RIWAYA: CHOKORAA
MTUNZI: GEORGE IRON MOSENYA
MAWASILIANO: 0655727325 au 0757727324
SEHEMU YA THELATHINI NA MOJA
Wakati Dembele akihangaika kupitisha maamuzi sahihi kichwani mwake. Binti shujaa na jemedari wa vita hii alikuwa katika mahangaiko. Ni siku nyingi sana zilikuwa zimepita bila kukumbwa na tatizo hili ambalo lilimsababisha apotezane na Frida maeneo ya posta huku akiwa nusu mfu na nusu hai.
Mwanaidi aliwaza ni kifo gani ambacho bwana Dembele atawachagulia. Mawazo hayo yakapandisha shinikizo la damu. Shinikizo hili likaambatana na ugonjwa wake wa tangu kuzaliwa.
Pumu.
Mwanaidi akaanza kuikosa hewa murua. Akaanza kuhangaika huku na kule. Dawa yake ya kupuliza ilikuwa katika pochi yake.
Alijaribu kuita akiomba msaada lakini hakuna aliyesikia. Aliita kwa juhudi zote lakini ilikuwa sawa na bure.
Alijaribu tena na tena. Nguvu zikaanza kumuisha, akaanza kutapatapa. huku akipepesuka.
Roho ikalazimisha kuuaga mwili. Mwanaidi hakuwa radhi kuondoka. Hakutaka kuondoka kwa sababu aliamini alikuwa binti mdogo sana kupumzika wakati ana harakati kubwa za kufanya ili kuwakomboa wenzake.
Mwanaidi hakutaka kufa wakati anazo mbio ndefu za kuwapigania Chokoraa. Alimwomba Mungu amuache walau kidogo lakini alipangalo mola………
Mwanaidi shujaa wa machokoraa, Mwanaharakati aliyepigana kwa nguvu zake zote. Sasa alianguka chini, kiza kikatanda. Akatulia tuli.
Macho yakakutana na mkoba wake, mkoba wenye kile kichupa cha dawa yake ya kupulizia, ambayo humpa ahueni kila anapokuwa katika hali hii. Akili ikakiri kuwa ndani ya ule mkoba ipo dawa lakini haiwezi kutoka bila kutolewa. Nani wa kuusogeza ule mkoba? nani wa kuiokoa roho hii??
Viungo vyote vikasita kufanya kazi, yakabakia masikio ambayo yalisikia vishindo vya miguu kuelekea katika chumba kile. Vishindo hivyo vikaambatana na sauti zinazovuma mithili ya kelele. Mwanaidi hakuweza kutikisika.
Picha mbalimbali zikaanza kumpitia katika akili yake. Anazaliwa, anakulia mitaani, anachukuliwa na mjomba wake, anafukuzwa kwa kumsaidia Frida.
Anarudi kituo cha watoto yatima, anafukuzwa akiwa na Frida, anamsaidia Frida kutoa mimba, anakaribia kupoteza uhai kwa ugonjwa wa pumu, anaokolewa na mama mbaya muuza miili ya wasichana, anauzwa kwa mwanaume anayetaka kumlawiti, kwa mara ya kwanza anafanya mauaji, mara picha ya mama muuza miili akiuwawa nayo ikampitia, anakutana tena na Frida na Isha, wanaunganika na George, George anawekewa sumu, Frida na Isha wanakamatwa, anakutana na mama yake George akiwa mlemavu.
picha zinaendelea kwa kasi ya ajabu. Mwili unapatwa joto kali sana.
Jasho linatiririka.
Kiza kinazidi kutanda.
****
Usilolijua ni sawa na usiku wa kiza kinene. Hali hii ilimkabili bwana Dembele pia, baada ya kuwa amewamiliki mateka hawa katika himaya yake akafikiri sasa yupo huru, hakutambua kuwa hakuna siri inayodumu milele, na sasa siri yake ilikuwa imetapakaa, na alikuwa ananuka hatia.
Tamaa zikamponza.
Amakweli mshika mbili moja humponyoka.
Dembele alikuwa anatamani kuua na wakati huohuo akatamani kuwatumia wale wafu watarajiwa katika biashara yake ya madawa ya kulevya.
Ngoja ngoja hii ikamponza. Hakuwa na mtu wa kumshauri, akahisi pombe pekee inaweza kuwa suluhu ya matatizo yake. Dembele akahamia katika baa iliyopo jirani na nyumbani kwake.
Chupa moja baada ya nyingine zikazidi kusalia chupa tupu mezani. Na ulevi nao ukaingia kichwani.
Katika meza yake awali alikuwa peke yake lakini sasa akaanza kuona kama wapo watatu hadi wanne lakini cha ajabu kila akiwashika anaambulia hewa.
Alitambua kuwa sasa amelewa. Akafanya tabasamu dogo. Kisha akamimina kilevi zaidi katika glasi yake.
Alipoanza kunywa mara wale watu wakaongezeka tena. Akajaribu kuwashika.
Maajabu. Mara hii walikuwepo kweli. Wakamkamata mkono. Akajaribu kufurukuta akaona wanaonyesha vitambulisho.
Ulevi mwingi uliokuwa umemkabili hakuweza kusoma maandishi. Akahisi ni wezi wanataka kumuibia.
Akajaribu kufurukuta akakumbana na pigo kali katika shavu lake. Bia kadhaa alizokunywa zikatoweka mwilini.
Alipoongezwa mapigo mengine mawili fahamu zikamrejea vyema. Ikabakia harufu tu.
Aliweza kuvisoma vile vitambulisho.
Walikuwa ni askari!!
Alhamdulilah!!
Dembele akapagawa. Wakamvuta pembeni, wakamuuliza iwapo alikuja na gari. Akasema hapana!!
Wakaingia naye katika magari yao.
Vumbi likatimka. Ving'ora vikipiga mayowe.
Dembele akasindikizwa kituoni.
Wakati anashuka, suruali yake ilikuwa tepetepe kwa mikojo.
Askari mmoja akamcheka.
Moja kwa moja katika chumba cha mahojiano. Mwanzoni Dembele alijifanya mbishi, askari wakawa wabishi zaidi yake.
Lile tipwatipwa lilipominywa kidogo likatiririka mistari zaidi ya George.
Dembele akasema kila kitu anachofahamu.
Kwa uoga aliokuwanao akakiri kuwa ni yeye aliyemuua mke wa Kasuku. Maajabu!!
Maelezo yake ya awali yalitosheleza kwa askari hawa wazoefu.
Upesi sana wakatoweka wakiwa wameambatana na Kasuku hadi nyumbani kwa Dembele.
Msako ukaanza.
Msako wa ukombozi.
Chumba hadi chumba.
Kamata mke wa Dembele, kamata watoto. Wote wakatupwa katika kalandinga.
Msako ukaendelea katika vyumba vya siri. Huku ndipo walipopatikana, George, Mama George, Suzi, Frida, Isha. Mmoja hakuonekana.
Kimya kikatawala.
Mwanaidi!! Walikumbuka, jina hili halikuwa katika orodha ya waliopatikana japo katika maelezo yumo.
Msako haukukoma, uliendelea hadi pale alipopatikana. Akiwa hawezi kusema neno. Alikuwa ametulia tuli uso wake ukitazama mkoba uliokuwa mbali naye, mikono yake ikiwa kama inayohitaji kuuchukua mkoba ule. Lakini haikuweza kuufikia.
Wakambeba katika gari ya wazi, akakimbizwa hospitali.
Wale wengine wakafikishwa katika kituo cha polisi kwa usalama wao.
Walihifadhiwa pale hadi majira ya saa kumi na moja jioni.
Kila mmoja akiwa ametoa maelezo yake juu ya chochote alichokuwa anafahamu kuhusiana na maovu ya Dembele.
Majira ya saa mbili usiku yule diwani aliyenunua taarifa juu ya Dembele naye alikuwa mahabusu, kuingia kwake mahabusu kukaambatana na taarifa mbaya kupita zote katika riwaya ya CHOKORAA.
Yule mwanaharakati kijana kabisa, tena wa kike. Alikuwa amejaribu kuupigania uhai wake kwa namna zote lakini madaktari bingwa wakakiri kuwa hali si shwari na muda wowote anaweza kuiaga dunia. Ama la Mungu aweke mkono wake muujiza utendeke.
Kila mmoja aliumia kwa namna yake. Frida aliangua kilio.
Kwikwi ikamshika mama George.
George akaugulia kiume!!
Wote wakaomba kwa namna zao. Mwanaidi asipotee kirahisi hivyo katika uso wa dunia.
****
Makala ya Kasuku ilifanya vizuri sana katika magazeti.
Watu walibaki midomo wazi. Kwa wote waliomfahamu Dembele walibaki wakijiuliza? Maswali yasiyo na majibu.
Hakuna aliyetegemea anaweza kuwa bwana mbaya namna ile.
Lakini ilibaki kuwa hivyo.
Baada ya bwana Dembele, kila aliyemsoma mwanadada jasiri, yatima na chokoraa aliyewapigania wenzake. Bila kuwa na mhimili na kisha kuishinda vita hii, alitamani kumuona.
Umri wa Mwanaidi uliwashangaza wengi. Haukuendana na harakati alizokuwa anafanya.
Harakati zile zilihitaji mtu msomi.
Mwanaidi akasubiriwa anyanyuke kutoka kitandani aweze kupewa heshima yake. Lakini hakuamka mapema kama wanavyotaka.
Hadi usiku mchana fulani ambapo Frida alikuwa amelala. Alishtuliwa na ndoto mbaya. Ndoto ya maajabu. Alishtuka na kujikuta akiwa anatokwa jasho lakini jasho pekee halikuwa linamtia kero, kuna kitu alikuwa anahisi kinamtokea kwa mara ya kwanza katika maisha yake.
Maumivu !! maumivu makali sana. Frida akajikaza lakini yaliongezeka, akapiga kelele kubwa, kelele ikavuka mipaka ikawafikia walengwa waliopewa kazi ya kumtunza.
Wakafika na kugundua kuwa binti huyu alikuwa ameshikwa na uchungu.
Upesi zikachukuliwa hatua.
Baada ya masaa kadhaa Frida alikuwa hoi huku macho yake yaliyolegea yakimtazama mtoto wake. Mtoto asiyekuwa na baba.
Japokuwa alikuwa amechoka sana aliweza kuwasikia manesi wakimpa hongera ya kujifungua mtoto wa kike.
"Mwana….Mwanaiiiidi." alijitutumua akakiita kitoto kile jina hilo.
Kikalipuka kwa kilio cha kitoto.
Jina kubwa!! Mwanaidi.
Kwa sababu Frida alikuwa bado kitandani hakupewa taarifa yoyote mpya juu ya maendeleo ya Mwanaidi aliyekuwa anapumulia mipira.
Lakini ndoto yake ya kuota kuwa anajifungua mtoto anayefanana na Mwanaidi huenda ilikuwa sahihi. Alikuwa amejifungua Mwanaidi mpya na kumbatiza jina hilohilo.
Alipopewa taarifa juu ya umauti uliomkumba Mwanaidi, alifanya tabasamu hafifu kisha akasema.
"Ili itimie ile ndoto. Ndoto ya Mwanaidi kuishi maisha mapya ya furaha akiwa na mzazi wake ambaye ni mimi. Ni muda wa kumtunza aliyenitunza na kuniokoa." Maneno yale yaliamsha hisia, George akawa wa kwanza kudondosha chozi. Frida akalipuka na kilio kisichozuilika. Alikuwa anamlilia Mwanaidi.
Bahati nzuri alikuwepo Mwanaidi mwingine kichanga.
Isha akiwa mama mdogo, George baba mlezi, mama George bibi, Suzi shangazi, Frida akibaki kuwa mama mzazi wa Mwanaidi mpya.
Yule shujaa wa mapambano, asiyeogopa kufa wala asiyehofu kuua, ugonjwa wa pumu ukautwaa uhai wake.
Alikufa akiwa anapambana, hakuwahi kupumzika kamwe.
Kwa kifo chake akawaokoa wengi!!
****
Mali za bwana Dembele zilitaifishwa baada ya kuwa amehukumiwa kumalizia maisha yake yote jela huku akisindikizwa na diwani ambaye alivuliwa madaraka kutokana na kuficha siri kubwa kama ile baada ya kuuziwa na hayati Mwanaidi kisha kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela, mali zile zikawekwa mnadani. Zilikuwa mali nyingi sana. Mauzo yake yakawezesha kujengwa kituo kikubwa cha watoto yatima. Ili kuenzi harakati za mapambano yale ya siku nyingi. Kwa heshima ya yule mtoto aliyekufa akipigania watoto kituo kile kikaitwa jina lake ‘MWANAIDI'.
Ilikuwa huzuni wakati wa kukifungua kituo hicho.
Utepe ulikatwa na yule mtoto mdogo aliyezaliwa na chokoraa kisha akaitwa Mwanaidi.
Maisha yakaendelea.
****
Muonja asali haonji mara moja.
George Emmanuel. Alikuwa muonja asali, na ladha ya shubiri hakuitambua. Suluba walizopitia wenzake yeye alikuwa hajazipitia kwa kiasi kikubwa hivyo.
Starehe alizoendekeza baada ya kuwa amepata pesa za bwana Dembele akaendelea nazo tena baada ya kupata kazi katika kituo kile cha watoto yatima cha MWANAIDI.
Starehe yake aliyoendekeza zaidi ilikuwa wanawake.
Ukiyaendekeza mapenzi lazima uupoteze uelekeo, George aliyaendekeza huku akiisaka ile ladha aliyoipata kwa yule binti wa kitanga aliyemuingiza katika ulimwengu huu.
Alijisahau kuwa aliwahi kuwa chokoraa, alisahau kila kitu akavimba kichwa.
Machoni pa watu alijionyesha kuwa yu mwema sana tena mkarimu lakini ndani alificha mengi. Alikuwa zaidi ya mchafu.
Frida na Isha walijaribu kumshauri, aliwasikiliza kwa makini na kuahidi kubadilika lakini kamwe haikuwa hivyo.
Kila yatima aliyekuja katika kituo cha MWANAIDI ilimradi alikuwa ni mrembo George alifanya juu chini ili aweze kushiriki naye mapenzi.
Yote haya yalifanyika kimyakimya. Bila mtu yeyote kutambua.
George alitumia pesa!!
Kweli pesa mwanaharamu.
Tabia hii ilizidi kukomaa hadi pale alipotembelewa na binti nyumbani kwake. Binti mrembo lakini asiye na tabasamu usoni pake.
George alijiuliza kwa nini binti huyu anashindwa kutabasamu?
Binti akaketi katika moja ya viti pale sebuleni.
Hakuongea neno kwa muda akawa anamtazama George.
Baadaye uso wake ukaanza kumeremeta kwa hasira. George akashangaa, lakini mshangao haukudumu sana yule binti akamvagaa, George ambaye hakuwa amejiandaa kwa shambulizi hili, akaanguka chini.
Binti juu yake. Binti mwenye hasira kali. Binti ambaye hadi wakati huo hakuwa amesema neno lolote lile.
Hata salamu hakuwa ametoa!!
***MWANAIDI amefutika katika uso wa dunia….lakini amezaliwa Mwanaidi mwingine…….je kuna mapambano zaidi??
**GEORGE anaendekeza uasherati…anasahau alipotoka……
Sasa ametembelewa na mgeni wa kike..mgeni hajasema neno ila amezua balaa….JE HUYU NI NANI NA KWA NINI AMEZUA BALAA??
mangimeza Khantwe culbby Toplady Igunga Moja BPM showtie Samaya