Rais wa Zanzibar ataka sheria ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi wajue haki zao

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,500
9,279

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameitaka Jumuiya ya Majaji na Mahakimu ya Nchi za Afrika Mashariki (EAMJA) kuhakikisha sheria zinatafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.

Alisema hatua hiyo itawasaidia na kuwarahisishia wananchi kupata haki zao sambamba na kuzifahamu vyema sheria za nchi yao.

Alisema jambo hilo lina umuhimu mkubwa katika kutafuta haki kwa wananchi hali itakayowafanya kuwa raia bora na wenye kutii sheria za nchi.


Alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mkutano wa mwaka wa EAMJA, uliofanyika hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni.

Alisema ufahamu wa sheria ni jambo muhimu katika kupata haki kwa wananchi, hivyo Majaji na Mahakimu wana dhima ya kushirikiana na taasisi nyengine za nchi wanachama kuiendeleza lugha ya Kiswahili ili iendelee kukua kwa kasi zaidi na kutumika katika mikutano ya kimataifa.

Aliwataka kuhakikisha lugha hiyo inakuwa na msamiati wa kutosha katika masuala ya sheria pamoja na masuala mengine ya kiuchumi, teknolojia na kijamii ili iwe rahisi kufahamika.

Alipendekeza katika mikutano ijayo ya Jumuiya hiyo ni vyema ikatumika lugha ya Kiswahili.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria kwa juhudi inazozichukua kutafsiri sheria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.

Alieleza kuwa wananchi wa Afrika Mashariki wanaona fahari kuona lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazokua haraka duniani.

Aliongeza kuwa tayari lugha ya Kiswahili imepitishwa kutumika katika mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Umoja wa Afrika na kusisitiza kuwa Kiswahili kinaweza kutumika kitaifa na kimataifa katika kuendeleza sera na programu za kukuza uchumi.

Alisema lugha ya Kiswahili inasaidia kuimarisha uhusiano na ushirikiano mwema kati ya nchi na Jumuiya za kimataifa hali ambayo pia, imewaunganisha Watanzania na kuwa wamoja licha ya kwamba wanazo lugha za makabila yao yapatayo 147.

Itakumbukwa kwamba mnamo Agosti 8, 2019 akifunga maadhimisho na maonyesho ya nne ya wiki ya viwanda ya (SADC) katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Dk. Shein alisema, ni jambo jema kukifanya Kiswahili kuwa ni miongoni mwa lugha rasmi za jumuiya hiyo.

Alieleza kuwa hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha umoja na mshikamano kwa Wanachama wa (SADC) pamoja na kukuza shughuli za biashara na viwanda kwani historia inaonyesha kuwa Kiswahili kimewaunganisha Watanzania kuwa wamoja.

Alieleza kuwa Kiswahili kina mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Watanzania Kama sheria za mtaani tu hatuzifati na zimeandikwa kwa kiswahili tena kwa miandiko migumu si ile ya kidigital,utafsiri wa sheria uende na kuhamasisha kusoma maana yashanikuta nakuja kuonyeshwa bango usikojoe hapa raia wa watu nishakojoa zamani😎😂😂
NB;unapojua wewe mvunjaji wa sheria kwa kutokusoma jitahidi kuwa mpole na mwenye maneno ya hekima😂
 
Back
Top Bottom