*NYUMA YAKO (MSIMU WA TATU) -- 07 & 08*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Wao na James wanashea kitu kimoja, wote wanakutafuta wewe. Ni swala la conflict of interest. Pengine James amepata kitu kuhusu wewe hivyo wanakitaka, ama wanataka swala hili la kukutafuta liwe binafsi kwenye mhimili mmoja ulio karibu nao, na si mwingine bali FBI.”
“Kwahiyo vipi kuhusu Marietta? Unadhani atakuwa kwenye hatari pia?”
“Bila shaka, kama tu watakuwa wamejua kuwa ulikutana naye.”
“Ni lazima watakuwa wanajua hilo!”
Basi Danielle akamtazama Marshall na kumwambia, “Kama ni hivyo, tutarajie Marietta kuuawa ama kupotea muda si mrefu.”
ENDELEA
Wakafika kwenye makazi yao mbali na jiji, huko wakapumzika wakiwa wamkutana na Jack alafu baada ya muda kidogo wakajumuika kwa pamoja kupata chakula cha usiku.
Wakiwa hapo wakawa wanajadili mambo kadhaa. Mambo ambayo yametokea na ambayo yanafuatia.
Lakini katika hayo swala la bwana Willy lilishika sana hatamu.
“Unadhani bwana James atakuwa anafahamu kuwa jamaa huyo aliyekamatwa anahusika na bwana Ian?” akauliza Jack Pyong akitafuna.
“Hataweza kujua,” akajibu Marshall baada ya kumeza. “Pengine kama atatumia njia mbadala ya kumlazimisha mwanaume huyo aongee kila kitu. Kitu ambacho ni ngumu sana kutokea!”
Kukawa kimya kidogo wakitafuna. Baada ya vijiko viwili vitatu, Jack akasema,
“Napata mawazo sana juu ya hili. Leo nimepekuwa magazeti kila moja na habari yake. Nimejiuliza, kama huyu bwana amekamatwa akiwa amejikamilisha kisilaha, yupo kwenye nyumba ya inspekta, vipi kuhusu maajenti wengine? Hamna ambao wapo pamoja naye pale shirikani?”
Akiwa anasema hayo alimtazama Danielle. Mwanamke huyo akangoja kwanza ameze nipi ajibu. Ni Jack Pyong peke yake ndiyo alikuwa anaweza kuongea na chakula mdomoni.
“Jack,” Danielle akaita na kugusia, “shirika ni kitu kikubwa chenye watu wengi. Ndani yake haiwezekani wote wakawa wema, kuna ambao ni mahasidi na kuna ambao wanalipigania taifa lao.”
Basi baada ya hapo kukawa kimya zaidi watu wakila na kunywa. Baada ya kumaliza wakaendelea na mjadala wao.
“Natazamia kama nitapata nafasi ya kuonana na rafiki yangu,” alisema Danielle na kuongeza, “pengine yeye atakuwa ananieleza ni nini kinaendelea kule shirikani.”
“Itakuwa vema,”Marshall akaunga mkono, “Nadhani kutakuwa na mtandao fulani kwenye shirika na FBI unaoongozwa na wadhalimu. Endapo tukibahatika kumpata mtu hata mmoja, basi atatusaidia sana kwenye upelelezi wetu.”
“Kabisa,” Danielle akaafiki. “Lakini pia wakati Jack anaongea kuhusu magazeti, nimejikuta napata wazo.”
“Lipi hilo?” Jack akawahi kuuliza.
“Mnaonaje kama tukaanzisha chombo cha habari?” Danielle akapendekeza.
“Danielle, huoni ni gharama sana? Tutawezaje kuendesha chombo hicho ikiwa kinahitaji pesa sana kwenye uwekezaji?” Jack akawahi kupinga hoja.
Lakini Marshall yeye alitulia. Alijua kuna kitu kichwani mwa Danielle hivyo akampa muda zaidi mwanamke huyo aongee.
“Si kama unavyowaza, Jack,” akasema Danielle. “Ni gazeti tu! Na gazeti hilo litakuwa limesajiliwa na ‘farm’ yetu ya upelelezi. Litakuwa linatoa habari kwa kina na matazamio ya mambo mbalimbali kisiasa, kijamii na hata kiuchumi.
Mitazamio ambayo itakuwa yakinifu na ya kiundani sana. Napata kuamini gazeti hilo litakuwa kubwa sana kutokana na habari zake, na hivyo basi litakuwa na wateja wengi, haswa kwenye kipindi kilichogubikwa na matukio kama hiki.
Au mnasemaje?”
Danielle akauliza akimtazama Marshall.
“Ni wazo jema!” Jack akapaza sauti. “Naunga mkono hoja!”
“Na vipi kuhusu wewe Marshall?” Danielle akauliza. “Wewe unalionaje hili?”
Marshall akakuna kidevu akifikiri, kidogo naye akaunga mkono hoja na kuongezea habari, “itapendeza kama mhariri na waandishi wa hilo gazeti wakawa watu wasiofahamika kwa ajili ya ishu za usalama.
Waandishi hao hawatakiwi kujulikana na jamii wala na vyombo vya usalama. Hilo pia litawafanya wafanye kazi kwa uhuru pasipo kuhofia.”
“Ni wazo jema!” Danielle akasema akiliza vidole vyake. “Kama ni hivyo basi, hamna haja ya kusema gazeti hilo linamilikiwa na ‘farm’ yetu ya upelelezi. Mnaonaje?”
“Ni wazo jema,” Marshall na Jack wakaunga mkono, lakini wakakubaliana kwamba jambo hilo litafuata baada ya kumaliza kwanza kusajili taasisi yao ya kipelelezi.
Muda ulikuwa umebakia mchache kukamilisha hilo na kila jambo lilikuwa limeshawasilishwa kwenye mamlaka husika.
Basi mjadala huo ukafungwa na sasa wajamaa hawa wakawa wamemwazima masikio bwana Jack ambaye alikuwa anaeleza yale ambayo ameyang’amua toka kwenye msako wake mitandaoni.
Haswa kwenye lile swala la mkutano wa kimataifa uliokuwa unafanyika kule Ujerumani. Mkutano ambao ulifanyika muda mfupi baada ya Raisi wa Marekani kupotea.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, bwana Jack alipata kubaini kuwa jambo kubwa lililokuwa linangojewa kwenye mkutano huo kama ajenda kuu ni swala la mabadiliko tabia nchi na kivipi nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo zitachukua hatua kuhusu swala hilo.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Marekani ilikuwa radhi kuunga mkono jitihada za kupunguza idadi ya viwanda na haswa vinu vya nyuklia duniani, lakini si kila taifa lilikuwa linaunga mkono jambo hilo.
Na zaidi, kulikuwa na mjadala mkubwa juu ya soko la mafuta na ushawishi wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani.
Kwenye sakata hilo, Marekani alikuwa amesimama kidete kupinga mfumuko wa bei ya mafuta duniani na haswa vikwazo ambavyo amewekewa dhidi ya mataifa ambayo yanaongoza kuzalisha mafuta duniani.
Baada ya Jack kueleza hayo, Marshall na Danielle wakaanza kuchanganua taarifa hizo vichwani mwao kubaini wapi ulipotoka mkono uliompoteza Raisi.
Ni aidha kwenye mataifa ambayo hayaungi mkono jitihada za kukabili mabadiliko ya tabia nchi, ama kwenye swala la mafuta.
Japo walighani mawazo mbalimbali wawili hawa walikubaliana kwamba bwana Ian ndiye kipande cha fumbo kinachokosekana.
Huenda bwana huyo akawa na taarifa nyeti kwenye hili yeye kama mmoja watu waliohusika na kupeleka familia ya siri ya Raisi nchini Ujerumani.
Hawakuwa na budi kumtafuta kwa udi na uvumba kumtia mkononi, lakini swala hilo halikuwa jepesi. Bwana huyo amekuwa ni mtu wa kuhamisha makazi na ofisi yake mara kwa mara, kama vile baada ya kila miezi kadhaa.
Hata wafanyakazi wake baadhi hawajui ni wapi haswa alipo bwana huyu. Kitu pekee kinachowafanya waone uwepo wake ni kwa kupitia akunti zao za benki tu. Pesa inakuwa ikiingizwa kila mwisho wa mwezi.
Kwa wale wanaofahamu makazi yake na wapi anapopatikana, walikuwa hawazidi watano.
Yote hayo kwasababu za kiusalama.
Hata Marietta, mpenzi wake, hakuwa hafahamu lolote kuhusu wapi anapopatikana bwana Ian.
Kumpata iliwapasa watulie na kuja na mpango kabambe.
“Vipi, una wazo lolote?” Danielle aliuliza akimtazama Marshall. Baada ya Marshall kufikiri kidogo akasema, “Kuna njia mbili. Moja kwa kupitia Willy na nyingine kwa kupitia Marietta.”
Kisha akamalizia,
“Lakini kote kuna changamoto.”
Danielle akatabasamu na kusema,, “Changamoto ndiyo raha ya mchezo, Marshall.”
**
*SEHEMU YA 08*
Asubuhi ya saa nne …
“Sitasema kitu,” alibwabwaja bwana Willy akimtazama Inspekta James. Bwana huyo alikuwa amefungwa mikono na pingu iliyojishikiza mezani. Miguu yake pia ilikuwa imefungwa minyororo iliyozungushiwa kwenye kiti.
Hakuwa na uhuru.
Uso wake ulikuwa na majeraha, haswa upande wake wa kushoto ambapo ulikuwa na rangi ya zambarau kuonyesha amevilia damu.
Bwana huyo tangu ameketishwa hapo kwa ajili ya mahojiano, amekuwa mkaidi haswa. Hakuna swali hata moja alilojibu, muda mwingine alimtazama tu muulizaji pasipo kufungua kinywa.
“Nakuuliza kwa mara nyingine, kwanini ulikuwa unataka kunimaliza? Na kwanini ulikuwa unataka niachie kesi?”
Bwana Willy akamtazama inspekta kama mdoli. Hakutia neno.
“Ukaidi wako hautakupeleka kokote, ndugu. Na ninakuhakikishia, utasema kila kitu ambacho unakificha,” akasema James akinyanyuka. Bwana Willy akamtazama akimsindikiza na macho alafu akasema akitikisa kichwa,
“Kamwe!”
Inspekta akaachana naye ajiondokee lakini kabla hajaufikia mlango, Willy akamtahadharisha, “kuwa makini, inspekta. Maisha yako yako kwenye mstari.”
Inspekta asijali sana maneno hayo, akaenda zake nje.
Alikutana na Harold na Gerrard akawapa maagizo waende wakapekua kila kitu ambacho kipo huko, na chochote wanachoona kinaweza kuwasaidia kwenye upelelezi wao, basi wakilete mara moja kituoni.
Baada ya Harold na Gerrard kuondoka zao, inspekta akajirusdisha kwenye ofisi yake na kutazama baadhi ya mambo ya kazi. Muda kidogo akanyanyua simu yake na kumpigia Marietta. Alitumia namba ya simu ambayo ipo kwenye kadi ya biashara ya mwanamke huyo.
Simu ikaita mara mbili, ikapokelewa.
“Ni inspekta James Peak hapa,”
“Ndio, inspekta.”
“Habari yako?”
“Njema kabisa. Unaendeleaje?”
“Vizuri, nashukuru. Nimeona kimya nikaona nikutafute hewani. Vipi hauna jambo la kunishirikisha?”
Kukawa kimya.
“Madam Marietta …?”
“Ndio, inspekta.”
“Una chochote cha kunishirikisha?”
“Aahm, hapana, inspekta. Namba yako ninayo, nitakapopata jambo, usihofu nitakutafuta kama nilivyofanya awali.”
“Kweli?”
“Ndio, usijali.”
“Samahani, kama hutojali. Tangu ulipotoka hapa kituoni, haujakutana na kitisho ama maneno yoyote?”
Kukawa kimya kidogo.
“Madam Marietta,” inspekta akaita.
Mara tiiiiiiiii! Simu ikakata.
Inspekta akajaribu kumpigia tena mwanamke huyo pasipo mafanikio. Alikuwa hapatikani!
“Ana shida gani huyu?” inspekta James akajiuliza akiweka simu yake chini. Alitambua kutakuwa na tatizo na haja ndani yake ilimtuma amtafute mwanamke huyo kwa maongezi zaidi.
Kwenye ulimwengu wa kiitelijensia, kila mtu ni mtuhumiwa, hakuna wa kuaminika kwa asilimia zote.
Alifikiria jambo hilo la Marietta kwa muda kidogo kabla hajaachana nalo na kuendelea kupitia rekodi za bwana Willy kwenye shirika lake la kazi, FBI.
Ripoti hizo aliziomba toka huko shirikani na pasipo tatizo, wakampatia.
Likapita lisaa limoja akiwa anazipitia. Hakuwa anaona kama kuna jambo la kumtilisha maanani hivyo kidogo akaanza kuboreka, ila kwakuwa hana budi, akaendelea kupitia.
Kidogo akiwa katika zoezi lake hilo, hodi ikapigwa kwenye ofisi yake na kabla hajaitikia, akaingia afisa mmoja aliyemtazama kwa kukodoa,
“Mkuu, inabidi uone hili!”
Upesi bwana James akanyanyuka na kuongozana na afisa huyo mpaka mahali alipokuwa amehifadhiwa bwana Willy, selo.
Hapo aliporusha macho, akastaajabu kuona bwana huyo akiwa amelala, anavuja damu puani na mdomoni!
“Nini kimetokea?” inspekta akauliza akizama ndani. Mapigo ya moyo ya bwana Willy yalikuwa yanasikika kwa upole mno. Macho yake yalikuwa yanarembua akihema kwa uzito.
Basi upesi bwana huyo akanyanyuliwa na haraka akakimbiziwa kwenye gari la wagonjwa kuwahishwa hospitali. Pamoja naye, wakaongozana maafisa wawili wa polisi.
Bwana James akiwa amepigwa na butwaa, alishika kiuno akitazama gari la wagonjwa likitokomea. Alimtazama afisa yule aliyemletea habari, akamuuliza,
“Ni nini kimetokea?”
Bwana huyo akamwambia anadhani Willy ametiliwa sumu kwenye chai yake.
“Alianza kubadilika muda mfupi baada ya kunywa chai. Sikujua nini kilikuwa kinamtokea, alikuwa anagugumia na kujikunjakunja akishika tumbo. Ndani ya muda mfupi ndiyo nikamwona akiwa anatokwa damu, nikaja kukufuata!”
“Nani aliyempatia chai!” akauliza inspekta akitoa macho.
“Ni mimi, mkuu!” akajibu afisa. Uso wake ulikuwa umejawa na mashaka lakini pia woga. Alitoa macho yake kwa kukodoa na mdomo akiuachama.
Inspekta akamkwida nguo yake na kumsogeza karibu.
“Umetia nini kwenye chai?” akamuuliza akimkazia macho.
“Sijatia kitu mkuu. Kweli nakuapia!” akasema afisa kwa woga mkuu. Alikuwa amekunja ndita jasho likimchuruza.
“Nimetoa chai kantini nikamletea moja kwa moja baada ya kuniambia anahitaji kitu cha kupasha tumbo lake!”
Basi inspekta akaenda mpaka jikoni napo akauliza lakini hakupata majibu. Mpishi na watu wanahudumia walikana kabisa kuhusika na jambo hilo na hata kujaribu chai ile wao wenyewe kuthibitisha kwamba haina tatizo.
Inspekta akabaki akiduwaa.
Aliamua kurudi ofisini na kuketi huko akitafakari. Aliona ni vema akangoja majibu ya daktari kugundua nini haswa tatizo.
Lakini uvumilivu nao ukamshinda, akanyanyuka na kujieka koti lake, moja kwa moja akaelekea hospitalini yeye mwenyewe.
Alichukua kama lisaa kufika kutokana na foleni. Alipowasili na kujitambulisha akapewa habari kwamba bwana Willy amekwishafariki!
Bwana huyo alifariki njiani kabla hajafika hospitalini.
“Amefika hapa akiwa tayari ni mfu kwa kama robo saa!” alisema daktari. Alikuwa ni mwanamama mwenye makamo ya miaka thelathini na kitu hivi, macho yake madogo alikuwa ameyajaladia kwa miwani.
“Ni nini kimemuua?” James akauliza.
“Ni sumu kali ya kemikali!” akasema daktari kisha akajaribu kwa ufupi kumwelezea inspekta juu ya sumu hiyo. Ni mchanganyiko wa kemikali kadhaa ambazo huathiri mfumo wa hewa na wa chakula kwa muda mfupi mno!
“Yampasa mtu mtaalamu kutengeneza kitu kama hicho!” alisema daktari na kuongeza, “miligramu moja tu inatosha kabisa kumaliza uhai wa mtu!”
Inspekta akachoka.
**
“Nimekamilisha kila kitu,” alisema afisa wa polisi akiwa ananong’ona na simu. Afisa huyo alikuwa amejibana mahali na kwa kuzuia sauti isisambae, akawa ameziba mdomo kwa kiganja chake.
Afisa huyo alikuwa ndiye yuleyule ambaye alikuja kumpasha habari inspekta juu ya hali ya bwana Willy baada ya kunywa chai!
“Ndio, tayari amekwishakufa,” alisema bwana huyo na punde akakata simu na kutoka chooni alipokuwapo. Akachomekea vema sare yake na kuendelea na kazi zake.
**
“Mkuu!” sauti ilipaza kwenye simu ya inspekta James. Bwana huyo alikuwa akiongea na mtumishi wake, Harold, ambaye alimpigia akiwa kwenye mazungumzo na daktari.
Kwasababu mazungumzo yao ni faragha, akatoka ndani ya chumba cha daktari apate kuwa huru.
“Vipi Harold?”
“Tumezingirwa!” Harold akabwatuka. “Tumezungukwa nje ya jengo na watu waliobebelea silaha!”
“Serious?”
“Ndio! Wamekuja muda si mrefu. Ni sita kwa idadi!”
“Nakuja! Nakuja!”
Inspekta akaweka simu mfukoni kisha akanza kukimbia kama mwehu akielekea nje ya hospitali.
**