Ulikua unakula wale wa kienyeji au wa kishua mkuu...
Maana huwenda tukawa tunakosa madini ya kiswazi tukijua wewe ni wa kishua from the root
Angel alikuwa si binti fukara, lakini si tajiri pia. Utajiri wa network haukukosekana kwao.Kati ya mabinti wenye bashasha ya kupumbaza akili na urembo wa kumfanya aonekane kama pambo tu, wakati kiuhalisia alikuwa na mengi zaidi ya urembo.
Familia yake ikijuana na yangu tangu wazazi wakifanya kazi pamoja Ikulu ya Nyerere, lakini kwa bahati mbaya mzazi wake mmoja alitangulia mbele ya haki.
Kwa namna moja familia zikifanana, kwa namna nyingine yalikuwa kama mapenzi ya Romeo na Juliet kati ya watu wa familia mbili tofauti kabisa.
Kwa hakika binti alikuwa mtulivu, mstahimilivu, mwenye bashasha na mapenzi ya kweli. Ingawa pia alikuwa na uchakaramu wake wa kufuatana na mabinti wa mjini wenye majina makubwa na vituko vingi, wapenda muziki na mitindo, waliokuwa na aibu za kiutamaduni lakini pia wakianza kuhoji uhalali wa ustaarabu huo.
Wapenda muziki. Muziki ulikuwa kiunganishi kikubwa. Tukikutana kuanzia kwenye mashindano ya "Yo Rap Bonanza" niliposhiriki, mpaka clubs kama La Dolce Vita home ground Coco Beach na mjini Billicanas.
Binti akapata mfariji, na Kiranga akapata somo komo. Mtu jitu akapata kwenda Kimicho kula asikirimu adimu za Gelato na watu waliotulia, wenye nchi, si wananchi tu. Huku akijua hapo ni sehemu yake lakini kiundani akifanya Hegelian dialectic za kifalsafa na kikomunisti kujinasua na wimbi la anasa za wale ma "petty bourgoisie" aliowaona hawana akili za kimapinduzi zaidi. Kama vile muhusika wa riwaya ya "The Spook Who Sat by The Door" akiwa katika mazingira anayotaka kujinasua.
Alikuwapo Nancy pia, lakini Nancy alishachukukiwa na rafiki Chacha. Isitoshe Nancy alikuwa na scandal kubwa ya mapenzi mjini. Na vile baba yake alivyokuwa mkubwa jeshini, nani anataka misukosuko na majenerali wa jeshi waliogeuka mbogo kwa sababu binti zao wamepagawishwa na machizani?
Akili za kimapinduzi?
Akili za kimapinduzi tena? Tumefikaje huku? Kwenye mapenzi kuna akili za kimapinduzi? Mapenzi si yamewateka mpaka ma rasta kina Bob Marley wakaimba "Satisfy My Soul" kama machekibobu wanaojivika u Cassanova?
Ndiyo, mapenzi ndiyo mapinduzi makubwa kabisa duniani, yaliyomfanya Walis Simpson, mwanamke mtalaka kutoka Baltimore Marekani, apelekee kuuvuruga ufalme mkubwa kabisa wa Uingereza na kumuondoa Mfalme Edward wa Nane wa Uingereza kutoka katika Ufalme wake na kuishia kuwa kama pauni wa chesi, Duke wa Windsor aliyeishi na kufia uhamishoni Ufaransa.
Alikuwapo Angel wa pili. Maana mmoja tu hakutosha. Kabla ya kuwapo Michelle wa Bronx na Michelle wa Brooklyn, alikuwapo Angel wa Oysterbay na Angel wa Kurasini. Mtoto wa RPC. Hawa watoto wa wanajeshi na watu wa usalama walikuwa na nini? Mtoto kachanganya damu ya Kitutsi, kapanda juu, akitembea kama mwanamitindo aliyepotea njia kutoka runways za Milan akafika Tanzania kutalii tu. Anajua hesabu pure kwa namna ambayo haikuyumkinika mtoto mzuri vile ajue hesabu vile. Humble like a child. Nikitembea naye mtaani mpaka madada wa mtaani wakiniita pembeni kuniulizia "Yule nani, umemtoa wapi?".
Lakini yote yamepita hayo. Kama mto unaoelekea baharini kwa kutiririka kwa namna ambayo maji hayawezi kurudi juu kwenye mkondo mlimani.
Sasa hivi nimetulia, raia mwema, alcohol free, makaratee yote chini, kaka mkubwa wa familia, baba muhifadhi wa amani.
Naelekea kumuunga mkono Shaaban Robert katika biografia yake ya "Maisha Yangu Baada ya Miaka Hamsini".
Ni wakati wa kuandika "Utenzi wa Hati na Adili" wangu.
Excerpts from "Kiranga : The Life"
Coming to a bookstore near you.