Nyuma yako (Riwaya ya S. Mollel)

Nyuma yako (Riwaya ya S. Mollel)

Uzuri wa Steve akitupia anatupia ep kibao. Hii simulizi haijawahi kunipa kiwewe katika kusubilia.

Steve naomba na Mimi uwe unanitag
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA TATU) -- MWISHO WA MSIMU*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

"Uhakika?" Abdulaziz akauliza.

"Ndio. Nakuhakikishia," Jamal akasema kisha mabwana hawa wakapeana mikono ya makubaliano.

Waliteta mengi. Na huyo ambaye kichwa chake kilikuwa kinaenda kuvunwa alikuwa ni wa kwanza kati ya wengi wanaofuata.

Damu itamwagika.

Bwana Jamal akaenda zake ambapo ndani ya muda mchache, kama lisaa moja, akawa amekutana na wanaume wanne. Wanaume wa kazi. Wanaume hao akawapa maelekezo lakini pia na deadline.

Anataka kichwa cha mtu usiku huu.

ENDELEA

Nani angedhani usi huu ungeleta shari? Hakuna. Upepo ulikuwa unapuliza na watu, wengi wao, walikuwa wameshajiweka kwenye maskani zao kujipumzisha.

Wazazi na watoto wao wakiwa wamejumuika kwenye meza kula. Wengine wakiwa wamekaa nje vibarazani ama huko mjini wakirandaranda kibiashara.

Lakini kwenye muda kama huu kwa ujumla kulikuwa ni kimya. Maeneo mengi yalikuwa yamemezwa na ukimya lakini pia na kiza. Kama kuna mwanga basi ni zile za nje, za ndani zimepumzishwa watu wakiwa wamefumba macho yao kupumzika.

Lakini sio wote. Mabwana hawa takribani wanne waliokuwa wamevalia kombati nyeusi za kazi walikuwa tayari wapo kwenye lindo. Mikono yao imebebelea bunduki na nyuso zao zimefunikwa kwa barakoa nyeusi za mipira.

Walikuwa ni makomando. Na usiku huu walikuwa na kazi moja tu, kumuua Marietta, kisha mwili wake ukateketezwe na kichwa chake kihifadhiwe na mtoto wa mfalme Abdulaziz.

Hapa walipokuwa wamesimama ilikuwa ni kama robo kilometa tu kufikia makazi ambapo wanaamini Marietta yupo. Basi kwa kufanya ufanisi, mabwana hawa wakajigawa, wawili waende mashariki na wawili waende magharibi kisha wakakutanie mahali pa tukio.

Wakiwa wanafanya vivyo, wawe wanawasiliana kujuzana kinachoendelea.

Basi wanaume wawili wakatembea kwa tahadhari mpaka karibu kabisa na makazi ya Mahmoud. Wakawasiliana na wenzao na yote yalikuwa sawa. Nao muda si mrefu wakawa wamefika eneo la tukio wakiwa salama salmini.

Wakatazamana na kisha kiongozi wao akaamuru wawili waende nyuma ya jengo na wawili wabaki kwa mbele ili kuzuia kutoroka kwa mlengwa. Walipofanya vivyo, wanaume wale wawili wakatumia pini maalumu kutengulia vitasa vya mlango alafu wakazama ndani wakiwa wamebebelea kila aina ya tahadhari.

Bunduki zilikuwa mbele na macho yakiwa yanaruka na kuambaa-ambaa huku na kule. Kulikuwa ni kiza, lakini si kile totoro, lah! Kiza cha kuweza kuona hata panya akikatiza.

Wakapita sebuleni, wakaendelea kusonga, mpaka kufika chumbani. Chumba cha kwanza kabisa wakakifungua, lakini katika namna ya ajabu wakakumbana na moshi mzito haswa.

Ilikuwa kosa wao kuvuta hewa hiyo. Walijikuta wanakohoa kwanguvu na kwa kufululiza kiasi kwamba hata kushikilia silaha zao ilikuwa haiwezekani.

Wenzao walioko nje waliposikia hayo, upesi wakafanya namna kwenda kukuta wenzao lakini kwa tahadhari hawakusonga ndani. Walishatambua ni sumu. Basi wasiwe na namna wakawatazama wenzao wakiwa wanateketea.

Mmoja wao akiwa anakohoa na kutetemeka, akawakimbilia wenzake kana kwamba mwehu. Macho yake yalikuwa yamebadilika rangi, yamekuwa ya kijani.

Mdomo wake ulikuwa mkavu kupita kiasi mpaka kupasukapasuka. Ulimi wake nao ulikuwa mkavu kama tambara bichi lililokakamazwa na mwanga mkali wa jua.

Haikujulikana hata ni muda gani alivua barakoa yake. Hakikuwa kitu cha kuambiwa, alikuwa anapitia maumivu makali. Nguo ambayo ilikuwa imembana hapo awali, ilikuwa sasa imepwaya!

Hakudumu muda mrefu, akadondoka chini akiwa na mwili kama uji! Akafa kifo cha ajabu kabisa.

Hata baadae hewa ya sumu ilipoambaa, wakaenda kumkuta mwingine ndani, kiongozi wao, akiwa amerojeka vibaya mno angalau ya yule aliyekimbilia nje.

Basi wanaume hao, wawili waliobaki, wakatoa taarifa kwa mkuu wao Jamal kuhusu walichokutana nacho. Wameshindwa kumpata muhusika na zaidi wamepoteza wapambanaji wawili!

Taarifa hizo zikamfikia pia na Abdulaziz asubuhi na mapema. Akaumwa sana na kukasirika. Hata mke wake akalazimika kukaa naye mbali. Mwanaume huyo alijiwazia wapi atakapokuwepo Marietta. Wapi atakapokuwepo Mahmoud?

Alitaka kuonana na Jamal haraka iwezekanavyo.

Jamal akiwa amepaliwa na hofu, akafika nyumbani kwa Abdulaziz upesi kwenye majira ya saa tatu. Akamkuta Abdulaziz akiwa amefura, ameweka kahawa yake kwenye kikombe lakini hajainywa mpaka imepoa.

Uso wake ulikuwa mwekundu, macho yake ameyakodoa na ndita amezikunja. Hata Jamal alifahamu mambo yalikuwa yameenda kombo. Abdulaziz hakuwa na msalia mtume kwenye njia yake ya kwenda ufalmeni. Alikuwa anaona anakawia.

“Nini kimetokea??” akafoka Abdulaziz. Alikuwa anamtazama Jamal kana kwamba ni mtu mkaidi. “Uliniahidi nini Jamal?”

“Najua, mkuu lakini haikuwa vile ambayo tumetarajia.”

“Jamal!” Abdulaziz akaita. “Hakuna kitu chochote cha kutaraji katika ulimwengu huu bali unakitengeneza.”

“Najua. Kila kitu kilikuwa kimepangwa lakini adui yetu ni kama alikuwa anatutaraji kwani alishapanga mipango yake. Mitego ya sumu ilikuwa imewekwa ndani ya vyumba vyote. Tena sumu kali kupita kiasi.”

Abdulaziz akafikiria kwa muda kidogo kabla hajatikisa kichwa chake na kusema, “Mahmoud!”

Akanyamaza tena kidogo akikuna kidevu.

“Ni Mahmoud,” akatia neno akitazama chini. Alikuwa anafahamu fika kuwa bwana huyo, yaani Mahmoud, ni mtaalamu haswa wa mambo hayo ya utengenezaji wa sumu kwakuwa mbobevu kwenye taaluma ya kemia.

Kwenye mambo mbalimbali aliwahi kumtumia bwana huyo na kumpa matokeo chanya. Ikiwemo pia kwenye misheni ya kumpoteza Raisi wa Marekani.

Kwenye misheni hiyo bwana Mahmoud alitumia taaluma yake kutengeneza gesi kama kilevi ambacho kilitumika kumziraisha Raisi mara moja punde tu alipovuta.

“Sasa tunafanyaje?” Jamal akauliza . abdulaziz akafikiria kidogo kabla hajasema, “Najua mahali Mahmoud alipo.”

Kisha akamtazama Jamal.


**

Saa yake ya mkononi ilikuwa inasema ni saa sita mchana. Alimalizia kunywa juisi yake kisha akalipa na kunyanyuka kutoka ndani.

Alitazama kushoto na kulia. Alikuwa yu sawa, alitengenezea koti lake mwilini alafu akaendelea na safari.

Mwanamke huyu alikuwa amebana nywele zake vema na macho yake ameyafunika kwa miwani rangi nyekundu ya kufifia. Mwendo wake ulikuwa wa kiukakamavu utadhani hajavalia viatu vya visigino virefu.

Alipotembea kwa muda kidogo akatoa pipi ya kijiti na kuimumunya. Alitembea kwa kama dakika nne kabla hajachoropoa simu yake na kuwasiliana na Marietta.

“Unakuja lini?” lilikuwa swali la kwanza. Kelly akachomoa pipi yake mdomoni.

“Muda si mrefu, madam. Passport ipo ndani ya makazi yangu. Unajua siwezi kusafiri pasipo kuwa nayo.”

“Haitakuwa imebebwa?”

“Hapana! Niliweka sehemu ya siri. Hakuna mtu anayeweza kuibaini isipokuwa mimi pekee.”

“Sawa. Utakapoipata, angalia kama kuna uwezekano wa kupata ndege yoyote ya mapema, hata kama ni ya leo. Sawa?”

“Usijali.”

Kelly akarejesha simu yake mfukoni na kuendelea kuchapa mwendo.


**


SEHEMU YA PILI …


Baada ya mwendo wake kutimiza dakika kumi na tano, mwanamke huyo akazama ndani ya jengo moja ghorofa. Halikuwa lile la makazi yake, lah! Lilikuwa ni jingine ambalo lilikuwa limechoka kidogo.

Humo akapandisha ngazi mpaka juu kabisa kwenye paa. Akavua viatu vyake na kurukia ghorofa la kwanza kisha akasonga na kurukia ghorofa la pili. Alipokuwa huko juu, akavua koti lake na kuligeuza. Lilikuwa na rangi nyingine.

Kwa kulitazama upesi ungelidhani ni jingine.

Basi akashuka kwenye ghorofa hilo na punde, akashika chumba fulani kisicho na tija, humo akapanda juu na ndani ya muda mfupi akashukia ndani ya chumba chake.

Japo mwanamke huyo alikuwa amevalia viatu vya visigino virefu, sauti haikutoka hata punje. Kila kitu kilikuwa kimya kimya.

Basi akaendea chumbani, huko akapenyeza mkono wake nyuma ya kabati na kupapasapapasa. Kidogo akashika kitu, akakivuta na kukitazama. Kilikuwa ni karatasi. Akashangaa. Hakuacha karatasi hapo.

Alipofungua karatasi hiyo akakutana na ujumbe ulioandikwa kwa marker pen nyekundu.

“Vitu vyako ninavyo. Nitafute.” baada ya ujumbe huo kulikuwa na namba za simu kwa chini.

“Shit! Shit! Shit!” Kelly akalaani kwa herufi kubwa. Alishika nywele zake kwanguvu akizinyongorota. Alipatwa na msongo wa mawazo upesi. Alianza kuhisi anawehuka.

Akarudi tena nyuma ya kabati na kupapasa, kweli hakukuwa na kitu! Inawezekanaje?

Tukio hilo likamfanya mwanamke huyu afanye ukaguzi wa eneo lake. Na asitafute sana akajikuta akiuona mwili wa mtu nyuma ya kochi. Alipoutazama mwili huo vema akagundua ni wa afisa polisi.

Kidogo akauona tena mwili mwingine. Ulikuwa unafanana tu na huo wa kwanza. Mwanamke huyo akajikuta akishusha pumzi ndefu.

Haraka akaendea glovu chumbani mwake kabatini, akajiveka na kuipima miili hiyo kwa mkono. Bado ilikuwa hema. Bado ilikuwa hai! Akastaajabu na hili. Mabwana hao wawili walikuwa wamepoteza fahamu wakiwa kwenye usingizi mzito sana. Hata mapigo yao ya moyo yalikuwa yanapiga kwa mbali.

Nani aliyewaziraisha?

Akaketi akiwaza. Aliyewatenda hao maafisa ndiye ambaye amebeba vitu vyake. Amejuaje kama vipo kule? Na kwanini avibebe?

“Marshall,” Kelly akajikuta akisema kwa sauti ya chini. “Ni Marshall. Hakuna mwingine!” upesi akatoa simu yake na kupiga zile namba, baada ya muda kidogo, simu ikapokelewa na sauti ya kiume.

“Naona umepata ujumbe wangu. Sasa njoo kwenye anwani ntakayokutumia,” sauti ikasema na kisha simu ikakata.

Kelly akatikisa kichwa.

“Nini hiki?”

Kidogo akasikia sauti za watu huko nje. Akashtuka. Alitupa macho yake ya tahadhari mlangoni.

Huko nje kulikuwa kuna maafisa wawili wa usalama. Maafisa hao walikuwa wamebebelea vikombe vya take-away vya kahawa. Walifungua mlango na kuzama ndani. Kelly alikuwa tayari ameshapotea!

Ni punde, wakaona miili ya wenzao chini.


**

“Serious?”

“Ndio, serious!” Kelly akasema akiwa anatembea. Mwendo wake ulikuwa ni wa haraka. Alikuwa anatazama nyuma mara kadhaa. “Sijajua nifanyeje? Anataka kuonana na mimi!”

Kukawa kimya.

“Nifanyeje?” Kelly akauliza. “Nime stuck kabisa. Kichwa kimegoma.”

“Nenda kaonane naye.”

“Serious?”

“Hakuna namna. Nenda kamskize anasemaje.”

Basi Kelly akakata simu na kutekeleza kile ambacho ameambiwa. Akatuma ujumbe kwenda kwenye ile namba kwamba yu njiani anakuja.

Kidogo akajipaki kwenye usafiri kuanza safari.


**

Alasiri …


“Kelly, mimi sina mengi sana ya kujua toka kwako isipokuwa yale maswali yangu ya mwanzoni,” aliema Marshall akimsogezea Kelly glasi ya maji. Eneo lilikuwa limetulia na watu wako tenge. Macho ya Marshall, Danielle na Jack yote yalikuwa yanamtazama Kelly.

Mwanamke huyo alikuwa ameketi kwenye kiti cha peke yake akiwa amekunja nne. Japo mwili wake ulikuwa umetulia, moyo wake ulikuwa unakita bum-bum-bum-bum kifuani.

“Naomba unikumbushe maswali hayo,” akasema Kelly.

“Sawa. Labda niyageuze na kuyafanya yawe ya moja kwa moja zaidi,” akasema Marshall na kuuliza, “Unamfanyia kazi nani?”

Kabla Kelly hajajibu swali hilo, simu yake ikaita. Alikuwa ni Marietta. Alipokea simu hiyo na kuiweka sikioni.

“Umefika?”

“Ndio.”

“Naomba niongee na Marshall.”

Kelly alidhani amesikia vibaya. Marietta akarudia tena ombi lake. Anataka aongee na Marshall.

Basi Marshall akapewa simu.
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA NNE) -- 01*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA
“Naomba unikumbushe maswali hayo,” akasema Kelly.
“Sawa. Labda niyageuze na kuyafanya yawe ya moja kwa moja zaidi,” akasema Marshall na kuuliza, “Unamfanyia kazi nani?”
Kabla Kelly hajajibu swali hilo, simu yake ikaita. Alikuwa ni Marietta. Alipokea simu hiyo na kuiweka sikioni.
“Umefika?”
“Ndio.”
“Naomba niongee na Marshall.”
Kelly alidhani amesikia vibaya. Marietta akarudia tena ombi lake. Anataka aongee na Marshall.
Basi Marshall akapewa simu.
ENDELEA
"Marshall," Marietta akaita, kisha akajitambulisha na baada ya hapo akamweleza Marshall juu ya namna gani mambo yalivyo. Yeye ni mke wa Raisi na angemtaka Marshall amruhusu Kelly aende Morocco kumsaidia kumkomboa Raisi.
"Najua nitakuwa nakuchanganya, Marshall. Mambo ni mengi muda ni mchache. Nitaeleza kila kitu nitakapopata muda."
Kidogo Marshall alikuwa amekanganyikiwa. Ina maana Marietta alikuwa anajua mahali ambapo Raisi yupo? Muda wote ule?
"Marshall, mimi ni mkosaji. Nataka tu nimkomboe mume wangu kabla ya kufa kwangu. Tafadhali."
Basi Marshall akakata kwanza simu. Akawaza kwa kitambo kidogo kabla ya kuwashirikisha wenzake juu ya kinachoendelea.
"Huko Morocco sehemu gani?" Marshall akamuuliza Kelly. Macho alikuwa ameyakaza kana kwamba mbogo aliyejeruhiwa.
"Morocco kwa mwana wa mfalme," akasema Kelly. "Anaitwa Abdulaziz na ndiye yeye aliyemteka Raisi akimtumia Marietta na wengineo."
"Kwahiyo una uhakika kuwa Raisi yupo huko?"
"Uhakika ni asilimia zote. Hapa ninapokuambia, tayari vita ya madaraka ya kifalme imekwisha anza. Abdulaziz alituita kwenda kumsaidiza, mimi pamoja na K. Lakini mimi sikuwa upande wake."
"Ndiyo maana ukamuua K?"
"Ndio. Ilibidi niwahi kummaliza kabla yeye hajanimaliza."
"Kwanini akumalize?"
"Kwasababu mimi na yeye tuna interest tofauti."
"Zipi hizo?"
"Mimi namtumikia Marietta. Yeye anamtumikia Abdulaziz."
Kukawa kimya kidogo. Ni kama vile watu walikuwa wamemezwa na bumbuwazi. Ilikuwa ngumu kuamini kinachotukia.
Walipofikiri baada ya muda kidogo na kujadiliana, Marshall akapiga simu kuongea na Marietta.
"Kama ni hivyo, nasi tunakuja huko," akaema maadhimio yao.
"Lakini Marshall, huku si salama. Na pia ikigundulikana kuna mkono wa Marekani itazorotesha mahusiano ya kidiplomasia," Marietta akatoa angalizo.
"Kama kungekuwa na haka ya kutunza mahusiano ya kidiplomasia, wasingemteka Raisi wetu. In fact, tunakuja huko kama genge na si watu waliotumwa na serikali ya Marekani.
Na kuhusu usalama, hilo lisikupe tabu. Tumeshazoea maisha hayo kiasi kwamba tukiyakosa, tunahisi kupungukiwa."
Kukawa kimya.
"Kwahiyo tumekubaliana?" Marshall akauliza.
"Ndio," Marietta akajibu. "Nitafanya namna ya kuwafikisha hapa," akaongezea na taarifa kabla ya kukata simu yake.
"Tujiandae," Marshall akawaambia wenzake. "Safari ya kwenda Morocco ipo njiani!"
Basi ndivyo muda ukaenda vivyo. Baadae, kama lisaa limoja lilipopita, Danielle akakutana na Marshall kando na kumweleza kumhusu bwana James. Bwana huyo amemfuata na kumtaka ampe ushahidi wote kumhusu Ian.
Kama asipofanya vivyo, basi ataruhusu picha alizowapiga zitumike kwenye upelelezi.
"Ametupata sehemu dhaifu hivi sasa," alisema Danielle. "Hatuna ujanja, Marshall. Ni lazima sasa tushirikiane naye."
Marshall akawaza kidogo. Akashusha pumzi ndefu na kuuliza, "Unavyoona itakuwa threat kwetu?"
"Sidhani," Danielle akajibu. "Kama ingekuwa threat basi angeshavujisha mpaka sasa."
"Sasa tunafanyaje?"
"Mimi nina wazo."
Marshall akamtazama Danielle. Macho yake yalikuwa yanauliza kuhusu wazo hilo.
"Inabidi tuwe karibu sasa na James."
"Serious?"
"Yah, Marshall. Serious. Kadiri James anavyokaa mbali nasi anaweza kutuumiza. Sasa kulidhoofisha hili yatupasa tukae naye karibu. Ni mtu mwenye lengo jema. Tunaweza pia kumtumia akatusafisha kila tunapoacha nyayo. Unaonaje?"
Marshall akafikiri kidogo. Ni kweli mawazo ya Danielle yalikuwa yanaleta 'sense' ndaniye, basi akaridhia kufanyika kwa kile alichosema.
"Lakini inabidi tuwe waangalifu sana, Danielle. Mtu yeyote anaweza akawa nyuma yako na kukuchoma kisu cha mgongo."
Danielle akatabasamu. Alikuwa amebeba agizo hilo.
Basi baadae ikiwa ni usiku wa saa nne, mwanamke huyo akasogeza gari lake mpaka mahali ambapo amekubaliana na James wakutanie. Hapo akazima gari na kuwasiliana na mlengwa wake kwa ujumbe.
Muda si mwingi, James akafika eneo husika akiwa amekuja na bwana Smith. Lakini hakuwa ameongozana na bwana huyo bali alimwacha kwenye gari.
"Umewahi!" Danielle akamkaribisha mwanaume huyo kwa tabasamu.
"Nashukuru, nilikuwa nipo tenge tangu tumekubaliana kukutana muda huu," akasema bwana James. Bwana huyo alikuwa amevalia suti kama ilivyo kawaida yake. Lakini mara hii nywele zake alikuwa amezilaza vema akiwa amezipaka nywele dawa kana kwamba mate.
Alipendeza.
Alimtazama Danielle na kumuuliza kama amekuja kama vile walivyokubaliana. Danielle kabla ya kujibu akatabasamu.
"Nawezaje kuja kama sipo kamili?"
Naye James akatabasamu. Ni punde Danielle akatoa bahasha ya kaki na kumkabidhi mwanaume huyo. James akatazama ndani na kisha akatabasam tena.
"Naweza nikakuamini?" Akauliza.
"Bila shaka," Danielle akamhakiki. Basi James akaweka bahasha hiyo ndani ya koti lake na kisha akatazama mbele kuangalia gari alilokuja nalo.
Kuna kitu alikuwa anawaza. Alishusha pumzi ndefu puani alafu akamtazama Danielle na kumuuliza, "Hamna kingine ungependa kunishiriki?"
Danielle akatikisa kichwa. "Hapana." Akamtazama mwanaume huyo akiwa anajiuliza kitu kichwani. "Kwanini umeniuliza vivyo?"
"Kwasababu nahisi una kingine."
"Mimi?"
"Ndio. Sikia Danielle, najua kuna mengi mtakuwa mnayafanya nyuma ya pazia. Sidhani kama itakuwa vema mtu mwingine akawa wa kwanza kuyaona kabla yangu. Itawaweka matatizoni."
Danielle akawa kama mtu aliyeganda. Alibaki kumtazama James.
"Ni sawa," akasema bwana James akishika kitasa cha gari. "Unajua wapi pa kunipata kama ukinihitaji." Aliposema hayo akaenda zake kwenda kukutana na Smith.
Kitendo cha kufunga gari lake, Danielle akaondoka zake. Wakamtazama mwanamke huyo akiishia.
"Vipi?" Smith akauliza. "Umefanikisha?"
James akawasha gari wakaenda zao.
**
Saa nne usiku ...
"Unahisi hapa tupo salama?" Aliuliza Marietta akimtazama Mahmoud.
"Yah! Kiasi chake," akajibu Mahmoud akitafuna. Mkononi alikuwa amebebelea mirungi kana kwamba majani ya kumlisha sungura. Zainab yeye alikuwa ameketi jikoni akipika.
Mazingira ya hapa yalikuwa pweke kiasi. Hakukuwa na nyumba nyingi, makazi machache yanayoweza kuhesabika. Makazi haya yalikuwa yanafanana kwa kiasi fulani kwenye muundo.
"Kiasi chake?" Marietta akauliza. "Una maana gani kiasi chake?"
Mahmoud akamtazama Marietta. Bado mwanaume huyo alikuwa anatafuna majani yake kana kwamba mbuzi.
"Kwakuwa bado tupo Morocco hamna mahali itakuwa salama kwetu kwa kiasi hicho unachotaka. Abdulaziz ana mkono mrefu. Cha kufanya ni kwenda mahali ambapo itamchukua angalau muda kupajua."
"Ndiyo hapa?" Marietta akauliza.
"Ndio, Shanny. Hujaridhika napo?"
Kabla Marietta hajajibu, Zainab akawa amefika na sinia lililobebelea vikombe vitatu vya kahawa. Akawapatia Mahmoud na Marietta kisha naye akachukua cha kwake na kuketi chini.
Mahmoud akamtazama mkewe alafu akatabasamu. Alikuwa anafurahi kumwona mkewe papo. Naye mkewe alitabasamu kabla hajamtazana Marietta na kumuuliza,
"Mmefikia wapi?"
"Pazuri. Kama mipango yangu ikienda vema basi keshokutwa watu watakuwepo hapa."
"Una hakika watakusaidia?"
"Sana. Nimepata ziada ya watu, watanisogeza sana. Nadhani mipango yetu itakaa sawa endapo wakifika hapa."
"Na vipi ule mpango Aziz?" Akauliza Zainab akimtazama Mahmoud. Mahmoud akabinua mdomo wake na kutafuna.
Mpango wa Aziz ulikuwa ni wa kumtafuta kaka yake na Mahmoud kwa ajili ya kumshawishi awe upande wao kumshinda Abdulaziz.
Aziz alikuwa ndiye 'crown prince', yaani mwana mfalme ambaye ndiye mwenye wakfu wa kuwa mfalme punde baba yake atakapochoka ama kufa.
Kiuhalisia Aziz alikuwa ni mwana mwenye nguvu kuliko wote. Karibia robo tatu ya jeshi yote ilikuwa chini yake, kutimiza jeshi lote ingempasa mpaka pale baba yake atakapofariki ama kuachia madaraka.
Basi mwana huyo kwakuwa ndiye ambaye anatazamia kupokea kijiti cha ufalme, ulinzi wake ni mkubwa. Si rahisi kumwingilia katika nyakati zote.
Ana ushawishi mkubwa ndani ya nchi kama kiongozi ajaye.
"Mke wangu," Mahmoud akaita akimtazama Zainab. "Unajua si rahisi kumpata Aziz. Mbali na mfalme yeye ndiye mtu anayelindwa zaidi. Jambo letu litachukua muda kidogo kutimia."
"Laaziz," Zainab akaita akiuweka mkono wake juu ya kiganja cha Mahmoud. "Hatuna muda wa kungoja sana. Ni ngumu kumpata Aziz maana hajajua adhma ya wito wako. Laiti angelijua basi ni yeye ndo' angekuwa anakutafuta."
"Saa tutafanyaje unadhani?"
"Tafuta namna ya kuwasiliana naye. Njia yoyote ile. Mwambie una ujumbe wake nyeti."
Mahmoud akashusha pumzi ndefu. Akamtazama Marietta na kumuuliza, "unasemaje, Shanny?"
"Yuko sawa. Nadhani tumtafute yule mpambe wake. Yeye atakuwa njia nyepesi kumwingilia Aziz."
Mahmoud akafikiri kidogo. Alikubaliana na wazo hilo lakini kulikuwa na tatizo kidogo.
"Sikuwa nataka kwenda huko kabisa. Si salama kwangu. Ilaa ..... sina budi, nitafanya tu."
"Lini?" Zainab akawahi kuuliza. Mahmoud akamshika mkono mwanamke huyo na kumtazama ndani ya macho. "Kesho ama keshokutwa."
Alipomaliza tu hiyo kauli, akasikia vishindo vya mtu. Kutazama malangoni, akamwona mwanaume fulani aliyekuwa amevalia kanzu na kichwa chake amekifumba kiremba.
Mwanaume huyo alikuwa ametoa macho, uso wake ulikuwa umebebelea hofu. Alishika kingo za mlango akaropoka, "wamefikaa!"
Mwanaume huyo alikuwa anavuja damu mgongoni kwa wingi. Kitendo tu cha kumalizia kusema kauli yake, ikasikika sauti kubwa paaaaah! Kisha mwanaume huyo akadondoka chini vumbi la damu likimwagika toka shingoni!
"Amka upesi upesi!!" Akafoka Mahmoud. Haraka akiongozana na Marietta na Zainab wakaenda chumbani ambapo huko walijifungia na mwanaume huyo akabonyeza kitufe fulani ukutani.
Kitufe hicho kikasafirisha habari kwenye vijumba vyote vilivyokuwapo maeneo hayo. Kukawa na mlio wa king'ora kana kwamba gari la polisi.
Na katika king'ora hicho zikasikika na sauti za risasi huku na kule. Zilikuwa zinarindima kana kwamba mvua! Wafuasi wa Mahmoud walikuwa wakipambana na wavamizi.
Basi Mahmoud akiwa ndani ya chumba, akafungua mlango wa andaki wakazama humo. Lilikuwa ni andaki refu kama chemba ya kusafirishia maji machafu.
Wakatembea humo kwa upesi Mahmoud akiwa amemshika mkono mke wake, Zainab. Kama baada ya hatua kadhaa, wakasikia sauti
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA NNE) -- 02*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA
Na katika king'ora hicho zikasikika na sauti za risasi huku na kule. Zilikuwa zinarindima kana kwamba mvua! Wafuasi wa Mahmoud walikuwa wakipambana na wavamizi.
Basi Mahmoud akiwa ndani ya chumba, akafungua mlango wa andaki wakazama humo. Lilikuwa ni andaki refu kama chemba ya kusafirishia maji machafu.
Wakatembea humo kwa upesi Mahmoud akiwa amemshika mkono mke wake, Zainab. Kama baada ya hatua kadhaa, wakasikia sauti ya vishindo vikuu ndani ya handaki!
ENDELEA
Ilikuwa ni tafrani! Iliwapasa wakimbie zaidi na zaidi kwa ajili ya kukomboa nafsi zao. Lakini ndani ya humo humo handaki kulikuwa na mahali na mahali, kidogo walipokimbia, Mahmoud akasimama mahali na kubandua kitu ukutani. Kulikuwa na kama kadroo hapo.
Mahmoud akachomoa bunduki humo, tatu kwa idadi, akamkabidhi kila mmoja wao silaha na kuwataka waikoki kwa ajili ya kujilinda.
Baada ya hapo wakaendelea tena kukimbia na kukimbia. Walipofika tena mahali fulani, sasa wakiwa wamekaribiwa zaidi na watu wanaowakimbiza, bwana Mahmoud akaendea tena ukuta.
Bwana huyu alikuwa na ramani yote ya handaki kichwani. Alikuwa anajua kila mahali na kwa kila hatua.
Hapo ukutani akafunua tena. Humo hakukuwa na silaha tena kama mwanzoni bali kulikuwa na kifaa fulani cha mstatili, kilikuwa cheusi kwa rangi.
Upesi Mahmoud akakifungua kifaa hicho na kubinya mahali, mara kifas hicho kikawaka na kuanza kuonyesha muda.
Kwa haraka Mahmoud, akabinyabinya vitufe kutunza muda. Aliweka dakika mbili tu. Wakaendelea kukimbia na basi sasa kile kifaa kikawa kinazidi kuongeza sauti kulia ikihesabu muda chini.
Punde muda ukawa umebakia sekunde thelathini. Kidogo tu, wakafika hapo wanaume watatu waliokuwa wamebebelea silaha kubwa.
Walitambua hapo kuna kifaa kinacholia kwani kilikuwa kinatoa mwanga. Walipotazama ukutani - doh! - Wakabaini walikuwa wamekawia. Muda ulikuwa umewaishia!
Lakini nani hukubali roho yake kutoka kwa urahisi? Basi mabwana hao wakakimbia kurudi walipotokea. Wasipige hata hatua nne, bomu likalipuka na kuwatupa haswa!!!
Si kuwatupa hai, hapana, vipandevipande vya nyama na damu. Lakini pia kama haitoshi moto ukashika humo ndani ya handaki kwenda pande zote.
Joto lilifukuta moto ukikimbia haswa.
Mahmoud na wenzake walikuwa bado hawajatoka humo ndani ya handaki. Mlango ulikuwa kama hatua thelathini toka walipo, bado walikuwa wanaendelea kukimbia!
Kwasababu ya bomu kulipuka humo, kulikuwa ma mtetemeko mkubwa na ilikuwa ni swala la muda tu kwa handaki zima kumomonyoka. Vumbi lilikuwa linateremka na pia vipandevipande vya mawe na vikokoto.
"Kimbia! Kimbia!" Alifoka Mahmoud akiongeza ukubwa wa hatuaze. Walikimbia sana. Walipobakiza hatua kama nane hivi kufikia lango, mara jiwe likaporomoka toka darini na kumkita Zainab kichwani! Tih!
Mwanamke huyo akadhoofu akipoteza fahamu! Alikuwa anatiririsha damu pomono kichwani. Ni punde tu hijab yake ikawa imetepeta damu!
"Zainab!" Mahmoud akaita akiwa anamtazama mkewe. Alihofia sana uhai wa mwenza wake. Macho yake yalimezwa na hofu, woga.
"Mahmoud twende!" Marietta akasihi. Alimvuta mwanaume huyo waende kwani hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya humo. Joto ni kali na pia handaki lilikuwa linaelekea kumomonyoka.
"Twende la sivyo tutakufa humu! Twendee!!" Marietta akaendelea kusihi. Mahmoud akanyanyuka na akiwa amembebelea mkewe akasonga wakikwepa mawe na mitaro ya vumbi iliyokuwa inatiririka toka juu.
Walifikia lango wakakwea na kwenda nje. Walikuwa wametokea mahali ambapo palikuwa pametulia na pia pametingwa na msitu mkubwa.
Hapo Mahmoud akamlaza mkewe chini akimtazama kwa huruma. Mwanamke huyo alikuwa ametulia kana kwamba maji mtungini.
Basi alichokifanya Mahmoud ni kufungua hijab ya mkewe na kuifungia jerahani kisha akamtaka Marietta abaki hapo ingali yeye akienda kutafuta dawa hata ya mizizi.
Mwanaume huyo akatoka upesi kuelekea mashariki. Alikuwa anakimbia huku akitupa macho yake huku na kule.
Mpaka kuja kuona anachokitaka, ikawa imemchukua kama dakika sita hivi. Aliuendea mti lengwa alafu hapo akakata tawi na kuanza kulitumia kufukulia ardhi.
Alifukua na kufukua mpaka kukuta mzizi. Akaung'ata na kuchomoa vipande alivyokuwa anavihitaji - vitatu kwa idadi!
Mizizi hiyo ilikuwa michungu haswa. Na mbali tu na hivyo baada ya muda kidogo ilipoozesha kinywa cha Mahmoud kwa muda. Hakuwa anauhisi ulimi wake tena.
Basi haraka akarudi kule alipowaacha wenziwe, ikamchukua kama dakika sita. Alipofika hakukuta mtu!!
Akatahamaki.
Akatazama kushoto na kulia kwake. Kidogo akahisi mlio wa risasi ukimpitia. Upesi akajificha nyuma ya mti kwa ajili ya usalama wake.
Hapo akahema kwanguvu. Alihema kwa hofu lakini pia kwa kuchoka. Alijiuliza mkewe na Marietta watakuwa wapi akakosa kabisa majibu.
Watakuwa hai ama watakuwa wameuawa? Alichomoza uso kuchungulia lakini kabla hajafanya jambo risasi ikatupwa upande wake! Upesi akarudisha uso kujificha.
Moyo wake ulikuwa unakita ti-ti! Ti-ti! Ti-ti!
Mawazo yake yote yalikuwa kwa mkewe. Kama yeye anawindwa hivi, mkewe huko atakuwa salama ukizingatia hali yake.
Kidogo akasikia risasi zikirindima kwa kama sekunde tano mfululizo! Hapo naye akachungulia kujua kinachoendelea, mkononi akiwa ameshikilia bunduki yake.
Kwa mbali kidogo akamwona mwanaume akikimbia. Alikuwa ni mwanajeshi. Mkononi mwake alikuwa amebebelea silaha. Alikuwa ndiye yule mwanaume aliyekuwa anamfyatulia risasi Mahmoud.
Basi upesi Mahmoud akatoka hapo mtini na kuanza kumfukuza mwanaume yule. Alikimbia haswa. Kidogo akawa anamkaribia karibu na karibu.
Ghafla mwanaume huyo akageuka nyuma, kabla hajafanya kitu, Mahmoud akamtupia rizasi na kumfanya mwanaume huyo awe 'helpless' chini.
Alikuwa anavuja damu tu.
Mahmoud akamjongea mwanaume huyo na kumuuliza, "mke wangu yuko wapi?"
Alimkwida mwanajeshi huyo kwa nguvu. Alikuwa akimtikisatikisa kana kwamba kibuyu. Lakini mtu anayekufa anawezaje kuongea? Mwanajeshi huyo alikuwa anamimina damu mdomoni kwa wingi.
Macho yalikuwa yamemtoka kwenda kifoni.
"Mke wangu yupo wapi???" Mahmoud akaendelea kufoka. Kidogo tu mwanajeshi huyo akafa.
"Shit!" Mahmoud akalaani. Akautupia mzoga huo pembeni kisha akaendelea kukimbia kwenda kule mwanajeshi yule alipokuwa anaenda.
Akiwa anaenda akawa anaita jina la mkewe na pia la Shanny. Kidogo ndipo akakutana na walengwa wake, Marietta alikuwa amejilaza kando na mto, Zainab akiwa amepoa kabisa.
"Shanny, nini kimetokea?" Mahmoud alifoka kuuliza huku akimkimbilia mkewe. Alipomfikia akamshika na kumuita mara kadhaa.
"Ilibidi tukimbie. Maadui walikuwa wanatuwinda!" alisema Marietta.
"Maadui gani?" Mahmoud akauliza. Marietta akanyooshea kidole upande wake wa magharibi. Huko Mahmoud alipotazama akaona miili minne ya wanaume ikiwa imelala mfu.
"Samahani, Mahmoud. Nimeshindwa kumsaidia Zainab."
Machozi yakaanza kummiminika Mahmoud mashavuni. Zainab alikuwa amekufa! Mwili wake ulikuwa unaelekea kuwa wa baridi.
"Hapana!" Mahmoud akalia. "Hapana, Zainab! Hapanaa!!" Akalia kwa sauti kuu. Lakini wasidumu hapo kwa muda mrefu, wakasikia watu wakija.
Hawakuwa na muda bali kuondoka hapo upesi.
Lakini Mahmoud alikuwa amebebelea kinyongo kikubwa kifuani mwake. Alikuwa anahisi kifua chake ni kizito sana. Uzito kuliko mwili wa mkewe ambao ameubeba mgongoni.

**

Baada ya risasi moja kupiga, mtu alidondoka chini kana kwamba gogo. Abdulaziz alimtazama mtu huyo ambaye sasa alishakuwa marehemu akatoa agizo mwili huo ukatupiwe mbali.
Basi wakaja wanaume wawili ambao waliuburuza mwili huo kwenda nao nje. Sakafu ikiwa inajaa damu.
Walipotoweka, Abdulaziz akakaa kitako akiwa analaani. Akiwa anatusi. Alikuwa amekwazika. Jasho jembamba lilikuwa linamchuruza kwenye paji la uso.
Macho yake yalikuwa mekundu haswa.
"Jamal, mara hii sitau hawa washenzi wako. Nitakumaliza wewe!!" Abdulaziz akafoka akimtazama Jamal.
Jamal alikuwa amekaa kama mbwa mwitu aliyepokonywa nyama.

**
Siku mbili baada ...

Wimbi kubwa lilipiga chombo na kukiyumbisha haswa. Marshall aliyekuwa amelala kwenye chumba kidogo akaamka na kuangaza. Kidogo alikuwa aanguke toka kitandani.
Alinyanyuka na kuangaza namna chombo chao kinavyoyumba. Ikachukua kama sekunde thelathini chombo hicho kutulia.
Basi Marshall akatoka ndani ya chumba chake na kwenda koridoni. Akashika kingo ya boti na kutazama maji. Ilikuwa ni usiku. Maji yalikuwa yamechafukwa kiasi chake!
Chombo kilikuwa kinaenda juu na kurudi chini ... chini tena na juu kwa kadiri mawimbi yalivyokuwa yanakwenda.
Upepo nao haukuwa haba. Ulikuwa unapuliza sana.
Basi Marshall akiwa hapo akasikia mtu akitapika. Akajikuta akipata hamu ya kujua, akasonga kutazama chumba kinachofuata, huko akamkuta Jack akiwa anatapikia kwenye mfuko. Tumbo lilimvuruga.
Kajasho chembamba kalikuwa kanamchuruza.
Marshall akiwa hapo anamtazama mwenzake, kabla hata hawajazungumza kitu, akastaajabu mwanga unammulika. Alipogeuza shingo yake kutazama, akaona boti kubwa umbali wa kama kilomita moja toka walipo.
Mara kidogo sauti toka kwenye kipaza sauti ikapaza kwanguvu,
"Mpo kwenye mpaka wa maji wa Morocco. Ninyi ni wakina nani?? Jitambulisheni na mtuonyeshe nyaraka zenu upesi!!"
Marshall akang'ata lips yake ya chini kisha akasema, "oh God! Mbona mapema hivi?"

**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA NNE) -- 03*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Basi Marshall akiwa hapo akasikia mtu akitapika. Akajikuta akipata hamu ya kujua, akasonga kutazama chumba kinachofuata, huko akamkuta Jack akiwa anatapikia kwenye mfuko. Tumbo lilimvuruga.
Kajasho chembamba kalikuwa kanamchuruza.
Marshall akiwa hapo anamtazama mwenzake, kabla hata hawajazungumza kitu, akastaajabu mwanga unammulika. Alipogeuza shingo yake kutazama, akaona boti kubwa umbali wa kama kilomita moja toka walipo.
Mara kidogo sauti toka kwenye kipaza sauti ikapaza kwanguvu,
"Mpo kwenye mpaka wa maji wa Morocco. Ninyi ni wakina nani?? Jitambulisheni na mtuonyeshe nyaraka zenu upesi!!"
Marshall akang'ata lips yake ya chini kisha akasema, "oh God! Mbona mapema hivi?"

ENDELEA
Marshall aliwaza cha kufanya na punde akaona ni vema akawataarifu wenzake kuhusu tukio hilo, lakini kabla hajafanya vivyo akabaini wenzake tayari wameshatoka ndani kutazama.

Watu hao walikuwa ni watatu kwa idadi: Kelly, Danielle na Jack. Wote walikuwa wametoa macho wakijaribu kuelewa kuna nini kinachoendelea. Kidogo Kelly akasafisha koo lake kama ishara alafu akasema,

“Acha niongee nao. I can handle this.”

“Sure?” Marshall akapata shaka kidogo. Alimtazama Kelly anavyosonga karibu naye.

“Yah! Si mara ya kwanza nafanya hivi,” akasema Kelly kwa kujiamini. Akasonga karibu kabisa na kushika kingo ya boti akitazama wale wageni wao. Muda si mrefu mwanamke huyo akakutana na hao wageni kwenye boti yao, boti ya serikali.

Ilikuwa ni boti kubwa yenye maafisa kama kumi na tano kwa idadi. Wawili walikuwa ni manahodha, wengine watatu wakiwa ni watu wanaohusika na ufundi na wengineo waliobaki wakiwa ni kama walinzi. Hao ndo walikuwa wamebebelea bunduki na wapo tenge kwa lolote litakalotokea!

Basi Kelly akiwa anatembea kwa madaha, akasonga mpaka kwa ‘captain’ wa boti na kumweleza kidogo kumhusu. Mwanamke huyo alijitambulisha kwa kusema kuwa yeye ni moja wa washiriki wa bwana Abdulaziz, mwana wa mfalme.

“Bila shaka mimi si mgeni machoni mwako,” alisema Kelly akimtazama captain kwa kurembua. Captain akatabasamu kidogo, akamtazama mwanamke huyo na kumwambia, “ngoja!” kisha mwanaume huyo akaenda zake ndani kufanya mawasiliano.

Kelly hakuwa na hofu. Haikuwa mara yake ya kwanza kukumbana na kadhia kama hiyo. Akiwa amerelax akangoja kwa kama dakika tatu kabla ya captain hajaja na kumwambia,

“Sijapata uhakiki wake.”

“Una maana gani hujapata uhakikiki wake?” Kelly akauliza upesi.

“Simu haijapokelewa kwahiyo hatuwezi kuwaruhusu,” akasema captain kisha akatoa ishara kwa watu wake wa usalama, wale waliobebelea bunduki, punde mabwana hao wakafuata wakina Marshall na kuwaweka chini ya ulinzi.

Wakawaamuru waende kwenye boti yao, nao walengwa wakatii.

“Hamuwezi kutufanyia hivi!” akasema Kelly akikunja sura. “Punde Abdulaziz atakapojua mlichofanya mtakuwa mahali pabaya.”

Hakuna aliyemsikiliza, wakasweka ndani ya chumba fulani na kufungiwa humo kwa komeo. Ndani kulikuwa ni kiza. Boti likawashwa na kutimka kuendelea na doria katika usiku huo.

“Sasa tunafanyaje?” akauliza Marshall. Alikuwa haonekani bali kusikika tu. Kwa mbali sauti ya mawimbi ilikuwa inasikika yakiwa yanakatwa na ncha ya boti.

“Tungoje kwanza,” akasema Kelly. “Nadhani hatuna haja ya kutumia nguvu hapa.”

“Tutangoja mpaka muda gani?” Danielle akauliza. “Endapo jua likichomoza itakuwa ni hatari zaidi kwetu.”

“Jua halitachomoza,” akasema Kelly kwa kujiamini. “Muda si mrefu Abdulaziz atapiga.”

“Lakini ulisema wewe haumfanyii kazi bwana Abdulaziz,” Jack akatia neno.

“Ndio, lakini bwana Abdulaziz hatambui hilo,” akasema Kelly. Basi wakangoja humo kwenye boti kwa kama robo saa, kimya. Wakaendelea kuvuta subra.

Ilipopita dakika ishirini na tano, sasa hata Kelly na yeye akaanza kupata wasiwasi na ukimya ule, akanyanyuka aende kugonga mlango asikizwe. Kabla hajafika, mara boti ikayumba na kumdondosha chini! Puh!

Boti ikayumba na kuyumba kwa muda kidogo kiasi kwamba akashindwa kabisa kusimama. Bahari haikuwa shwari.

Hawakukaa sana mara maji yakaanza kuzama humo ndani! Boti ilikuwa inayumba sana kwa sasa! Mawimbi yalikuwa makubwa na upepo nao ulichachamaa.

Boti ilipelekwa kushoto na kulia, juu na chini! Marshall pamoja na wenzake wakawa wanagongana na kuvamiana wakitupwa huku na kule.

“Inabidi tufanye jambo!” akasema Marshall. “La sivyo tutakufa humu!”

Ni wazi moja ya madirisha yaliyokuwa kwa chini humo chumbani yalikuwa yamepasuka. Maji yalikuwa yanazama ndani kila mara boti unavyoyumba!

Kidogokidogo yalikuwa yanaongezeka!

Punde kidogo mara king’ora kikaanza kulia. Boti ilikuwa imefungiwa mtambo wa kutambua hitilafu ya kuzamia kwa maji chomboni. Basi upesi wale mabwana wanaohusika na ufundi wakaanza kufanya namna kukabiliana na hatari hiyo.

Kidogo ndipo wakabaini tatizo. Ni chumba cha chini!

Basi upesi wakafungua mlango na kuanza kufanya marekebisho! Lakini haikuwa rahisi hata kidogo. Bado boti ilikuwa inayumbayumba kupelekeshwa na mawimbi. Utulivu ulikuwa ni mgumu kupatikana.

Kuna muda bwana mmoja akajikuta akitupwa na kwenda kujikita ukutani, akapoteza fahamu papo hapo! Mwingine naye almanusura kudondoka kama isingalikuwa kujishikiza na nguzo.

“Mmekamilisha?” akauliza captain. Akiwa amekaa karibu na usukani alikuwa amejishikza asiyumbe. Kulikuwa na sauti kubwa ya king’ora kwenye ‘system’ kumjulisha kwamba boti halipo salama.

Alama ya tone la maji lenye rangi nyekundu ilikuwa inamwekamweka chini ya usukani wake.

“Bado, hali si nzuri kabisa!” sauti ikamjibu toka kwenye ‘radio call’ ya boti. “hatupati utulivu wa kufanya kazi kabisa!”

“Fanyeni upesi!” captain akafoka. “Hatuna muda mrefu hapa. Mpaka chombo kiz--” wimbi kubwa likachapa kioo cha mbele kabisa ya boti na kufanya chombo hicho kisimame karibia na kubinukia huko nyuma!

Wimbi lilipopita, boti likarudi chini kwanguvu! Maji yakaruka juu na kuifunika boti hiyo kana kwamba mvua! Ni kheri boti ilisimama japo kwa mrama.

Upande wa kushoto wa uso wa Captain ulikuwa unavuja damu. Alikuwa amechoka. Bega lake pia la kulia lilikuwa linamvuta kwa maumivu makali. Akashika chombo cha mawasiliano na kuuliza,

“Mmekamilisha? --- mmekamilisha?”

Akatambua kifaa hicho hakikuwa kinafanya kazi tena. Maji yalikuwa yanachuruza toka ndani yake. Akatupia kifaa hicho chini na kujaribu kusonga aende kuangalia kinachoendelea.

Akamtaka mwenzake ashikilie usukani kurudisha chombo nchi kavu mara moja ingali yeye akitazama usalama.

Akafika kule chumbani, japo kwa shida, akakuta chumba kikiwa kimejawa na maji mengi! Akamulika na kurunzi asione mtu yoyote humo.

Akaita. Kimya.

Kidogo akatambua kuwa kuna sauti inatokea upande mwingine. Alipoenda kutazama, akakuta watu wake wakiwa chini, wanne kwa idadi! Na upande wa kushoto wa kile chumba kilichokuwa kimejaa maji, pia kulikuwa kunapenyeza maji kwa vingi vilevile!

Hajakaa muda mrefu pia akatambua kuwa boti haikuwa inakwenda kama vile alivyomuachia maagizo captain mwenzake! Kwa muda kidogo akashindwa kujua cha kufanya.

Tih!!! maji yakachapa tena boti! Mara hii yalipiga kwanguvu sana kiasi kwamba captain hakuweza kumudu kujizuia. Alitupiwa ukutani na akapoteza fahamu mara moja!

“Boti inazama! Narudia, boti inazama!” ilikuwa sauti ya captain aliyeachwa kwenye usukani. Hakuwa na kingine cha kufanya kuokoa chombo chao. Akiwa anaongozana na wenzake kadhaa wakanyofoa maboya na kujivika kisha wakatumbukia ndani ya maji.

Hata hawakuwakumbuka wenzao.

Walipookoa nafsi zao ndipo wakaanza kuulizana juu ya wengine.

“Watakuwa wamekufa!” mmoja akasema. Alikuwa ameshikilia boya na huku pia ameshika bunduki, bunduki iliyojawa na kushiba maji.

“Vipi tukaenda kuwatazama?” mmoja akauliza, lakini uso wake haukuwa unaonyesha kama kweli anamaanisha alichosema.

“Tutaendaje kwenye boti inayozama?” akauliza mwingine. Kabla ya yule aliyetoa wazo hajaongezea neno, akahisi jambo. Alibinyabinya boya lake kisha akawatazama wenzake kwa macho ya mshangao na kusema,

“Nahisi boya langu linapungua upepo!”

Wenzake nao walipotazama yao, wakagundua wote walikuwa kwenye mkondo mmoja. Hawajakaa sawa, wakafunikwa na wimbi kubwa lenye urefu wa nchi zisizopungua kumi na tano!

Bwaaaah!!


**


“Umefanya vema!” akasema Kelly akimgusa bega Marshall. Mwanamke huyo alikuwa ametoka kuchungulia kwenye vioo vya hadubini. “Hawataweza kudumu baharini. Watakufa kama wenzao!”

Marshall akamtazama Kelly, mwanamke huyo hakukaa nao sana akaelekea ndani ya chumba. “Sasa tunaweza kuendelea na safari yetu,” ikawa ndo kauli ya mwisho ya Kelly kabla hajaufunga mlango.

Kidogo kukawa kimya kwa mazungumzo. Danielle alimtazama Marshall kisha akamuuliza, “Una uhakika huyu ni mtu wa kumuamini?”

Wakati akiwa anauliza vivyo alikuwa anatazama mlango alimozama mwanamke huyo.

“Hatuna budi kuwa naye,” akasema Marshall. “Yeye ndo njia pekee ya kumpata Marietta, na hatimaye Raisi.”

Marshall aliposema hivyo akawaacha wenzake hapo na kwenda kule alimo Kelly. Alifungua mlango na kuangaza, akamkuta mwanamke huyo anatapikia kwenye mfuko.

“Nawe umeanza kutapika?” Marshall akauliza. “Nilidhani ni mzoefu!”

Kelly akauweka mfuko kando kisha akajifuta mdomo wake kwa mgongo wa kiganja. Akamtazama Marshall kisha akatazama chini na kuvuta hewa ndefu kwa pua yake nyembamba.

“Ni nini unataka Marshall?”

“Sikaribishwi?”

Marshall akasonga karibu na mwanamke huyo. Akamtazama kidogo na kumuuliza, “Kwanini Abdulaziz alitoa amri uuawe?”

Kelly akabinua mdomo wake. Akajifuta tena na mgongo wa kiganja chake na kutulia.

“Kuna tatizo lolote? Tujuze. Unajua tupo pamoja kwenye hili.”

Mara boti ikayumba kwanguvu! Ni kheri walikuwa wamejishikiza. Angalu boti ilivyotuliatulia, Kelly akamtazama Marshall na kumwambia kwa sauti ya chini,

“Sijui ni nini kinatokea. Huenda Abdulaziz akawa ameshamshtukia Marietta.”

“Kivipi? - ulisema yeye hajui kama unamtumikia?”

“Sijui, Marshall! Nami nipo njia panda kama wewe. Tutakapofika nchi kavu nitawasiliana na Marietta nipate kujua.”

Kukawa kimya.

“ … Pengine Captain alimwambia tupo zaidi ya idadi,” Kelly akaongezea maneno. Mara hii Marshall akawa kimya kumtazama Kelly kwa umakini. Mwanamke huyo alikuwa anaonekana hayuko sawa. Uso wake ulikuwa kielelezo.

“Kelly, kuna shida yoyote?”

Kimya.

“Kelly, unaweza uka-share nasi. Tupo kwenye boti moja.”

Kelly akamtazama Marshall usoni. Macho yake yalikuwa yamelegea kiasi. Mdomo wake ulikuwa wazi akihema.

“Nataka tu kuwa mwenyewe, Marshall. Hilo tu.”

Marshall akanyanyuka.

“Tutaonana baadae!”


**


Saa kumi na moja asubuhi …


“Nasemaje! --” Abdulaziz akafoka. “Sitaki kusikia mtu yeyote amegusa nchi kavutokea huko baharini isipokuwa kwa bandari pekee!” mate yalikuwa yanamruka toka kinywani. Macho yalikuwa yamemtoka.

“Ongezeni walinz bandarini na pwani yote!” aliposema hayo akapachika simu mezani. Akang’ata meno yake na kunyanyua tena simu kumpigia Jamal.

“Bado!!” alifoka haswa. “Jamal, Jamal, kama hao watu hawatapatikana kwa siku ya leo. Utafute mahali pa kujifichia. La sivyo ni----” simu ikakata -- tiii-tiiii!

“Pumbavu!” akatusi. Akaweka namba tena na kupiga. Namna alivyokuwa anabonyeza namba hizo ni kana kwamba anataka kutoboa simu.

Simu ikaita pasipo kupokelewa. Akatusi na kutusi kupita kiasi.

**

“Jamal, anachosema Mahmoud kina ukwel wowote?”

Kwenye sebule hii ya kifahari walikuwapo watu wanne: wa kwanza alikuwa ni Aziz, crown prince, pili bwana Mahmoud, tatu Jamal na nne mpambe wa Aziz, bwana Ramadan.

Aziz, mwana wa mfalme anayeandaliwa kupokea madaraka, alikuwa amevalia kanzu yenye darizi za dhahabu. Mkono wake wa kushoto ulikuwa na saa aghali mno. Miguuni alikuwa amevaa sendozi zilizosanifiwa kwa ngozi ya simba.

Kitendo cha bwana Mahmoud kuwapo hapa, kulikuwa ni kumaanisha kuwa mpango wa ule wa bwana Aziz waliokuwa wameuadhimia ulikuwa umetimia.

Mahmoud alifanikiwa kuonana na bwana Ramadan na kumpa kila ‘sumu’. naye bwana Ramadan, akitaka kuonekana mtu mtenda kazi, akafikisha habari upesi kwa ulimi wake. Sasa alikuwa hapa akitazama kwa macho yake makubwa namna mambo yanavyoenda.

“Ni kweli kabisa,” akasema Jamal. “Abdulaziz anataka madaraka yako kwa njia yoyote ile. Na hapa tuongeapo, anamshikilia bwana yule wa Marekani akilenga kumtumia kama ushawishi kwenye kikao cha hadhara.”

Basi bwana Aziz kusikia hayo, akaamuru Abdulaziz akamatwe mara moja na aletwe mbele yake upesi!

**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA NNE) -- 04*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Kitendo cha bwana Mahmoud kuwapo hapa, kulikuwa ni kumaanisha kuwa mpango wa ule wa bwana Aziz waliokuwa wameuadhimia ulikuwa umetimia.

Mahmoud alifanikiwa kuonana na bwana Ramadan na kumpa kila ‘sumu’. naye bwana Ramadan, akitaka kuonekana mtu mtenda kazi, akafikisha habari upesi kwa ulimi wake. Sasa alikuwa hapa akitazama kwa macho yake makubwa namna mambo yanavyoenda.

“Ni kweli kabisa,” akasema Jamal. “Abdulaziz anataka madaraka yako kwa njia yoyote ile. Na hapa tuongeapo, anamshikilia bwana yule wa Marekani akilenga kumtumia kama ushawishi kwenye kikao cha hadhara.”

Basi bwana Aziz kusikia hayo, akaamuru Abdulaziz akamatwe mara moja na aletwe mbele yake upesi!

ENDELEA

Baada ya lisaa limoja tangu kikao kihairishwe …

“Kama haya yote yakija kuwa kweli, basi utakuwa na nafasi kubwa sana,” alisema bwana Ramadan. Kinywa chake kilikuwa wazi kwa furaha. Macho yake yalikuwa yamebebelea ahadi.

Ingawa akiwa anaongea, alikuwa ameweka mkono wake kwenye bega la Mahmoud. Walikuwa wapo koridoni wakitembea pasi na haraka.

“Unasema kweli?” Mahmoud akauliza. Uso wake ulikuwa unaonyesha anajua jibu. Alikuwa anasanifu.

“Kweli kabisa!” Ramadan akaapa kwa kuchinja shingo yake na kidole. “Nasema kweli tupu, kweli kabisa, Mahmoud! Umekuwa rafiki yangu sasa, tutasaidiana sana mbeleni. Vivyo ndo’ maisha yalivyo!”

Wakapeana mikono.

“Tutaonana muda si mrefu, Ramadan,” Mahmoud akasema akitikisa kichwa.

“Insha-allah. Hakikisha unakuwa karibu na mawasiliano.”

“Bila shaka.”

Basi Mahmoud akaenda zake. Kwa usalama wake akawa amekabidhiwa wanaume wawili wa kumlinda. Walikuwa wamebebelea bunduki wakivalia sare za jeshi. Wanaume hao akaongozana nao kwa kama nusu njia kabla hajawataka waende zao kumwacha peke yake.

“Una uhakika?”

“Yah. Nitakuwa salama, nashukuru.”

Mahmoud akaendelea na safari yake akitumia usafiri wa umma. Alipokuwa chomboni, akapigiwa na Marietta. Punde akapokea na kuweka simu sikioni.

“Wamefika,” sauti ya Marietta iliteta kwenye simu.

“Umeshaonana nao?”

“Hapana. Ndo nafanya namna hivi sasa.”

“Sawa. Utanambia kitakachotokea.”

“Wewe upo wapi?”

“Njiani. Nadhani kila kitu kimeenda sawa.”

Simu ikakata.

Mahmoud akaendelea na safari yake. baada ya mwendo wa kama lisaa hivi, mara gari likasimama. Kulikuwa na foleni hapo ndefu kidogo.

Kwa mbele kidogo barabarani kulikuwa na kizingiti. Magari yalikuwa hayapiti hapo pasipo ukaguzi. Hapo kwenye kizingiti walikuwapo wanajeshi kama nane kwa idadi. Walikuwa wamebebelea bunduki na nyuso zao zikiwa ni za kazi.

Haikuwa inafahamika nini wanachokisaka.

Basi muda kidogo tu ukapita hapo, kwa kupitia maneno ya watu ndani ya basi bwana Mahmoud akatambua kuwa msako huo ulikuwa umeanza jana yake na hakuna mtu anayetambua haswa ni nini mabwana hao wanachokitafuta.

Wanachokifanya ni kukagua ndani ya gari na pia sehemu ya mizigo. Huwataka watu wanyooshe nyuso zao juu na hata kutoa vitambulisho vyao vya uraia mara moja.

Endapo kama mtu ni mgeni basi atahojiwa kwa muda mchache kabla ya kuachiwa huru.

Basi likasonga kidogo mbele. Bwana Mahmoud akawa anajiuliza kichwani mwake juu ya msako ule. Kwakuwa alikuwa ameketi dirishani, basi akachomoza kichwa chake na kuangaza.

Akaona namna ambavyo wanajeshi wanavyowashusha watu kwenye baadhi ya magari na pia wanavyopekenyua kila kona ya usafiri. Kidogo akapata shaka.

Kichwani mwake akaanza kuunda mawazo ambayo yalimtaarifu kuwa hayuko salama. Hivyo kidogo akanyanyuka na kuanza kusonga kuelekea mlangoni. Akashuka toka kwenye gari na kutazama kule mbele kwenye kizingiti.

Pasipo kurejesha tena uso huko, akayeya zake!

Lakini mmoja wa mabwana wale waliokuwa wanahusika na kulinda pale kwenye kizingiti, alimwona bwana Mahmoud akiwa anatembea kwa kasi kwenda mbali zaidi na walipo.

Basi akamshtua na kumjuza mwenzake. Upesi mwanajeshi aliyekuwa amebebelea kipaza sauti akatupa sauti yake kumtaka huyo mwanaume asimame mara moja hapohapo alipo!

Mahmoud asijali, akaongeza mwendo maardufu! Na isipite muda akaanza kukimbia kwa kadiri ya miguu yake. Alishikilia kanzu yake akikata mitaa haswa.

Baada ya kama dakika moja tu, magari mawili ya jeshi yakaanza kumfukuza. Ilikuwa ni jijini. Haikuwa rahisi sana kwa magari kupenya baadhi ya maeneo ambayo Mahmoud aliyakatiza.

Na kwa kutumia nafasi hiyo Mahmoud akajibana kwenye uchochoro na kutulia hapo tuli. Punde gari lililobeba wanajeshi likakatiza kwenye barabara ya mbele likiwa linaenda kwa mwendo wa wastani.

Wanaume wawili walikuwa wanarusha macho yao kumtafuta mlengwa lakini hawakufanikiwa. Mahmoud alikuwa amejibana kana kwamba mtoto mdogo nyuma kidogo ya ndoo ya kuhifadhia takataka!

Gari lilipopita, akatoka papo na kuchungulia. Alipoona hewara, akachoropoka kukimbilia mbali zaidi.


**

Zii-ziii-ziiii! Zii-ziii-ziiii! Simu ilinguruma kwenye mfuko wa Marietta. Mwanamke huyo alikuwa amevalia nikabu nyeusi akiacha macho peke yake kuonekana.

Alisimama akachomoa simu yake mfukoni na kutazama. Alikuwa ni Mahmoud.

“Kuwa makini, wanajeshi wametapakaa ndani ya jiji,” Mahmoud alitahadharisha.

“Wa upande gani?” Marietta akauliza. Macho yake yalikuwa yanatazama kukagua usalama.

“Sijajua wa upande gani lakini si salama kukutwa na wa upande wowote ule kwa sasa.”

“Nilidhani umeyaweka sawa na Aziz!” Marietta alinong’ona akikazana.

“Shanny, hamna mtu anayejua kuhusu wageni wako. Ulitaka nisemeje kuwahusu?”

“Sawa. Nikukute wapi?”

“Ngome ya zamani,” Mahmoud akajibu na simu ikakatwa. Marietta akaendelea na safari. Muda kidogo akakutana na wageni wake ndani ya boti, Marshall na wengineo. Wakaungana kwa pamoja kuchukua taksi kuwapeleka kule kwenye ‘Ngome ya zamani’ kama ambavyo Mahmoud alivyoagiza.

“Poleni, ilikuwa bahari rafu sana. Natumai mpo salama. Karibuni Morocco,” alisema Marietta kwa sauti. Taksi ikaenda kidogo kwenye lami kabla ya Marshall kuulizia usalama wao ndani ya jiji.

“Ilikuwa almanusura huko baharini. Hawakutaka kuelewa wala kuskiza. Laiti tusingekuwa na plan ya pili basi kazi nzima ingeishia huko,” alisema Kelly.

Marietta akatabasamu kidogo, ungeweza kuhisi tabasamu lake hilo kwa kutazama macho yake. Alitazama nyuma kwa kupitia ‘sight mirror’ - kioo kinachoning’inia kwenye paa la gari kisha akasema,

“Najua mngedumu. Msingeweza kufa upesi hivyo!”

“Ni nini kinatokea?” Kelly akadadisi. “Mbona walikuwa wakaidi?”

“Ni bayana kuna mpasuko hivi sasa. Unajua ni ngumu kuelewa kila kitu kinavyoendelea ndani ya nchi kwa sasa. Jambo hili linaweza likawa jema kwetu kama tukilifanya likatunufaisha!”

“Kivipi?” Marshall akauliza.

“Ngoja tuone,” akajibu Marietta. “Hapa si sehemu sahihi kuzungumza.” akisema vivyo akamtupia jicho dereva.

Basi taksi ikaendelea kusonga.

Wakatembea kwa kama dakika nane kabla ya taksi kujikuta lipo kwenye foleni. Ilikuwa ni foleni ndefu kiasi. Ilikuwa pia ni ya ukaguzi!

Marietta akatazama kwa mbele na kubaini uwepo wa wanajeshi wawili wenye silaha. Wanajeshi hao walikuwa wanapita kutazama gari moja baada ya jingine. Kwa magari makubwa walikuwa wanazama ndani na kwa yale madogo basi wakiinamisha kichwa kuangaza.

Alipotazama nyuma, hakukuwa tena na nafasi ya kutoka. Tayari magari matano yalishaweka uzio nyuma ya taksi!

“Dereva, hatuwezi tukachoropokea njia ya kurudi?” Marietta akauliza. Macho yake yalikuwa hayatulii. Alishahisi ukosefu wa amani ndani ya nafsi yake!

Dereva akamtazama kwa mshangao kidogo,

“Tutarudije?” akauliza na kuongeza, “Unaona njia ya kurudi ilivyojaa alafu mbele kuna ukaguzi!”

“Tafuta namna!” Marietta akabweka. Macho yake yalitoka kumtazama dereva kwa kitisho.

Lakini kiuhalisia hakukuwa na namna hapa. Upande wao wa kushoto ulikuwa unapitiwa na watu wengi wanaotumia miguu. Upande wao wa kulia kwenye njia ya kurufi pia kulikuwa kumetingwa na magari mengi.

Dereva angelifanyaje?

“Namna gani madam? Nitapita wapi hapa? Nitapaa?”

Marshall akatazamana na Danielle kisha na Jack. Vifua vyao vilikuwa an fukuto kiasi.

Mara Marietta akatoa bunduki na kumwonyeshea dereva, kisha akafoka,

“Utafanya nitakachokuambia, sawa!?”

Dereva akahofu sana. Pumzi yake ilibadili kasi na mikono yake ikatetemeka. Hakuwa anajua cha kufanya. Lakini pengine hakuwa na haja ya kujua cha kufanya kwani angelipewa maelekezo na ‘mtekaji’ wake.

“Sawa!” akasema akitikisa kichwa. “Sawa, sawa, nitafanya!”

“Haya geuza gari upesi turudi tulipotoka!” Marietta akaamuru.

“Hapana!” Marshall akapaza sauti. “Hamna haja ya kufanya vivyo.”

“Tufanyeje?” Marietta akamtazama mwanaume huyo kwa maulizo.

“Hataweza kugeuza gari kabla hatujakamatwa,” akasema Marshall. “Nyuma kuna gari ipo karibu mno, na mbele pia. Akiwa anahangaika kutoka tutakamatwa kwa upesi zaidi!”

“Sasa tufanyeje?” Marietta akapaza. “Tukae hapa kungoja kukamatwa?”

“Ni salama zaidi wakija kuliko tukitoroka hapa,” Marshall akapendekeza, “Wapo wawili, tunaweza kuwamudu kama kukiwa na ulazima huo!”

Kabla Marietta hajafanya jambo, akamtazama Danielle, Jack na kisha Kelly. Akatazama na mbele yao. Wanajeshi walikuwa magari matatu tu mbali na wao.

Akashusha pumzi na kutulia. Damu ilikuwa inazunguka kwa wepesi mwilini.

Baada ya kama dakika sita, mwanajeshi mmoja akawa ameshafika kwenye dirisha la gari yao. Bwana huyo akainama na kutazama waliomo ndani.

Dereva alikuwa anachuruza jasho haswa. Macho yake alikuwa ameyakodoa na pumzi yake iko ‘marathon’. Ukimtazaa vidole vyake vya mkononi, vilikuwa vinatetemeka!

“Hey, uko sawa?” afisa akamuuliza dereva. Dereva akatikisa kichwa pasipo kusema jambo.

“Afisa, mimi ni mwongoza watalii,” akasema Marietta, “Hawa ni wageni wetu tokea Uingereza nikiwaonyesha mandhari ya jiji letu.”

Afisa akawatazama tena Marshall na wenzake kisha akarejesha macho yake kwa Marietta.

“Fungua nikuone uso wako!” akaamuru.

“Hapana, afisa. Siwezi nikafanya vivyo,” alisema Marietta. Alijua fika angeacha uso wake bayana basi angetiliwa shaka. Hakuna mtu asiyejua uso wa mke wa Raisi, ama tuseme wa aliyewahi kuwa Raisi wa Marekani.

“Nimesema fungua nikuone. Sitarudia mara mbili!” afisa akafoka. Basi taratibu Marietta akaupeleka mkono wake kwenye bunduki.


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA NNE) --- 05*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Afisa akawatazama tena Marshall na wenzake kisha akarejesha macho yake kwa Marietta.

“Fungua nikuone uso wako!” akaamuru.

“Hapana, afisa. Siwezi nikafanya vivyo,” alisema Marietta. Alijua fika angeacha uso wake bayana basi angetiliwa shaka. Hakuna mtu asiyejua uso wa mke wa Raisi, ama tuseme wa aliyewahi kuwa Raisi wa Marekani.

“Nimesema fungua nikuone. Sitarudia mara mbili!” afisa akafoka. Basi taratibu Marietta akaupeleka mkono wake kwenye bunduki.

ENDELEA

Kabla hajafanya jambo basi bwana yule mwanajeshi akajikuta akipokea muito toka kwenye ‘radio call’. ilikuwa ni sauti nzito kidogo na ilikuwa inasikika vema toka kwenye chombo.

“Sitisha mara moja zoezi hilo!” sauti ilisema toka kwenye radio call. “Narudia, sitisha mara moja zoezi hilo!”

Ilikuwa ni agizo toka kwa mkuu! Nani atabisha? Basi upesi bwana huyo mwanajeshi akasitisha zoezi lake na kwenda kukutana na mwenzake kumpasha habari.

Tunatakiwa kusitisha zoezi letu mara moja!

Hiyo ikawa salama ya Marietta na watu wake. Na basi watu hao wakaelekea moja kwa moja kule kwenye ‘Ngome’ ambapo ndipo Mahmoud alipomwelekeza mwanamke huyo.

Huko kulikuwa ni jumba fulani lililotekelezwa. Jumba hili lilikuwa ni kuukuu haswa.

“Kama nilivyokueleza, Aziz ameshatoa amri ya kukamatwa kwa Abdulaziz hivyo tungoje tuone itakavyokuwa,” akasema Mhmoud.

“Hapana!” Marietta akatikisa kichwa. “Huu ndo muda wa kufanya kazi yetu inavyotakiwa Mahmoud. Wakati hawa ndugu wakiwa wamekorofishana. Haufikirii vivyo?”

Mawazo hayo ya Marietta yakaungwa mkono na wote. Sasa ni wafanye namna kumkomboa mume wa Marietta katika muda huo.

“Sasa tutampatia wapi?” akauliza Marshall. Hapo hata Marietta akamtazama Mahmoud. Ni yeye ndo’ alikuwa na taarifa zaidi kuhusiana na hilo.

“Kuna sehemu mbili nipadhaniapo. Moja kwenye makazi yake ya zamani, pili kwenye makazi yake mapya. Hamna sehemu nyingine anaweza mficha mtu zaidi ya hapo.”

“Una uhakika?” Danielle akauliza. “Kama ni moja ya kiongozi mkubwa si kwamba atakuwa ana maeneo kadha wa kadha?”

“Ni kweli lakini Abdulaziz si mtu wa kujiamini sana na watu wanaomzunguka. Huamini mikono yake kuliko ya mtu mwingine. Huko nilipotaja ni sehemu bora zaidi kuanzia.”

Wakakubaliana kufanya kazi hiyo kesho punde pale jua litakapozama. Ni misheni kubwa inayofanyika mahali penye ulinzi mkali hivyo yawapasa kujipanga haswa.

“Nna hoja,” akasema Danielle. “Kama Abdulaziz akikamatwa na Aziz kama ambavyo imedhamiriwa, si kwamba itakuwa hatari zaidi kwetu kumpata mlengwa wetu? Hamwoni kama Aziz anaweza kutumia nafasi hiyo kujinufaisha?”

Hoja hiyo ikazua maneno miongoni mwao. Ilikuwa na kweli ndani yake. Habari inaweza ikabadilika kabisa punde Aziz atakapomweka Abdulaziz mikononi. Hakuna aliyekuwa na uhakika na masaa machache mbele yao.

Vipi Aziz akitumia mwamvuli huo kwenye mvua hii?

Sasa?

“Tutafanya leo usiku,” akasema Marietta. Akamtazama Mahmoud na kumuuliza, “Sawa?”

Mahmoud akashusha pumzi ndefu asiseme jambo.


**

Ndani ya usiku huu mambo hayakuwa madogo. Bwana Marshall pamoja na wenzake walikuwa tayari wameshasonga kwenye eneo la tukio, makazi ya bwana Abdulaziz, kwa ajili ya kutekeleza kazi yao.

Kwa ujumla alikuwapo Kelly, Danielle, Marietta, Mahmoud na Marshall mwenyewe. Watu hawa walikuwa kwenye gari umbali mfupi tu toka kwenye kasri ya mlengwa wao.

Walishavalia nguo za kazi na vifaa pia wanavyo. Walibebelea bunduki na kwa mkono wake bwana Mahmoud alikuwa ameshatengeneza gesi ya sumu kwa ajili ya kazi.

Gesi hiyo alikuwa ameihifadhi kwenye mtungi mkubwa mweusi. Mtungi huo haukua wenyewe, lah! Kulikuwa pia na mitungi mingine minne, yani kwa kila mmoja.

Basi punde wakavaa vinyago vya kujikinga na madhara ya sumu kisha wakashuka wote isipokuwa Mahmoud. Yeye aliacha kwenye usukani. Watu hao kwa utulivu wakajongea zaidi na zaidi kufuata eneo walilolenga.

Ndani ya kasri …

Bwana mmoja mlinzi aliyekuwa amevalia nguo za jeshi alikuwa yu kwenye zamu. Bwana huyo alikuwa na mustachi mpana na mrefu. Macho yake yalikuwa ya kufumba na mwendo wake ulikuwa mpana ndani ya buti.

Alisonga akitazamatazama usalama. Uso wake ulikuwa wa kazi haswa. Nyuma yake kwa kama hatua kumi na tano alikuwa amesimama mwenzake pia kuhakikisha usalama.

Basi bwana huyu mwenye mustachi akaendea kona na kuikata. Ilikuwa ni ubavuni wa mashariki wa kasri Alipotembea kidogo akahisi harufu fulani asiyojua inatokea wapi.

Akavutavuta harufu hiyo akijitahidi kuitambua ni ya nini, mara kidogo akadondoka chini kama mzigo, akaachama kinywa na macho akayarembua.

Yule mwenzake aliyekuwa nyuma yake kwa hatua kadhaa naye akasonga mbele zaidi akielekea upande alodondokea mwenzake. Hakuwa na hili wala lile.

Alipiga hatua kujongea konani lakini kabla hajafika akahisi harufu pia. Hakuwa anajua harufu hiyo ni ya nini. Alipomaliza kona akamwona mwenzake akiwa yu chini!

Upesi akachomoa ‘radio call’ yake atoe taarifa lakini kabla hajafanya hilo akajikuta akiishiwa nguvu! Macho nayo yanapoteza uwezo wa kuona. Kidogo akadondoka chini kama mwenzake na akawa kimya tuli!

Basi zikapita dakika kadhaa. Harufu ile ikazidi kusambaa ndani ya makazi. Taratibu lakini kwa uhakika. Watu waliokuwa wamejifunika vinyago vya kujizuiza walikuwa wana ‘pump’ gesi toka kwenye mitungi yao mgongoni!

Ndani ya kasri, kwa juu kabisa, kulikuwa na wanaume walinzi wawili ambao nao walikuwa wanafanya doria ya kuhakikisha usalama. Mabwana hao walipotazama chini wakabaini kuna wenzao walikuwa wamejilaza chini.

Walijaribu kuwasiliana nao kuona nini tatizo lakini hakukuwa na mrejesho. Ingali bado hawajatambua vema ni nini kinachoendelea, ukizingatia mabwana hao hawakuwa wanaathirika na gesi ya sumu huko juu, wakadhamiria kutoa taarifa mbali zaidi kuhusu tukio hilo.

Lahaula! Kabla nao hawajafanya jambo wakatunguliwa na risasi. Risasi ya masafa ya mbali.

Risasi hiyo ilitumwa na mwanaume Mahmoud aliyekuwa ameketi ndani ya gari kwa kutumia bunduki ya mdunguaji. Bunduki yenye kioo cha hadubini kali inayoweza kuvuta vitu vya mbali kwa ukaribu bora kabisa.

Basi ndani ya dakika kumi na tano tu, kasri nzima ikawa ndani ya himaya ya wavamizi. Walikuwa wameshika kila pembe walinzi wakiwa hoi chini.

Marshall pamoja na wenzake wakakagua chumba kimoja baada ya kingine kumtafuta ‘mtu wao’. Kwenye moja ya chumba kilichopo chini kabisa. Chini. Huko wakakuta mabaki tu ya nguo lakini kusiwe na mtu,

“Hayupo hapa!” akasema Marietta. Kwakuwa alikuwa amejivika kinyago, sauti yake ilikuwa ya kunguruma. “Upesi tutoke na kwenda mahali pengine!”

Sasa wakatoka humo ndani upesi. Wakatembea makoridoni na kupita milangoni wakiwaruka wajakazi waliokuwa chini na pia walinzi waliokuwa hoi.

Walipofika kwenye gari wakajipaki na Marietta akamtaka Mahmoud awapeleke kwenye eneo la pili. Huko wakaendeleze msako.

“Hata Abdulaziz hayupo?” akauliza Mahmoud.

“Hayupo,” Marietta akajibu. “Nyumba nzima imekaliwa na walinzi na pia vijakazi!”

Mahmoud akatia neno, “Hata wale walinzi si wa Abdulaziz. Watakuwa wametumwa hapo na Aziz kutazama usalama!”

Basi wakatimka.


**



“Naomba uniletee kahawa hivi sasa!” alisema Azizi akimwagiza kijakazi. Bwana huyo alikuwa amekunja nne akiwa ameketi kwenye kiti chake cha thamani. Alikuwa amevalia suruali nyeusi maridadi na shati jeupe la dizaini ya kupendeza.

Begani upande wa kulia kulikuwa na michirizi mekundu mitatu iliyoshuka mpaka kifuani mwake, na kwenye kola ya shati kulikuwa kumedariziwa na rangi ya kijani.

Rangi hizo zilikuwa zinawakilisha bendera ya Morocco.

Mbele yake alikuwa ameketi mpambe wake, bwana Ramadan. Bwana huyo alikuwa amevalia kanzu ya njano iliyofifia na kizibao cheusi pamoja na kofia yake.

Meza ndogo ya kioo iliyokuwa mbele yao ilikuwa tupu.

“Nashindwa kuelewa shida ni nini?” akasema bwana Aziz. “Mpaka sasa hivi Abdulaziz hajapatikana. Hii si ishara nzuri kabisa.”

“Usijali, mwana mfalme. Abdulaziz atatapatapa tu lakini mwisho wake ni uleule. Kama si hivyo basi ataishi maisha yake kama digidigi. Hamna haja ya kuhofia kabisa!”

“We unadhani atakuwa wapi kwa sasa? - kwenye makazi yake yote hakuwapo!”

“Atakuwa anarandaranda huko kwengine. Lakini yatupasa tuwe makini sana. Kuna namna Abdulaziz akawa anapata maneo haya. Najua jeshini kuna watu ambao ni watiifu kwake, watu wa kutoka upande wa kabila la mama yake.”

“Unataka kusema Jamal?”

“Hapana. Jamal yu tayari upande wetu lakini kuna watu wengine mbali na yeye.”

Aziz akaguna. Akakuna kidevu chake na kuwaza kidogo.

“Unajua sitaweza kukaa kwa amani mpaka bwana huyo atakapokuwa mikononi mwangu. Kila muda unavyosonga nahisi kuna jambo.”

Ramadan akatabasamu.

“Jambo gani mwana wa mfalme? Hakuna kitakachotokea kipya. Abdulaziz hana nguvu kama yako kwa watu na wala serikalini.”

“Unadhani vivyo?”

“Ndio. Hata wewe unalijua hilo.”

Basi kidogo mlango ukafunguliwa na mmoja wa watu wa usalama. Bwana huyo alikuwa amevalia sare za jeshi na mkononi alikuwa amebebelea bunduki - SMG. Bwana huyo akampasha Azizi kuhusu yale yalotokea kule kwenye kasri la Abdulaziz.

“ … watu wote wapo hoi. Wanapata shida kuhema na miili yao imekuwa ya baridi kana kwamba barafu!”

Haabri hizo zikamchanganya sana Aziz. Mawazo yake yalitambua kuwa ni mdogo wake ndiye aliyafanya hayo. Ameua watu wake!

Basi akakung’uta ngumi nzito mezani mpaka kuivunja.

“Nalijua haya!” akafoka. Akanyanyua simu yake na kumtaarifu Jamal kwamba anamtaka Abdulaziz haraka! Haraka iwezekanavyo kabla hajasababisha maafa mengine.

Aliposema hayo akashika kiuno kwa mkono wake wa kulia wa kushoto akiweka tama. Alimezwa na mawazo.

Punde kidogo akaingia bwana aliyebebelea sinia lenye vikombe vya kahawa. Meza haikuwapo. Bwana huyo aliyekuwa amejawa na ndevu akarusha macho yake huku na kule asitambue la kufanya.

Alipotaka kuondoka afanye mbadala mwingine, Aziz akamwita na kumtaka ampatie kahawa yake mkononi.

“Muda wote huo mlikuwa mnafanya nini?” Aziz akauliza kwa hasira, akagida kinywaji chake na kuweka kikombe chini.

“Nenda sasa!” akamwambia mhudumu. “Wangoja nini hapa?”

Lakini mhudumu hakwenda. Badala yake akasimama hapo kumtazama Aziz. Naye Aziz alipomtazama vema mhudumu huyo akatambua machoye hayakuwa mageni.

Ngoja …

Yalikuwa ni macho ya Abdulaziz!

**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA NNE) --- 06*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Alipotaka kuondoka afanye mbadala mwingine, Aziz akamwita na kumtaka ampatie kahawa yake mkononi.

“Muda wote huo mlikuwa mnafanya nini?” Aziz akauliza kwa hasira, akagida kinywaji chake na kuweka kikombe chini.

“Nenda sasa!” akamwambia mhudumu. “Wangoja nini hapa?”

Lakini mhudumu hakwenda. Badala yake akasimama hapo kumtazama Aziz. Naye Aziz alipomtazama vema mhudumu huyo akatambua machoye hayakuwa mageni.

Ngoja …

Yalikuwa ni macho ya Abdulaziz!

ENDELEA

Hakika moyo wake ukapiga fundo kubwa akitaharuki. Mlango ulifungwa na Abdulaziz akatoa bunduki na kuwaweka chini ya ulinzi Aziz na Ramadan.

“Mtatulia kama maji mtungini na basi haya yote yataisha vema. La sivyo, maiti zenu zitaokotwa msituni. Ni kheri kama zikikutwa na binadamu kabla ya wanyama.”

Basi Aziz na Ramadan wakatii amri. Hawakuwa na la kufanya na wala nguvu zao hazikuwa na msaada mahali hapo.

“Wewe ni shetani!” Aziz akafoka. “Uroho wa madaraka ndo unakufanya uwe mnyama kiasi hiki?”

Abdulaziz akatabasamu. “Nadhani umesahau, Aziz. Mimi na wewe ni watu tofauti kabisa. Siwezi nikakubali wewe ukae kwenye kiti ilhali nipo hai.”

Kusikia maneno hayo, Aziz akamtemea mate Abdulaziz na kufoka kumtusi. Akimlaani na kumtupia maneno makali. Basi kidogo tu, Abdulaziz akakoki bunduki yake na kutungua kichwa cha kaka yake.

Aziz akalala mfu!

“Nisamehe!” Ramadan akabweka. “Nisamehe, naomba usiniue!”

Bwana huyo alikuwa anatetemeka kweli. Moyo wake ulikuwa unakita haswa. Alikuwa anatokwa na jasho akiwazia kifo. Abdulaziz akamtazama bwana huyo na kisha akaketi kitini.

Kuna jambo alikuwa analiwaza. Alikuna kichwa chake kwa bunduki yake alafu akamuuliza Ramadan maswali kadhaa kuwahusu Marietta na wenziwe.

“Kama unataka uendelee kuhema, basi yakupasa ufanye kama ninavyokuagiza,” akasema Abdulaziz. Huko nje watu walikuwa wakiendelea na mambo yao kama kawaida. Hawakuwa wanajua kinachoendelea ndani kwani Abdulaziz alitumia kiwamba cha kumeza sauti kwenye mdomo wa bunduki alotumia.

“Sawa!” akabwatuka Ramadan. Alitazama mwili wa Aziz uliokuwapo chini ukiwa hauna uhai akachanganyikiwa zaidi. Alikuwa anahofia sana. Kama angeendelea kuwapo kwenye hali hiyo basi angejikojolea si muda.

“Usidhani kunidanganya kabisa. Ukifanya hivyo utajikuta unakufa na kuacha familia yako.”

Baada ya vithisho hivyo bwana Abdulaziz akampatia Ramadan kazi ya kufanya na kumpa onyo kabisa kwamba familia yake itakuwa chini ya uangalizi mpaka pale atakapomaliza kazi.

**

Saa moja jioni …


Kila mtu ndani ya kasri alishafahamu kwamba Aziz amefariki dunia. Japo bado habari hiyo haikuwa imevuja kwenda popote pale. Ilikuwa ni habari ya simanzi sana na kila mmoja aliyekuwapo hapo kundini alikuwa ameguswa nayo kwa kiasi kikubwa, ilikuwa ni tishio kwa ajira zao.

Lakini mbali na hapo Aziz alikuwa ni mtu ambaye aongea na kila mmoja. Kiongozi ambaye hakuwa na makuu wala karaha. Japo ni vijakazi lakini walifurahia uwepo wake kasrini na walitarajia makubwa zaidi endapo bwana huyo ngeingia madarakani.

Sasa inakuaje?

“Inabidi tufikishe taarifa kwa mfalme. Hatuwezi liweka hili zaidi!” alisema kiongozi mkubwa wa wajakazi wa kasri. Bwana huyo alikuwa ni mnene lakini asiye na kitambi. Kichwa chake kilikuwa kimefunikwa na kofia nyekundu yenye utepe mweusi.

“Lakini yatupasa tuwe makini sana,” akasema bwana mwingine, yeye alikuwa naibu wa yule kiongozi mkuu wa vijakazi. “Kama tukilipeleka hili jambo upesi tunaweza kumuua Mfalme mara moja. Mnajua vema hali yake ilivyo. Ni mwezi sasa yupo hospitalini akisaidiwa na mashine.”

“Ni kweli,” akasema kijakazi mkubwa. “Lakini nina hofu sana juu ya hili. Litatuweka matatani haswa sisi vijakazi. Tutasema nani kamuua mwana wa mfalme?”


**


“Hamna kitu!” Marietta alisema akitikisa kichwa. Sasa walishasaka nyumba zote za Abdulaziz pasipo mafanikio. Hawakumwona mlengwa wao popote pale.

“Sasa tunafanyaje?” akauliza Kelly. “Hamna mtu mwenye makisio ya ziada?”

“Tutamfute Abdulaziz popote alipo!” akasema Marshall. “Kama tukimpata basi atatuelekeza wapi.”

“Si rahisi kumpata Abdulaziz kwa sasa,” Mahmoud naye akatia neno. “Anajua kuwa anatafutwa, unadhani atakuwa karibu?”

“Na vipi kuhusu familia yake?” akauliza Marshall. “Tunaweza kuitumia familia yake kama chambo cha kumpata!”

Wakiwa hapo wanaendelea kuteta, simu ya Mahmoud ikaita. Alipotazama akabaini ni Ramadan. Upesi akapokea.

“Tafadhali tuonane upesi.”

“Kuna nini?”

“Tukikutana tutaongea. Hakikisha mmekuja nyote.”

Bwana huyo akataja na mahali pa makutano kisha akakata simu. Mahmoud akawajuza wenzake juu ya makubaliano hayo na basi upesi wakaanza mkakati wa kwenda huko walipoelekezwa.

Wakiwa njiani, wamepakia taksi, wakasikia habari za kifo cha Aziz. Habari hizo zilikuwa zinatangazwa na kituo cha kuaminika cha redio, na kwa taarifa zaidi muuaji hakuwa bado amegundulikana.

Vijakazi wote wamewekwa chini ya ulinzi kwa mahojiano zaidi.

“Ni Abdulaziz!” akafoka bwana Mahmoud akibonda ‘dashboard’. Alipatwa na mawazo. Kama Aziz amekufa basi nini hatma yao na nchi kwa pamoja?

Mahali walipopakimbilia napo pamemezwa!

“Sasa tutafanyaje?” Marietta akauliza upesi. “Ndo’ maana Ramadan akataka kutuona?”

“Inawezekana,” Mahmoud akajibu. Hakuongezea neno jingine kwani alikuwa amebanwa na mawazo, alikuwa anafikiri kuliko kuteta. Alihisi kichwa kimekuwa cha moto.

“Lakini,” Danielle akapaza sauti yake. Yeye alikuwa ana hofu na Ramadan. Kwa mujibu wa akili yake aliona yawapasa kuwa makini kwani kama vijakazi wote wamewekwa chini ya ulinzi na tukio kubwa kama hilo limetokea, vipi kuhusu Ramadan?

Yeye alikuwapo wapi? Kama alikuwapo eneo la tukio, kitu ambacho kina asilimia kubwa, imekuaje yeye akanusurika na kifo?

Kwa muda kidogo gari likawa kimya. Watu walikuwa wamefumba vinywa vyao lakini akili zikiwa zinaongea na kupiga kelele.

Marshall akamtazama Danielle na kumuuliza,

“Wewe unawazaje?”

“Chochote kinaweza kutokea hapa,” Danielle akajibu. Marshall akaelewa ni nini mwanamke huyo anamaanisha, basi akajikuta akitabasamu na kutupia maneno kadhaa,

“Pengine njia imepatikana!”

**

Bwana Ramadan alitazama saa yake ya mkononi kisha akarusha macho yake barabarani. Juu ya ‘dashboard’ alikuwa ameweka kikombe cha ‘take away’ chenye kubebelea kahawa nyeusi ya moto.

Uso wake ulikuwa mzito na kwa kumtazama tu ungalijua yu shidani. Kahawa yake ambayo ameiweka kwenye dashboard hakuinywa hata kidogo.

Koo lake lingepitishaje kahawa hiyo ingali familia yake ikiwa kifungoni? Na bwana aliyekuwa anamtumikia miaka yote hiyo amekufa, tena mbele ya macho yake?

Aliegemeza kichwa chake kwenye kiti. Alitamani kulia lakini haikuwa sahihi. Aliporejesha macho yake barabarani ndipo akaona taksi ikiwa inakuja kwa mbali.

Akachukua simu yake kutuma ujumbe fulani upesi kisha akaweka simu yake mbali.

“Imetumwa ujumbe hivi sasa,” sauti ndogo ilisikika kwenye sikio la Marshall kwa kupitia kifaa sauti. Bwana huyo alikuwa anawasiliana na Jack ambaye alikuwapo nyumbani mbele ya kitu anachoweza kutumia kushinda vyote duniani: tarakilishi.

Mmarekani huyo mwenye asili ya China alikuwa tayari ameshadukua njia za mawasiliano ya Ramadan punde tu alipopewa namba na bwana Mahmoud muda si mrefu.

Sasa alikuwa anaona kila ujumbe na kusikia kila sauti atakapoongea.

“Unasemaje?” Marshall akauliza.

“Wameshafika,” Jack akamjibu na basi Marshall akatulia na kuwajuza wenzake. Punde taksi ikasimama, kulikuwa na umbali toka kwenye usafiri wa Ramadan, bwana Mahmoud akiongozana na Kelly na Marietta wakashuka toka kwenye gari na kumfuata Ramadan.

Walijikwea kwenye gari bwana Ramadan akilazimisha tabasamu usoni.

“Nafurahi mmeitikia wito wangu,” aliposema hayo akatazama ile taksi na kuuliza, “Hamna wengine?”

“Hapana. Ni sisi tu,” bwana Mahmoud akajibu.

“Mbona taksi haiondoki?”

Punde taksi ikageuza na kwenda. Ni kama vile ilisikia kile kilichosemwa. Taksi ilivyopotelea, kwa mbali yakaonekana magari mengine mawili. Kelly alitambua ujio wa magari hayo.

“Nadhani mmesikia habari za msiba. Hapa tuongeapo bwana Aziz ameaga dunia kwa kufyatuliwa na risasi kichwani … sina haja ya kuwaeleza nani muuaji, mnamfahamu vilivyo.”

Bwana huyo akaweka nukta kwa sekunde tatu. Wakati huo Mahmoud akafanikiwa kutazama nguo ya Ramadan na kubaini kuwa na mabaki ya damu upande wa kushoto wa kanzu yake.

“... Nimeumiza sana. Sikutaraji kama haya yangetokea,” akasema Ramadan jicho likiwa jekundu. Akatoa leso yake na kujipangusa. “Samahanini sana lakini jambo hili ni kubwa sana kwangu. Sijui nitalibebaje.” akavuta kamasi nyepesi puani na kuendea kwenye lengo lake sasa,

“Najua mahali alipo yule kiongozi. Nipo radhi kuwapeleka ili mkamuokoe kabla ya Abdulaziz hajatimiza adhma yake!”


**


“Sasa wanaanza kusogea,” sauti ilisikika kwenye sikio la Marshall. Ilikuwa ni sauti ya Jack aliyekuwa anatazama kioo cha mashine yake kutazama mwelekeo wa namba aliyoidukua.

Akawaelekeza wenzake mwelekeo kwa kutumia majina ya barabara na ncha za dira, upesi Marshall akamtaka dereva wa taksi aelekee huko maelekezo yanapotaja lakini kwa kutumia njia nyingine kuepusha kugundulikana upesi.

Kila walipotembea kwa muda fulani Jack akawa anawajuza zaidi na zaidi nao wakazidi kusonga kufuata maelezo. Walipokaribia na eneo la tukio wakawa wanapunguza mwendo kutoa nafasi ya usalama.

“Itakuwa wanaelekea jangwani,” sauti ya Jack ikasema kifaani.


**

Kelly alikunja shingo yake kutazama nyuma. Hakuyaona yale magari mawili tena na hakuwa anajua wapi yalielekea.

Alirusha macho zaidi asipate kitu. Kuangazangaza kwake kukamfanya Ramadan amtilie shaka. Alikuwa anamwona mwanake huyo kwenye ‘sight mirror’.

“Vipi? Kuna tatizo?”

“Hapana. Hamna!”

Wakaendelea kutembea. Kwa kama baada ya dakika sita, Kelly akayaona yale magari mawili kwa mbele. Kila moja lilikuwa limechipukia njia yake yakakutana kwenye njia kuu.

Mwanamke huyo akamtazama Marietta kwa macho ya ujumbe. Lips zake hazikusema jambo.

Aliporudisha macho yake mbele, akakutana na mboni za Ramadan kwenye ‘sight mirror’.


**
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom