Nchi za Afrika zafaa kuiga mbinu za kisasa za kilimo kutoka China

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
Na Tom Wanjala

gfdhgfdhfd.jpg



Mnamo mwaka wa 1978, China ilikuwa miongoni mwa mataifa maskini duniani. Kutoka mwaka huo, taifa hili likaja na mikakati na harakati za kujitoa kwenye hali hii ya umaskini iliyokuwa tishio kwa mamilioni ya raia wake. Ikiwa ni nchi pekee ulimwenguni yenye idadi kubwa zaidi ya watu, China imejizatiti kuinua raia wake na kuwa taifa lenye uchumi unaokua kwa haraka.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2015, pato la taifa la China limekuwa likiongezeka kwa asilimia nane kila mwaka tangu mwaka wa 1978. Kinyume na China, bara la Afrika liliandikisha pato la chini mno kati ya mwaka wa 1976 na miaka ya tisini. Miaka ya hivi karibuni, Afrika imejitahidi na kushuhudia baadhi ya mataifa yake yakifanya vizuri kiuchumi. Hata hivyo, ikumbukwe kuwa, mataifa yanayonawiri kiuchumi Afrika, ni machache mno, huku mengi yakisalia na uchumi dhaifu. Je, ni kipi China inafanya ambacho Afrika haifanyi?

Akizungumza na idhaa ya CRI Kiswahili, mtaalam wa kilimo kutoka kaunti ya Murang’a, Bwana William Kibe anasema kuwa siri ya kumaliza umaskini nchini China, ilikuwa kuwekeza kwenye kilimo, kisha baadaye kwenye teknolojia.

“Taifa lenye njaa haliwezi kujitegemea na kuwa imara. Kwanza kabisa, lazima raia wawe na chakula cha kutosha, wapate nguvu ya kujenga taifa. China ilianza kwa kutilia mkazo kilimo bora mashambani,’’ anasema Kibe.

Kibe ambaye pia ni mkufunzi wa kilimo anasema kuwa China imewainua raia wake wengi sana kutoka kwenye umaskini kwa kuzingatia sana kilimo na uzalishaji wa chakula. Aidha, baada ya kuhakikisha kuwa raia wake wana chakula cha kutosha, China kwa sasa inasambaza chakula chake kote duniani haswa kwa mataifa yanayostawi.

“Sio siri kwamba hivi sasa kote duniani, China inaongoza katika uzalishaji wa vyakula mbali mbali. Mataifa mengi duniani yananufaika sana na vyakula kutoka China. Si mpunga, matunda na hata mboga,’’ aliongeza Kibe.

Kwa ushirikiano na raia wake, serikali ya China ilikuwa na majukumu muhimu ya kutimiza ikiwemo mipango ya kubadilisha maeneo kame kuwa ya mashamba ya upanzi. Wakulima walikuwa tayari kujaribu mbinu mpya za kilimo.

Katika miaka ya 1980, kilimo cha kisasa kilishika kasi nchini China na uzalishaji wa chakula ukafanikiwa zaidi kuliko hapo awali huku pembejeo mpya za kusaidia kulima, kupanda mbegu na kufanya kazi nyingine zikitumiwa kila siku na wakulima zaidi na zaidi. Kaya ndogondogo za wakulima ambazo zilikuwa sehemu kubwa ya idadi ya wakulima, zikawa sehemu ya mtazamo wa nchi wa kufanikisha kilimo cha kisasa, kwa msaada wa teknolojia mpya na huduma bora za kibiashara. Na ili kuwawezesha wakulima hao kushiriki kilimo hicho cha kisasa, baadhi ya maeneo ya vijijini yalikumbatia teknolojia mpya ili kuboresha ufanisi wa uzalishaji. Droni, kwa mfano, kwa sasa zinatumika pakubwa kwa upanuzi wa kilimo.

Mataifa mengi ya Afrika yana nafasi nzuri sana ya kujiinua kwenye sekta ya kilimo. Kama mashamba yapo na hali ya hewa ni shwari kabisa. Aidha, tatizo kubwa la kilimo Afrika ni mbinu za ukulima. Maeneo mengi bado yameshikilia mbinu za jadi, ambazo zimepitwa na wakati.

Joseph Muriithi ambaye ni mmoja wa maafisa wa kilimo kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Kenya anasema kuwa Afrika ina uwezo wa kuwa kiwango kimoja na China, katika uzalishaji wa Chakula. Aidha, anaongeza kuwa, kwa hili kuafikiwa, lazima wakulima wahamasishwe kutumia mbinu za kisasa za kilimo.

“China inatumia sana teknolojia katika kilimo. Hapa ndipo Afrika inapopata ugumu kufaulu,,” anasema Muriithi.

Ikiwa mwandani wa Afrika, China imekuwa ikitoa mafunzo ya kilimo kwa wakulima wengi barani hapa. Isitoshe, ikumbukwe kuwa shamba la mpunga la Wanbao lililoko nchini Msumbiji ni mfano mwema wa ushirikiano huu. Mradi huo, unaotekelezwa na kampuni ya China umekuwa gumzo kote duniani kwa uzalishaji wa mchele mzuri ambao umekuwa ukiuzwa kwa mataifa mengi.

Yapo matumaini makubwa kwa Afrika kujiinua kwenye kilimo. Hii ni kutokana na ushirikiano wa karibu na China, ambayo tayari imeweka mikakati mbalimbali ya kuinua sekta ya ukilimo Afrika.
 
Technology za kisasa za kilimo zipo tele China tuwape ushirikiano zisambae nchini kuwainua wakulima.
 
Back
Top Bottom