Mwalimu alishasema viongozi na serikali si malaika, yapo mapungufu yaachwe na mazuri yachukuliwe na serikali zinazofuata.
Kabla ya kumpongeza au kumlaumu Mwalimu kuna mambo ya msingi kuangalia. Mwalimu alichukua nchi ikiwa katika hali gani hasa upande wa viongozi na elimu zao? Mwalimu alifanya nini baada ya hapo, na alituachia nini alipoondoka.
Winston Churchill ni PM wa Uk anayekumbukwa sana na mwenye heshima sana UK na duniani kote. Hata baada ya kuiongoza Uingereza kuepeuka aibu kubwa mbele ya Mjerumani, bado alishindwa uchaguzi uliofuata. Lakini mapungufu yake ya kiutawala hayajaondoa heshima yake ndani ya Taifa lake.
Mwl alichukua nchi kukiwa hakuna wasomi na wananchi wakiwa mbumbu kabisa kama alivyosema mmoja wetu humu. Ni kwa kutumia uadilifu na uzoefu nchi ikaanza kutambaa na hatimaye kusimama. Ushahidi kwa sisi tulioona kwa macho yetu, form vi walikuwa wanapangiwa kazi (sio kutafuta) kuziba pengo la wasomi. Ni wakati huo Mwl alikuwa anaomba Scholarship kwa nchi marafiki na zilitolewa kwa mtu mwenye sifa na si kwa kabila au dini. Haya yote yakiendelea Mwl alikuwa anajenga Chuo kikuu ambacho leo asilimia 90 ya wasomi wamepitia hapo.
Elimu wakati wa Mwl ilihakikisha kuwa hata mtoto wa masikini alipata Warrant ya kwenda shule. Leo tuna maprofesa waliotoka kwenye kuokota maembe na kuchunga ng'ombe na sasa wanalisaidia taifa.
Upande wa Afya, Mwl alijenga vituo vya Afya, Hospitali za mikoa na Wilaya. Leo tembelea vituo vya Afya kama Magomeni, Mnazi mmoja au Temeke uone nani aliweka jiwe la msingi au kufungua. Kote nchini utaona majina kama Mustafa Songambele, Kawawa, Nyerere, Karume, Mwakawago, n.k
Mwl alikuta umeme wa Pangani, akajenga Nyumba ya mungu, Mtera, Kidatu, na hata kuvusha kwenda Zanzibar. Ni mabwawa hayo ambayo leo tumeshindwa kujenga mengine kama si kulinda maji na vyanzo vyake.
Mwl akaona njia ya kuinua uchumi wa nchi si kwenda kuomba misaada ya kuletewa mitumba, akajenga viwanda kama Mwatex, Mutex, Urafiki, Tanganyika Packers, Bora, UFI, Kilitex n.k. Kwa wale tuliokuwapo enzi hizo kulikuwa na Shift za kazi, Asubuhi, mchana na usiku. Tulitumia bidhaa zetu wenyewe na malighafi zetu. Leo tunauza ng'ombe Uarabuni ili tuagize nyama za makopo Brazil na South. Tunanunua nguo hafifiu za kichina na hatusafirishi tena vitenge vya urafiki.
Wakati tulipokuwa na janga la njaa nchi nzima, Mwl alihakikisha kuwa huo unga wa yanga au bulga unamfikia mtu wa mwisho kijijini. Si kweli kuwa alizuia watu wasihifadhi chakula.
Vyuo vyote vya ufundi, uganga na kilimo vilijengwa wakati wa mwalimu, leo tumeviua vyote kwasababu hatuna pesa za kuvihudumia na kule vijini wana lima kama wajuavyo, wanajitibu kwa Tetracyline kwa maana hakuna wataalamu, bado tunawadangaya na kilimo kwanza
Mwl akatuachia TAZARA, moja ya infrastructure kubwa barani , leo mahindi yanaoza Sumbawanga kwasababu reli haifanyi kazi.
Akajenga reli ya Segera Ruvu, na kuiendeleza ya kati hata baada ya kufa kwa EAC. Pamoja na yote hayo tumeshindwa kuweka mafuta kwenye mabehewa na leo tunaomba ''visa'' kwenda Mwanza au Bukoba.
Hayo ni machache tu mazuri ya Mwl ambayo huwezi kuyafananisha na awamu yoyote kwasababu mwalimu alianza na msingi, sasa hawa wa sasa hata kurepea paa hawawezi.
Mapungufu ya Mwl ni pamoja na kutaifisha mashamba ya mkonge na kuyaacha mapori. Ni pamoja na kutofanya marekebisho ya uchumi mapema kabisa, kuua vyama vya ushirika na kuingiza siasa hata katika utaalamu kwa uchache tu.
Kama tutaangalia uwepo wa TV kama kigezo cha maendeleo basi hatutamtendea Mwl haki.Kipaumbele cha Mwl hakikuwa TV, na sijui TV inmsaidiaje mtoto kwenda shule kama hana karo. Mimi nimeishi zama za Mwl nakuhakikishia kuwa tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Lakini sifa moja ambayo watu hawaisemi ni kujenga taifa lenye watu waadilifu,kama mwl angekuwa kama hawa wa leo, angeweza kuuza hata mkoa mmoja na tusingejua. Madini aliyoacha si ndiyo yanasaniwa mikataba mahotelini uingereza!!
Kimataifa mwl alikubalika sana, soma Declassified information ya CIA kuhusu Mwl. Wao wanasema kama kuna kiongozi waliyemuogopa alikuwa ni Mwl, na walisema endapo ujamaa ungefanikiwa basi Afrika ingekuwa sio wanayoitaka, na walihakikisha hilo halitokei. Haya si maneno yangu tafadhali!!
Namalizia kwa kusema, Mwl kama mwanadamu ana mapungufu yake, lakini kwa ugumu na changamoto zilizomkabili, matokeo ya kazi yake hatutayafananisha na mwingine aliyefuata. Maendeleo ya miaka 24 ni makubwa kuliko yale ya Mwinyi/Mkapa/ JK. Tuliokuwepo zama hizo hatuhitaji kusimuliwa.
Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.