RIWAYA: Anga ya Washenzi na Gilbert Evarist Mushi

RIWAYA: Anga ya Washenzi na Gilbert Evarist Mushi

Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.

Msimu wa Kwanza.
Sehemu ya 08

Daniel kwa tahadhari kubwa aliinama kidogo na kuunyoosha mkono wake kuelekea katika kifua cha Ochewa Owechi ili kusikilizia mapigo ya moyo.
Lilikuwa ni kosa la mwaka kuupeleka mkono ule, Kwa kasi ya ajabu Ochewa aliuvaa mkono ule na kumvutia Daniel Mwaseba pale chini. Kabla Daniel Mwaseba hajatua chini, Ochewa alijinyanyua kwa kasi ileile na kujizungusha hadi nyuma ya mgongo wa Daniel. Kwa kasi ileile akamdaka Daniel aliyekuwa anaelekea chini kutokana na mvuto ule wenye kasi ya ajabu. Hakika Daniel Mwaseba hakutarajia tukio lile, lilikuwa ni tukio la ghafla sana ambalo hata Dokta Yusha pamoja na wale polisi watatu walipigwa na butwaa. Hadi wanatoa silaha zao na kuzielekeza kwa Jasusi yule tayari Daniel alishawekwa mbele kama kizingiti kiasi kwamba kama wangezifyatua risasi basi zingempata Daniel Mwaseba.
Amini usiamini Ochewa Owechi alishaipora bastola ya Daniel Mwaseba kitambo sana, ni wakati ule anauvuta mkono wa Daniel aliweza kuichomoa bastola hiyo iliyokuwa katika kiuno chake. Mkono wake mmoja ulioishika bastola ile aliuegesha katika mbavu za upande wa kushoto wa Daniel Mwaseba huku mkono mwingine ukiweka kituo katika shingo ya Daniel kiasi kwamba Daniel Mwaseba mwenyewe hakuwa na ujanja wowote ule wa kujitoa pale.

"Rudini nyuma taratibu mnipishe niondoke zangu ama niondoke na roho ya huyu mjinga wenu" Ochewa alivunja ukimya na kuzungumza kwa ujasiri mkubwa akiwa bado amejihifadhi nyuma ya mwili wa Daniel Mwaseba.

"Anafahamu kiswahili, ni Mkenya kabisa" Daniel Mwaseba alijisemea akiwa bado ametulia kimya.

Dokta Yusha na wenzake walibaki wameduwaa huku wakishikilia bastola zao mikononi, ni kama hawakusikia alichosema jasusi yule, walikuwa wakiwaza ni nini cha kufanya kwa wakati ule. Walitazamana kwa sekunde mbili, wakayarejesha macho yao kule kwa Daniel.

Daniel Mwaseba alikuwa ametulia kama vile alimwagiwa maji ya baridi, alikuwa akitafakari ni njia ipi ya kujitoa mbele ya adui aliyesimama nyuma yake. Aliiona njia moja tu, lakini njia hii kidogo ilikuwa na uhatari. Kidoleni alikuwa na pete ile yenye sumu, na angeweza kuifyatua sindano iliyojificha katika uso wa pete ile ili aweze kumchoma Ochewa na kujiokoa, lakini tatizo lilikuwa ni juu ya uhai wa Ochewa. Aliona kama angemchoma nayo tena kwa mara nyingine basi ni lazima sumu ile ingeutoa uhai wake safari hii, lakini bado alikuwa na haja ya kufahamu vingi zaidi kutoka kwa jasusi huyu, maswali mengi alikuwa akijiuliza, na wa kumjibu pekee aliona ni jasusi huyu. Hilo tu lilimfanya Daniel Mwaseba aendelee kutulia na kusuburi kosa lolote litendwe na jasusi huyu ili aweze kumtia nguvuni.

*****

Ndani ya viwanja vya Ushirika Moshi wananchi walianza kutawanyika baada ya msafara wa Rais Mark pamoja na viongozi wake kuondoka. Msanii wa bongo fleva aitwaye Young Chilwey alimaliza kutumbuiza kwa kuuinamia ukumbi, kukafwatiwa na makofi ya pongezi kwa baadhi ya watazamaji waliokuwa wamesalia uwanjani hapo. Chifu Abdallah Ntenga pamoja na Mkuu wa majeshi ya Tanzania, Jenerali Evance walikuwa wamesimama kwa pamoja wakijadiliana mambo kadhaa yaliyojitokeza katika ziara ile. Mbele yao waliwaona Elizabeth Neville pamoja na Gilbert Mwaitika wakija upande walipo, Chifu Abdallah na Jenerali wakayaelekeza macho yao kuwatazama kina Elizabeth wakija.

"Vipi Elizabeth Neville mmefikia wapi?" Chifu aliuliza huku akimtazama Elizabeth Neville machoni.

"Ni jambo la kushangaza sana Chifu. Tulipoipaisha helikopta yetu angani hatukuona hata kidogo dalili ya kuwepo kwa helikopta nyingine angani, ilitoweka ghafla. Tumezunguka karibu mji wote wa Moshi lakini hatujaiona kabisa, sio chini wala angani helikopta haijaonekana." Alisema Elizabeth Neville

" Hili ni jambo kubwa sana Neville, lazima tufahamu ni nini haswa kinaendelea kabla mambo hayajaharibika." Chifu alizungumza kwa hisia kubwa. Yeye kama mkuu wa kitengo cha idara ya usalama wa taifa aliiona hatari ikisogea karibu.

"Kwani si mmeshamtia mikononi David?" Jenerali Evance alivunja ukimya na kuuliza. Elizabeth Neville na Gilbert Mwaitika wakatazamana kwa sekunde mbili kisha wakayarejesha macho yao kwa Jenerali.

"Tangu tuwatume watu wa kwenda kumkamata hatujawasiliana nao bado Mheshimiwa" Gilbert Mwaitika alijibu huku akipiga saluti. Saluti hii ilikuwa ikimaanisha kuomba msamaha kwa walichokifanya. Kutokuwasiliana na wanajeshi wale aliowatuma kwenda kumchukua David na wenzake ilikuwa ni uzembe.

"Mapema hii mshaanza kufanya uzembe tutafika kweli? Wasilianeni nao sasa hivi tujue kazi kama tayari wamemtia nguvuni" Jenerali Evance alisema. Palepale Gilbert Mwaitika alikamata simu ya upepo na kutafuta mawasiliano na Salum

Zilipita kama dakika mbili hivi wakimsubiri Gilbert Mwaitika awape mrejesho baada ya kuwasiliana na Salum. Baada ya kuzungumza na Salum, Gilbert Mwaitika alimgeukia Jenerali Evance na kumpa ripoti

"Salum ameniambia wamemfikisha salama Njiro, wamemuweka sero wanatusubiri."

"Kazi nzuri. Uchunguzi wenu fanyeni kwa usiri mkubwa kabla Rais hajafahamu chochote kile, mkishakusanya taarifa za kutosheleza ndipo tutamweleza Mheshimiwa Rais tukio hili. Wasilianeni na Daniel ameelekea KCMC sasa hivi muweze kuungana. Kuanzia sasa kazi hii itakuwa chini yenu watatu. Wewe, Gilbert Mwaitika pamoja na Daniel Mwaseba" Chifu Abdallah Ntenga alimwambia Elizabeth Neville. Ni juu yenu kuangalia ni nani anafaa kuongeza nguvu kwenu ama mfanye kazi hii wenyewe.

"Hatutokuangusha Mkuu, tutapambana mchana na usiku hadi tufahamu yaliyositiriwa sirini" Elizabeth Neville alimjibu Chifu wake kwa kujiamini. Chifu akaachia tabasamu, aliwaamini sana vijana wake.

"Na Kazi iendelee" Jenerali Evance alisema. Palepale Elizabeth Neville pamoja na Gilbert Mwaitika waliongozana hadi kwenye gari yao aina ya Land Cruiser na safari ya kuelekea KCMC ikaanza.

Wakati huohuo Chifu Abdallah pamoja na Jenerali Evance walikuwa wakishauriana namna ya kumshirikisha mkuu wa Jeshi la polisi IGP Kilazi kuhusiana na tukio lililotokea. Walikubaliana wasubiri kwanza waone vijana wao wanaendelea vipi na misheni hii kwanza.

Gilbert Mwaitika alikuwa ni dereva ndani ya gari huku Elizabeth Neville akikalia siti ya pembeni ya kiti cha dereva. Elizabeth Neville alimpigia Daniel Mwaseba simu zaidi ya mara mbili lakini simu ile haikupokelewa. Alijaribu kutumia kile kisikilizio alichopachika sikioni lakini nacho hakikumwezesha kumpata Daniel Mwaseba. Mapigo yake ya moyo yalianza kwenda kwa kasi kidogo huku kijasho chembamba kikichomoza katika uso wa pua yake. Gilbert Mwaitika alikuwa akimtazama tu Elizabeth Neville kupitia kioo cha mbele, aliweza kugundua kwanini Elizabeth Neville yupo katika hali ile.

Daniel pamoja na Elizabeth walikuwa ni mume na mke wa ndoa kabisa. Hivyo haikuwa jambo la kushangaza kumwona mke akihofia usalama wa mumewe katika nyakati kama zile. Gilbert Mwaitika aliongeza kasi ya gari ili kuwahi KCMC.
ITAENDELEA

Una Tshs 1000 nikupe ofa ya wekend uisome Anga ya Washenzi? Lipia msimu wa pili ili upate msimu wa kwanza kama zawadi. Nambari ya Malipo ni M Pesa namba 0765824715
WhatsApp namba 0621249611
CapaEbook_464f34d3-74f5-47e7-902c-a4c278ee7a39.jpg
 
Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.

Msimu wa Kwanza.
Sehemu ya 09

Tulipoishia...
Daniel pamoja na Elizabeth walikuwa ni mume na mke wa ndoa kabisa. Hivyo haikuwa jambo la kushangaza kumwona mke akihofia usalama wa mumewe katika nyakati kama zile. Gilbert Mwaitika aliongeza kasi ya gari ili kuwahi KCMC.

Songa Nayo....
Baada ya dakika nne gari ya kina Elizabeth Neville ilikuwa ikiingia katika viwanja vya hospitali ya KCMC, Gilbert Mwaitika aliiegesha gari ile eneo maalum la maegesho ya magari, wakashuka kutoka garini na kuanza kupiga hatua kuelekea mapokezi. Walipofika tu mapokezi ilisikika sauti ya nesi mmoja pembeni ikiliita jina la Elizabeth, sauti hii ilimfanya Elizabeth Neville ageuke kutazama

"Elizabeth ni wewe kumbe! Kweli hutaki kumwacha kabisa mumeo, atakapoenda nawe humfuata. Uko poa lakini?"
Elizabeth Neville alimtazama nesi yule kwa sekunde kadhaa, ndipo akamkumbuka. Alikuwa ni rafiki yake.

"Aah Tina, kumbe ni wewe. Vipi za masiku? Kuna jambo tunalifwatilia huku ndio maana tupo hapa bwana, kwani Daniel yupo hapa?" Elizabeth akauliza kwa lengo la kupotezea ili isijulikane kama alikuja kwa nia ya kumfwata Daniel Mwaseba.

"Ndiyo, Daniel alifika hapa dakika kadhaa zilizopita. Bila shaka yupo kule kwa rafiki yake, si unajua tena yule rafiki yake alihamishiwa huku kutokea Hospitali ya Kilwa Kivinje?" Tina akasema

"Rafiki yake! Yupi huyo? Maana ana marafiki wengi kweli"

"Nawewe bwana, kwani kuna rafiki yake mwingine ambaye ni daktari zaidi ya Yusuph Shaweji?"

"Ohoo, kumbe ni Dokta Yusha, mambo mengi sana kichwani rafiki yangu. Ngoja tuelekee kwanza kufanya kilichotuleta kisha nitaelekea huko kuwasabahi" Elizabeth Neville alisema huku akijitahidi kuficha ili Tina asijue kama ni huko alipo Daniel ndipo anapohitaji kuelekea.

Elizabeth na Gilbert walitoka pale na kuelekea katika ofisi ya Dokta Yusha baada ya kuelekezwa ilipo na daktari mmoja aliyekuwa akikatiza karibu. Kwa msaada wa maelekezo yale walifika katika ofisi ya Dokta Yusha, lakini hawakumkuta humo, kwa kuwa Elizabeth Neville alikuwa na namba yake aliamua kumpigia, lakini kama ilivyokuwa kwa Daniel vivyohivyo simu ya Dokta Yusha iliita kisha kukata.

"Kwa nini hawapokei sumu yangu? Kuna nini kinawafanya hadi washindwe kupokea? Daniel Mwaseba kutokupokea simu yangu si jambo la kawaida, kuna kitu kimetokea bila shaka." Elizabeth Neville alikuwa akiwaza peke yake akizungusha macho huku na kule.
Walikubaliana wapande ngazi waelekew sakafu ta kwanza ya ghorofa. Mbele kidogo Elizabeth Neville alimwona daktari akipita baada ya kufika ghorofa ya kwanza, alimsimamisha na kumuulizia kama amemwona Yusuph Shaweji.

"Bila shaka atakuwa katika vyumba maalum, kuna mgonjwa wake huko anamshughulikia. Nendeni mkakae pale kwenye kile kiti mumngoje" Daktari yule aliwaeleza. Nao bila kusita wakaelekea pale walipoelekezwa, lakini daktari yule alipotokomea katika mboni za macho yao haraka walifuata njia ya kuelekea vyumba maalum vya kupumzisha wagonjwa. Gilbert Mwaitika alikuwa akigonga mlango mmoja mmoja katika vyumba vilivyokuwa upande wa kushoto, wakati huo Elizabeth Neville alikuwa akivifuata vyumba vya upande wake wa kulia. Lengo likiwa ni kumpata Daniel, simu yake kutokupokewa ilimpa shaka juu ya usalama wa Daniel ambaye alikuwa ni mume wake wa ndoa. Kila chumba walichokuwa wakikifungua waliambulia patupu ama kumkuta mgonjwa amelala kitandani

"Gilbert njoo uone," Elizabeth Neville aliita baada ya kufungua mlango wa chumba kimoja baada ya kuvipita vyumba kadhaa

"Ona Gilbert, bila shaka kulikuwa na purukushani hapa." Elizabeth Neville alisema huku akinyoosha mkono kuelekea katika kitanda kilicho pembezoni kidogo ya ukuta, juu ya kitanda kulikuwa na vipande vingi vya mashuka vilivyochanwa, pingu pamoja na kamba zilizofunguliwa. Pia sakafuni waliona michirizi ya damu pamoja na mpira wa kunyonya damu kutoka kwenye chupa kwenda kwenye mshipa wa damu. Gilbert Mwaitika alitazama mazingira ya chumba kile kwa sekunde kadhaa, akakizunguka kitanda kile taratibu huku mkono wake mmoja ukiwa karibu na kiuno chake, tayari kwa kuitoa bunduki yake pindi ikitokea hali ya utofauti, alifanikiwa kuona kamba iliyotengenezwa kwa vipande vya mashuka waliyoyaona juu ya kitanda, vipande hivyo viliunda kamba iliyofungwa katika mguu mmoja wa kitanda na kuelekea dirishani.
Gilbert Mwaitika akazipiga hatua zake taratibu kuelekea katika dirisha lile lililo wazi, kwa tahadhari akaichomoa na bastola yake kiunoni kwa lengo la kujihami kwa lolote.

"Nevi njoo uone, bila shaka yule ni Daniel, na yule ni Dokta Yusha pia. Daniel kama vile katekwa, tufanye kitu kumsaidia" Gilbert Mwaitika alisema huku akisisitiza asemacho akitoa ishara ya mkono kumwita Elizabeth.

Wote kwa pamoja walishuhudia mwanaume mmoja aliyesimama nyuma ya Daniel huku akimdhibiti kwa kumwekea bastola katika mbavu ya kulia, mbele yao walisimama kina Dokta Yusha na polisi wawili walioipeleka mikono yao juu ishara ya kujisalimisha. Mwanaume yule aliyemfanya Daniel kama kinga yake alikuwa akizipiga hatua taratibu huku akiwa bado amemshika Daniel. Dokta Yusha na polisi wale walikuwa kimya wakitazama huku silaha na simu zao zikionekana kuwa chini, ishara ya kwamba walilazimishwa kuziweka

"Tunaweza kumpiga kwa risasi halafu tukamuua ukute Daniel hataki afe, siamini kama pale wameshindwa kumuua, nahisi Daniel kuna jambo analiwaza. Hebu ngoja nishuke halafu niwasiliane nae kwa ishara, kisha nitakupa jibu huyu mtu auwawe au lah." Elizabeth Neville alimwambia Gilbert Mwaitika, palepale alitoka nje na kumwacha Gilbert ndani ya chumba kile.

Wakati huo Daniel Mwaseba alikuwa akifuata maelekezo ya Ochewa Owechi aliyejificha nyuma yake, walianza kuondoka eneo lile taratibu kuelekea mahali yanapopaki magari. Jasusi yule alimwamuru Daniel aongoze kuelekea ilipo pikipiki yake huku akimhakikishia ujanja wowote atakaoufanya basi angemchapa na risasi. Wakina Dokta Yusha na wale polisi wawili nao walibaki wamesimama kama sanamu. Silaha zao walizitupa chini hatua mbili kutoka waliposimama baada ya kushurutishwa na Ochewa.

Daniel Mwaseba alipokuwa akizidi kuzipiga hatua taratibu sambamba na jasusi yule, alifanikiwa kumwona Elizabeth Neville aliyekuwa amejificha nyuma ya mti mmoja mkubwa. Daniel aliyaona macho ya Elizabeth pamoja na mkono yakitoa ishara, yalikuwa yakuzungumza kwa ishara.

"Tumuue?" Ishara aliyoonyesha Elizabeth Neville ni kama iliuliza hivyo. Na Daniel aliielewa ishara ile, ilikuwa ni moja kati ya ishara zao za siri.

Daniel Mwaseba naye alijibu ishara ile kwa kukutumia macho yake, aliyapeleka kushoto kisha kulia kwa uharaka mkubwa. Alikuwa alimaanisha hapana mtu huyu asiuwawe. Naye Elizabeth Neville akaielewa ishara hii na kumpatia taarifa Gilbert Mwaitika kupitia kisikilizio alichopachika katika sikio lake la kushoto

"Daniel ana kazi naye, fanya juu chini asipoteze uhai. Ikiwezekana mjeruhi akose umakini ili Daniel amdhibiti" Gilbert Mwaitika alimsikia Elizabeth Neville kupitia kifaa alichoweka sikioni. Palepale aliingiza mkono wake wa kushoto mfukoni na kutoa kikopo kidogo cha plastiki, akakifungua kikopo kile ambacho ndani yake zilionekana sindano nyingi nyembamba mithili ya zile za kushonea nguo. Akachomoa sindano moja kisha kikopo kile akakirejesha katika mfuko wake. Sindano ile ilikuwa katika mkono wake wa kuume, akaihamishia katika mkono wake wa kushoto, akauingiza mkono wake wa kuume katika mfuko wa shati lake na kuitoa kalamu ya kuandikia.

Gilbert Mwaitika alikuwa ni mwanajeshi kutoka jeshi la Tanzania lililo chini ya Jenerali Evance. Gilbert Mwaitika alikuwa anafahamu ni aina gani ya silaha aitumie na katika muda gani. Kalamu ile haikuwa kalamu ya kawaida kama tunayoijua mimi na wewe, ilikuwa ni silaha tosha kwake. Sindano ile ilikuwa na ncha mbili tofauti, upande mmoja wa sindano ile ulikuwa na rangi ya Shaba, huku upande wa pili wa ncha ulitawaliwa na rangi ya kahawia. Upande wenye rangi ya shaba katika sindano ile ulikuwa ni upande wenye sumu aina ya Proxine, ilikuwa ni sumu kali sana, na upande wenye rangi ya kahawia ulikuwa ni upande wenye dawa aina ya MEZO. Dawa hii ilibeba mchanganyiko wa dawa mbili, yaani Melatonin na Zolpidem inayoweza kumfanya mtu akapata usingizi wa ghafla kwa muda uleule pindi anapochomwa.
Kwa kasi akaifungua kalamu ile ambayo kwa ndani kulikuwa na mrija mdogo wenye tundu la wastani, akaichukua sindano ile na kuiingiza ndani ya mrija kwa kuitanguliza ile ncha yenye rangi ya shaba. Baada ya hapo akairejesha kalamu ile kama ilivyokuwa awali.

"Elizabeth, huyu mtu nitamdunga na sindano ya usingizi. Nikisema 'Done' utapaswa kukimbia kumuwahi kwenda kuichomoa nyuma ya shingo yake maana sindano hii pia ina sumu na kama itadumu katika mwili wake kwa sekunde kumi inaweza kumuathiri." Gilbert Mwaitika alisikika akisema kusikia kifaa kile cha sikioni.

"Sasa wewe upo juu unamchomaje sindano?" Elizabeth Neville alinongona kwa sauti ya chini. Wakati huo Daniel na yule jasusi walikuwa wanaikaribia pikipiki aliyokuja nayo Daniel Mwaseba.

"Done" Gilbert Mwaitika alitamka, palepale kalamu ile ilikohoa na kuachia sindano iliyoenda kwa kasi na kuzama katika nyama ya shingo ya Ochewa Owechi upande wa nyuma.
Elizabeth Neville akatoka nyuma ya mti ule kwa kasi ya ajabu na kuelekea pale walipo kina Daniel. Lakini kwa upande wa Daniel alitahamaki baada ya kumwona Jasusi yule akilegeza mkono uliomkaba shingoni pamoja na mkono ulioishindilia bastola katika ubavu wake, ndipo akaamua kugeuza shingo yake nyuma ili kutazama kulikoni, akashangaa kumwona jasusi yule akienda chini taratibu akionekana kama kukosa fahamu. Hakujua kama Gilbert Mwaitika alishafanya yake, wala hakujua kama Elizabeth Neville alifika pale hospitalini akiwa sambamba na Gilbert.

Elizabeth Neville alipofika kwa kasi alimgeuza jasusi yule na kutazama shingoni, hakufanikiwa kuiona sindano ile zaidi ya tone la damu. Hapo akayakumbuka yale maneno ya Gilbert Mwaitika akimsihi awahi kuchomoa sindano ile angalau zisipite sekunde kumi maana inaweza kuleta athari

"Gilbert siioni sindano, naona tu tone la damu katika shingo yake," Elizabeth Neville alisema na kisikilizio alichokipachika sikioni.

"Mmmh! Unasema kweli?" Sauti ya Gilbert ikasikika ikijibu katika hali ya kutahamaki.

Nini kitatokea? Tukutane Jumatano kuumaliza Msimu wa Kwanza hapahapa Simulizi Za Gilbert . Ukiuhitaji msimu wa pili utapaswa kuchangia Tshs 1000 tu na utazawadiwa na msimu wa kwanza bure. Lipia Tshs 1000 kwenda M pesa namba 0765824715 kisha njoo whatsapp kwa namba 0621249611 nikutumie. Kama huna whatsapp nitext inbox hapahapa nitakupa maelekezo namna ya kuipata.
 
Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.

Msimu wa Kwanza.
Sehemu ya 10

"Gilbert siioni sindano, naona tu tone la damu katika shingo yake," Elizabeth Neville alisema na kisikilizio alichokiweka sikioni.

"Mmh!" alimsikia Gilbert Mwaitika akiachia mguno. "Chukua kisu haraka pekenyua hapo kuzunguka hiyo alama. Hiyo sindano imeingia ndani. Fanya haraka sana Elizabeth" Gilbert Mwaitika alisema katika hali ya kuharakisha
Gilbert Mwaitika alipotaja tu neno kisu tayari Elizabeth Neville alishakitoa kisu alichokuwa amekihifadhi ndani ya nywele zake alizozibana, kisu kile kilikuwa mfano wa kibanio cha nywele kwa macho ya kawaida lakini ukweli ni kwamba hakikuwa kibanio cha nywele tu, ilikuwa ni kama silaha pia. Elizabeth Neville aliipeleka ncha ya kisu kile hadi nyuma ya shingo ya jasusi yule na kuanza kupekenyua bila kuwa na huruma yoyote ile. Alipekenyua kikatili kuendana na muda.

"Mbona sikuelewi Elizabeth unafanya nini?" Daniel aliuliza huku akiitazama ile sehemu Elizabeth aliyokuwa anaipekenyua, hapohapo alimwona Elizabeth akiupeleka mkono wake na kuchomoa sindano nyembamba iliyotapakaa damu. Wakati huohuo Dokta Yusha pamoja na polisi wale walifika huku wakionekana kuhema kwa pupa kama watu waliokuwa kwenye riadha.

"Elizabeth sekunde kumi hizo zimekatika, hatunaye tena huyo mtu" Sauti ya Gilbert Mwaitika akisema ilisikika kupitia kisikilizio cha Elizabeth Neville,

"Nimeshamtoa, kila kitu kipo shwari sasa" Elizabeth Neville alisema. Dokta Yusha akamsogelea Daniel Mwaseba taratibu huku akimtazama.

"Daah, nisamehe sana Daniel, sikujua kama jamaa alikuwa anatutega muda ule. Kumbe ningemsogelea basi habari yangu wenda ingeisha leo" Dokta Yusha alisema huku akimtazama Daniel Mwaseba machoni, Daniel alimtazama tu na kuachia tabasamu. Gilbert Mwaitika naye alifika pale chini, baada ya kusalimiana na Daniel walianza kushauriana kwa pamoja.

"Joseph na John nyie mtakuwa nyuma yetu mkihakikisha hakuna gari inayotufwatilia, huyu mtu tunapaswa kumtoa hapa hospitalini muda huu kabla mambo hayajaharibika. haya tuondokeni haraka kabla hatujajaza watu hapa." Daniel aliwaambia polisi wale wawili baada ya majadiliano baina yake na kina Gilbert Mwaitika na Elizabeth Neville.

"Dokta utakuwa free tuongozane?" Daniel alimuuliza Dokta Yusha

"Daniel nyie nendeni tu tutawasiliana zaidi, mimi kutoka tena itakuwa ni ngumu kidogo maana kama sipo kuna pengo linaonekana katika idara ya upasuaji. Si una namba ya Dokta Kalita? Au kama vipi baadae maana leo jioni nitakuwa nyumbani" Dokta Yusha alimwambia Daniel

"Basi utanitumia namba yake maana niliipoteza," Daniel alisema huku akishirikiana na Gilbert Mwaitika kumnyanyua Ochewa Owechi pale chini,

"Tangulieni naye kwenye gari, kuna kitu nimekumbuka nakuja sasa hivi" Daniel alimwambia Gilbert Mwaitika huku akiliachia bega la Owechi baada ya kuhakikisha Gilbert amemshikilia vyema. Daniel aliongozana na Dokta Yusha hadi katika chumba kile alicholazwa Ochewa kabla hajafanya jaribio la kutoroka. Lengo la kurudia chumba kile ni kwenda kulichukua lile briefcase pamoja na koti la Ochewa. Dokta Yusha alimtolea vitu vile chini ya uvungu wa kitanda na kumkabidhi

"Hadi sasa najiuliza aliwezaje kuifungua pingu ile na kukata pia kamba ilihali tulimfunga miguu na mikono nakosa jibu Daniel" Dokta Yusha alisema baada ya kumpatia Daniel brufcase lile.

"Ochewa ni Jasusi, tena ni komandoo. Mtu kama huyu kutoka Nchini kenya na kuja Tanzania kwa lengo la kufanya shambulio lazima kuwe na watu nyuma yake, ataenda kusema kila kitu pindi tukifika. Tafadhali fanya siri hili jambo lisivuje, pia naamini lazima walio nyuma yake waanze kumsaka ili kumuokoa au kumuua, kuwa makini pia na hilo, wenda pia wakafika hapa. Kwaheri Dokta"
Daniel alisema, akatoka nje na kwenda kuungana na kina Gilbert ambao walishapanda kwenye gari kitambo. Ile Gari waliyokuja nayo Gilbert na Elizabeth Neville ilitumika kumhifadhia Jasusi yule ndani ya buti, Gilbert na Elizabeth wakakaa siti za nyuma huku Daniel akiwa ndiye Dereva wa gari ile. Gari ya pili waliyokuja nayo polisi wale wawili ilitumika kubebea pikipiki aliyokuja nayo Daniel, na polisi hao kwa pamoja walipanda gari ile, safari ya kuelekea walipopajua wao ikaanza

Zilipita dakika thelathini na mbili tangu wakina Daniel watoke hospitalini pale, polisi wale walielekea katika kituo chao cha kazi wakati kina Daniel walikuwa wakiingia maeneo ya Stesheni ya treni iliyopo Mjini Moshi, mkabala na stesheni hiyo kulikuwa na kiwanda kikubwa cha kahawa ambacho kilikuwa hakifanyi kazi za uzalishaji tena, jengo la ghorofa la kiwanda hicho lilikuwa ni chakavu sana likionesha kutotumika kwa miaka mingi. Wakina Daniel walifika hapo, walipofika tu Geti kubwa la kuingilia lilifunguliwa, mbele yao alisimama mwanamke mwembamba mweupe kiasi, mwanamke yule aliwatazama na kuachia tabasamu pana kisha kutoa ishara ya mkono kuwaruhusu waingie

"Mmh, ina maana Daniel ulishayaandaa mazingira hapa kitambo bila hata kutuambia? Ulifanya hivyo saa ngapi?" Elizabeth Neville aliuliza

"Baada ya kumbananisha jamaa kule ghorofani katika hoteli ya five star niliwasiliana na Cara pamoja na Songelael Ntenga, niliwaambia watafute chimbo ambalo tunaweza kuifanya kazi yetu bila kadhia yotote, waliona hapa panafaa." Daniel alisema

"Daniel kuna pikipiki inatufwatilia tangu tunatoka pale hospitalini, nilikuwa naitilia shaka lakini kadiri tulivyokuwa tukizidi kuja huku mashaka yalizidi kuongezeka. Nimejiridhisha ni kweli inatufwatilia" Gilbert Mwaitika aliingilia kati maongezi yale na kuelezea mashaka yake.

"Unazungumzia ile ambayo Dereva wake kavaa jaketi la rangi ya kijani?" Daniel aliuliza

"Yeah, kumbe na wewe ulishaiona kama mimi Daniel?" Gilbert Mwaitika akauliza na kuachia swali, Daniel Mwaseba alimgeukia na kutabasamu

"Umenishangaza sana kwa uwezo wako mkubwa, huyo ni Songelael Ntenga maarufu kama Mwanasheria Mlevi alikuwa anatulinda, nilimwambia atufwatilie kwa nyuma apeleleze kama kuna mtu anatufwatilia, pia nilimwambia atufwatilie bila kutoa mwanya wa kujionesha kama anatufwatilia kwa nyuma. Mwanasheria Mlevi ni afisa usalama kutoka idara yetu ya usalama wa taifa. Kama tu umeweza kubaini alikuwa anatufwatilia basi timu yetu hii itakuwa imekamilika. Upo makini sana Gilbert" Daniel alisema huku akitabasamu, wakati huo Mwanasheria Mlevi alishafika pale getini, wote kwa pamoja wakaingia ndani na geti likafungwa

"Usifungue, wacha mimi nifungue mwenyewe, wenda jamaa kashazinduka" Daniel alimzuia Mwanasheria Mlevi aliyekuwa anakaribia kufungua buti la gari kumtoa jasusi Ochewa Owechi.

Naam, Daniel akabofya batani mahususi iliyopo katika mlango wa buti na kufungua.
Looh!..
Teke zito la mguu wa Ochewa likakipangusa kidevu cha Daniel Mwaseba na kumfanya Daniel ayumbe kiasi na kuelekea chini bila kutarajia, lilikuwa ni teke zito lililopigwa kwa kasi pindi tu Daniel alipoufungua mlango wa buti. Daniel akiwa pale chini alianza kutema damu, na meno yake mawili ya mbele yalikuwa yamelegea, lakini hayakung'olewa. Daniel Mwaseba alinyanyuka kwa hasira, wakati huo Ochewa alisharuka na kutoka ndani ya buti.

Gilbert Mwaitika, Daniel Mwaseba mwenye hasira kuu kutokana na kujeruhiwa, pamoja na Mwanasheria Mlevi walimzunguka Ochewa Owechi kwa pamoja na kuanza kumsogelea.

Wakati huo Elizabeth Neville pamoja na Cara walishaingia ndani na hawakujua ni kipi kinaendelea huko nje.

"Ndugu yangu lala chini haraka na uelekeze mikono yako nyuma kabla hatujakuharibu sura" Mwanasheria Mlevi alisema kwa sauti ya kilevi, hakuwa amelewa lakini ongea yake ilikuwa ni kama mtu aliyekunywa pombe kupita kiasi. Ochewa alibaki amesimama, akavikunja viganja vya mikono yake tayari kwa kujitetea, kujitetea mbele ya anga tatu chafu zisizo na hata chembe ya huruma.
Naam, wote watatu kwa pamoja walimvamia Ochewa na kumshambulia kila mtu kwa staili yake. Daniel alikuwa akimshambulia kwa kumpiga ngumi za kwenye taya ili kulipa kwa kile alichofanyiwa muda mfupi uliopita. Alihakikisha Ochewa ametema angalau meno mawili ndipo hasira yake ikapungua.
Gilbert Mwaitika alikuwa akimpapasa Ochewa kwa kasi ya ajabu katika nyonga zake, yalikuwa ni mapigo ya aina yake yaliyomfanya jasusi yule kulegea kuanzia kiuno hadi miguu na kumfanya aelekee chini kukaa, lakini kabla hata ya kukaa Mwanasheria Mlevi kwa mwendo wa kilevi alikuwa akitumia miguu na mikono yake kumwinua, Ilikuwa pindi Ochewa anapokaribia kukaa chini basi anakutana na mguu imara wa Mwanasheria unaomzuia asiweze kuanguka, na hii ilimfanya aendelee kupigika. Ndani ya dakika mbili tu Ochewa alikuwa hatamaniki kabisa. Uso ulitapakaa damu huku akipoteza meno mawili ya mbele

************

Huu ni Mwisho wa Msimu wa Kwanza. Ahsante kwa kuwa nami kuanzia mwanzo hadi mwisho wa msimu huu wa kwanza. Ungana nami katika msimu ujao. Msimu wa pili utaanza rasmi Ijumaa jioni, Kama utauhitaji leo gharama yake ni Tshs 1000 tu inatosha kunisapoti kwa Bando[emoji4]. Lipa kwenda M pesa namba 0765824715 kisha njoo whatsapp kwa namba 0621249611
Like na sambaza kwa marafiki. Usisite kuwashirikisha kuhusu kufuata ukurasa wetu wa Simulizi Za Gilbert
 
Msimu wa Pili Wa Anga ya Washenzi unaanza rasmi episode ya kwanza [emoji116][emoji116]
 
Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.

Msimu wa Pili. Sehemu ya 01
Katika Hoteli ya Five Star, alipotiwa mbaroni Ochewa Owechi masaa machache yaliyopita na Daniel Mwaseba. Katika uwanja wa hoteli hiyo ilionekana gari aina ya Harrier Hybrid nyeusi ikipaki, walishuka wanaume watatu waliovalia suti za gharama sana. Wanaume wale walionekana kuelekea ndani ya hoteli huku simu mojawapo aliyoshika mwanaume aliyeonekana kama kiongozi ikiwaongoza kwa kutumia mfumo wa GPS. Walikuwa wakifuata uelekeo kama simu hiyo ilivyokuwa ikiwaongoza.
"Ni huku"
Mwanaume aliyeshika simu aliwaambia wenzake, wote kwa pamoja wakaelekea eneo la mapokezi katika hoteli ile. Walipofika mapokezi walikaribishwa kwa uchangamfu na muhudumu wa kike aliyeonekana kuijali kazi yake.
"Karibuni sana Five Star hotel" Sauti laini ya dada wa mapokezi ilisema

"Ahsante, Sisi ni wapelelezi kutoka idara ya Usalama wa Taifa," Mwanaume mmoja kati ya watatu wale alielezea huku akionyesha kitambulisho kilichoonyesha ni kweli ametokea Usalama wa taifa.

"Karibuni sana, naomba niwasiliane na meneja wetu ili aweze kufika hapa" Alisema mhudumu yule huku akichukua mkonga wa simu na kubofya nambari kadhaa. Muhudumu yule akaonekana kumweleza Bosi wake ambaye ni meneja wa hoteli hiyo.
Baada ya dakika moja Bosco ambaye ni meneja wa hoteli ya Five star aliwasili akitokea ofisini kwake, naye akaonyeshwa kitambulisho kinachowaonyesha ni ni maafisa kutoka idara ya usalama wa taifa. Napo kwa wakati huo Bosco akaanza kuelezewa kinagaubaka tukio halisi lililotendeka katika hoteli yao.

"Masaa machache yaliyopita kuna mwanaume alifika hapa kwa ajili ya kuchukua chumba, mwanaume huyo ni mgeni wetu kutoka Nchini Kenya, cha kushangaza tangu alipowasili hapa mawasiliano kati yetu na yeye yalikatika ghafla jambo ambalo linatuaminisha kwamba ametekwa na kuhifadhiwa sehemu fulani ndani ya hoteli hii" Mwanaume mmoja alianza kuelezea.

"Ni jambo la kushangaza kidogo maana siku ya leo hatujapata mgeni yeyote kabisa, mna uhakika ni hoteli hii lakini?" Meneja Bosco akauliza

"Sisi ni Wapelelezi kutoka idara ya usalama wa taifa, hivyo basi kitendo cha kuikanyaga ardhi ya hoteli hii maana yake ni kwamba tumejiridhisha ni hapa. Bwana huyo tulimwekea pia kifaa cha kumuonyesha popote pale alipo kwa ajili ya usalama wake zaidi maana alikuwa na maadui wengi, na hadi sasa anaonekana bado yupo humuhumu hotelini." Mwanaume wa pili alizungumza katika hali ya kuonyesha msisitizo na kuashiria anachosema ni kweli.

"Mnaweza kwenda kumchukua hivi sasa kama ni kweli, lakini mimi ninaamini hakuna mgeni aliyepokelewa leo katika hoteli yetu" Meneja alisema kwa kujiamini

"Yamkini kabla hata hajafika hapa kujiandikisha kwenye kitabu cha wageni alitekwa akiwa njiani, au labda baada ya kushuka kwenye gari yake. Lakini nakuhakikishia yupo hapa" Mwanaume aliyeshika simu mkononi alisema. Simu ilikuwa ikimwonyesha mtu waliyekuwa wakimfwatilia yupo karibu yao kabisa eneo hilohilo la hoteli.

"Tageti yetu inaonyesha kutulia eneo moja, hii inaonyesha wenda mtu huyo amefungwa au amelala" Mwanaume yule aliyeshika simu alikazia.
Wanaume wale watatu wakiambatana na meneja wa Five Star hotel walianza kumtafuta mtu aliyesemekana ametekwa ndani ya hoteli ile.

"Huku chini hayupo, location inaonyesha yupo juu, tuelekeeni sakafu ya juu ya ghorofa." Mshika simu aliwaambia wenzake wawili.
Hoteli ya Five star ilikuwa na jumla ya ghorofa nne tu, wanaume wale wakiongozana na Bosco walipanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza. Huko hawakuambulia chochote, wakapandisha tena juu hadi ghorofa ya pili, lakini walipotaka kupandisha tena ghorofa ya tatu, mmoja wao ambaye ndiye aliyeshika simu alisita. Aliitazama simu yake na kisha kuwatazama wenzake.
"Eneo hilihili" Aliyeshika simu alisema, ni baada ya kuona katika kioo cha simu yake alama inayowaongoza ikizidi kutanuka na kutoa ishara ya mawimbi kama mawimbi ya sauti.

"Nina uhakika hakuna mtu yeyote kwenye ghorofa hii ya pili. Vyumba vyote katika sakafu hii ya pili ya ghorofa vimefungwa kupisha ukarabati baada ya hitilafu ya umeme kutokea juma lililopita." Bosco ambaye ni meneja wa hoteli alisema huku akimtazama mwanaume aliyeshika simu. Hakuna aliyejali maneno yake, walikuwa wakizidi kusonga kadiri ishara inavyowaonyesha kupitia simu waliyokuwa nayo.

"Ni Hapa. Fungua mlango wa chumba hiki" Mshika simu aliamuru baada ya kukomea mbele ya mlango ulioandikwa 'CHUMBA CHA DHARURA'
Meneja alisogea hadi mbele na kuugusa mlango ule.
"Huu mlango haujawahi kufungwa tangu ukarabati uanze, mnaweza kuingia."Alisema Meneja baada ya kukinyonga kitasa cha mlango ule na kuufungua. Alianza kuingia mwanaume yule mshika simu, akafuatiwa na Meneja kisha mwanaume wa pili. Yule wa tatu alipoanza kuzipiga hatua zake kuingia ndani alisikia mjomgeo wa kitu ardini, ni baada ya yeye kuunyanyua mguu wa kushoto na kuusogeza mbele ndipo uliposikika mjongeo ule. Ilikuwa ni ile chipu Daniel Mwaseba aliyoiona baada ya kuvua buti la Ochewa Owechi. Kama utakumbuka vyema, Daniel Mwaseba aliitupa chipu hiyo wakati anashuka kwenye ngazi kutoka ghorofa ya tatu kuelekea ya pili. Na baada ya chipu hiyo kuachiwa katika mkono wa Daniel ilidondokea mbele ya mlango huo ambao wanaume hawa wameufikia.
Waliotangulia mbele nao waligeuka baada ya kusikia mjongeo ule ulioambatana na mkwaruzo mkali, wote kwa pamoja walitazama chipu ndogo iliyokuwa ikiwaongoza kumpata Ochewa Owechi.
Hawakuamini macho yao. Walidhani labda wangempata Ochewa lakini badala yake wanaiona chipu ile na si Ochewa Owechi.
Wote kwa pamoja walitazamana, hatimaye wakajifanya wakiendelea kumtafuta mtu wao ili kumpotezea Meneja aliyekuwa haelewi kinachoendelea. Yule mwanaume wa mwisho aliiokota chipu ile, huku wengine wakiendelea kufanya upekuzi ndani ya chumba lakini hawakuambulia chochote. Mwishowe walisogea pembeni kidogo kuzungumza

"Tumeambiwa tuende naye akiwa hai ama tuende na maiti yake, lakini tumekipata tu kifaa alichokuwa nacho. Tunafanyaje sasa?" Aliuliza mmoja kati ya wanaume wale

"Tusemeni tulichokiona, nadhani sote tumeona kabisa chipu tuliyompatia aiweke katika kiatu chake ipo hapa bila yeye. Tutoe taarifa nadhani tunaweza kuambiwa tufanye nini" Mwanaume wa pili alitoa wazo. Wote kwa pamoja wakamtazama mwanaume wa tatu, ni kama walikuwa wakisubiri naye atoe wazo lake.

"Kumbukeni Mkuu huwa hapendi majibu marahisi, msako ufanyike kwa kila chumba ndani ya hoteli hii, uwezo wa kuingia kila kona tunao maana wamekwishaamini kwamba sisi ni maofisa wa Polisi. Hapo tukimkosa tunaweza kupiga simu na kutoa maelezo" Alieleza yule mwanaume wa tatu, na huyo ndiye yule aliyekuwa ameshikilia simu iliyokuwa ikiwaongoza kumtafuta Ochewa. Wote kwa pamoja walikubaliana kufanya upekuzi kwanza ndani ya hoteli ile. Walimsogelea Meneja Bosco na kumweleza maamuzi yao. Kwa kuwa walikuwa na vitambulisho tena kutoka usalama wa taifa basi waliruhusiwa, walianza kumtafuta Ochewa kila pande bila kujua Ochewa yupo mikononi mwa Daniel Mwaseba.
*********
Majira ya saa 11 jioni kulikuwa na kikao kikifanyika ndani ya hoteli ya Red night mjini moshi. Kikao hicho kilijumuisha watu watano ambao ni Daniel Mwaseba, Gilbert Mwaitika wakiwa pamoja na Mkuu wa majeshi, Jenerali Evance, pia alikuwepo Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Chifu Abdallah Ntenga pamoja na Mkuu wa jeshi la polisi la Tanzania, IGP Kilazi. Kikao hichi kilifanyika kwa lengo la kujadili kile kilichotokea majira ya Saa nne asubuhi wakati Rais Mark akiendelea na ziara yake.
ITAENDELEA

Huu ni Msimu wa pili wa Anga ya Washenzi. Msimu wa pili unapatikana kwa Tshs 1000 tu. Kama umeshausoma msimu wa pili, wa tatu unakuhusu leo. Ni Tshs 1000 tu
 
Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.

Msimu wa Pili. Sehemu ya 02
Majira ya saa Tisa na nusu alasiri kulikuwa na kikao kikifanyika ndani ya hoteli ya Red night mjini moshi. Kikao hicho kilijumuisha watu watano ambao ni Daniel Mwaseba, Gilbert Mwaitika wakiwa pamoja na Mkuu wa majeshi, Jenerali Evance, pia alikuwepo Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Chifu Abdallah Ntenga pamoja na Mkuu wa jeshi la polisi la Tanzania, IGP Kilazi. Kikao hichi kilifanyika kwa lengo la kujadili kile kilichotokea majira ya Saa nne asubuhi wakati Rais Mark akiendelea na ziara yake.

"Kama nilivyowaeleza awali, IGP tumeona ni vyema tukushirikishe swala hili ili ukae ukijua kuna hali ya hatari. Hatujajua hadi sasa ni nani haswa alipaswa kuuwawa katika tukio lile, kwa kuwa tayari Daniel na wwnzake wameshawashikilia watuhumiwa basi tunaweza kujua chochote baada ya kuwafanyia mahojiano." Mkurugenzi wa usalama wa taifa alisema akiwatazama wenzake.

"Dah! Hii ni hatari sana. Umesema pia kulikuwa na helikopta yenye rangi ya jeshi ambayo hamkuwa mkiitambua?" IGP aliuliza

"Ni kweli. Tena cha ajabu sasa.... baada ya helikopta iliyopaswa kufanya ruti kurushwa angani, ile tusiyoitambua ikatoweka ghafla." Alieleza jenerali Evance.

"Elizabeth Neville alikuwa sahihi kumtilia shaka David. David anadai waliwekewa dawa ya usingizi ndani ya Helikopta wakasinzia. Cha kushangaza hadi hivi sasa wale wengine wawili hawajarejewa na fahamu lakini David alirejewa na fahamu mapema sana na anazo nguvu za kutosha tu. Kupitia yeye tunaweza kufahamu chochote chifu." Daniel alisema.

"Lakini pia huyo David awekewe ulinzi mkubwa maana waliyemtuma wanaweza kufanya lolote kwa wakati wowote. Daniel tupo pamoja nanyi, lolote mtakalolihitaji katika upelelezi wenu mtapatiwa, mnayo ruhusa ya kupita katika idara zote na wakati wowote ule ilimradi kufanikisha uchunguzi wenu. Hata yule mdunguaji akisema ametumwa na mimi njoo unikamate. Mnaweza kulitumia jeshi la polisi, jeshi la wananchi pia. Upo wewe, Gilbert Mwaitika kijana shupavu kabisa, Elizabeth Neville na Songelael Ntenga. Nyie mmepewa dhamana katika jambo hili. Ni maamuzi yenu muongeze vijana wengine katika timu yenu ama mfanye wenyewe. Uwezo mnao na nia mnayo". Chifu Abdallah Ntenga alimweleza Daniel Mwaseba kwa kirefu mbele ya meza ile iliyozungukwa na watu watano akiwemo yeye.

"Tutapambana bila kuchoka Chifu, nakuahidi mimi kama Daniel nitashirikiana vyema na wenzangu katika mazingira yoyote hadi tufahamu sababu ya yote haya na waliopo nyuma ya haya. Tunaomba pia ulinzi uongezwe kwa Rais kwani hatuwezi kujua adui yupo wapi." Daniel Mwaseba alisema kwa ujasiri mkubwa.

"Kuna Gabriel, Godwin na Deusderi. Nadhani unawafahamu vyema Daniel, wapo karibu kabisa na Mheshimiwa muda wote, hivyo ondoa shaka. Nyie hakikisheni mnafanya kila linalowezekana mfahamu ni nani aliyemtuma yule Jasusi kutoka nchini Kenya." Chifu akamwambia Daniel

"Sasa mnaweza kwenda Njiro alipopelekwa David. Hivyo mchukueni na mtajua mfanye nini kwa kuwa kwa sasa atakuwa chini yenu." Jenerali Evance akamalizia na kuhitimisha kikao kile.
Baada ya kutamatika kwa kikao, Daniel Mwaseba aliongozana na Gilbert Mwaitika kuelekea Njiro mahali walipopelekwa David na wanajeshi wenzake wawili waliokuwa wakishikiliwa kwa ajili ya kupisha upelelezi kutokana na lile sakata la helikopta ya jeshi. Gilbert Mwaitika pamoja na Daniel walikuwa wakielekea huko kwa lengo la kwenda kumchukua David ili waende wakamhoji mahali walipoweka kambi yao. Wakiwa njiani mara kadhaa Daniel Mwaseba angewasiliana na kina Elizabeth Neville kuuliza kama Ochewa alishazinduka kwani baada ya kipigo kile walichompatia alipoteza fahamu kabisa.
Lakini pia Daniel Mwaseba alikuwa akiugulia maumivu makali sana ya jino. Teke alilopigwa na Ochewa wakati ule lilimsababishia dhahma kubwa katika meno yake ya mbele. Meno haya yalilegea sana kiasi kwamba ilimpasa kuyatoa lakini hakuwa tayari kuwa na mapengo, tena mapengo ya mbele kabisa ambayo kila mtu angemwona. Alipanga kumtafuta Dokta Yusha baadae aangalia kama kuna dawa itakayoweza kuyaweka sawa meno yake.
**********

Makamu wa Rais, Mheshimiwa Eliud Sumbi alifikia hoteli ya KiliNight baada ya kutamatika kwa ziara ile. Yalishapita masaa matatu tangu ziara ile itamatike lakini hakupata mawasiliano na Ochewa tena. Hii ilimpa hofu kidogo kwani tangu atume ujumbe wa kumtaka Ochewa atoke eneo lile haraka baada ya kuhisi Daniel Mwaseba amegundua, alipateza kabisa mawasiliano naye. Lakini fikra za kuwaza kama Ochewa alikamatwa hazikuwepo kwani aliamini juu ya uwezo wake. Ni kweli Ochewa Owechi ana uwezo mkubwa sana, na ni moja kati ya majasusi hatari kutoka Kenya, lakini kitu ambacho Mheshimiwa Eliud alisahau ni kwamba uwepo wa mtu kama Daniel Mwaseba ni hatari kwa mpango wake kuliko hata uhatari wa Ochewa.
Mheshimiwa Eliud Sumbi akiwa kwenye kochi hakupata utulivu kabisa. Alijaribu kunywa maji lakini ilikuwa ni kama anameza mchanga. Alimwita mpambe wake aitwaye Elton Tonny.

"Hebu wasiliana na yule Mwanajeshi sasa hivi namhitaji hapa" Mheshimiwa Eliud Sumbi alisema baada ya Elton Tonny kuingia ndani ya chumba chake.

"Mheshimiwa tumejitahidi sana kumtafuta lakini naye hapatikani, pia wale watu watatu tuliowatuma kule Five Star hotel hawajafanikiwa kumpata Ochewa. Wameipata tu ile chipu tuliyomwekea kwa ajili ya kutrack uelekeo wake." Elton Tonny alisema. Mheshimiwa Eliud Sumbi sura yake ilibadilika baada ya kuyasikia maneno yale. Alitetemeka kwa ghadhabu kubwa. Alikumbuka majira ya mchana wakati ziara ya rais ikiendelea. Alimwona Daniel Mwaseba akionyesha kila dalili ya kugundua jambo, hii ni baada ya kumwona Daniel akitazama sana juu ya hoteli ya Five star wakati ziara ile ikiendelea.

"Naona sasa Daniel Mwaseba anazishika sharubu zangu. Ni yeye aliyeyafanya haya mwanaharamu mkubwa yule. Ametangaza vita na mimi huyu mtoto wa kahaba. Daniel atafutwe kila kona aletwe hapa, tena akiwa hai, nitafanya kila liwezekanalo na kwa mikono yake atamuuwa Waziri wa Ulinzi, na atamuuwa Rais Mark pia, na njia ya kwenda ikulu itakuwa nyeupe kwangu. Hiki ni kiapo changu kwa huyu mtoto wa kahaba." Mheshimiwa Eliud Sumbi alisema kwa jabza kuu.
Aliapa, akaapa tena, kutekeleza kiapo alichoapia.
Akisema hayo simu ya mpambe wake ilianza kuita. Elton Tonny alimtazama mheshimiwa Eliud kisha akaipokea simu ile na kuiweka sikioni. Aliisikiliza simu ile kwa sekunde kumi bila kuzungumza lolote kisha ikakatwa.

"David amekamatwa, tena anashikiliwa na jeshi la polisi kupisha uchunguzi juu ya lile swala mkuu.. " Elton Tonny alisema kwa woga. Alimwona mheshimiwa Eliud Sumbi akivuta pumzi kwa kasi. Mapigo ya moyo yalikuwa yakimpiga kwa kasi sana.

"Wapigie simu kina Henry na wenzake walioenda kumtafuta Ochewa, waambie wakamchukue David haraka sana kabla hajapata kuhojiwa. Watajitambulisha kama maofisa kutoka usalama wa taifa" Mheshimiwa Eliud Sumbi alisema. Palepale Elton Tonny alitoka nje na kuwapigia simu vijana watatu waliokuwa katika hoteli ya Five star.
********************

Daniel Mwaseba na Gilbert Mwaitika walikuwa wakiingia katika viunga vya jeshi huko Njiro. Walipofika katika lango kuu la kuingia ndani ya kambi walipishana na gari aina ya Harrier Hybrid nyeupe ikitoka. Pale getini waliwakuta wanajeshi watatu waliovalia sare za jeshi la wananchi wa Tanzania. Gilbert Mwaitika pamoja na Daniel Mwaseba walitoa vitambulisho vyao na baada ya ukaguzi pale getini waliruhusiwa kuingia ndani.

"Gilbert bila shaka wewe ni mwenyeji wangu eneo hili. Ni wakati wako sasa kuniongoza tuelekee kwa Kanali ili tukaeleze dhima yetu ya kutaka kuondoka na David" Daniel Mwaseba alimwambia Gilbert Mwaitika. Gilbert akatangulia mbele, kisha Daniel akafuatia nyuma kuelekea ofisi ya Kanali ili kueleza nia ya ujio wao.
Walipokelewa na Kanali wa jeshi Bwana Samson Mungiro, Baada ya ukaribisho walianza kueleza lengo la ujio wao. Walipewa kibali kutoka kwa Mkuu wa majeshi nchini, Jenerali Evance kuja kumchukua David. Majibu ya Kanali yaliwaacha mdomo wazi

"Umesema nini?" Daniel Mwaseba aliuliza kwa mshangao huku akimtazama bwana Samson Mungiro

"Hata dakika mbili hazijaisha, kuna maofisa watatu wameshamchukua kutoka idara yenu hiyo. Tulitaka kuwakatalia lakini baada ya kuangalia vitambulisho vyao tuliwapatia David na wameenda naye" Bwana Samson Mungiro alirudia kumweleza Daniel Mwaseba kwa sauti ya juu kidogo ili apate kusikia vyema.

Huu ni Msimu wa pili wa Anga ya Washenzi. Msimu huu unapatikana kwa Tshs 1000 tu, lipa kwenda M pesa namba 0765824715 kisha nitext whatsapp kwa namba 0621249611 nikutumie.
Msimu wa tatu pia upo Tayari. Wahi Tuwahi
Akili Media Storika na Gilbert #AngaYaWashenzi
 
Riwaya ya Kijasusi: Anga ya Washenzi
Mwandishi: Gilbert Evarist Mushi
Phone: +255765824715.

Msimu wa Pili.
Sehemu ya 03
Walipokelewa na Kanali wa jeshi Bwana Samson Mungiro, Baada ya ukaribisho walianza kueleza lengo la ujio wao. Walipewa kibali kutoka kwa Mkuu wa majeshi nchini, Jenerali Evance kuja kumchukua David. Majibu ya Kanali yaliwaacha mdomo wazi

"Umesema nini?" Daniel Mwaseba aliuliza kwa mshangao huku akimtazama bwana Samson Mungiro

"Hata dakika mbili hazijaisha, kuna maofisa watatu wameshamchukua kutoka idara yenu hiyo. Tulitaka kuwakatalia lakini baada ya kuangalia vitambulisho vyao tuliwapatia David na wameenda naye" Bwana Samson Mungiro alirudia kumweleza Daniel Mwaseba kwa sauti ya juu kidogo ili apate kusikia vyema.

"Maofisa kutoka usalama wa taifa!" Daniel alisema kwa mshangao huku akitafakari itakuwa ni maofisa gani hao.
"Vitambulisho vyao mmeviangalia vinasemaje?" Gilbert Mwaitika aliuliza

"Hebu nipatie kitambulisho chako" Kanali akamwambia Daniel. Daniel akakitoa kitambulisho chake kinachoonyesha yeye ni Askari mpelelezi kutoka idara ya usalama wa taifa.
"Tofauti kati ya hiki cha Daniel na chao ni vyeo tu. Hiki ni cha askari mpelelezi kutoka idara ya usalama wa taifa, lakini vyao vinaonyesha wao ni maofisa kutoka idara hiyohiyo." Kanali alijibu na kukirejesha kitambulisho cha Daniel

"Daniel itakuwa ni kina nani hao?" Gilbert Mwaitika alimtazama Daniel na kumkazia macho.

"Huku Moshi tulikuja na maofisa wanne tu kutoka idara yetu. Mmoja ni yule tuliyemwacha kule tulipoweka kambi yetu" Daniel alisema

"Unamaanisha yule mwenye sauti ya kilevi?" Gilbert Mwaitika aliuliza.

"Ndiyo Gilbert, ni yule Mwanasheria Mlevi. Jina lake halisi ni Songelael Ntenga. Wengine watatu waliambatana na msafara wa Rais kuelekea ikulu ndogo ya hapa Kilimanjaro kwa ajili ya mapumziko mafupi kabla ya kuelekea Arusha. Maofisa hao ni Gabriel, Deusderi na Godwin" Daniel Mwaseba alisema huku akijitahidi kuitoa simu yake iliyokuwa ikiita kwa kutoa mtetemo katika mfuko wake wa suruali.

"Subiri.... Nimekumbuka kitu ulivyotaja hayo majina, Vitambulusho vyao vilikuwa vikisomeka majina hayo hayo uliyoyataja." Bwana Samson Mungiro aliingilia kati na kusema.
Daniel alishtuka kusikia vile. Majina aliyoyataja yalikuwa ni ya maofisa wakubwa kutoka katika idara yao. Alijua kabisa ni ngumu kwa Maofisa wale kumwacha mheshimiwa Rais na kuja huku kumchukua David. Na kama wamekuja kumchukua David basi ni nani aliyewaambia kuhusu David? Yote haya yalipita kwenye kichwa cha Daniel. Alipoitazama simu yake aliona ni Chifu Abdallah Ntenga anampigia. Aliipokea na kuweka sikioni.

"Unasema wamekutwa wakiwa hawana fahamu! " Daniel aliropoka kwa nguvu akiwa haamini alichokisikia.

"Oooh My God. Hii inawezekanaje?" Daniel alikuwa bado haamini alichokisikia.
Taarifa aliyopewa na chifu Abdallah Ntenga ilikuwa ni nzito sana. Chifu Abdallah alimwambia kuhusu kupatikana kwa miili mitatu ya maofisa kutoka idara yao ikiwa haina fahamu huku vitambulisho vyao vikiwa havionekani. Ndipo Daniel Mwaseba akaanza kumuelezea Chifu Abdallah walichokutana nacho katika kambi ya jeshi. Chifu Abdallah naye alishangazwa sana na taarifa ile. Kila upande wa taarifa ulikuwa wa moto haswa.

"Omba msaada wa wanajeshi hapo muwafwatilie watu hao haraka sana. Wataeleza vitambulisho vya kina Gabriel wamevitoa wapi. Na pia David atakuwa anafahamu kitu ndio maana wamemchukua" Chifu Abdallah alimwambia Daniel na kisha kuikata simu yake.

"Inaonekana hawa waliokuja kumchukua David ndio haohao waliowazimisha na kuwaibia kina Gabriel vitambulisho vyao. Gabriel, Godwin na Deusderi walikuwa na uwezo mkubwa sana kimapigano. Si rahisi kuwazimisha kisha kuwaibia vitambulisho, Bila shaka watu hawa wanao uwezo mkubwa sana" Daniel alijisemea peke yake akimtazama Gilbert Mwaitika aliye pembeni yake.

"Hawa watu inabidi wadhibitiwe kabla hawajafika mbali, kwanza vitambulisho walivyonavyo si vyao, na wahusika wa vitambulisho hivyo wamekutwa hawana fahamu. Tunaomba mtupatie msaada wa wanajeshi wachache tukawakamate kabla hawajafika mbali." Daniel Mwaseba akasema na kumtazama Kanali Samson Mungiro baada ya kuirejesha simu yake mfukoni

"Hebu jaribu kuwasiliana na wanajeshi wanaoweka lindo kule lango kuu tujue kama hao watu wamepita dakika kama ngapi zilizopita" Gilbert Mwaitika alitoa wazo. Bwana Samson Mungiro akavuta mkonga wa simu na kutwanga mawasiliano. Baada ya kuuliza alimgeukia Gilbert Mwaitika na kusema..

"Ni kama bahati, Wanasema ile gari imekwama pale getini baada ya tairi yao moja kupata pancha, hivyo wanasubiri gari nyingine ije kuwachukua maana wameshapiga simu kuita msaada"

"Hiyo ndiyo nafasi yetu ya pekee tukaitumie kuwashika kabla gari wanayoisubiri haijafika." Daniel alisema "Pale lango kuu kuna wanajeshi wangapi?" Daniel Mwaseba aliachia swali kwa Kanali.

"Wapo watatu tu. Wanazo silaha za moto pia" Kanali akasema

"Hebu waambie wawazuie kwanza hadi tufike, wanaweza kukimbia kwa miguu kwenda kutafuta usafiri mwingine mbele." Daniel akasema tena.
Kanali akauvuta mkonga wa simu kwa mara nyingine tena. Lakini alipojaribu kupiga tena simu, iliita tu bila kupokelewa. Milango yake ya fahamu ikamcheza na kuihisi hatari.

"Hii si kawaida kutokupokea simu. Nendeni sasa hivi nadhani kuna jambo huko linaendelea" alisema Bwana Samson Mungiro.
Punde walipatiwa vijana watano walioshiba kwa mazoezi, wakaongozana nao kuelekea getini kuwawahi wamaume wale waliomchukua David. Walikuwa ndani ya Land Cruiser hardtop waliyopatiwa palepale jeshini huku mwanajeshi mmoja akikabidhiwa jukumu la kuongoza gari ile. Umbali wa kutoka makaoni hadi katika lango kuu la kuingilia ilikuwa ni takribani kilomita mbili tu. Gari ilitimka kwa kasi na walipomaliza kilomita moja na nusu waliliacha gari na kwenda kwa miguu ili kuondoa uwezekano wa kushtukiwa. Mikononi walibebelea silaha nzitonzito kwa ajili ya kukabiliana na adui pindi panapohitajika kutumia.
Hali ilikuwa ni tulivu sana, ni sauti za miti tu zilikuwa zikisikika kutokana na upepo unaovuma. Kila mtu alikuwa makini kwa kila hatua anayoipiga. Milango yao ya fahamu ilikuwa wazi ikifanya kazi kama mashine, kwa umakini mkubwa. Walikuwa ndio kwanza wanalisogelea lango kuu. Kwa mbali walifanikiwa kuona Harrier Hybrid nyeupe waliyopishana nayo wakati wakiingia. Lakini wanajeshi watatu waliokuwa na jukumu la kuangaza kila aingiaye na atokaye ndani ya kambi hii walikuwa wamelala chini kila mtu kwa sehemu yake. Daniel na wenzake waliongeza umakini zaidi baada ya kuliona lile. Kwa macho ya haraka haraka ukiwatazama wanajeshi wale hakukuwa na haja ya kuhitaji kuwakagua uweze kugundua kama wamekufa. Kwa namna walivyojilaza haikuwa rahisi kwa mwanadamu wa kawaida aliye hai kulala vile. Miili yao ilishatengana na roho zao dakika chache tu zilizopita kwani hata walipoigusa miili hiyo bado ilikuwa na joto la binadamu.

"Hawajafika mbali hawa, kwa namna yoyote watakuwa bado hawajapata usafiri wa kuwatoa eneo hili. Tujigawe hapa. wewe na wewe piteni upande huu, Gilbert utaambatana na huyu kule, mimi na huyu tutaelekea upande ule. Halafu huyu aliyebakia atatoa taarifa kwa Kanali kwa kile tulichokutana nacho. Na kazi ianze mara moja." Daniel alisema na palepale wakajigawa kuingia ndani ya miti mirefu inayoizunguka kambi.
Mwanajeshi mmoja kati ya wale watano walioambatana na kina Daniel alitoa taarifa kwa Kanali kwa kutumia ile simu iliyokuwa katika kibanda kilichokuwa pembeni ya lango kuu la kuingilia. Punde tu baada ya taarifa ile, Land Rover defender mbili zenye rangi ya kijani ya kupoza zilizowabeba wanajeshi na silaha zilikuwa zikielekea lango kuu kwa lengo moja tu. Kuwatia mikononi wanaume watatu waliomchukua David kwa kudai wao ni maafisa kutoka usalama wa taifa na kufanya pia mauaji ya wanajeshi watatu.

SURA YA TATU
Wanaume watatu waliopatiwa kazi ya kumtorosha David kutoka mikononi mwa kambi ya jeshi walikuwa wakizidi kuliacha eneo la jeshi. Tayari walishagundua mambo yameshaharibika, ni wakati ule wakingoja usafiri baada ya gari yao kupata pancha katika lango kuu la kuingia kambi ya jeshi ndipo walipobaini jambo hilo. Pale langoni walimwona mwanajeshi mmoja akizungumza na simu katika kibanda kilichopo mkabala na mahali gari yao ilipopatia pancha. Katika mazungumzo hayo walikariri sentensi moja iliyotamkwa na mwanajeshi yule.
"Wamekwama hapa langoni, gari yao imepata pancha hivyo wanasubiri gari ingine ije kuwachukua Mkuu"
Sentesi hii iliwaamsha vichwa vyao na kuanza kuitafakari. Kwanza iweje wauliziwe kama wameshapita? Hii iliwaaminisha wenda wameshabainika kuwa wao si maofisa kutoka usalama wa taifa. Hii ikawafanya kutazamana na kuamua kuwakatilia mbali wanajeshi wale. Hawakutumia risasi zao kutokana na kuhofia sauti, walikuwa na sindano zenye sumu kali ambazo walizitumia kuwarushia wanajeshi wale kwa pamoja na kuwamaliza. Hii ikawa ahueni kwao kutoroka na David eneo hili. Lakini bado waliamini wanajeshi wengine wangefika hivyo wakaona si vyema kunyooka na barabara. Walikuwa wakikimbia kwa kupita katikati ya msitu wenye miti mirefu iliyosongamana.

"Mkuu tupo kwenye hatari ya kukamatwa. Nasikia kwa mbali sauti za magari zikijongea, bila shaka wanatutafuta na hapa usafiri hatuna" Mmoja kati ya wanaume wale, aliyeonekana ndiye kiongozi alipiga simu na kuwasiliana na Mheshimiwa Eliud Sumbi ambaye ni makamu wa rais.
Alipatiwa maelekezo mafupi sana na kisha kukata simu ile. Aliyepiga simu anaitwa Henry, Na ndiye kiongozi wa wenzake. Yeye alikuwa ametangulia mbele kidogo na kuwaacha wenzake wawili pamoja na David hatua moja tu. Aliwasimamisha wenzake huku akiirejesha simu yake mfukoni na kuchomoa bastola yake ndogo.

"Mkuu amenipatia maelekezo ni kitu gani cha kufanya. Tunapaswa kuwa na maamuzi magumu mno ili tuweze kuondoka eneo hili tukiwa salama. Maamuzi hayo ni haya amesema,"

Ni Maamuzi gani hayo? Henry anataka kufanya nini? Je kina Daniel watafsnikiwa kumpata David?
Huu ni Msimu wa Pili. Hii ni Anga ya Manyambizi, Washenzi. Mwandishi wako ni Gilbert.
Msimu wa pili unapatikana kwa Tshs 1000 tu. Lipa kwenda M pesa namba 0765824715 kisha njoo whatsapp kwa namba 0621249611 nikutumie. Kama huna whatsapp nitext hata messenger hapa hapa fb nitakutumia. Kama umeshausoma msimu wa pili basi Msimu wa Tatu pia upo Tayari. Ni kwa Tshs 1000 tu. Wengine tutasubiri hapahapa, ila tutaenda taratibu.
 
Back
Top Bottom