Watu weusi tuna akili ndogo? Privatus Karugendo Toleo la 004 21 Nov 2007 Padri Privatus Karugendo
pkarugendo@yahoo.com More information about text formats Text format JAMES Watson, mwanasayansi maarufu sana
duniani na mshindi wa nishani ya Nobel katika
tiba mwaka 1962, ameleta mjadala mkubwa
baada ya kudai kwamba mtu mweusi ana akili
ndogo kuliko mtu mweupe. Kauli yake hiyo
imeshikiwa bango na wapinzani wa ubaguzi wa rangi kwa kuwa inamdhalilisha mtu mweusi. Huyu si mtu wa kwanza kusema hivyo, tofauti ni
kwamba yeye ameisemea kisayansi zaidi. Siku za
nyuma waziri mkuu mmoja wa Japan alipata
kusema maneno kama hayo kwamba anatilia
shaka uwezo wa mtu mweusi. Waziri mwingine
wa Japan na yeye alishanukuliwa kusema hivyo hivyo. Wote baadaye waliomba radhi lakini
ujumbe ulifika. Chika Onyeani katika kitabu chake cha Capitalist
Nigger naye anashangaa ni kwa nini Mwafrika
atukanwe namna hiyo na mawaziri wa Japan
lakini bado waendelee kununua bidhaa toka
Japan. Anaelezea pia kwamba jamii yote ya watu
weusi inafanana kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano ukikutana na Mmarekani mweusi
aliyezaliwa na kukulia Marekani au Carribean au
Afrika kwenyewe, bado wana tabia zile zile
ambazo zinatia shaka kama kweli akili za
Waafrika si ndogo kwa kiasi fulani. Ukianza kuangalia matokeo mbalimbali
yanayotokea Afrika, kuanzia enzi za miaka ya
nyuma, unaanza kuwa na wasiwasi kuhusu hali
na uelewa wa mtu mweusi. Historia inatuambia
kwamba, hadi karne ya 16 kiwango cha
maendeleo kati ya Ulaya na Afrika kilikuwa sawa. Tunaambiwa pia kwamba miaka ya 1960 baadhi
ya nchi za Kiafrika zilikuwa mbele kimaendeleo
au katika usawa mmoja na nchi za Asia ambazo
leo ziko mbali kimaendeleo. Bado unajiuliza ni
wapi kwenye matatizo? Kwa nini Waafrika
waachwe nyuma kila leo? Inavyoelekea ni kwamba bara la Afrika linakuwa
kama kigezo kizuri cha kupima maendeleo na
mabara mengine. Ripoti za umasikini duniani
zinaonyesha kwamba umasikini duniani
umepungua kwa kiasi kikubwa lakini kwa Afrika
unaonyesha kuongezeka. Mbaya zaidi hakuna ishara ya watu hao kutoka katika utando huo wa
umasikini walikonasa kabisa. Idadi ya watu waliopungua umasikini kidunia
unatokana na kukua kwa uchumi wa China na
India, nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watu
duniani. Kwa hivyo, uwezo wao wa kupunguzia
watu wao umasikini unachangia takwimu za
kidunia zionekane nzuri lakini kwa Afrika hakuna mabadiliko mazuri. Ukipima baadhi ya kauli za hawa tunaowaita
wabaguzi utagundua kuna ujumbe
wanawasilisha. Kama tukichukulia Tanzania
kama mwakilishi wa Waafrika, tunaweza
tukajadili baadhi ya hoja na kujipima ni kweli
tuna akili ndogo kijenetiki au mazingira yetu yanatufanya tuwe na uwezo mdogo wa kutumia
akili zetu au tujiulize ni wapi tumeteleza? Tanzania hii ina rasilimali nyingi sana lakini
bado hatujaweza kufika popote pa maana.
Tunasaini mikataba ya hovyo kabisa ambayo
inampa mgeni mamlaka ya kuchukua rasilimali
jinsi anavyotaka huku wenyeji tukibaki hoi
kabisa. Tuna mapori ya kutosha na mito na maziwa ya kutosha lakini bado tunaagiza
chakula nje ya nchi. Tuna watu wanajilundikia mabilioni ya fedha
benki huku watu wa kijijini kwake hawana maji
ya kunywa. Kuna watu wananunua samani za
mabilioni ya Shilingi kwenye nyumba
walizojengewa na Serikali wakati ambapo Shule
ya Sekondari ya Azania, iliyopo katikati ya jiji kuu la nchi, ina wastani wa tundu moja la choo kwa
wanafunzi 300! Shule karibu zote mpya zilizojengwa, kuanzia za
msingi hadi za sekondari, zina uhaba mkubwa
wa vyoo. Hivi ni vitu vya msingi kabisa lakini
bado hatujaweza kuvitatua. Bado tunazipa likizo ya kodi kampuni kubwa
huku tukifuatilia vikodi vidogo vidogo vya
wafanyabiashara wadogo au hata wachuuzi.
Kampuni kubwa zinaruhusiwa kubeba hasara na
kuipeleka kwenye mahesabu ya mwaka ujao
kwa miaka kadhaa lakini hiyo hiyo kampuni inayopata hasara inaendelea kufanya biashara! Sasa hivi tunasifiwa kwa kuweza kufuatilia kodi
kwenye biashara ndogo ndogo huku tukiwa
hatujafanya lolote la maana kwenye kodi za
makampuni makubwa. Uwezo wa Serikali wa
ukusanyaji hupimwa na kuongezeka kwa kodi za
makampuni makubwa (Corporate Tax) na si kuongezeka kwa kodi za mapato zinazotokana
na kuajiri watu wachache. Ni lazima tukae chini tujiulize: Kunani katika akili
zetu? Tunavuna madini ya Tanzanite lakini
hatuwezi kuyauza. Tunasema tuna mafuta lakini
tukitaka kuyachimba tunamwita Mzungu,
japokuwa tumekuwa tukizalisha wahandisi na
wanajiolojia kila mwaka. Lazima tujiulize kama elimu yetu ina mushkeli au la! Sasa hivi tunajigamba kuwa na vyuo vikuu
karibia 30 lakini bado tunaagiza vijiti vya
kuchokonolea meno kutoka Malaysia. Ni lazima
tujiulize tulipoteleza. Ni lazima wakati mwingine
tujiulize kama kweli hatuna mushkeli kwenye
akili zetu. Maamuzi yenye maslahi ya taifa yanachukua
muda mrefu kuchukuliwa. Wananchi wamekuwa
wakipigia kelele suala la Richmond lakini
imechukua miezi kadhaa kuchukua uamuzi wa
kulichunguza. Kampuni iliyoshindwa kazi. Katika hali ya kawaida, ilibidi maamuzi ya haraka
yachukuliwe na taarifa ipatikane ili wananchi
waondoe hisia mbovu. Wapi? Imechukua miezi
ndio maamuzi yanatoka. Ni dhahiri mazingira
haya yataifanya hata taarifa yake itiliwe shaka. Maamuzi yenye maslahi ya taifa yanatakiwa
yachukuliwe mapema ili kusafisha hisia mbovu.
Wenzetu wanaosemwa kuwa na akili kuzidi sisi
leo wameweza kushughulikia mambo yenye
maslahi ya taifa na kuondoa umimi kwanza. Ni
lazima tujitathimini na kujiuliza kama kweli tuko sawa na wengine. Kwenye makala yangu ya juma lililopita, nilitoa
hoja kwamba tunajipima kwa viongozi wetu.
Katika hali ya kawaida kiongozi wa watu maskini
ni lazima aishi maisha yanayofanana na watu
wake; maisha ya kimaskini. Lakini kama kiongozi
wa watu maskini anaishi kwenye utajiri unaopindukia, ni lazima kuna kasoro. Magari zaidi ya 30 yenye thamani ya Shilingi
milioni 60 kila mmoja, kupita katika vijiji vya
watu maskini kwa kisingizio cha kukagua
maendeleo, ni jambo la kuleta mashaka kama
kweli hatujateleza mahali au kuzua wasiwasi juu
ya ubora wa akili zetu. Viongozi wetu wanapokwenda kuomba pesa
kule nchi za nje, wanafikia na kuishi kwenye
mahoteli ya kitalii. Kwa nini akili zetu zisitiliwe
shaka? Kiongozi wa watu maskini, anayekwenda
kuomba misaada ya watu maskini, anafikia
hoteli ya kitalii! Yamekuwepo malalamiko ya chini chini ambayo
kwa namna fulani ni matusi, kwamba wale
wanaotoa pesa wakija kuzifuatilia, wanasafiri
kwa usafiri wa kawaida. Kama ni ndege
wanapanda daraja la tatu, lakini viongozi wetu
wanasafiri daraja la kwanza! Ipo mifano mingi inayoonyesha dalili nyingi za
kuwafanya wenzetu wawe na mashaka juu ya
ubora wa akili zetu. Mheshimiwa Ndesamburo,
juzi, bungeni, alitoa ushuhuda kwamba asilimia
98 ya watu walio na simu za viganjani
wanazitumia kutongoza wanawake, kuzungumza umbea, kutuma ujumbe wa
mapenzi na kupanga mipango ya ujambazi.
Labda asilimia mbili ndio wanatumia simu kwa
mipango ya biashara na maendeleo. Hili ni jambo la kushangaza kwani Tanzania ni
kati ya nchi zinazosifika Afrika kwa kuingiza kwa
wingi simu za viganjani na makampuni ya simu
hizi yanapata faida kupindukia. Siku za karibuni Benki ya Dunia ilitoa taarifa ya
mamilioni ya dola zilizotolewa barani Afrika kwa
ajili ya kukuza kilimo lakini wanashangaa na
kujiuliza; mbona mapinduzi ya kilimo kwa bara
la Afrika hayajafanikiwa kama ilivyotokea Asia? Najua vyombo hivi navyo vina unafiki wa
kutosha kwa sababu wanatumia nchi masikini
kujineemesha pia. Lakini cha kujiuliza mbona
fedha za namna hiyo zimefanya mapinduzi
sehemu nyingine? Kwa nini zisifanye mapinduzi
Afrika? Kwa nini tukubali kutumiwa kama nguruwe wa majaribio na sisi tusifaidi kama nchi
nyingine? Tunapaswa kujitathmini hapa. Mara nyingi sana
wanaharakati wanaopingana na misaada ya nje
huwalaumu watoaji kwamba wanakuja na
misaada yao kuja kuitumia huku kwetu
wakijineemesha wenyewe. Mimi huwa nauliza
kama umeona msaada hautafaidisha taifa kwa nini uukubali? Kwa hivyo tunawalaumu pia wanaopokea
misaada isiyo na tija. Lakini wanaopokea
wanaangalia maslahi yao binafsi kwamba
watafaidi wao na si taifa. Wenzetu wa Asia
wanawarudishia wataalamu wa Benki ya Dunia
na IMF fedha zao kama wakigundua hazitakuwa na manufaa, na ndio maana kuna ushahidi wa
kitaaluma kwamba mikopo na misaada mingine
imeweza kusaidia sana kuleta mapinduzi Asia.
Sisi bado tunalia. Tujiulize tatizo lilipo. Tutalaani wabaguzi hawa, tutashika mabango
na kuandamana lakini kabla ya kwenda tujiulize
sababu ya kukwama kwetu. Tusikimbilie
kulaumu Wazungu kama chanzo cha matatizo
yetu. Kuna wale rafiki zangu wanaolaani ukoloni na
ukoloni mamboleo. Malaysia na Ghana zilikuwa
zote koloni la Uingereza na zilipata Uhuru
mwaka mmoja (1957). Wamalaysia walikuwa
wanakwenda Ghana kujifunza kilimo cha
mawese. Leo hii Ghana inajifunza kila kitu toka Malaysia kikiwemo kilimo cha mawese! Tanzania ni mika 46 ya Uhuru sasa. Tuache
kuendelea kulia na kulalamikia ukoloni. Sisemi
haukuleta madhara lakini tutalia mpaka lini?
Tunachukua hatua gani za kuondoa hayo
makovu? Au hatua zenyewe ni hizo za kuwaita
tena wakoloni waje kuwekeza kwa kuwasamehe kodi? Hawakatai kuja. Watakuja watatula halafu
watatutukana. Hawasemi hadharani lakini
wanasemea chinichini kwamba hawa Waafrika
ni wajinga. Wazungu wengi wanaobishana na
kauli ya Watson si kwamba wanasikitika sana.
Wanaonyesha usoni kwamba wamechukia lakini moyoni wanasema ni kweli hawa wana ujinga
wao mkubwa. Wanatutetea ili waendelee
kutuvuna. Hawataki tukae chini na kujitathmini
tulipoenda mrama. Nachukia sana kuitwa kiumbe dhaifu hasa
kiakili. Nachukia kwa sababu naupenda Uafrika
na weusi wangu. Nawapenda Waafrika
wenzangu. Nachukia sana wanapoambiwa
kwamba wana ubongo dhaifu. Lakini nahisi kuna
mahali kama watu weusi tumeteleza. Kuna ushaidi unaoonyesha kwamba tumefanya
mambo ambayo akili zetu zinatakiwa zihojiwe.
Kama mtu anaiba mabilioni ya fedha za umma
kwenye nchi masikini na kuyaweka Ulaya au
kuwekeza mahali popote, huku kukiwa na
wananchi wanaokufa kwa kukosa dawa ya Malaria, basi, tuna ulazima wa kujiuliza tuliko na
kasoro. Kama viongozi wanawaibia wanachi wao
waliowachagua kuwawakilisha bila aibu yoyote
inabidi tuhoji akili zetu. Kama wananchi nao
wanaridhika na hila za viongozi wao bila
kuchukua hatua madhubuti, basi tuhoji akili
zetu. Kama kijenetiki tuna akili ndogo, basi, hatuna
cha kufanya labda ufanyike utaratibu wa
kutuunganisha kijenetiki na hao wenye akili
zaidi. Kama akili ndogo zinatokana na kukataa
kutumia uwezo tuliopewa basi tunaweza
kujirekebisha. Hata kama Watson ataomba radhi kama wale
mawaziri wa Japan walivyofanya, atakuwa
ameshapeleka ujumbe mzito wa watu weusi
kujichunguza! Ujumbe huu ni mzito kwa taifa
letu la Tanzania.