SoC02 Nimehitimu shahada ya kilimo. Je, kuna haja ya mimi kusubiri kuajiriwa?

Stories of Change - 2022 Competition
Aug 15, 2022
7
3
Kabla hata sijamaliza kusoma shahada yangu ya kilimo (general agriculture) pale chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine, swali ambalo nilikuwa najiuliza mara kwa mara je hivi nikimaliza kusoma hapa nisubiri kuajiriwa au ninaweza kujiajiri mwenyewe
Kadri nikiendelea na masomo swali hili lilikuwa bado sijalipatia ufumbuzi maana nikifikiria kujiajiri swali linakuja ni wapi nitapata mtaji.

Mawazo haya nilianza nayo toka niko mwaka wa pili wa masomo lakini mwaka uliisha nikiwa sijui nitafanya nini baadae baada ya kuhitimu.

Baada ya kumaliza mwaka huo wa pili nilikwenda likizo nyumbani ambako ni Tabora. Mazingira niliyoyakuta yalinikatisha zaidi tamaa maana nilikuta vijana wenzangu kama mimi wapo hawana cha kufanya na wanalalamika hali ya maisha kuwa ni ngumu sana, fursa za ajira hakuna. Kila tukizungumza mada yetu kuu ni nini tufanye ili baadae tujikomboe kiuchumi.

Ila chakushangaza vijana wenzangu walikuwa wanaona kama mimi tayari nimeshayapatia maisha, yaani kwa kuwa nilikuwa nasoma chuo kikuu. Kila nikichangia mada ananyanyuka mmoja na kusema bora yako we mwenzetu ukimaliza kusoma tu unaanza kazi na pesa unapata.

Nilitamani sana kuwaelezea uhalisia ni upi lakini nilishindwa maana ingekuwa ni vigumu sana kuwaelezea na kunielewa.

Hali hiyo ilizidi sana kuniumiza na kunifikirisha na kujiuliza maswali mengi, hivi nikihitimu na kwa bahati mbaya nisipopata ajira hawa jamaa zangu watanionaje.

Bhasi kadri muda ulivyokuwa unakwenda na likizo inakaribia kumalizika nilipata mawazo ni nini nifanye. Mawazo ya nini chakufanya yalikuja baada ya kumtazama baba yangu mzazi ambaye biashara yake ilikuwa ni kukusanya mazao na kusubiri bei ifike nzuri Ndio auze. Kupitia biashara ya baba yangu niliona naweza kuwekeza pesa ndogo ambayo itanipata faida kiasi.

Baada ya kufikia uamuzi huo niliongea na baba kumuelezea mpango wangu na kumuomba anisaidie kunikusanyia mazao kipindi cha mavuno kitapofika. Baba aliniuliza pesa ya kukusanya mzigo naitoa wapi. Ni swali ambalo nilikuwa nimejipanga vizuri kulijibu na nilikuwa natarajia kuuulizwa pia.

Kipindi hicho nilikuwa na 270000/= ambayo niliibana kutoka kwenye pesa yangu ya matumizi nikiwa chuo, na nilipiga hesabu nikaona ninaweza kufikisha laki 5 mpaka muda wa mavuno utakokuwa umeanza ambao kwa kawaida kwa sisi huku kwetu huwa ni mwezi februari mpka mwezi june lakini ni kulingana na zao husika na masika huanza mwezi Novemba.

Kwahiyo nilimuelezea baba mpaka ukifika mwezi wa Februari ninaweza kuipata hiyo pesa ambayo ni laki 5. Ila kabla ya kumaliza mazungumzo nilimuliza kwa pesa hiyo ninaweza kukusanya zao gani. Baba aliniambia kwa sasa zao ambalo linafaida nzuri ni KARANGA, na kama msimu unakuwa vizuri litakupa faida.

Nilihitaji mchanganuo kutoka kwa baba ni vipi pesa hiyo ataigawa, na mchanganuo ulikuwa kama ifuatavyo.

Kipindi cha mavuno gunia la debe sita la karanga ni 30000/= kutoka kwa ukulima shambani ( karanga zinakuwa bado mbichi kwahiyo kazi ya kuzikausha kwenye jua inakuwa ni yangu).

Kwahiyo kwa laki tano ninapata gunia 16 ambazo ni sawa na 480000/=

Pesa inayobakia ni 20000/= , na kusafirisha gunia moja kutoka kituo ambako mkulima na mlanguzi wanakutana mpaka nyumbani ni 2000/= na usafiri unaotumika ni baiskeli kwahiyo inahitajika 32000/= lakini pesa iliyobakia ni elfu 20 kwahiyo aliniahidi ataniongezea kiasi kilichozidi ambacho ni 12000/=

Na muda wa kuuza ukifika gunia moja linakadiriwa kufika hadi 60000/= kwa kima cha chini lakini pia unaweza kuzimenya na kuuza kwa kilo.

Hata hivyo alinisisitizia kuwa hayo yote yanategemea na msimu umekuaje na pia uvumilivu unahitajika kusubiri mpka bei itakapokuwa nzuri na kuna uwezokano wa bei kutokuwa nzuri pia.

Mahesabu hayo ya baba yangu yalinitia moyo na kuona naweza kufanya kitu japo kuwa malengo yalikuwa ni kujishughulisha na kile ambacho nimesoma lakini nikaona naweza kuanzia huku ili nipate mtaji wa kuwekeza kwenye kilimo.

Kutokana na maeneo ninayotoka uwezokano wa kufanya kilimo niliuona hasa kilimo cha mpunga kwahiyo niliweka malengo huko.

Hatimae nilifungua chuo kwenda kumalizia mwaka wangu wa mwisho, ilikuwa ni Novemba 2019. Kama nilivyomuahidi baba kuwa mpaka mwezi wa pili nitakuwa nishaipata pesa ya kukamilisha mradi ninaotaka kuanzisha, bhasi ilikuwa kama nilivyopanga nilipata 230000/= kutoka kwenye pesa ya matumizi na nikamtumia baba.

Huku nikiendelea na masomo bado nilikuwa naumiza kichwa kuchagua ni zao gani nikalime baada kuhitimu ingawa awali kilimo cha mpunga ndio lilikuwa ni lengo
Mwenyezi Mungu alitia neema zake mnamo mwezi wa 7 ( July) 2020 nilihitimu shahada yangu ya kilimo na nikarudi nyumbani ili nianze utaratibu wa kufanya kile ambacho nimepanga.

Kipindi hicho ndio ulikuwa msimu wa mavuno umeisha na kiangazi kimeisha kwahiyo ilinibidi nikae tu kwanza nyumbani nikisubiri masika ianze na mimi nianzie shughuli alafu pia kipindi hicho karanga zilizokusanya zilikuwa bado hazijauzwa na tulikuwa tunasubiri bei iwe nzuri.

Baada ya miezi minne kupita masika ya msimu ujao ilianza na bei ya karanga ilikuwa imeshakuwa nzuri, gunia moja lilikuwa limefika 68000/= lakini nilipata changamoto ya baadhi ya maguni kuharibiwa na panya mahali nilipokuwa nimezihifadhi ingawa changamoto hiyo haikuwa kubwa ya kutisha maana ilikuwa ni magunia manne ndio yalikuwa yamefumuliwa na panya kwahiyo nilipoyafumua vizuri na kuyapanga upya ilikuwa ni kama gunia moj ndio limeharibiwa.

Nilifanikiwa kuuza magunia 15 yakiwa hayajamenywa na kufikisha 1M, na hiyo ndio ilikuwa lengo langu kuwa nikianza kilimo na mtaji wa 1M itakuwa ni vizuri. Kabla ya msimu wa masika kufika nilikuwa tayari nimeshafuatilia mashamba ya kukodi na ilikuwa heka moja inakodishwa kwa shilingi 50000/= kwahiyo nilikodi heka 1 na nusu ambazo zilinigharimu 80000/=

Pia ilinigharimu 550000/= kwa ajili ya wafanyakazi na kukodi jembe la ng’ombe na kwa bahati nzuri nilipata wanakijiji wanne ambao walinipigia kazi ya kutosha kwa malipo nafuu.

Kwa kipindi hicho sikutumia mbegu za kisasa nilitumia mbegu za kawaida tu ambazo nazo zilinigharimu laki 1 amabyo ni sawa na gunia moja la mpunga kwa kipindi hicho.
Kwa msimu huo wa kwanza kiukweli mambo hayakuwa vizuri kama nilivyotarajia na changamoto kubwa ilikuwa ni ugeni kwenye kilimo licha ya kuwa ndicho nilichosema nikiwa chuo na nikagundua kuwa kuna ugumu mkubwa sana kwenye kuyageuza maarifa kwenda kwenye vitendo.

Ila mpka sasa namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kiasi nimeweza kujikomboa kutoka na janga la uhaba wa ajira kwa kuweza kujiajiri kwenye kilimo.

Kilimo kinalipa changamkia fursa
 
Umejitaidi na umeonyesha udhubutu ,na amini utafika mbali sana .ubarikiwe na asante Kwa madini .
 
Back
Top Bottom