Natangaza rasmi dhamira ya kugombea Ubunge 2010

John Mnyika

JF-Expert Member
Jun 16, 2006
712
1,240
WanaJF, nawaletea taarifa ambayo niliitoa jana kupitia http://mnyika.blogspot.com na katika Kongamano la Vijana la Demokrasia na Maendeleo Jimbo la Ubungo. Nawatakia mjadala mwema.

Ni wakati wa mabadiliko ya kweli; tuwajibike

Utangulizi

Wapendwa wananchi wezangu na marafiki zangu ndani na nje ya jimbo la Ubungo. Ninayofuraha kuwatangazia rasmi dhamira yangu ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Nimefikia uamuzi huu baada ya kusikia maoni ya wengi wenu na kuisikiliza pia nafsi yangu katika kipindi cha kuanzia mwishoni mwa mwaka 2009 mpaka mwanzoni mwa mwaka 2010. Wakati wa kampeni bado, hivyo sitazungumzia kwa sasa ahadi zangu kwenu wala ilani ya chama; lakini inatosha kuwaambia tu kwamba: ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike. Naamini katika kuwa na uongozi bora wenye dira na uadilifu wa kuwezesha uwajibikaji katika kusimamia rasilimali za umma ikiwemo kodi zetu na mali asili za nchi yetu kwa ajili ya kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa wote.


Nautambua wajibu; tushirikiane

Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake ni diwani katika halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri ya umuhimu).

Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.

Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.

Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria unaosubiriwa kutungiwa kanuni. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.

Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii.

Nilisema wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, na narudia leo. Kipaumbele cha wananchi wa Jimbo la Ubungo ni kupata mbunge mkweli, mwadilifu, mwajibikaji, mwenye dira, atayewasilikiliza na kuwawakilisha ipasavyo. Iwe ni wananchi wa Kwembe, Mloganzila na maeneo mengine yenye migogoro ya ardhi. Ama wale wa Saranga, Baruti na kwingineko kwenye matatizo ya maji huku mabomba makubwa ya maji yakipita jimboni na uwepo wa Chuo cha Maji, na Wizara ya Maji ndani ya jimbo letu. Iwe ni wale Bonyokwa, Mpiji Magoe na kote kwenye udhaifu wa mipango miji na matatizo ya usafiri huku Chuo cha Usafishaji cha Taifa kikiwa ndani ya jimbo hili hili.

Iwe ni wafanyakazi wa Kiwanda cha Urafiki hapa Ubungo ama wa sekta umma na wa binafsi waoishi ndani ya jimbo hili wenye kubebeshwa mzigo mkubwa wa kodi na kuzongwa na maslahi duni. Iwe ni wafanyabiashara ndogo ndogo wanawake kwa vijana pale Manzese, Makurumla na kwingineko; iwe ni wanafunzi wa sekondari na vyuo Mbezi na Ubungo ambao kwa ujumla wake wanaishi katika mazingira yenye mifumo dhaifu yenye kudorora kwa ubora na upatikanaji nafuu wa huduma za kijamii.

Iwe ni mwananchi wa Jimbo la Ubungo anayeathirika kwa bei na mgawo wa umeme huku akipita na kuona mitambo ya kampuni feki ya Dowans inayotakiwa kurejesha mabilioni iliyolipwa mara mbili (double payment) na serikali; mitambo ambayo imeendelea kukaa pembeni na makao makuu ya TANESCO yaliyopo jimbo la Ubungo bila kutaifishwa. Iwe ni mtanzania wa kawaida anayeelemewa na mzigo wa kodi na kupanda kwa gharama za maisha. Wote wanahitaji mbunge wa kuwasikiliza, kuwawakilisha, kushiriki kutunga sheria bora na kuziwajibisha mamlaka zinazohusika. Tanzania bila mafisadi inawezekana. Huu si wakati wa kuahidi nitafanya nini kwa kuwa si kipindi cha kampeni. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.


Tunahitaji mabadiliko ya kweli kuliko ahadi kedekede utekelezaji legelege

Natambua kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (pamoja na ubovu wake) imetaja katika ibara ya 9 Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha: kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa; kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa; kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumyonya mtu mwingine; kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja; kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini; kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi. Misingi hii na mingine, haitekelezwi wala kuzingatiwa kikamilifu kutokana na ombwe la uongozi, udhaifu wa kitaasisi na upungufu wa uwajibikaji. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Aidha naelewa kuwa katiba hiyo hiyo (pamoja na mapungufu yake) inatamka katika Ibara ya 63 kifungu cha pili na cha tatu kuwa Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kupitia maswali, mijadala, kuidhinisha mipango (zikiwemo bajeti), kutunga sheria na kuridhia mikataba.

Madaraka hayo ya bunge na majukumu ya wabunge hata baada ya uongozi wa awamu ya nne kuahidi kuyatekeleza kwa ari, nguvu na kasi mpya na Spika wa Bunge kuahidi kuyasimamia kwa kasi na viwango; hali kwa sehemu kubwa iko vile vile; ahadi kedekede, utekelezaji lege lege.

Hasara kwa taifa iliyotajwa kwenye orodha ya mafisadi (list of shame) na ile inayotokana na ufisadi kwenye serikali za mitaa pekee kwa ujumla wake inafikia takribani trilioni mbili. Hivyo Tanzania ni nchi tajiri wa rasilimali huku wananchi walio wengi wakiishi katika lindi la umasikini na ugumu wa maisha.

Naamini hali hii inachangiwa na kufilisika kiitikadi na kidira kwa chama tawala, hodhi (monopoly) ya chama kimoja bungeni, bunge kukosa uhuru wa kikatiba na udhaifu wa taasisi za kusimamia uwajibikaji. Hali hii inachochewa pia na udhaifu wa kiuongozi ikiwemo uzembe wa sehemu kubwa ya wabunge wengi wao wakiwa wameingia kwa nguvu ya ufisadi katika uchaguzi wa mwaka 2005 na hivyo kukosa nguvu ya kimaadili na dhamira ya kuleta mabadiliko ya kweli. Hata wale wachache wenye dhamira ya kufanya mabadiliko wanadhibitiwa na kamati za chama chao (party caucus) chenye mmomonyoko wa kimaadili. Hivyo, harakati za ukombozi zinapaswa kuungwa mkono na watanzania wote wakiwemo wanachama wa chama hicho wanaokerwa na hali ya mambo. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.


Tuchukue hatua; kwa pamoja tunaweza

Jukumu lililo mbele yetu la kuwezesha mabadiliko ya kweli ni kubwa linalohitaji hatua za haraka kujitoa sadaka na kutumia talanta kuanzia sasa mpaka wakati wa uchaguzi Oktoba 2010; kabla ya majukumu makubwa zaidi kuanzia wakati huo na kuendelea. Kwa pamoja tunaweza, pamoja tutashinda.

Hatua ya kwanza ni kuhakikisha kila mmoja mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea ama atayefikisha umri huo wakati wa uchaguzi kama bado hajajiandikisha anajitokeza kujiandikisha katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura unaonza katika Mkoa wa Dar es salaam kuanzia kesho tarehe 22 mpaka 27 Machi, 2010 ikiwa ni awamu ya mwisho kabla ya uchaguzi mkuu. Aidha kwa waliohama makazi, huu ndio wasaa mwafaka pia wa kwenda kubadilisha taarifa zenu ili muweze kupiga kura katika maeneo mliyopo.

Hatua ya pili ni kushiriki kwa hali na mali katika kujenga oganizesheni ya chama mbadala. Kuhamasisha wagombea mbadala kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali, kuwaunga mkono na kueneza ujumbe wa matumaini wa mabadiliko kwa watanzania wengine katika maeneo yenu. Izingatiwe kuwa kipindi cha kuanzia mwezi Aprili mpaka Julai ni cha wagombea kuonyesha nia, kuchukua fomu ndani ya vyama, kampeni za ndani ya vyama, kuingia katika kura za maoni na uteuzi kufanywa na vyama vyao kwa kuwa serikali mpaka hivi sasa imekataa matakwa ya umma ya kutaka wagombea binafsi waruhusiwe.

Kampeni kwa umma zinatarajiwa kuanza baada ya wagombea kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi mwezi Agosti na zinatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2010. Hatua muhimu wakati huo ni pamoja na kushiriki katika kampeni kwa hali na mali, kupiga kura na kuunganisha nguvu ya umma katika kulinda kura. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Haturudi nyuma kamwe; matumaini yapo mbele

Mwaka 2005 Mwezi Machi kama huu nilipochukua fomu kwa mara ya kwanza kugombea ubunge, CHADEMA haikuwa na mtandao imara katika jimbo la Ubungo tofauti na sasa ambapo ina mtandao madhubuti na ipo fursa bado ya kuufanya kuwa mzuri zaidi. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Hivyo Disemba 2005 (pamoja na kukubalika kwa wananchi) baada ya mvutano wa siku kadhaa matokeo ya uchaguzi yalitangazwa kwa shuruti bila kupitia utaratibu wa kupitia na kujumlisha kituo hadi kituo na kufanya jumla ya wapiga kura waliotangazwa kupiga kura katika ubunge kuzidi wale waliopiga kura za urais kwa zaidi ya kura elfu thelathini (30,000) katika uchaguzi uliofanyika katika siku moja.

Kutokana na hujuma hizo na nyinginezo zilizohusisha pia ufisadi katika uchaguzi niliamua kufungua kesi namba moja ya mwaka 2006 katika Mahakama Kuu kupinga matokeo hayo. Kesi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikipigwa danadana za kiufundi bila kuingia katika kusikiliza msingi wenyewe wa kesi.

Wakati najiandaa kutangaza rasmi dhamira ya kugombea nikitazama mbele kwa matumaini, nimepokea simu toka kwa Wakili wangu katika kesi hiyo Ndugu Tundu Lissu akinieleza kwamba hatimaye Mahakama Kuu imepanga kuwa kesho tarehe 22 Machi 2010 ndio siku ambayo mahakama itatoa hukumu juu ya kesi hiyo.

Bila kuingilia uhuru wa mahakama, nieleze wazi tu kwamba kwa mtiririko wa mambo mpaka sasa hukumu hiyo itahusu zaidi ombi langu la kuondolewa kuweka dhamana ya milioni tano kama sharti la kufungua kesi na kupita kwa muda toka kesi ifunguliwe badala ya utata wa matokeo na kasoro za uchaguzi husika.

Hata hivyo kwa miaka takribani mitano ambayo nimekuwepo katika siasa na kushiriki katika chaguzi mbalimbali za kiserikali, mmoja nikiwa kama mgombea na zingine nikiwa kwenye timu za kampeni nimejifunza kuwa pamoja na uwepo wa katiba na sheria mbovu zenye kusababisha tume ya uchaguzi kutokuwa huru na kukosekana kwa uwanja sawa wa kisiasa kwa ujumla; bado vyama mbadala vinaweza kuunganisha nguvu ya umma kupata kura nyingi na kushinikiza mshindi kutangazwa pale ambapo kunakuwa na mikakati thabiti, oganizesheni makini na uongozi mahiri. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Naweza nikalazimika kutangaza upande wa kugombea

Tunahitaji mabadiliko ya uongozi na mfumo wa utawala ili kutumia vizuri kodi za wananchi na rasilimali za taifa kuwa na miundo mbinu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kuwezesha ustawi wa wananchi.

Badala ya kuelekeza nguvu zaidi katika azma hii, serikali ya sasa inaongeza nguvu katika matumizi ya anasa na mzigo mkubwa wa gharama za utawala na sasa inajadili kuongeza zaidi idadi ya wabunge.

Mathalani mwaka wa fedha 2009/2010 kiasi cha bajeti kilichotengwa kwa ajili ya Bunge ni shilingi bilioni 62 ambayo ni sawa na wastani wa zaidi ya milioni 190 kwa kila mbunge kwa mwaka. (Pato la mtumishi wa umma wa kima cha chini halifiki hata asilimia 1% ya fedha hizo).

Ndio maana binafsi siungi mkono ongezeko la majimbo lisiloangalia tija na ufanisi wa wabunge katika kutimiza majukumu ya msingi ya kibunge. Kwa mtizamo wangu, tunapaswa kupunguza idadi ya majimbo ya uchaguzi badala ya kuyaongeza kwa kufanya wilaya za sasa za kiutawala ndio ziwe kitovu cha mgawanyo wa majimbo.

Mathalani, wilaya ya Kinondoni badala ya kuwa na majimbo matatu ya Kawe, Kinondoni na Ubungo iwe na jimbo ni jimbo moja tu la Kinondoni. Badala yake Halmashauri ya Kinondoni bila kushirikisha vyama vya siasa ilipeleka mapendekezo kwa Baraza la Mashauriano la Mkoa (RCC) wa Dar es saaalam ambalo nalo limepeleka mapendekezo ya kugawa majimbo kadhaa ya mkoa huu likiwemo jimbo la Ubungo.

Kwa mujibu wa mapendekezo yao Kata za Kimara, Makuburi, Mbezi na Kibamba zimependekezwa kuwa kwenye jimbo la Kibamba toka Jimbo la sasa la Ubungo. Kwa msingi huo wanapendekeza sasa jimbo la Ubungo libaki na kata za Mabibo, Manzese, Makurumla, Ubungo, Sinza na Mburahati na kuongezewa pia kata ya Kigogo (ambayo kwa sasa iko ndani ya Jimbo la Kinondoni).

Kwa hiyo, pamoja na kutangaza dhamira yangu ya kugombea ubunge katika eneo ambalo ni Jimbo la Ubungo; haiwezekani kwa sasa kutangaza kwa hakika nitagombea katika jimbo gani mpaka pale Tume ya Uchaguzi itakapotangaza maamuzi yake kuhusu mgawanyo wa majimbo baada ya kupokea mapendekezo hayo toka kwa serikali. Iwapo Tume ya uchaguzi italigawa jimbo la Ubungo nitalazika kutangaza upande ambao nitagombea. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.


Hitimisho:

Maneno na matendo yangu katika harakati za umma katika kipindi cha mwaka 2000 mpaka 2005 wakati nikiwa kwenye uongozi wa kijamii katika asasi za kiraia na katika kipindi cha mwaka 2005 mpaka 2010 nikiwa kiongozi wa kisiasa yanaweza kurejewa kama msingi wa kuashiria ni watu gani nitawawakilisha na masuala gani nitayasimamia katika uongozi wa umma kabla hata sijateuliwa rasmi na kutoa hotuba katika kampeni. Naomba uwasiliane nami kwa kunitumia ujumbe kupitia johnmnyika@gmail.com au 0784222222 tuwe pamoja hatua kwa hatua katika safari ya ushindi. Ni wakati wa Mabadiliko; tuwajibike mpaka kieleweke.

Wenu katika demokrasia na maendeleo;


John Mnyika
Jimboni Ubungo-21/03/2010
 
Safi mkubwa nakutakia mafanikio ila uwe na dhamira kweli ya kumkomboa mwananchi.
 
In a "lost" country like Tanzania,People like you are few and far in between,although it is nice to get a glance once in a while.

Hilo la hiyo mibunge kutumia 190M kw amwaka ni ushahidi wa jinsi gani hawawezi kutatua matatizo ya Wananchi wa kawaida,kwani wao sio sehemu ya matatizo hayo.

Nikiamini kuwa utakuwa mbunge 2010,umejipanga vipi kupunguza cost per MP atleast iwe nusu ya hizo 190M?

I wish angekuja Mh,Raisi atakayepa BUNGE lisitumie zaidi ya 20M per head per year.

Kila la heri.
 
Kila la heri mkuu na imani mwaka huu utashinda kwani yule aliyekuibia kura 2005 kasema hagombei tena
 
Nakutakia kila la kheri katika safari unayoianza tena kwa mara ya pili. Ni matumaini yetu wapenda mabadiliko na maendeleo kuwa safari hii utaweza kuvuka vigingi ulivyokutana navyo kipindi kilichopita na hatimaye kuliona bunge lenye damu mpya na mwendo wa kasi kuielekeza Tanzania kule wengi tunakokutamani.
 
Mnyika,kwanini usingejaribu mikoani?Maana Dar pagumu pale.
Ni ushauri tu mkuu
 
Hongera sana bali kazi ni kubwa maana hapo Dar mtoni mafisi wengi, utakumbana na sharuba za kila aina lakini inshalah huu ni mwaka wa vitendo kwa wanaoweza.
 
- Mkuu Mnyika, heshima sana ndugu yangu naona tutakutana huko maana mimi ninam-support mgombea wangu tayari hapo ubungo, lakini cha muhimu ni mmoja wenu apite na kuingia bungeni, binafsi nitakuwepo huko Ubungo very soon na nitakutafuta.

- I am looking forward kupambana na your challenge, ninaamini wananchi wa Ubungo watafaidika sana midahalo ya kampeni, soon nitakua right there mkuu looking forward to meet you!

Kila la heri mkuu na Mungu Aibariki Tanzania.

Respect.


FMEs!
 
Kila la heri ila angalia uwezekano wa kubadilisha rangi ya blog yako, rangi ya pink kwa dume la nguvu ina mushkil.

Tunataka kuona vijana wana nafasi muhimu sasa, propoganda za vijana ni taifa la kesho zimepitwa na wakati.

Good luck!!
 
WanaJF, nawaletea taarifa ambayo niliitoa jana kupitia http://mnyika.blogspot.com na katika Kongamano la Vijana la Demokrasia na Maendeleo Jimbo la Ubungo. Nawatakia mjadala mwema.

Kwa hiyo, pamoja na kutangaza dhamira yangu ya kugombea ubunge katika eneo ambalo ni Jimbo la Ubungo; haiwezekani kwa sasa kutangaza kwa hakika nitagombea katika jimbo gani mpaka pale Tume ya Uchaguzi itakapotangaza maamuzi yake kuhusu mgawanyo wa majimbo baada ya kupokea mapendekezo hayo toka kwa serikali. Iwapo Tume ya uchaguzi italigawa jimbo la Ubungo nitalazika kutangaza upande ambao nitagombea. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.


Pasi shaka kwa kuzingatia taratibu, CHADEMA imeridhia na kukupitisha kugombea katika jimbo lolote lile?...ikiwa hivyo, pana shaka, sie wananchi twategemea maendeleo ya vitendo na sio porojo za kisiasa kama ilivyo sasa kwa waheshimiwa wengi si tu wa chama tawala bali pia wa upinzani!.Mkianza kuomba "kula", propaganda nyingi za kuleta maendeleo kwa vitendo, lakini tukiwapa "kula", yote huwa ni nadharia tu!,.
 
- Mkuu Mnyika, heshima sana ndugu yangu naona tutakutana huko maana mimi ninam-support mgombea wangu tayari hapo ubungo, lakini cha muhimu ni mmoja wenu apite na kuingia bungeni, binafsi nitakuwepo huko Ubungo very soon na nitakutafuta.

- I am looking forward kupambana na your challenge, ninaamini wananchi wa Ubungo watafaidika sana midahalo ya kampeni, soon nitakua right there mkuu looking forward to meet you!

Kila la heri mkuu na Mungu Aibariki Tanzania.

Respect.

FMEs!

Du nilidhani unakwenda kugombea wewe kumbe unakwenda kumsupport mtu mwingine halafu unatuambia ili iweje?
 
John,

Ungeanza sasa kuhimiza wafuasi wako kujiandikisha kupiga kura.Nina wasiwasi na mashaka ya watu kujaa kwenye mikutano ya hadhara halafu hwakupigii kura.Moja ya setbacks za ucahguzi mkuu mwaka huu ni low voter turnout. Ni mkakakati wa serikali ili CCM ipate % win kubwa si unajua hata wakijiandikisha watu 10 na 9 wakapigia CCM ushindi ni 90%? ...

I support and salute you though.....
 
Asante sana JJ kwa uamuzi wako wa kusimama tena Ubungo. Naamini umejiandaa kwa mengi katika safari yako hii ya ukombozi wa jimbo la Ubungo, character asassinations za kila aina zitatumika kuhakikisha hausimami. Nakuhakikishia jimbo la Ubungo ni lako.. unless otherwise!.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom