CABO-DELGADO-PART 34
Komandoo "JS" ndani ya Gorongosa Camp"
Komandoo "JS" alijaribu kulifukuzia lile lori la mbuga ya wanyama ya Gorongosa, lakini hakufanikiwa kulipata. Mpaka alipoifuata barabara ya vumbi ndipo alianza kuona alama za matairi ya Lori na bahati kulikuwa kumenyesha mvua nyepesi hivyo ilikuwa rahisi kuona alama za matairi ya gari. Mpaka akafika njia panda ambayo ukiifuata kulia unaelekea mbugani na kuna kibao cha kuonyesha unaelekea mbugani.
Hapo akasimama kutafakari uelekeo wa yule Bob-Chinanga ni wapi amepita kuelekea kambini kwao alipowekwa Kachero Manu. Wakati hajui aelekeee uelekeo gani ghafla akamuona kijana wa makamo anatimua mbio kwa taharuki kuelekea uelekeo wa gari la komandoo "JS".
Komandoo "JS" akachomoa bastola yake na kuelekeza usawa wa yule kijana, kisha kwa sauti yenye maamrisho ndani yake yenye kuonyesha usipotii utakipata chamoto. Akanena Komandoo "JS", kumwambia yule kijana, "simama hapo hapo ulipo, unatoka wapi na unakwenda wapi usiku huu"?. Kijana alipigwa na bumbuwazi na kugwaya, kulikojionyesha dhahiri usoni kwake.
Alifahamu hiyo ni kauli mutlaki isiyo na chembe ya mashaka kuwa akibishia kutii atauliwa. Mwenyewe alijua anakimbilia kwenye usalama kumbe anakwenda kukutana na mtihani mwingine.
Huyu kijana ni wa bodaboda ni yule kijana anayevusha nyara haramu za asili ambaye alipokonywa bodaboda yake na Bob Chinanga. Hapo alikuwa amekimbia karibia kilometa 2 na ushee ili kuokoa uhai wake na hakuamini kama kafanikiwa kumchoropoka Bob Chinanga. Mtu ambaye hamna asiyemfahamu katika mji wa Gorongosa awe mtoto au mkubwa juu ya ukatili wake.
Alikuwa ameshachoka vibaya sana kutokana na mbio. Sasa alipoona taa za gari kwa mbali akapata nguvu mpya za kuongeza mwendokasi ili aweze kupata msaada. Lakini alivyokaribia akashtushwa na sauti ya kuamrishwa kusimama. Pale pale kijana yule akasimama huku amenyoosha mikono juu.
Komandoo JS akaanza kujongea anamfuata kwa tahadhari akihofia huenda akawa ni adui. Mpaka alipofika usawa wa karibu zaidi, akamhoji "wewe ni nani? na unatokea wapi usiku huu"?."Mimi ni dereva bodaboda, nilikuja mbugani kubeba mzigo", alijibu kijana yule kwa sauti ya uoga.
"Bodaboda yako umeacha wapi, na mbona unakimbia kama wewe sio mhalifu na ni raia mwema"? aliendelea Komandoo "JS" na mahojiano yake. "Nimeporwa bodaboda na Bob-Chinanga" alijieleza kijana yule. Komandoo "JS" kusikia jina la Bob Chinanga, vinyweleo vya mwili vikamsisimuka akatambua ameshazidiwa akili na akizubaa itakula kwake.
Anaweza kumpoteza Kachero Manu na yeye pia akaingizwa kwenye mtego wa kukamatwa kisha kupotezwa pia. "Haya twende haraka tuondoke na gari, hii sio sehemu salama hata kidogo" alisema Komandoo "JS". Chapuchapu kijana yule na komandoo "JS" wakakimbilia kwenye gari.
Mwanzoni yule kijana alidhania wanaondoka kuelekea Mjini, lakini akashangaa kuona gari linaenda uelekeo wa kule kule alipotoka kuporwa bodaboda yake na Bob Chinanga. Ikabidi awe mpole tu asiulize ulize maana hata huyu alikuwa hajui kama ni shirika moja na Bob Chinanga au ni watu tofauti.
"Na kama ni watu tofauti kwanini anamiliki silaha? na kwanini anaenda kule kule alipotoka yeye ambapo maadui zake ndipo walipo?" ni maswali ambayo alikuwa anajiuliza hapati majibu.
Walipoenda kama dakika 10, Komandoo "JS" akavunja ukimya, "Nimekuja kumsaka Bob-Chinanga kanitoroka huko njiani ndio maana kakupora bodaboda yako. Hivyo naomba msaada wako wa kunielekeza kambini kwao".
Kijana yule akavuta pumzi ndefu za uoga na kuzishusha kisha akakohoa kidogo akaanza kuzungumza "kwa kweli huko kambini kwao sijawahi kufika ila kuna siku katika harakati zetu hizi za magendo wakati tunapita njia za panya kuwakwepa askari wanyama pori waliokuwa wanatufukuza tumeshawahi kuona helikopta ndogo inatua kwenye kiwanja kidogo, ilibidi tujifiche na bodaboda zetu kwa kuogopa tusije tukakamatwa tulikuwa tunajua ni askari wanyama pori wa anga.
Lakini tulivyochunguza wakati abiria wanashuka alikuwa ni Bob Chinanga na hawara zake kama wawili na rubani wa helikopta wanashuka. iIikuwa ni usiku wa manane na tuliweza kuwatambua kwa sababu waliwasha taa za hapo kiwanjani. Hivyo inaonyesha kambini kwao sio mbali na huo uwanja mdogo wa ndege vinginevyo wasingeshukia hapo.
Pia baadhi ya askari wa hiyo kambi yao tunashirikiana nao kwenye biashara za magendo huwa wanatupa mizigo ya dili tunawapelekea Mjini, sasa mmoja wao kuna siku alilewa sana akaanza kuropoka ropoka mazingira ya kambi yao, akafikia hatua ya kusema hawezi kiumbe yoyote kukanyanga kambini kwao akatoka salama akaleta kejeli kuwa hata kama jeshi zima la Marekani, litafanikiwa kufika kambini kwao basi halitoweza kutoka salama wote watateketezwa hivyo imaonyesha ni kambi iliyojitosheleza kwa kila namna ya ulinzi na vifaa", akamaliza maelezo yake marefu yule kijana yaliyovuta hisia za Komandoo "JS".
Maelezo ambayo yalimpa mawazo mapya Komandoo "JS" ya kuwa kwa muda mchache uliobaki asingeweza kupambana na kikosi chote cha kambi akiwa peke yake, ila anachoweza kufanya ni kwenda kuvizia kwenye huo uwanja wa ndege, ili kama atajitokeza hapo Bob Chinanga aweze kupambana nae kwa kumteka na kumtumia kama ngao ya kuingia kambini kirahisi ili kumkomboa Kachero Manu.
Lakini alikuwa anajua anacheza bahati nasibu ya pata potea. Maana Bob Chinanga anaweza kuondoka kambini kwa kutumia usafiri wa gari, lakini hisia zilimtuma hawezi kutumia tena gari kwa sababu anafahamu kuwa anaviziwa na adui yake, hivyo atataka kuondoka kwa helikopta akiwa na yakini asilimia mia kwa mia kuwa Komandoo "JS" hafahamu uwepo wa kiwanja kidogo cha ndege kwa namna kilivyojificha.
Akakumbuka kanuni yake muhimu inayomuongoza kwenye kazi zake za kijasusi alifundishwa na mwalimu wake toka CUBA kuwa ukitaka kuwa mpelelezi mahiri heshimu sana hisia zako na pia kila kitu unachokutana nacho usikipuuzie hata kidogo. Mwalimu wake huyu toka CUBA alikuwa anampenda sana Komandoo "JS" hasa akikumbuka kwenye jaribio la siku ya kwanza tu ya somo lake, Komandoo "JS" alipata alama 99/100.
Yule Mcuba aliingia darasani siku ya kwanza afu mbele kulikuwa na ubao na meza iliyojaa vitu aina tofauti tofauti zaidi ya ishirini kama boksi la biskuti, chupa ya maji, daftari na vinginevyo halafu kabla hajaanza kufundisha akaomba dharura ya dakika tano akatoka nje ya darasa. Halafu kabla hajarudi vile vitu vikatolewa pale mezani alivyorudi yule mwalimu darasani akaanza kugawa karatasi nyeupe zimeandika jaribio la kwanza, wanafunzi walishangaa hawajafundishwa kitu wanaanza kupewa mtihani!.
Swali lilikuwa moja tu utaje vitu vilivyowekwa pale mezani kabla havijaondolewa. Komandoo "JS" alifanikiwa kutaja vitu kumi na tisa kati ya ishirini vilivyokuwa vimewekwa mezani. Kitu ambacho toka siku ya kwanza alitabiriwa na Mwalimu huyu toka Cuba kuwa atakuja kuwa jasusi mahiri sana. Na ndio ilivyokuja kutokea, ukitafuta Makomandoo watano bora barani Afrika huwezi kumuweka pembeni Komandoo "JS" hata kidogo. Utakuwa umetenda dhambi kubwa sana ukimtenga kwa sababu ya kijiba chako cha roho na chuki binafsi.
"Basi nipeleke karibia na huo uwanja tukifika karibu niambie tulifiche gari mimi nitakwenda wewe utabaki humu ndani ya gari ukinisubiri. Usijaribu kutoka, na kama utaona helikopta inapaa ikipita nusu saa sijarudi, basi fahamu usalama wangu upo hatarini ondoka mara moja na hili gari ukaliache popote pale katikati ya Mji na upotee zako. Wenye gari lao watalipata kwa sababu linauwezo wa kujulikana lilipo kwa njia za kimtandao". Kijana alipewa maelekezo fasaha na Komandoo "JS".
Komandoo "JS" akaendesha gari kwa maelekezo ya yule kijana kuelekea kwenye uwanja mdogo wa ndege. Walipokaribia na uwanja wa ndege ambao upo meta kama 600 kutoka kwenye lango kuu la kuingilia kambi ya Gorongosa. Kijana yule wa bodaboda alimuelekeza Komandoo "JS" ukaribu wao na uwanja hivyo wakatafuta kichaka kimoja makini sana wakalisekwa gari. Kisha wakazifunika viakisi mwanga vya gari kwa kitambaa ili lisionekane kirahisi.
Kijana akabakizwa ndani ya gari akiwa kaachiwa funguo za gari na bahati nzuri alikuwa ni kijana wa mjini anajua vizuri tu kuendesha gari. Kisha Komandoo "JS" akaelekea uelekeo wa uwanja wa ndege mdogo ili kujaribu bahati yake ya kumvizia Bob Chinanga.















Kachero Manu katika harakati za kuisambaratisha "Gorongosa Camp"
Baada ya kuhakikisha ameshawaua Bob Chinanga na msaidizi wake, haraka haraka akavua nguo za yule msaidizi wa Bob Chinanga akazikung'uta kuondosha mavumbi kisha akazijaribisha kuvaa. Zikawa zimemkaa vyema kama amepimishwa yeye na fundi nguo. Akavaa na kofia yake na viatu vya yule msaidizi ingawa vilimbana kiasi ila vilimuenea kwa dharura vilikuwa vinavalika.
Kisha akampekua Bob Chinanga akakuta anazo bastola mbili za kisasa moja ina kiwambo cha kuzuia sauti, na vipisi kadhaa vya bangi kwenye pensi yake ya dangirizi na rundo la funguo. Akazichukua zile funguo na bastola zote mbili akajimilikisha kisha akaokota tochi ya yule msaidizi wa Bob Chinanga kisha akaiweka vizuri miili yao kisha akatoka nje ya selo na kufunga lango kuu kwa nje.
Nje kulikuwa ni giza totoro lakini kwa msaada wa tochi mkononi aliyoichukua selo, akawa anaweza kuona anapoelekea umbali wa mpaka meta 10 mbele yake. Kutokana na namna alivyoisoma ramani ya selo kuu kutoka kwenye karatasi aliloletewa kijanja kwenye pipa la kutupia takataka na Dr.Anabella, aligundua kuna njia kama sita za kutoka nje ya Selo. Lakini njia nyepesi zaidi ya kutoka kwa haraka kwa muda mfupi ni kwa kupitia handaki lililochimbwa karibu na chooni ambalo linakuja kuibukia karibu na lango kuu la kutokea nje linalotumiwa na magari kutoka nje ya kambi.
Hivyo alivyotoka tu selo alitembea kama hatua 30 kwa makadirio akaanza kushuka ngazi kuelekea chini ya jengo akaanza kukumbuka siku aliyopelekwa kwenye mateso akajipigiza kiwambazani ilifanana na njia hii kisha alipofika chini ya ngazi ya mwisho akaona kwa mbele yake kuna bwawa la matope lenye kutoa harufu mbaya ambalo alipitishwa siku ile ya mwanzoni.
Akasimama kidogo kutafakari njia ya kupita akawa anafanya kumbukizi ya ramani maana kulikuwa na njia ya kushoto na kulia, baada ya muda akachukua maamuzi ya kufuata njia ya kulia ilikuwa ni njia nyembamba yenye kokoto ndogo ndogo akatembea kama takribani dakika 5. Baada ya hapo, njia ikaanza kuwa pana kwa mbele akaanza kuona mwangaza wa taa akazima tochi yake na kujibana kwenye nguzo kuchungulia ni eneo linalohusika na kitengo gani.
Akawa anaona watu wanapishana kila wakati huku na kule wakiwa wamevalia makoti rangi nyeupe na kofia nyeupe wamebeba maboksi kichwani, wanayatoa chumba kimoja wanapeleka kwenye chumba kingine.
Akasita kidogo huku akijiuliza aendelee kwenda mbele au asitishe kwa sababu njia ya kuelekea kwenye handaki ipo katikati ya vile vyumba viwili vinavyotazamana kwa mbele yake ndio kuna vyoo kisasa moja ya kile choo sio choo cha kweli bali ni njia ya chini kwa chini ya handaki.
Njia hiyo huwa inatumika mara chache chache kwa dharura kufika kwa haraka karibu na lango kuu la kutokea. Eneo lile lilikuwa ni kiwanda kidogo cha kufungasha madawa ya kulevya yanayoletwa kupitia bandari ya Beira nchini Msumbiji yakitokea nchi za Pakistani na Brazili kisha yanafungashwa hapo "Gorongosa Camp" na kusafirishwa kwa boti za kasi kuelekea sokoni nchini Afrika ya kusini kwa njia za panya.
Wakati anatafakari kitu cha kufanya akaona mtu ambaye ni mmoja wa walinzi, kavaa nguo kama zake ameshika bunduki anatoka chumba kimoja kwenda kingine akashukuru Mungu kwa uamuzi wake wa kuchukua nguo za yule mlinzi wa Bob Chinanga. Hivyo akajihakikishia kuwa sasa anaweza kusonga bila kushtukiwa kirahisi.
Akaanza kuvuta hatua zake taratibu kuelekea mbele kule kwenye vyumba viwili mkabala kwa kila kimoja, mpaka alipowakaribia wale watu akaanza kukatiza katikati yao huku anapiga miluzi, ameweka viganja vya mkono mfukoni kuonyesha kujiamini.
Mbinu yake ikasaidia sana akakatisha bila kikwazo chochote. Alikuwa anasikia miungurumo ya mashine zinatoa mlio kiwandani huku masikio yametega kwa kusikiliza chochote kitakachotokea, alivyowapita tu akaanza kuongeza kasi ya mwendo wake.
Alipofika kwa mbele kidogo akaanza kukanyaga marumaru nzuri zilizosakafiwa kwenye korido yote iliyo nyembamba. Akazidi kusonga mbele kidogo kisha akapinda kulia akaanza kusikia sauti za vyombo vya muziki akafahamu kuna ukumbi wa disco maalumu kwa wafanyakazi wa kambi ya Gorongosa wapate sehemu ya kujiliwaza baada ya masaa ya kazi.
Akasogelea uelekeo wa ule ukumbi kisha alipoenda kushoto kidogo akaupa mgongo mlango wa kuingilia kwenye ukumbi akakuta kuna mlango wa lifti. Bila kupoteza muda akabonyeza kitufe kitakachompelekea roshani namba 03.
Ikaanza kuja ile lifti mpaka ikafika usawa wake ulivyojifungua mlango wa ile lifti kulikuwa na mtu ndani yake alivyomuona akajiskia kama mapigo ya moyo yanataka kusimama kwa muda kutokana na mshtuko alioupata. Miguu na mwili wake vinakosa ushirikiano msawazo wa kumuwezesha kutembea kuingia kwenye lifti.