*NYUMA YAKO (MSIMU WA NNE) --- 07*
*Simulizi za series*
*ILIPOISHIA*
Kelly alikunja shingo yake kutazama nyuma. Hakuyaona yale magari mawili tena na hakuwa anajua wapi yalielekea.
Alirusha macho zaidi asipate kitu. Kuangazangaza kwake kukamfanya Ramadan amtilie shaka. Alikuwa anamwona mwanake huyo kwenye ‘sight mirror’.
“Vipi? Kuna tatizo?”
“Hapana. Hamna!”
Wakaendelea kutembea. Kwa kama baada ya dakika sita, Kelly akayaona yale magari mawili kwa mbele. Kila moja lilikuwa limechipukia njia yake yakakutana kwenye njia kuu.
Mwanamke huyo akamtazama Marietta kwa macho ya ujumbe. Lips zake hazikusema jambo.
Aliporudisha macho yake mbele, akakutana na mboni za Ramadan kwenye ‘sight mirror’.
*ENDELEA*
Basi baada ya kitambo kifupi wakafika mahali ambapo Ramadan amewapeleka. Ilikuwa ni jangwani, makazi yalikuwa machache na kumetulia. Hapo kulikuwa na nyumba kubwa kiasi mithili ya kiwanda kwa umbo.
Humo ndo’ Ramadan akawaambia yu mlengwa wao.
“Siwezi kwenda huko, mnaweza kuingia sasa kwenda kuhakikisha wenyewe. Tafadhalini, hakikisheni mmemuua Abdulaziz kwa namna yoyote ile!!”
Basi wakashuka wakimwacha Ramadan kwenye gari, hata hawakumbughudhi, kidogo waliposonga Ramadan akapiga simu kutaarifu utendaji wake wa kazi.
“Nadhani nipo huru sasa!”
Walipoondoka naye akawasha gari yake na kutimka. Basi baada ya muda kidogo Mahmoud na wenzake wakawa wamezama ndani kwa tahadhari. Kama walivyotaraji, wakawekwa chini ya ulinzi na watu kumi waliokuwa wamebebelea bunduki kisha wakalazimishwa kunyamaa na kusalimisha silaha zao.
Walipofungwa, Abdulaziz akatokea akiwa anatabasamu pana. Akawatuhumu watu hao kwa ujinga na kudanganyika kiurahisi.
“Sikutaraji kama kazi hii ingekuwa nyepesi kiasi hiki,” akasema Abdulaziz kwa dhihaka. “Nalijua ningetumia rasilimali nyingi na muda. Kumbe ningejichosha tu!”
Aliposema hayo akamjongea Kelly na kumtazama kwa ukaribu. Alimshika mashavu mwanamke huyo na kumweleza;
“Samahani sana. Ulichagua upande usio sahihi! Ningalikusamehe ila umekawia sana kwa sasa.”
Pua ya Kelly ilikuwa inanusa mkono wa Abdulaziz. Mwanamke huyo alihisi harufu kali kiasi kwamba akalazimisha kuchoropoa kichwa chake toka kwenye mkono katili wa Abdulaziz. Alikuwa anahisi kutapika. Mkono ulikuwa unanuka damu!
Abdulaziz akadhihaki kila mmoja na mudawe kisha akaamuru watu hao wafungiwe ndani kwani hana haraka ya kuwamaliza. Huenda akapata matumizi yao hapo mbeleni.
Basi Mahmoud na wenzake wakatupiwa ndani ya chumba chenye mwanga hafifu. Madirisha madogo yalikuwa juu kabisa yakipitisha mwanga wa jua kwa kubagua.
Mara Marietta akamuuliza Kelly, “Vipi, umefanikiwa?”
“Ndio,” Kelly akajibu akitikisa kichwa. “Kila neno lake nimelirekodi vema.”
Kiunoni mwa mwanamke huyo kulikuwa na kifaa kidogo kilichokuwa kinanasa sauti.
“Sasa wale watakuja muda gani?” akauliza Mahmoud. Kidogo alikuwa ana shaka. Alijiuliza kama mule chumbani mtakuwa ndo hatma yao, lakini tofauti kabisa na yeye, Marietta alikuwa amejawa na imani. Hakuona haja ya kuhofia. Yeye alikuwa anajua wakina Marshall wata--
Mara wakasikia kishindo.
Huko nje wanaume walikuwa wameshadondoshwa kimyakimya. Tayari Marshall na Danielle walikuwa wameshafika ndani ya eneo na kufanya kazi kwa ustadi. Walikuwa wamelenga kufanya kila kitu ndani ya ukimya lakini ndani muda mfupi mpango wao huo ukafeli, iliwabidi watumie risasi kuwafyatulia baadhi ya walinzi waliokuwapo mbali haswa baada ya kuonekana.
Risasi zilitupwa haswa, Marshall na Danielle wakitumia ujuzi wao wa kijeshi wakakakwepa na kuwalenga walengwa kwa ufasaha. Ndani ya muda mfupi wakawa wameshikilia eneo hilo kwa ukubwa. Walikuwa wameshawamaliza maadui zao kwa kiasi kikubwa.
Basi wakasonga zaidi lakini kwa tahadhari sana. Bunduki zao zilikuwa zimebanwa vema mkononi na macho yao yamekodoa kuangaza.
“Mkuu, twende upesi! Tumezidiwa!” alikuwa ni mwanajeshi akimsihi bwana Abdulaziz aliyekuwapo ndani. Mwanajeshi huyo alikuwa ametokea nje hivyo anajua hali halisi. Kidogo bwana Abdulaziz akasita. Hakuamini kama ameshindwa. Alikuwa anaona kuondoka hapo ni kujidhalili na kujishusha.
Basi akiwa ametingwa na hasira, akakwapua bunduki yake na kunyanyuka aende kuwamaliza wakina Mahmoud kabla hawajakombolewa.
“Watawakuta wenzao wakiwa maiti!” akafoka akikoki silaha, lakini hakukuwa salama huko anapoenda. Kufikia kile chumba ingempasa apite mahali ambapo pangehatarisha maisha yake kama akionekana na adui.
Mmoja wa wajakazi wake akamtahadharisha kuhusu hilo. Hakutaka kusikia. Akarusha mguu wake kujiendea. Alipofika mahali pa wazi akatambua ni ngumu kukatiza hapo baada ya risasi mbili kutupwa aliponyoosha mguu.
“Shit!”
Alijaribu kutazama punde risasi ikapunyua ukuta, upesi akajirudi. Hakuwa na uhakika maadui walikuwa wangapi. Basi upesi akawarudia watu wake na kuwataka watimke upesi.
**
“Mko salama!” Marshall aliuliza akiwa anamfungua Mahmoud kamba. Danielle naye akainama kuwasaidia wengineo. Wote walikuwa salama.
“Mmemdhibiti Abdul?” Mahmoud akauliza.
“Hapana,” Marshall akamjibu, “Amefanikiwa kutoroka!”
Basi wakatoka hapo na kutokomea. Ndani ya masaa manne, wakitumia msaada wa maelezo toka kwa Jack Pyong, wakafanikiwa kumtia mikononi bwana Ramadan. Bwana huyo alikuwa anatorokea nchi jirani kujinusuru na kikombe cha kifo cha Aziz.
Pamoja naye ilikuwa familia yake: mke na watoto wawili.
“Sikufanya kwa kusudi!” akalia Ramadan. “Nisingefanya anachotaka basi anegeimaliza kabisa familia yangu. Sikuwa na namna nyingine. Niwieni radhi sana!”
Wakamtoa shaka. Hawakuwa na haja ya kumdhuru bali kumtumia. Kifo chake kisingewapa manufaa yoyote yale. Lakini zaidi walimsihi kwamba akifanya kazi kwa moyo wote basi hatolazimika kukimbia nchi, jina lake litakuwa safi kwa mdhalimu kuwekwa bayana.
“Unadhani itawezekana?” alikuwa ana mashaka. “Upande wote wa kabila lake sasa unamuunga mkono. Baba yake yu hoi kitandani na ndugu zake wengine hawana ushawishi kama ilivyokuwa kwake na kaka yake, Aziz.”
“Itawezekana,” akasema Danielle. “Hakuna lisilowezekana. Cha muhimu ni kujua wapi tutampata Abdulaziz. Nadhani unaweza kutusaidia kwenye hilo.”
“Bila shaka,” Ramadan akatikisa kichwa. “Nina huo uzoefu, najua karibia kila mahali ambapo kila kiongozi hufika ama kukaa.”
“Basi itakuwa vema,” Marshall akahitimisha kabla hawajaichukua familia ya bwana Ramadan na kutimka.
**
Saa kumi na mbili jioni …
“Unaweza ukaingia sasa,” alisema daktari punde baada ya kutoka ndani ya chumba. Hapo mulikuwa ni kasri kubwa ya mfalme. Daktari huyu bingwa wa magonjwa ya moyo alikuwapo hapa kwa muda akilipwa pesa ndefu kuzuia kifo cha mfalme wa Morocco. Ni kwa kitambo sasa yu hapa.
Basi baada ya kauli hiyo, Abdulaziz akaamka toka kitini nje na kuzama ndani kwenda kukutana na baba yake aliyekuwa amejilaza kwenye kitanda cha kifo. Mzee huyo akiwa hapo hakuwa anaona tena thamani ya uongozi wake wala pesa yake. Alikuwa mwenyewe.
Kitu pekee sasa anachokipigania kikiwa ni pumzi yake tu na vinginevyo. Ufalme wake haukuwa na msaada kwa wakati huo. Si pesa wala nafasi yake serikalini ingeweza kumrejesha kwenye afya yake isipokuwa Mungu peke yake aliyemuumba.
Basi Abdulaziz akaketi pembeni ya kitanda na kumshika baba yake mkono wa kuume.
“Baba,” akaita kwa sauti ya wastani. Kidogo baba akafungua macho yake kwa mbali kumtazama mwanaye. Mzee huyo alikuwa ameelemewa na mipira mwilini. Mdomo wake mkavu ulikuwa wazi. Kwa kumtazama tu ungelibaini hakuwa anasumbuliwa na moyo pekee, kuna mengine. Lakini hayo mengine yakiwa yamesababishwa ama kuchochewa na hili la moyo kwanza.
“Abdul…” baba akaita kwa mbali na kisha akajaribu kutabasamu. Sauti yake ilikuwa kavu. Alikuwa akitumia nguvu nyingi kuongea, lakini pia alikuwa na furaha kumwona mwanaye pembeni yake. Hakuona tabu kujitutumua.
“Abdul, kaka zako wanaendeleaje?” akauliza akijaribu kutabasamu. Abdul akamshika vema mkono wa baba yake na kunyamaza kwanza kwa kama sekunde nne. Alikuwa anawaza namna ya kujibu. Baada ya kupiga moyo konde akamweleza baba yake kwamba Aziz hayuko sawa.
Hadhani kama anaweza kubeba majukumu ya kuwa mfalme hapo siku za usoni.
Kidogo taarifa hiyo ikamshtua baba. Alikamata mkono wa Abdul kwanguvu kisha akahangaika kusema kwamba Aziz ndiye anayetakiwa kuwa mfalme. Ni yeye ndiye mwenye baraka naye hata kama akifa siku hiyo.
“Vipi kama Aziz akifa?” Abdul akauliza. Macho yake yalikuwa makavu kumtazama baba yake.
“Basi atatwaa Ilham,” baba akajibu kisha akauachia mkono wa Aziz. Aliona uchu ndani ya macho ya mtotowe. Akalia moyoni. “Abdul, hauwezi kuwa mfalme. Bado haujajiandaa,” baba akakoroma. Abdul asiseme jambo akanyanyuka zake na kwenda.
Baba akatiririsha chozi. Kidogo kifaa cha kusomea mapigo yake ya moyo kikaanza kwenda mrama.
Abdul alikaa nje ya chumba akitafakari. Muda si mrefu akampigia simu mmoja wa majamaa wake ndani ya jeshi kwa jina Masoud Saleh. Bwana huyo hakuwa mbali na alipo na Abdul, alikuwa tu chini ya jengo pamoja na wenzake hivyo upesi akaitikia wito. Alikuwa ni mwanaume mwenye mwili mrefu uliojaa. Alikuwa amevalia kombati na koti kwa juu.
Basi wakajadiliana na bwana huyo kwa muda wa kama nusu saa kabla Abdulaziz hajatikisa kichwa na kuchukua hatua kurejea tena ndani ya chumba alimo baba yake, lakini kabla hajafika daktari akamzuiza.
“Hali yake sio nzuri. Ngoja kidogo!”
Abdul hakutaka kungoja. Alimsukumia daktari pembeni akazama ndani. Alimkuta baba yake akiwa anavuja jasho, anatazama kwa kurembua kwa udhaifu.
Akaita,
“Baba.”
Baba yake akamwazima macho na masikio.
**
Saa mbili usiku …
Gari lilikuwa linaenda kwa kasi. Ndani yake upande wa dirishani kwenye viti vya nyuma Abdul alikuwa ameketi akiwa ameegemea dirisha. Alikuwa ana mawazo kichwani. Pembeni yake alikuwa ameketi bwana Masoud Saleh, mara kadhaa bwana huyo alikuwa akimtazama Abdul kisha asitie neno.
Nyuma yao kulikuwa na magari mawili na mbele pia magari mawili yakiwaongoza.
Baada ya muda kidogo, Abdul akamuuliza Masoud, “Sasa tunafanyaje?”
“Tumeshafanya kila kinachotakiwa kufanywa kwa sasa. Wadugu wote wapo korokoroni, pia na jamal. Ni kitendi cha kungoja muda tu.”
“Mpaka saa ngapi??”
“Sidhani kama mfalme atachukua muda. Mambo haya yatakuwa makubwa kuliko uwezo wa moyo wake,” Masoud aliposema vivyo kukawa kimya kidogo.
“Lakini lile tulilolifanya ni jema zaidi,” akasema bwana Masoud. “Kumwambia mfalme kwamba Wamarekani wamevamia nchi na kummaliza Aziz kutamfanya akupe ruhusa ya kuongoza jeshi zima. Hiyo ni habari njema kwetu.”
“Vipi kama akawapa ruhusa wengineo? Kama vile Ilham?”
“Atawapaje na wapo korokoroni? Amna chaguo lolote isipokuwa wewe tu.”
Kukawa tena kimya. Abdul alibiduabidua lips zake akiwaza. Wakasonga na safari yao lakini wasidumu muda mrefu tangu wakomeshe maongezi yao wakastaajabu gari imesimama.
“Kuna nini?” Abdul akawahi kuuliza.
“Kuna gari kwa mbele limeharibika!” dereva akajibu. Ni punde tu alikuwa amepokea taarifa hiyo toka kwa dereva wa gari ya mbele kabisa.
Wakasimama hapo kwa kama sekunde kumi.
Kidogo mlio wa risasi ukita mara nne!
***