Mengi jino kwa jino na Masha
Habari Zinazoshabihiana
• Polisi avunjwa jino kwa chupa ya bia 03.08.2007 [Soma]
• Shekhe jino kwa jino na Mchungaji kuhusu Dito 22.03.2007 [Soma]
• Kupanda kwa bei za mafuta:Masha asema Serikali inafanyia kazi mapendekezo 27.05.2006 [Soma]
*Serikali yampa siku saba ajieleze kuhusu kutishwa
*Yeye asema nyingi, amtaka Waziri ampeleke kortini
Na Waandishi Wetu
SERIKALI imempa siku saba Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Bw. Reginald Mengi, kuthibitisha madai yake kwamba kuna waziri kijana katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete amemtishia na kwamba kuna mikakati ya kufilisi biashara zake.
Akizungumza na Kituo cha Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) na kurushwa jana asubuhi Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Laurence Masha, alisema madai yaliyotolewa na Bw. Mengi yanaonesha kwamba Serikali haiwalindi vyema raia wake.
Waziri Masha alisema Mwenyekiti huyo anapaswa katika muda huo awe amethibitisha madai hayo, ili Serikali iweze kuangalia taratibu za kuyashughulikia.
Alisema jana angemwandikia rasmi barua ya kumtaka kuthibitisha madai yake ambayo aliyatoa juzi mbele ya vyombo vya habari, Dar es Salaam.
Kabla ya kutolewa agizo hilo jana, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilisema lilikuwa halijapokea taarifa yoyote kutoka kwa Bw. Mengi kuhusu kutishiwa na Waziri na hivyo lisingeweza kuliingilia suala hilo.
Akizungumza na Majira, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Bw. Evarist Mangala, alisema hadi juzi Desemba 3 hawakuwa na taarifa yoyote ambayo iliripotiwa kuhusu kutishiwa maisha kwa Bw. Mengi na badala yake walizisoma taarifa hizo kwenye vyombo vya habari.
Kuhusu siku saba alizopewa na Bw. Masha kuwasilisha ushahidi wake, Bw. Mengi alisema siku hizo ni nyingi na kumtaka Waziri kumpeleka Mahakamani haraka iwezekanavyo.
"Vitisho ni vingi sana, lakini si kila kitu ninaweza kupeleka taarifa Polisi, hivyo ninaangalia kikubwa ni kipi kinachotisha zaidi ndipo ninatoa taarifa Polisi, lakini iwapo itagundulika kuwa niliudanganya umma kuwa nilitoa taarifa katika kituo cha Polisi wakati sijatoa, niko tayari kwenda jela,
"Lakini pia iwapo itagundulika kuwa Waziri pia ameudanganya umma kuwa sikutoa taarifa Polisi wakati nilitoa, je yuko tayari kujiuzulu wadhifa wake?" alihoji Bw. Mengi.
Kuhusu suala la kumtaja Waziri kijana na msomi aliye katika Wizara nyeti, Bw. Mengi alisema kwa kawaida Mwenyezi Mungu ana nguvu kubwa na za kipekee, hivyo zinaweza kumfanya mtu huyo kujitaja mwenyewe.
"Kwa kawaida Mungu ana nguvu kubwa na za pekee sana, hivyo katika mazingira ya sasa, nguvu hizo zinaweza kumfanya mhusika kujitaja mwenyewe," alisema.
Bw. Mengi alisema ameshindwa kuelewa majukumu ya Waziri Masha katika jambo hili alilosema kupitia TBC1, kwani hajawahi kusikia kama yeye ni Msemaji Mkuu wa Serikali au wa Wizara.
"Kitu nisichokielewa ni majukumu ya Waziri Masha katika suala hili, alikuwa akitoa tamko hilo kama Msemaji Mkuu wa Wizara au Serikali, alikuwa akizungumza kama nani, nauliza hivyo kwani sijui taratibu za Serikali kama yeye ni msemaji wa sehemu hizo.
"Nilizungumzia Waziri kijana wa wizara nyeti, mawaziri vijana wako wengi, yuko Ngeleja (William, 41), Kamala (Deodorus, 40) na yeye Masha (38) hivyo umri wao unashabihiana, sijui atakuwa amezungumza kwa niaba ya vijana wengine ama vipi?," alisisitiza Bw. Mengi.
Bw. Mengi alihoji kuwa iwapo suala la kuripoti Polisi linalomhusu yeye katika Wizara yake ameshindwa kukubaliana nalo, je kuwapo kwa suala la kumfilisi ambalo haliko katika wizara yake, atakuwa tayari kulikubali? Waziri Masha alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu suala la kumpeleka Bw. Mengi mahakamani haraka iwezekanavyo na kumpelekea barua ikimtaka kutoa ushahidi ndani ya siku saba, alisema suala la kumpa siku saba Bw. Mengi si sababu, hivyo angeweza kupeleka ushahidi huo hata jana.
Bw. Masha alisema alishindwa kupeleka barua hiyo jana asubuhi, kutokana na kuwa mkutanoni, hivyo aliahidi mara baada ya kutoka mkutanoni angeipeleka barua hiyo mara moja.
Hata hivyo, hakuweza kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, kutokana na kuwa mkutanoni na Waziri mwenzake wa Burundi.
Awali vyombo vya habari viliripoti kuwa Bw. Mengi anadai kutishiwa kifo na mtu aliyemtaja kuwa ni Waziri kijana katika Serikali ya Rais Kikwete akihusisha vitisho hivyo na msimamo wake wa kukemea ufisadi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari ambao ulifanyika juzi, Mengi alidai kuwa amekuwa akitumiwa ujumbe ambao unavituhumu vyombo vyake vya habari kuwa vimekuwa mstari wa mbele katika kukemea ufisadi jambo ambalo 'waziri kijana' kuwa si jambo zuri kwa sababu linawanyanyasa baadhi ya watu.