RIWAYA: BANGUZI
NA: HASSAN O MAMBOSASA
______SEHEMU YA SABA______-
"Nilizoea ni tatizo lenye kuwakumba watu wanene tu ila nashangaa hata huyu, ila nasikia ukifanya mazoezi unaipunguza na kuwa ya kawaida"
"Ni kweli, ila kwa huyu ni hapana hatakiwi kufanya hivyo. Ndiyo maana siku ile aliyopelekwa Muhimbili alikuwa vile ingawa ni sehemu ya mazoezi", Mjomba alifafanua.
____________TIRIRIKA NAYO
Matabibu wawili, mmoja mwenye cheo ndani ya jeshi la ulinzi nchini. Mwingine akiwa nitumishi wa kawaida wa nchi pasipo kuwa na wadhifa mwingine wowote, walitosha kumfanya Heriety akose swali la kuuliza. Alirdhika nayo kutokana na taaluma ya watu hao wawili. Mjomba wa Jamal na pia Dokta Doreen, alisalia humo ndani kwa muda mfupi tu, akaaga na kuondoka ili aweze kurejea hosteli ambapo alihitaji haswa kuondoka na kurejea nyumbani.
Aliwaacha watatu tu ambao ni wenye kujua mengine zaidi. Muda wa kutoka kwake ndipo Mjomba akaeuza shingo kwa Jamal na kusema, "napendelea sana ufanye kile unachokitaka mjomba lakini inapofika muda ambao usalama wako ni wa muhimu. Basi walau ruhusu maamuzi yangu, walau unisikilize hata mimi".
Jamal aliposikia hayo alitabasamu kisha akasema, "Anko mimi nakusikiliza haswaa tatizo ni the way nataka mimi niishi. Wewe ni mkubwa kwangu, nitakusikiliza na pia sitoacha kukusikiliza. Nyumbani kule ninaishi na watu wa aina fulani, ila nikitoka na kuja shule huku ninakutana na wengine wa tofauti kabisa. Napenda nijue wengine wana experience gani kwenye maisha haya, thats all"
"Shehoza, huyu mpwa anko wako ana maisha ya maajabu sana. Maneno yake yamenvutia mno. Binadamu wa kipekee sana", Dokta Doreen alisema.
"Unajua Kapteni huyu mtoto muda mwingine najihisi hata nipo na mtu mzima mwezangu. Ni mwenye maneno na pia maamzi ya kipekee, ndiyo maana namchunga sana sitaki hata kumpoteza", Shehoza alisema kisha akamgeukia Jamal na kumwambia, "Jamal you are my everything anko, ndiyo maana nataka nihakikishe kuwa upo salama kila siku"
"Anko najua hilo ila napenda niwe na furaha, nadhani fuiraha yangu pia ni ya kwako. Staili yangu ndiyo inanifanya niwe na furaha, je hutaki kuona nikiwa hivyo?"
"Napenda mno, kwa hilo siwezi kukuzuia ila naomba uchunge haswa jicho langu lisije kuwa jekundu kwa ajili yako Jamal", Shehoza alisema.
"Hiyo hali ni haipepukiki anko, ila tusiende mbele sana. Najivunia sana uwepo wako".
_____________
SIKU KADHAA BAADAYE
__Uwanja wa Majani mapana, Tanga_
Ndege binafsi ya kukodi, ilidhihirika ikishuka kwa kasi kwenye njia ya kurukia za uwanja mdogo wa ndani. Hatimaye iligusa ardhi ya uwanja huo na kuanza kwenda mbio, mwishowe ilisimama eneo la maegesho. Haikuchukua muda mashine ilizimwa, halafu mlango ulifunguliwa. Alionekana kijana anayelekea utuzima akishuka, nyuma yake kukifuatiwa na kijana mdogo aliyependeza haswa akiwa amebeba mkoba mdogo mno huku machoni akiwa amevaa miwani ya giza.
Kitendo cha wao kukanyaga ardhi ya uwanja huo, walianza kujongea kuelekea eneo la kutokea nje. Ambapo kwa mbele yao alionekana kijana aliyevalia sare za wafanyakazi wa uwanjani hapo akisogea, huyu alimfikia mkadala kabisa mkubwa aliyeshuka mule ndegeni. Alimpa mkono huku akitabasamu, hatimaye wakasalimiana salamu ya vijana kuonesha hawakuwa wameuacha umri wa damujoto.
"Ismail ni adimu wewe kuonekana huku", Mwenye sare za uwanja huo alisema.
"Tony acha tu yaani kazi nyingi kupitiliza, yaani leo unavyoona nimeomba ruhusa mara moja nimlete mdogo wangu nyumbani kuna ishu ndogo ya kufanya", Mkubwa mwenyewe ambaye aliitwa Ismail, ndiyo alizungumza.
Hakukawia sana kubadilishana maneno na mtu hyo aliyeonesha wazi kujuana naye kabla, aliondoka na kutoka hadi nje ya uwanja huo. Hapo alikuta gari binafsi ikiwa inamsubiri, kutokeza kwao kwa nje. Alionekana Mzee wa makamo ambaye aliwasalimia kwa pamoja, kisha akawaongoza hadi ndani yake.
"Karibuni sana Tanga, mwongozo unaanza wapi Ismail?, Mzee aliwakaribisha kisha akauliza.
"Kwanza tupeleke kwa kliniki ya Mgiriki, halafu tukitoka hapo ni moja kwa moja nyumbani. Nina muda mrefu sijatia mguu huko", Ismail alieleza.
Safari ya kutoka mahali hapo ilichukua nafasi yake, waliondoka moja kwa moja hadi wakafika katikati ya jiji la Tanga. Walichukua uelekeo wa raskazone, huko walifika mahali husika. Baada ya kuvuka hospitali ya Bombo walisimama mahali ambapo kuna jengo la ghorofa moja, hapo Ismail na yule mdogo walishuka na kuingia ndani. Mzee alibaki kuwasubiri mahali hapo.
____________
Majira ambayo Ismail yupo jijini Tanga, upande wa Dar es salaam eneo lenye mabwawa ya kuogelea kadhaa. Kukiwa na vibanda kadhaa vya makuti huku ambavyo vilitamalaki idadi ya watu wakiwa na vinywaji wakifurahi. Ilidhihirisha ni eneo ambalo wengi hupenda kuja kufurahia, kwa jinsi walivyokuwa wakinywa na kuburudika huku wengine wakipiga mbizi kwenye maji yaliyopo hapo.
Upande wa ukingo wa sehemu moja ya kuogelea, mvulana na msichana ambao walikaa kimahaba huku miili yao ikichuruzika maji. Walidhihirika wakiongea kwa sauti ya chini tena kwa furaha, huku wakiegemeana kimzaha na kucheka.
Kila maneno yaliyokuwa yakitoka kinywani kwa mmojawapo ingawa hayakusikika, yalimfanya mwingine aachie tabasamu. Walifikia hatua ya kupigana mabusu mashavuni mwao, hii ikiendelea na ni wachache waliyowatzama ila asilimia kubwa ya wengi walikuwa wakiendelea na mambo yao.
Haikuwa jambo la jabu kuona wandani wapo namna hiyo, ila upendezwaji wao kuwa namna ile ulifanya wachache watamani kuwa mmojawapo pale. Iwe wa kiume alitamani walau kuwa na banati kama yule, wa kike naye hamu ya kukaa na kijana yule iliwajaa. Wachache waliyovutwa na mahaba hayo kutokana na utamani wa macho, ndiyo waliweka mawazo hayo.
Miongoni mwao hao, binti mmoja mwenye umbo matata akiwa amekaa na wadogo zake wawili. Naye alishikwa na hisi hizohizo, haswaa akitazama umbile maridadi la kijana yule aliyevaa kaptura fupi. Mwili wenye rangi mchanganyiko, pamoja na nywele ziso asili barani Afrika, huyu alijikuta akikaa kabisa kwenye ukingo ambao yupo mkabala na wandani wale wenye kujua kujiachia vilivyo. Mbele yake kukiwa na mabinti wadogo wakiwa wanaogelea, ambao hawakuwa na muda wa kumtazama jinsi alivyohamisha macho mahali kule ambapo kuna wa umri wake wakiendelea kufurahia.
Hata alipoitwa na wasichana wale waliyopo mbele wala hakuwa akisikia, alipokuja kuguswa ndipo akagutuka na kutambua ni mwenye kuhitajika na wasichana wale. Kitendo cha kutolewa ndani ya mawazo, kilipelekea aingiwe na mshtuko na kuwafanya wale wadogo watazame kule alipokuwa akiangalia. Walipokiona hiko, walijikuta wakicheka na kisha wakamtolea macho yeye, watoto hawa ingawa bado ni wadogo wa kustahiki kukaa na wazazi wao. Walishaanza kujua jema na baya, asali na tango na hata nyumba na chumba.
Hiyo haikuwa swala gumu kwao kuweza kumaizi binti yule alitekwa mno na wale waliyopo mbele yao, waliishia kucheka tu kwa jinsi alivyo. Hata mkubwa wao huyo aliingiwa na soni, kuona amebainiwa kuwa alipumbazwa na vipendezesha macho. Wasichana wale hata kile ambacho walitaka kumwambia, walighairi papo hapo. Wakajikuta wakirejea kuogelea, kitendo hicho kilimfanya banati yule awaone ni jipu karaha kwa kumvuruga mawazo yake.
"Mlikuwa mnaniitia nini?", Aliwauliza ila alipokea kicheko huku akiwashuhudia wakiendelea kuogelea kama kawaida.
Aliamua kuwapuuzia na kisha akarejesha macho kule walipo wandani, loh! Hakuwaona tena wakiwa namna ile, safari hii aliwashuhudia wakiwa wapo ndani ya maji kwenye ukingo wa mbali kutoka alipo. Hii ilimfanya alaani haswa, alikosa burudani ya kutosha kuweza kuwashuhudia wapenzi wale. Kuwaona wakiogelea kwake haikuwa kivutio tena, alihitaji haswa kuendelea kuufaidi ule ukaribu wao wa mwanzo lakini ndiyo hivyo mambo yalibadilika.
"Hawa watoto shenzi kabisa", Alijisemea kwa sauti ya chini akiwalaani wale waliyomshtua kutoka kwenye burudani ya kipekee.
Binti huyu mwenye kustahiki kuitwa mrembo, alijikuta akisimama juu na kudhihirisha umbile lake matata lenye unene ule uliyojijenga kiupekee. Kudhihirisha uundi wa Muweza kuweza kusani umbo hilo, vazi la kuogelea ndiyo kabisa likaendelea kuweka kila kitu wazi. Kiasi kwamba laiti kama angelikuwepo fukwe zile ambazo zimejaa waswahili kupitiliza, basi angelikuwa chakula cha jumuiya kwa kilazima kwa jinsi watu walivyochafukwa na akili wakiona miili ya namna hiyo.
Kukaa kwake wima, hakuchukua muda, alijitumbukiza ndani ya maji kwa mtindo maarufu kama 'kupiga mchomo'. Alianza kuyakata maji kwa ufundi kuelekea kule ambapo wadogo wale waliyomshtua wapo, wao walipomwona walibadili uelekeo huku wakiendelea kucheka. Kitendo hiko hakukifurahia ila aliamua kuacha tu lipite, maana hapo hakukuwa mahali stahiki kuzozana nao.
__________________
"Ismail huyu mdogo wako hali yake ni serius kabisa. Unatakiwa kuwa makini naye, kama ulivyoelezwa hapo awali kwa situation yake hakuna tiba tena. Bali kumchunga ndiyo kitu pekee kinachoweza kumfanya akaishi muda mrefu", Daktari mwenye asili ya kizungu alisema huku akiwatazama watu wawili wenye asili ya kiafrika.
"Kwahiyo Dokta hakuna njia nyingine zaidi, maana hili swala wewe ndiyo mtalamu pekee uliyobaki hapa nchini", Ismail alisema huku akimtazama kijana aliyepo pembeni yake kimasikitiko mno.
"Nafikiri umeweza kujua kwamba anasumbuliwa na mengi mno, hayo mengine hayatibiki na ndiyo yanapelekea tatizo hilo. Nitamwandikia dawa tu awe anazitumia kila siku ya maisha yake mara moja tu asubuhi, naamini hizi ndiyo zitaweza kumsaidia. Kuwa naye makini sana",
"Sawa Dokta hakuna shaka juu ya hilo", Ismail alijibu.
"Kimweri hakuna kiumbe awezaye kuishi bila changamoto katika maisha haya, unavyoona hapa kila mmoja anazo ila tu tunajitahidi kuzificha. Hali yako pia ione ni sehemu ya changamoto, huwezi jua Mungu amekupa nini mbeleni kuwa na jambo kama hilo. Kuwa imara na mchangamfu kama ulivyo hivi sasa, niliwahi kusikia uwepo wa kijana wa aina hii huko Muhimbili. Hajapona ila hadi sasa hivi yupo na anaendelea na kazi zake mjini, na ana familia" Dokta alieleza.
"Natambua hilo Dokta, hadi hivi sasa. Hili si kitu kwangu, ilimradi bado ninaendelea kupumua kama kawaida". Kimweri alijibu.
"Ninachoweza kukushauri hivi sasa ni uwe makini na masomo yako, mapenzi ya ujana ni hatari sana kwako. Kaa nayo mbali kabisa, uje kuchukua mwenza wa ukweli wa maisha yako"
"Sijawahi kufikiri kuhusu mapenzi na sitokuja kufikiria juu ya suala hilo, muda huu ambao ninahitaji nijijenge kimaisha"
"Vyema sana kijana, Ismail naamini wewe unaweza kumtunza na kumwepusha. Hii ni mboni yako ilinde isiingie pabaya. Niwatakie maisha mema"
"Tunashukuru Dokta", Walitoa shukrani wote kwa pamoja, haikuchukua mdua waliamua kuagana.
Ismail pamoja na mdogo wake kama alivyomtambulisha waliondoka mahali hapo, wakimwacha Dakari akiendelea na shughuli zingine. Wageni hawa walifika kumwona mbobezi huyu aliyelowea nchini Tanzania kwa muda mrefu, huo ukawa ni mwanzo wa mengine kwenye maisha yao wote watatu waliyokuwa hapo.
____________
_Siku mbili baadaye___
Mabadiliko ya hali ya hewa ya ghafla ambayo wala hayakutarajiwa na wakazi wa jijini Dar es salaam. Yalipekea kuanza kuongezeka kwa mji kwenye mito inayokatiza jijini, haikueleweka suala hilo lilitokana na nini katika kipindi ambacho hakikutegemewa kunyesha mvua kubwa. Wingu zito lilitanda majira hayo ya saa nne asubuhi, kufanya hali ilbadilike na kuonekana ni jioni kumbe ndiyo kwanza mwanzoni mwa siku mpya. Yakiendelea hayo maeneo ya barabara ya Morogoro ipitayo jirani na viwanja vya jangwani, watu waliichukulia hali hiyo ni ya kawaida.
Kuanza kuongezeka kwa maji kwenye mto Msimbazi, wao walipaona ni jambo la ada. Muda huo yakiendelea kujaa, walikuja kugutuka wakati ambao yameanza kufika kwenye kingo za mwisho za madaraja ya hapo. Kipindi ambacho kuna foleni kubwa iliyopo makutano ya 'Fire', ambayo yalitokana na kusimama Askari wa barabarani badala ya taa za kuongozea magari.
Muda huo wachache waliyokuwa na wasiwasi mkubwa walishaanza kupiga honi kwa nguvu mno kusihi huko mbele magari yaruhusiwe, Askari wa barabarani aliyejawa na kiburi wala hakuonekana kujali hilo. Aliendelea kuyaacha magari yakiwa namna hiyo, aliporuhusu pia hayakwenda yote isipokuwa ni machache tu na asilimia kubwa yakabaki. Wakiendelea kuhimmiza hivyo maji yalizidi kuingia darajani, awali yalipita kama mfejeji uliyoziba juu ya barabara. Lakini yalipozidi wingi ndipo walipozidi kiwango, magari yaliyopo karibu na madaraja yalianza kuyumbishwa. Yalipelekwa kushoto na kunapoelekea maji, gari dogo aina 'toyota saloon' iliyopo darajani ndiyo ilikumbwa na masaibu mazito.
Ilivutwa hadi ikafika kwenye kingo za machuma mafupi mno, muda huo hakuna ambaye alithubutu kusoge jirani na maji yenye nguvu. Waliishia kuona tu mikono ya mtu ikiwa inagonga kioo cha gari, kwa kushindwa kufungua upande huo mwingine kutokana na nguvu ya maji ilivyo. Gari ilipofika ukingoni mwa vyuma na kuzuiwa, bado hakuna ambaye aliyejaribu kusogea. Wingi wa maji ulipozidi kwa mara nyingine, walishuhudia ikianza kuinuliwa magurumu ya upande wa kulia taratibu. Likitokea hilo, raia walimshuhudia kijana mmoja akijitumbukiza kwenye maji kwa ghafla. Hapo ndipo wanadamu walibaki mdomo wazi, wakiwa wanaliwaza jambo lile haikupita muda kijana yule alirejea kwenye ukingo wa mkondo huo mkubwa wa maji ambapo umati wa watu upo.
"Nisaidieni chuma jamani haraka sana, kabla gari haijapinduliwa mtoni. Atakufa yule", Alihimiza.
"Wee kijana usijifanye unajua sana kuokoa watu utakufa", Mzee mmoja alipaza sauti na kupuuzia alichosema.
"We Mzee kwani utaishi milele ndani ya dunia hii, kila mtu kaandikiwa kifo chake na wewe huwezi jua utakuja namna gani. Labda hapo uliposimama ardhi itaporomoka na kuingia ndani, unategemea nani atakuwa msaada wako kama huhitaji kusaidia wengine", Kijana huyo alimpazia sauti huyo mzee, alipoona watu wamekaa kimya na hakuna anayetoa msaada aliamua kuokota kipande kigumu cha jiwe na kurejea tena majini.
*ISMAIL NA KIMWERI WADHIHIRIKA NDANI YA RIWAYA, WANA YAPI?
*BINTI AZAMA KWENYE PENZI LA KUTAZAMA, NINI KITAKACHOFUATA?
*KIJANA ANAJITOLEA AJITOLEA KUMSAIDIA ASIYEMJUA, NI NANI HUYU?
ITAENDELEA!!!