SoC02 Nini/kipi kifanyike ili tuwe na elimu bora Tanzania?

Stories of Change - 2022 Competition

luddo17

Member
Apr 17, 2010
5
8
Nikiwa kama mdau wa elimu, nafahamu kwamba kufundisha na ujifunzaji ni mchakato mgumu sana. Unahitaji utekelezaji na ufuatiliaji.

Katika insha hii, lengo langu halisi ni kuangalia cha kupaswa kufanywa ili kupatikane ufundishaji na ujifunzaji bora, yaani kwa maneno mengine, tupate elimu bora.

Kwa mtazamo wangu, yafuatayo ni mapungufu makubwa sana yaliyomo kwenye mfumo wetu wa elimu hapa Tanzania.

i. Idadi kubwa sana ya walimu hawana taaluma ya ualimu, lakini wako mashuleni wakifundisha. Hata wale wenye taaluma, wengi bado ni wale waliofeli kwenye masomo wanayoyafundisha. Ukifanya tathmini ya kuangalia mwalimu aliyepata daraja la kwanza au alama A kwenye somo lake, utapata mmoja kati ya mia moja. Walimu wengi ni watu waliopata madaraja hafifu kwenye mitihani yao wakati wakiwa wanafunzi.

ii. Walimu wengi wanajishughulisha na biashara kutokana na mishahara isiyokidhi mahitaji. Maisha ni magumu na hawawezi kumudu kujikimu ipasavyo. Hili linapelekea hali za walimu kuwa duni.

iii. Walimu wanakosa motisha na hamasa nyingine na hivyo kujikuta wakiuona ualimu kama sawa tu na kada nyingine.

iv. Walimu wengi wanafundisha bila kuwa na zana/vitendea kazi vya kutosha mfano chaki, vitabu vya ziada na kiada, maabara na vingine vya kufundishia.

v. Walimu wengi wanaishi kwenye mazingira duni na magumu na wengine wako kwenye makazi yasiyo na hadhi ya kuishi mwalimu au walimu.

vi. Walimu wengi wamepoeza ari na moyo wa kazi kwa sababu wameshaathirika kifikra na hivyo hawajisumbui tena kufundisha ipasavyo.

Kwa upande wa wanafunzi, nako kuna mapungufu yafuatayo:

i. Kiwango cha taaluma kwa wanafunzi wengi kimezorota. Wanafunzi wengi wa shule za msingi, wanamaliza shule wakiwa hawajui hata kusoma na kuandika.

ii. wanafunzi wa shule za sekondari wengi wanamaliza shule wakiwa na matokeo mabaya, wengi wakiwa wamepata daraja la nne au Daraja sifuri kabisa

iii. vifaa vya kujifunzia havitoshi. Matokeo yake wanafunzi wanakosa fursa ya kufundishwa sehemu ya mihutsari ya masomo

iv. Kuna utoro mkubwa sana mashuleni ambao unasababishwa na kukosekana kwa hamasa miongoni mwa wazazi, uwezo duni wa kulipia karo pamoja na uwezekano finyu wa kupenya kwenye soko la ajira baada ya kuhitimu masomo.

v. Maudhui ya mtaala hayaakisi mahitaji halisi ya wanafunzi kwani hayaangalii vipaji ambavyo kila mwanafunzi amejaaliwa na wala hayawawezeshi wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa maisha. Mtaala umepitwa na wakati kulinganisha na mahitaji ya ulimwengu wa sasa.

vi. wanafunzi wanakosa vifaa vya burudani kwa vile hakuna michezo ya kutosha mashuleni.

vii. Wanafunzi wanakosa huduma za maktaba na maabara zilizotimilika mashuleni.

viii. Wanafunzi wengi wa kike hawamalizi masomo kutokana na mimba na matendo mengine ya kimaadili.

ix. Tabia njema miongoni mwa wanafunzi wengi imeporomoka kutokana na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kwenye eneo la mazingira ya kufundishia, kuwekuweko na ongezeko kubwa la shule katika miaka ya hivi karibuni, ongezeko lisilowiana na idadi ya ongezeko la walimu.

i. Shule hizi nyingi hazina vifaa vya maabara, majengo ya maabara, viwanja vya michezo, samani na vitabu.

ii. Madarasani kumefurika wanafunzi wengi wasioendana na idadi ya walimu. Hakuna uwiano wa walimu na wanafunzi.

iii. Shule nyingi hazina maktaba, miundo mbinu ya maji taka, umeme na maji.

iv. Shule nyingi hazina vifaa vya kielektroniki kama mtandao wa intaneti, tarakilishi, luninga, redio pamoja na vifaa vya kufundishia kwa macho na kwa kusikiliza.

HATUA MTAMBUKA

i. Elimu ni lazima itoe ujuzi, maarifa na mtazamo kwa kufuatana na itikadi na mwelekeo wa kijamii na kiuchumi wa jamii kwa wakati husika.

ii. Ni lazima kujitahidi kuipata elimu iliyo bora kupitia maboresho ya kiwango cha elimu.

iii. Ni lazima kujitahidi kuwa na utawala na uongozi bora wa kielimu

iv.Tunahitaji rasilimali za kufundishia, raslimali watu na raslimali fedha.

v. Tutafakari aina ya mitihani yetu kama kweli inakidhi na kuwapima wanafunzi wetu ipasavyo. Je ni sahihi kumpima mwanafunzi aliyekaa darasani kwa miaka saba kwa karatasi yenye maswali 45, tena kwa maswali ya kuchagua? Akipata maswali yote, anaonekana amefaulu; akishindwa kujibu maswali hayo, anaonekana amefeli. Vivyo hivyo mwanafunzi wa sekondari. Je ni kweli kuwa mwanafunzi aliyeshindwa kujibu ipasavyo maswali ya mtihani, hana akili na amefeli?

SULUHISHO: NINI KIFANYIKE?
Kwa maoni yangu, ili kupata elimu bora nchini Tanzania, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:

1. Kuwepo na mwamko wa kuhimiza ari ya kujifunza kupitia hamasa na msisitizo, vitu ambavyo ni vichocheo chanya. Mfano mzuri ni sheria ya kuzungumza kiingereza mashuleni.

2.Yaanzishwe mambo mapya ya kielimu yanayowashirikisha wanafunzi wengi mfano semina, midahalo, makongamano, warsha nk

3. Wanafunzi wahamasishwe na kumotishwa kwa zawadi, tuzo na vivutio vyenye kuleta na kuinua ari ya ujifunzaji. Kwa mfano, wanafunzi wakitembelea mojawapo ya vivutio lukuki vya utalii vilivyopo nchini, watahamasika kujifunza zaidi darasani. Sio rahisi kwa mwanafunzi anayetaka kuwa rubani, akapekwa uwanja wa ndege, akaiona ndege na kuipanda na kisha akazembea darasani.

4. Wanafunzi washindanishwe kupata madaraja au alama za juu darasani. Kila mwanafunzi ashughulishwe kupata alama A.

5. Wanafunzi wote wanaofaulu vizuri wazawadiwe. Wale waliofanya vibaya, wasichekwe au kuzomewa au kuadhibiwa bali watiwe moyo na wahamasishwe kutokata tamaa. Kumkatisha tamaa mwanafunzi ni kichocheo hasi katika suala zima la ujifunzaji.

6. Walimu waanzishe vikundi vya pamoja vya kujisomea darasani vyenye mchanganyiko wa wanafunzi wenye uwezo wa juu, wenye uwezo wa kati na wale wenye uwezo wa chini kwa usimamizi wa walimu husika.

7. Walimu, hasa wa madarasa, wahimizwe kupitia na kuzibaini changamoto binafsi za wanafunzi wao.

8. Walimu wa malezi mashuleni wawe wabunifu wa kuandaa semina na mikutano ya mara kwa mara na wanafunzi ili kuondoa tabia zote zisizofaa na zinazozorotesha maendeleo yao.

Kwa upande wa mazingira ya kujifunzia, napendekeza yafuatayo:

1. Pawepo na vifaa vya kutosha vya kujifunzia kwa kila mwanafunzi ili aweze kujifunza kwa usahihi, utulivu na umakini.

2. Kila shule iwe na maabara mbalimbali zilizosheheni vifaa vyote vya kujifunzia pamoja na walimu waliobobea kwenye masomo hayo.

3. Wanafunzi wapewe muda mrefu na mwingi wa kujifunza wao wenyewe kwa vitendo badala ya walimu kuwa viongozi muda wote na kwa kila kitu darasani.

4. Shule zianzishe mradi ya kujitegemea na kujiongezea kipato mfano ufugaji wa kuku, migahawa, nk. Hii itawawezesha pia wanafunzi kujifunza mbinu za maisha na ujuzi wa kujitegemea pindi wamalizapo masomo.

5. Shule zote nchini ziwe na huduma ya umeme wa gridi ya Taifa ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa umakini muda wote. Shule kama haina umeme, itawezaje kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kikamilifu?
 
Back
Top Bottom