
Ng'ombe aliyetumbukia bwawani akiokolewa huko Motcombe, Dorset
NGOMBE mmoja aliyekuwa amepotea alijikuta akiogelea katika bwawa moja huko Dorset, Uingereza, baada ya kukimbia kutoka katika shamba moja.
Haikufahamika ni kwa nini ngombe huyo alikimbilia kwenye bwawa hilo, lakini watoa huduma wa sehemu hiyo walilazimika kufanya juhudi za kumwokoa ambazo zilichukua masaa kadhaa kumtoa majini.
Kioja hicho kilitokea asubuhi jana, wakati mnyama huyo aliyepewa jina la Daisy na waokoaji alipotoroka kutoka shambani huko Motcombe, na kuanza kuzurura katika eneo la nyumba ya jirani.
Daisy akiwa ameokolewa.
Kikosi cha zimamoto kutoka Shaftesbury, kundi la kuokoa wanyama kutoka Poole, daktari wa wanyama na gari maalum la kufanyia kazi hiyo, vilitumika katika operesheni hiyo.
Ofisa wa zimamoto Michael Stead, aliyefika kwenye eneo la tukio, alisema ngombe huyo aliyekuwa hajafikisha hata umri wa mwaka mmoja angeweza kukaa majini humo kwa masaa kadhaa bila kudhurika.
Kitu cha ajabu, alionekana kuwa mtulivu, alisema Stead, lakini alifanya matata kidogo tulipotaka kumfunga kamba ili kumtoa.
Hata hivyo, Daisy alibidi kudungwa madawa ya usingizi kabla ya kuondolewa majini na kurudishwa kwa tajiri wake.
Alionekana mchovu kama vile amelewa, bila shaka kwa kushangaa na kile kilichokuwa kimemtokea, alisema ofisa mmoja wa zimamoto na kuongeza: Nimeshiriki katika matukio kadhaa yanayohusu ngombe lakini hili limenishangaza. Hata hivyo, tunafurahi hakupata madhara yoyote.