*NYUMA YAKO (MSIMU WA TATU) -- 20 & 21*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"Asalaam aleykum!" Akasalimu kisha akaketi kitini.
"Umeniweka sana. Kulikuwa na shida?" Akauliza Marietta.
"Ndio, kulikuwa na tabu kidogo, Shanny, lakini nadhani sasa kila kitu kitakuwa poa," alisema Mahmoud. Sauti yake ilikuwa inatetema.
Basi kidogo Marietta na Mahmoud wakaondoka hapo na kwenda kujipaki kwenye gari kuondoka zao. Zainab akawatazama wakiyoyoma kisha akanyanyua mikono yake na kusema,
"Alhamdulillah!"
Akarudi zake ndani.
ENDELEA
Ndani ya muda mfupi Marietta ambaye huku anatambulika kama Shanny akafika kwenye jumba moja kubwa sana la kifahari. Hapo gari likasimama na wakajitua.
Kwenye uwanja wa nyumba kulikuwa na magari takribani kumi na mbili na yote yakiwa yale ya kifahari, bei mbaya. Magari hayo yalikuwa yameandikwa namba kwenye ‘plate’ yani moja, mbili, tatu na kuendelea.
Walipokelewa na wahudumu wawili ambao wamevalia hijabu. Wanawake wembamba warefu wenye matabasamu mazuri kabisa kisha wakaelekezwa mpaka mahali pa kumsubiria mwenyeji.
Mahali hapo palikuwa na makochi yenye maumbo ya mitumbwi. Makochi hayo yalikuwa yamejaa minofu ya magodoro huku yakiwa yamefunikwa na kitambaa kigumu kilichodariziwa na uzi wa dhahabu.
Kwa chini kuliwa na zulia zito la manyoya, rangi nyeupe. Manyoya ya zulia hilo yalikuwa ni marefu kiasi kwamba miguu ya wageni ilikuwa imepotelea manyoyani!
Kwa juu kulikuwa na taa kubwa zenye nakshi zikininginia. Ukutani kulikuwa na urembo wa kila aina mathalani rangi mbalimbali, marumaru, mawe na pia picha kubwa kubwa.
Kwa hapa wanapopumzikia wageni, kulikuwa na picha nne kubwa za kijana wa kiarabu aliyevalia nguo za kisherehe. Sare nyeupe zenye mkanda wa dhahabu, kofia ameweka kwenye kwapa la mkono wake wa kushoto na jambia refu amelishika kwa mkono wake wa kuume.
Kijana huyo alionekana mkakamavu, lakini zaidi anayeahidi kwa yajayo. Mdomo wake uliozungukwa na ndevu ulikuwa unatabasamu na macho yake ya ukubwa wa wastani yalikuwa yanakodoa.
Kidogo, kama baada ya dakika tano tangu Marietta na Mahmoud wafike hapo, akaja mwanaume aliyevalia kanzu ya thamani. Kichwani alikuwa amevalia baraghasia yenye unyoya uliodondokea kushoto mwa uso wake.
Alitabasamu alipomwona Marietta na hapo ndipo picha yake kamili ikaja. Alikuwa ni yule mwanaume aliyebandikwa ukutani! Kwa jina ni Abdulaziz Mohammed.
“Nimefurahi kukuona Shanny,” alisema Abdulaziz tabasamu lake likiongezeka upana. Marietta akamjibu kwa tabasamu la uongo.
“Niambie, kuna tatizo? Mbona uso wako hauna furaha?” akauliza Abdulaziz.
“Unajua kwanini,” akasema Marietta. “Nadhani utakuwa umebadili mawazo yako kama vile tulivyoongea.”
Abdulaziz akatabasamu. Lilikuwa ni tabasamu la wongo. Aliweka mkono wake kwenye akasugua hapo akiwaza.
“Shanny, si rahisi kama unavyowaza,” akasema Abdulaziz. “Ninajitahidi kadiri niwezavyo lakini bado inakuwa ngumu. Nipatie muda zaidi.”
“Mpaka lini?” Shanny akapaza sauti. Mishipa ya shingo ilikuwa imemsimama akikodoa macho. Abdulaziz alimtazama pasipo kusema jambo, na punde Marietta akatambua alichokifanya si sahihi.
Akashusha pumzi ndefu na kuomba radhi. “Sikudhamiria kufanya vivyo. Samahani kwa kushindwa kujihimili.”
“Usijali, lakini nadhani tumeelewana,” akasema Abdulaziz kisha akanyanyuka.
“Mbona unaenda?” Marietta akatahamaki.
“Tumemalizana,” Abdulaziz akamjibu kisha akataka kwenda zake.
“Ngoja!” Marietta akasimama. “Naomba nisamehe upuuzi wangu, sikudhamiria.”
Abdulaziz akamtazama mwanamke huyo kisha akamsogelea karibu na kumtazama machoni. “Kama ningelikuwa sijakusamehe, basi ungelikuwa umeshakufa muda mrefu tu.”
Aliposema hayo akamgeuzia mgongo Marietta.
“Abdul! Tafadhali. Ulichokuwa unakitaka umeshakipata sasa. Kuna nini kingine?” Marietta alizungumza nusu ya kulia. Abdulaziz akamtazama kwa macho ya kebehi alafu akamuuliza, “Una uhakika nimekipata?”
“Kwani ni nini unataka?” Marietta akauliza.
“Utakijua muda si mrefu ni nini nataka. Upo Morocco, ardhi jua linapolalia. Hauna haja ya kuhofia. Kama unataka ulinzi, nitakupatia kama linavyolindwa hekalu!”
Abdulaziz alipomaliza kusema vivyo akaenda zake. Marietta akamtazama Mahmoud. Mwanaume huyo alikuwa anatazama akifinyafinya vidole vyake.
“Mahmoud, ulikuwa unayajua haya yote sio?”
Marietta alimsogelea Mahmoud na kurudia swali lake kwa ukali. “Kwanini haukuniambia Mahmoud?”
“Usingenielewa, Shanny” Mahmoud akasema kwa upole kisha akasimamisha uso wake kumtazama Marietta. “Niliona nikuache ujionee mwenyewe.”
“Siwezi nikakubali!” Marietta akafoka. “Siwezi nikakubali kabisa! Kabisa!” macho yake yalijawa na machozi upesi. Mdomo wake ulipinda kona taya zikitetemeka.
“Tafadhali, Shanny, naomba twende. Tutaongelea mengine huko. Hapa si mahala sahihi, labda tu kama unataka kufa,” Mahmoud akasihi. Basi wakaenda nje na kujipaki kwenye gari. Wakati huo Abdulaziz akiwa dirishani anawatazama.
**
Saa tisa jioni …
Zainab alijaza kahawa kikombeni kisha akakisogezea kwa Marietta. Alipofanya vivyo, akamiminia pia na kwenye vikombe viwili zaidi kisha akaketi. Kikombe kimoja akachukua Mahmoud na kilichobaki Zainab mwenyewe.
Marietta alikuwa amenywea. Ni kama vile hakuona kikombe alichopewa. Macho yake yalikuwa yanatazama meza lakini fikra zikiwa mbali.
“Ulisema unahitaji kahawa,” Zainab alisema kumshtua mwanamke huyo. Marietta alipozinduka akaangaza, akakidaka kikombe na kunywa fundo moja. Mahmoud na Zinab walikuwa wanamtazama.
“Pole sana, Shanny,” akasema Mahmoud. “Kama kuna kuna kitu ningekushauri hivi sasa basi ni kuondoka Morocco haraka iwezekanavyo. Si salama tena kwako.”
Marietta akanywa kahawa mafundo mawili. Hakusema jambo. Aliweka kikombe mezani akatulia.
“Abdulaziz anataka nafasi ya baba yake,” akasema Mahmoud. “Ni kijana wa mwisho hivyo ni wazi, ni ngumu kwake yeye kuwa mfalme mbele ya kaka zake wanne waliomtanngulia. Hivyo mateka wake watamfanya apate haki hiyo ya lazima anayoililia.”
Hapo Marietta akanyanyua uso wake na kumtazama Mahmoud kwa umakini.
“Lakini sivyo tulivyokuwa tumekubaliana!”
“Ni kweli. Alikulaghai. Mahmoud sio mtu wa kutumia akili lakini kwa hili alituzidi. Ametufanya tuonekane wapumbavu.”
“Na kisha akifanya vivyo?” Marietta akauliza.
“Akishakuwa mfalme, bila shaka ataanzisha vita ya kisasi dhidi ya Marekani,” akasema Mahmoud. “Kitu ambacho kitaweka taifa hatarini. Bado hatuna uwezo wa kupambana na Marekani!”
Marietta akashusha pumzi. Kidogo akatekwa na mawazo na kukumbuka mbali sana.
Kichwa chake kilimpeleka ndani kabisa ya ikulu mwaka mzima uliopita. Akiwa amesimama koridoni, alichungulia ndani ya chumba alimokuwa mumewe. Mwanaume huyo akiwa amekwisha vaa suti yake, alikuwa anaongea na mtu kwenye simu.
“Ndio, hakikisha familia yangu inakuwa salama tu. Niko tayari kuupoteza Uraisi ila si familia yangu … nitafanya chochote mnachotaka … I will take the consequences ...”
Hakuishia hapo, akakumbuka mpaka siku ambayo alikuwa amesimamisha gari lake nje kidogo ya uwanja wa ndege mpaka pale alipopokea taarifa kuwa zoezi la kumteka Raisi limekamilika!
Na zaidi, akakumbuka pia siku alipotoa maagizo kuwa nyumba ya bwana Ian ichomwe moto.
Kumbe si Ian aliyechoma nyumba yake na kupotea, bali ni Marietta! Baada ya Ian kumtaarifu mwanamke huyo, akamwambia atumie nafasi hiyo kupotea kwani ni wazi atakuwa anatafutwa na serikali kwa kutuhumiwa kumpoteza Raisi kwani siku hiyo alikuwa zamu.
Zamu ambayo Marietta alimfanya asiitekeleze kwa kuficha nguo zake punde walipotoka kufanya mapenzi.
Wakati Ian akipanga yake huko Ujerumani, Marietta aliyapanga yake Marekani. Ian alidhani anamtumia Marietta, ila yeye ndiye aliyetumika kwa kufanyiwa ‘framing’ ingali Marietta akiwa huru. Hakuna aliyemdhania.
Mwanamke huyo hakutaka kabisa mumewe kwenda Ujerumani baada ya kuona ataenda kupoteza kila kitu kwa mwanamke ambaye ni mcheza ngono sababu tu amemzalia mtoto.
Aliona ni kheri, akamtoa mumewe sadaka kwa familia aliyobebea ubini kuliko kumpoteza kwenye mikono ya ‘malaya’.
Shanny.
**
*SEHEMU YA 21*
Lakini aliwezaje kuyafanya yote hayo?
Ni kwa kipindi kifupi sana, ndani ya siku nne tu, Marietta aliweza kubadili mchezo wote ukawa juu chini. Baada ya kugundua kuwa ataenda kupoteza kila kitu, Marietta aliwasiliana na Mahmoud, binamu yake wa mbali, akamwambia hali ilivyo akiwa hatambui kabisa anachotaka kukifanya.
Kwakuwa Mahmoud anafanya kazi kwenye kasri ya mfalme na alikuwa ana mahusiano mazuri na bwana Abdulaziz, wakasuka mipango katika muda mfupi mno ambapo Abdulaziz alimtafuta shushushu ngangari na timu yake (mercenaries) akawakabidi kazi ya kumsaidia Marietta kufikisha lengo lake.
Mashushu hao wa viwango vya juu kabisa, wakiwa wanashirikiana na Marietta aliyekuwa anachota taarifa toka kwa Ian, wakafanikiwa kuwapata wanaume watatu wa USSS na kuwamaliza kabisa kisha wakachonga sura zao na kwenda kumteka Raisi uwanja wa ndege!
Walipomaliza zoezi lao wakasafisha pia na wale waliokuwa wanaonekana ni hatarishi kwa siri zao, akiwemo bwana O’neil, rafiki wa Raisi, na wanaume wengine watatu kisha wakaacha wenzao wawili kuendelea kutazama hali.
Lakini haya yote yalifanyika kwa Marietta na familia ya ubini wake kuahidiwa pesa kubwa sana huku Abdulaziz akisema anataka taarifa kadhaa tu toka kwa Raisi huyo kuhusu Marekani.
Lakini mpaka muda huo hakuna chochote ambacho kilikuwa kimetolewa na Abdulaziz zaidi tu ya ahadi. Hata sasa Marietta hakuwa anataka pesa tena, bali tu mumewe awe huru na yeye apotelee zake mbali.
Kitu ambacho Abdulaziz hakuwa radhi kukiafiki.
**
Usiku wa saa sita …
Marshall alikuwa ameketi kwenye kiti akitazama tarakilishi yake ndogo mezani. Alikuwa amezama haswa. Yu bize akichati mtandaoni.
Alikuwa akiandika na kusoma jumbe kadha wa kadha. Lakini akaunti aliyokuwa anatumia haikuwa yake bali ya Jack Pyong, na mtu aliyekuwa anachat naye hakuwa mwingine bali Kelly.
Wakati huo Marshall akifanya hayo, Jack alikuwa amelala fofofo kitandani. Kwa makusudi, Marshall alimtilia rafiki yake madawa kwenye soda ili apate kutimiza adhma yake.
“Marshall,” sauti ya kike ikamuita. Hakusikia. Alikuwa bize sana. Sauti ikarejea mara mbili na sasa akatazama. Alikuwa ni Danielle amesimama pembeni kidogo ya korido. Amevalia gauni la kulalia na mkononi amebebelea kikombe cha udongo.
“Haujamaliza tu?”
“Bado … bado kidogo.”
“Mpaka saa ngapi?”
“Musa di mrefu ntakuwa nimemaliza.”
Danielle akanywa kilichopo kikombeni huku akimtazama Marshall. Punde akamwona Marshall akimfanyia ishara ya kumwita, akasonga karibu.
“Tazama!” Marshall akamwonyeshea Danielle kiooni. Danielle akatazama asitambue jambo, akauliza, “Kuna nini?”
“Tazama location hizo,” Marshall akamsihi. “Hamna hata picha moja ambayo location yake ni New Zealand!”
Danielle akamtazama Marshall.
“Kwani kuna shida gani? Sijakuelewa.”
“Mara ya kwanza tulivyokutana na huyu mwanamke kule Hongkong alisema kwao ni New Zealand. Nimekagua profile yake na mara zote alipokuwa tagged, hamna New Zealand hata sehemu moja.”
Kabla Danielle hajatia neno, Marshall akamwonyesha tena picha nyingine. Ilikuwa ni ya mwanaume mfupi aliyevalia miwani akiwa amevalia kombati ya kaki na kaushi.
“Huyu ni Keen!”
“Ndo’ nani?”
“Sijajua ni nani, ila wakati niliposaka jina la Kelly niliona mwanaume huyu akiwa amemtag Kelly kwenye mojawapo ya picha zake za mwanzoni.”
“Sasa Marshall kumtag Kelly kuna shida gani?”
“Yeye ndo’ mtu pekee aliyemtag Kelly. Sijaona popote mtu mwingine pale. Atakuwa anajuana na Kelly bila shaka. Na zaidi mwanaume huyu yupo Marekani!”
“Marshall unataka kuniambia utamfuatilia huyo mwanaume?”
Kabla Marshall hajamjibu Danielle akamwonyesha mwanamke huyo picha moja ya Keen ambayo aliizoom na kutazama magharibi yake.
“Umepaona hapa?” Marshall akaonyeshea kidole kwenye sehemu ndogo ya jengo inayoonekana pichani. “Ni moja ya sehemu inazohifadhi kundi kubwa la kihuni nchini Mongolia.”
Aliposema hayo akamtazama Danielle na kusema, “Pengine Kelly hayupo Marekani kusoma.”
**