Richmond + TANESCO: The complete deal

Watu wanauliza huyu Gire ni nani? Hebu cheki hapa kwenye mtandao wa RDC: http://www.rdevco.com/principals.html

----
Nina swali, hivi huyu Julius Sarota kwenye huu mkataba ni nani huyu? Unajua nahangaika na mawazo, isijekuwa ndiyo yule jamaa aliyehawi kuchemsha vibaya vidato vya juu Mzumbe Sekondari miaka kadhaa iliyopita. Kama ndiye, kafikaje hapa?

I bet ndiye...

Gire ninayemfahamu mie na hizi sifa nakuwa mgumu kuamini. Itanibidi nifanye uhakiki kwanza kabla sijamshusha ama kumkweza.

Thanks for the link NajiVunia
 
Hmm! Nimecheki website ya Richmond, na najiuliza, is there a way to follw up hizi projects? Another thing nimeona documentary about Enron na nimekumbuka na wao walikuwa 'big wigs of the energy industry'. Is this another sham? But I don't have any evidence to support this. What do you know about RDC?
 
Check this topic before you proceed with discussions in this thread:

Nilikuwa naungojea huu mkataba utoke ili nimalizie puzzle yangu, i final conclude Richmond get the deal.
Ukiangalia kwenye post yangu moja ya nyuma i explained kwamba JK alijua kabisa hii deal ya Richmond tangu summit ya UN mwaka jana.
wamarekani weusi wanasema :"oooohhh boy they cooking with alot of greece"
 
I know Mohamed, he never participate in energy business before. He moved to Houston in late 70's, he is a successful business man in Houston area ( a millionaire), he is very close to mayor Bill White.
Mohamed went to school with one of those members who sign that contract, also we know to this point that Mr. Gire get in touch with JK through in law of one of the members, this happened last year in NY. This in law and Kikwete are buddies from Bagamoyo. again i was wait for this mkataba kuvuja so i can connect my dots.
 
Kama kawaida ya serikali iliyosinzia karibu mwaka mmoja na nusu baadaye, leo mkataba wa Richmond unatarajiwa kujadiliwa Bungeni. Kakasi ya CCM walikuwa wamekutana jana na inaonekana baada ya kusafishwa na TAKUKURU sasa wako tayari kuzungumzia suala Richmond. Wakati huo huo habari zimenifikia kuwa ripoti ya Ukaguzi wa Benki Kuu kwa mwaka 2005/2006 imepelekwa Bungeni kinyemela bila kufuata taratibu za sheria ya Benki Kuu. Ripoti hiyo ambayo ina mapungufu mengi inashangaza imewezaje kupelekwa kwa wabunge kiujanja wakitumia njia za kijanja ili isiweze kujadiliwa.... still monitoring...
 
wewe umeonekana unakubaliana nao,sasa leo swali hili umelitoa wapi?
 
Sasa hapa nani alisema Tanzania kuna Democracy? Sasa hapa hivi CCM wanaongoza nchi kwa kuwatumikia waliowapa dhamana au wanaongoza kwa kufuata maslahi ya Chama? Na kama hili suala halitajadiliwa Bungeni kwa mapana na Marefu basi wananchi tuna haja ya kukaaa chini kuangalia ni njia gani ambayo tunaweza kuitumia kuwaonyesha hawa watu thamani ya kura zetu by any cost.

Pia naangalia kwa makini vipengele vya katiba kuhusu kama tunaweza kupata mwanya kwenye katiba yetu ya kupiga kura za kutokua na imani na Bunge letu.

Kwani sisi wananchi kama haturidhishwi na mwenendo wa wale tuliowachagua ndani ya huu muda wa miaka mitano kabla hatujasubiria kuwatoa kwa kura kwenye election hapa katikati ni kitu gani tunaweza kufanya kujinusuru?

Kwa nini tusianzishe kampeni KABAMBE ya kupiga kura ya kutokua na imani? Hebu tusubiri tuone hoja zitakavyozimwa leo ila Jamani sijui nitaweza vipi kudaka mjadala moja kwa moja through net.

We need radical changes,niko tayari kwa hilo.Hatuwezi kuishi kwa umaskini namna hii huku watu wachache wakileta mzaha na raslimali zetu.Wahadzabe kule wanakufa njaa halafu mtu mzima aliyesoma chuo kikuu anavaa suti bungeni na makaratasi yake akigani mashairi eti,TANZANIA INAPAA,inapaa in terms of what?

Leo hii akina mama wanakufa mahospitalini,watoto yatima wanageuka kuwa ombaomba mtaani wakiishi kama viumbe visivyostahili kuzaliwa hapa duniani,watoto wa maskini wanasoma kwa taabu vyuo vikuu bila mikopo huku sisi tukichezea hela kwa interest za wachache huku nchi jirani kama Kenya kwa Mujibu wa report ya NEPAD juzi ikiwa Ya tatu kwa nchi za Afrika zenye uchumi mkubwa zaidi nyuma ya SA, na Nigeria.Hapa kwetu tuliowachagua wanagani mashairi.

Sasa ngoja tuone huu moto utaishia wapi potelea mbali

Mungu tusaidia kwa hili hii vita tutashinda tu.
 
hii inaweza kuwa na marekebisho machache ikiwamo lile la kuohakikisha KAMATI TEULE INAUNDWA.

TAARIFA YA KAMATI YA UWEKEZAJI NA BIASHARA KUHUSU UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA
KAMATI KWA MWAKA 2006

1.0 UTANGULIZI

1.1 Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 88 (11) ya Kanuni za Bunge Toleo la 2004, naomba kwa niaba ya Wajumbe wenzangu wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara nitoe taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Kamati kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

1.2 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii ni Taarifa ya kwanza ya mwaka mzima ya Kamati ya Uwekezaji na Biashara, nawajibika kunukuu majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Kanuni ya 95 (1) na (2) ya Kanuni za Bunge Toleo la 2004.

1.3 Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni hiyo, Kamati ya Uwekezaji na Biashara inasimamia shughuli za Wizara mbili nazo ni:
• Nishati na Madini;
• Viwanda, Biashara na Masoko.

1.4 Mheshimiwa Spika, majukumu ya Kamati katika Wizara hizo ni:-
(i) Kushughulikia Bajeti za Wizara hizo;
(ii) Kushughulikia Miswada ya Sheria na Mikataba inayopendekezwa kuridhiwa na Bunge ambayo chanzo chake ni Wizara hizo;
(iii) Kushughulikia taarifa za kila mwaka za utendaji na Hesabu zilizokaguliwa za Mashirika ya Umma yaliyo chini ya Wizara hizo;
(iv) Kufuatilia utekelezaji unaofanywa na Wizara hizo kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (b) ya Katiba. Ibara hiyo inatamka kwamba (nanukuu):

"Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii" mwisho wa kunukuu.

1.5 Mheshimiwa Spika, Kamati ya Uwekezaji na Biashara imetekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali kama ifuatavyo:-
(i) Kamati imeshirikiana na Wizara zote kuelewa maeneo yote ya utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, Kamati imepata fursa ya kushiriki katika semina na Mikutano ya kuelimisha juu ya majukumu ya Wizara hizo na vyombo chini yao;

(ii) Kamati imeshiriki katika mchakato wa Bajeti za Wizara hizo za mwaka wa fedha wa 2006/07;

(iii) Kamati imepata fursa ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mashirika chini ya Wizara hizo na pia makampuni binafsi katika sekta za Nishati, Madini, Viwanda, Biashara na Masoko;

(iv) Vilevile, Kamati imepata wasaa wa kushiriki katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa katika Uwanja wa Maonyesho ya Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere mwezi Julai, 2006;

(v) Kamati pia imepata nafasi kwa baadhi ya Wajumbe wake kushiriki katika ziara za mafunzo nje ya nchi, chini ya Wizara zinazosimamiwa na Kamati hii;

(vi) Fursa pia imetolewa na Wizara zote kwa baadhi ya Wajumbe wa Kamati hii kushiriki katika semina zinazohusu Wizara hizo ndani ya nchi; na

(vii) Kamati vilevile imeshiriki katika mchakato wa kupitia Miswada ya Sheria za Wizara hizo.

1.6 Mheshimiwa Spika, kuhusu eneo la jukumu la uwekezaji kwa ujumla, hapa tunapenda kueleza kuwa uwekezaji mkubwa nchini ambao unalenga kwenye uzalishaji bidhaa moja kwa moja uko katika maeneo ya madini, nishati na viwanda. Kwa hiyo, Kamati ilipata nafasi ya kutembelea maeneo yenye uwekezaji mkubwa au yanayoandaliwa kwa ajili ya uwekezaji kama vile maeneo ya miradi ya gesi asilia, maeneo ya makaa ya mawe na chuma, maeneo ya madini ya Tanzanite n.k.

1.7 Kamati vilevile imepata nafasi ya kutembelea Mashirika ya Umma yaliyo binafsishwa na pia yale yanayoandaliwa kubinafsishwa kuona jinsi mikataba inavyotekelezwa na hali ya utekelezaji wa shughuli za Mashirika hayo.

1.8 Aidha, Kamati imepata nafasi ya kutembelea wawekezaji wadogo wadogo Wazalendo katika maeneo ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite (Mererani), uchimbaji wa chumvi (Lindi) n.k.

1.9 Kamati pia imepata nafasi ya kukutana na wawekezaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi hasa katika sekta za madini na nishati na kupata maelezo ya nia yao za kuwekeza hapa nchini, mfano kwenye gesi asilia, makaa ya mawe na chuma, nishati ya kupikia kwa makaa ya mawe, nishati ya upepo (wind energy) n.k.

2.0 MAENEO YALIYOSHUGHULIKIWA NA YALIYOJITOKEZA

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na Wizara pamoja na Taasisi, Mashirika na Asasi mbalimbali (Tazama Kiambatisho Na. 2), Kamati imeweza kutekeleza majukumu hayo kwa kutoa maoni na ushauri katika sekta zake kama inavyoelezwa katika aya zifuatazo.

3.0 SEKTA YA NISHATI
Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua kwamba sekta ya nishati ni moja ya sekta muhimu muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu kwa kuwa utekelezaji wa shughuli nyingi unategemea sekta hii. Kwa mantiki hiyo, Kamati mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali yanayojihusisha na sekta hii, imeweza kutoa maoni na ushauri utakaoweza kuboresha sekta hii kama ifuatavyo:-

3.1 SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO)
(i) Mheshimiwa Spika, Kamati imefarijika na hatua za dharura ambazo Serikali ilichukua nusu ya pili ya mwaka 2006 ili kuepusha nchi isikumbwe na janga la kukosa nishati ya umeme. Aidha, TANESCO iliingia mikataba na wawekezaji binafsi wa nje kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kutumia gesi asilia na dizeli.

(ii) Mheshimiwa Spika, Kamati pia imeridhishwa na utendaji wa baadhi ya makampuni yaliyoitikia wito wa Serikali kwa haraka kama vile kampuni ya kuzalisha umeme ya Aggreko, ambayo ilianza uzalishaji umeme wa dharura bila kuchelewa, hivyo kusaidia mapema kuondoa kero na wasiwasi mkubwa uliozikumba sekta za viwanda, biashara na utoaji huduma nchini.

(iii) Mheshimiwa Spika, baada ya kufuatilia taarifa za Serikali na za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Kamati haikuridhishwa na utendaji kazi wa Kampuni ya Richmond Development Corporation ya Marekani na mrithi wake Dowans Holdings S.A. ya Falme za Nchi za Kiarabu (UAE) kwa kushindwa kukamilisha mradi wa umeme wa dharura katika muda muafaka,
yaani ndani ya kipindi ambacho nchi ilikuwa inakabiliwa na tatizo la upungufu wa umeme. Kwa mujibu wa taarifa za Kamapuni ya DOWANS, ufungaji wa mitambo ya kuzalisha na kuingiza umeme wa megawati 100 kwenye gridi ya Taifa ulitegemewa kukamilika mwezi Juni, 2007, badala ya mwezi Februari kama iliyosainiwa kwenye mkataba, miezi kadhaa baada ya hali ya dharura kumalizika.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa tunapowasilisha taarifa hii DOWANS wamekamilisha kazi hiyo. Kwa mujibu wa Mkataba DOWANS walitakiwa kuilipa TANESCO kiasi cha Dola za Marekani 10,000 kwa siku kutokana na uchelewashaji wa ufungaji wa mitambo ya umeme wa dharura. Kamati ingependa kufahamu ni kiasi gani cha fedha ambacho TANESCO imelipwa na DOWANS mpaka sasa kwa mujibu wa mkataba.

(iv) Mheshimiwa Spika, utendaji kazi usioridhisha wa Richmond na ushahidi bayana uliojitokeza polepole wa kampuni hiyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kifedha na kukosa kabisa uzoefu katika miradi ya umeme, umezua maswali mengi miongoni mwa wananchi kuhusu umakini uliotumika katika kuiteua kampuni hiyo kutekeleza mradi nyeti kitaifa wa aina hiyo na wenye gharama kubwa (Sh. Billioni 172.9) .

(v) Mheshimiwa Spika, viwingu vya mashaka vilivyotanda juu ya suala hili haviwezi kuondoka kwa kuvifumbia macho au kwa kuvipuuzia bali kwa kuvifanyiakazi kwa uwazi na ukweli ili kukidhi matakwa ya demokrasia na utawala bora. Kamati imefarijika na hatua ambazo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imechukua za kuchunguza uwepo wa rushwa katika zoezi zima lililopelekea Richmond kuteuliwa. Pamoja na mchango huo wa TAKUKURU unaoliangalia suala hili kijinai, bado yako maswali ya msingi (nje ya sheria ya jinai) yanayohusu miiko, maadili na taratibu za kazi za Serikali, uadilifu, umakini na uwajibikaji katika utendaji kazi, ambayo hayakuangaliwa na yanadai majibu ya uhakika:

a) Je, ni sababu zipi za msingi zilizopelekea Serikali kuacha kuifanyia uchunguzi wa awali (due diligence) kampuni hiyo ya Richmond (tofauti na kampuni nyingine zilizoshiriki kwenye zabuni hiyo) ili kujua uwezo wa kampuni hiyo kifedha, kitaalamu na kiutendaji?

b) Njia mojawapo ya haraka ya kujua umakini na uhodari wa kampuni yoyote ile, ni kukagua tovuti yake. Je, Serikali ilipata fursa ya kuikagua kwa dhati tovuti ya kampuni hiyo? (http://www.rdevco.com/economy.html)

c) Serikali ilikuwa na taarifa za kutosha kuhusu uwezo duni kiutendaji wa Richmond hasa baada ya kampuni hiyo kushindwa, bila sababu za msingi, kutekeleza mradi wa bomba la mafuta (kutoka Dar-es-Salaam hadi Mwanza) mwaka 2005 kinyume cha makubaliano (Memorundum of Understanding) kati ya Serikali na kampuni hiyo. Je, ni sababu zipi za msingi zilizoisukuma Serikali kuufumbia macho udhaifu wa Richmond uliojidhihirisha kwenye mradi mwingine mkubwa wa kitaifa, yaani mradi wa bomba la mafuta?

d) Taarifa za awali za Serikali zimeeleza kuwa madai ya Richmond kuwa na uhusiano wa karibu na kampuni yenye jina kubwa duniani ya Pratt & Whitney, ndiyo yaliyoishawishi Serikali kuipa Richmond ushindi kwenye zabuni hiyo. Je, Serikali ilipewa ushahidi wowote wa kimaandishi kuhusu uhusiano wa kisheria wa kampuni hizo mbili? Je, kwa nini basi mkataba wa mwisho wa kuzalisha umeme wa dharura nchini, haukuitaja wala kuihusisha kwa namna yoyote ile kampuni ya Pratt & Whitney?

e) Serikali ilitaka kampuni yenye uwezo wa kuingiza nchini mitambo ya umeme wa dharura kwa kutumia gesi kwa kipindi maalum cha mwaka mmoja hadi miwili. Je, ni sababu zipi zilizoifanya Serikali iruhusu kufunguliwa LC ya uingizaji wa mitambo ya kampuni ya Richmond?

f) Ni kiasi gani cha hasara nchi imepata kwa mradi huu kutokamilika ndani ya muda wa dharura ya umeme?

(vi) Mheshimiwa Spika, maswali haya hayana budi kupatiwa majibu ya uhakika ili wananchi waridhike. Kutokana na ugumu uliojitokeza awali wa kupata mkataba kati ya serikali na Richmond Kamati kwa kutumia Kanuni ya 104 na 105 ya Kanuni za Bunge Toleo la 2004 ilipendekeza Bunge liunde Kamati Teule itakayokuwa na uwezo kisheria kuupitia mkataba huo na kuchunguza mchakato mzima uliopelekea kampuni hiyo ya Richmond kuteuliwa. Kamati mkatika kutekeleza kazi hii itatumia vigezo vipana zaidi kuliko kuliko vile vya makosa ya kijinai vilivyotumiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

(vii) Mheshimiwa Spika, Kamati inaona umuhimu wa kuwepo taarifa bayana kuhusu mchakato mzima wa kumpata mzabuni zikihusisha specification, thamani, uwezo na uzoefu wa mzabuni husika.

3.2 MPANGO KABAMBE WA UMEME
(i) Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kuwa tatizo la umeme limekuwa sugu na linaathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini. Kamati inashauri Serikali iandae mpango madhubuti wa muda wa kati na muda mrefu (Power System Master Plan) ukionyesha ni namna gani nchi itakabiliana na tatizo hili la mfumo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa umeme. Hii itaipunguzia Serikali gharama ya kuingia mikataba ya dharura kwa lengo la kupata ufumbuzi wa tatizo la umeme. Aidha, mpango huo ujumuishe pamoja miradi kama ya Stiglers Gorge ya kuzalisha umeme wa megawati 2100 na zaidi, makaa ya mawe ya Mchuchuma, umeme wa nishati ya upepo, maporomoko ya maji pamoja na vyanzo vingine vya umeme.

(ii) Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua hali mbaya ya kifedha inayolikabili Shirika la Umeme Tanzania ambapo gharama za uendeshaji zinazidi mapato ya Shirika. Hivyo basi, Kamati inaunga mkono Mpango Maalumu wa Kurekebisha Hali Mbaya ya Fedha ya Shirika hilo (Financial Recovery Plan) wa 2006 – 2010 ambao unalenga kulikwamua Shirika kifedha. Aidha, Kamati inaishauri Serikali kuidhamini TANESCO ili iweze kukopeshwa fedha na Taasisi za fedha badala ya kutegemea Bajeti ya Serikali.

(iii) Mheshimiwa Spika, katika harakati za kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, Kamati inaishauri Serikali iharakishe kukamilisha mpango wake wa kukinunua Kituo cha Uzalishaji Umeme (Independent Power Transmission Limited (IPTL) pamoja na zoezi la kukigeuza kituo hicho kitumie gesi asilia badala ya mafuta mazito.

4.0 SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI (TPDC)
4.1 Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lina umuhimu mkubwa katika kufanikisha utafiti na hatimaye upatikanaji wa mafuta na gesi asilia nchini. Kwa hiyo, Kamati inaishauri kuwa Shirika hilo lipewe fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa majukumu yake.

4.2 Mheshimiwa Spika, Kamati imeona kwamba kuwe na utaratibu wa kubakiza fedha TPDC (Retention) ili Shirika libaki na kiasi fulani cha fedha hizo zinazotokana na mauzo ya gesi asilia.

4.3 Mheshimiwa Spika, Kamati inakumbusha kwamba utaratibu uliotangazwa na Serikali wakati wa Hotuba ya Bajeti ya Serikali 2006/07 kwamba TPDC ishiriki katika kuagiza mafuta nje ili kudhibiti bei za mafuta, utekelezwe.

4.4 Mheshimiwa Spika, Kamati imesikitishwa na madai ya fidia na kusitishwa mkataba wa uagizaji wa mafuta kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na ADDAX mwaka 1999/2000. Hali hii imelifanya Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC) kutozwa riba kubwa (Compound interest) kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipa deni hilo la Dola za Marekani 1,898,562 Kutokana na hali hiyo Serikali inalazimika kulipa riba ya Dola za Marekani 62,929 kwa Wakili wa madai M/S Hunton Williams kila mwaka huku deni la msingi likiendelea kuongezeka. Kamati inaishauri Serikali itafute fedha ili deni hilo la msingi lilipwe lote haraka kwa shabaha ya kuondoa gharama za malipo ya riba juu ya riba na hivyo kuligharimu taifa fedha nyingi.

4.5 Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliahidi kuwa Shirika la TPDC litahusika na mpango mzima wa hifadhi ya Taifa ya Mafuta (Strategic Oil Reserves), Kamati inashauri kwamba mpango huo utekelezwe kwa kiasi inayostahili kwa kuiwezesha TPDC kifedha na Bunge lipewe taarifa hatua kwa hatua.

4.6 Mheshimiwa Spika, kuhusu Jengo la Mafuta (Mafuta House) ambalo lilitolewa bure kwa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) baada ya TPDC kushindwa kulimalizia, Kamati inashauri kuwa, jengo hilo liendeshwe kwa ubia kati ya Mashirika hayo mawili pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kulingana na kila shirika lilivyochangia.

4.7 Mheshimiwa Spika, kuhusu kutokuanza kwa utafutaji wa
mafuta katika baadhi ya vitalu vinavyomilikiwa na makampuni ya ''Shell International '' na ''Antrim Resources'' eneo la Zanzibar, unaotokana na kutokukamilika kwa upatikanaji wa ufumbuzi wa matatizo yaliyopo kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kamati inashauri Serikali ya Muungano kuharakisha kukamilisha mazungumzo kati yake na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili muafaka upatikane na kampuni husika ziweze kuanza kazi ya utafutaji wa mafuta.

5.0 MNAZI BAY- VISIMA VYA GESI ASILIA (MB1 NA MB2)
Mheshimiwa Spika, Kamati imeridhishwa na juhudi zinazofanywa na Kampuni inayotafiti kuwepo kwa gesi asilia eneo la Mnazi Bay Mkoani Mtwara. Kampuni hiyo yenye visima viwili vya gesi asili (MB1 na MB2) ambapo mpaka sasa imegundua gesi nyingi sana katika kisima cha pili ambacho kitaiwezesha Kampuni hiyo kuzalisha umeme hadi megawati 200 na zaidi. Kampuni hiyo hivi sasa inachimba kisima cha tatu (MB 3). Kwa sasa Artumas inazalisha umeme wa MW 18 kwa ajili ya Mikoa ya Lindi na Mtwara. Kamati inaipongeza kampuni hii kwa kutimiza malengo yake kwa wakati. Aidha, Kamati inaishauri Serikali kujiandaa na upatikanaji huo wa umeme kwa kuhakikisha kwamba miundombinu ya kusafirishia umeme huo inakuwepo ili kuondoa tatizo la nishati ya umeme kwa Mikoa ya Kusini.

6.0 SEKTA YA MADINI
6.1 Mheshimiwa Spika, Sekta ya madini ni moja kati ya sekta zilizojipatia umaarufu mkubwa kwa kuweza kuitangaza nchi na kukuza Pato la Taifa. Kamati imeweza kubaini mambo mbalimbali katika sekta hii na inatoa maoni na ushauri ufuatao:-

6.2 Mheshimiwa Spika, Kamati inapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa hatua aliyochukua ya kuunda Tume Maalum ya kufuatilia mikataba ya madini iliyoingiwa na wawekezaji hapa nchini. Aidha, Kamati imefarijika sana na uamuzi huo na inaamini kwamba suala la umilikaji wa machimbo ya madini kwa njia halali unadumishwa.

6.3 Mheshimiwa Spika, Kamati imeona kwamba wananchi wengi walioondolewa katika maeneo ya uchimbaji wa madini wameachwa bila kupatiwa fidia kama walivyostahili. Kamati inashauri kwamba Serikali ihakikishe wananchi hao wanapatiwa fidia zao kulingana na kanuni na taratibu zilizowekwa. Aidha, Kamati inatoa angalizo kwamba kama fidia ilitolewa lakini haikuwafikia walengwa basi hatua zichukuliwe kurekebisha dosari hiyo.

6.4 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hivi sasa wananchi walio katika maeneo ya uchimbaji wa madini wameonekana kukosa faida zitokanazo na uchimbaji wa madini. Kamati inashauri kwamba mikataba ya madini iwe na kipengele kinachotoa fursa kwa wakazi wa maeneo husika kuwa na hisa katika makampuni ya uchimbaji wa madini, hasa kupitia Halmashauri zao za Wilaya. Hapa tunazingatia kwamba ardhi sasa inathamani na inaweza kutumiwa kama sehemu ya hisa zao.

6.5 Mheshimiwa Spika, Kamati inaishauri Serikali kuelekeza Makampuni ya Madini kutoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania hususan waliopo maeneo ya uchimbaji wa madini.

6.6 Mheshimiwa Spika, kuhusu michango ya maendeleo inayotolewa na Makampuni ya uchimbaji wa Madini, Kamati inashauri kwamba michango hiyo iingizwe kwenye Makubaliano (Memorandum of Understanding) kati ya Makampuni ya Madini na Halmashauri za Wilaya ili sasa isiwe hisani bali jukumu la msingi.

6.7 Mheshimiwa Spika, kiasi kikubwa cha madini husafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kusafishwa na kukatwa kutokana na kutokuwepo kwa viwanda hivyo hapa nchini. Kamati inaishauri Serikali iharakishe utekelezaji wa uamuzi wa kuanzisha viwanda vya kusafisha na kukata madini hapa nchini badala ya madini hayo kusafirishwa kwenda nje ya nchi yakiwa hayajachakatwa.

6.8 Mheshimiwa Spika, kuhusu uchimbaji wa (gemstones), Kamati inashauri kwamba uchimbaji huo ufanywe na wazalendo/kampuni za kizalendo kwa kushirikiana na kampuni nyinmgine za nje kwa ubia isipokuwa mikataba iliyopo iendelee kuheshimiwa.

7.0 SEKTA YA VIWANDA
Mheshimiwa Spika, Kamati inathamini mchango wa sekta ya viwanda ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuvutia wawekezaji nchini. Ni katika mantiki hiyo, Kamati mara baada ya kutembela maeneo mbalimbali yanayojihusisha na sekta hii imeweza kutoa maoni na ushauri utakaoweza kuboresha sekta hii kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua kwamba nchi yetu ina malighafi nyingi zinazoweza kutumika katika kuendesha viwanda vyetu. Hivyo Kamati inashauri kwamba, Serikali ihakikishe kuwa kwa kiasi kikubwa viwanda vyetu viwe vinatumia malighafi zinazopatikana hapa nchini sambamba na kuhamasisha uzalilishaji wa malighafi hizo kama vile kwenye viwanda vya nguo, mafuta ya kupikia n.k.

(ii) Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini kwamba, zipo faida kubwa zinazopatikana kutokana na ushindani wa Biashara. Kwa kuwa kumekuwepo na baadhi ya Makampuni makubwa yanatumia mbinu mbalimbali za kuuwa Makampuni madogo yanayozalisha bidhaa zinazofanana na zao kwa njia ya kuleta ushindani wa kibiashara, Kamati inashauri kwamba itolewe elimu ya Sheria kuhusu Ushindani Halali (Fair Competition) ili kuweza kulinda Viwanda vichanga kwa mfano hali ya mgogoro wa biashara ya sigara baina ya kampuni ya sigara Tanzania (TCC) na kampuni ya sigara ya Mastermind (Mastermind Tobacco Tanzania Ltd).

(iii) Mheshimiwa Spika, kuhusu viwanda vya korosho vilivyonunuliwa na wazalendo kushindwa kupata mikopo kutoka kwenye mabenki kutokana na viwanda hivyo kutofanyiwa tathimini upya kwa bei za kununulia viwanda hivyo na hivyo kuvifanya viwanda hivyo kutokuwa na hati miliki. Kamati inashauri kwamba Serikali iviwezeshe viwanda vya korosho vilivyonunuliwa na wazalendo kufanya kazi, na kuhakikisha kwamba vinafanyiwa tathimini na kupata hati miliki haraka baada ya masharti muhimu kukamilika ili kuweza kutumia Hati hizo kama dhamana ya kupatia mikopo kwenye mabenki.

(iv) Mheshimiwa Spika, Viwanda vilivyopo sasa vinasimamiwa kisekta kwa maana ya kwamba viwanda chini ya Sekta nyingine haviangaliwi na Wizara yenye jukumu la Viwanda. Utaratibu huu si mzuri kwa hiyo Kamati inaishauri Serikali kuwa, viwanda vyote visimamiwe na Wizara moja ambayo ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko. Hali hii itaweka utaratibu mzuri wa kuratibu shughuli za maendeleo ya viwanda na masoko nchini wakati wizara za kisekta zikiendelea kutoa ushauri wa kitaalamu.

8.0 SEKTA YA BIASHARA NA MASOKO
Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua kwamba masoko ni moja ya maeneo muhimu sana ambayo yanategemewa na sekta nyingine kama vile viwanda, madini na biashara, kwa kuwa uwepo wa masoko unawezesha bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi kupata wanunuzi ndani na nje ya nchi. Kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Masoko Kamati inatoa maoni na ushauri kama ifuatavyo:-

8.1 Mheshimiwa Spika, Kamati imeona kwamba utaratibu wa ujenzi wa masoko katika maeneo mbalimbali ni mzuri ila inaishauri Serikali iendelee na utaratibu huo kwa kuhakikisha kwamba masoko yanajengwa haraka mfano soko la Segera na Makambako, na kutumika katika muda muafaka.

8.2 Mheshimiwa Spika, Kamati baada ya kutembelea viwanda vya korosho katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, imebaini kwamba ununuzi wa korosho unafanywa kwa bei za chini sana na hivyo kuonekana kuwakandamiza sana wakulima wadogo na kuwanufaisha wanunuzi. Kamati inashauri kwamba bei ya ununuzi wa korosho iendane na bei ya bidhaa hii katika Soko la Dunia ili kumuwezesha mkulima kupata faida baada ya kuondoa gharama zake za uzalishaji. Hili likifanyika litawapa ari na moyo wakulima hao kuweza kuendeleza zao hilo linalowaingizia kipato na kukuza Pato la Taifa.

8.3 Mheshimiwa Spika, kuhusu uzalishaji wa chumvi, Kamati inaishauri Serikali itilie maanani uzalishaji chumvi nchini hasa inayozalishwa Mkoani Lindi kwa kuwaongoza wazalishaji wadogo wanunue mashine za kusagia chumvi na kuwezesha chumvi hiyo kutumika nchini badala ya kuagiza chumvi kutoka nje.

8.4 Mheshimiwa Spika, Shamba la Mpira la Kihuhwi linakabiriwa na tataizo la ulipaji mishahara wafanyakazi wake. Kamati inaishauri Serikali iandae utaratibu mzuri wa kubinafsisha na kulipa mishahara ya Wafanyakazi wa Shamba hili lililopo Muheza. Mpira unaopatikana pale ni wa hali ya juu sana na unaweza kuwa chanzo kizuri cha malighafi ya Kiwanda cha General Tyre (EA) Arusha ambacho kina hisa za Umma. Sambamba na hilo Serikali ihamasishe kilimo cha zao la Mpira kwa Wananchi wa kawaida Wilayani Kilombero, Handeni, Muheza na Zanzibar.

8.5 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mpira ulioko Tanzania ni bora baada ya kupimwa na kampuni ya Continental Tyre (Germany) ambayo ina hisa asilimia 24 katika General Tyre (EA), Kamati inashauri kuwa Mashamba ya Mpira ya Muheza na Kilombero yakabidhiwe Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ili Waziri wa Viwanda ashirikiane na Mhisa Continental Tyre kutafuta mwekezaji ambaye ataweza kuendeleza mashamba hayo chini ya uangalizi wa General Tyre na pia kushawishiwa kuingia kwenye ubia katika Kiwanda cha General Tyre (EA). Hili ni muhimu maana Tanzania inatumia Jina la biashara (Brand name) la "Continental Tyre" na "General Tyre" ambapo Tanzania haiwezi kulibinafsisha kama ilivyofanyika kwenye Viwanda vya Magunia, Ngozi n.k.

8.6 Mheshimiwa Spika, Kamati imeona kuwa upo umuhimu wa Serikali kuandaa utaratibu mzuri wa kuwawezesha wajasiriamali wadogowadogo si tu kuwapatia mikopo bali pia kuwaendeleza ili waweze kufikia viwango vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuwatafutia masoko ya kuuza bidhaa zao.

9.0 MAONI YA KAMATI YA UJUMLA
Mheshimiwa Spika, baada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika sekta za nishati, madini, viwanda, biashara na masoko zilizokwisha elezwa hapo awali, Kamati inatoa maoni na ushauri wa jumla kwa ajili ya kuboresha maeneo mengine muhimu kama ifuatavyo:-

9.1 Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kuwepo ucheleweshaji wa Taarifa za Ukaguzi wa Hesabu katika baadhi ya Taasisi na Mashirika ya Wizara ambazo inazisimamia kutokana na Taasisi/ Mashirika hayo kuingia katika utaratibu mpya wa kufanya ukaguzi wa hesabu zao yaani "International Financial Reporting Standards"(IFRS) na kutoka kwenye utaratibu wa Tanzania Financial Reporting Standards. Kwa kuwa suala la ukaguzi wa Hesabu linahitaji uteuzi wa Wakaguzi, Kamati inashauri kwamba uteuzi wa wakaguzi ufanywe mapema ili kuziwezesha hesabu za taasisi hizo kukaguliwa mapema na Taasisi hizo kuwasilisha taarifa za hesabu zao zinazoendana na wakati na sio kuwasilisha taarifa zilizokwisha pita miaka 2 au 3 nyuma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ambaye ndiye huteua Wakaguzi hao mara baada ya kupata mapendekezo ya Bodi za Mashirika ya Umma aweke utaratibu ambao utaharakisha uteuzi huo.

9.2 Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie upya utaratibu wa ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma kwa kuhakikisha kwamba mashirika hayo hayaorodheshwi (specified) na Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma kwa muda mrefu na pia Makubaliano (Memorandum of Understanding) na Makubaliano ya Kununua (Sales Agreement) yawekewe utaratibu endelevu wa ufuatiliaji na utekelezaji baada ya Kampuni/Shirika kubinafsishwa.
9.3 Mheshimiwa Spika, Serikali iandae utaratibu ambao utawezesha uwekezaji kwenye Vyuo Vya Kufundisha Masomo ya Hoteli na Utalii ili wahitimu wake waweze kuajiriwa katika Hoteli za Kitalii sambamba na kuitangaza nchi kwa ajili ya utalii. Kamati imebaini kwamba Mameneja wengi katika Hoteli za Kitalii ni Wageni.

9.4 Mheshimiwa Spika, Serikali ihakikishe kuwa uchafuzi na uharibifu wa mazingira unadhibitiwa hasa kwenye vyanzo vya maji na kwenye maeneo yanakofanyika uchimbaji wa madini bila kuzingatia hifadhi ya mazingira.

9.5 Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Serikali ivitangaze vivutio vilivyopo kwenye utaratibu wa Maeneo Tengefu (Export Processing Zones) kwa ajili ya kuuza nje ya nchi ili makampuni mengi ya nje na ya ndani yaweze kuanzisha viwanda katika maeneo hayo. Aidha, Serikali iboreshe miundombinu katika maeneo hayo ili yaweze kufikika kwa urahisi.

9.6 Mheshimiwa Spika, Kamati imeona kuwa, ni muda mrefu sasa tangu Serikali ilete mipango ya "Mtwara Development Corridor" na "Central Development Corridor", hivyo hapana budi mipango hiyo ianze kutekelezwa ili kuhamasisha ukuaji wa Uchumi. Aidha, kwa kuwa utaratibu wa kushirikiana na nchi jirani ni wa kutumia Kamati za Mawaziri na Watendaji. Kamati inashauri kwamba sasa iundwe Kamisheni ya Maeneo hayo.

9.7 Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Serikali kuwa Taasisi za Utafiti zipewe umuhimu kwa kupatiwa fedha za kutosha za kufanyia utafiti pamoja na vitendea kazi. Sambamba na hilo Serikali iweke utaratibu wa kutumia matokeo ya tafiti hizo. Aidha, tatizo la Shirika la Utafiti na Uendelezaji Viwanda (TIRDO) kutopatiwa Hati Miliki, Kamati inashauri kwamba tatizo hilo lishughulikiwe haraka iwezekanavyo ili kuliwezesha Shirika hilo kuwa na uwezo wa kuvutia wawekezaji.

9.8 Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri kuwa Serikali ipitie upya mikataba iliyoingiwa wakati wa kuuza yaliyokuwa Mashirika ya Umma. Mengi ya Mashirika hayo hayajafanya kazi tangu yaliponunuliwa. Mengine mitambo iliyokuwepo imekwishang'olewa na waliokuwa wafanyakazi kuachwa wasijue la kufanya. Kwa mfano Viwanda vya magunia, ngozi n.k.

9.9 Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa upatikanaji, uzalishaji na matumizi ya Gesi Asilia, Kamati inashauri Kwamba Serikali itunge Sheria mpya ya matumizi ya gesi asilia ili iweze kusimamia nishati hii muhimu kwa ufanisi.

9.10 Mheshimiwa Spika, Sheria za Mashirika ya Umma chini ya Kamati ya Uwekezaji na Biashara ni za muda mrefu wakati kumetokea mabadiliko mengi ya sera kitaifa na za Kimataifa Kamati inashauri kwamba sheria hizo zirekebishwe ili ziendane na mazingira ya shughuli za sasa. Aidha, Serikali ilete Bungeni Mpango wa Kutunga na Kurekebisha Sheria (Legislative Programme) ili zifanyiwe ufuatiliaji na Bunge ambalo ndilo lenye jukumu la kutunga Sheria.

10.0 HITIMISHO

10.1 WAJUMBE WA KAMATI

10.2 Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kututeua sisi kuwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara mwezi Januari, 2006 kwa mujibu wa Kanuni ya 87(4) ya Kanuni za Bunge. Pia naomba niwashukuru Wajumbe wenzangu waliofanya kazi bila kuchoka na kuyafikia maeneo yote yanayoonyeshwa kwenye Taarifa hii. Mawazo waliyokuwa wanayatoa kwa nia ya kupata majibu ya matatizo ya maeneo hayo yamesaidia sana hadi kuwasilishwa kwa taarifa hii. NAWASHUKURU KWA DHATI.
Naomba niwatambue Wajumbe hao kwa majina:-

(1). Mhe. William H. Shellukindo,Mb - Mwenyekiti
(2). Mhe.Dk.Harrison G.Mwakyembe,Mb - M/Mwenyekiti
(3). Mhe. Muhammad A. Chomboh, Mb - Mjumbe
(4). Mhe. Yahya K. Issa, Mb - Mjumbe
(5). Mhe. Asha M.Jecha, Mb - Mjumbe
(6). Mhe. Siraju J. Kaboyonga,Mb - Mjumbe
(7). Mhe. Mwajuma H. Khamis, Mb - Mjumbe
(8). Mhe. Vuai A. Khamis, Mb - Mjumbe
(9). Mhe. Fuya G. Kimbita, Mb - Mjumbe
(10).Mhe. Eng.Stella M. Manyanya,Mb - Mjumbe
(11).Mhe. Fatma A. Mikidadi, Mb - Mjumbe
(12).Mhe. Herbert J.Muntangi, Mb - Mjumbe
(13).Mhe. Mohammed H. Mnyaa, Mb - Mjumbe
(14).Mhe. Luhanga Joelson Mpina, Mb - Mjumbe
(15).Mhe. Mbaruk K. Mwandoro, Mb - Mjumbe
(16).Mhe. Saverina Silvanus Mwijage,Mb - Mjumbe
(17).Mhe. Dkt. Lucy S. Nkya, Mb - Mjumbe
(18).Mhe. Christopher O. Ole-Sendeka, Mb - Mjumbe
(19).Mhe. Lucy F. Owenya, Mb - Mjumbe
(20).Mhe. Ahmed Ally Salum,Mb - Mjumbe
(21).Mhe. Haji J. Sereweji, Mb - Mjumbe
(22).Mhe. Ahmed Mabkhut Shabiby, Mb - Mjumbe
(23).Mhe. Mohammed S. Sinani, Mb - Mjumbe
(24).Mhe. Abdallah Salum Sumry, Mb - Mjumbe

10.3 Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena naomba kutoa shukrani zangu kwako kwa kunipa nafasi niweze kuwasilisha taarifa ya Kamati kwa kipindi cha Mwaka mmoja (2006) uliopita wa Bunge hili Jipya.
10.4 Mheshimiwa Spika, ANGALIZO: Kamati yangu imebaini kuwa Taarifa za Kamati zinawasilishwa Bungeni wakati Bajeti zimekwisha kupitishwa hivyo ushauri unaonekana kutokwenda na wakati na hivyo kutotekelezwa. Kamati yangu inashauri kwamba Taarifa za Kamati za mwaka zijadiliwe kwenye Bunge la mwezi Januari/Februari kila mwaka ili ushauri unaotolewa uweze kuzingatiwa kwenye Bajeti ya mwaka unaofuata.

10.5 Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru Mawaziri, Mhe. Nazir M. Karamagi (Mb), alipokuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko na aliyekuwa Naibu wake Mhe. Dkt. David Mathayo David (Mb). Pia namshukuru Mhe. Dr. Ibrahim Msabaha (Mb) aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na aliyekuwa Naibu wake Mhe. Lawrence K. Masha kwa ushirikiano waliotoa kwa Kamati hii.

10.6 Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru Mawaziri, Mhe. Basil P. Mramba (Mb), Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, na Naibu wake Mhe. Hezekiah Chibulunje (Mb). Pia nawashukuru Mhe.Nazir M. Karamagi (Mb) Waziri wa sasa wa Nishati na Madini, na aliyekuwa Naibu wake Mhe.Bernard K.Membe (Mb) ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano walioutoa kipindi chote Kamati ilipokuwa kazini. Aidha, napenda kumpongeza Mhe. William Ngeleja (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii wakati wa kukamilisha taarifa hii. Ninamkaribisha kwa dhati katika familia ya Nishati na Madini. Napenda pia kuwashukuru Makatibu Wakuu wa Wizara hizi mbili, Dk. Stergomena Tax- Bamwenda wa Wizara ya Viwanda Biashara na Masoko, Ndugu Arthur Mwakapugi wa Wizara ya Nishati na Madini, Ndugu Wilfred Nyachia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko pamoja na watendaji wote wa Wizara hizo, kwa utendaji wenye ufanisi

10.7 Mheshimiwa Spika, kwa ujumla ziara za Kamati Mikoani zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mapokezi na ushirikiano ambao Kamati ilipata kutoka kwa Wakuu wa Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Lindi, Manyara, Mtwara na Tanga; Mikoa ambayo Kamati ilifanikiwa kuitembelea na kuweza kujionea shughuli mbalimbali za Wizara za Nishati na Madini na Viwanda, Biashara na Masoko zinazofanywa katika Mikoa hiyo (Tazama Kiambatisho Na. 1). Kamati inapenda kutoa shukrani kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zao kwa ushirikiano mkubwa waliotoa na kushauri ushirikiano huo uzidi kuendelea. Aidha, katika Ratiba ya Kamati kwa mwaka 2007 itazingatia kutembelea maeneo ambayo Kamati haikupata fursa ya kuyatembelea na kuona utekelezaji wa shughuli za Wizara hizo na Taasisi zake.

10.8 Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee Kamati yangu inapenda kukushukuru wewe mwenyewe kwa kuliongoza kwa "Speed and Standard" Bunge letu na pia kwa heshima uliyotupa kwa kututeua kuwa Wajumbe wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara. Kwa pamoja tutatekeleza majukumu yetu kwa lengo la kutimiza utekelezaji wa majukumu ya Bunge letu ya kusimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake katika kutekeleza matakwa ya Katiba ya Nchi.

10.9 Mheshimiwa Spika, naomba pia kumshukuru Katibu wa Bunge Ndugu Damian S. Foka na Ofisi yake kwa kuwezesha Kamati yetu kufanya kazi bila matatizo yoyote. Mwisho, naomba niwashukuru Makatibu wa Kamati Ndugu Aggrey N. Nzowa Ndugu Abdallah Hancha na Ndugu Lina Kitosi kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuhudumia Kamati hii kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naomba Bunge lako Tukufu lipokee Taarifa hii, liijadili na kuishauri Serikali ipasavyo.

Mhe. William H. Shellukindo (Mb)
MWENYEKITI
KAMATI YA BUNGE YA UWEKEZAJI NA BIASHARA
Novemba 2007

KIAMBATISHO Na. 1
MIKOA AMBAYO KAMATI ILITEMBELEA
Na MKOA MAENEO YALIYOTEMBELEWA
1. ARUSHA 1. Kiwanda cha Mipira ya Magari (General Tyre)
2. Umoja wa Wafanyabiashara wa Vito
2. DAR ES SALAAM 1. Shirika la Viwango Tanzania (Tanzania Bureau of Standards)
2. Shirika la Umeme Tanzania - (TANESCO)
3. Chuo cha Elimu ya Biashara - (CBE)
4. Shirika la Maendeleo la Taifa - (NDC)
5. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania-(TPDC)
6. Halmashauri ya Biashara ya Nje -(BET)
7. Shirika la Kuendeleza Viwanda vidogo - (SIDO)
8. Shirika la Utafiti na Uendelezaji Viwanda Tanzania (Tanzania Industrial Research Development Organization (TIRDO)
9. Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya IPTL
(Independent Power Ltd )
10. Kampuni ya kuzalisha umeme ya Songas
11. Kampuni ya Kuzalisha Bia
(Tanzania Breweries Ltd)
12. Murzah Oil Mills.
13. BIDCO Oil Mills.
14. Millennium Business Park
15. Kilimanjaro Kempinski Hotel
16. Tanzania Engineering and Manufacturing Development Organization(TEMDO)
17. Centre for Agricultural Mechanization and Rural Technology Centre (CARMATEC)
3. IRINGA 1. Kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera
2. Mradi wa Chuma Liganga
3. Mradi wa Makaa ya Mawe -Mchuchuma
4. MANYARA 1.Mchimbaji Mkubwa wa Tanzanite (Tanzanite One)
2. Wachimbaji wadogo wa Tanzanite Kitalu B Mererani

5. LINDI 1. Ukarabati wa Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Buco Investment Holding.
2. Mashamba ya kuzalisha Chumvi Mjini Lindi

3. Kituo cha Kuzalisha Gesi Asilia Songo songo.

6. MTWARA 1. Bodi ya Korosho
2. Kiwanda cha Kubangua Korosho cha OLAM
3. Ukarabati wa Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Likombe
4. Ukarabati wa Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Mtwara (EOTF).
5. Eneo la Mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji Kilambo
6. Mnazi Bay Visima vya Gesi Asilia (MB1 na MB2)
7. Mitambo ya Kampuni ya ARTUMAS ya kuzalisha umeme mjini Mtwara.
8. Bandari ya Mtwara.

7.
TANGA
1. Kiwanda cha Kupasua Mbao cha Mkata- Handeni (Mkata Saw Mills)
2. Eneo la Soko la Kimataifa Segera
3. Shirika la Kuzalisha Umeme
(TANESCO Hale)
4. Kiwanda cha Chuma Tanga
(Unique Steel Mills)
5. Kiwanda cha Kutengeneza Chokaa Pongwe Tanga (ARM)
6. Kiwanda cha Saruji - Tanga
7. Mashamba ya Mpira Kihuhwi Muheza
8. Kiwanda cha Chai Mponde Lushoto
9. Kiwanda cha Miwati Soni - Lushoto
(Lion Wattle Company)
10. Kiwanda cha Matunda na Maji, Soni - Lushoto

KIAMBATISHO Na. 2

WIZARA ZINAZOSIMAMIWA NA KAMATI PAMOJA NA MASHIRIKA NA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA HIZO

1.0 Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko

1.1 Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC)
1.2 Shirika la kuendeleza Viwanda vidogo (SIDO)
1.3 Halmashauri ya Biashara ya nje (BET)
1.4 Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)
1.5 Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
1.6 Shirika la Utafiti na Uendelezaji Viwanda Tanzania (Tanzania Industrial Research and Development Organisation (TIRDO)
1.7 Tanzania Engineering and Manufacturing
Development Organisation (TEMDO)
1.8 Centre for Agricultural Mechanisation and
Rural Technology Centre (CARMATEC)
1.9 General Tyre (EA) Arusha
1.10 Wakala wa Usajili na Uandikishaji wa Biashara (BRELA)

2.0 Wizara ya Nishati na Madini

2.1 Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

2.2 Shirika la umeme Tanzania (TANESCO)

2.3 Shirika la Madini Tanzania (STAMICO)

2.4 Kituo cha Kimataifa cha Nishati na Madini.

2.5 Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA)

KIAMBATISHO Na. 3

SHERIA ZA MASHIRIKA YA UMMA ZINAZOHITAJI MAREKEBISHO

1. National Development Cooperation (NDC) Act, 1965
2. Tanzania Petroleum Development Cooperation (TPDC) Act, 1969
3. Tanzania Bureau of Standards (TBS) Act,1977
4. Centre for Agricultural Mechanization and Rural Technology (CARMATEC) Act, 1981
5. Tanzania Industrial Research and Development Organization (TIRDO) Act, 1979
6. Tanzania Engineering and Manufacturing Design Organization (TEMDO) Act, 1980
7. Small Industries Development Organization (SIDO) Act, 1973
8. Board of External Trade, (BET) Act, 1978
9. College of Business Education (CBE) (Amendment)Act, 1974
10. State Mining Corporation (STAMICO) Act 1969
 
hii inaweza kuwa na marekebisho machache ikiwamo lile la kuohakikisha KAMATI TEULE INAUNDWA. Wakati tunasubiri FINAL EDITED, tuanza kuipitia hii hapa.

...baada ya muda wote huu na hasara ya mabilioni leo ndio wanakurupuka huko walipotoka eti uchunguzi,sina imani kabisa na hawa watu zaidi ya kutuongezea mzigo wa kodi kwa matumizi ya hizo kamati,na kwa nini chombo chenye nguvu kama bunge wanachofanya hapo ni TUNAPENDEKEZA why not subpoena all alledged wahalifu wote waje wajibu mbele ya bunge publicly...huo upuuzi wa TUNAPENDEKEZA tayari ni red flag,SINA IMANI na hawa watu na hizo pesa hazitarudi,tunawasubiri 2010 tuu!
 
Hii ndio ripoti ambayo imefanyiwa uhariri. Kutokana na ripoti iliyotolewa kwa wabunge.
 
Attachments

  • UB Final Report-EDITED.doc
    153 KB · Views: 191
Mwambieni Mh. Shelukindo na kamati yake kuwa waje hapa JF na wataweza kuupata mkataba wa Richmond na sio kwa bunge kuunda kamati nyingine ikale pesa za kuutafuta mkataba unaopatikana hapa jf.

Kamati kwa ujumla imeuliza maswali ambayo kila mtanzania amekuwa akiyauliza, nilitegemea kuwa kamati ingekuja na majibu ya maswali husika na sio kurudia kuyauliza tena ,wakati hayo ndio yanahitaji kupatiwa majibu ya kina na kamati yake ya bunge.

Hapa hakuna jipya kwani hawajatupatia majibu ila wameuliza maswali yaleyale ya siku zote.
 
Kamati ilipewa mkataba haraka haraka ili wasiunde kamati teule, lakini wakashituka wakasema lazima waunde kamati... Hali ilivyo ni kwamba hivi sasa wachangiaji wote wa CCM na upinzani wanasema lazima iundwe kamati teule na wananukuu Ripoti ya PPRA ambayo humu JF imo na kila mtu anaichota humu.... Waliochangia na kutaka kamati teule ni pamoja na Sendeka, Dr Slaa, Mnyaa na wengine wote akiwamo Ruth Msafiri, ambaye anasema Watanzania wote wameathirika sana na mkataba wa Richmond ili kuwafanya waweka mikataba wawe makini kwa maslahi ya taifa,.... Nadhani sasa wanaiogopa JF kuliko chochote... Hii ni hatari kweli kweli
 
mwisho wa safari ndio mwanzo wa safari nyingine,kama ukipata kushudia hivyo vikao vyoa utacheka ufe maana,wataanza kikao saa mbili asubuhi kwa kusoma magazeti na kusimuliana yaliyopia jana yake,saa nne chai,baada ya hapo wengi watatoa udhuru wa kuhudhuria shughuli fulani basi watasema tukutane mchana baada ya msosi.waisha shiba si mnajua kinachotokea .......................
 
Back
Top Bottom