CAG ashindwa kukagua hesabu za Meremeta na Tangold
ZITTO ASEMA NI LAZIMA ZIKAGULIWE
Na Ramadhan Semtawa
WINGU zito limegubika hesabu za mwaka 2007 za makampuni mawili nyeti ya Buhemba Goldmine (Meremeta) na Tangold baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kushindwa kukagua hesabu za kampuni hizo.
Kushindwa kwa CAG kukagua hesabu za Meremeta na Tangold kumekuja wakati tayari uendeshaji na mitaji ya makampuni hayo mawili, mojawapo ikiwa chini ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), ukigubikwa na utata huku watendaji wakipata kigugumizi kuzizungumzia na wakati fulani Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiapa kutozungumzia, hasa Meremeta.
Pinda alishawahi kubanwa bungeni kuhusu suala hilo, lakini akawataka wabunge kutojadili suala hilo, akieleza kuwa Meremeta inahusiana na masuala ya jeshi na hivyo haifai kujadiliwa kwenye chombo hicho.
Wakati kukiwa na wingu hilo, hali ya mashaka zaidi kuhusu Meremeta na Tangold imezidi kujitokeza mwaka huu ndani ya ripoti ya kwanza ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, inayoongozwa na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Katika ripoti hiyo, ambayo imeingia kwa undani katika kuangalia mashirika yote 193 yanayomilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na yale ya ubia, hesabu za Meremeta hazijakaguliwa na CAG.
"Kuna uwezekano mkubwa kuwa thamani ya uwekezaji mitaji ya umma itakuwa ni kubwa zaidi kutokana na taasisi nyingine 51 ambazo zipo kwenye orodha ya msajili lakini hazijawasilisha hesabu zao za sasa zilizokaguliwa," inasema sehemu ya ripoti ya kamati.
"Vilevile kuna taasisi mpya ambazo hazikuwa zimekaguliwa hesabu zao pia, miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na kampuni ya Buhemba Goldmine (Meremeta) TanGold.
"Kamati inaamini kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atahakikisha kuwa mashirika haya yanawasilisha hesabu zao kwa ukaguzi ili kuhakikisha mitaji ya umma haipotei au kutumika vibaya."
Akizungumza na Mwananchi kuhusu utata huo, Zitto alisema hesabu za mashirika hayo lazima zipelekwe kwa CAG kwa ajili ya ukaguzi.
Zitto alisema kamati itamwita msajili wa hazina aeleze uwekezaji wa serikali katika Meremeta na Tangold.
"Ni kweli CAG hajazikagua Meremeta na Tangold kwa sababu hazipeleka hesabu zao. Kamati imemuagiza CAG aikague Meremeta na pia itamwita msajili wa hazina aeleze uwekezaji wa serikali katika Meremeta na Tangold," alifafanua Zitto.
Kikatiba, CAG ana mamlaka ya kukagua hesabu zote za mamlaka za serikali kuu na mitaa na mashirika yote ya umma.
Habari zinadai kuwa ripoti ya Kamati ya Bomani iliyoundwa na rais kuangalia sekta ya madini na kutoa mapendekezo inaeleza kuwa ilishindwa kupata maelezo ya kutosha kuhusu uanzishwaji, umiliki na kufilisiwa kwa Meremeta na baadaye uanzishwaaji wa kampuni ya Tangold nje ya nchi. Inadaiwa kuwa Tangold ndiyo iliyorithishwa mgodi wa Buhemba.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, ambayo Mwananchi inayo nakala yake, Meremeta na Tangold ni miongoni mwa mashirika 51 ambayo CAG alishindwa kukagua hesabu zake.
Ripoti hiyo ilifafanua zaidi kwamba, licha ya serikali kuwekeza mtaji wa sh 4.1 trilioni katika jumla ya mashirika 193, bado hesabu za baadhi ya mashirika hayo 51 zimejaa utata.
Katika jumla ya mashirika hayo, ripoti imebainisha mashirika 152 yanamilikiwa na serikali kwa kiwango cha hisa cha asilimia 100, ambayo ndiyo pekee yaliyokaguliwa na CAG.
"Mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30 2007, serikali iliwekeza kiasi cha Shilingi 4.1 trilioni katika jumla ya mashirika 193, Serikali ilikuwa na hisa asilimia 100 katika mashirika na taasisi 152, hizi ndizo zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali," inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Ripoti hiyo inaonyesha kwamba, katika jumla ya mashirika 9, serikali ilikuwa na hisa asilimia 50 au zaidi na katika mashirika 32 serikali ilikuwa na hisa chini ya asimilia 50.
Mchanganuo huo wa ripoti unaonyesha zaidi kwamba, kati ya mashirika 193 ya Umma, mashirika 48 ni ya kibiashara, taasisi 119 ni za huduma, mashirika 13 yako kwenye hatua mbalimbali za ubinafsishaji na mengine 13 yako kwenye ufilisi.
Ripoti hiyo, ambayo tayari imesisitiza umuhimu wa kubadilishwa kanuni za bunge kuipa nguvu kamati, inaonyesha kwamba mashirika yote ambayo serikali inashikilia hisa za asilimia 50 na chini ya hapo hayana usimamizi (oversight) wa kibunge.
"Hivyo kamati hii haikupata fursa ya kukagua hesabu zao na hatimaye kutokujua mtaji wa umma unaendeshwa namna gani," inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kuhusu gawio kwa serikali kutoka katika mashirika hayo, ripoti ilifafanua kwamba yaliweza kuchangia mapato serikalini.
Ripoti hiyo inaongeza kwamba gawio kutoka mashirika ya umma liliongezeka kutoka Sh12.2 bilioni mwaka 2005/2006 hadi kufikia Sh13.4 bilioni mwaka 2006/2007.
"Kwa ujumla, Mashirika ya Umma yalichangia serikalini makusanyo ya gawio na kiasi kingine cha michango ya jumla ya Sh26.05 bilioni ukilinganisha na Sh60.7 bilioni mwaka uliotangulia.
"Makusanyo haya ni pungufu ya zaidi ya asilimia 50 na ni faida ya chini ya 10% ya mtaji, uliowekezwa kwa mwaka mzima wa 2006/2007,"inafafanua.
Meremeta ni kampuni yenye uhusiano na JWTZ ambayo ilianzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kama moja ya kitegauchumi kusaidia jeshi kujiendesha.
Hata hivyo, kumekuwa na utata kuhusu uwekezaji wa serikali na kama bado iko chini ya Benki Kuu (BoT) huku kampuni ya Tangold nayo ikigubikwa na wingu kuhusiana na umiliki wa fedha zake zenye uhusiano na Meremeta.
Tayari, serikali imekuwa ikigoma kutoa ufafanuzi wa hilo ikisema Meremeta inahusu mambo ya Usalama wa Taifa, hivyo si rahisi kuanika utendaji wake hadharani. Hata hivyo, kumekuwa na maswali mengi kuhusu kauli hiyo kwani serikali imegoma kutoa taarifa bungeni, lakini miongoni mwa wanahisa wa kampuni hiyo yaani British Law Association ni wageni, hivyo kuweza kujua siri za usalama wa taifa kuliko bunge.