HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE. GRACE KIWELU KUHUSU OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA JUU YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2007/2008.
I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 43 (5),(b),(c) na 81(1) toleo la 2004 kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusiana na Bajeti ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa leo kujadili mambo muhimu kwa maslahi ya umma wa Watanzania, na kwa mema yote amabayo amekuwa akitujaalia. Ni matumaini yangu kwamba majadiliano yetu yataweka mbele maslahi ya Umma. Mungu atusaidie.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kwa nafasi ya kipekee kabisa kukishukuru chama changu cha CHADEMA kwa kuendelea kuniunga mkono katika kazi walizonikabidhi katika kipindi cha 2005-2010. Nawaahidi kuwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nitawatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa. Aidha, natoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Shoka Khamis Juma (MB), Msemaji Mkuu wa upinzani - Utawala Bora na Mheshimiwa Phares Kabuye (MB), Msemaji mkuu wa upinzani - Siasa na Mahusiano ya Jamii, kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha uandaaji wa hotuba hii, kwani na wao ni wasemaji wakuu katika wizara zinazojumuishwa katika hotuba hii. Vile vile, natoa pongezi za dhati kwa viongozi wetu wa Kambi ya Upinzani Mhe. Hamad Rashid Mohammed (MB) na naibu wake Mhe. Dr. Wilbrod Slaa (MB) kwa kutoa muongozo sahihi kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
4. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2006/2007 tumempoteza mwenzetu, Hayati Juma Jamaldin Akukweti na hivi majuzi tu Hayati Amina Chifupa. Hivyo kwa majonzi makubwa, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba kutoa salamu za pole kwa ndugu, rafiki, jamaa na familia za marehemu. Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amin.
5. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuungana na wenzangu kutoa pole kwa wale wote waliofikwa na misiba na ajali katika kipindi hiki chote tukiwa hapa Bungeni. Mungu awafariji katika wakati huu mgumu.
II. MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA
6. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inatambua kwa kina umuhimu wa Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma kama sehemu muhimu sana katika kuimarisha utawala bora katika uendeshaji wa shughuli za serikali, kuweka mfumo wa uendeshaji wa serikali unaoleta tija na ufanisi, kujenga uwezo wa watumishi wa umma, na kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma. Mheshimiwa Spika, kwa kuelewa hilo ni muhimu sana idara hii iangaliwe kwa umakini kwa sababu Watumishi wa Umma ni moja ya kiini cha maendeleo ya Taifa.
7. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inayaona mengi ambayo kimsingi yamekuwa yakidhoofisha swala zima la utendaji na uwajibikaji wa Watumishi wa Umma. Mambo haya yanatokana na kutokuwepo kwa umakini na ufuatiliaji thabiti ambao umepelekea kuporomoka kwa maadili na uwajibikaji wa Watumishi wa Umma, maisha duni, ubinafsi, na urasimu na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya taifa hili.
ONGEZEKO LA MISHAHARA KWA WATUMISHI WA UMMA.
8. Mheshimiwa Spika, maboresho ya maslahi ya Watumishi wa Umma ni jukumu muhimu sana la Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya nne haikubaki nyuma na ndio maana ikaahidi Maisha bora kwa kila Mtanzania. Tumaini la kila mtumishi lilikuwa ni nyongeza ya mshahara kulingana na kiwango cha kupanda kwa hali ya maisha kiujumla.
9. Mheshimiwa Spika, tofauti na matarajio ya wengi, hususan wale walipwao kima cha chini, hali imeendelea kuwa ngumu kutokana na kutopanda kwa mshahara kwa kiwango kinachoridhisha. Bajeti kuu ya Serikali mwaka 2007/2008 inaonesha kwamba mshahara utaongezeka kwa 12%. Hili ni ongezeko dogo sana ukizingatia kwamba kima cha chini cha mshahara ni shilingi 75,000 tu. Hii inamaanisha kwamba kima cha chini kitaongezeka na kufikia shilingi 84,000 tu. Kwa hali hii bado maisha ya Mtanzania yataendelea kuwa magumu sana huku gharama za maisha zikiendelea kupanda kutokana na Bajeti ngumu iliyowasilishwa na Serikali mwaka huu wa fedha.
10. Mheshimiwa Spika, wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikisikia kilio cha Wafanyakazi nchini wakiomba nyongeza ya mshahara ifikie Shs.315,000 kwa kima cha chini kutokana na kupanda kwa hali ya maisha.
11. Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu sehemu ya Risala ya Wafanyakazi iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa TUCTA Ndugu Nestory Ngula katika kilele cha maadhimisho ya Mei Mosi kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mjini Mwanza mwaka 2007. Wafanyakazi walisema
. Vyama vya Wafanyakazi viliwasilisha mapendekezo ya kuboresha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Umma cha Shs. 75,000/= kwa mwezi kinacholipwa sasa hadi kufikia Shs. 315,000/= kwa mwezi. Kima hicho cha chini cha mshahara tulichopendekeza cha Shs. 315,000/= ndicho kiwango cha chini kabisa cha mshahara kitakachomwezesha mfanyakazi wa ngazi ya chini mwenye familia ya watu sita yaani Mume, Mke na watoto wanne chini ya umri wa miaka 18 kuweza kumudu mahitaji muhimu ya maisha kwa mwezi. Mshahara huu wa Shs. 315,000/= wa kima cha chini unamwezesha Mfanyakazi kutumia Shs.142,000/= kwa ajili ya kupata mlo asubuhi, mchana na jioni kila mwezi kama kima hiki cha mshahara hakitakatwa kodi yeyote wala michango mingine. Kima hicho pia kitakidhi pia gharama zingine za Shs.173000/= kwa mwezi mmoja kulipia usafiri wa kwenda kazini, usafiri wa watoto wanne wa shule ya msingi, sare za watoto, kodi ya nyumba (vyumba vitatu), Mavazi, matibabu, maji, umeme na akiba ya dharura
Mwisho wa kunukuu.
12. Mheshimiwa Spika, cha kushangaza ni kwamba kiasi kilichoongezeka hakifikii hata robo ya maombi yao. Hili linasikitisha sana. Hata hivyo, kambi ya upinzani inatambua kwamba kutokana na hali ya uchumi ongezeko hili kwa ghafla lisingeweza kufikiwa. Pamoja na hayo, bado tunaamini ya kwamba kama serikali ingepokea ushauri wa kuboresha bajeti uliotolewa na Kambi ya Upinzani, ongezeko hilo lingeweza kufikiwa angalau nusu.
13. Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya fedha mwaka 2007/2008 kama ilivyowasilishwa na Waziri Kivuli wa Fedha inaonyesha kwamba kima cha chini cha mshahara kingefikia kiasi cha shilingi 215,000 kutokana na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya ndani. Kwa ngazi nyengine mshahara ungepanda kwa asilimia ambayo ingeleta uwiano baina ya kipato cha chini na cha juu. Ni wazi kwamba hili limeshindikana kwa serikali ya awamu ya nne kukataa mapendekezo yaliyotolewa ambayo yangeongeza makusanyo ya mapato ya ndani katika sekta mbali mbali kama vile madini, utalii, uvuvi wa bahari kuu, misitu na bandari, bila kusahau kupunguza misamaha ya kodi.
14. Mheshimiwa Spika, licha ya kupendekeza kima cha chini kuwa Shs. 215,000, hatukubaliani na ushauri wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini kuwa kima cha chini kisilipwe kodi. Kambi ya upinzani inasema, kima cha chini kingeongezwa mpaka kufikia kiasi tulichotaja lakini pia lazima kodi ilipwe. Kulipa kodi ni wajibu wa kila raia.
15. Mheshimiwa Spika, haitakuwa busara kwa kambi ya upinzani kusahau kutetea maslahi ya watumishi wasiokuwa wa Umma. Sekta binafsi nayo imekuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa ajira kwa Watanzania, lakini ubaya wake unaonekana pale sekta hii inapojilimbikizia faida na kuwanyonya watumishi wake. Kwa sasa kima cha chini katika sekta binafsi ni kati ya shs.35,000 na shs. 48,000, kiasi ambacho ni kidogo sana kulingana na hali ya maisha ilivyo sasa. Kiwango hiki cha mshahara kinamwezesha mfanyakazi kugharamia chakula cha asubuhi, mchana na jioni kwa muda wa wiki moja tu bila kulipia gharama zingine. Kambi ya upinzani inaiomba serikali itangaze kiwango kipya cha kima cha chini kwa watumishi wasio wa Umma.
16. Mheshimiwa Spika, kwa kuangalia Bajeti kuu ilivyo ni wazi kwamba vipengele vyengine si vya msingi kiasi cha kutengewa mabilioni ya fedha kila mwaka, huku watumishi wa Umma wakiachwa solemba. Mfano, katika Bajeti ya mwaka huu 2007/2008 zimetengwa bilioni 5.5 kwa ajili ya ukarabati wa Ikulu, mwaka 2006/2007 zilitengwa bilioni 6.125 na mwaka 2005/2006 zilitengwa bilioni 3.2 kwa ukarabati huo huo wa Ikulu. Kambi ya upinzani inahoji uhalali wa mabilioni haya yanayotengwa kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa Ikulu. Kuna nini huko? Je, serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kupunguza baadhi ya matumizi ili kujali maslahi ya Watumishi wa Umma?
17. Mheshimiwa Spika, TUCTA pia katika Risala yao wanahoji juu ya matumizi ya kifahari na yasiyo ya msingi. Naomba ninukuu
Hatukatai sababu zinazotolewa na Serikali kuwa uchumi wetu bado ni mchanga, lakini tunashangaa kuona kwamba pamoja na uchumi kuwa mdogo bado matumizi ya Serikali katika baadhi ya maeneo ni makubwa kuliko hata katika nchi ambazo uchumi wake ni mkubwa kuliko wa nchi yetu. Matumizi haya ya Serikali yasiyofanana na hali ya uchumi ni katika manunuzi ya magari makubwa ya kifahari aina ya VX (Landcruiser, Mitsubishi Pajero, Prado, Nissan Patrol n.k) ambayo yananunuliwa kwa bei kubwa na yenye gharama kubwa katika matumizi ya mafuta na matengenezo. Inashangaza kuona kwamba kuna magari mengi ya aina hiyo katika ofisi nyingi za Serikali kuanzia Wizarani, Mikoani, Wilayani na Taasisi nyingine za Umma.
Takwimu toka Wizara ya Miundombinu zinaonyesha kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha wa mwaka 2005/06 jumla ya magari makubwa na ya kifahari yapatayo 6,000 yalikuwa yamenunuliwa na Serikali kwa gharama kubwa inayokadiriwa kufika T.Shs.Bilioni 160. Miongoni mwa magari hayo ya gharama kubwa na ya kifahari yaliyonunuliwa na Serikali hadi mwaka 2005/2006 ni aina ya Toyota Landcruiser (VX/GS, STD, Prado) yapatayo 1,655, Nissan Patrol na Landcruiser 885, Mitsubishi Pajero 400 na mengineyo. Serikali ingekuwa inafanya matumizi yake kwa kuzingatia hali ya uchumi kama inavyofanya kwa wafanyakazi kwa kuwalipa mishahara isiyotosheleza mahitaji muhimu ya maisha, basi ingeweza kubana matumizi kwa kununua magari madogo ya kawaida na kuweza kuokoa mabilioni ya fedha ili kuboresha mishahara ya wafanyakazi au kuimarisha huduma za jamii.
Aidha umezuka mtindo wa kununua samani (furnitures) za ofisi za Serikali toka nchi za nje kwa gharama kubwa badala ya kununua kwa watengenezaji wa samani hizo toka hapa nchini ili kubana matumizi, kuongeza ajira, na kuinua uchumi wa nchi yetu. Wakati vyama vya Wafanyakazi vilipokutana na Tume ya Rais ya kuboresha Mishahara ya Watumishi wa Umma wakati inakusanya maoni, tulishauri mambo mengi ambayo yangesaidia kupatikana kwa fedha kwa ajili ya kuboresha mishahara ya wafanyakazi. Ushauri tuliotoa ni pamoja na kupunguza magari ya kifahari, kupunguza misafara mikubwa ya viongozi ndani ya nchi wakati wanatembelea Mikoani na Wilayani. Misafara hiyo hutumia gharama kubwa kugharamia mafuta na matengenezo kwa ajili ya misululu mikubwa ya magari yanayotumika kwenye ziara hizo ikiwa ni pamoja na kulipa posho za kujikimu viongozi na watendaji. Matumizi ya aina hii huwafanya wafanyakazi wasielewe kabisa wanapoelezwa kuwa uchumi wetu ni mdogo na hauwezi kubeba gharama kubwa za mishahara wakati wanaona matumizi ya Serikali hayalingani na hali ya uchumi mdogo
Mwisho wa kunukuu.
18. Mheshimiwa Spika, kama kumbukumbu zetu zitakuwa sawa wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani na kulihutubia Bunge, pamoja na mambo mengine aliunda Tume ya kurekebisha mishahara ya watumishi wa umma ambayo ilikuwa chini ya Mwenyekiti Ndg. Deogratias Ntukamazima, na kwa sasa ni dhahiri tume hiyo itakuwa imemaliza kazi. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iiweke hadharani ripoti hiyo ili wabunge na wawakilishi wa wafanyakazi waweze kuona kama yaliyopendekezwa yanalingana na mapendekezo ya maoni ya vyama vyao vya wafanyakazi.
19. Mheshimiwa Spika, kuchelewa kulipwa kwa nyongeza ya mshahara kwa Watumishi wanaopandishwa cheo ni kero nyengine miongoni mwa kero zinazowasumbua Watumishi wa Umma. Kambi ya upinzani inaomba kuelezwa sababu zinazopelekea kucheleweshwa kwa malipo ya nyongeza ya mshahara kwa baadhi ya watumishi.
III. UTAWALA BORA
20. Mheshimiwa Spika, Utawala Bora ni pamoja na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa umma. Utawala bora pia ni pamoja na kutoa majibu kwa wakati kulingana na masuala yanayoulizwa na muulizaji. Katika kipindi hiki cha uongozi, Serikali inashindwa kuwapatia majibu wananchi ambao wanaandika barua zao kwa misingi ya kupata ufafanuzi kulingana na masuala mbali mbali. Na jambo hili kwa ujumla wake linadhalilisha nchi inayojiita kuwa inafuata sheria na utawala bora. Mfano mzuri ni Mheshimiwa Waziri kivuli wa Utawala Bora alipoandika barua kupitia Kiongozi wa Upinzani alipomuandikia Mhes. Rais kuhusu maafa Jimboni kwake, alipata majibu baada ya miezi mitatu. Je, Watanzania wa kawaida inawachukua miaka mingapi?
21. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia haya ni lazima Ofisi hii itupiwe jicho makini na pembuzi zaidi ili kugundua mianya yenye kudhoofisha utendaji wake.
HAKI ZA BINADAMU
22. Mheshimiwa Spika, Utawala Bora unahusu pia utawala wa sheria na kuheshimiwa kwa misingi ya haki za binadamu. Hivi karibuni tu jumuiya mbili za kiraia, Legal and Human Rights Centre (LHRC) na Zanzibar Legal Service Centre (ZLSC), kwa pamoja zilishirikiana kutoa Ripoti ya Haki za Binadamu nchini Tanzania kwa mwaka 2006. Ripoti hiyo imeonyesha kukithiri kwa matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu yanayofanywa na raia na pia vyombo vya dola. Inataja matukio ya kuendelea kutumika kwa adhabu ya kifo, kutozingatiwa kwa haki za wafungwa na mahabusu, matukio ya vikosi vya ulinzi na usalama vya Muungano na vikosi vya SMZ kutumia nguvu za ziada na kuvunja haki za binadamu yakiwemo kuua, kuuliwa kwa vikongwe kwa kudhaniwa wachawi, uhuru wa vyombo vya habari kufinywa, kutoheshimiwa kwa haki na uhuru wa kisiasa, wa kujikusanya na kujumuika, kutozingatiwa haki za wafanyakazi, haki za makundi maalum yakiwemo wanawake na watu wenye ulemavu, wazee, wakimbizi, wagonjwa wa UKIMWI, rushwa na utumiaji mbaya wa madaraka.
23. Mheshimiwa Spika, hali inayoelezwa katika Ripoti hii inatisha na haiendani na majigambo ya Serikali kwamba Tanzania inafuata na kuongozwa na misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu. Kambi ya Upinzani inapenda kupata maelezo juu ya hatua zinazochukuliwa na Ofisi ya Rais (Utawala Bora) katika kufanyia kazi yale yaliyomo katika ripoti hii ili matukio ya aina zilizotajwa yasijirejee tena.
UTEKELEZWAJI WA HUKUMU ZA MAHAKAMA
24. Mheshimiwa Spika, tunategemea utawala bora katika nchi unaendelezwa kupitia mihimili mitatu ya dola ambayo ni Bunge, Mahakama, na tawi la utendaji kwa kutengana kimamlaka (Separation of Powers) kwa mujibu wa Katiba. Kila mhimili kati ya hiyo mitatu unapaswa kuwa huru na kuwa na mamlaka ya kuangalia utendaji wa mhimili mwengine (Checks and Balances). Hivyo basi, maamuzi ya kila mhimili yanapaswa kuheshimiwa kikatiba na mihimili mengine. Kwa mfano; uamuzi unaopitishwa na Bunge juu ya sera na sheria unapaswa kutekelezwa na tawi Tendaji (Executive) huku Mahakama ikiwa na jukumu la kutafsiri na kusimamia sheria hizo.
25. Mheshimiwa Spika, ili maamuzi ya Mahakama yatekelezwe ni lazima Bunge lipitishe sheria inayohusu kadhia hiyo. Cha kushangaza ni kwamba tangu Mahakama Kuu ya Tanzania ilipotoa hukumu ya kufuta sheria ya takrima Serikali haijaleta Bungeni muswada unaohusu hukumu hiyo. Aidha, tangu Mahakama Kuu ilipotoa hukumu juu ya mgombea binafsi Serikali haijaleta Bungeni muswada wa kutekeleza hukumu hiyo? Na je kisheria ni muda gani tangu mahakama kuu inapotoa hukumu juu ya jambo fulani na Serikali au chombo kingine cha dola kinatakiwa kutekeleza hukumu hiyo? Kambi ya Upinzani inaitaka mihimili hii mitatu kuheshimiana na kuangaliana kiutendaji kama katiba inavyotaka. Ili dhana ya utawala bora ionekane, maamuzi ya kila muhimili yaendanayo na katiba, lazima yatekelezwe katika muda wake.
USALAMA WA TAIFA
26. Mheshimiwa Spika, Katika Idara ya Usalama wa Taifa kumekuwepo na ongezeko kubwa la fedha. Kutokana na unyeti wa kitengo hiki tunaweza kuona hata bajeti yake inakuwa kubwa kuliko bajeti ya mihimili miwili ya dola kwa pamoja yaani bajeti ya Ofisi ya Spika, ambayo ni Tshs.42 bilioni, na Mahakama ambayo imetengewa Tshs.37 bilioni. Kwa ujumla mihimili hii imetengewa Tshs. 79 bilioni ikilinganishwa na kitengo cha Usalama wa Taifa ambacho kimetengewa Tshs. 110bilioni kama inavyoonyesha kwenye vote 30 programu ya kumi, Utawala.
27. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa kufuatana na Sheria ya Usalama wa Taifa, kitengo hiki shughuli zake nyingi huwa hazizungumzwi wazi wazi, ndio maana hata waheshimiwa Wabunge huwa hatuulizi maswali mengi juu ya kitengo hiki. Lakini pamoja na utamaduni huo wa usiri, Kambi ya Upinzani inaomba ielezwe sababu za kitengo hiki kuongezewa mabilioni ya fedha kadiri siku zinavyoongezeka.
MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
28. Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha utaratibu wa kutoa fomu za maadili kwa madiwani. Kwa mujibu wa maelezo ya Mhe. Waziri anayeshughulikia masuala ya Utawala Bora, asilimia 70 ya madiwani hawakujaza fomu hizo. Kwa kuwa sheria zinamlazimisha kiongozi wa umma kufanya hivyo, kambi ya upinzani inamuomba Mhe. Waziri atuambie kwa nini nafasi hizo zisitangazwe kuwa ziko wazi kutokana na wahusika kushindwa kutekeleza matakwa muhimu kisheria kama hayo?
29. Mheshimiwa Spika, pia Waziri alikiri kwamba sio fomu zote zinazokaguliwa bali mtindo wa sampling hutumika akitoa sababu kuwa viongozi ni wengi. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inaona kuwa mtindo huu wa ukaguzi kwa njia ya sampling (yaani kupitia fomu chache tu) unaua dhana nzima ya sheria husika ambayo lengo lake ni kuhakikisha kwamba Watumishi wa Umma wakiwa kwenye madaraka hawatumii madaraka yao kujilimbikizia mali.
30. Mheshimiwa Spika, suala hili la uzembe wa kuwawajibisha viongozi wanaoshindwa kujaza fomu za maadili inathibitisha jinsi ambavyo Sekretarieti ya Maadili ya Watumishi wa Umma ama imeshindwa kufanya kazi yake kiumakini (kwa kuwa iko juu) ama imezidiwa na kazi hivyo kuwa na haja ya kupanuliwa zaidi kufikia ngazi ya halmashauri.
31. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni vyombo vya habari vimeandika juu ya madai kwamba Rais mstaafu, Mhe. Benjamin Mkapa, alitumia Ikulu ya Watanzania kufanya biashara kwa manufaa binafsi. Je, Serikali inaweza kuweka utaratibu utakaomruhusu raia wa nchi hii kupekua nyaraka za matamko ya Mali na Madeni ya Mhe. Mkapa ili kujiridhisha kuwa, biashara yake iliendeshwa sawa sawa kwa kufuata sheria za nchi?
32. Mheshimiwa Spika, na kama Rais anaruhusiwa kufanya biashara akiwa Ikulu kwa ajili ya kujitafutia maisha yake ya baadae akitoka katika Ofisi hiyo, Kambi ya Upinzani ingependa kujua nini ulikuwa msingi wa Bunge hili tukufu kupitisha Sheria Na. 3 ya 1999 (Political Service Retirement Benefit Act, 1999) pamoja na marekebisho yake?
UBADHIRIFU WA MALI ZA UMMA
33. Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na ubadhirifu mkubwa wa mali za Umma kutokana na rushwa na ufisadi ambapo kila mwaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali anatoa taarifa Bungeni akionyesha fedha nyingi ambazo zimepotea na hazina maelezo ya kutosha kwenye Wizara na idara husika za serikali. Katika mwaka wa fedha 2002/2003 Shilingi 65 bilioni ziliripotiwa kupotea, mwaka 2003/2004 Shilingi bilioni 82, mwaka 2004/2005 shilingi bilioni 203, na mwaka 2005/2006 shilingi bilioni 273. Kati ya hizo shilingi bilioni 242 ni za serikali kuu. Ni dhahiri kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa kwani kama si hivyo tunaelezaje ongezeko hilo la fedha zinazokosa maelezo kila mwaka? Kambi ya upinzani inahoji ni hatua gani zimechukuliwa kwa upotevu huu mkubwa wa fedha kwa maana ya kuwawajibisha wahusika.
34. Mheshimiwa Spika, ni muhimu pia ikaeleweka kwamba kiasi cha bilioni 242, ambazo zilifanyiwa ubadhirifu na idara mbali mbali za serikali kuu, zingeweza kufanya kimoja kati ya yafuatayo kwa ukamilifu wake:-
i) Kulipa mishahara ya mwaka mzima ya walimu zaidi ya 160,000 wa shule za msingi.
ii) Kununua vitabu zaidi ya 100 milioni.
iii) Kujenga ofisi za serikali na maktaba ya kila kijiji Tanzania.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizi ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Haki Elimu.
35. Mheshimiwa Spika, katika kupambana na ubadhirifu mkubwa wa mali za serikali, mara baada ya kuchaguliwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania alitangaza kwamba CAG atapewa mamlaka ya kisheria ya kufuatilia taarifa mbaya za fedha. Vile vile, alisema kwamba watumishi watakaohusika na makosa ya matumizi mabovu ya fedha za Umma watafikishwa mbele ya vyombo vya dola washitakiwe na si kupitia mabaraza ya kiutawala ambayo hutoa hatua za kinidhamu zaidi. Kambi ya upinzani si tu inaomba ielezwe kauli hii ya Rais imetekelezwa kiasi gani, bali pia inataka wahusika katika ubadhirifu wa mali za serikali wawajibishwe kama Mhe. Rais alivyoahidi bila kujali cheo au madaraka ya mhusika.
36. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla dhana ya Utawala Bora imeendelea kudhoofika kwa kuwepo ubadhirifu mkubwa wa mali za Umma, matumizi mabovu ya fedha za Umma na upotevu wa fedha za umma usiotolewa maelezo ya kutosha. Mambo mengi ambayo yanaweza kutajwa katika kadhia hii ni kama vile; masuala yanayohusu mijadala ya mikataba ya Richmond, ununuzi wa Rada, ununuzi wa Ndege ya Rais, mikataba mibovu ya madini, ujenzi wa Majengo marefu ya Benki Kuu kwa thamani kubwa mno kuliko hata gharama za kujenga New York, London na Tokyo, na matumizi mabaya ya nyadhifa za Serikali kwa kujipatia maslahi binafsi. Kama Serikali itafumbia macho uoza kama huu Tanzania kamwe haitaweza kujigamba kuwa na Utawala Bora ambao utaleta maendeleo.
MUINGILIANO BAINA YA SERIKALI KUU NA ZA MITAA
37. Mheshimiwa Spika, ili kuboresha ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya kimaendeleo serikali za mitaa zinapaswa kupewa kiasi kikubwa cha uhuru ambacho kitaziwezesha kusimamia shughuli za kimaendeleo. Shughuli hizi pamoja na kushirikisha wananchi kwa ukaribu zaidi, pia huhitaji fungu maalum lenye kutosheleza utendaji wa shughuli hizo.
38. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa programu ya kurekebisha mfumo wa serikali za mitaa ulioanza mwaka 1996 (Local Government Reforms Programme) serikali za mitaa zimepewa uhuru fulani wa kiutendaji (Devolution). Lakini pamoja na juhudi hizo zote, kambi ya upinzani inaona bado uhuru huo wa serikali za mitaa unadunishwa katika maeneo yafuatayo:-
i) Katika uandalizi wa bajeti. Imebainika kwamba vipaumbele vya bajeti vinavyopendekezwa na wananchi kupitia halmashauri zao huwa havizingatiwi katika ngazi za juu za uandaaji wa bajeti kama vile katika ngazi za Wizara. Matokeo yake ni kupangwa kwa fungu la bajeti lisilowiana na matatizo na mahitaji ya halmashauri husika.
ii) Kupitishwa kwa muswada unaompa mamlaka Waziri anayehusika na serikali za mitaa kuteua madiwani watatu kwa ridhaa yake, kunafinya demokrasia ya wananchi kujichagulia viongozi wao wote katika ngazi za halmashauri.
39. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inaona muingiliano huo si jambo bora hata kidogo katika suala zima la kuziimarisha serikali za mitaa na kuleta maendeleo katika halmashauri. Hivyo basi, tunapendekeza yafuatayo:-
Kwanza, vipaumbele vya bajeti vinavyopendekezwa na wananchi katika ngazi za serikali za mitaa vizingatiwe katika uandaaji wa bajeti kuu kwani vipaumbele hivyo huendana na uhalisia wa matatizo na mahitaji ya wananchi. Kambi ya Upinzani ina kila sababu ya kulizungumzia suala hili kwani, tunaelewa kuwa Serikali kuu inatumia takriban robo tatu ya fedha yote. Fedha hizi hugharamia mlolongo wa huduma kadhaa ambazo husimamiwa kwenye ngazi ya serikali kuu, kama vile mishahara ya wafanyakazi, miradi mikuu ya ujenzi, elimu ya sekondari na afya huku Serikali za mitaa zikipewa kiasi kidogo tu cha fedha kisichotosheleza mahitaji.
Pili, wananchi wapewe mamlaka kamili katika kujichagulia wawakilishi wao wenyewe. Mheshimiwa Spika, ni jambo la kushangaza katika nyakati hizi za kidemokrasia, bado viongozi wanapewa mamlaka ya kuwachagulia wananchi wawakilishi wao!!!
MALALAMIKO YA URASIMU TASAF
40. Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tanzania Social Action Fund - TASAF) ni moja ya chachu za maendeleo ya kijamii. Hata hivyo, yamekuwepo malalamiko mengi yanayohusu urasimu katika TASAF hasa baada ya kuhusishwa kwa Ofisi ya TAMISEMI. Kama baadhi ya Wabunge wengi walivyoweza kuchangia katika kipindi cha maswali na majibu kumebainika kuwepo kwa ucheleweshaji wa fedha za utekelezwaji wa miradi ya maendeleo. Zaidi ni kwamba kuchelewa kwa michakato inayofanywa wilayani imetajwa kuwa ndiyo moja ya sababu za ucheleweshwaji wa fedha hizo.
41. Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inataka mfuko huu utambuliwe kisheria ili kuwezeshwa kuwa endelevu mpaka pale mkopo wa benki ya dunia utakapokwisha mwaka 2009 hasa ikizingatiwa kwamba gharama kubwa zimeshatumika kuwajengea uwezo watalaam mbalimbali wa TASAF.
UANZISHWAJI WA IDARA YA MIPANGO NA SERA, NA KITENGO CHA UKAGUZI WA NDANI
42. Mheshimiwa Spika, Idara mpya ya Mipango na Sera imeanzishwa katika Ofisi ya Rais. Kambi inahoji uhalali wa kitengo husika hasa ikizingatiwa kwamba kuna Wizara inayohusika na Mipango, ambayo ina idara lukuki. Ni muhimu serikali ikatueleza kama Mhe. Waziri na Wizara yake wameshindwa kufanya kazi kiasi cha kuhitaji usaidizi wa idara mpya. Mheshimiwa Spika, kuundwa kwa idara nyingi zenye muingiliano wa kimajukumu ni matumizi mabovu ya fedha za Umma. Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kwamba Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji inatosheleza kushughulikia majukumu hayo.
43. Mheshimiwa Spika, dhana mpya ya Utumishi wa Umma inatilia mkazo kuipunguzia Serikali shughuli kwa kuachia shughuli zake kufanywa na taasisi mbali mbali kwa niaba yake. Dhana hii kwa kiasi kikubwa inapunguza matumizi ya Serikali na vile vile kuongeza ufanisi katika sekta husika. Hivyo, kitendo cha kuanzishwa kwa idara ya mipango katika Ofisi ya Rais ni kuongeza ukiritimba na kinapingana na dhana hiyo ambayo ilikwisha anzishwa na ilitakiwa iendelee kwa manufaa ya Serikali na Watanzania kwa ujumla.
44. Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali itueleze sababu za msingi kabisa za kuwepo kwa idara hiyo mpya.
45. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani pia ingependa kuelezwa sababu za kuanzishwa kwa kitengo cha ukaguzi wa ndani. Ongezeko la bajeti ndilo linalotajwa kama sababu ya msingi kwa kuanzishwa kwa kitengo hicho. Kambi ya upinzani inaelewa kwamba taasisi zote nyeti za serikali zina wakaguzi wa ndani. Je uundwaji wa kitengo hiki unamaanisha kwamba wakaguzi wa ndani hawapo kama ambavyo tunafahamu au wameshindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa? Kambi ya Upinzani inatiwa shaka na uundwaji wa kitengo hiki kwani bado sababu za msingi hazijawekwa bayana na hivyo hatuoni sababu za kitengo hiki kuendelea kuwepo. Lengo la hoja hii ni kuhakikisha kwamba hakuna muingiliano wa kimajukumu au uundwaji wa vitengo ama idara zenye majukumu sawa. Hili likizingatiwa litaokoa matumizi holela ya fedha za walipa kodi na kuzielekeza fedha hizi katika shughuli za maendeleo.
IV. SIASA NA MAHUSIANO YA JAMII
46. Mheshimiwa Spika, halitokuwa jambo la busara kwa Kambi ya Upinzani kutoshukuru kwa uwepo wa Ofisi hii muhimu sana. Ofisi hii ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha uwepo wa siasa bora na mahusiano mema ya jamii katika taifa letu. Ofisi hii inatarajiwa kuhakikisha kuwa migogoro ya kisiasa na ya kijamii inatafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili kudumisha taifa lenye umoja na amani ya kweli. Pamoja na umuhimu wa ofisi hii bado yamekuwepo mapungufu ambayo yamedhoofisha ama utendaji wa ofisi hii au kuhatarisha amani ya taifa letu (hususan kule visiwani Zanzibar).
MAMBO YA SIASA
47. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapongeza kuanzishwa kwa mazungumzo kati ya CCM na CUF ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa kisiasa Zanzibar. Hata hivyo, mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu hasa ikizingatiwa ni miezi 18 tokea Mheshimiwa Rais alipotoa ahadi ndani ya Bunge hili tukufu ya kulishughulikia suala hili na hadi sasa hakuna maelezo juu ya hatua iliyofikiwa. Kambi ya Upinzani inapenda kupata maelezo juu ya mazungumzo hayo ambayo yakiendelea kuchelewa yanaweza kuiweka nchi yetu katika mtihani mkubwa wa utulivu wa kisiasa.
48. Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa kuwa Watanzania wengi ambao walipiga kura kwa ujumla wao walimpatia Mhe. Rais ridhaa ya kuongoza nchi yetu bila ya kuangalia kuwa ni wa itikadi gani. Kwa imani yao hiyo kwa Rais wao, ni matarajio yao pia kuwa Rais huyo atakuwa ni wa wote bila ya kubagua.
49. Mheshimiwa Spika, vile vile, kwa kuwa Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati mmoja, hivyo, kutokana na nyadhifa zake hizo mbili, tunategemea kwa kufuata katiba ya nchi, atatumia kila kofia yake kwa mahali, wakati na rasilimali mwafaka kufanya shughuli inayoendana na kazi mojawapo ya kofia zake hizo mbili.
50. Mheshimiwa Spika, tumeamua kulisema hili ili liwekwe bayana kwa ukweli na Serikali kwamba katika ziara za mikoa ya Kigoma na Rukwa, Mhe. Kikwete alikwenda huko kama Rais wa nchi, na kwa kutumia pesa za walipa kodi wote wa Tanzania. Kitendo chake cha kugeuza mikutano ya hadhara ya kiserikali kuwa uwanja wa kubomoa vyama vya upinzani kinakwenda kinyume na misingi ya utawala bora, hakikubaliki, hakivumiliki, na si cha kistaarabu kwa mpenda demokrasia yeyote yule.
51. Mheshimiwa Spika, hili lilikuwa ni msingi wa malalamiko yaliyotolewa na viongozi wa vyama vya siasa nchini kama ilivyolalamikiwa katika tamko la Wakuu wa Vyama Vilivyoko Kwenye Ushirikiano (CHADEMA, CUF, TLP, NA NCCR MAGEUZI) lililotolewa kwa Wananchi na kwa vyombo vya Habari mnamo tarehe 7 juni, 2007 makao makuu ya CHADEMA Kinondoni, lililobeba kichwa cha habari TAMKO LA KULAANI JITIHADA ZA RAIS JAKAYA KIKWETE ZA KUUVUNJA UPINZANI NCHINI TANZANIA.
52. Mheshimiwa Spika, kwa Rais yeyote anayefuata maadili ya utawala bora na anayependa kukuza demokrasia katika nchi yake, kitendo cha kuwa katika ziara ya kiserikali, na kutumia fedha za walipa kodi na madaraka yake kuvunja maadili na misingi ya utawala bora kwa kufanya kazi za kisiasa, ni kitendo cha kumfedhehesha Rais wetu aliyechaguliwa na Watanzania bila kujali itikadi zao.
53. Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo, katika kupitia vitabu vya bajeti kwa Wizara na Idara za Serikali kwa mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga kiasi cha Tshs. 220,000,000/= kwa ajili ya mambo ya siasa. Je, Serikali inataka kufanya siasa gani nje ya siasa zinazofanywa na vyama vya siasa? Ikumbukwe kuwa ahadi ya kuonana na vyama vya siasa iliyowahi kutolewa na Rais haikuwahi kutekelezwa. Je, fedha hizo zitatumiwa na Rais kukutana na viongozi wakuu wa vyama vya siasa? Kama siyo hivyo, ni kwa nini hasa itajwe kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya siasa? Tunamuomba Mhe. Waziri afafanue matumizi halisi ya fedha hizo ili kama ni mkopo kwa vyama vya siasa vielewe ili viweze kwenda kukopa huko kwa ajili ya shughuli zao za kisiasa.
54. Mheshimiwa Spika, katika kikao cha Bajeti cha mwaka jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Mahusiano ya Jamii) alilieleza Bunge lako tukufu kuwa Ofisi yake haikuwa imeanza kazi zake rasmi kwa vile ilikuwa ikijijenga kitaasisi na kazi hiyo ilikuwa ndiyo kwanza imekamilika. Kambi ya Upinzani inapenda kujua sasa baada ya mwaka mzima kupita tokea kauli hiyo kutolewa, Ofisi hii imefanya lipi katika kumsaidia Rais kuimarisha mahusiano ya kisiasa na ya kijamii hapa nchini.
AHADI ZA RAIS
55. Mheshimiwa Spika, moja ya sifa kuu ya Serikali ya awamu ya nne ni jinsi ambavyo iliweza kuwajaza wananchi matumaini kwa ahadi kedekede wakati wa kampeni na hata baada ya Serikali hiyo kuingia madarakani. Ahadi hizi zililenga kutoa picha ya Maisha bora kwa kila Mtanzania. Cha kusikitisha ni kwamba kadiri siku zinavyokwenda maisha ya Mtanzania yanazidi kuwa duni. Baya zaidi ni uamuzi wa serikali kupitia Bajeti kuu mwaka 2007/2008 kupandisha kodi katika mafuta, bidhaa ambayo inagusa na kuathiri maisha ya kila siku ya Mtanzania kwa namna tofauti tofauti. Kinachojidhihirisha ni kuwa ahadi hizi zilitumika kama danganya toto tu kwa wapiga kura
56. Mheshimiwa Spika, swali ambalo kambi ya upinzani inajiuliza ni kama wananchi wamesahaulika au ahadi hizo zimeshindwa kutekelezeka? Ahadi hizo ni nyingi sana, kama baadhi yake zilivyoorodheshwa katika makala iliytolewa na HAKIELIMU kwa jina la Government Promises ya mwaka 2006 na nyenginezo ambazo zimeendelea kutolewa wakati Rais akiwa madarakani. Kambi ya upinzani inayo shauku ya kujua zimeshatekelezwa ahadi ngapi katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa Serikali ya Awamu ya Nne na ngapi zimebaki, hasa ikizingatiwa kauli ya Mheshimiwa Waziri kwenye kamati kwamba ahadi zinatolewa katika kipindi cha miaka 5 na hivyo ahadi hizo zote zinatakiwa ziwe zimetekelezwa katika kipindi cha miaka 5.
57. Mheshimiwa Spika, Baada ya kuyasema hayo, kwa mara nyengine natoa shukurani zangu kwako kwa kunipa fursa hii, na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Nasema Asanteni sana. Na naomba kuwasilisha.
..
SHOKA KHAMIS JUMA (MB)
K.N.Y MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI,
OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UMMA.
02. 07. 2007