Nusu Karne na CCM? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nusu Karne na CCM?

Discussion in 'Great Thinkers' started by Zitto, Oct 30, 2008.

 1. Zitto

  Zitto MP Kigoma Urban

  #1
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 2, 2007
  Messages: 1,197
  Likes Received: 109
  Trophy Points: 160
  Wana JF,

  Ninaomba kuwashirikisha katika makala yangu hii kuhusiana na hali ya nchi yetu. Nimeandika kufuatia kauli ya Chiligati kuwa nchi ipo shwari na nini nimeona katika Mkoa wa Kwanza wa Operesheni Sangara.

  Tujadiliane  -----------------------------------------------

  Nikiwa Mjini Mugumu Serengeti katika ziara ya kikazi ya viongozi wote wa CHADEMA katika kujenga chama chetu, ninapata taarifa ya mkutano wa waandishi wa habari ambao Katibu Mwenezi wa CCM ndugu Kapteni John Chiligati amekanusha kwamba nchi imekosa mwelekeo. Alikuwa akijibu hoja ya Mwenyekiti wa CHADEMA ndugu Freeman Mbowe kwamba kwa hali ya sasa ya nchi Rais Jakaya Mrisho Kikwete hapaswi kupewa kipindi cha pili cha utawala. Chiligati anasema nchi imetulia, ni shwari kisiasa, kiuchumi na kijamii.

  Chiligati aling’aka na kuanza kutoa matusi yasiomithilika dhidi ya ndugu Mbowe kana kwamba ndugu Mbowe alimtukana ndugu Kikwete. Mbowe hakumtukana Rais Kikwete. Mbowe alisema Uongozi umemwelemea Kikwete na hivyo asipewe kipindi kingine cha uongozi.

  Nilikaa na kutafakari kwa kina sana kwa nini Chiligati amesema maneno ambayo hayaendani na taswira yake kama mtu mpole na mwungana? Mimi ninamwona Chiligati hivyo. Sikumjua kabla sijawa Mbunge, nimemjulia Bungeni tena baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, wakati huo wizara hiyo ilikuwa imebakia na vitengo vya Magereza, Uhamiaji na Zimamoto. Haikuwa Wizara kubwa sana, lakini wizara muhimu kwa usalama wa nchi. Nilimwona ni mtu mwungana, alikuwa akishirikiana kwa karibu sana Waziri wetu kivuli katika Wizara hiyo ndugu Mhonga Ruhwanya. Nilishangazwa sana alipoamua kutoka kwenye hoja na kuamua kumtukana ndugu Mbowe!

  CHADEMA imezindua kampeni maalumu ya kuimarisha chama katika maeneo ya vijijini. Operesheni hii tumeiita ‘OPERESHENI SANGARA’. Kwa nini Sangara? Kwa kweli wala hatukufikiria kwa kina sana kuna nini katika jina hilo, tuliamua kutafuta kitu kinachowaunganisha wananchi wa mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mwanza na Mara. Tulitafuta kitu ambacho kinahusiana na maisha ya wananchi ya kila siku. Tukakuta Sangara ni jina murua kwani ni samaki alie katika ziwa Viktoria na ni samaki ambae analiingiza Taifa mapato mengi sana. Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa zinaonesha kuwa Samaki wa Ziwa Viktoria wanachangia takriban asilimia 8 ya mauzo yetu nje ya nchi. Thamani ya mauzo ya samaki kutoka Ziwa Viktoria ni karibia Tshs. 150 Bilioni kwa mwaka. Hata hivyo sehemu kubwa ya fedha hizi zinabaki kwa wawekezaji wachache na Taifa halipati kiasi kinachostahili cha mapato yake kutokana na utajiri huu. Vilevile wananchi wanalalamika kuwa kitoweo cha samaki kimekuwa ghali sana kufuatia samaki wote kuuzwa nje na wao kubakia na Mapanki. Jina hili lilitosha kuwa sehemu ya kampeni ya uimarishaji wa chama katika Kanda ya Ziwa Viktoria.

  Nimepata fursa ya kutembelea majimbo yote ya Mkoa wa Mara isipokuwa Jimbo la Musoma Vijijini. Musoma Vijijini nimewahi kwenda; Butiama katika misa ya Baba wa Taifa kwa mwaliko maalumu wa Mbunge wa Jimbo hilo na Buhemba kwa ziara ya Kamati ya Rais kuhusu Mikataba ya Madini. Ninaamini kabla hatujaenda Mkoa wa Mwanza kuendelea na Operesheni mnamo tarehe 11 Novemba, tutapata fursa ya kupita katika Jimbo la Musoma Vijijini ili kuongea na wananchi na kuimarisha chama chetu cha CHADEMA.

  Ziara hii imenifumbua macho ya maisha ya Watanzania. Nilipomsikia Chiligati anasema hali ni shwari, kisha nikaangalia maisha ya wananchi wa Buhare (Musoma Mjini), Bukura (Rorya), Nyanungu (Tarime), Muriba (Tarime), Nansimo (Mwibara), Hunyari (Bunda) na Nyamuswa (Bunda), nikasema kweli viongozi wetu hawapo na wananchi (out of touch). Nikachunguza mara ya mwisho ndugu Chiligati alikwenda kutembelea wananchi wa vijijini lini toka amekuwa Katibu Mwenezi wa CCM, nikapata taarifa kuwa hajawahi hata siku moja. Nikathibitisha kuwa sio tu Chiligati alipaniki ‘panick’ bali yeye na wenzake wapo ‘out of touch’! Wanajifungia katika maofisi yao yenye viyoyozi Dar es Salaam na kuitisha ‘press conferences’ na kusema nchi ipo shwari.

  Hali ya nchi sio nzuri hata kidogo, nitatumia mifano halisi niliyoiona katika vijiji vya mkoa wa Mara na kuihusanisha na takwimu za Serikali kujenga hoja zangu kwamba CCM imeshindwa kuongoza Taifa letu, imebaki inatawala na ndio maana wao wenyewe wanapenda kujiita ‘Chama Tawala’. Kwa maoni yangu, hatupaswi kuruhusu CCM kutimiza nusu karne katika Utawala, kwani mwaka 2011 tunatimiza miaka 50 ya Uhuru wa upande mmoja wa Taifa letu (Tanzania Bara). Wazalendo wote wa Taifa hili wanapaswa kujiandaa na kuizuia CCM kutufikisha nusu karne kwani kwa hali ya sasa CCM ni hatari kwa usalama na ustawi wa Taifa letu. Nitajieleza!

  Mwaka 2005, wakati wa Kampeni za Uchaguzi CCM waliahidi katika Ilani yao ya uchaguzi kuwa ifikapo mwaka 2010 watakuwa wamepunguza umasikini wa Watanzania kutoka asilimia 38 ya Watanzania mpaka asilimia 19. Mwaka 2005 kulikuwa kuna Watanzania Masikini takribani milioni 11. Hapa tafsiri ya Masikini ni wale watu wote ambao kipato chao kwa mwezi ni chini ya shs 14,000, yaani chini ya sh 400 kwa siku. Hiki ni kiwango cha chini sana kwani kufuatia kupanda bei kwa bidhaa na hasa chakula, hata mwenye kipato cha shs 30,000 kwa siku bado ni mtu masikini tu.

  Mnamo tarehe 3 Oktoba, Waziri wa Fedha ndugu Mustafa Mkulo alitangaza takwimu mpya za hali ya Umasikini nchini. Takwimu hizo zimefuatia utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu nchini na utafiti huo unaitwa kwa kimombo ‘Household Budget Survey’. Takwimu hizi mpya zinaonesha kuwa Watanzania walio masikini wa kutupwa sasa wamefikia Milioni 12.7. Hii inaonesha kuwa Serikali ya CCM ya awamu ya nne katika kipindi cha miaka 3 ya utawala wake badala ya kupunguza umasikini miongoni mwa Watanzania, imeongeza masikini zaidi ya Milioni 1. Hii imetokana na ukweli kwamba chama hiki kimekuwa ‘nzee’, kimechoka na hakina mawazo mapya. Chama hiki tukikiacha madarakani, tena kikiwa na ukiritimba wa Bunge ambao hivi sasa CCM inao, kitaingiza watu wengi zaidi katika dimbwi la umasikini.

  Njia mojawapo ya kuokoa Taifa letu, ni kutoruhusu CCM kuuunda serikali tena ifikapo mwaka 2010. Ikitokea hivyo, basi CCM isiwe na ukiritimba Bungeni kama ilivyo sasa ambapo asilimia 86 ya wabunge wanatoka chama hicho kimoja. Hii ndio mantiki ya Mbowe kusema tusimruhusu JK kuchukua muhula wa pili. Mbowe hakuwa na maana ya Kikwete kama mtu binafsi bali CCM. Kwani ikiwa ni suala la Kikwete kama mtu binafsi, CCM watabadili mtu na hivyo kuendelea kutawala. Tunachosema, CCM ya awamu ya nne haistahili kupewa muhula wa pili kwani wamechoka na hawana mawazo mapya ya kuondoa umasikini wa Watanzania.

  CCM ya sasa haina idara ya sera wala utafiti na hivyo, hawaongozi tena sera za serikali wanayoongoza bali wanategemea serikali kutengeneza sera na wao wanazikariri katika ilani zao. Lengo la kupunguza umasikini kutoka asilimia 38 mpaka asilimia 19, lilikuwa lengo la MKUKUTA ambapo CCM kwa kutaka kura tu, waliamua kukariri MKUKUTA na kuuweka katika kitabu cha kijani na kicha kuiita ilani.

  Watu wa Gazeti la The Economist waliwahi kuita ilani ya CCM kuwa ni ‘wishlist’. Sasa imedhirika kuwa lengo hili kubwa la kupunguza umasikini, limeshindikana. CCM wataweza nini?
  Leo CCM imetengeneza mataifa mawili ndani ya Taifa moja la Tanzania. Hivi sasa kuna Taifa la Masikini na Taifa la Matajiri. Masikini wana shule zao zinazoitwa Sekondari za Kata. Matajiri wana shule zao zinazoitwa ‘Academies au English Medium’. Watoto wa masikini katika Sekondari za Kata wanasoma katika mazingira magumu sana. Shule hazina walimu, madarasa hayana madirisha na hata vitabu hakuna.

  Nilipokuwa Wilaya ya Rorya nilitembelea Kata ya Bukura. Pale Bukura nilipata bahati ya kutembelea shule ya Kata na kuzungumza na wanafunzi. Shule hii inayoitwa Shule ya Sekondari ya Bukura ina kidato cha Kwanza na cha pili. Shule ya Sekondari Bukura ina Walimu 4 tu na wanafunzi waliniambia walimu wote ni wa masomo ya sanaa. Hakuna Mwalimu wa Sayansi. Shule ya Sekondari Bukura haina uhakika kama mwakani wataweza kuingiza kidato cha kwanza kwani wao wamejenga madarasa mpaka uwezo wao, lakini msingi wa darasa la kidato cha tatu bado upo chini kabisa. Hawana msaada wa serikali.

  Nimejionea madarasa ambayo hayana madirisha wala milango. Kuna watoto wanatembea kilometa nane kufika shule na matokeo yake katika kipindi cha mwaka huu peke yake, watoto wa kike 5 walipata uja uzito.

  Wanafunzi wa Bukura, wanaonekana ni wenye akili sana, waliniambia kwa nini vyama vya siasa tunapewa ruzuku badala ya ruzuku hiyo kujenga miundombinu ya shule zao. Niliwaeleza umuhimu wa vyama vya siasa katika uongozi wa nchi. Nikawaambia lazima vyama viendeshwe na bila ruzuku matajiri wachache watamiliki vyama. Wakaniambia mbona tayari vyama vimeshikwa na matajiri? Wakanisuta na kuniambia mbona ninyi wabunge hamshindi bila kutoa takrima? Wakaniambia mbona wameona rushwa katika uchaguzi wa viongozi wa CCM katika ngazi ya Kata na Tawi?

  Niliwaangalia watoto wale na kukumbuka takwimu za serikali kuhusu elimu. Kwamba hivi sasa kila mwalimu mmoja anafundisha watoto 65 (Rejea PHDR 2007), kwamba watoto 20 wanachangia kitabu kimoja shuleni, kwamba wakati uandikishaji wa watoto umeongezeka na kuvuka malengo ya MKUKUTA, hakuna ufuatiliaji kujua watoto wanasoma nini shuleni. Kata ya Bukura yenye vijiji vya Nyambori, Bwiri, Thabache na Bubombi wananchi wake wanaweza kusema kweli hali nchini ni shwari wakati watoto wao hawapati elimu wanayostahili kama Raia wa Taifa Huru? Hivi Chiligati alipokuwa anamtukana Mbowe kuwa ni muhuni alikuwa anaelezea kadhia hii ya Elimu?

  Lakini Chiligati anajua fika kwamba, fedha zilizoibwa Benki Kuu kwa akaunti ya EPA peke yake zingeweza kujenga madarasa 24,000. Madarasa 24,000 ni sawa na madarasa 2 kila Kijiji maana Tanzania ina vijiji 12,000. Hivyo kama mafisadi wasingefisadi fedha hizi, watoto wa Bukura wasingekuwa wanamlalamikia Mbunge wa Kigoma Kaskazini kuhusiana na vyumba vya madarasa. Kama fedha za EPA zingejenga vyumba za Walimu, zingejenga nyumba 19,000. Lakini CCM iliona ni bora ichukue michango ya watu waliokwapua fedha za EPA ili wanunue fulana na kofia za kampeni kuliko kutunza fedha hizi ziweze kujenga mashule.

  Chiligati anasema nchi ipo shwari, itakuwaje shwari wakati Serikali ya CCM imeshindwa kutunza hazina yetu? Kama wameshindwa kuaminika kwa hazina yetu na kupata tamaa kuchota fedha za kampeni zao 2005, tuwaamini kweli waendelee kuangalia hazina yetu mpaka 2015? Tunaposema wasipewe miaka mingine 5 tuna maana kuwa CCM haiaminiki tena kutunza fedha zetu za kodi. Hawana ujasiri wa kutochota kidogo waende kupigia kampeni.

  CCM na viongozi wake hawajui kuwa kila saa inayopita kuna mwanamke mmoja wa Tanzania anafariki dunia kwa matatizo ya uzazi (Maternal Mortality). Taarifa ya Hali ya umasikini nchini ya mwaka 2007, inaonesha kuwa katika kila Watanzania wanawake 100,000, wanawake 578 wanapoteza maisha kwa ukosefu wa huduma nzuri za afya kwa kina mama. Hii ni sawa na kupoteza Mtanzania mwanamke 1 kila saa. Miaka 47 baada ya uhuru, tunashindwa kulinda afya ya kina mama zetu! Tunajiita Taifa huru na kwamba Taifa hili halina matatizo. Lazima Chiligati anaota! Haiwezekani hali ya Taifa ikawa nzuri ilhali tunapoteza mwanamke mmoja kila saa kwa matatizo ya uzazi.

  CCM kwa uchovu wake imeshindwa kuona ya kwamba kuna chumi mbili nchini na uchumi mmoja unakua na mwingine umedumaa. Uchumi wa mijini (Urban Economy) unakua na kukuzwa na sekta za madini, ujenzi, mawasiliano na utalii. Sekta hizi ndizo sekta zinazokua kwa kasi ikiwemo pia sekta ya fedha kama mabenki na bima. Wenye kushika sekta hizi ni matajiri wenye fedha. Kwao hali ya uchumi ni shwari sana.

  Uchumi wa Vijijini (Rurak Economy) umedumaa. Uchumi huu unaendeshwa na sekta ya Kilimo ambacho ukuaji wake umebakia asilimia 4 tu kwa takribani miaka 3. Hivyo watu wa vijijini hali zao zimekuwa mbaya sana kwani wanauza bidhaa zao kwa bei za vijijini na wananunua bidhaa kama mafuta, sukari nk kwa bei za mijini. Hivyo wananchi wa vijijini wanapigwa kweli kweli na maisha. Serikali ya CCM labda inashindwa kuelewa kuwa baada ya Ndugu Benjamin Mkapa kujenga misingi imara ya uchumi mkubwa (macro) , hii ya Ndugu Kikwete ilipaswa kutafsiri uimara wa misingi hii kwa maisha ya wananchi wa kawaida wanaotegemea kilimo.

  Nilitaraji hii ndio ilikuwa kazi ya msingi ya serikali ya CCM ya awamu ya nne. Imeshindikana miaka 3 ndani ya utawala. Ndio maana tunasema hawastahili kupewa kipindi kingine. Kwa kweli kama chama upinzani, hatuna lingine la kusema. Nchi imekosa mwelekeo.

  Wiki ijayo....... Rushwa, Madini, Uaminifu na uchambuzi zaidi wa umasikini.
   
 2. M

  Mama JF-Expert Member

  #2
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 24, 2008
  Messages: 2,858
  Likes Received: 20
  Trophy Points: 0
  kwanza kabisa nawapongezeni CHADEMA kwa kuanzisha hiyo operation. Nilikuwa baadhi ya members wanaoulizia sana mipango yenu katika maandalizi ya uchaguzi 2010. Nashukuru na hongereni sana kwa hilo. Hii operation ikifanikiwa nchi nzima, mtatoa nuru ya matumaini ya kumkomboa Mtanzania kutoka kwenye lindi la umaskini.

  Baada ya kusema hayo, article?? uliyoweka hapo inahitaji uchambuzi yakinifu. Tuko pamoja, God bless.
   
 3. W

  WildCard JF-Expert Member

  #3
  Oct 30, 2008
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Kwa Wanasiasa kama wewe Mh. Zitto, tena wa upinzani, hatutarajii zaidi ya hayo uliyoyaandika hapo juu. Nadhani umefika wakati sasa muwe mnakwenda mbali kidogo zaidi ya hapo. Mtueleze mikakati yenu inayoelekeza kuyatatua haya matatizo. Tunachohitaji ni SERA mbadala wa hizi za CCM. Tukiwasikiliza nakuwatazama tuwe na IMANI kwamba hizo sera zenu mtazitekeleza, kwamba ninyi viongozi wa upinzani ni tofauti kabisa na hawa walioko madarakani. Kenya wameiondoa KANU kwa mbwembwe na tambo nyingi! Hakuna jipya. Zambia wameiondoa UNIP ya Mzee Kaunda. Hali ni ileile. Ni nini kinakufanya wewe na wenzako muamini mnaweza kuleta mabadiliko yanayohitajika?
   
 4. Zitto

  Zitto MP Kigoma Urban

  #4
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 2, 2007
  Messages: 1,197
  Likes Received: 109
  Trophy Points: 160
  www.chadema.net
   
 5. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #5
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Wildcard, mikakati na sera za upinzani zinatatua vipi tatizo lilipo sasa? Ili kuweza kuja na mapendekezo ya uhakika na ambayo yanawezekana la kwanza ni kutambua tatizo na kina cha tatizo hilo. Siyo tu kulitambua lakini kuweza hata ikibidi kulichambua katika sehemu zake ndogondogo.

  Katika makala hiyo ya Zitto hapo juu ninachoona ni jinsi gani daktari mpasuaji anapomuandaa mgonjwa kwa upasuaji mkubwa na kabla ya kuanza upasuaji au kukusanya timu ya upasuaji maandalizi ya kulielewa tatizo yanafanyika. Hivyo mazungumzo na mgonjwa, x-rays, c-scans n.k n.k

  Tusipolielewa tatizo kiusahihihi ni rahisi kwa watu kuja na mapendekezo ya "Aspirin"!
   
 6. I

  Interested Observer JF-Expert Member

  #6
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 27, 2006
  Messages: 1,402
  Likes Received: 434
  Trophy Points: 180
  Hi Wildcard, huoni hiyo narrative start ya Mr. Zitto; kwanza appreciate hiyo maverick start; alivyo-define matatizo ya tanzania ambayo CCM hawajayaona almost half a century. Let us combine our forces and joint this guy; he made points! For me it is a ground breaking! Go on Zitto!!
   
 7. M

  Mwafrika wa Kike JF-Expert Member

  #7
  Oct 30, 2008
  Joined: Jul 5, 2007
  Messages: 5,194
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  Tanzania sio Kenya kama vile ilivyo kuwa Tanzania sio Zambia
   
 8. N

  Natasha Ismail JF-Expert Member

  #8
  Oct 30, 2008
  Joined: Jul 14, 2008
  Messages: 511
  Likes Received: 153
  Trophy Points: 60
  ZITTO,
  Big up tuko pamoja.
  `SLAA FOR PRESIDENCY 2010'.
   
 9. AbdulKensington

  AbdulKensington Member

  #9
  Oct 30, 2008
  Joined: Oct 21, 2008
  Messages: 72
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nafurahi kuona kwamba CCM ina upinzani na nimefurahishwa zaidi na jitihada ya upinzani huo, ningependa kuwaomba wana-CHADEMA waendelee na mwelekeo wao....kwa kweli nchi hii iko kwenye hali mbaya na sidhani kwamba CCM watatusaidia....ni muda mwafaka sasa kwa Watanzania kupata muamko wa ki-siasa na kuona kwamba hii serekali haifai, faida gani ya kuwa na demokrasia kama hatuwapi CHADEMA nafasi ya kuongoza nchi? Wakishindwa na wao tuwatimue 2015...jamani hii ndo raha ya Demokrasia!
   
 10. J

  JokaKuu Platinum Member

  #10
  Oct 30, 2008
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,794
  Likes Received: 5,068
  Trophy Points: 280
  WildCard,

  ..wa-Tanzania tujaribu hata hao upinzani. wakishindwa tuwaondoe kwa kura.
   
 11. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #11
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Zitto umejitahidi kujenga hoja lakini hapo ulipomalizia umenikuna sana. TUNAJENGA CHUMI MBILI. Kwa mtindo huo, kila siku watanzania walio wengi wataendelea kusikia maendeleo ya kiuchumi kupitia takwimu bila kuona takwimu hizo zikiakisi maisha yao ya kila siku
   
 12. s

  sumar Member

  #12
  Oct 30, 2008
  Joined: Jun 15, 2008
  Messages: 36
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kwani sh. Zitto- haiwezekani kuwa na serikali ndani ya serikali. Kwanini vyama vya upinzani visianze kuchochea mabadiliko ya uchumi. Kama wanavijiji wanyonge wakihamasishwa na kuongozwa kujiletea mabadiliko si ndo maendeleo yenyewe.
   
 13. s

  sheshe New Member

  #13
  Oct 30, 2008
  Joined: Oct 30, 2008
  Messages: 4
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Chadema juu! Zitto nakufagilia!!!
   
 14. M

  MkamaP JF-Expert Member

  #14
  Oct 30, 2008
  Joined: Jan 27, 2007
  Messages: 7,313
  Likes Received: 1,452
  Trophy Points: 280

  Nani amekudaganya kwamba vyama vya upinzani vichochee mabadiliko ya kiuchumi??

  wewe hujui Sera ya upinzani TZ uchochezi wa uchumi ni lazima wapewe u Rais na serikali??
   
 15. s

  sheshe New Member

  #15
  Oct 30, 2008
  Joined: Oct 30, 2008
  Messages: 4
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  chadema mnatisha,mmefanya kazi nzuri sana.Watanzania tunawaunga mkono kwa juhudi zenu za kuwatumikia wananchi.
   
 16. Mwita Maranya

  Mwita Maranya JF-Expert Member

  #16
  Oct 30, 2008
  Joined: Jul 1, 2008
  Messages: 10,569
  Likes Received: 104
  Trophy Points: 145
  niwapongeze kwa hii strategy, naamini itawapa mafanikio makubwa sana.
  watanzania wengi wa vijijini hawajitambui, na hata pale wanapojaribu kufumbuka macho wanapofushwa na vitenge,kofia na t-shirts za ccm.
  mkiweza kujikita vizuri kuanzia ngazi za shina kama ilivyo ccm mtaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wananchi.
  ccm wanapata ufuasi mkubwa mashinani kwa kuwa hadi leo wajumbe wa mashina wa ccm ndio hao hao wawakilishi wa serikali za mitaa,kwahiyo ni rahisi sana kuwashawishi wapiga kura kwakuwa wako nao siku zote.mkiweza kuwa na wajumbe wa mashina kila kona ya nchi hii, itasaidia sana kuwaelimisha watanzania faida ya kufanya mabadiliko ya uongozi wa nchi hii na hasara tunayoendelea kuipata kwa kuendelea kukichagua chama failure kutuongoza.
  ila niwakumbushe isije ikawa ni nguvu ya soda,hakikisheni mnatembelea majimbo yote ya tanzania,maana vuguvugu la songea lilianza vizuri lakini hatujui limepotelea wapi!!!
   
 17. Nono

  Nono JF-Expert Member

  #17
  Oct 30, 2008
  Joined: Feb 11, 2008
  Messages: 1,305
  Likes Received: 86
  Trophy Points: 145
  Mh. Zito nashukuru sana kwa makala yako nzuri. Ila nachelea kidogo kusema kuwa, je upo ukweli kuwa uchumi wa vijijini umekuwa kwa asilimia 4? au ulikuwa unamaanisha -4% (yaani unashuka kwa 4%)? Nasema hivi kwa sababu, uweza wa wanakijiji umekuwa ukipungua kila mwaka, huko tulikotoka wanakulima walikuwa na uweza wa kununua japo mbegu, mbole na madawa, siku hizi hawawezi. Sina hakika kuwa kilimo cha pamba, korosho, tumbaku kimeongezeka vipi tukilinganisha na miaka ya nyuma na wakulima wameweza kujitegemea zaidi kwa asilimia 4? Kilimo cha mazao kama kahawa ndio usiseme, kwani tangu mkapa alipoingia madarakani ndio wakulima walizikwa, mtakumbuka hata wakati wakulima walipopewa fedha za ruzuku na EU, serikali kupitia waziri wake wakati huo "Keenja", waliwanyima wakulima kwa kisingizio kuwa fedha hizo zingeingizwa kwenye ujenzi wa miundombinu, mpaka kesho (Nadhani walikuwa wanatafuta fungu la ushindi wa kimbunga).

  Nasikitika kuwa kuna umasikini wa kutisha mno vijijini, Watu wanapata shida sana kupata mlo mmoja wa ugali kwa mchicha, watu wakiona nyama, MACHO yanatoa machozi ya damu. Maisha yamewafanya wakulima wengi mno wamekata tamaa, na sasa wameamua kunywa GONGO kwa kwenda mbele, sijui ni maneno ya mithali kuwa "MPE KILEO ALIYE MASKINI ILI ALEWE AISAHAU SHIDA YAKE"

  Inasikitisha, ile wenye mustakabali wa nchi yetu ni sisi watanzania wenyewe.

  Kama Marekani inakaribia kutawaliwa na mtu mweusi, iweje watanzania kuwa wagumu kuruhusu watanzania wenzetu wa mrengo mwingine kutawala nchi?

  Sijui, kwa nini watanzania tunaendelea kuwa wazito, tubadilike?
   
 18. s

  sheshe New Member

  #18
  Oct 30, 2008
  Joined: Oct 30, 2008
  Messages: 4
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  nchi imeuzwa mirerani tunateseka lakini Tanzanite inasafirishwa na Tanzanite one kila siku.wazawa tunakufa,viongozi wajuu wanalijua ilo,sema ufisadi umewazidi.zito wewe ni kama Barack Obama.
   
 19. Zitto

  Zitto MP Kigoma Urban

  #19
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 2, 2007
  Messages: 1,197
  Likes Received: 109
  Trophy Points: 160

  Nina maanisha 4%! ukuaji wa sekta ya kilimo mwaka 2007 ulikuwa 4% na imekuwa hivyo kwa miaka mitatu iiliyopita. Hii maana yake 'stagnation'. Haiwi -ve. Kiuchumi ikiwa negative growth ni balaa kubwa. Bei ya kahawa mwaka jana imepanda sana na hata mchango wa kahawa katika mauzo nje umeongezeka kidogo. Haijawa hasi bado.

  Ili umasikini vijijini uondoke inabidi uzalishaji vijijini uongezeke kwa takribani asilimia 8 kwa miaka 3 mfululizo. Hapo tunaweza kuona mabadiliko katika vijiji vyetu. Tumeshindwa so far kuweka mikakati muafaka ya kufikia hilo na matokeo yake sisi na mbolea ya ruzuku tu ambayo nao inapanda bei sana katika soko la dunia na hivyo inakuwa haina maana.
   
 20. Zitto

  Zitto MP Kigoma Urban

  #20
  Oct 30, 2008
  Joined: Mar 2, 2007
  Messages: 1,197
  Likes Received: 109
  Trophy Points: 160
  Hapana. Mama yangu Mtanzania, Baba yangu Mtanzania. Sina bibi kontinenti lingine. Havent done my biography. Obama did 2.
  This country has ceased to be the land of opportunities where the rich and the poor kids share the same desk at school and the rich and poor woman meet at the same clinic.

  Are we being judged according to the content of our characters or according to the zeros in our bank accounts?
   
Loading...