RIWAYA: CHOKORAA
MTUNZI: George Iron Mosenya
SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO
Kichwa kilikuwa kinamuuma sana Kasuku. Kifo cha mpenzi wake na mkewe mtarajiwa kilikuwa kimemchanganya sana.
Gari lilikutwa limeegeshwa katika hoteli, mwili wa marehemu ukakutwa katika mtaro mkubwa ukiwa na mpini wa kisu uliozama ipasavyo katika mgongo wake.
Kifo hiki sio kwamba kiliishia kumsisimua na kumuumiza Kasuku lakini kilimtia wazimu kabisa.
Alijiuliza maswali mengi. Hakupata jawabu.
Huzuni!! Huzuni ikawa rafiki yake.
Akachukua likizo isiyokuwa na malipo aweze kuipumzisha akili yake.
KASUKU alizoea kufuatilia matukio ya hapa na pale yasiyomuhusu, haya yalikuwa mepesi na alikuwa anafurahia kuyafuatilia kisha kuyaandika.
Matukio aliyokuwa anayafuatilia na kuyaandika yalikuwa makubwa sana. Tena ya kushangaza. Cha kushangaza tukio hili la kifo cha mkewe hakujua ni wapi ataanzia.
Gari limekutwa barabarani, mwili umekutwa mtaloni.
Ataanzia wapi kupeleleza.
Alama za vidole zilizokutwa katika mwili wa marehemu zilikuwa za mwanamke.
Usukani haukukutwa na alama zozote zile. Hii inamaanisha muuaji alikuwa makini sana na kazi yake. Hakukubali kuacha ushahidi kirahisi.
Hapa kila aliyeufuatilia mlolongo huu alichanganyikiwa na kupoteza tumaini la kumpata muuaji.
Kasuku alikumbwa na fedheha kubwa sana. Simu kutoka katika ukoo wa mwanamke kila siku kumuuliza ni wapi amefikia zilimkwaza sana lakini hakuwa na jeuri ya kukataa kupokea simu yao wala kujibu maswali yoyote watakayouliza.
Ilikuwa bahati kuwa alikuwa amejaaliwa mwili mwembamba. Hata alivyopungua haikushangaza sana tofauti kama angekuwa na mwili mkubwa.
Mwenzake aliyekuwa na mwili mkubwa alikongoroka kwa kasi kubwa sana. Kitambi kikaanza kufutika. Mali alizokuwanazo zikakosa maana. Akawa mkali katika familia yake, kila mara anamgombeza mkewe, mara apige watoto wake.
Alikuwa kama amechanganyikiwa.
Siri kubwa ilikuwa inamtesa. Atamshirikisha nani? Hakuwepo wa kumshirikisha.
Habari za upelelezi unaendelea zilikuwa zinamchanganya mzee Dembele. Kila alipozisikia jitihada hizi zinaendelea aliona namna anavyokaribia kuumbuka.
Mbaya zaidi hakuwa anafahamu ni wapi Frida na Mwanaidi pamoja na yule mama mwendawazimu ni wapi walikimbilia.
Akili ilikuwa imechoka kujiuliza ilikuwaje mkewe Kasuku akakutwa amekufa katika nyumba yake ya siri.
Alizihitaji roho zao ili kujiweka mahali salama. Ni roho hizi pekee ambazo zingetoa jawabu kwake.
Uhuru wake ulikuwa matatani. Na laiti kama ingefahamika kuwa alikuwa anajihusisha na na uuzaji wa madawa ya kulevya kwa njia ya kutoa misaada kwa yatima maisha yake yangemalizikia katika kitanzi.
Alikuwa muuaji!!
Siku zilizidi kukatika bila bwana Dembele kugusiwa lolote juu ya kuhusika kwake katika katika kifo cha mke wa Kasuku.
Wasiwasi wake haukupungua kamwe. Aliamini bado alikuwa katika wakati mgumu sana.
Hakuwa na la kufanya akaungoja wakati uzungumze!!
****
Mwanaidi hakuwa na mamilioni ya pesa kuweza kuwahifadhi watu hawa wawili. Mama George na Frida. Lakini alijitahidi kadri ya uwezo wake kuwahifadhi wawili hawa kwa kidogo alichokuwa nacho.
Pesa aliyoipata kwa kumwibia marehemu mkuu wa kituo cha watoto yatima isingeweza kudumu kamwe. Hasahasa ikiwa inatumika pasi kujizungusha. Mwanaidi aliamini kuwa akifikia uamuzi wa kumpeleka mama hospitali basi pesa itaishia hapohapo.
Baada ya siku takribani tano za mapumziko katika chumba alichokuwa amepanga Mwanaidi sasa likaibuka wazo la kutazama nini cha kufanya ili maisha yaweze kuendelea.
Mwanaidi hakutaka kurejea tena katika maisha ya uchokoraa.
Kwanza kwanini arejee?? Wakati sasa anaye mama anayemwona kama mzazi kwake?
Hapakuwa na haja ya kujiita yatima tena.
Alikuwa na dada aliyeitwa Frida na bado mwingine anayeitwa Isha na kaka anayeitwa George. Hapa alipungua mzazi wa kiume pekee kuweza kuikamilisha familia hii ya maajabu.
Mwanaidi alipofikiria na kujitoa katika uyatima akagundua kuwa amefanya ubinafsi wa hali ya juu sana. Kummiliki yule mama ilhali kuna yatima wengi mtaani.
Atakuwa mama wa wasiokuwa na mama mtaani!! Alipitisha kauli hiyo katika ubongo wake.
Kila neno lahitaji kitendo liweze kuonekana.
Mwanaidi akafikiria cha kufanya ili neno lake liweze kuishi katika matendo.
Frida na yule mama walikuwa wamelala bado.
Akawatazama kwa jicho la huruma.
Moyo wake ukakiri kuwa alikuwa anawapenda sana!!
Mwanaidi alingoja baada ya siku tatu. Sasa akawa amefikiria nini cha kufanya.
Katika hili alihitaji sana kumpata mtu mwenye taaluma kidogo anayeweza kuzungumza na msomi.
Atampata wapi? Alijiuliza. Mara akapata wazo.
"Frida!!" aliita.
"Sema kamanda." Alijibu kwa utani huku akiwa analamba kipande chake cha limao kukata kichefuchefu cha mimba.
"Ulisema kuwa unapafahamu nyumbani kwa George."
Frida akatikisa kichwa juu na chini kuashiria kukubali.
Mwanaidi akaelezea nia yake ya kutaka kuonana na George.
Frida aliposikia jina George na mpango wa kuonana naye alifadhaika sana kutokana na mzigo alioubeba tumboni.
Hakusita kumueleza ukweli Mwanaidi. Mwana akamuelewa.
Wakazungumza kuwa, kwa kuwa tumbo bado halijachungulia sana basi George hataelezwa ukweli. Mwanaidi aliongezea kumweleza Frida kuwa yule mwanamke ni mama yake George hivyo wanampelekea zawadi kwa ukarimu wote aliowahi kuwatendea.
Kwa kusikia hivyo, Frida akasahau yote yaliyopita akakubaliana na Mwanaidi.
Wakamuacha mama nyumbani.
Kisichokuwa ridhiki hakiliki!! Alipokuwa anaishi George hakuwepo tena. Na hapakuwa na taarifa yoyote ya wapi alipohamia.
Chokoraa hana makazi ya kudumu. Mwanaidi akafadhaika.
Lakini hawakuwa na jinsi wakaamua kurejea walipotokea.
****
SIASA ni mchezo mchafu. Lakini mchezo huu hauchezeki bila pesa. Pesa hunogesha mchezo huu. Na iwapo hauna pesa ni vyema usijiingize kabisa katika mchezo huu.
Cha kushangaza bwana Seba Sebastian aliingia katika mchezo huu bila pesa na akaweza kuucheza.
Wengi walijaribu kumuiga njia yake ya maneno matupu lakini hawakufanikiwa kitu zaidi ya kuangukia pua na kusahaulika.
Msimu huu wa kuelekea uchaguzi hali haikuwa kama zamani.
Mgombea wa chama alitakiwa kuteuliwa kwa kura za wajumbe wa chama.
Hapa sasa pesa haikuwa na budi kutumika.
Seba alikuwa bahili sana, hakuwa tayari kutumia pesa nyingi kununua nafasi ya uongozi.
Sasa anafanya nini kuwashawishi wajumbe wakati ukifika wamchague tena? Hili lilikuwa linamuumiza kichwa. Alitakiwa kuwa na pesa nyingi sana kuweza kumkabili mpinzani wake mtarajiwa, kwani alikuwa na pesa nyingi tena za kutisha
Mlango wa ofisi ya diwani wa kata ulipogongwa hakuusikia vyema mpaka ulipogongwa tena.
Akamruhusu aliyegonga. Akaingia.
"Shkamoo."
"Marahaba binti karibu" alijibu kiuchovu bwana huyu.
Binti akaketi. Bwana Seba kwa kumtazama yule binti akaanza kuweka ubashiri wa nini kimeletwa mbele yake. Aidha amefaulu anataka kuchangiwa ada ama ana matatizo na familia yake amekuja kutoa taarifa.
Udiwani nao una kero zake!!
"Nakusikiliza."
Binti akajiweka sawa katika kiti. Akamtazama diwani. Akakohoa kuweka koo sawa.
"Naitwa Mwanaidi." Alijitambulisha bila chembe ya wasiwasi.
"Nakusikiliza binti zungumza." Alisema kwa hasira.
"Nimekuja hapa mimi na wewe tusaidiane, iwapo tutashindwana naweza kwenda kwa mwingine japo wewe itakusaidia sana." Alianza kuzungumza chokoraa huyu aliyekuwa ngazi ya cheo cha dada mkuu kabla ya kushindwa kuendelea na shule.
Diwani akatoa miwani yake akaifuta kisha akamtazama tena yule binti.
Hakusema neno. Akaendelea kumsikiliza.
"Ni kuhusu Dembele…Mathias Dembele."
Diwani akashtuka. Binti mdogo kama huyu ana nini cha kuzungumza juu ya Dembele. Akastaajabu.
"Upo tayari." Badala ya kumruhusu diwani amalize kushangaa Mwanaidi akamtupia swali.
Diwani akaduwaa, hakujua nini cha kumuuliza yule binti. Midomo ikawa kama inataka kusema lakini inashindwa kuendelea kusema, ikawa inatetemeka.
"Umesema unaitwa nani?" akauliza bila kutarajia.
"Upo tayari tusaidiane?" Mwanaidi hakumwambia jina lake tena.
Ule uoga aliokuwanao awali ulikuwa umetoweka na hakuona maana ya kuwa na uhitaji wa msomi kuweza kufanya jambo hili.
"Nipo tayari, ni nini kwani?"
"Kuna jambo unatakiwa kujua kuhusu jamaa." Mwanaidi akazungumza kwa sauti ya chini.
"Jambo gani?"
"Ndo nahitaji tusaidiane."
"Kivipi?"
"Nataka nikwambie na wewe unilipe kidogo tu."
Diwani akakuna kichwa.
"Kwani kuniambia mpaka nikulipe?" Seba akaingiza ubahili wake wa kuzaliwa.
"Jamaa zungu la unga." Alisema huku akitabasamu.
Diwani akashtuka kusikia habari hiyo.
"Kivipi? Nani kakwambia?" aliapagawa.
"Unapenda kuuliza hupendi kulipia. Naondoka wapo wengi tu wa kuilipia siri hii." Alinung'unika Mwanaidi huku akisimama aweze kuondoka.
"Hapana sikiliza..sikia wewe niambie kisha nakulipa."
"Naomba niondoke."
"Haya bei gani."
"Mshahara wako wa mwaka mzima. Halafu faida yako wewe itakuwa mara mia. Kwanza utaupata tena udiwani, na serikali itakulipa kwa kumfichua jamaa." Mwanaidi aliongea kwa kujiamini sana, maneno hayo hakuyapanga hapo awali.
"He!! Nini, nipishe nipishe." Bahili alipagawa kusikia mshahara wa mwaka mzima uishie kumpa binti yule mdogo.
Mwanaidi akasukuma kiti nyuma akasimama. Akaufungua mlango akimuacha diwani bahili akitukana matusi yote anayojua.
Diwani alijikuta akiwa kimya ghafla. Akayakumbuka maneno ya Mwanaidi, akamfikiria na Dembele ambaye ndiye alikuwa mpinzani wake mtarajiwa.
Mbiombio akatoka nje ya ofisi. Kimya kimya hadi akamfikia Mwanaidi akamsihi warejee ofisini.
"Tunaenda kumalizana ama..sitaki maneno kuna mahali naipeleka habari hii na nitalipwa mara moja." Alikoroma sasa chokoraa.
Diwani akaubali yaishe. Alikuwa anaupenda udiwani na pesa pia alikuwa anaipenda.
Wakarejea ofisini.
Mwanaidi akauza habari. Mauaji ya mke wa Kasuku akamuuzia bwana Dembele. Kila uozo ukawa juu yake. Akampa diwani vithibitisho vyote. Wakaenda hadi katika ile nyumba ambayo bwana Dembele hufanyia maasi yake.
Wakati akizungumza haya alikuwa na milioni nyingi katika mkoba wake, pesa iliyotoka katika akiba ya diwani bahili, Mkoba ulikuwa na kisu chake iwapo kuna ujanja wowote unaoweza kufanyika.
Mwisho wa biashara!!
Mwanaidi akarejea nyumbani akiwa ndani teksi. Hakuamini kama alikuwa amefanya jambo hilo kwa wepesi kiasi kile.
Sasa alikuwa na jeuri ya kusema kuwa alikuwa na pesa ya kuweza kufanya jambo.
Nani kama Mwanaidi??
****
MCHIKICHINI almaarufu kama ‘Mchikidown'. Mwanafunzi gani wa jijini Dar es salaam mwenye nia ya kufaulu na shule anayosoma haina waalimu bora halijui eneo hili?
Hapa kuna vibanda vingi sana vinavyofundisha masomo ya ziada kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Ni eneo maarufu ambalo huchangia wanafunzi wengi wasihudhurie vipindi vya kawaida shuleni na badala yake hujikita Mchikichini kwa ajili ya masomo ya ziada.
Cha kufurahisha. Mchikichini mwanafunzi unalipa kwa siku kupata huduma. Hapana masuala ya malipo kwa mwezi.
Jina George likatambaa kama upepo likafika Mchikichini.
Huduma zake zikahitajika.
Hesabu ugonjwa wa taifa. Daktari kapatikana.
George alikuwa ana utaratibu wa kurejea nyumbani mapema baada ya kumaliza vipindi vyake mahali alipoajiriwa.
Alipohitajika Mchikichini mambo yakaanza kuwa tofauti.
Pesa huenda pale penye pesa. George alivyoanza kuikamata pesa ndogo na nyingine ndogo iliongezeka na kuwa kubwa. Pesa ikazidi kutiririka.
Furaha kwa chokoraa huyu.
Thamani yake ikapanda.
Akatingwa haswa. Na akapokea pesa murua.
George hakuwasahau watoto wa mitaani. Kila mara alipopata nafasi alifanya kitu alichoweza kwao.
Kuna vitu kadhaa ambavyo humfanya mwanadamu anukie, sahau kuhusu marashi. Kuna umaarufu, kipaji, na kingine ni pesa.
Pesa ikikuzoea hukufanya unukie, ukishanukia kuna viumbe wataisikia ile harufu, wakiisikia wataanza kukumendea ili wakunuse vizuri. Ole wako wakunuse!!
George alianza kunukia.
Akinadada wakatamani kumnusa. Akawakwepa kwa jitihada zote akafanikiwa kwa awamu kadhaa.
Huo haukuwa mwisho wa mchezo.
Mwanamke ni sumu, huua pale anapotaka. Lakini hukuua kama ukishawishika. Na hakuna jambo gumu kama kuikwepa sumu hii.
Sumu iliyommaliza Adam na kujikuta akila lile tunda.
George akapokea simu kutoka mahali asipopajua.
Sauti ya mwanamke. Akajitambulisha kama mama Sakina.
Akazungumza na George kuhusu kibarua cha kumfundisha mwanaye anayejiandaa na mitihani ya kidato cha sita.
Sharti ni kwamba alitakiwa kumfundishia nyumbani.
George hakuwa ameikinai pesa. Akakikubali kibarua.
Malipo yalikuwa mazuri.
George alikuwa na muda usiku pekee. Hivyo majira ya saa mbili alikuwa anafika katika nyumba hii kutimiza wajibu baada ya malipo.
Alaaniwe binti yule aliyeubadili uelekeo wa kijana George.
***NI BINTI GANI ANAUBADILI UELEKEO WA GEORGE.
***MWANAIDI shujaa wa yatima ana pesa kibindoni…je harakati zitaendelea vp.
***DEMBELE…siri imevuja..nini hatma ya mwanaharamu huyu???
ITAENDELEA
muuza ubuyu ram culbby mbalu BPM Jullie Z Khantwe nifah