Ubunge Wa CCM Mbeya Mjini Fomu Itakuwa Moja Tuu ya DK Tulia.

ChoiceVariable

JF-Expert Member
May 23, 2017
45,536
52,612
Hii ndio habari inayobamba huko biunga vya CCM Mbeya ,kwamba Spika wa Bunge na Rais wa Mabunge Duniani atakuwa mgombea pekee wa Jimbo la Mbeya Mjini Kwa time to ya CCM.
---
Kauli ya baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kuwa wamejipanga kumkingia kifua mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson katika Uchaguzi Mkuu 2025 kwa kuhakikisha inatolewa fomu moja ya kuwania nafasi hiyo uchaguzi utakapowadia, imezua gumzo.

Viongozi tofauti katika mkoa huo wametoa kauli hizo kuwa kutakuwa na fomu moja ya mgombea ubunge ya Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa za ndani ya mkoa huo zinaeleza kuna upinzani mkali ndani ya chama katika jimbo hilo, baadhi ya makada wanadai ameanza kampeni mapema, jambo linalowasukuma viongozi wa chama hicho kumkingia kifua Spika Tulia na kumhakikishia njia nyeupe kwenye uchaguzi ujao.

“Tatizo la mbunge wetu ameanza kampeni mapema, yote anayoyafanya ni maandalizi ya uchaguzi na sasa viongozi wa chama mkoa wanamuunga mkono, kila mara wanazungumzia uchaguzi,” amesema kada mmoja wa chama hicho mkoani Mbeya kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Juzi, Aprili 9, 2024 kwenye iftar maalumu mjini Mbeya iliyoandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust ambayo mkurugenzi wake ni Dk Tulia, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amedai chama hicho kimemwekea kinga na ulinzi, ili kuhakikisha anapata kura za kishindo.

Pia, amesema watahakikisha wanashughulika na wasaliti ndani ya chama, huku akiwaonya watu wachache wanaojipanga kuwania nafasi hiyo kujipima misuli kwanza, huku akisisitiza chama kinatambua kuna fomu moja ya mgombea ubunge na urais.

Mjumbe huyo amebainisha chama kimejipanga kikamilifu kuhakikisha Dk Tulia anapata kura za kishindo na kushughulika na watu wachache watakaotunisha misuli na kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

“Dk Tulia tayari ana ulinzi ndani ya chama, viongozi wa dini, kimila, vijana, sasa nani ataingia hapo? Hapa hapaingiliki, atalindwa, hakuna atakayemgusa na tutahakikisha anaibuka na kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu 2025,” amesema Mwaselela.

Ametumia fursa hiyo kutuma salamu kwa vyama vya upinzani kuwa watafute biashara za kufanya, kwani Dk Tulia ataendelea kuongoza jimbo la Mbeya mjini.

“Umefika wakati wale wanaojipanga kuja kugombea jimbo la Mbeya Mjini, nafasi zimejaa, waende kufanya biashara na watakaotunisha misuli wajipime nyonga kabla ya kuruka msamba,” amesema.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Mwalunenge ameema mambo yanayofanywa na Dk Tulia ni ibada ya kimungu, huku akisisitiza chama kitamlinda kwa hali na mali kuhakikisha anapata kura za kishindo mwaka 2025.

Msimamo wa Dk Nchimbi
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kuzungumzia suala hilo amesema yeye kwa ngazi ya chama ni mkurugenzi wa uchaguzi Taifa, hivyo hawezi kulizungumzia, hivyo akaelekeza aulizwe Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya ambaye ndiyo mkurugenzi wa uchaguzi CCM mkoa wa Mbeya.

“Anapaswa kujibu swali hilo kwa kuwa yeye ni katibu wa CCM kwa ngazi hiyo, lakini ndiye mkurugenzi wa uchaguzi mkoa, mimi ni mkurugenzi wa uchaguzi Taifa, siwezi kuzunguzia yanayojitokeza mikoani, mzigo utakuwa mkubwa,” amesema Dk Nchimbi.

Alipoulizwa kuhusu kauli za viongozi wake, Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Lengael Akyoo amesema kwa kuwa chama hicho kinaongozwa kwa misingi ya katiba, mwakani anatarajia kukata mzizi wa fitina, kuwataka makada wa chama hicho kutokuwa na wasiwasi.

“Chama chetu ni kikongwe, kinaongozwa na misingi ya kanuni na taratibu zilizopo kwenye katiba yetu, jambo hili la uchaguzi mimi kama mkurugenzi wa uchaguzi, ni mapema kulizungumzia, lakini nitaliweka wazi mwakani muda ukifika,” amesema.

Akyoo amesema misimamo ya chama hicho inaeleweka kutokana na miongozo iliyowekwa kwa kuzingatia katiba yao, japo kumekuwa na maneno mengi yanasemwa katika mkoa huo.

‘Kinavuruga utaratibu wa chama’
Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema kinachoendelea ni kuvuruga utaratibu wa chama kwa sababu kauli hizo zitakwenda kuathiri moja kwa moja mchakato wa kura za maoni.

“Utaratibu upo na ikifika Julai mwakani chama kitakwenda kwenye kura za maoni na Dk Tulia ataingia kwenye uchaguzi wa ndani kama wagombea wengine wa nafasi hiyo na yeyote anaweza kushinda na akapita, sasa kiongozi huwezi kunyanyuka leo kusema unakwenda na Tulia,” amesema.

Amesema viongozi kutoa kauli za namna hiyo wanawakatisha tamaa wanachama wengine waliokuwa na malengo ya kutia nia, ili kufurahia na kutumia uhuru wao wa kuwa wanachama wa chama hicho kwa kugombea nafasi hiyo.

“Jambo hilo unaweza kulielewa kwa ngazi ya Rais, ingawaje nalo halipaswi kuwa hivyo kwa sababu si utaratibu, lakini kwa wabunge lazima waingie kwenye kura za maoni. Kwa viongozi kusema maneno kama haya ni kukiuka mfumo wa chama. Natamani chama kingetoa tamko kukemea wanaofanya hivyo,” amesema.

Dk Mbunda amesema athari za kuacha tabia hiyo ijengeke inatoa fursa kwa makada wengine wa chama hicho waliotaka kuweka nia kuona hakuna fursa tena kwa kuwa wamejipanga, hivyo wanaweza kuchukua uamuzi wa kwenda kuunga mkono upinzani.

“Wanaondoka mapema kwenda kuunga mkono upinzani na kwa Mbeya uchaguzi utakuwa mgumu na inafahamika wazi Joseph Mbilinyi (Sugu) yuko pale na anasema anautaka ubunge, anataka kurudisha heshima ya Mbeya,” amesema.

Amesema watu wakianza kuondoka wakati huu kwenda kuunga mkono upinzani, uchaguzi utakuwa mgumu zaidi, hivyo ni muhimu kwa viongozi kuheshimu na kuzingatia utaratibu uliopo kwa maslahi ya chama chao.

My Take
Hongera sana CCM Kwa huu utaratibu Mpya
 
Back
Top Bottom