozi alishauri.
“Kwa namna ipi?” DDGSS Mabele aliuliza.
“Hakika naiona kila dalili ya ushindwa mbele yangu. Hakuna tena matumaini, yanayoniaminisha kuwa ni washindi katika hii misheni,” Kamishna Ndirimwe aliendelea kulalama. Wajihi ukiwa umemjaa wahka.
“Endapo sisi tutakata tamaa mapema hivi, vipi kuhusu wale waliotuamini? Vipi wananchi? Haina haja ya kujisalimisha. Mapambano lazima yaendelee.”
“Ki-vipi?”
“Kama utapita muda wa nusu saa pasipo kupokea wito kutoka Ikulu, misheni lazima iendelee.”
“Ndiyo. Ki-vipi? Tusije kujipa imani wakati wenzetu wanatuchora tu.”
“Sisi sote ni makamanda. Tulishayavulia maji haya mambo tangiapo. Hatua zilizosalia ni chache sana kuliko tulizokwisha zipiga. Ni heri watukamate wakiwa wanafahamu hatufurahii utawala wake, kuliko kushusha silaha chini na kuruhusu tusilolifurahia kuendelea.”

***

Mwanzo wa mazungumzo baina ya DDGSS Mabele na Kamishna Ndirimwe yalisikika kwa Rais Sharabu na Killa kama walivyopanga. Waliyafuatilia mazungumzo hayo wakiwa idarani, ofisi husika iliyobeba mitambo ya mapokeo.

Lakini isivyo bahati, hawakufanikiwa kusikiliza mpaka mwisho. Kompyuta itumikayo kupokea sauti ilizima ghafla, kitendo kilichowaghadhibisha Rais Sharabu na Killa.
“Nini shida? Iwasheni haraka tuwasikilize hawa mbwa kabla hawajamaliza mazungumzo yao,” Rais Sharabu aliamuru. Muda wote akipara uwalaza wake, sambamba na kutokwa na kauli kwa sauti ya chini. Ambazo wengine hawakuzisikia. Na kama walisikia, hawakuelewa akitamkacho.

Haikuchukua muda mrefu, vijana walishughulika na kuifanya iwake. Ilivyokaa sawa, walirudi kwenye mfumo, wapate kusikia kiendeleacho! Hakukuwa na muendelezo. Maongezi yaliishia pale pale yalipozimia.
“Nini tatizo?” Rais Sharabu alifoka.

Killa na wale vijana waongozao wakaingiwa na woga.

“Killa! Nini hiki?” Rais Sharabu aliendelea kufoka. Lakini awamu hii alipunguza ukali kidogo.
“Nashindwa hata kuelewa mheshimiwa Rais.”
“Kama mambo yenyewe ndiyo haya ungeniacha nitimilize kile nilichokuwa nimekikusudia.”
“Natambua uchungu ulionao mheshimiwa Rais. Niamini, na endelea kuniamini. Ninafanya haya kwa lengo la kuficha ukweli wa matendo dhidi ya wananchi. Sitaki upoteze sifa zako kwao.”
“Killa, ukicheka na nyani...?”
“Utavuna mabua.”
“Mambo ya intellijensia yameshaisha. Huu ni muda wa action. Muweke kizuizini huyu mtu. Si salama kwangu. Tena wote wawili, yawezekana ni washirika.”
“Bado tuna chambo chao kwetu. Tuzidi kukitumia hicho.”
“Una maanisha nini?”
“Si wanahitaji mzigo wa pesa? Watajileta kuufuatilia, na ndipo tutapowakamatia.”
“Una uhakika?”
“Nina waamini sana vijana wangu. Hawawezi kutuangusha.”
“Yangu macho, nasubiri kuliona hilo likitimilika.”

***

Usiku wa saa tisa, Luteni Mwaipeta, Koplo Namaya na Konstebo Babaa walivamia ofisi za usalama wa Taifa, zilipohifadhiwa zile pesa. Muonekano wao ulikuwa ki-ninja. Kwani walivaa barakoa na mavazi mazito yaliyozuia kuwatambulisha kirahisi.

Bunduki za kimapigano; masafa ya mbali, kwa masafa mafupi zikiwa na utimamu wa hali ya juu. Kwa lolote litakalojitokeza lenye kuzuia misheni yao, ziwe msaada.

Hadi wanafanikiwa kulifikia jengo lilipo, huku nyuma walitatua viunzi kadhaa. Kama vile; kuruka uzio wa ukuta, kukwepa watu wa ulinzi na kamera mbalimbali walizoelekezwa zipo kwenye njia ya kulifikia jengo.

Picha ya ramani zima ilichorwa na DDGSS Mabele. Yeye ndiye aliwaonyesha wapi wapite, wapi wasiweke pua zao na uhitajika mwingine wa kuwafanya wanakuwa salama.

Wawili kati yao ndiyo walipiga hatua hadi mjengoni. Mmoja akiwa mratibu wa namna gani waingie, mwingine mlinzi-kwa kuangaza huku na kule kuhakikisha usalama wao. Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa ndiye walikuwa wahusika wa hilo. Koplo Namaya alichukua maficho mahali kwa ulinzi zaidi. Sniper!

Walilitawala na kulimiliki lile eneo kwa muda mchache kiasi cha kudhania ni wahusika wa kudumu mazingira yale. Baadaye Luteni Mwaipeta alibandika kitu fulani kwenye kitasa cha mlango wa kuingilia mjengoni; mjengo wa ghorofa moja, uliojengwa sehemu pweke na majengo mengine ya ofisi.
“Kazi kwako,” Luteni Mwaipeta alizungumza kwa unong’ozi. Wakati huo akishindilia kisikilizio sikioni.
“Yap! Nimekisoma vyema. One target,” Koplo Namaya aliongea. Taratibu akioanisha vilengeo kuelekezea kwenye lile bandiko. Ambalo lilikuwa katika mfumo wa reflactor. Mahususi kwa kutoa dira ya ushambuliaji kwa mtu aliyopo mbali.

Lile eneo lilitawaliwa na kiza.

Baada ya sekunde kadhaa, Koplo Namaya alifanya mitupo mitatu ya risasi na kuvunja lock za kile kitasa. Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa wakapata Mwaya wa kuchoma ndani.

Bahati, milango mingi ya vyumba vya lile jengo ilikuwa wazi. Hivyo hawakuhangaika sana. Na kwa kupitia msaada wa tochi ndogo waliyotumia kuangazia sehemu fulani fulani baada ya kuiwasha, iliwasaidia kuona yale mabegi ya hela. Tena yakiwa yamehifadhiwa sehemu ya wazi isiyohitaji kutumia nguvu kubwa kuyaona.
“Mbona mambo yameenda rahisi hivi?” Konstebo Babaa aliingiwa wasi wasi.
“Usitake tupoteze muda. Chukua mzigo tutambae.”
“Hili jambo limeenda kirahisi sana. Kama tumeingia nyumbani kwa mtu hohehahe.”
“Kwa hiyo unataka kusemaje?”
“Nahisi uwepo wa mtego.”
“Siku hazifanani dogo. Beba begi tusepe.”

Hofu ya mazungumzo haya yalisikika kwa Kamishna Ndirimwe, DDGSS Mabele na Luteni Jenerali Kipozi wakiwa kwenye jengo fulani wakifuatilia kwa ukaribu kila hatua ipigwayo na vijana wao.

Konstebo Babaa akaafiki. Lakini kwa shingo upande. Moyo haukuridhia kabisa kama kuna usalama wao mahali pale.

Taratibu, kila mmoja akiwa amebeba begi lake begani kwa mfanano wa ubebaji wa majeruhi kwenye mapambano, ule unaoruhusu mkono mmoja kukamatia mzigo husika, mwingine kukamatia bunduki, walipiga hatua za upole lakini zenye uharaka. Walivyoufikia mlango, wanatoka tu, kunusa mazingira ya nje, jengo zima, na maeneo jirani, yakatawaliwa na mwanga wa taa uliowaka ghafla. Wakatupa mabegi na kurudi ndani kujipanga.
“Nadhani sasa umeamini nilichokuwa namaanisha,” Konstebo Babaa alisema.
“Dogo, umebadilika kichizi siku hizi. Tatizo nini?”
“Ina maana umeshasahau mara hii? Kuwa mke wangu yupo hospitalini na sijui afya yake inaendeleaje?” Konstebo Babaa alifoka kwa uchungu.

Kwa upande wa kina Kamishna Ndirimwe.

“Huyu kijana anaweza kutuharibia misheni yetu. Anaonekana kuwa mapepe sana,” Luteni Jenerali Kipozi aliongea.
“Tumvumilie. Atarudi mstarini akishafahamu ukweli wa mambo.”
“Una uhakika anaweza kukuelewa?” DDGSS Mabele aliuliza.
“Yeah! Kwa sababu lile tukio lilikuwa sehemu ya mpango mkakati wetu.”

Idarani.

Baada ya mabishano mafupi walipatana. Namna gani watoke na kuziokoa zile pesa ndiyo mpango uliopo kwa ule wakati.
“Kuna watu wawili wanaokuja. Lakini nahisi hawapo peke yao,” Koplo Namaya aliwataarifu. Akiwa kaweka maficho kwenye moja ya mti, uliotumika kama sehemu ya urembo wa mazingira.
“Kwa hiyo tunafanyaje?”
“We shall think as a active shooter’s.”
“Sahihi.”
“Basi pokeeni kiza. Tumieni kiza nitakachozalisha kujikomboa.”
“We are ready for that.”

Walivyohitimisha mazungumzo Koplo Namaya alikita bunduki kwenye nyama ya bure, na kuruhusu mashambulizi kadhaa kuelekezea kwenye taa zilizozunguka jengo upande wa mbele na upande wa kushoto.

Luteni Mwaipeta na Konstebo Babaa walishambulia zile za upande mwingine.
Kiza kikatamalaki kama awali.
“Hii ndiyo nafasi yenyewe,” Koplo Namaya aliongea.
“We need your cover,” Luteni Mwaipeta alimsihi. Wakati huo wakipiga hatua za mnyato kuelekea mlangoni.

Walivyotoka walijigawa. Mmoja aliangaza upande huu, mwingine ule, bunduki zikiwa mkao wa ushambuliaji. Walivyohisi ukaribu wa watu walioambiwa, walibeba yale mabegi kwa haraka na kuanza kuondoka.

Hawakufika mbali, wakaanza kushambuliwa kwa risasi na wale watu. Tena walishambuliwa huku wakizidi kusogelewa. Walivyohisi wanaelemewa, waligeuka nyuma kujibu mashambulizi kwa kutumia mkono moja kisha safari ya kusonga mbele iliendelea.

Katika ile hatua ya kujibu mashambulizi ndipo Koplo Namaya alijitokeza. Alitumia mwanya huo ili asitoe ubainisho kama kuna mtu mwingine wa ziada. Aliwasaidia kushambulia. Na namna alivyokuwa na shabaha, hakukosa aliponuia kupalenga.

Walivyompita Koplo Namaya walichanja mbuga kwa haraka hadi kwenye geti fulani ambalo walipaswa kutumia kwa kutokea. Koplo Namaya alikuwa amesalia pale pale kukabiliana na wale watu. Ambao ni Shida na Mauten.
“Kiongozi wameshalifikia geti wale wahi kuwashambulia wasivuke,” Mauten aliongea. Maneno yaliyomfungua Koplo Namaya na kuafiki kile alichokihisi. Kuna mshambuliaji mwingine tofauti na wale. Akatega masikio vyema kusikilizia wapi kulipo na purkushani za huyo mtu.

Alifanikiwa kuzipata. Zilitoka nyuma ya lile jengo. Kulikuwa na mti mkubwa ambapo huyo mtu alikuwepo. Kinyonga. Alifahamu kwa haraka kupitia mwanga fulani uliokuwa unacheza cheza matawini. Akanyoosha mtutu wa bunduki kuelekezea huko, wakati huo Shida na Mauten wakizidi kusogea kwa kujivuta vuta kule alipo.

Walikuwa na majeraha sehemu kadhaa yaliyotokana na kufikwa na mashambulizi kadhaa ya risasi.

ITAENDELEA...

BADO HUJACHELEWA. KITABU CHA RIWAYA YA NENDA SASA KINAPATIKANA NCHI NZIMA. WASILIANA NAMI KWA 0693097151 KWA MAELEZO ZAIDI.
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 08.

Rais Sharabu hakutuliana ofisini kwake. Muda wote alizunguka zunguka huku na kule, kichwa kimelowana kwa jasho, sura imefura kwa hasira. Ukiachana na sauti ya vishindo vya utembeaji vilivyotokana na viatu alivyovaa, sauti nyingine iliyosikika ni ya runinga.

Baada ya muda aliingia Killa na Maua.

“Mumeipata hiyo habari?” Rais Sharabu aliuliza pasi na salamu.
“Ndiyo nimetoka kuisikia,” Killa alijibu huku akitumbua mboni zake pima runingani.

Habari iliyokuwa inasomwa muda huo ilikuwa ya dharura. Iliyopata kunena; Ndalama awa huru, baada ya kulipa faini. Alighafirika sana.
“Fanyeni muwezavyo, huyo mtu awekwe kizuizini kwa mara nyingine. Ikiwezekana kaeni na DPP (Director of Public Prosecution) mu-frame kesi yoyote. Hii iwe upande wa chama na serikali. Tena ni amri. Maua tumeelewana? Msivyofanikiwa. Msivyofanikiwa, mnh!” Rais Sharabu alimalizia kwa kufoka.

Kwa pamoja walitii kwa utiifu wa hali ya juu, uliochanganyika na woga. Maana si kwa sura ya Rais Sharabu. Akasirikapo, hutisha zaidi ya mara mia moja ya sura halisi.

Wakaondoka.

Hitimisho la safari yao lilikuwa Rest house ya polisi mkoa wa Nufaiko. Huko walijumuika pamoja na Mkuu wa majeshi, Jenerali Wilson Namkumba, Inspekta Jenerali wa polisi, Moh’d Lukanga, DPP Mmalla na kamanda wa polisi kanda maalum ya Nufaiko, Sacp Chiwila Kadewele.
“Ndugu zanguni, hali ni tete kwa mzee,” Killa aliongea mara baada ya kuketi sofani.
“Kuhusu hili tukio la Ndalama?” Jenerali Namkumba aliuliza.
“Yote kwa ujumla. Hana amani kabisa. Hana amani huyu mtu kuwa uraiani. Na kitendo cha kutoonekana Babigamba ndiyo kinazidi kumtatanisha. Vipi wawili hawa wakionana?”

Ukapita ukimya mfupi.

Jenerali Namkumba akaufukuza, “Nadhani DPP na kamanda hapa Kadewele wanaweza kuwadhibiti kwa namna yao. Au unasemaje IGP?”
“Sahihi kabisa.”
“Mwisho katupa onyo kama wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, tusivyofanikiwa kuwadhibiti, tukae mkao wa kula.”
“Hapaswi kuwa na shaka. Hatuwezi kuruhusu mpango ovu umtokee dhidi yake,” Jenerali Namkumba alisisitiza.

***

Ndalama alikuwa ndani ya gari iliyoandaliwa kumchukua mara baada ya kutoka gerezani. Toyota Land cruiser V8. Aliketi siti ya nyuma. Upande wa kushoto wa dereva. Ambaye ni kijana wa makamo, akadiriaye miaka thelathini.

Taratibu yule dereva alikanyaga mafuta. Mwendo ukiwa wa wastani, vioo full tinted, kiyoyozi kikipuliza vyema, na kufanya ubaridi mdogo uenee ndani ya gari.

Mwendo ukiwa umechanganyia, Ndalama akakumbuka jambo. Lililomsafirisha kifikra kutoka garini na kukumbuka tukio fulani lililopata kutokea wiki tatu zilizopita kabla hajahukumiwa.

WIKI TATU ZILIZOPITA KABLA YA HUKUMU.

Chumba kilitawaliwa na mwanga hafifu. Harufu ya uvundo wa vumbi ukihanikiza vibaya mno, kiasi cha kutoa shinikizo la kupiga chafya kwa mtu yeyote aingiaye kwa mara ya kwanza. Hakikuwa katika mazingira safi. Ijapokuwa si kigezo cha kutotumika. Kilitumika mara kwa mara kihitajikapo. Hasa na askari wa kitengo cha intellijensia. Wakiongozwa na Kamishna Ndirimwe.

Ule mwanga hafifu uliingizwa mule ndani kupitia dirisha dogo lililopo juu karibu na mwanzo wa paa. Pasi na kusahau urembo fulani uliopo mlangoni. Zaidi ya hivyo, hakukuwa na chanzo kingine cha mwanga. Jambo lenye kuleta karaha kwa watu wageni walioingizwa chumbani humo kuhojiwa. Mmoja wapo, Ndalama Machicho.

Ilikuwa ni alhamis, Ndalama alivyoingizwa ndani ya hicho chumba. Asubuhi na mapema, pindi akipelekwa mahakamani kusikiliza shitaka lake. Alipitishwa hapo kwa usiri mkubwa, uliofanywa na Kamishna Ndirimwe baada ya kuwarubuni askari kadhaa waliopo kwenye msafara wa usindikizaji.
“Unaweza kuketi,” Kamishna Ndirimwe alimuamuru. Apate kuketi kwenye kiti kilicho mbele ya meza. Yeye aliketi kwenye kiti kilichopo nyuma yake.

Ndalama akaketi huku akiwa na wajihi uliojengwa kwa udadisi. Ku’nani hadi aingizwe hapo?
“Pole na matatizo,” Kamishna Ndirimwe aliendelea kuzungumza.

Ndalama hakujibu. Aliishia kumtathmini Kamishna Ndirimwe huku akijisemeza nafsini mwake. Aliona anakashfiwa.
“Aaah! Nina jambo moja kwako. Na nipo hapa kama mwakilishi wa wale wenye hitajio wa hilo suala...” Kamishna Ndirimwe akatulia kwa sekunde chache. Alimsaili Ndalama apokeavyo, kisha aliendelea, “...kwanza naomba utambue, kwa namna yoyote lazima uhukumiwe. Japo sifahamu kwa muda gani. Lakini mimi nahitaji nikutoe baada ya hiyo hukumu.”

Ndalama akaingiwa shauku ya kutaka kufahamu kwa kina zaidi hiyo stori. Wake fuadi ulifunguka kwa ushawishi. Lile ghadhibiko lilianza mtoka.
“Nahitaji nikutoe. Lakini kwa makubaliano maalum. Je, upo tayari?”

Ndalama hakujibu kwa uharaka. Alifikiria kwanza kwa sekunde chache kisha akafungua kingo za mdomo wake kuzungumza. Alizungumza kwa sauti ya unyonge, “Yapi?”
“Wanaolilia uhuru ni wengi, hivyo nahitaji uwe sehemu ya mkakati wangu kuurejesha.”
“Kwa hiyo mumeamua kunileta hapa ili munipime? Kisha mumfikishie mtukufu wenu vizuri?”
“Hapana.”
“Hapana nini? Mwambieni anifanyie lolote atakalojisikia. Lakini akumbuke, nguvu ya umma haishindwi. Ipo siku wenye umma wataamua.”
“Mimi ni sehemu ya huo umma. Nimedhamiria kwa dhati kuanzisha huu mkakati. Mkakati halisi, usio na chembe ya kuzidi kukuumiza. Bali nahitaji kulizuia umizo la wananchi kutoka serikalini.”

Wakatazamana kwa sekunde kadhaa pasi na kuzungumza jambo.

Baadaye Kamishna Ndirimwe aliita. Muda mfupi baadaye akaingia kijana mmoja kati ya waliomuongoza Ndalama kuingia humo chumbani awali.
“Mchukue.”

Yule kijana alimuinua Ndalama na kuondoka naye. Walivyofika mlangoni, Kamishna Ndirimwe alipaza sauti kwa wastani, “Ndalama, huu sio mzaha. Hakikisha unaufanyia kazi.”

Akarejesha kumbukumbu garini.

Alianza kwa kuvuta pumzi na kuzitua kwa nguvu. Mwisho, alipangusa uso kama ishara ya kushukuru.

Safari iliendelea, kwa mwendo ule ule pasi na mbwembwe. Mwisho, ulikuwa Bondeni. Dereva akaegesha gari nje ya jengo moja la kifahari. Wakatumia sekunde kadhaa kusalia ndani ya gari pasipo kuteremka. Baadaye akaja kijana fulani mfupi, mnene-mweusi, akafungua mlango upande alioketi Ndalama.
“Karibu sana,” yule kijana alisema mara baada ya Ndalama kuteremka.

Ndalama hakujibu.

Hatimaye aliongozana na yule kijana aliyemfungulia mlango kuingia ndani ya lile jengo, wakati huo dereva akiliondoa gari kuelekea eneo la maegesho. Walipofika sebuleni, mpokeaji alirudi nje na kumwacha Ndalama na watu waliowakuta. Watu waliompa butwaa kwa muda, na maulizo yaliyokosa majibu.
“Karibu Mwamba,” mmoja wa wale watu aliongea. Luteni Jenerali Kipozi. Wengine walikuwa ni Kamishna Ndirimwe na DDGSS Mabele.

Ndalama alishusha pumzi akiwa anaketi sofani. Baadaye akamsaili mmoja baada ya mwingine.
“Nina hakika utakuwa umefanyia kazi ujumbe wangu?” Kamishna Ndirimwe aliuliza.

Kawaida Ndalama hakuwa mtu wa kukurupuka katika maongezi yake. Mara nyingi apewapo nafasi; iwe kwa kuuliza swali, au maelezo ya kawaida, alikuwa anajipa nafasi ya kutafakari. Aridhikapo ndipo hutoa mrejesho. Na hutoa kauli kwa sauti iliyojaa unyenyekevu na ushawishi kwa amsikilizaye.
“Yeah! Nimefanya maamuzi kuhusu hilo,” Ndalama alijibu na kutulia kwa sekunde chache. Baadaye aliendelea, “ Nipo tayari. Lakini kuna kitu nahitaji nifahamu.”
“Kuhusu nini?”
“Nyote ni sehemu ya mpango?”
“Hakika.”

DDGSS Mabele akadakia, “Kama ulivyopata kuambiwa ndugu Ndalama, sisi tumeamua kuwa wawakilishi katika wengi, kuhakikisha yale anayoyapoteza bwana mkubwa yanarejea kwenye mstari wake. Kila chombo kiwe na uhuru wa maamuzi. Kuanzia Bunge, Mahakama na vinginevyo.”
“Kipi kimewashawishi kufanya hivyo?”
“Baada ya kuwabadilikia wale vijana waliomsaidia kuwaondoa maadui waliokuwa wanapinga jitihada za mradi wa bwawa la umeme kule Kilioni. Ukiachilia mbali hilo, manyanyaso anayoyafanya dhidi ya wananchi. Kwa mfano; leo hii si mwajiriwa wa serikali, ama taasisi binafsi, wote wapo kwenye hofu. Hawafanyi kazi yao kwa amani.”
“Kwa hiyo mnataka nini kutoka kwangu?”
Kamishna Ndirimwe akadakia, “Tunahitaji ukakalie kile kiti kupitia uchaguzi unaokuja.”
“Mnawezaje kuongea kishujaa hivyo?”
“Kwa nini?”
“Mnapingana dhidi ya uvunjifu wa katiba. Halafu bado mnataka kuvunja katiba.”
“Ki-vipi?”
“Katiba hainiruhusu kuwa mgombea wa kiti cha urais baada ya ile hukumu. Kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu, mtu yeyote akihukumiwa kwa kosa la uhujumu uchumi, moja kwa moja anapoteza sifa ya kuwa mgombea urais.”

Kamishna Ndirimwe akawaangazia wenzake, lengo kutambua, wameipokeaje ile kauli. Walionekana kupoa.

Ndalama akaendelea kuzungumza, “Inabidi mutafute mtu mwingine. Kuhusu mimi, imeshaungua.”

Ukapita ukimya mfupi. Uliofukuzwa na Kamishna Ndirimwe baadaye, “Ndalama. Ewe bado ni sehemu ya msaada katika hili. Una nafasi ya kutusaidia.”
“Kwa namna ipi?”
“Mfumo wa taifa letu ndiyo mbaya. Nikimaanisha na katiba iliyopo sasa. Mfumo uliopo ndiyo unapelekea yote haya ya leo. Hivyo pindi tukielekea kwenye harakati za uchaguzi, basi nahitaji tufute hatua chache katika nyingi za mpango wetu.”
“Sijakuelewa unamaanisha nini?”
“Lengo kuu ni kubadilisha mfumo. Dhamira yetu kuu, ni kupunguza mamlaka ya kiti cha Rais.”
“Are you serious katika hili?”
“Yeah!” Kamishna Ndirimwe alijibu na kutulia. Alivuta bilauri lililo na maji, akapiga funda kadhaa, baada ya hapo aliirejesha bilauri mahali pake, kisha akaendelea, “Hivyo mfumo inabidi ubadilike kuanzia chamani, ili iwe rahisi kubadilisha katika kiti cha Rais.”
“Siamini kama mna mipango ya hatari namna hii.”
“Hiyo hatari ndiyo uhuru wenyewe. Tukiiondoa, tutakuwa wabwerere.”
“Enhee!”
“Ewe una ushawishi japo haupo chamani. Tufanyie hii kazi, wakati tukiendelea kumtafuta mtu wa kupambana na bwana mkubwa.”
“Mnataka nikafanye nini ndani ya chama?”
“Si lazima, Rais akawa mwenyekiti wa chama.”

Ndalama akashikwa na butwaa.

“Nataka ukaifute hiyo dhana kama ipo ki-katiba. Baadaye tutaondoa mamlaka kwenye kiti cha urais, kwa kumuondolea nguvu ya kuteua baadhi ya watumishi katika nyanja za ki-serikali.”
“Watawala wengi wanaogopa kupinduliwa. Ndiyo maana wamejilimbikizia msururu mrefu wa mamlaka. Huyo mutakayempata, munaamini atakubaliana na matakwa yenu?”
“Tunaamini hivyo pasi na shaka lolote. Lazima tuurejeshe uhuru wetu, na kuuondoa uhuru wa kuazima.”
“Sina budi kuungana nanyi kwa ajili ya watuleane. Mukiachana na ninyi, kuna mtu mwingine anayefahamu huu mpango?”
“Kama yupo utamuona wakati ukifika, kama ulivyotuona sisi leo hii.”

ITAENDELEA...

HABARI NJEMA.

KITABU CHA RIWAYA YA NENDA BADO KINAPATIKANA KWA GHARAMA YA TSH. 10,000/= WASILIANA NAMI KWA 0693097151 KWA MAELEZO ZAIDI.
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 09

Ndalama akashikwa na butwaa.
“Nataka ukaifute hiyo dhana kama ipo ki-katiba. Baadaye tutaondoa mamlaka kwenye kiti cha urais, kwa kumuondolea nguvu ya kuteua baadhi ya watumishi katika nyanja za ki-serikali.”
“Watawala wengi wanaogopa kupinduliwa. Ndiyo maana wamejilimbikizia msururu mrefu wa mamlaka. Huyo mutakayempata, munaamini atakubaliana na matakwa yenu?”
“Tunaamini hivyo pasi na shaka lolote. Lazima tuurejeshe uhuru wetu, na kuuondoa uhuru wa kuazima.”
“Sina budi kuungana nanyi kwa ajili ya watuleane. Mukiachana na ninyi, kuna mtu mwingine anayefahamu huu mpango?”
“Kama yupo utamuona wakati ukifika, kama ulivyotuona sisi leo hii.”
***
Koplo Namaya alifanikiwa kuwadhibiti vilivyo Kinyonga na wenzie. Kwani ndani ya sekunde mbili, alifanikiwa kumshambulia Kinyonga kule juu ya mti na kuwageukia Shida na Mauten ambao walishampita hatua kadhaa pasipo kumuona.
Alivyowageukia, alipiga hatua za haraka kwa mnyato, alipowafikia, aliigeuza bunduki yake, akakamatia kule kwenye mtutu, sehemu ya kitako aliielekezea walipo kina Mauten. Akawapimia kwa sekunde chache, bado hawakugundua kama kuna mtu nyuma yao.
Akamgusa mmoja wao kwa kumshika bega. Alivyogeuka, alimpiga kwa kitako cha bunduki usoni na kubaki kuwa mgugumizi kwa maumivu. Hakuyahimili, kwani yalimpeleka chini huku akiona maruwe ruwe.
Mwenzie, ambaye ni Shida akageuka kwa kasi huku akikielekeza kidole cha shahada kwenye kifyatulio (trigger) lakini hakukiwahi, Koplo Namaya aliinua bunduki yake kwa kasi akampiga nayo usoni. Ukamtoka ukunga wa nguvu, uliohisiwa kufika mbali. Jambo ambalo lingeleta hatari kwa Koplo Namaya na wenzie. Akaona isiwe tabu, akatimua mbio kuwafuata wenzeke.
Walivyofikia lango walivunja kufuli kwa risasi kadhaa kisha wakalifungua. Dakika moja, iliwatosha kuondoka na kuwa ndani ya gari waliyokuja nayo mahali hapo.
Baadaye zile pesa walizikabidhisha kwa Kamishna Ndirimwe, na ndiye aliyefanya utaratibu wote wa kumtoa Ndalama gerezani.
***
Baadaye Ndalama aliondoka. Kamishna Ndirimwe na wenzie wakaendelea kusalia na kuendeleza mazungumzo pale walipoishia.
“Kilichobaki ni kuongeza udhibiti. Waambie vijana wasibweteke,” DDGSS Mabele alisema.
“Wanafahamu. Tena wote, hata yule aliyopo nje ya nchi.”
“Huu mchezo lazima tuushinde.”
“Hatua inayofuata ni ipi?” Luteni Jenerali Kipozi alidakia.
“Babigamba.”
“Ndiye mwanzilishi?”
“Ndiyo.”
“Kwa hatua ipi?”
“Kujiuzulu uanachama.”
DDGSS Mabele akaingilia kati, “Tusitishe kuhusu hilo. Kwani tunaweza kuwa kwenye wakati mgumu?”
“Ki-vipi?”
“Babigamba anapaswa aendelee kuwepo chamani, ili iwe njia rahisi ya kutumika na Ndalama. Halafu, napendelea huyu ndiye tumweke kwenye ile nafasi.”
“Ya urais?”
“Naam!”
Wakatazamana, nyuso zikiwa zimejaa udadisi.
“Lakini...”
“Ndiyo.”
“Lazima tutengeneze mtafaruku ndani ya chama ili tufikie hatua ya mafanikio.”
“Wazo zuri sana.”
***
Dc/cpl Amina alipiga hatua za haraka kuhakikisha anamuwahi Dkt Chota kabla hajafika kwenye vyumba vya choo. Alijiambiza amuwahi barazani, patenganishapo vyoo vya kike na kiume. Kwani angelimuacha afikie vyumba vya choo, ingelimpatia wakati mgumu wa utekelezaji.
Bahati ikawa upande wake.
Alimkuta Dkt. Chota pale pale barazani akiwasiliana na mtu kwa njia ya simu. Akatega sehemu. Mboni zote kaziangazia kwake, huku akifuatilia kila hatua aifanyayo.
Uzuri, hakukuwa na pita pita nyingi za watu.
Dkt. Chota alivyomaliza maongezi na kuanza kupiga hatua za kuondoka kurudi ukumbini, naye alijitokeza pale alipojificha na kupiga hatua za kusonga mbele. Lengo wapishane. Alinuia kuitekeleza hatari yake katika mpishano huo.
Wakapishana.
Lakini Dc/cpl Amina alifanya vile alivyodhamiria. Ule mpishano haukwenda bure, kwani alichomoa sindano alipoihifadhi na kumdunga Dkt. Chota kwa haraka, kisha aliirejesha mfukoni.
Ilikuwa sindano yenye sumu. Sumu ya Arsenic (As)
Dkt. Chota aligugumia kidogo kwa maumivu, huku akijiparata parata na kuangalia kitu gani kimemchoma. Alimwangalia Dc/cpl Amina mara mbili mbili, ambaye alikuwa anapotelea kwenye vyumba vya vyoo vya wanawake. Baadaye alimpotezea na kuendelea na mwendo.
Kule chooni Dc/cpl Amina alizuga tu. Takribani dakika moja, kisha alirejea ukumbini. Hakufikia kuketi pale alipokuwa awali. Aliondoka mazima. Alivyofika nje aliita teksi na kumuamuru dereva ampeleke uwanja wa ndege.
Kitu cha kwanza baada ya kuingia garini, alikumbuka simu yake. Akajipapasa, ili aitoe kisha atume taarifa kwa Kamishna Ndirimwe hatua gani aliyofikia. Lakini hakukuwa na simu. Akashikwa na sintofahamu.
“Dereva simama kwanza.” Dereva alitii.
Aliegesha gari pembeni, akateremka na kuanza kujipapasa upya. Zoezi lililomchukua dakika kadhaa kuhitimika. Hakukuwa na simu.
“Nimeiacha wapi?” Dc/cpl Amina alijiuliza huku akiichakatisha akili yake kwa ajili ya kumbukizi. Tena aliichakatisha kwa uharaka uliochanganyika na wasi wasi.
Akakumbuka. Pale barazani, pindi anamchoma sindano Dkt. Chota, alihisi kupwaya kwa kitu mfukoni mwake. Ina maana kwamba Dkt. Chota aliichomoa simu. Alijilaumu kutolitambua hilo mapema.
Baadaye alirudi ndani ya gari, safari ikaendelea. Walivyowasili uwanja wa ndege alifanya malipo na kuteremka, kisha kwa haraka, aliongoza kuingia jengo la ki-usalama kukamilisha taratibu aianze safari. Safari ya kurudi jijini Nufaiko, aungane na kampani yake.
Vipi simu ikipekuliwa na kutumwa taarifa kwa mheshimiwa Rais?
Hili swali lilimkosesha amani. Na kumpa jutio lililomtoa machozi kwa muda fulani.
Taratibu zilivyokamilika aliingia ndani ya ndege paswa safari ikaanza. Muda wote akiwa mwenye maombi, ndege iongeze kasi apate kuwahi kufika, ili atoe taarifa kwa wenzake, waone namna gani watatatua.
Kama alivyohisi, Dkt. Chota baada ya kutoka ukumbini, huku afya ikizidi kuzorota kadri sekunde zilivyozidi kusonga mbele, aliipeleka ile simu kwa moja ya mtaalamu na kumwamuru atume taarifa katika barua pepe aliyompatia. Lilikuwa tukio la nusu saa.
“Pokea hizo taarifa, zichambue na uzifanyie kazi. Juu ya hilo, hali yangu haiwezi kuhimarika tena, kwa sababu ya kile alichonifanyia muhusika wa hayo mawasiliano. Nimebainika,” Dkt. Chota aliambatanisha hiyo kauli, kisha alimtumia Killa.
Ilivyomfikia Killa alifanya kama alivyoambiwa. Aliisoma, aliichambua na kubaini yaliyomo. Ulikuwepo mkakati wa kumuondoa Dkt. Chota kama ulivyofanyika, na mikakati mingine ya kumfanya Rais Sharabu anakuwa Rais wa muhula mmoja.
Hakuamini. Kiasi kwamba alirudia mara mbili mbili kuisoma ile taarifa. Alivyoridhika nayo, alifungua safari hadi Ikulu kumpasha Rais Sharabu.
“Kwa hiyo tunafanyaje Killa?” Rais Sharabu aliuliza kwa sauti iliyojaa unyonge kiasi. Mara baada ya kusoma taarifa aliyopatiwa.
“Napendekeza tukaweke ulinzi uwanja wa ndege. Ili akiteremka tu, tupo naye.”
“Huyu ni mtu wa tano katika orodha yangu. Halafu hamna matokeo yaliyochukuliwa kuwadhibiti. Kama hawa wanne wa awali umeshindwa, una uhakika huyu utamuweza? Au kwa sababu ni mtoto wa kike?”
“Kupitia haya mawasiliano, nina hakika watatu katika orodha yako tutakuwa nao safe house kuanzia leo hii.”
“Nani na nani?”
“Kamishna Ndirimwe, DDGSS Mabele na huyu binti. Amina.”
“Vipi kuhusu Babigamba na yule mpuuzi aliyemtorosha?”
“Kama wapo kundi moja, naamini tutawapata kupitia hawa tutakaoanza kuwashikilia.”
“Okay! Fanya ulivyoniambia kwa uhakika.”
“Hamna shida.”
Baadaye Killa aliandaa vijana kwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya kumkamata Dc/cpl Amina. Akishirikiana na Kamanda wa polisi kanda maalum ya Nufaiko, Sacp Chiwila Kadewele. Askari wa jeshi la polisi na vijana wa usalama wa taifa wakajaa kila kona, mithili ya mtu waliyemfuata ni gaidi, aliyesumbua mataifa makubwa kwa miaka mingi.
Wengine walitumwa nyumbani kwa Kamishna Ndirimwe na DDGSS Mabele.

ITAENDELEA...

KITABU CHA RIWAYA YA NENDA BADO KINAPATIKANA RENICS BOOKSHOP TAWI LA MOSHI. JIPATIE NAKALA YAKO KWA TSH. 10,000/= MAWASILIANO; 0767826134
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 10.

Taarifa za kutumwa vijana wa usalama wa taifa, na askari wa jeshi la polisi kwenda kumkamata Dc/cpl Amina zilimfikia Kamishna Ndirimwe akiwa na wenzie kwenye jengo lao la siri maeneo ya Ngowe.
Hakuna aliyetuliana baada ya kufikwa na taarifa hii. Kila mmoja alikuna kichwa na kufikiria mara mbili mbili, nini hatma baada ya Dc/cpl Amina kukamatwa.
“Tutamfikishia vipi taarifa? Inabidi aokokane na hili, ndiyo usalama wetu,” Luteni Jenerali Kipozi aliongea,wahka ukiwa umemjaa.
“Tambua yupo hewani. Ni ngumu kupata mtandao,” Kamishna Ndirimwe alijibu.
“Kwa hiyo upo radhi mpango wetu uvuje?”
“Naamini kufikia hapo umeshavuja tayari. Kitendo cha kutumwa...” Kamishna Ndirimwe alisema. Lakini hakumalizia kauli yake, akakatishwa na miito kutoka kwenye simu; za wote, iliyoashiria kuna ujumbe umeingia.
Walitoa walipozihifadhi na kuzisoma.
“Mupo hatarini. Wawili miongoni mwenu, watakamatwa hivi punde. Kuweni salama,” ulisomeka ujumbe waliotumiwa.
Wakatazamana kwa unyong’onyo. Luteni Jenerali Kipozi mara mbili yao.
“Hamna cha ziada,” DDGSS Mabele alisema akiwa anajiketisha sofani.
“Kwa hiyo huu ndiyo mwisho wa mpango wetu? Kweli tunaruhusu kufeli?” Luteni Jenerali Kipozi aliuliza.
“Nina hakika, ewe haupo katika orodha iliyomaanishwa hapa. Utakuwa nje, hivyo usisite kuendeleza mapambano. Wanatuleane wanahitaji kwa udi na uvumba kile tunachokipigania. Kukamatwa kwetu kukupe hamasa, ya kuzidi kufanya kweli mpango usitetereke,” Kamishna Ndirimwe alijibu.
Baadaye waliondoka; kila mmoja na uelekeo wake. Hawakupaswa kukamatwa wakiwa pamoja, ndiyo maana ya ule ujumbe waliotumiwa. Kwani kukamatwa kwao pamoja, ingeliwaletea hatari zaidi.
***
Luteni Mwaipeta, Koplo Namaya na Konstebo Babaa nao walipata taarifa kuhusu Dc/cpl Amina. Amani iliwatoka. Nafsi zilitukuta kwa hasira na wasi wasi, atakamatwa? Au atafanikiwa kutoroka?
Konstebo Babaa ndiyo akawa muathirika zaidi, ukizingatia ni mkewe.
“Alifanikiwa kupona? Mbona hakunitafuta baada ya hapo? Imekuaje hadi agundulike?” Konstebo Babaa alijiuliza maswali mengi pasi na kuyapatia ufumbuzi.
Yale maswali yakamfanya hadi atokwe machozi, kwa jinsi ambavyo alijisikia kuumia.
“Kuna chochote ambacho nilifichwa na hawa watu?” aliendelea kujiuliza. Baadaye akakumbuka ile kauli aliyowahi kuambiwaga na Kamishna Ndirimwe, ‘nini utafanya endapo ukija kubaini mimi ni muhusika wa kushambuliwa kwa mkeo?’
Luteni Mwaipeta na Koplo Namaya wakamsogelea pale alipo.
“Mbona unatuangusha ndugu?” Luteni Mwaipeta aliuliza.
Konstebo Babaa alifuta chozi lililokuwa linamtiririka kisha alijibu, “Hamjui maumivu ninayopitia. Naomba muniache kwanza nipumzike.”
“Wewe ni kamanda, hupaswi kuwa hivyo. Kinachopaswa kwa sasa ni kufikiria ni namna gani tunahitimisha hii misheni.”
“Misheni gani ambayo haina kichwa wala miguu? Haina uelekeo. Ndiyo maana tunafeli kila wakati. Imekosa mipango na mikakati,” Konstebo Babaa alifoka. Kijasho chembamba kikimnawiri wajihini.
Baadaye walipokea ujumbe kwenye simu zao. Ukakatisha malumbano na kuelekekeza akili huko. Haukutumwa kwa wao pekee, ulitumwa pia kwa; Babigamba, Ndalama na Luteni Jenerali Kipozi.
Ulisomeka, “Huu ni kama mchezo wa mpira. Iwe; wa miguu, pete ama kikapu, utokapo uwanjani, hakosekani mtu wa kwenda kuuokota na kuurejesha tena uwanjani mechi ipate kuendelea.”
Ukawapa fikirio.
Nani katuma? Ukizingatia namba ni ngeni. Walivyojaribu, kila mmoja kwa wakati wake kuitafuta ile namba haikupatikana.
“Isije kuwa mambo yamezidi kuharibika huko, kwa hiyo hapa tunategwa kama tumoo,” Konstebo Babaa alilalama.
“Acha kulalamika basi. Unakuwa kama mtoto mdogo kwenye hii mambo,” Koplo Namaya alichangia.
“Wameniudhi bhana.”
Luteni Mwaipeta akadakia, “Kama umeudhika acha kushiriki.”
“Nitaacha tu.”
“Eeh! Acha ili ukamuokoe mkeo vizuri.”
***
Ule muda wa ujumbe, hata kwa Jackson pia uliingia. Lakini haukuwa sawa na waliotumiwa watu wengine. Aliotumiwa ulisomeka, “Rejesha utulivu wa nafsi zilizokata tamaa.”
***
Pindi fukuto la kina Kamishna Ndirimwe halijaisha; machoni, mdomoni na masikioni mwa wengi, Jackson alitumia nafasi hiyo kutekeleza alichoamriwa kwenye ule ujumbe. Yeye hakuwa na hofu na mtumaji, alionekana kumfahamu.
Aliachia barua mtandaoni. Barua iliyoonyesha Babigamba anajiuzulu nafasi zote za ki-uongozi alizonazo ndani ya chama cha Chautu. Atasalia kuwa mwanachama wa kawaida.
“Nimelazimika kuchukua maamuzi haya pasi na shinikizo lolote. Sijalazimishwa na mtu. Ni hiyari yangu. Hivyo nawaomba wanachama, wa chama cha Chautu, wasio wanachama wa chama cha Chautu na wakereketwa wote wa siasa nchini na duniani kwa ujumla, ambao walipendezwa na aina ya uongozi nilionao chamani, kupokea maamuzi haya kwa mikono miwili. Hatua niliyochukua ni sehemu pia ya ujenzi wa chama,” sehemu ndogo ya ile barua ilisomeka hivyo.
Watu wakapokea kwa maono tofauti.
Kwa Rais Sharabu alivyopata taarifa aligeuka mbogo. Moja ya mkono wake ulikesha tamani, huku mboni kaziangazia mithili ya goroli za mawindo kwenye simu aliyotumia kusoma hiyo barua.
“Mbona sielewi elewi?” alijiuliza huku akimpigia simu Babigamba. Lakini namba yake haikupatikana.
Baadaye akampigia Killa.
“Tukutane safe house walipohifadhiwa wale mbwa,” alisema mara baada ya simu kupokelewa.
“Sawa mheshimiwa.”
Akakata simu.
Kwa mujibu wa taratibu za ki-usalama wakamatwapo wahalifu wengi walioshiriki kutenda kosa moja; kwa wakati mmoja, na sehemu moja huwa wanatenganishwa katika uhifadhi. Yaani hawahifadhiwi pamoja. Hufanywa hivyo, kwa ajili ya kukwepesha ushirikiano wao wa kujitetea. Kuachiangana mawazo namna ya kukabiliana na tuhuma.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Kamishna Ndirimwe na DDGSS Mabele. Walihifahdiwa nyumba tofauti. Lakini uhitaji wa Rais Sharabu kuwaona, wakalazimika kuwekwa chumba kimoja, Rais Sharabu atakavyomaliza mambo yake watenganishwe tena.
Kwa muda mchache walioshikiliwa walionekana kuwa na utofauti. Muonekano wao ulibadilika. Kuanzia rangi ya ngozi na uhalisia wa maungo. Walikuwa na mauvimbe, pasi na kusahau michubuko, iliyotoa ishara kuna kichapo walishachezea.
Rais Sharabu alivyowasili wala hakukuwa na salamu. Moja kwa moja alienda kwenye dhamira yake.
“Nyie, huu ujinga mumefanya ninyi ili mnichanganye?” Rais Sharabu aliuliza huku akiwaonyeshea ile barua simuni.
Waliitazama kwa nukta chache, kisha wakakanyagana nyayo. Ilikuwa kama ishara ya kupongezana. Kwani hata wajihi ulionesha nuru kwa tabasamu.
“Tuna hiyo jeuri ya kufanya hivyo?” Kamishna Ndirimwe alimjibu kwa mtindo wa swali. Tena kwa sauti ya unyenyekevu.
“Ndiyo mnajeuri. Kwa muda mrefu tumefuatilia matendo yenu. Ni matendo ovu, yaliyojaa usaliti kwangu. Yule binti ambaye alikuwa mpelelezi ametuthibitishia hilo kupitia mawasiliano yenu tuliyoyakamata.”
“Mungemuuliza vizuri. Yumkini kuna mtu kamuhifadhi kwa ufanano wa jina langu kwenye simu yake. Si mumeangalia namba ya huyo Ka...”
“Acha ujinga wewe mzee,” Killa alidakia.
“Mumeingia pabaya. Kwa sababu hamkutaka kuendana nami. Sasa nitawanyoa vilivyo, ili wenzenu, na wale wenye matamanio kama ya kwenu wapate funzo. Mimi sio wa kuchezewa chezewa,” Rais Sharabu aliendelea kuongea kwa kufoka. Vi-mate vikimruka ruka.
“Huu si wakati sahihi wa kufanya mtakayo. Kaeni chini mutafakari upya,” Kamishna Ndirimwe alijitetea. Kauli iliyochangia ukimya kwa nukta chache, na kufanya wasailiane huku wakitafakari ile kauli.
Baadaye waliingia vijana wawili mule ndani wakiwa wameongozana na Dc/cpl Amina, aliyekuwa amejawa uso wenye mashaka na jutio. Hatua zake zilikuwa fupi fupi zenye kujiamini.
Rais Sharabu akamtumbulia mboni zake kumsaili. Akafuatia kusonya.
Wale vijana walimketisha kitini Dc/cpl Amina kwa nguvu kisha waliondoka. Rais Sharabu akapiga hatua kumfuata. Alivyomfikia alimshika kidevu chake na kuanza kumtingisha tingisha.
“Ewe hayawani,” Rais Sharabu alisema na kumtandika kofi.
Dc/cpl Amina alikunja uso kwa hasira huku akiwazua hali ya maumivu apitiayo nafsini mwake kuwa chanzo cha yale yanayojiri muda huo.
“Kipi munachohitaji kutoka kwenye utawala wangu? Eeeh! Nyie wazee, hamlipwi mshahara?” Rais Sharabu aliendelea kutawala mule ndani kwa kusikika yeye tu.
Wakati Dc/cpl Amina anaingizwa ndani ya lile jengo, Konstebo Babaa alikuwa mita chache akishuhudia. Uwepo wake mahali hapo haukuwa wa ghafla. Bali alifuatilia msafara uliomleta mkewe toka uwanjani.
Alisimama mahali hapo mboni zote kaziangazia mjengoni. Hasira ikimtukuta, mwili ukitetemeka kutokana na mapigo ya moyo kwenda kasi. Hasira ilivyomzidi alitamani aingie ndani akamuokoe mkewe. Kwani yeye ndiye mtu wa kwanza ambaye alipaswa kumuondolea utata alionao.
“Liwalo na liwe. Heri tushikiliwe wote,” alijisemeza huku akipiga hatua taratibu kulifuata lango la kuingilia.
Alipiga hatua mbili tu, akahisi kuna kitu kinamvuta kwa nyuma. Akageuka ajionee. Hakuamini! Hakuamini awaonaye.
“Usipige hatua ndefu kwa haraka hivyo. Kwani utavivuka vitu vingine nyuma, ambavyo vina umuhimu wa kushuhudiwa,” mmoja wa wale watu alisema.

ITAENDELEA...

HABARI NJEMA

KITABU CHA RIWAYA YA #NENDA SASA KINAPATIKANA RENICS BOOKSHOP TAWI LA MOSHI. FIKA JENGO LA FRESH COACH SAKAFU YA CHINI UJIPATIE NAKALA YAKO KWA GHARAMA YA TSH. 10,000/= AU, UNAWEZA KUJISOMEA KWA GHARAMA ISIYOZIDI TSH. 5,000/= KATIKA #SIMULIZI_AFRICA_APP.
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 11.

Wakati Dc/cpl Amina anaingizwa ndani ya lile jengo, Konstebo Babaa alikuwa mita chache akishuhudia. Uwepo wake mahali hapo haukuwa wa ghafla. Bali alifuatilia msafara uliomleta mkewe toka uwanjani.
Alisimama mahali hapo mboni zote kaziangazia mjengoni. Hasira ikimtukuta, mwili ukitetemeka kutokana na mapigo ya moyo kwenda kasi. Hasira ilivyomzidi alitamani aingie ndani akamuokoe mkewe. Kwani yeye ndiye mtu wa kwanza ambaye alipaswa kumuondolea utata alionao.
“Liwalo na liwe. Heri tushikiliwe wote,” alijisemeza huku akipiga hatua taratibu kulifuata lango la kuingilia.
Alipiga hatua mbili tu, akahisi kuna kitu kinamvuta kwa nyuma. Akageuka ajionee. Hakuamini! Hakuamini awaonaye.
“Usipige hatua ndefu kwa haraka hivyo. Kwani utavivuka vitu vingine nyuma, ambavyo vina umuhimu wa kushuhudiwa,” mmoja wa wale watu alisema.
***
Sintofahamu na mvurugano ulitokea ndani ya chama cha Chautu. Barua ya kujiuzulu kwa Babigamba ikiwa chanzo. Si viongozi waandamizi, wala wanachama wa kawaida, kwa pamoja waligawanyika. Na kuunda makundi matatu kulingana na mapendo waliyonayo. Wapo; walioegemea upande wa Babigamba, wengine upande wa Rais Sharabu, na wengine kati. Mtu-kati, kwa sababu ya hofu.
Hiyo ikawa nafasi kwa Ndalama.
Kitu pekee alichohitaji hiyo hila iendelee kudumu. Ili apate mwanya wa urahisi wa kushawishi. Kwa sababu mgawanyiko ulimtengenezea njia, alitumia nguvu kubwa upande wanaomuunga mkono Rais Sharabu. Alianza kuwafuata wao, hasa wanachama wenye nguvu. Na waandamizi waongozao jumuiya; ya wazazi, na wanawake.
Alianza na wenyeviti wa jumuiya hizi. Jumuiya ya vijana hakuigusa kabisa, kwa sababu alifahamu, wengi wao ni watu wa kujipendekeza kwa ajili ya uhitaji wa madaraka.
Baadaye aliwafuata wenyeviti kadhaa wa mikoa, huko aliwapata kumi na tano. Kati ya ishirini na saba waliokuwa wanamuunga mkono Rais Sharabu. Kisha alihamia kwa wale wanaomuunga mkono Babigamba. Upande huu alikuwa kama anamsukuma mlevi. Hakupata ukinzani wowote, japo hofu haikukosekana.
“Tukikamatwa si kesi ya uhaini hiyo?” mmoja kati ya wale aliowashawishi alimuuliza. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake Taifa. Bi. Siti Likuluta.
“Haitotokea hiyo nafasi. Kwanza, ndani ya chama hakuna uhaini. Huko mnatimiza wajibu kama wanachama.”
“Kwa hiyo ni lini huo mpango utakaa sawa?” Mwenyekiti Jumuiya ya wazazi naye aliuliza. Bw. Njaidi Kalindima.
“Utaanza mwezi juni. “
“Kuna hakika yoyote katika hili?”
“Naam! Ondoeni hofu.”
“Lazima tuwe na hofu, kwa sababu wewe mwenyewe hauna uhakika na maisha yako mbele ya bwana mkubwa. Muda wowote unaweza kuwa mtu wa nyuma ya nondo.”
“Aliweza mwanzo. Sasa hivi itakuwa ngumu kufanikiwa. Labda, nitolewe nje ya hii misheni.”
“Na kina nani?”
“Yenu macho. Sipo peke yangu. Tupo wengi, na kila mmoja ana jukumu lake. Mimi langu ni hili, ninyi lenu ni lile la mwezi juni. Wao, lao ni kuhakikisha utulivu wa nafsi za wengi unarejea nchini. Aidha; kwa kumuondoa Rais Sharabu madarakani, ama hata akiwepo madarakani.”
“Sawa. Twa-subiri.”
“Kikubwa, msiniangushe.”
“Tumekuelewa,” waliitikia wale wenyeviti kwa pamoja.
Alivyohitimisha zoezi la urubuni alikutana na Luteni Jenerali Kipozi kwenye lile jengo alililowakuta siku ya kwanza mara baada ya kutoka gerezani.
“Naamini mambo yananyooka,” Luteni Jenerali Kipozi alifungua mjadala.
“Tena kwa kiwango kikubwa. Wengi wao wanasubiri muda tu, wafanye utekelezaji.”
“Ni jambo la kushukuru. Tuendelee kuwa madhubuti, yasitokee, yaliyotokea.”
“Imani yangu ipo kwako. Wewe ndiyo kioo uliyebakia, kamwe usivunjike, ili nami, na wengineo, tupate sehemu ya kujitazamia.”
“Tunaenda kushinda, haina haja ya kujijengea hofu moyoni.”
***
Usiku. Ukimya ulitamalaki maeneo mengi jijini. Mihangaiko ya watu ikawa ya haba, kiasi cha kuleta uogofyaji kwa wenye roho nyepesi.
Wakati huo Rais Sharabu alikuwa kikaoni Ikulu na waandamizi wachache wa chama cha Chautu; Katibu Mkuu, Katibu wa itikadi, siasa na uenezi na Naibu Katibu Mkuu.
“Hili suala la barua ya huyu Babigamba limekaaje kaaje?” Rais Sharabu aliuliza.
“Ni tata mheshimiwa. Kwa sababu hakuna barua yoyote iliyoletwa ofisini ambayo inaonyesha imetolewa naye,” Katibu Mkuu alijibu.
“Ina maana wananichezea akili?”
“Tujaribu kumtafuta...” Naibu Katibu Mkuu naye alichangia hoja. Lakini kabla hajamaliza akakatishwa na Rais Sharabu.
“Maua, jitihada za kumtafuta zimefikia wapi? Na ule mpango wa kumpatia kesi umefikia wapi?”
“Kazi ni nzito mheshimiwa. Mpaka sasa vijana hawafahamu alipo, na isitoshe mawasiliano yake hayapatikani.”
“Mwandishi aandikaye hizi habari?”
“Naye anaendelea kufuatiliwa.”
“Munachukua muda gani kumfuatilia? Kituo chake cha kazi si mnakifahamu? Nendeni hapo, kama Mkurugenzi ataleta janja janja tufunge kituo.”
Ukapita ukimya mfupi. Rais Sharabu akaufukuza baada ya muda kwa kuita, “Katibu!”
“Ndiyo.”
Katibu Mkuu hakujibu kwa uharaka. Alifikiria kwa muda mfupi kwanza, ndipo alijibu, “Kwa taratibu za chama huu ni utovu wa nidhamu. Lakini ki-ubinadamu nadhani sote tunafahamu ni mgonjwa, hivyo yawezekana alipo anafanya jitihada za kujitibu...”
Rais Sharabu akamkatisha, “Unashaurije?” alifoka.
“Tujipe muda wa kuendelea kumtafuta. Kwani naamini huko alipo ni kwa ajili ya usalama wake.”
“Sio naye tumfukuze kama mwenzake?”
“Haina haja ya kufanya haraka hivyo. Nashauri, atafutwe mwandishi aliyechapa hii barua atauambie wapi kapata hayo maelekezo ya kufanya hivi. Kupitia yeye, nadhani tutapata uamuzi sahihi kumuhusu Babigamba, maana siku hizi wamejaa waandishi makanjanja, wasio na weledi juu ya hii taaluma. Yumkini alijitungia tu,” Naibu Katibu Mkuu alishauri.
“Yeah!” Katibu Mkuu aliafiki.
Kwa pamoja wakaafiki ushauri wa Naibu Katibu Mkuu.
***
Katika hali ya kuutafuta usalama Babigamba alipelekewa nchini Marekani, katika jiji la Washington DC. Mambo yote akawa anayafuatilia akiwa huko. Hakuna lililompita. Ile siku iliyozua taharuki kwa wengi yeye alipokea ujumbe kwenye barua pepe aitumiayo. Ujumbe uliosomeka, “Tunaelekea kukamilisha hatua zetu. Utarudi nchini mwezi juni kwa ajili ya kugombea urais.”
Akaingiwa na sintofahamu.
Ukinzani ulimchipua kwa nguvu, upi usahihi wa kitendo alichoambiwa.
Alipata hofu. Na aliyemfanya aipate hofu hiyo ni Rais Sharabu. Kwa sababu anafahamu, hali apitiayo yeye ndiyo chanzo. Hali afanyiwayo Ndalama yeye ndiye chanzo. Vipi akiingia kwenye kinyang’anyiro pamoja? Ilihali tamaa ya Rais Sharabu ni kuona hajitokezi mtu ndani ya chama akaitamani hiyo nafasi.
“Huu mbona ni mtihani?” Babigamba alijiuliza mara mbili mbili huku akiusaili ule ujumbe.
“Huu utakuwa mwanzo wa kujiweka kwenye matatizo zaidi. Kamwe hawezi kuniacha salama nikitekeleza hili,” Babigamba aliendelea kujisemeza.
Baadaye alivuta pumzi na kuzitua kwa nguvu.
Akazama, mawazoni. Yaliyomshinikiza akatae mpango alioambiwa kwa ajili ya usalama wake na familia kwa ujumla. Alichukua simu na kuingia sehemu ya barua pepe. Lengo amjibu yule aliyempatia ile taarifa.
Akaanza kuandika, “Msaada niliowapatia unatosha. Kwenye hili la sasa, mtafuteni...” Akasita kwa sekunde chache. Hasa baada ya kupatwa na kumbukizi ya siku kadhaa nyuma, kwa mara ya kwanza alipokutana na Kamishna Ndirimwe akashirikishwa kwenye mpango, “Tunafanya haya, kwa niaba ya wale wa chini wanaokosa nafasi ya kupaza sauti. Hebu tubebe sauti zao, kisha tuziamulie.”Akaufuta ule ujumbe na kuitua simu mezani.
Akafuatia kujiangusha sofani huku akizidi kuyatafakari maneno ya Kamishna Ndirimwe. Yalimpa ujasiri wa kupambana na Rais Sharabu.

ITAENDELEA...

HABARI NJEMA

RASMI, KITABU CHA RIWAYA YA #NENDA SASA KINAPATIKANA #RENICS_BOOKSHOP TAWI LA MOSHI. FIKA JENGO LA FRESH COACH SAKAFU YA CHINI UJIPATIE NAKALA YAKO KWA TSH. 10,000/= MAWASILIANO: 0767826134
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 12.

“Jenerali!” ilisikika sauti ya upande wa pili pindi Luteni Jenerali Kipozi akiwasiliana kwa njia ya simu.
“Ndiyo.”
“Hapa nilipo nipo na maaskofu karibia wote unaowafahamu nchini. Ukiachana na hao, nina viongozi wa dini ya kiisilamu pia, wakiongozwa na Mufti. Hongera sana.”
“Ya nini tena?”
“Hiyo harufu haifukizi chumbani kwenu pekee. Hata kwetu pia inatufikia.”
Luteni Jenerali Kipozi akaangusha kicheko kwa sekunde chache.
“Mumeamua. Mumedhamiria, hakuna cha kuwapatia zaidi ya kukuambia hongereni sana. Sisi tupo nyuma yenu, mkihitaji msaada wa aina yoyote musisite kutuambia.”
“Mupo tayari kufuta machozi ya wengi?”
“Ni tamanio la siku nyingi sana. Tulikosa muanzishaji tu.”
“Basi huo moshi ufukize taratibu. Usienee, ili tuufaidi wenyewe. Majirani hawapaswi nobe! Kuvuta harufu yake.”
“Hamna shida.”
Akakata simu.
***
Ilikuwa ni alhamis, Maua alivyoenda hobela hobela kwa Rais Sharabu. Hakuwa katika hali ya umakini-alionekana kuchanganyikiwa, kwani hakuwa kwenye mavazi yaliyovaliwa kinadhifu. Yalikuwa machafu, aidha kwa makusudi ya kuyavaa, au sehemu alizopita kabla ya kumfikia Rais Sharabu. Pasi na kusahau wajihi ulimuenea jasho jingi.
“Sijazoea kukuona ukiwa hivyo,” Rais Sharabu aliongea. Pindi wameketi kwenye viti bustanini.
“Mambo si mambo. Jambo la kushukuru tumefanikiwa kuwadhibiti hawa watu mapema.”
“Mbona unazunguka, ku’nani?”
Badala ya kujibu, Maua alitoa simu janja kwenye pochi yake. Aliperuzi kwa sekunde chache kisha alimpatia Rais Sharabu.
Rais Sharabu hakuishia kuipokea tu. Aliangazia ni nini kilichomsukuma apatiwe ile simu. Ulikuwa ni ujumbe.
Akausoma, “Mpe heko mheshimiwa. Kwa kuweza kuwadhibiti hao watu, kwani walikuwa na nia ya kumuondoa madarakani kwenye kinyang’anyiro kijacho cha uchaguzi.”
Akaurudia kuusoma mara mbili mbili.
“Nani kakutumia?” Rais Sharabu aliuliza pindi akimrejeshea Maua simu yake.
“Mwenyekiti wa chama chetu mkoa wa Zama.”
“Alijuaje?”
“Alifuatwa na Ndalama aunge jitihada.”
“Kwa hiyo Ndalama ndiyo master plan?”
“Inavyoonekana.”
Ukapita ukimya mfupi. Kabla haujafukuzwa na Rais Sharabu, “Kwa mantiki hiyo tumeshamla mbuzi wa shughuli kwa tulichokifanya.”
Wakaangusha kicheko cha nguvu.
Kile kicheko kilikatishwa na sauti ya ufunguaji mlango. Wote wakageuka kumwangalia aingiaye. Alikuwa Killa.
“Hima hima, kulikoni?” Rais Sharabu alimvaa kwa ulizo kabla hajaketi.
Killa aliketi kwanza ndipo alijibu lile swali, “Mambo yanazidi kwenda vyema upande wetu.”
“Kuna’ni tena?”
“Vijana wamefanikiwa kumpata mwandishi wa hizi habari zituchafuazo.”
“Ni nani?” Rais Sharabu na Maua wakajaa nyuso zenye matamanio ya kutaka kufahamu kile alichonacho Killa.
“Jackson.”
“Yule mjinga ambaye aliandika ile taka taka waliyoipachika jina la ushauri?”
“Yeah! Ndiye mwenyewe.”
“Wamefahamu anapopatikana?”
“Bado. Lakini wapo mbioni kupafahamu. Nina hakika hawatochukua muda mrefu.”
“Wahimize. Vile vile naona hawa wajinga tuwashikiliao huu ndiyo muda wa kuwaandalia safari ya kuzimu. Hawapaswi kabisa kuwa hai.”
“Sahihi. Lakini tusifanye kwa kukurupuka. Tuendelee taratibu, ili wananchi wasipatwe hofu na shauku ya kutaka kufahamu upande wetu wa pili wa shilingi,” Maua alipendekeza.
“Umenena. Mheshimiwa, alichoongea kamanda hapa kipo mule mule,” Killa alikazia. Huku akitingisha kichwa, juu-chini.
“Ninyi ndiyo ngumi ya mkono wangu wa kulia. Naamini hamuwezi kuniangusha.”
Wakatabasamu.
***
Mtuma ujumbe, ule ulioingia kwenye simu za kina Luteni Jenerali Kipozi na watu wake alikuwa Makamu wa Rais, Lilian Mkumba. Na ndiye aliyemsitisha Konstebo Babaa kuingia safe house. Aliambatana na Mkuu wa majeshi, Jenerali Wilson Namkumba.
Wakaingia ndani ya gari na kuondoka.
Mwisho wa safari ulikuwa pale walipo kina Luteni Mwaipeta. Waliteremka, na kuongoza moja kwa moja ndani. Waliwakuta Luteni Mwaipeta na Koplo Namaya wakitazama mechi runingani.
“Ndugu, umeondokaje ondokaje hapa?” Luteni Mwaipeta alimvaa vaa Konstebo Babaa kwa ulizo.
“Nilikuwa hapo jirani nikinyoosha nyoosha viungo.”
Makamu wa Rais akaingilia kati, “Tuachane na hayo. Sogeeni jirani tupate kuteta. Lakini kabla hatujaanza maongezi, mtaarifuni Luteni Jenerali Kipozi naye awepo hapa.”
Wakafanya hivyo.
Luteni Jenerali Kipozi alivyowasili kikao kikaanza.
“Ndugu zanguni hali si hali. Bado tuna wakati mgumu,” Makamu wa Rais, Lilian Mkumba alifungua mjadala.
Wengine wakawa makini kusikiliza.
“Kama mjuavyo, bwana mkubwa hana dogo. Kwa nyapio nililolipata, anahitaji kuwaondoa duniani watu wetu anaowashikilia. Kwa namna ipi? Bado sijataarifiwa. Lakini huo ndiyo mkakati alionao kwa ajili ya kuzima matakwa yetu.”
“Mmmmh!” Koplo Namaya aliguna.
“Ni hatari kweli kweli.”
“Tena sana. Ni namna gani tutawaokoa? Ndicho cha msingi tunachopaswa kukijadili wakati huu, kabla hajaweka vihunzi vitakavyotugharimu.”
Luteni Jenerali Kipozi akatingisha kichwa huku amebana kingo za mdomo. Alionekana kutafakari jambo.
“Ina maana hawafikishi mahakamani?” Luteni Mwaipeta aliuliza.
“Sina hakika na hilo, kwa sababu mtoa taarifa wangu hajapata habari kamili.”
Ukapita ukimya mfupi.
“Mwokozi wetu katika hili anafahamika,” Luteni Jenerali Kipozi aliufukuza ule ukimya na kutulia kwa sekunde chache. Baadaye aliendelea, “Babigamba,” alisemana kutulia tena. Awamu hii ilikuwa muda mfupi zaidi ya mwanzo. Akaendelea, “Ni lazima Babigamba aingie madarakani ili tuweze kuwaokoa.”
“Na vipi kama hatofanya jinsi unavyofikiria?” Jenerali Namkumba aliuliza.
“Hana njia nyingine ya kufanya zaidi ya hii niliyoihisi. Atafanya hivyo, ili kujiweka salama mtaani.”
“Asipofanya?” Makamu wa Rais, Lilian Mkumba aliuliza.
“Tuna vijana. Watatimiliza tukitakacho, kabla hawajatimiliza matakwa yao.”
***
Kufahamika kwa Jackson kulileta jamba jamba kwenye kampuni ya habari aliyokuwa anafanyia kazi. Rais Sharabu alitoa amri, na ikatekelezwa kwa haraka sana. Yote, wafahamishe Jackson apatikanapo. Lakini haikuwa kwa urahisi. Waulizwa, hawakufungua kingo za midomo yao kuzungumza wapi Jackson anapatikana.
Ugumu ulivyozidi, Rais Sharabu alitoa amri kwa mara nyingine kupitia kwa Waziri mwenye dhamana. Waziri wa habari, sanaa na michezo kituo hicho kifungwe; na kikafungwa. Tena sio kwa muda maalumu.
“Tumechukua maamuzi haya, kwa sababu ni kituo kinachohalalisha uchochezi. Kina nia ya kuharibu amani ya nchi yetu, hivyo hatuwezi kukifumbia macho. Hata kama kina mkono wa kigogo nyuma,” ndiyo kauli aliyonena Waziri mwenye dhamana siku alipokifungia.
Hawakuishia hapo. Walienda mbali zaidi, kwa kumkamata Mkurugenzi wa kampuni na kumshinikiza awatajie Jackson alipo. Walipoona hamna dalili za mafanikio, walimtwisha kesi ya uhujumu uchumi.
Tukio hili lilienda sambamba na kina Kamishna Ndirimwe, DDGSS Mabele na Dc/cpl Amina. Walifunguliwa kesi ya uhaini.
“Siwahitaji hao watu warudi uraiani,” Rais Sharabu alitoa amri kwa Jaji Mkuu. Naye aliishusha chini kwa Jaji anayehusika na kesi.
Mamlaka ya kiti cha Rais. Hayana kupingwa!
Hivyo mashtaka yao yalipelekwa kwa haraka mno. Na kufanya ndani ya muda mfupi kuhukumiwa. Mkurugenzi wa Kampuni ya habari ya Fikra Huru alihukumiwa kifungo cha miaka nane na kulipa faini ya milioni mia tano. Wakati kina Kamishna Ndirimwe na wenzie walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Yakabaki masikitiko na manung’uniko mtaani, yaliyoongeza hasira za wanaharakati wenye uhitaji wa kumuondoa Rais Sharabu madarakani wafanye mipango yao kwa umakini na haraka.

ITAENDELEA...

HABARI NJEMA.

Kitabu cha riwaya ya #NENDA sasa inapatikana sehemu zifuatazo;

MOSHI
Renics Bookshop— 0767826134
Hassan Mboneche— 0673056571

MANGAKA & MTWARA
Aziz Mtando— 0787774977

Pia, kinatumwa kwenye mji wowote ambao haujaorodheshwa.
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 13.

Mamlaka ya kiti cha Rais. Hayana kupingwa!
Hivyo mashtaka yao yalipelekwa kwa haraka mno. Na kufanya ndani ya muda mfupi kuhukumiwa. Mkurugenzi wa Kampuni ya habari ya Fikra Huru alihukumiwa kifungo cha miaka nane na kulipa faini ya milioni mia tano. Wakati kina Kamishna Ndirimwe na wenzie walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Yakabaki masikitiko na manung’uniko mtaani, yaliyoongeza hasira za wanaharakati wenye uhitaji wa kumuondoa Rais Sharabu madarakani wafanye mipango yao kwa umakini na haraka.
***
DPP alikamilisha mwenendo wa mashtaka dhidi ya Ndalama kama alivyoamriwa. Akayawasilisha kwa Rais Sharabu. Yalikuwa zaidi ya mashtaka tisa, akayasaili; moja baada ya lingine, alivyohitimisha akawa mwingi wa tabasamu na cheko lililomuumiza mbavu.
“Hapa hawezi kuchomoka?” Rais Sharabu alimuuliza DPP, Mmala Makumbi.
“Kwa zaidi ya asilimia mia moja. Akiwa mbishi ataozea jela. Akihitaji uhuru lazima arudi kwako akunyenyekee.”
Wakaangua kicheko.
Hakikuwa cha muda mrefu. Cha muda mfupi tu, kisha Rais Sharabu alikifukuza, “Rudisha kwa wahusika. Na Jaji atakayesimamia kesi hii awe Ngoliga. Na afanye vile nitakavyoamuru.”
“Hilo halina shida. Mimi ni mtiifu kwako.”
“Naamini hivyo. Na utiifu wako kwangu ndiyo neemesho lako la leo na kesho.”
DPP Mmala alitekeleza agizo la Rais Sharabu kwa haraka mno. Faili la kesi lilirejeshwa polisi, halafu alifikisha lile hitajio la Jaji sehemu husika.
Jaji Ngoliga alipewa amri. Na kuitii kwa unyenyekevu uliochangamana na hofu. Hofu iliyomkosesha amani nafsini mwake. Atende kwa mujibu wa sheria? Au kwa mujibu wa Rais Sharabu?
Rais Sharabu aliingilia uhuru wa kila mahali.
***
Taarifa zilimfikia Luteni Jenerali Kipozi na timu yake kwa ujumla. Kile kilichoamriwa na Rais Sharabu. Chanzo cha habari, ni Whatsapp Status. Kuna askari, alipiga picha faili hilo na kutupia kwenye group kadhaa za Whatsapp. Wana-whatsapp wakajipakulia na kuweka status. Huko ndiko Luteni Jenerali Kipozi akajionea.
Alishtuka! Lakini baadaye alituliza mshtuko wake na kujiweka sawa, ili apate wasaa mzuri wa kufikiri. Nini hatma ya kitendo hicho endapo watakiacha kitokee?
Timu salia ikakutana kwa dharura; Luteni Jenerali Kipozi, Makamu wa Rais, Lilian Mkumba, Jenerali Namkumba, IGP Lukanga, Luteni Mwaipeta, Koplo Namaya na Konstebo Babaa.
“Hii ni hujuma nzito,” Makamu wa Rais, Lilian alifungua mjadala baada ya kila mmoja kusoma taarifa ya ile kesi.
“Zaidi,” Jenerali Namkumba alidakia.
IGP Lukanga naye hakuwa mbali kutoa dukuduku lake, “Endapo tutazembea, nikiwa na maana tuache kesi iendelee ni sawa na kuwaruhusu wale wote walioshawishiwa na Ndalama kumuunga mkono Rais Sharabu.”
Makamu wa Rais, Lilian akaingilia kati, “Kwa hiyo tunafanyaje?” akatulia kwa sekunde chache, kisha akaendelea, “Kipozi. Mbona kimya tunahitaji maoni yako katika hili.”
Luteni Jenerali Kipozi alijikohoza kidogo na kubadilisha mkao. “Nilikuwa nafikiria tufanye nini?”
“Enhee! Umepata? Kuna chochote ulichokipata ambacho unahisi kinaweza kuwa msaada kwetu?”
“Yeah!”
“Lipi?”
Wote wakatega masikio vyema. Na kumuangazia kwa mboni zilizojaa uchu wa ufahamu.
“Yampasa Ndalama akalambe miguu ya bwana mkubwa,” Luteni Jenerali Kipozi alisema na kutulia.
Makamu wa Rais, Lilian akadakia kwa mshtuko, “Hilo unazungumza kutoka moyoni?”
“Hakika. Kama mjuavyo, asili ya adui yetu ni ipi. Hiyo asili ndiyo udhaifu wake, tukihitaji kumshinda kwa haraka hatuna budi kuutumia huo udhaifu alionao.”
“Naomba utufafanulie,” Jenerali Namkumba aliongea.
“Hatuna budi katika hili. Ndalama akienda kulamba miguu yake itampunguzia hasira. Hasira zikipungua, kwa namna yoyote ile kesi atafutiwa.”
“Huoni kama tutapoteza wale tuliowashawishi? Na maelfu ya wananchi wanaomkubali Ndalama?”
“Tusiogope hilo. Mwishoni watatuelewa tu. Kwamba alifanya kile kitendo kwa sababu ya kitu fulani.”
“Huo ulambaji utachukua muda gani?”
“Hauna muda maalumu. Lakini utakuwa ulambaji uliovikwa barakoa mbele.”
“Unamaanisha nini?”
“Barakoa itamficha na yale yaliyopo moyoni.”
Ukapita ukimya mfupi, uliompeleka kila mmoja kwenye fikirio. Mwisho, waliafikiana na kile kilichoshauriwa na Luteni Jenerali Kipozi.
Akataarifiwa Ndalama kwa njia ya simu. Whatsapp video call.
***
Ndalama aliomba miadi ya kuonana na Rais Sharabu hata kabla kesi haijaanzwa kusikilizwa. Kitendo hiki kiliwashangaza wapendwa wake. Hawakuishia kumshangaa, walimchukia pia, na kumuona mchumia tumbo.
Wale aliowashawishi na kukubaliana na mpango wake wakabaki njia panda. Kulikoni? Walitegwa? Hawakuisha kujiuliza. Lakini maswali yote yalikosa majibu. Hawakuwa na jibu lililojitosheleza upande wao, kukata mzizi wa fitna, baadhi walimpigia simu Ndalama, huku wakiwa wenye hofu.
“Tunashindwa kukuelewa?”
“Sijabadilika. Nanyi endeleeni kusalia nilipowaweka.”
“Tutakuaminije? Wakati mwenzetu unaenda kuunga juhudi? Au ulikuwa unatuchora ili utuchomee kwa bwana mkubwa?”
“Hapana. Endeleeni kuniamini. Ni kitendo cha kusubiri muda tu uwadie. Hapo mutafahamu nini maana ya kitendo hiki nilichokifanya.”
Aliwaondolea hofu kwa namna hiyo.
Wapo waliomuelewa. Wengine hawakumuelewa. Wale wasioelewa wakaamua kujiengua. Uenguaji uliowagawanya njia mbili; baadhi walimuunga mkono Rais Sharabu, waliosalia walibaki neutral.
Siku ya miadi ilivyowadia Ndalama alialikwa Ikulu. Naye bila ajizi, alifunga safari kuelekea. Alivyowasili, alipokelewa kwa bashasha, kamera zikiwa hima hima kurekodi kila tukio. Kamera kutoka kwa waandishi wa habari wa Ikulu na wale wa Chama cha Chautu. Waandishi wa habari toka vyombo binafsi, hawakuruhusiwa kuingia ndani ya uzio uliozunguka jengo la Ikulu.
“Oooh! Karibu sana,” Rais Sharabu alimlaki Ndalama huku kakenua kwa tabasamu-meno yote nje.
“Nimeshakaribia mheshimiwa Rais. Mkuu wa hili taifa.” Ndalama akatabasamu. Rais Sharabu pia.
Wakaingia ofisini tayari kwa mazungumzo.
Wakiwa huko Ndalama aliteta yaliyomshinikiza kumpeleka. Awali, alimuomba radhi Rais Sharabu na kumtaka amuondolee vizingiti amuwekeavyo.
“Nakuahidi, nitakuwa mtiifu kwako. Nitaachana na ujinga ujinga niliokuwa nauendekeza. Nipo tayari kuungana nawe kuendeleza gurudumu la taifa letu.”
Rais Sharabu akamtupia swali kwa udadisi, “Una uhakika na uyazungumzayo? Yanatoka moyoni kweli?”
“Mimi ni mtu mzima. Nimefahamu, kuwa ni tamaa tu ndizo zilizokuwa zinaniendesha.”
“Kwa hiyo tamaa zimeshaisha?”
“Tena pasi na kubaki chembe ya aina yoyote. Nipo tayari kuwa mtumwa wako.”
Rais Sharabu akaangusha cheko la dhihaka. Ilhali Ndalama akitabasamu. Tabasamu bandia.
Rais Sharabu alitingisha kichwa, akafuatia kutokwa na kauli, “Nimekuelewa. Nikupongeze kwa kulielewa hilo. Una lingine?”
Ndalama hakujibu kwa uharaka. Alivuta subira kwa sekunde chache ndipo alijibu, “Kuhusu kesi.”
Wakaangua kicheko. Huku wakipiganishana mikono.
Baada ya saa moja maongezi yalihitimika. Yalihitimika kwa kufikia muafaka, ambao uliwekwa wazi mbele ya waandishi wa habari. Lakini si yote, ni baadhi tu. Yale yaliyohitaji usiri kamwe hayakuzungumzwa. Hasa lile la kusamehewa mashtaka yake.
Ndalama alijihalalishia apigwe mawe zaidi.
Ndicho kilichojiri. Kitendo cha kusema anamuunga mkono Rais Sharabu kiliwapa chukizo wale waliokuwa nyuma yake. Hivyo walimshambulia kwa matusi na kila aina ya kejeli.
Uzuri. Kile alichohitaji alikifanikisha. Shitaka lilifungwa pasi na kupelekwa kesi mahakamani.
“Tumefuta moja ya hatua iliyokuwa inatutatiza,” Makamu wa Rais, Lilian alifungua mjadala walivyokutana jioni moja.
“Ni jambo la kujipongeza. Lakini sio kwa uridhisho. Kwani lililosalia ndilo ngumu zaidi ya yote,” Luteni Jenerali Kipozi alitoa maoni yake.
Siku hii, walionekana kuwa makini katika kujadiliana.
“Hatupaswi kukata tamaa. Tuzidi kupambana mpaka tone la mwisho. Kuhakikisha uhuru unarudi kwa wahitajika.”
Rais Sharabu alijipiga pasi na kufahamu. Walichohitajika, ni kukazia pigo. Mpigwa, asitetereke na kupata mwanya wa kujitetea.

ITAENDELEA...
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 14.

Taifa lilizizima.
Kila kona ilienea habari moja tu, kuanza kwa mchakato wa kuwatafuta wawakilishi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu. Sio chama tawala, wala chama cha upinzani, Maendeleo Tuleane (MATU) ambacho kilikaa pasi na kushughulikia jambo hili. Lengo, wapate wagombea makini wanaokubalika kwa wananchi.
Kwa upande wa Matu, walikuwa na watu wawili tu wenye nguvu. Na ndiyo ambao waliingia kwenye kinyang’anyiro; Prof. Geugeu Makashata, mwanachama aliyejiunga na chama hicho siku chache zilizopita akitokea chama tawala. Mwingine ni Mwenyekiti wa chama, Masabi Wakwetu-lakini mwenyekiti ndiyo alikuwa na uhakika zaidi wa kupita. Masabi!
“Kuna mazingira yoyote yaliandaliwa kuhusu watu wa upinzani?” Makamu wa Rais, Lilian alimtupia swali Luteni Jenerali Kipozi.
“Nina hakika hilo lipo.”
“Ina maana nawe hauna uhakika?” Jenerali Namkumba alikazia.
“Kamishna...” Luteni Jenerali Kipozi alijibu. Lakini kabla hajamaliza alikatishwa na muito wa simu.
Alitoa alipoihifadhi na kupokea.
Wote wakawa kimya kumsikiliza anenacho.
“Hallo!” Luteni Jenerali Kipozi aliita mara baada ya kuipokea ile simu.
“Masabi naongea.”
“Ndiyo.” Akatoa simu sikioni na kuipazisha sauti. Kila mmoja apate kusikia atakachozungumza Masabi.
“Nina ujumbe kutoka kwa Kamishna Ndirimwe.”
Wote wakasogea jirani na Luteni Jenerali Kipozi.
“Endelea.”
“Naweza kuonana nawe?”
Luteni Jenerali Kipozi akasita kwa muda. Akaangalia nyuso za kila mmoja ndipo akafuatia kujibu, “Yeah!”
“Basi nipe uelekeo.”
Nusu saa baadaye Masabi alijumuika na timu ya kina Luteni Jenerali Kipozi.
“Ni jambo la kushangaza,” Masabi alisema baada ya salamu.
“Yeah! Na haupaswi kuondoka na mshangao. Inabidi uuache hapa hapa.”
Wakaangua kicheko.
“Twende kwenye hoja,” Jenerali Namkumba aliamuru.
“Nina ujumbe kutoka kwa Kamishna Ndirimwe.”
“Usisite, uweke wazi.”
“Aliniambia nikuone wakati chama chetu kikielekea kwenye mchakato wa uchaguzi.”
Wakahamaki.
Na kuwafanya wenye tafakuri kwa muda.
“Vipi?” Masabi aliuliza.
“Kamishna Ndirimwe hakunipatia ujumbe wowote kuhusu wewe.”
“Kwa hiyo niondoke?”
“Hapana.”
“Sasa nitabaki kufanya nini?”
“Naamini kuna sehemu yako. Keti nasi tujadiliane tuone namna gani tunafikia muafaka.”
“Kama hatutofikia?”
“Itakuwa ishu nyingine. Ambayo kwa upande wetu hatutokuwa tayari kuiona inatoka nje. Lakini nina hakika haitofikia huko.”
“Una maanisha nini?”
“Chukua nafasi tuzungumze.”
Wakaketi pamoja kwa majadiliano zaidi.
***
Upande wa Chautu walikesha kwa vifijo na nderemo kuwa Rais Sharabu ndiye pekee anayeenda kuchukua fomu na kupeperusha bendera ya chama. Hakuna aliyehisi, kama kuna mwingine atakayejitokeza. Hasa kwa imani ya siku zote, mgombea anayefanikiwa kuongoza muhula wa kwanza, ndiye huyo huyo atakayechaguliwa kwa muhula ujao.
Hivyo milango ilivyofunguliwa Rais Sharabu alijitokeza mapema tu kuchukua fomu. Tena hakuacha zake mbwembwe, na mikogo ya kujiona yupo sahihi muda wote. Ile ya kucheza cheza na kujipitisha pitisha kwa watu wa daraja la chini wamuone naye ni mtu wa aina kama yao.
Alivyokamilisha taratibu aliirejesha, kisha akatega macho na masikio kutazamia nani atasema mbovu juu yake. Sambamba na atakayeleta kiherehere cha kuwania nafasi hiyo.
***
Baada ya maongezi ya muda mrefu, Masabi aliafikiana na kina Luteni Jenerali Kipozi. Awe kivuli cha mipango yao. Agombee, lakini asiweke nia ya dhati.
“Kwa maana hiyo nitakosa uwakilishi kwa wananchi?” Masabi aliuliza.
“Sahihi. Lakini tutakutengenezea mazingira ya kuhakikisha hii nia baada ya awamu ijayo inatimia.”
“Ina maana mtanisaidia kuwa Rais?”
“Pasi na shaka. Kwani tunaamini, tukimweka huyu tumtakaye atamaliza kila hitajio tunalolitaka.”
“Oooh! Natamani ningeliifahamu mipango yenu mapema.”
“Ni makini. Na yenye kuleta nuru kwa wote.”
“Lakini...”
Luteni Jenerali Kipozi akadakia, “Tutakupoza kiasi katika hili. Na kukupa uhakika wa utekelezaji wa nia yako. Tuache tumweke msafisha njia, ukishaingia madarakani userereke tu.”
Wakaangua kicheko.
“Ewe ni Rais ajaye. Tuamini.”
Maongezi yalivyohitimika waliondoka. Waliondoka, kila mmoja akiwa na deni nafsini mwake, ya kuhakikisha mipango haiyumbi.
***
Ilikuwa jumatatu usiku wa saa tano, Babigamba alivyowasili nchini akitokea Marekani. Akapokelewa na Luteni Jenerali Kipozi kisha waliongozana kuelekea kwenye jengo lao la maficho.
“Hatuna haja ya kupoteza muda. Pumzisha mwili, ukishajiona uko fit, ingia kati uanze mapambano,” Luteni Jenerali Kipozi aliongea.
“Mambo yatakaa sawa? Maana nina hakika bwana mkubwa macho yake yote yapo huko.”
“Nakuhakikishia, ni lazima uchukue fomu. Na utakuwa Rais wa nchi yetu kupitia uchaguzi ujao.”
“Ninachohitaji ni ulinzi wangu. Pasi na kusahau familia.”
“Katika hili hawezi kukugusa kwa ubaya. Huko alipo amejawa na imani, akifanya hivyo ataharibu picha yake kwa wananchi. Hivyo inabidi tutumie hapo kuzidi kumpiga.”
Siku iliyofuata Ndalama aliwakumbusha watu wake aliowashawishi wajiandae, tayari kwa mpango. Baadhi walishikwa na sintofahamu. Hawakuamini amini.
“Hueleweki?”
“Ndiyo maana awali niliwaambia muniamini. Huu ndiyo muda sahihi wa kuanza kumwangusha Sharabu.”
“Kwa namna ipi?”
“Yatupasa tuende na mpinzani atakayejitokeza ndani ya chama.”
“Mbona unatuletea ndoto za alinacha? Nani atajitokeza kushindana na Sharabu?”
“Vuteni subira. Hiyo siku yaja.”
Muda wa kuchukua fomu ulivyokaribia kufikia hitimisho, ndipo Babigamba alijitokeza kwenda kuchukua fomu za kuwania kinyang’anyiro cha kupeperusha chama katika kiti cha urais. Mtoa fomu, Katibu Mkuu, alishikwa na kigugumizi. Aliiwazua ile taarifa mara mbili mbili pasi na kupata jibu.
“Mzee! Ni nini unataka kufanya? Utaratibu wa chama si unaufahamu?” Katibu Mkuu wa chama cha Chautu aliuliza. Wakati huo bado akiwa na fukuto nafsini mwake. Imekuaje Babigamba kaamua kufanya hivyo.
Babigamba akajibu kishujaa, “Nafuata katiba ya chama, na sio utaratibu wa kiholela.”
“Bhana! Upo timamu kweli? Unataka kufanya nini? Muache Sharabu amalizie muhula uliosalia.”
“Wewe huna mamlaka ya kunizuia, nipe fomu, mkutano mkuu ukaamue kama nafaa au sifai.”
“Siwezi kukupa fomu,” Katibu Mkuu aliongea huku kijasho cha woga kikimtiririka. Akanyanyuka alipoketi na kupiga hatua zilizokosa uelekeo mule ofisini. Alienda na kurudi zaidi ya mara sita. Vidole viwili vya mkono wa kuume kakamata kidevu.
Pindi Babigamba na Katibu Mkuu wanazidi kulumbana Jackson alitumia nafasi yake kurahisisha kazi kwa Babigamba. Aliachia taatifa mtandaoni. Kwa njia ya picha mnato na jongefu. Taarifa ilisema ‘Babigamba, kuchuana vikali na Rais Sharabu katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kuwakilisha chama kwenye nafasi ya urais.’
Moja ya picha; ile ya mnato, ilimuonesha pindi akiteremka ndani ya gari. Wakati picha jongefu ilimuonesha akiingia ndani ya jengo la chama, hadi ndani ya ofisi ya Katibu Mkuu. Ikajenga shangwe kwa wapinzani wa Rais Sharabu kiitikadi.
Rais Sharabu alivyofikwa na taarifa alikasirika. Hasira zilizomshinikiza atengeneze kisasi cha nguvu dhidi ya Babigamba.
“Sheenz! Yaani mimi nilikuwa nakulea lea kumbe mwenzangu...” Rais Sharabu alijisemeza huku akiiangalia ile picha jongefu imuonyeshayo Babigamba.
Baada ya kuiangalia kwa muda mrefu na hasira kupoa kwa kiasi, alimpigia simu Katibu Mkuu.
“Mpe akitakacho,” Rais Sharabu alisema, mara baada ya simu kupokelewa. Akakata simu. Kabla ya mtu wa upande wa pili kujibu.
Akampigia mtu mwingine. Killa.
“Nahitaji Babigamba ashughulikiwe haraka iwezekanavyo. Familia yake isisahaulike. Ili udhibiti uwe na nguvu.”
Kupitia amri ya Rais Sharabu Babigamba alikabidhiwa fomu na kuondoka ofisini. Nje, akakuta tuksi la waandishi wa habari waliokuwa wanamsubiri kwa hamu. Wakamvaa kwa maswali.
“Kulikoni Makamu?”
“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, imekuaje uchukue fomu ya kuwania kuwakilisha chama katika kinyang’anyiro cha urais wakati utaratibu wenu ni...”
Waandishi wa habari waliuliza maswali hayo huku wakipiga hatua za kasi kuendana na mwendo wa Babigamba. Ambaye alionekana kupotezea nia ya wanahabari. Alivyoifikia gari yake alisimama na kujibu yale maswali.
“Tulieni. Haina haja ya kuwa na jazba, kwa sababu nilichofanya ni kitu cha kawaida sana. Nimetimiza matakwa ya katiba ya chama.”
“Lakini haijazoeleka ndani ya chama chenu kuwa na tukio la namna hii?” mmoja wa waandishi alimtupia swali.
“Nimevunja mwiko ambao watu wengi walikuwa wanauogopa kuuvunja. Vile vile, huu ni wakati sahihi wa hiki nilichokifanya kwa hali ya taifa letu ilipofikia. Hivyo niwaombe wanachama wenzangu wanipokee kwa mikono yote.” Akaingia ndani ya gari na kuondoka.
Mtaani kukapasuka.
Kila mmoja alipokea kwa namna yake hili tukio. Wapo waliombeza na kumpongeza. Lakini mwenyewe aliziba masikio asisikie lolote kutoka kwao. Alichojalisha ni kile kilichopo kwenye mkakati wa kufanikisha azma yao.

ITAENDELEA...

HABARI NJEMA

KITABU CHA RIWAYA YA #NENDA KINAPATIKANA RENICS BOOKSHOP TAWI LA MOSHI KWA GHARAMA YA TSH. 10,000/= WASILIANA KWA 0767826134 KUJIPATIA NAKALA YAKO.
received_2945314115533687.jpg
 
RIWAYA: MKOLONI MZAWA—2
MTUNZI: HASSAN MBONECHE
SEHEMU YA 15.

Waandishi wa habari waliuliza maswali hayo huku wakipiga hatua za kasi kuendana na mwendo wa Babigamba. Ambaye alionekana kupotezea nia ya wanahabari. Alivyoifikia gari yake alisimama na kujibu yale maswali.
“Tulieni. Haina haja ya kuwa na jazba, kwa sababu nilichofanya ni kitu cha kawaida sana. Nimetimiza matakwa ya katiba ya chama.”
“Lakini haijazoeleka ndani ya chama chenu kuwa na tukio la namna hii?” mmoja wa waandishi alimtupia swali.
“Nimevunja mwiko ambao watu wengi walikuwa wanauogopa kuuvunja. Vile vile, huu ni wakati sahihi wa hiki nilichokifanya kwa hali ya taifa letu ilipofikia. Hivyo niwaombe wanachama wenzangu wanipokee kwa mikono yote.” Akaingia ndani ya gari na kuondoka.
Mtaani kukapasuka.
Kila mmoja alipokea kwa namna yake hili tukio. Wapo waliombeza na kumpongeza. Lakini mwenyewe aliziba masikio asisikie lolote kutoka kwao. Alichojalisha ni kile kilichopo kwenye mkakati wa kufanikisha azma yao.
***
Kinyonga na wenzake; Mauten na Shida ndiyo waliopatiwa kazi ya kumdhibiti Babigamba. Hivyo walijigawa; wawili, walifuatilia mwenendo wa Babigamba, mwingine, alienda nyumbani kwa Babigamba. Lengo, yule aliyeenda nyumbani akaiteke familia. Ambayo ni mke na mtoto mmoja akadiriaye miaka kumi na mbili. Mtoto wa kike.
Shida ndiyo alikuwa na jukumu hilo. La kwenda nyumbani.
Upande wa pili.
Luteni Mwaipeta, Koplo Namaya na Konstebo Babaa nao walikuwa katika nyendo za kumpatia ulinzi. Lakini hawakutaka kujionyesha, wala Babigamba hakufahamu, kama kuna watu waliopo kwa ajili ya ulinzi wake. Walipiga hatua za mbali naye, mboni zikiwa kwake muda wote.
Mwendo aliotoka nao Babigamba pale ofisini haukuwa wa kasi. Aliendesha gari taratibu, huku akiunda picha namna atakavyokalia kiti cha urais. Alivyofika umbali wa kilomita kadhaa zile fikra zilibadilika na kujengeka fikra zenye wasiwasi. Alianza kuingiwa wasiwasi, kiasi cha kumshinikiza muda mrefu asaili nyuma na pembezoni kwake kuna nini kiendeleacho.
Alihisi ujio wa jambo baya.
“Mbona najiona sipo sawa? Au kuna kitu nimekisahau?” alijiuliza, pindi akiegesha gari kwenye moja ya chochoro ili ajipe muda wa kutafakari vizuri zile hisia.
Alivyoliweka sawa, alizima. Alivuta pumzi na kuzitua kwa nguvu, kisha alipangusa uso.
Baadaye alitoa ile fomu sehemu aliyoihifadhi na kuanza kuichunguza. Ilimchukua takribani dakika mbili, alivyoridhika aliirejesha kisha aliinua rununu kutoka kwenye dashibodi, akampigia Luteni Jenerali Kipozi.
“Ndiyo ndugu,” Luteni Jenerali Kipozi alisema mara baada ya kupokea simu.
“Najiona sipo sawa.”
“Ki-vipi? Fomu si unayo?”
“Ndiyo. Lakini najishangaa kujiona ni mwenye wasiwasi mwingi.”
“Ondoa hofu. Hakuna mtu atakayekudhuru.”
Babigamba alikata simu na kuirejesha kwenye dashibodi. Akajipa wasaa wa kutafakari kwa mara nyingine. Majibu ya Luteni Jenerali Kipozi hayakuondoa wasiwasi alionao.
Wasiwasi ulivyompungua aliungurumisha gari aianze safari. Kabla hajaitoa pale alipoegesha, aligongewa na mtu upande mmoja wa mlango. Alikuwa Kinyonga. Aliteremsha kioo, apate kumsikiliza.
Uzuri naye hakuwa kijinga. Kwani kabla hajaanza harakati za kisiasa alishawahi kupitia mafunzo ya kijeshi, na kuhudumu kwa muda wa miaka kumi na tano. Aliacha jeshi akiwa na cheo cha Kanali. Ndipo akajikita kwenye siasa. Baada ya kuteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilioni.
Aliamriwa kuteremka. Mdomo wa bastola iliyokamatwa na Kinyonga ukiwa karibu na wajihi wake. Upande wa pili alisimama Mauten, muda wote kamuangazia kwa uono mkali kuona kama atajitikisa kwa lolote. Na sehemu ya ulinzi pia kwa upande wao.
Pasi na ubishi aliteremka. Mikono kaiinua juu, akapiga hatua taratibu kufuata maelekezo aliyokuwa anapatiwa kulingana na mtutu wa bastola unavyoelekezwa.
“Simama hapo,” Kinyonga alimuamuru. Akiwa amepiga umbali takribani mita moja toka aliposimama Kinyonga na gari lake lilipo.
Baadaye Kinyonga alitoa ishara fulani kwa Mauten. Alitikisa kichwa, mtingisho mmoja, ulioashiria aingie ndani ya gari. Mauten alitekeleza hilo agizo kwa haraka. Aliingia, na kuanza kupekua kila mahali alipoona pana uhusika wa uhifadhi wa kitu. Hakutumia muda mrefu, alitoka akiwa amekamatia bahasha iliyo na ile fomu.
“Hili ni kama onyo. Na ukumbusho wa mipaka yako ni ipi,” Kinyonga alimzodoa Babigamba. Wakati huo Babigamba kapeleka fikra zake mbali na eneo hilo. Taswira ya Rais Sharabu ilimtamalaki, kiasi kwamba alianza kuchipukwa na uchungu.
Mauten akamfuata Babigamba pale aliposimama. Alimteremsha ile mikono na kumshika kwa nyuma. Akamuongoza kuingia kwenye gari yao.
“Kuna mamlaka huwa hayaingiliwi, mbwa wewe,” Mauten alisema. Kauli iliyofuatwa na kipigo. Alimpiga Babigamba kwenye makalio na goti.
Haraka sana Kinyonga alizungukia upande wa usukani. Mauten alifungua mlango wa mbele na kumuingiza Babigamba taratibu aketi kitini. Wakati anamuingiza alimtanguliza kichwa, miguu ilisalia nje, Babigamba akatumia nafasi hiyo vyema. Aliamini inaweza kumuokoa kutoka mikononi mwa hao mabaradhuli.
Kwa kasi ya ajabu, alifyatua moja ya mguu akampiga Mauten kwenye mamlaka ya jinsia. Mauten aligugumia kwa maumivu na kumuachia. Kitendo kilichompatia Babigamba nafasi nzuri ya kujitetea. Kwani alifurumusha ngumi mbili za chap chap usoni kwa Kinyonga ambaye hakuwa na mkao mzuri mara baada ya kuingia garini. Alikaa kwa kujiachia.
Kule alipopepesukia Mauten alipandwa na hasira. Hivyo maumivu yalivyopungua, alichomoa bastola aliyokuwa ameisundika kiunoni akanyoosha kumlenga Babigamba. Pindi, anaelekeza kidole cha shahada kwenye trigger akavamiwa kwa kumbo lililomdondosha chini pamoja na mkumbaji. Alikuwa Luteni Mwaipeta.
Luteni Mwaipeta ndiyo alikuwa wa kwanza kujiinua. Akapiga hatua kadhaa hadi pale alipoangukia Mauten, naye alimuinua. Wakati huo kakamatia ukosi wa shati alilovaa Mauten. Wajihi, umebuka vumbi, na kingo za mdomo zimepasuka kiasi cha kumtiririsha damu.
Mauten alilegea. Kama bamia changa iivapo jikoni.
“Nani kawapa mamlaka ya kuingilia uhuru wa kila mmoja ndani ya taifa hili?” Luteni Mwaipeta aliuliza na kumalizia pigo la kichwa kichwani kwa Mauten.
Mauten alijishika pale alipopigwa, huku kafura kwa hasira. Alivyotoa mkono na kuusaili aliona damu. Akabaini sehemu aliyopigwa pamechanika. Hasira ikamzidi maradufu. Akajitutumua na kurusha kwa nguvu mikono yake kuelekea kifuani kwa Luteni Mwaipeta. Luteni Mwaipeta alihepa pembeni hatua chache. Kabla hajasimama vizuri alimpiga ngwara Mauten lililomdondosha chini na kumkita tumboni kwa ule mguu aliotumia kumpigia.
Mauten aligugumia kwa maumivu huku akijaribu kuuondoa ule mguu.
Kwa upande wa Kinyonga mara baada ya kupigwa zile ngumi alitoka nje kwa haraka na kuchomoa bastola, ambayo alishaihifadhi kwenye holster aliyoifunga pajani. Alivyoikamata vyema alipeleka mashambulizi kadhaa kwa Babigamba lakini hayakumfikia. Kwani Babigamba alivyotambua adui yake anataka kufanya nini, alirudi nyuma haraka na ku-dashdown. Baadaye alijiviringisha mara kadhaa akielekea nyuma ya lile gari. Alivyohisi kizunguzungu, alitulia na kumpimia Kinyonga kupitia uvungu wa gari. Noah. Aliiona miguu yake ikielekea kule kule alikokimbilia.
“Oooh! Yarabi,” Babigamba alijisemeza. Hofu ya kuuwawa ikimtukuta. Kutokana na ile bastola.
Baada ya sekunde kadhaa alihisi kuna kitu kinamnyemelea. Akafahamu ndiye Kinyonga. Alivyojaribu kuangaza usawa wa mita kadhaa toka alipolala aliona kivuli kikinyata. Wazo la haraka lililomjia aingie uvunguni mwa gari. Lakini alilipuuzia, punde alivyopata wazo lingine, huko kunaweza kuwa sehemu itakayohalalisha kifo kwa urahisi. Ikambidi ajiinue, na kutembea mwendo wa kibata bata hadi mwisho wa gari, kabla hajaifikia sehemu ya nyuma.
Akatulia, tuli, akiwa amebana pumzi na kukifuatilia kile kivuli kinavyojongea.
Katika hali isiyotarajiwa, unyapio wa Kinyonga ulisitishwa ghafla na kitu kilichopita mbele yake kwa kasi na kuingia garini. Alivyotupa macho sehemu ya kupitia aliona pamepasuka. Akarudi nyuma kwa haraka na kujibanza pembozoni mwa gari na kuangalia upande uliotokea kile kitu. Alitazamana na mtu wa bunduki. Koplo Namaya alikuwa mita chache toka walipo, kaiketisha bunduki yake vyema kwenye nyama ya bega.
Kinyonga akasalimu amri. Aliitupa chini ile bastola na kunyoosha mikono juu.
Kuona hivyo Koplo Namaya alipiga hatua taratibu kumfuata alipo, Babigamba naye aliinuka na kwenda kuiokota fomu ambayo ilidondoshwa chini. Aliikung’uta vumbi na kuisaili kama ipo shwari. Alipojihakikishia, alimfuata Kinyonga. Luteni Mwaipeta pia, alimuinua Mauten, na kumburuza buruza hadi pale kwa Kinyonga. Akamwangusha. Wakati huo, Kinyonga kapiga magoti.
Kitendo cha Mauten kuangushwa pale chini kilipelekea Kinyonga aguswe na kuyumbishwa. Myumbo ulioelekea kule alipoidondosha bastola. Hakuwa mjinga, aliiokota na kukoki kwa haraka kisha alipeleka mashambulizi waliposimama Babigamba na Luteni Mwaipeta. Kwa kasi ya ajabu, walilala chini na kuviringika.
“Dogo amka tuondoke, pameshaharibika hapa,” Kinyonga alimnong’oneza Mauten, aliyekuwa chini akiugulia maumivu ya tumbo. Wakati huo Kinyonga kaelekezea mtutu wa bunduki walipo Kina Luteni Mwaipeta na Babigamba, mboni zake kamuelekezea Koplo Namaya. Ilikuwa ishara yenye kutoa kauli, ukitushambulia, nawashambulia wenzako.
Mauten alijiinua kwa shida. Alivyosimama wima, alipiga hatua taratibu, Kinyonga akiwa nyuma yake. Yeye ndiye alitangulia kuelekea garini, Kinyonga akawa nyuma kwa ajili ya kumkinga. Walivyolifikia gari waliingia na kuondoka kwa kasi eneo hilo.
Babigamba na wenzie wala hawakuhangaika nao. Waliingia kwenye magari na kuondoka. Mwisho wa safari ulikuwa nyumbani kwa Babigamba. Waliteremka garini na kuongoza ndani. Mazingira waliyokutana nayo yakawapa mashaka. Yalikuwa tafrani, kiasi kwamba yalitoa picha kwa urahisi kumfahamisha mtu hapo kulikuwa na mapambano.
Wakazidisha mwendo huku Babigamba akiita jina la mkewe na mwanaye.
Hadi wanaingia ndani, sebuleni, hakuna mtu aliyejitokeza katika hao walioitwa. Hali iliyozidi kuwapatia mashaka na hofu nafsini mwao. Baadaye ikabidi kila mmoja azunguke huku na kule lakini hakukuwa na muitikio wa aina yoyote.
Wakakutana tena pale sebuleni. Wakati huo Babigamba katawaliwa na jasho jepesi, mdomo umemjaa mate, na nguvu nazo zikimtoka. Alitamani kulia. Lakini, aliishia kutokwa na machozi yaliyochangamana na jasho.
Kwa ujumla wote walinyong’onyea. Akili zilifubaa, kiasi cha kushindwa kutambua wafanye jambo gani. Wakajitupia sofani wapate kupumzika. Na kuipa nafasi akili iwazue.
Kama walielekezwa kwa pamoja. Kitendo cha kuketi tu, waliiona karatasi chini ya meza iliyo na maandishi machache. Wakainuka kwa pamoja kutaka kuichukua, Konstebo Babaa ndiye aliiwahi.
Wakarejea kuketi.
Konstebo Babaa alianza kuiisaili kwa muda. Alisoma kilichoandikwa ki-moyomoyo, kisha alimpatia Babigamba, ambaye naye alifanya vivyo hivyo. Alipomaliza, aliitua juu ya meza wengine wajisomee.
Ujumbe ulisomeka, “Tutafute kwa hizi namba +25693 097 151 uipate familia yako.”
Hakuna aliyejawa nobe! Tabasamu, wote walipoa. Ujumbe uliwachoma na kuwaumiza. Babigamba ndiyo kuzidi. Maumivu yalimpooza, kuku mwenye kideri ana unafuu.

ITAENDELEA...

HABARI NJEMA.

KITABU CHA RIWAYA YA #NENDA SASA KINAPATIKANA #RENICS_BOOKSHOP TAWI LA #MOSHI KWA GHARAMA YA TSH. 10,000/= MAWASILIANO: 0767826134
AU, JISOMEE KWA GHARAMA NAFUU KATIKA #SimuliziAfrica_App.
received_2945314115533687.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom