[h=1]
[/h]
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Jumapili,Februari23 2014
Dodoma. Wakati mjadala mkali ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ukitarajiwa kuwa muundo wa Muungano, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesisitiza Serikali mbili.
Akifungua semina ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM jana, Pinda alihoji sababu za baadhi ya watu kudai kufa kwa Serikali ya Tanganyika wakati ilishatoweka miaka 50 iliyopita.
Pinda alisema Tanganyika ilidumu kwa miaka mitatu baada ya uhuru, kuanzia mwaka 1961 hadi 1964 na kuungana na Zanzibar.
Alisema kwa msingi huo, Watanzania wengi hawajui lolote kuhusu Tanganyika kwa sababu baadhi yao walikuwa hawajazaliwa.
Suala hili najua litaleta mvutano mkali katika Bunge la Katiba. Binafsi hata ukinikurupusha usiku nitakwambia nataka Serikali mbili, alisema.
Alisema hata Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kueleza wazi kwamba, alikuwa kiongozi wa Tanganyika kwa muda mfupi na ilikuwa Tanganyika ya wakoloni ndiyo maana likaibuka wazo la kuungana na Zanzibar.
Hivi sasa tuna miaka 50 ya Muungano wetu lakini wapo watu wanadai Tanganyika, hivi hiyo Tanganyika wanayoida ni ipi, unalalamika kuikosa Tanganyika ipi,alihoji.
Alisema kasoro zilizopo katika Muungano zinaweza kujadiliwa na ikapatikana suluhu ya kudumu.
Tayari CCM imeshatoa waraka maalumu kwa wanachama wake ikisisitiza msimamo wake wa Serikali mbili, msimamo ambao pia wataingia nao bungeni wakati wa kujadili rasimu ya Katiba ambayo imependekeza muundo wa Serikali tatu.
Rushwa
Akizungumzia rushwa Pinda alisema, Jumuiya inatakiwa kuwa mstari wa mbele kusimamia uendeshaji wa chaguzi ndani ya chama kwa misingi ya maadili kwani wanaomwaga fedha ili kupata uongozi ndani ya chama wanatuvuruga na hiyo siyo njia ya kukijenga chama.
Alisema viongozi wanaopatikana kwa njia ya rushwa siyo viongozi bora na kuhoji, Hivi mtu anayetumia fedha kuingia madarakani akipata madaraka fedha hizo atazirudishaje.
Katika hotuba yake Pinda aliwagusia wanachama wa CCM wanaopanga nani agombee na nani asigombee na kufafanua kuwa hali hiyo hujenga makundi ndani ya chama hicho.
Tunahitaji kupata viongozi kwa kuzingatia umoja wetu na mshikamano miongoni mwa wanachama. CCM ikiwa imara itaunda Serikali imara. Chama kikiwa dhaifu ni wazi kuwa hata Serikali yake nayo itakuwa dhaifu alisema.
Pia aliitaka Jumuiya hiyo kujipanga kwa kuimarisha mali zake ikiwa ni pamoja na shule ili siku za usoni shule hizo ziwe miongoni mwa shule 10 zinazofanya vizuri nchini, kuitaka kutumia majengo, viwanja na ardhi inayofaa kwa kilimo ili kuitumia kuimarisha jumuiya hiyo.
Aiponda Chadema
Katika mkutano huo Waziri Pinda alikipiga kijembe Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa licha ya kufanya kampeni zake kwa kutumia helkopta tatu, kiliambulia ushindi katika kata tatu tu, kwenye uchaguzi wa madiwani uliofanyika hivi karibuni katika kata 27.
Chama ni kujipanga na wakati mwingine fedha siyo kila kitu. Chadema wameruka kwa helkopta tatu na wameambulia ushindi katika kata tatu tu.