Mkapa aponda wanaombeza
*Asema sera yake ya ubinafsishaji ilikuwa 'poa'
Na Charles Mwakipesile, Sumbawanga
RAIS mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Benjamin Mkapa, amewataka wanaoponda sera ya ubinafsishaji aliyoianzisha waache, na badala yake waende kuangalia shamba la kisasa la mifugo na kiwanda kinachomilikiwa na mzalendo, Dkt. Chrisant Mzindakaya.
Alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya kutembelea shamba la mifugo la Nkundi lililokuwa linamilikiwa na Serikali na kubinafsishwa kwa Dkt. Mzindakaya ambaye ni mbunge wa Kwela.
Rais mstaafu baada ya kulikagua shamba hilo na kujionea ng'ombe zaidi ya 3,000 wenye uzito wa zaidi ya kilo 500 kila mmoja, alisifu na kusema hilo ndilo lilikuwa lengo lake la ubinafsishaji kwa ajili ya kuwawezesha wazawa.
"Kwa mtindo huu kama kuna Mtanzania atakayediriki kuniponda kwa kuanzisha sera hii, mimi naona atafute jambo lingine, lakini si hili ambalo kwa sasa naweza kusema limefanikiwa kwa kiwango kikubwa na midomo ya watu sasa itafungwa," alisema.
Aliwataka wanahabari kutangaza mafanikio hayo ya wazawa waliofanikiwa katika uwekezaji, ili kuwafanya Watanzania waweze kufahamu kinachoendelea na mafanikio ya sera ya ubinafsishaji kwa maendeleo ya Taifa.
"Huu ni ndio uwezeshaji niliokuwa naupigania kwa nguvu zangu zote kwa maendeleo ya Taifa, sasa naweza kusema nimetua mzigo kwa amani na kwa hakika napumzika nikiwa na raha kubwa moyoni mwangu, kutokana na kuacha wazawa wakiwa wawekezaji wakubwa kama Mzindakaya," alisema.
Alisema wakati anatangaza sera ya ubinafsishaji mali za Serikali watu wengi hawakuelewa lengo lake na hivyo kuzua mijadala mingi, lakini kwa sasa wataelewa kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika shamba hilo ambalo awali lilikuwa limekufa .
Bw. Mkapa alisema ili kumaliza ubishi huo, waliokuwa wanaiponda sera hiyo kama wanataka kuhakikisha kuwa kuna kitu kimefanyika waende katika shamba hilo wajionee jinsi lilivyo na ng'ombe wa kisasa, ambao ilikuwa ndoto kwa Mtanzania kumiliki shamba kama hilo.
Baada ya kufika, alipewa taarifa fupi ya mradi huo na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni inayomiliki shamba hilo na kiwanda cha kisasa cha kusindika nyama ya Sumbawanga Agriculture and Animal Food Industries (SAAFI), Dkt. Mzindakaya alisema alichokifanya katika mradi huo ni kumdhihirishia Rais mstaafu kuwa hata Watanzania wanaweza.
"Nakumbuka mzee, ulianiambia nilipokuja Ikulu siku moja, kuwa uliumia moyo ulipokwenda Uganda na kupelekwa na Rais Yoweri Museveni kwa mzawa wa Uganda aliyefanya uwekezaji mkubwa, sasa na mimi leo niliona uje uone kuwa hata sisi Watanzania tunaweza na akija atakuta mambo ya ajabu," alisema Dkt. Mzindakaya.
Alisema wakati akiadhimisha miaka 40 ya kukaa bungeni, aliona aunganishe kwa kumwalika Rais mstaafu ili ajionee sera aliyoianzisha na kuiacha, wakati akiondoka madarakani ikilenga kuwawezesha wazawa kumiliki uchumi na kupunguza umasikini.
Bwana Mkapa anasema uwongo:
(1) Sera ya kubinafsisha siyo kwamba aliitunga yeye. Ilikuwa ni shinikizo la vyombo vya fedha duniani na ilianza wakati wa Mwinyi, na ni rais Mwinyi aliyemaarufisha neno "kubinafsisha". Kwa hiyo Mkapa anataka kujizolea sifa kama ndiye mtu aliyeleta sera ya kubinafsisha wakati tunajua kuwa Mkapa ameondoka bila kuwa na signature initiative yoyote pale nchini. Alichofanya yeye ni kutekeleza sera hiyo bila kutumia akili yoyote.
(2) Lengo la sera ya kubinafsisha ilikuwa ni kuifanya serikale ichane na shughuli za biashara. Lengo halikuwa kuwafanya Watanzania wawe matajiri kama anavyodai.
(3) Sera haikuwa na ubaya wowote, anacholaumiwa ni kwenye utekelezaji. Kama sera ingetekelezwa vizuri bila kutumia njia za rushwa ni kweli ingeweza kuleta faida kubwa kwa nchi na bila shaka sehemu kubwa ya mashirika ya umma ingekuwa inamilikiwa na watanzania wenyewe. Hebu aangalia nchi zilizowahi kuwa na mashirika ya umma halafu yakabinafsishwa. Mifano mizuri ni pamoja na Japan na China; hakuna shirika la umma lililobinafsihwa na kupewa watu wa nje. Badala yake China iliyaambia makampuni ya nje kuwa fungueni viwanda vyenu nchini halafu viwanda vyetu vitajifunza technologia na mbeinu kutoka kwenu. Japan nayo ilipoamua kuuza mashirika kama NEC, JR ni wajapani tu walioruhusiwa kuyanunua wakati huo, siyo watu wa nje.
(4) Mzindakaya ni mmoja kati ya wachache sana waliobahatika kununua mashirika ya umma na wote wale walikuwa connected na serikali. Mzindakaya alikuwa mkali sana wa kuibana sana serikali bungeni kwa hiyo hatushangai kuwa serikali ilifanya jambo fulani kumnyamazisha kusudi waendelee kuuza kinyemela mashirika ya umma. Ni dhahili kuwa baada ya kumwuzia shamba hilo, Mzindaka hakuwahi tena kuulizia chochote kuhusu uuzwaji holea wa mashirika ya umma.
Mimi naona kama Mzee Mkapa anasumbuliwa na sense of guilt kutokana na serikali ya rushwa aliyoeendekeza na ndiyo maana tangu alipokaribia kuondoka madarakani amekuwa katika kampeini ya kujitetea na kujiandikia historia yake apendavyo badala ya kuachia historia yenyewe ichukue mkondo wake. Mabomu la rada ya asilimia 29 rushwa na mikataba bomu kama ile ya ITPL na madini vyote ni matokeo ya utawala wake wa rushwa. Pamoja na upungufu wa Kikwete, kuna ukweli kabisa kuwa amerithi mzigo mkubwa sana kutoka kwa Mkapa kwa vile mikataba mingi ilyofanywa na Mkapa haiwezi kubadilishwa bila kuiweka serikali kwenye matatizo ya kisheria. Mkapa alipokuwa akiambiwa kuhusu rushwa serikalini mwake alikuwa akibweta kwamba leta ushahidi huku akijua kabisa kuwa hakuna raia atakayefanya hivyo; ngija sasa ushaidi utatoka uingereza kuhusiana na rada.