View: https://youtu.be/KuUO1ItbOUU
Habari zenu Wana-JF.
Mara nyingi kukiwa na mjadala wa kiuchumi Afrika Mashariki, ubishi unakuwa kati ya Tanzania na Kenya. Lakini vipi tukiziweka nchi tano za Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi) kwenye mizani moja kwa kutumia takwimu za hivi punde za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na ofisi za takwimu za taifa (za Oktoba/Septemba 2026)?
Kwenye uchambuzi mpya wa video unaolinganisha nchi hizi kwa vigezo vitano, matokeo yameshangaza wengi.
Kanuni za Mchujo: Kila kigezo, nchi inayoongoza inapewa pointi 5 na ya mwisho pointi 1. Pointi za juu kabisa ni 25.
Hivi ndivyo walivyopambana kwenye vigezo 5:
1. Ukubwa wa Uchumi (GDP)Kenya ni jitu la ukanda huu. Ina uchumi wa Dola bilioni 151. Tanzania inafuatia kwa mbali ikiwa na Dola bilioni 96, kisha Uganda ($72B), Rwanda ($19B) na Burundi inavuta mkia na chini ya $8B.
(Kenya inabeba pointi 5)
2. Pato la Wastani kwa Mtu (Income per Person) Uchumi mkubwa lazima ugawanywe kwa idadi ya watu. Kenya bado inaongoza hapa ($2,785). Cha kushangaza, Uganda inashika nafasi ya pili ($1,453) na kuitupa Tanzania nafasi ya tatu ($1,325). Hii inatokana na Uganda kuwa na uchumi wa $72B lakini wanaugawanya kwa watu milioni 50 tu kulinganisha na Tanzania inayogawanya $96B kwa watu karibu milioni 73.
(Kenya inabeba pointi 5 tena)
3. Kasi ya Ukuaji wa Uchumi (Economic Growth) Rwanda inawasha moto hapa; uchumi wao unakua kwa kasi ya 7.4%. Uganda inafuatia (6.2%), Tanzania ni ya tatu (6.0%), kisha Kenya (4.5%). Burundi ni ya mwisho (3.6%). Hata hivyo, ikumbukwe kuwa 7.4% ya Rwanda inazalisha kiasi kidogo sana cha pesa mpya kwenye uchumi wao ($1.4B) ukilinganisha na 4.5% ya Kenya inayoingiza $6.8B.
(Rwanda inabeba pointi 5)
4. Mfumuko wa Bei (Inflation) - Mshindi ni Mwenye Asilimia Ndogo Hapa ndipo Tanzania tunapotamba. Wakati wengine wakilia na ukali wa maisha, Tanzania ina mfumuko mdogo zaidi (4.2%). Uganda (5.8%), Kenya (7.3%), na Burundi (7.4%). Rwanda hali ni tete, mfumuko wao uko juu kwa asilimia 17.2, ikisukumwa na kupanda sana kwa bei za chakula.
(Tanzania inabeba pointi 5)
5. Mzigo wa Deni la Taifa (Debt to GDP Ratio) - Mshindi ni Mwenye Deni Dogo Ukubwa wa uchumi sio tija kama wote unaishia kulipa madeni. Burundi ina deni dogo zaidi kulinganisha na pato lake (40%). Tanzania tupo vizuri tukiwa na 48%, ikifuatiwa na Uganda (55%), Rwanda (63%) hili huku Kenya ikiwa na mzigo mzito zaidi wa asilimia 73! Sehemu kubwa ya mapato ya kodi ya Kenya inaishia kulipa riba ya madeni.
(Burundi inabeba pointi 5)
MATOKEO YA JUMLA (Pointi 25)
- Nafasi ya 5: Burundi (Pointi 10)
- Nafasi ya 4: Rwanda (Pointi 12) - Inakua kwa kasi sana lakini mfumuko wa bei unawatafuna.
- Nafasi ya 3: Kenya (Pointi 16) - Ndio uchumi mkubwa na watu wake wana pato kubwa, lakini deni lao kubwa na ukuaji wa kusuasua unawaangusha.
- Nafasi ya 2: Uganda (Pointi 18) - Hawajashika namba moja kwenye kigezo chochote, lakini wako vizuri kwenye kila nyanja (hawana uliokithiri).
- Nafasi ya 1: TANZANIA (Pointi 19) - Sisi ndio vinara! Tanzania inashinda sio kwa sababu ni bora sana kuliko wote kwenye kila kitu, bali kwa sababu ime-balance vizuri kwenye kila sekta. Ipo vizuri kwenye kudhibiti bei za vitu, ina deni linalohimilika, inakua vizuri, na ni uchumi mkubwa wa pili.
Unaweza kutazama uchambuzi mzima, takwimu na chati zote kupitia link hii:
View: https://youtu.be/KuUO1ItbOUU
Mjadala kwa Wadau: Pamoja na kwamba takwimu zinaonyesha Tanzania ni kinara kwa wastani (Balanced Economy), hizi namba za kwenye makaratasi haziwezi kupima umasikini, ubora wa huduma za afya, au upatikanaji wa ajira.
Kati ya hivyo vigezo 5 (Ukubwa wa Uchumi, Pato la Mtu, Kasi ya Ukuaji, Mfumuko wa Bei, na Deni la Taifa);
Kigezo gani unaona ndicho kinagusa maisha halisi ya Mtanzania wa kawaida?
Karibuni tujadili kwa hoja!