MAJIBU YA LOWASA KWA NAPE KUPiTIA HUSSEIN BASHE:
Akizungumza kwa niaba ya Lowassa, Bashe alisema kinachotokea nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na Rais Kikwete wakati wa sherehe za CCM mjini Songea, mkoani Ruvuma alipowaruhusu watu wakashawishi wanaoona wanafaa kuwania urais.
"Rais hakusema kushawishi namna gani, hakusema kushawishi kwa barua wala kwa sms (ujumbe mfupi wa simu ya mkononi), bali alisema wawashawishi. Na huwezi kumshawishi mtu ndotoni, utamshawishi kwa kumfuata na kumwambia," alisema Bashe.
Aliongeza: "Ndiyo maana Nape yuko mikoani anashawishi Watanzania juu ya kukiamini Chama Cha Mapinduzi. Hajakaa chumbani kwake, amewafuata. Kuna watu wanamshawishi Mwandosya, kuna wanaomshawishi Muhongo na vyombo vya habari vinaripoti."
"Umefika wakati Nape atangaze mgombea wake wa urais hadharani, ambaye mimi Bashe namjua, badala ya kuwatisha wana-CCM wengine kwa kutumia kofia ya Ukatibu Mwenezi wa chama."
"Kwa hiyo, mimi kama Bashe, ambaye ni mwana-CCM nataka tu nimhakikishie Nape na wenzake kuwa hawana hatimiliki ya CCM. Wote wanaCCM tuna kadi moja ya rangi moja na tunalipia ada sawasawa. Hakuna mwanachama wa daraja la kwanza wala wa daraja la pili."
Bashe ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, alisema kauli ya Nape ya kumtaka Lowassa kwenda nje ya CCM, haiwezekani, kwani hajawahi kufanya hivyo kama alivyowahi kufanya yeye (Nape).
Hivyo, akasema wana-CCM wanaomshawishi Lowassa na Watanzania wanatekeleza ushauri uliotolewa na Mwenekiti wa chama hicho, Rais KIkwete.
"Imefika wakati sasa Nape atazamwe kauli anazoongea. Na sisi tunaomfahamu Nape hii kawaida ya kuropoka, siyo maa yake ya kwanza. Aliwahi kusema Kikwete akishinda mwaka 2005 atahama nchi, lakini hajahama , akapewa na U-DC (ukuu wa wilaya) na Kikwete na hivi sasa ni katibu mwenezi wa CCM," alisema Bashe.
Aliongeza: "(Nape pia) aliwahi kusema mkataba wa jengo la Umoja wa Vijana (UVCCM) ni wa kifisadi na yeye (Nape) leo anaishi kwenye jengo hilo hilo na linakipa chama mapato."
Alisema mtu pekee, ambaye anaweza kutengua kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa Songea mwezi uliopita, ni yeye mwenyewe (Rais Kikwete) kwa sababu ndiye aliyetoa maelekeo na sasa Watanzania wanayatekeleza.
Aliongeza: "Na mkumbuke mwaka 2011 kuelekea 2012, ni huyu huyu ndiye aliyekuwa anapita kwenye vyombo vya habari akiwaambia wanahabari kwamba, wanakwenda kumfukuza Lowassa Dodoma na leo anamhukumu kuwa anakosa sifa na kumwambia aende nje ya CCM.
"Nataka nimhakikishie kuwa Lowassa hawezi kuondoka CCM kwa sababu hajakutana na CCM barabarani.
Alisema wanaCCM wataendelea kuheshimu ushauri wa mwenyekiti wao na kwamba, Lowassa amekuwa akiheshimu kanuni na taratibu za chama.
"Na Nape na genge lake wakumbuke kwamba, Lowassa amevumilia mengi sana. Na asidhani yeye na wenzake wana hatimiliki ya chama hiki.
Aliongeza: "Hawa wanaosema haya leo, aliyasema mwaka 2009, 2010 na 2011 kwamba Lowassa hachaguliki, hakubaliki. Nyimbo yao ilipokosa soko, wakaja na nyimbo mpya ni fisadi, nayo ikakosa soko. Wakaja na nyimbo mpya ni mgonjwa, nayo ikakosa soko. walimtabiria hadi kifo, nayo ikakosa soko.
"Baada ya kuona kwamba, anaungwa mkono na makundi mengi ya kijamii mgombea wao wa kwenye brifkesi anakosa uhalali katika umma, sasa wanaanza kutoa kauli za vitisho na kusema watu wamenunuliwa.
Kuwadhalilisha Watanzania tuna bei. Kwamba, unanunulika. Na hiyo ni kudhalilisha utu wa Kitanzania na uwezo wa Watanzania wa kutafakari.
Alisema hakuna mtu anayenunuliwa na Lowassa, bali watu wote wanaongozwa na akili zao katika kutafakari na kuamua na kwamba, msingi wote wa chama chochote cha siasa, ni imani, demokrsia na haki.
"Nimtahadharishe Nape sehemu yoyote, ambayo haki na demokrasia kulazimishwa kufinywafinywa huathirika," alisema Bashe.
"Kwa hiyo, kama wanafikri njia zinazotumiwa na Watanzania kushawishi siyo sahihi, basi atoe maelekezo ya namna ya kushawishi. Hatutavumilia kuona haki haitendeki."
Karibu wiki mbili sasa, nyumbani kwa Lowassa, mjini Dodoma, makundi mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakipishana na kupigana vikumbo yakimshawishi agombee urais baadaye mwaka huu.
Awali, walianza wajumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM Wilaya ya Arumeru, kisha marafiki wa Lowassa, Kanda ya Kaskazini na Uongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma).
Baadaye, walikwenda nyumbani kwake masheikh 50 kutoka wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Masheikh hao walifuatiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu sita mkoani Dodoma, wenyeviti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, wamachinga na waendesha bodaboda zaidi 350 kabla wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu mbalimbali nchini kufuata nyayo hizo juzi.
CHANZO: NIPASHE