Na Mwandishi Wetu, Jijini
Taarifa ya jana ya Waziri Mkuu, Bwana Mizengo Pinda juu ya utekelezaji wa mapendekezo 23 ya Bunge, kuhusu mkataba tata wa Richmond, imezua vuguvugu kubwa miongoni mwa wananchi, ambapo hivi sasa, watu wanataka kila aliyeliingizia losi taifa , aburuzwe kortini.
Wakiongea na gazeti hili leo asubuhi, wananchi kadhaa wamedai kuwa Serikali imeingia mikataba kibao ya hasara wakati kuna watalaam wazuri wa sheria ambao wangeweza kuzuia hali hiyo.
Wamesema mtu wa kwanza anayepaswa kulaumiwa kwa suala hilo, ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Andrew Chenge ambaye wanadai alijua fika mikataba kadhaa inayosainiwa haina maslahi kwa taifa.
``Chenge ni mwanasheria mzuri tu na alijua yote hayo lakini hakuzuia...anapaswa kuchukuliwa hatua,`` amesema
Bw. Mahenge Fanuel na kuungwa mkono na Bi. Halima Salehe ambao wote ni wanafunzi wa chuo kimoja cha elimu ya juu Jijini.
Wakazi wengine wamesema kinachotakiwa kufanywa hivi sasa ni Serikali kuchukua hatua dhidi ya watalaam wote waliohusika na mikataba yote feki.
``Sio huo wa Richmond tu, ipo mikataba mingi ambayo watalaam wameliingiza taifa kwenye matatizo...wote hao waangaliwe na kuchukuliwa hatua,`` amesema Bi. Jamillah Shaaban.
Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa chama cha TLP,
Bw. Augustine Mrema naye amemshikia bango Bw. Chenge.
akitaka afunguliwe mashtaka ya jinai kuhusiana na mkataba wa IPTL.
Amesema Bw. Chenge alifahamu vema kuwa mkataba huo ni mbovu lakini akashindwa kuishauri vema Serikali.
``Inabidi ashitakiwe kwa mashtaka ya jinai ya kuisababishia nchi hasara kubwa wakati alikuwa akifahamu kinachoendelea katika mchakato mzima wa uingiaji mkataba huo,`` akasema Bw. Mrema.
Amesema jana alimshangaa Waziri Mkuu alipoliambia Bunge kuwa miongoni mwa wanasheria waliompa ushauri na maoni juu ya majadiliano ya mikataba ni Bw. Chenge.
``Haiwezekani mtu aliyehusika kulibebesha taifa hasara kubwa kutokana na kuishauri vibaya Serikali, akatoa ushauri mzuri,`` akasema.
Jana akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo 23 yaliyotolewa Februari mwaka huu, Waziri Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wanasheria watatu.
Alisema ofisi yake ilipata maoni kutoka kwa Bw. Chenge, Mbunge wa Musoma Vijijini, CCM, Namrod Mkono na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa sasa, Bw. Johnson Mwanyika.
``Maoni yao yataisaidia sana Serikali katika kuimarisha mfumo wetu wa majadiliano ya mikataba. Naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru waheshimiwa wabunge kwa maoni na ushauri wao mzuri sana,``alisema Bw. Pinda.
SOURCE: Alasiri ).