*NYUMA YAKO (MSIMU WA TATU) -- 09 & 10*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kwasababu mazungumzo yao ni faragha, akatoka ndani ya chumba cha daktari apate kuwa huru.
“Vipi Harold?”
“Tumezingirwa!” Harold akabwatuka. “Tumezungukwa nje ya jengo na watu waliobebelea silaha!”
“Serious?”
“Ndio! Wamekuja muda si mrefu. Ni sita kwa idadi!”
“Nakuja! Nakuja!”
Inspekta akaweka simu mfukoni kisha akanza kukimbia kama mwehu akielekea nje ya hospitali.
ENDELEA
Alijipaki kwenye gari yake nga kuendesha kwa kasi sana. Lakini kama haitoshi akawataarifu na polisi wengine waliopo karibu juu ya swala la wenzake kuvamiwa wakiwa wanatekeleza kazi.
Akakimbia haswa. Ilimchukua kama dakika ishirini tu kufika eneo la tukio lakini ajabu bado alikuwa amekawia. Alikuta wadhalimu wameshatoweka na watu wake wapo hoi sana.
Harold alikuwa ametobolewa na risasi mbili, na kwa upande wa Gerrard yeye alikuwa amekula risasi si chini ya tano! Wote walikuwa hoi. Haikupita muda mrefu, Gerrard akafa ikiwa ni muda mfupi kabla ya gari la wagonjwa halijafika.
Mwili wa Gerrard ulichukuliwa kwa ajili ya mahifadhi, na Harold akawahishwa hospitali baada ya kupata huduma ya kwanza upesi.
Inspekta James alipekua makazi yale ya bwana Willy na kubaini matundu mengi ya risasi ukutani, mlangoni na madirisha ya kioo yakiwa yamevunjwavunjwa.
Maganda ya risasi yalikuwa yametapakaa karibia kila eneo, na pia damu baadhi ya maeneo na maeneo.
Alibaini pia makabati na madroo yalikuwa yamefunguliwa, kupekuliwa na kuachwa wazi. Akiwa amevalia glovu, alitazama kitu kimoja baada ya kingine.
Baada ya muda mfupi wakaja watu wa ‘Forensic’ - watu wanaohusika kukusanya vielelezo vya kipelelezi, wakaanza kupekua na kukusanya kila kilicho cha muhimu.
Kitu kikubwa ambao mabwana hao walikipata ilikuwa mabaki ya damu. Walitunza sampuli za damu na kuzipeleka maabara kwa ajili ya upembuzi zaidi.
Mpaka yafikia majira ya jioni, tayari inspekta James alikuwa amempoteza Willy na Gerrard ikiwa yeye hajapata kitu! Siku mbaya kiasi gani?
Alionana na mkuu wake na kumweleza kila jambo, na kwa kupitia hayo basi, ili atimize kazi yake vema, akaona kuna haja ya kuongezewa nguvu maradufu.
Alikuwa anahitaji watu kama watano kwa ajili ya kazi.
Kazi ambayo alikuwa anaiona yeye kichwani.
Habari zilitapakaa kwenye vyombo vya habari vyote; redioni, runingani na zaidi mitandaoni. Mosi, kifo cha mazingara cha bwana Willy, pili mauaji ya maafisa wa polisi wakiwa wanatekeleza kazi zao juu ya kesi ya bwana Willy.
Mambo yalikuwa yanawaka na kuunguza.
Taifa zima la Marekani lilikuwa limezama kwenye bumbuwazi kutokana na matukio haya ya kufululiza. Watu walikuwa wanataka hitma. Walikuwa wanataka nchi yao irudi kwenye amani iliyozoeleka hapo nyuma.
Swala hilo lilitafuna kichwa cha inspekta. Aliona mzigo huo wote upo mgongoni mwake.
**
Saa sita mchana …
“Wamemuua asitoe siri!” alisema Jack akitoa macho. Marshall alikuwa anatazama tarakilishi yake mezani kwa udadisi. Alikuwa yu mtandaoni.
“Ni ajabu, wamemuua akiwa kwenye kituo cha polisi!” Jack aliendelea kubweka. “Si bure kuna watu kila eneo. Ni kazi kwelikweli.”
Jack aliweka kituo akamtazama Marshall.
“Kwahiyo naongea mwenyewe hapa, sio?” akauliza akipandisha nyusi.
“Kuna cha maana ambacho umeongea sijasikia?” Marshall akauliza pasipo kumtazama Jack, bado alikuwa bize na tarakilishi yake.
“Marshall, usikiite usichoweza kupambana nacho!”
“Kipi hicho?”
“Unakijua wewe. Yani mimi kuongea kote huko we hujaona la maana?”
“Kabisa.”
“Marshall, nikinyamaza, utajuta.”
“Nitanenepa maana utakuwa umeniepusha na ujinga.”
“Aaanh!”
“Sikia, Jack. Nipo bize hauoni? Waweza kunipa muda wa kuhema tafadhali.”
Basi Jack akakwapua mfuko wa chocolate uliokuwepo pembeni, kwa hasira akaufungua na kuanza kumumunya. Baada ya muda kidogo, akafunggua tarakilishi yake na yeye akaanza kufanya mambo yake.
Lakini muda kidogo, tarakilishi ya Marshall ikaanza kukonyezakonyeza. Ilifanya vivyo kwa kama dakika kisha ikazima!
Marshall akaibamiza,
“What the f*ck!” akalalama. Akajaribu kuiwasha tena lakini isidumu ikafanya kama awali na kuzima tena.
Alishindwa cha kufanya. Alimtazama Jack, akamwona mwaname huyo akiwa yu bize na tarakilishi yake kana kwamba hakuwa anamwona wala kumsikia akilalama.
Akajaribu kuchomoa tarakilishi yake toka kwenye umeme na kulazimisha kuizima kisha akangoja kwa kama dakika tano, akaiwasha tena!
Alikuwa amekunja uso kwa hasira. Alikuwa anafanya mambo kwanguvu na kwa upesi.
Tarakilishi iliwaka, akashusha pumzi ndefu ya ahueni, pheeeeeeww!
Asifanye kitu, sekunde tano tu mbele, tarakilishi ikaanza kukonyeza, mara ikazima tena! Marshall akatukana akibamiza meza.
“Jack, nini shida na hii mashine?” akauliza.
Jack hakumjibu, badala yake akawa analiza mluzi. Hapa ndio Marshall akapata jambo kichwani -- atakuwa ni --
“Jack, wewe ndo umefanya hivyo, sio?” akapaza kuuliza. Jack akamtazama pasipo kumjibu kisha akarudisha macho yake kwenye kioo cha tarakilishi na kuendelea kuperuzi.
Mdomoni alikuwa analiza mluzi.
“Jack, si naongea na wewe?”
“Huoni nipo bize, ama?”
Marshall akashindwa kujizuia kutabasamu.
“Jack, niko serious!”
“Sawa sawa, mimi nimekuelewa. Endelea kuwa serious na kazi yako, na mimi niko serious na kazi yangu. Kwani kuna shida?”
“Najua ni wewe, nirekebishie basi ndugu yangu?”
Jack hakujali, akaendelea na kazi yake. Marshall akambembeleza mpaka alipoona anyanyuka na kumfuata akimlazimisha ampatie tarakilishi yake atumie.
Wakiwa wanazozana na kuvutana, Danielle akaingia.
“Habari njeeeema!” mwanamke huyo alipaza sauti akiwa amenyoosha mikono yake juu. Mkono wake wa kuume ulikuwa umebebelea bahasha rangi ya kaki.
Akiwa na furaha, akaiweka bahasha mezani, upesi Marshall akawahi kuifungua bahasha hiyo, ndani akakuta nakala za vibali.
“Kila kitu kipo tayari sasa!” alisema Danielle. “Kuanzia kesho tutaanza kazi!”
Marshall aliendelea kupekua kwa macho yake nakala moja baada ya nyingine. Kulikuwamo na nyaraka nne.
“Hadi na ya gazeti?” akauliza Marshall akitazama nyaraka. Alitabasamu kwa ukubwa kabisa kisha akampongeza Danielle kwa kazi aliyofanya.
“Lakini imekuwa ni upesi sana! Sikujua kama hili swala la gazeti lingechukua muda mfupi,” alisema Marshall.
Danielle akatabasamu.
“Hiyo haili muda. Haina vigezo vingi kama kibali cha kufungua taasisi ya kipelelezi. Vilevile ghushi ambazo ametengeneza Jack zimesaidia sana!”
Baada ya kufurahia mafanikio hayo, wakaanza kujadili kuhusu matukio yaliyotokea siku hiyo. Moja ya jambo kubwa kabisa ambalo walikubaliana ni juu ya usalama wa bibie Marietta.
Kama Willy ameweza kuuawa kwasababu ya kuficha maneno, Marietta atapona?
Basi usiku mzima wakajadili kuhusiana na jambo hilo, na kwa kushirikiana wakaandaa habari ndefu na ya kina ambayo ndiyo ilikuwa ya kwanza kabisa kwa ajili ya gazeti lao la kesho.
Gazeti lao hilo wakalipa jina la MWAMBA.
Kumaanisha mwamba waliokataa waashi, umegeuka kuwa …
**
Asubuhi ya saa tatu …
“Haya hapa majibu, mkuu,” alisema afisa akiwa anamkabidhi inspekta James bahasha. Yalikuwa ni majibu ya vinasaba ambavyo vimepatikana kwenye mabaki ya damu yaliyokusanywa kwenye eneo la tukio na wataalamu - forensic experts.
Alipotazama zaidi ndani ya bahasha akapata kuona picha za wanaume wawili.
Wanaume ambao ni watuhumiwa wa tukio la kuwavamia maafisa na hata kusababisha kifo.
**
*SEHEMU YA 10*
Baada ya kupata picha hizo, inspekta akafanya namna zikuzwe na kutandazwa mitaani kwa ajili ya msako wa watu hao wawili. Lakini katika namna ya ajabu kidogo, ilibainika kuwa watu hao ni maafisa wa USSS! - shirika linalohusika na ulinzi wa Raisi, makamu na watu wengine wakubwa na familia zao.
Kwenye majira ya mchana, bwana James akaenda hospitali kuonana na Harold apate kumjulia hali. Alipofika huko akapata kuongea machache na mwanaume huyo kabla ya simu yake kuita mfukoni.
Alipotazama, akaona ni Marietta!
Basi akasonga kidogo kando apate kuongea.
“Inspekta, naweza nikaonana na wewe?” sauti ya Marietta ilisema. Ilikuwa inatikisika ikiakisi woga. Kabla inspekta hajatia neno, Marietta akaongeza,
“Naogopa sana. Nahisi sipo salama!”
Inspekta akamuuliza,
“Upo wapi muda huu?”
“Kwangu!” Marietta akajibu.
“Unaweza fika kituoni?”
“Sawa.”
Inspekta alipokata simu, akafanya namna kurudi kituoni apate kuonana na Marietta. Aliagana na Harold akimuahidi kuja tena kesho kumjulia hali.
Basi baada ya muda mfupi akawa ameshawasili kituoni, na isichukue muda, Marietta akafika pia.
“Nipo hatarini inspekta!” alisema Marietta kwa hofu. Uso wake ulikuwa umejikunja, mikono yake ameifumbata.
Alifungua pochi yake akatoa gazeti na kuliweka mezani. Inspekta aliponyanyua gazeti hilo na kulitazama, akaona picha ya Marietta na habari iliyokuwa inasomeka juu,
“MLENGWA ANAYEFUATA!”
Alisoma jina la gazeti hilo, akaona ni MWAMBA. Basi akajipa muda kidogo kupitia gazeti hilo na habari yake.
Akasoma namna ambavyo mwandishi alivyohariri kutabiri kuwa Marietta ndiye mtu anayefuata kuuawa sababu zikiwa yeye kuwa karibu na polisi lakini pia kuandamwa na mambo kadhaa yanayotishia usalama wake hapa karibuni.
Inspekta alipomaliza kusoma habari hiyo, akaliweka gazeti hilo pembeni na kumtazama Marietta,
“Una kitu cha kuniambia, madam?” akauliza.
Marietta alikuwa akitetemeka, anatazama chini. Macho yake yalikuwa mekundu akiwa anaminya lips.
“Kwanini unajihisi upo hatarini? Ni muda wa kuongea madam, siwezi kukusaidia kama umefunga kinywa.”
Basi baada ya Marietta kufikiria kidogo, akasema amekuwa akipokea jumbe za vitisho na anahisi kuna mtu anamfuatilia.
“Unahisi mtu huyo ni yule ambaye alikunywesha hotelini?” inspekta akauliza.
“Hapana, lakini kuna mahusiano naye,” Marietta akajibu na sasa kwa wazi akafunguka kwamba, anahofia taarifa alizompatia mtu yule hotelini ndizo ambazo zinamuweka kwenye hatari ya kupoteza maisha.
“Habari gani hizo unadhani ulimpa mtu huyo kiasi cha kukuhatarisha?” akauliza inspekta. Alikuwa anamtazama Marietta machoni ingali mwanamke huyo akitazama chini.
“Inspekta, sijui wapi pa kuanzia. Ni mlolongo mrefu sana.”
“Usijali, nina muda wa kutosha.”
Basi Marietta kwa woga, akaelezea yale yote anayoyafahamu. Akaelezea tangu alivyokuwa anamjua bwana Ian na namna gani ambavyo alikuwa na mahusiano naye kwa siri.
Alieleza kila kitu, kila kitu. Sasa inspekta akapata picha kamili juu ya kinachoendelea. Kumbe bwana Willy yupo nyuma ya bwana Ian, na mabwana hao pamoja na jeshi lao ni washukiwa kuhusu kupotea kwa Raisi.
Sasa kwanini wanataka kumuua Marshall? Inspekta akajiuliza.
Alipofikiri kwa muda akakubaliana na akili yake kwamba huenda Marshall ana taarifa ambayo mabwana hawa hawataki ivuje.
Lakini pia kama haitoshi, Marshall ndiye yule aliyemnywesha Marietta kisha akatokomea na habari ambazo ndizo zimechapishwa kwenye gazeti/
Na kuhusu yale mabaki ya damu yaliyokutwa kwenye nyumba ya Jack Pyong, yalikuwa ni ya afisa wa usalama ambaye anahusika pia na genge lan. Walikuwa kwenye mapambano haya kwa muda.
Na wale watu wote ambao Marshall anadaiwa kuuawa, watakuwa ni washirika wa bwana Ian pia vilevile!
Alishangazwa sana na namna ambavyo habari hiyo ilivyozunguka. Kwa namna moja ama nyingine aliikuta akipata hamu sana ya kuonana na Marshall. Pengine ulimwengu sivyo vile anavyouona.
Lakini atampatia wapi?
Alitazama gazeti lile la MWAMBA akajikuta akipata wazo.
“Madam, ina maana unataka kuniambia haujui kabisa mahali ambapo mumeo atakuwapo?” inspekta akamuuliza Marietta.
“Sijui kabisa!” Marietta akaapa. “Laiti ningelikuwa najua, basi ningeshafanya jambo. Najutia sana kwa nilichokifanya kwakweli. Najiona mkosefu kabisa!”
“Na vipi kuhusu Ian?”
“Sijui kuhusu yeye, ila naamini atakuwa anajua. Naomba unisaidie inspekta nimwone mume wangu. Nataka nimwombe radhi kabla sijafa ama kufungwa kama ikitokea.”
Marietta akaanza kudondosha machozi.
“Tunawezaje kumpata Ian?” inspekta akauliza.
“Si rahisi kumpata,” Marietta akajibu, “hana makazi maalum, anapohitaji kuonana nami huwa anakuja ofisini kwangu ama nyumbani.”
“Vipi kuhusu mawasiliano yake?”
“Ana namba kadhaa na barua pepe moja ninayoifahamu. Labda inaweza kusaidia.”
Inspekta akachukua namba hizo na kuzinakili kwenye kijitabu chake.
“Inspekta,” Marietta akaita. Alimtazama inspekta machoni na kumwambia, “kuwa makini sana, hata humu ndani kuna watu wa Ian.”
Inspekta akamtazama Marietta kwa umakini.
“Kifo cha Willy ni ishara tosha kuwa humu kuna maajenti wasaliti,” alimalizia Marietta.
Hilo jambo likazama kwenye kichwa cha inspekta.
**
Jioni ya saa kumi na moja …
“Changamka, hatuna muda wa kukaa hapa!” alisema jamaa mmoja aliyevalia koti la ngozi. Mkono wa kuume alikuwa amebebelea bunduki ndogo na wa kushoto kuna begi dogo.
Alikuwa amesimama akimtazama mwenzake ambaye alikuwa anakusanyakusanya vitu kuvitia kwenye begi.
Mwenzake huyo alikuwa amevalia sweta, suruali ya kadeti na viatu vyeusi imara vya ngozi. Walikuwa wapo kwenye haraka sana.
Upesi walifungua mlango na kutoka ndani, wakaelekea kwenye gari na kujipaki kisha wakatimka.
Mabwana hawa walikuwa ndiyo wale waliokuwa wakitafutwa baada ya picha zao kutandazwa mitaani kama wahusika wa mauaji ya bwana Gerrard na kujeruhiwa kwa bwana Harold.
Walinyooka na gari lao moja kwa moja mpaka kwenye makazi fulani tulivu. Humo waliketi sebuleni na baada ya muda mfupi wakaonana na bwana Ian.
Walipoongea kidogo, Ian akatoa ishara ya kichwa, wanaume hao wakauawa kwa kumiminiwa risasi kisha wakawekwa kwenye mfuko na kuwekwa ndani ya gari kwa ajili ya kwenda kutupwa.
Lakini kulikuwa na jambo …