Kuna watu wamejenga hoja ya kidini kuwa "katika Uislamu hakuna baba". Hii si kweli hata kidogo. Qurani Tukufu yenyewe inaweka wazi jambo hili kwamba wapo wanaoitwa "baba" kati ya wanadamu na tena ni waamini. Katika Surat Affat (37:102 na kuendelea) tunaona kuwa Ishmaeli anamuita Ibrahim "Baba". Waislamu wanaamini kuwa Mitume wote hata kabla ya Mohammed (SAW) walikuwa ni Waislamu. Kuwa hata Ibrahim alikuwa ni Muislamu. Kwa hiyo kama ni kweli hivi (Italiki na Msisitizo mweuzi wangu)
Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri (37:102)
Na katika sura hiyo hiyo Qurani inawasifia manabii wengine waliotangulia na inapofika kwa Nabii Ilyas (Elia) inasemwa hivi:
NaA hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume
lipo waambia watu wake: Hamwogopi?
Mnamwomba Baa'li na mnamwacha Mbora wa waumbaji
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani? 37:123-126
Kitu pekee ambacho kiko wazi katika Qurani na katika mafundisho ya Uislamu ni kuwa Mungu si Baba. Ukisoma mistari inayofuatia hapo chini hili liko wazi kabisa. Na kwa wanaosoma historia ya dini ni kuwa Uislamu umekataa kabisa toka mwanzo Kumuita Mungu "Baba" kwa sababu Wakristu walikuwa wanamuita Mungu "Baba" na iliaminika kana kwamba wanamaanisha Mungu alichukua mke akazaa naye. Hili Qurani Tukufu inalikataa hata kwenye sura hii:
Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema
Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo!
Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume? 37:151-153
Pia tunaona katika Sura 33:6 kuwa wake wa Mtume ni "mama wa waamini" na ndio maana hata leo Waislamu wanamuona Bi. Khadijah kama "mama yao". Je, kama mke wa nabii (kama mstari unavyosema) ni "mama" wa waumini je nabii mwenyewe anaweza kuchukuliwaje? Hasa ukizingatia kuwa Qurani inawatambulisha wale manabii wa zamani (hiyo sura ya 37) kuwa ni "baba" wa zamani? Je manabii nao ni kama baba zetu?
Kumbe ni rahisi kuona kuwa:
a. Uislamu unatambua nafasi ya "ubaba" na kuwa haikatazi kumuita mtu "baba". Katika Biblia labda ni kali zaidi kwa sababu Yesu ndiye alisema wazi kuwa "Usimwite mtu yeyote baba hapa duniani kwani baba yenu ni mmoja tu aliye mbinguni!" Mathayo 23:9.
b. Uislamu unakataza kumuita Mungu "Baba" kwa sababu Mungu "hakuzaa wala hakuzaliwa". Na ni kinyume na mafundisho yaliyokuwepo ya Wakristu waliomuita Mungu "Baba yetu".
c. Kama ndivyo ilivyo kwamba Qurani inawatambulisha mitume waliotangulia kama "baba" ni wazi kuwa haikatazwi kumuita mtu "baba" moja kwa moja; inakataza kumuita Mungu "baba". Na tunafahamu inaposema wake wa nabii ni "mama" wa waamini sidhani kama kuna mtu anaamini kwamba inasema huyo "mama" alizaa waamini wote kimwili. Ni wazi ni cheo na nafasi ya heshima ambayo mama hao wanazo. Hili ni kweli pia kwa wale manabii. Wanapoitwa "baba" zetu si kwa sababu waliwaingilia mama zetu!
Hivyo, hoja ya kuwa Nyerere hafai kuitwa 'baba' haina msingi na kuwa mtu aliyezaa asiitwe 'baba' nayo haina msingi vile vile!
Nasimama kusahihishwa.
Acha uwongo aya ulizo quote Qur: 37:126
Ni batili naomba usipoteshe watu..ok
Omba msamaha haraka please..