MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa, amepanda kwa alama nne, huku mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, akishuka kwa alama 10, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Synovate.
Matokeo hayo yanapishana na yale yaliyotolewa siku tano zilizopita na taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) ambayo ilimpa Kikwete asilimia 71.2, Dk. Slaa (12.3) na mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (10.3).
Akitangaza matokeo ya utafiti huo, jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Synovate hapa nchini, Agrey Oriwo, alisema utafiti wao wameufanya kuanzia Septemba 5 mwaka huu na umewahusisha watu 2000.
Alisema katika utafiti huo, uliohusisha mikoa 21 ya Tanzania Bara ulifanywa katika wilaya 63 na waliowahoji walikuwa 73 ambao walikuwa wakikusanya takwimu (data) za utafiti huo.
Alisema mbinu iliyotumika ni utafiti wa kimahesabu ambapo wahojiwa walichaguliwa kwa njia ya nasibu.
Alisema asilimia 53, waliohojiwa kwenye utafiti huo walikuwa ni wanaume na 47 wanawake ambapo asilimia 60 ya waliohojiwa ni wakazi wa maeneo ya vijijini, huku 40 wakiwa maeneo ya mijini.
Alisema miongoni mwa maswali waliyoulizwa ni Mtamchagua nani kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano mwishoni mwa mwezi huu? Ndipo yalipopatikana matokeo kuwa asilimia 61 wangemchagua Rais Kikwete, Dk. Slaa (16)na Profesa Lipumba (05).
Alisema asilimia 13 waligoma kujibu swali hilo, huku asilimia 5 wakijibu kuwa wangewachagua wagombea wa vyama vingine vya siasa.
Alisema katika utafiti huo, wananchi waliulizwa umaarufu wa vyama vya siasa ambapo asilimia 64 walisema CCM iko karibu nao, CHADEMA (22), CUF (7), asilimia 5 walivitaja vyama vingine, huku asilimia mbili hawakujibu swali hilo.
Swali jingine lilikuwa ni kama ingetokea nafasi ya kuwachagua vijana waliojitokeza na wenye vipaji vya uongozi kuwa rais wangemchagua nani, ambapo Zitto Kabwe aliibuka kidedea kwa kupata asilimia 38 akifuatiwa na Husein Mwinyi (15); na Makongoro Nyerere (12).
HABARI ZAIDI>>