RIWAYA: CHOKORAA
MTUNZI: George Iron Mosenya
SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
George hakuwahi kukutana na dhahama hii ya usumbufu. Lakini huu ulikuwa usumbufu wa maajabu, usumbufu usiokuwa na maneno ndani yake.
Usumbufu wa vitendo.
Mara huyu avae hivi mara yule arembue jicho. Ilimradi shaghalabaghala.
Mwanaume akajikaza!!
Lakini atajikaza mara ngapi iwapo usiku ule uvumilivu ulimshinda akataka kumbaka Isha??
Hata kama hakumbaka sasa ana ujauzito.
Hata George ni mwanadamu!!
****
MAJI ukiyavulia nguo sharti uyaoge. Mwanaidi alikuwa ameamua kupigana kwa ajili ya watoto yatima na wasiokuwa na makazi. Watoto ambao wameugeuza mtaa kuwa makazi yao. Watoto waliobandikwa jina nchini Kenya wakiitwa ‘chokoraa' jina ambalo linatumika sasa afrika mashariki kwa ujumla.
Kadri mwanaidi alivyoikamata pesa ndivyo alivyoona kuwa haitoshi katika harakati zake. Alitakiwa kufikiri zaidi anapata vipi pesa nyingi zaidi ili aweze kutimiza alichonuia katika akili yake.
Sasa alikuwa amefanikiwa kuikamata akili ya diwani na alikuwa amechota pesa nyingi.
Jambo la kwanza lilikuwa kumpeleka mama George katika huduma ya afya.
Huku aligharamika kiasi kikubwa cha pesa ikiwemo ya kuwahonga madaktari ili wasipeleleze zaidi alikumbwa na nini hadi kufanyiwa upasuaji mbovu namna ile.
Kwa hili alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Jambo jingine alilolifikiria kwa wakati uliopita na sasa alilitendea kazi ni kuhusu kutafuta nyumba kubwa.
Madalali wa mjini wakachukua pesa yao na nyumba ikapatikana.
Nyumba ya vyumba viwili pamoja na sebule.
Maisha mapya!!
Frida akaanzishwa kliniki. Kwa ajili ya ile mimba yake isiyokuwa na baba.
Mwanaidi akawa mlezi rasmi wa familia.
****
WIVU wa mapenzi. Hauchagui kaliba yoyote katika jamii. Maskini anao, tajiri anao vilevile.
Usiombe wivu ukauteka moyo wako. Waweza kujikuta unafanya mambo ambayo mjukuu wako akisimuliwa atakiri kuwa bibi ama babu yake alikuwa na wazimu. Si bure!!
Huwezi kutambua kama una wivu, wivu humfanya mtu awe mjingamjinga na kujiona anayofanya ni sahihi.
Ule wivu ulioiondoa roho ya mwanadada Emiliana. Sasa ulikuwa unashambulia na kuigalagaza roho nyingine katika mazingira mengine.
Huyu alikuwa anahangaika muda mrefu lakini hakuweza kulalamika popote kwa kuwa tu hakuwa na ushahidi wa kumpa uhuru wa kuongea.
Je? Ushahidi unajileta wenyewe? Jibu ni hapana. Ushahidi hutafutwa.
Binti huyu akalazimika kuutafuta ushahidi, kimya kimya kama alivyofanya marehemu Emiliana kwa mume wake mtarajiwa Kasuku.
Mitego aliyokuwa ameitega ili imnase ushahidi sasa ilikuwa imetoa majibu aliyoyasubiri. Majibu yaliyomkera na kumfanya ajute kufanya upelelezi ule.
Kichefuchefu kikamshika. Akatamani kutapika lakini hakutapika.
Akawahi limao lake akakikabiri.
Njiani aliona maluweluwe. Hakuamini alichokiona, lakini alijilaumu kwa nini alikitafuta.
Hakuitikia salamu ya mtu yeyote yule. Alitembea akiyumba huku na kule, akaufikia mlango wa chumba chake akaufungua. Akajitupa kitandani. Akamngoja adui yake aweze kurejea amkabili.
Mwanzoni hakuhisi usingizi kabisa lakini alikuja kushtuka asubuhi.
Adui alikuwa anamalizia kufunga mkanda wa suruali yake aende kazini.
Alitaka kumzuia lakini akajikuta anaagwa. Hakujibu!!
Subira yavuta heri endapo yule hasira ambaye majibu yakle ni hasara atakuwa likizo.
Lakini siku hii hasira alikuwa amejikunyata katika moyo wa mwanadada huyu. Hivyo subira akawa ameondoka zake.
Hakuweza kuikabili hasira hii.
Aliona yule bwana wake anachelewa kurejea akaamua kutoka mwenyewe aweze kumfuata. Alitegea mida ile ya siku iliyopita, alitegemea kumuumbua.
Akiwa njiani anakutana na kundi la akina dada.
Alikuwa anawafahamu wawili kati yao.
Hasira zikachachamaa. Akawakabili. Akawasimamisha.
"We malaya George ni nani yako?"
"Malaya? Nani Malaya..na George yupi?" alijibu kwa kiburi binti mnene mfupi.
"Nakuuliza George ni nani yako. Yule mwalimu." Alitoa maelezo ya ziada.
"Mwalimu wangu kwani vipi? Unataka namba yake? Kakujaza mimba nini?" alijibu kwa dharau. Wenzake wakacheka.
Sasa akakumbwa na msukumo wa hasira isiyosimulika. Akamvamia yule aliyetoa majibu yale. Akaanguka naye chini. Akaanza kumshambulia na makucha.
Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Wale wasichana wawili wakajiunga kumtetea mwenzao.
Kibao kikamgeukia yule binti. Ambaye alijuta kuzaliwa chokoraa na kisha kuitwa Isha. Akaijutia ile mimba aliyopewa na George.
Majuto hayo yakawa na thamani yake.
Akaupata msaada.
****
George, akiwa darasani siku hii alikuwa anawaza juu ya msichana wa kitanga ambaye alikuwa katika wakati mgumu sana kukabiliana na hisia hizi. Hisia za ajabu.
Alikuwa anajiuliza aliwahi lini kukumbana na hisia hizi.
Alipoumiza kichwa sana akamkumbuka Frida. Siku ya kwanza walipoonana wakati anasoma chuo kikuu.
Upendo!!
Aliamini alikuwa anampenda.
Lakini kikwazo kikubwa kilikuwa ni Isha. George alitambua kuwa licha ya kwamba anaishi na Isha bila kuwa na mipango yoyote ya mbeleni. Lakini alikuwa amembebea mtoto wake.
George aliogopa kujihusisha na msichana mwingine kwa kuhofia kumjaza msichana mwingine mimba kisha kuongeza wimbi la watoto wa mitaani.
Hakutaka kabisa kuhusika katika tatizo hili. Kwani yeye alikuwa katika harakati za kulipunguza tatizo na si kulitawanya kama hivi anavyowaza.
Binti huyu wa kitanga aliyekuwa kidato cha tano. Alikuwa na kila kigezo cha kuitwa mrembo. Lakini hili halikuwa na maana kubwa kwa George. Na alilipuuzia mpaka siku ambayo alichelewa kutoka kazini baada ya mabinti watatu kumsihi awasaidie maswali kadhaa ya somo la hesabu.
Kati ya mabinti hawa alikuwemo binti wa kitanga.
Baada ya kumaliza kufundishana, mabinti na mwalimu waliongozana njia moja.
Marafiki wawili wakapeana ishara. Mara George na Lisa wakabaki peke yao. Marafiki wawili wakifuata kwa nyuma.
Aliyesema mapenzi yalizaliwa Tanga huenda hakukosea.
Lisa akaanza kufanya yale aliyoyajua. Ilimradi tu kumtega bwana George.
George ni mwanaume na macho yake hayana pazia. Kilicho chema machoni naye kwake pia kilikuwa chema.
Akajisahau kama ni mwalimu. Akauvaa ujana.
Yaliyotokea, yaliwafanya waonekane kama wapenzi wa saiku nyingi.
Wakati yanatokea. Lilikuwepo jicho la mwanadada mjamzito Isha likifuatilia kwa ukaribu.
Isha hakutaka kuwavamia kwa wakati ule.
Akaachana nao akawahi nyumbani.
George alipoachana na Lisa alijutia alichokifanya. Japo hakikuwa na madhara yoyote, sawa lakini ni kosa kukamata kiuno cha msichana hadharani. Walionitazama watanionaje? Hata Isha angenifikiriaje?
Mimi ni mwanaharakati. Sitakiwi kuwa dhaifu!!
Nikirudi nyumbani nitamshirikisha Isha juu ya jambo hili. Najua atanishauri vizuri. Alijisemea George.
Hapo alikuwa katika basi akielekea nyumbani kwa akina Sakina. Kwa ajili ya somo la usiku.
Ilikuwa bora huku alipotoka kuliko hapa anapoelekea maana mitihani ilikuwa inamkabili.
Usiku aliporejea Isha alikuwa amesinzia fofofo.
Hayakufanyika mazungumzo yoyote yale.
Asubuhi kama ilivyo ada alitakiwa kuwahi kazini.
Alimuaga Isha. Lakini hakujibiwa.
Hakujali, aliamini ni mang'amung'amu ya usingizi.
Sasa ni jioni anakumbwa na mshtuko. Yule binti aliyemuacha kitandani. Akiwa katika lindi la usingizi.
Anakutana naye akiwa hana fahamu. Amezungukwa na wanafunzi wakimshangaa tumbo lake kubwa likiwa nje.
George anapigwa na butwaa kukutana na Isha katika hali ile.
Hapakuwa na haja ya kujiuliza maswali mara mbimbili. Hakuwepo wa kuyajibu.
Zikachukuliwa hatua.
Isha akapelekwa katika kituo cha afya kilichokuwa jirani.
George badala ya kwenda nyumbani kwa akina Sakina, aliandamana na gari la walilokodi kumpeleka Isha hospitali.
Hali tete!!
****
Seba Sebastian, diwani aliyaekuwa na nia ya kuwania tena kiti cha udiwani alikuwa anafurahia kila hatua aliyokuwa anapitia kwa wakati huu. Habari aliyoinunua kwa bei mbaya sasa ilikuwa inampa faraja.
Katika pitapita zake huku na kule aliweza kuzisikia tetesi juu ya bwana Dembele na shughuli zake za kuuza madawa.
Lakini kati ya hawa wote hakuna hata mmoja ambaye alikuwa na uhakika juu ya anachokizungumza.
Hali hii ilimpa faraja Seba na kujiamini kabisa kuwa ni yeye pekee anayehodhi habari ile.
Alihitaji sasa kuifanyia kazi. Asingeweza kwenda peke yake kufanya maamuzi haya. Yule mwanamke wake mbichi kabisa ambaye alikuwa anamuandaa kuwa mke wake baadaye ilikuwa lazima ashirikishwe.
Seba alikuwa na mke na watoto lakini bado alikiuka maadali ya dini yake akaweka nyumba ndogo.
Nyumba ndogo hii aliitunza tangu ikiwa shuleni. Alimlipia ada na kumgharamia kila kitu na sasa alikuwa amemaliza chuo kikuu. Alimchukulia seba kama baba yake wa kumzaa, wazazi wake wote walifariki kitambo na hakuwahi kuwatambua.
Walipishana sana umri kwa kiasi kikubwa lakini angefanya nini binti yule iwapo alikuwa anahitaji huduma za mzee Seba?
Hakuwa na ujanja.
Kwa kuwa Seba alikuwa na elimu duni. Alikumbwa na kihoro akaketi meza moja na mtoto wake huyu ambaye anamuandaa kuwa mke wa pili. Akamfungukia kila kitu juu ya habari aliyoinunua.
Habari kuhusu Dembele.
Binti alisikiliza kwa makini sana.
Kisha akachukua nafasi ya kutoa ushauri.
Akamshauri avute subira kidogo, uchaguzi ukikaribia ndipo amuumbue bwana yule.
"Yule mtoto hawezi kuiuza tena habari hii?" Seba aliuliza.
"Akiiuza bado itamchafua bwana Dembele na atakuachia kiti..tena hiyo itakusaidia sana maana hautakuwa na hatia yoyote na hawezi kukuwekea kisasi." Alijibu kwa utulivu, usomi ukichukua nafasi.
Seba akakolea.
"Sikukosea kukuchagua." Alisifia mzee huyu kisha akamkumbatia na kumbusu shavuni.
Siku ikaisha. Mzee seba alilala katika nyumba aliyompangia binti huyu.
Asubuhi akaondoka na kuiacha ile siri ikiwa sio siri tena.
Alijisahau kuwa hakuna siri ya watu wawili.
Kitita cha pesa kiliachwa mezani kama sumaku ya penzi. Asidanganyike na wajanja wa jiji akamsaliti.
****
MWALIMU wa kike hakuwa na amani hata kidogo moyoni. Mshawasha wake wa kumuona George ulikuwa unamwadhibu.
Siku hiyo alitambua kuwa lazima itakuwa siku ya kipekee kwake.
Siku ya kumshawishi kitu George.
Maajabu George kuchelewa kazini.
Dakika, masaa yakakatika. Bado George hakuonekana na hapakuwa na taarifa yoyote ile. Kibaya zaidi hakuna aliyejua nyumbani kwake.
Suzi akakosa amani. Jambo alilobeba moyoni lilikuwa linamsumbua sana.
Jioni ikafika, bado George hakuonekana.
Suzi akamlaani George kimoyomoyo kwa kutomiliki simu ya mkononi wakati uwezo alikuwanao.
Suzi hakuamini kabisa kama ataweza kupata usingizi katika hali hii ya mawazo. Lakini angefanya nini? Akaamua kuondoka huku amani ikizidi kumkimbia. Alimuhitaji sana George.
Wakati Suzi akihangaika kumuwaza George. Wakati huo George alikuwa akihangaika huku na huko kulipia pesa za matibabu.
Hakuwa na pesa ya kutosha kutokana na kuwaazimisha waalimu wenzake pesa pamoja na kulipia kodi ya nyumba. Sasa pesa ilihitajika.
Si kwamba hakuwa na akiba ya pesa nyingine la!!
Pesa ilikuwepo lakini anayefahamu pesa zilipo alikuwa amepoteza fahamu.
Isha alikuwa mtunzaji wa pesa nyingine katika njia ya kibubu, ambacho alifahamu mwenyewe ni wapi anakihifadhi.
Mwanaume alitakiwa kuchukua maamuzi. Akafikiria kukimbilia katika familia ya Dembele, moyo ukasita. Alihofia kujibiwa vibaya maana Sakina hakuwa anatabirika.
Suzi !!
Jina hilo likashambulia kichwa cha George. Akamkumbuka binti huyo mhitimu wa chuo kikuu ambaye kwa muda huo wa kutafuta kazi alikuwa anafundisha masomo ya ziada pia.
Suzi licha ya kuwa mwalimu na yeye alikuwa katika mpambano na wanafunzi wengine wengi wanaomuwinda George kimapenzi.
Aliwahi kumkaribisha George nyumbani kwake mara mbili lakini hakufanikiwa kumteka kimapenzi.
Suzi alikuwa akimuhitaji sana George. Lakini mazungumzo kati yao yalileta huzuni kubwa. Japokuwa maisha ya Suzi yalikuwa vyema kutokana na kutunzwa na diwani. Bado alibakia kuwa yatima, aliyepata adha ya uyatima utotoni pekee.
Historia ya George na mipangilio kabambe aliyokuwanayo katika kuwaokoa yatima na chokoraa ilimkosha Suzi na kuahidi kuwanaye bega kwa bega
Walihitaji pesa kufanikisha harakati hizi.
Pesa hiyo ilikuwa kikwazo na sasa pesa hiyo inayohitajika inamsukuma George kwenda kwa Suzi.
Suzi hakutegemea ujio wa George. Akiwa na kanga moja pekee alimkumbatia George kwa nguvu. Na ghafla akambusu. George akajilazimisha kutabasamu.
Suzi akaketa hovyo mbele ya George ambaye hakuwa na furaha.
"Una nini Gee"
" Acha tu…..Suzi kuna tatizo. Dada yangu mmoja amefikwa na tatizo. Yupo hospitali mi sina kitu nahitaji sana msaada wako we fanya kuniazima..halafu…"
"Mimi na wewe hatuazimani. Shilingi ngapi inahitajika. Pole sana G najua ni kiasi gani una upendo wa dhati kwa chokoraa na yatima"
George akataja kiwango cha chini kabisa. Akapewa mara mbili yake.
"George ukitoka huko hospitali pliiiz usiache kuja kuna jambo zito kwa faida yangu na yako. Usiache hata kama ni usiku vipi?" Suzi alimsisitiza George wakati anatoka.
George akakubali.
Akatoweka upesi kuwahi hospitali. Hakuamini ingekuwa rahisi kiasi hicho kukomba pesa kwa Suzi.
Kichwani aliamini kuwa Suzi alimhitaji usiku huo kwa ajili ya mapenzi tu hapakuwa na jipya lolote.
"Ameninunua tayari sina ujanja." Alikiri kwa sauti ya chini akiwa peke yake.
***SUZI ameipata siri ambayo anahitaji kumshirikisha GEORGE….Siri juu ya DEMBELE…….Siri ya kuuza madawa ya kulevya. KWANINI ANAHITAJI KUTOBOA SIRI HII??? Na je itakuwa na manufaa ama itazua majanga kwa chokoraa hawa??
***ISHA katika matatizo…..wivu umemsukumia pabaya…..sasa yu hoi hospitali.
***MWANAIDI, FRIDA NA MAMA GEORGE….Harakati zinaendelea.
muuza ubuyu ram culbby mbalu BPM Jullie Z Khantwe Excel ladyfurahia Igunga Moja