Ajali yaua watano, vibaka wapora maiti
na Francis Godwin, Iringa
WATU watano wamekufa papo hapo na mmoja kujeruhiwa vibaya katika ajali mbili tofauti zilizotokea wilayani Mufindi na Wilaya ya Iringa Vijijini jana, ikiwemo lori lililokuwa limebeba Mbolea, huku vibaka wakipora maiti kila kitu walichokuwa nacho.
Katika ajali ya kwanza iliyotokea juzi majira ya saa 2 usiku katika Kijiji cha Kinegembasi Wilaya ya Mufindi, kwenye barabara ya Iringa Mbeya, lori lenye namba za usajili T 144 BCU aina ya Scania lililokuwa limebebea mbolea tani 32, liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu watatu akiwamo mwanamke mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.
Wakizungumzia ajali hiyo, ndugu wa jirani Ibrahim Hamis, alisema lori hilo, lilikuwa limebeba mbolea aina ya UREA kutoka jijini Dar es Salaam kwenda nchini Malawi.
Alisema katika lori hilo, kulikuwa na watu wanne akiwemo dereva msaidizi wake na utingo pamoja na mwanamke mmoja ambaye ni abiria aliyekuwa amepewa msaada wa usafiri kutoka Mafinga.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Gulam Mahamudu shambe, Foward Shwambe na mwanamke mmoja ambaye jina lake halifahamiki, anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 20 na 22, huku utingo wa lori hilo akijeruhiwa vibaya.
Hata hivyo, alisema kuwa lori hilo lilikuwa limesheheni mbolea likitokea Dar es Salaam kwenda Malawi na kuwa mbolea yote iliyokuwemo katika gari hilo imeibwa na vibaka na kubaki mifuko isiyozidi kumi pekee. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo pamoja na ajali nyingine iliyosababisha vifo vya watu wawili iliyotokea katika kijiji cha Kivalali, kwa kuihusisha daladala yenye namba IT 2345. Katika ajali hiyo, iliyotokea jana majira ya asubuhi na kusababisha vifo vya watu wawili, akiwemo Swedy Samwel (40) na mtu mmoja mwanamume ambaye jina lake halijafahamika
chanzo:Tanzania daima