Mdunguaji wa Goma

Mdunguaji wa Goma

RIWAYA; MDUNGUAJI WA GOMA.

NA; BAHATI K MWAMBA.

SIMU; 0758573660/0624155629.

SEHEMU YA KUMI


Macho yake yalikuwa yameganda nyuma ya meza iliyokuwa mbele yake. Yaliganda kwa watu watatu ambao walikuwa wamekaa nyuma ya meza ile, wakiwa kimya wakimtizama.

Kilichofanya agande ni, kuona mkoba mweusi ukiwa juu ya meza, huku aliyempa kazi ya kuufuata akiwa amekaa katikati ya watu wengine wawili.

Kwa harakaharaka alishindwa kuelewa; ni kwa nini mtu aliyempa kazi na kumlia pesa nyingi, awe pale tena na mkoba aliouhitaji ukiwa mezani bila kuonekana ukimilikiwa na yeyote miongoni mwa wale watu watatu.

Je, mtu huyo katekwa na wale watu wawili waliomuweka pembeni, ama kuna kitu gani kilikuwa kikiendelea.

Haraka alitaka kufahamu kinachoendelea kupitia lugha ya hisia. Macho yake aliyapeleka usoni kwa mtu aliyempa ile kazi, akiwa na nia ya kuyasoma mawazo yake, iwe ya hofu ama shari.

Alipoona hakuna hisia za hofu kwa mtu yule, haraka alipeleka macho yake kwa mtu aliyekuwa kushoto kwa mwajiri wake, akiwa na lengo la kuona hisia za ubabe na utabe. Hakuishia hapo, alimtizama pia mtu wa mwisho ambae hakuwa amemzingatia tangu awali; napo hakuona hisia alizotarajia wala hakuona lugha ya picha kutoka kwao wote watatu.

Kiufupi, alikutana na watu ambao walimtizama kawaida, ikiwa na maana hakuna baya miongoni mwao.

Ilimshangaza na alibaki wakiwa amesimama na, asijue cha kufanya.

Mkoba mbele yake na mwajiri wake mbele yake.
Je, achukue mkoba ambao ndo ulimpeleka pale, au amchomoe mwajiri wake na kuuacha mkoba? Kipi ni kipi na je, hakuelewa alipoambiwa kuufuata mkoba? Ilikuwa ni mkoba kama mkoba, au ni mkoba ikimaanishwa mtu.

Mawazo lukuki yalipita huku ofisi ikiwa kimya, kama vile hakukuwa na watu ndani yake

Miguu ya Kuku aliamua kufuata utaratibu kama alivyolipwa. Mkono wake ukaufuata mkoba na kuunyanyua, kisha aligeuka na kuanza kutoka ndani ya ofisi ile.

Lakini kabla hajaufikia mlango, sauti ya chuma ikasikika na hakuwa mgeni wa sauti kama zile, alijua ni sauti ya bastola imeondolewa usalama.

Moyo ukamdunda kimdundiko.

‘Tuku..tuku…tuku' Ukazidi kudunda.

Taratibu aligeuka huku mkoba ukiwa kwenye mkono wa kushoto. Macho yake yaliangukia kwenye meza, ambapo aliishia kuona bastola aina ya revolva ikiwa imelazwa mezani huku magazini yake, ikiwa pembeni.

Alihamishia macho yake kwa wale watu watatu, ambao hakujua ni nani kati yao alikuwa amechezea bastola kwa kasi namna ile. Lakini licha ya kutomjua, alielewa ni nini maana ya kuweka bastola mbali na risasi zake.

Alitambu ile ilikuwa ni ishara ya amani na kusalimu amri, huku kukitakiwa kufanyika mazungumzo ya aina yoyote.

“Nakuomba ukae bwa Zuki Gadu.” Alfa'one alimwambia huku akimtazama.

Zuki p.a.k Miguu ya Kuku alikaa kwenye kiti kilichokuwa kando yake, huku macho yake yakitazamana na kundi la Boys Among Men, ambao walivaa suti nyeusi za kupendeza, simu za gharama kubwa na vito mikononi mwao. Uturi wa bei mbaya, huku vichwani wakipaka hina na kufanya nywele zao kuficha mvi, zilizokuwa zimetawala vichwa vyao kwa asilimia kubwa.

“Hatimae mkoba mweusi upo mkononi mwako bwana Zuki.” Aliendelea kusema Alfa huku akimtizama usoni na, alipoona ukimya umetawala aliendelea kuzungumza..

“Malipo yako yatafanyika nusu saa ijayo na naamini utapitia bandarini, kuchukua gari na pikipiki kama ulivyohitaji” Alfa alitua huku bado akiwa anamtizama Miguu ya Kuku.

“Naomba ufungue mkoba huo bwana Zuki Gadu” Alfa alimwambia.

Miguu ya Kuku aliuweka mkoba miguuni mwake, kisha alivuta zipu kubwa na kuishusha hadi alipohakikisha mkoba umebaki wazi, kiasi cha kuweza kuona kilichokuwemo.

Alitoa bahasha ya kaki iliyokuwa imefungwa vizuri na kuiweka juu ya meza. Alipohakikisha hamna kilichokuwa kimesalia kwenye ule mkoba, aliuweka pembeni na kuichukua bahasha. Aliifungua na kutoa kilichikuwamo.

Alikutana na picha sita tu.

Alizitizama moja baada ya nyingine, huku akili yake ikikariri sura alizoziona kwenye picha zile. Alipohakikisha sura zao zimekaa vema kichwani mwake, aligeuza nyuma ya zile picha na kukutana na majina ya wahusika waliokuwa kwenye kila picha.

Picha ya kwanza alikutana na jina la Papaa Deo, picha ya pili alikutana na jina la Swai Makambo, picha ya tatu alikutana na jina la Fredi Mutesa, picha ya nne alikutana na jina la Tatu Banenga, picha ya tano alikutana na jina la Jimmy Kasoki na picha ya sita alikutana na jina la Leti Kamirimana.

Alipohakikisha majina yote yamemkaa vema kichwani, huku kila jina akihakikisha lipo sambamba na sura aliyoikariri kutoka kwenye picha, alizikusanya picha zote na kuzirudisha kwenye bahasha, kisha aliziweka kwenye mkoba mweusi na kuurejesha juu ya meza.

Alisubiri maelekezo mengine kutoka kwa wale jamaa watatu, ambao walikuwa mbele yake.

“Hao jamaa sita uliowaona kwenye hizo picha ni, wakazi wa Jamhuri ya kidemorikrasia ya Congo. Hao wote wanamakazi yao kwenye mji wa Goma, jimbo la Kivu ya kaskazini. Ni watu wenye pesa, wanamiliki magenge ya uhalifu na wananguvu kubwa ndani ya mji wa Goma….” Omega alieleza huku akijaribu kuyapa uzito maneno yake, ili aeleweke kirahisi mbele ya Miguu ya Kuku.

Aliendelea…

“..Watu hao inatakiwa waondoke mmoja mmoja kadri uwezavyo. Ni lazima uwaue na si vinginevyo” Omega alitua maelezo yake, huku akimtizama kwa jicho kavu.

“Kwa kuongeza tu…”Rich alidakia kabla maelezo hayajapoa.

“Kuna mtu hapo anaitwa Papaa Deo, huyo jamaa kabla hujamalizana nae, inakulazimu uingie himayani mwake na uifungue kasiki yake, ambayo iko chumba chake cha kulala. Namba za siri za kasiki hiyo ni 6190. Ndani ya kasiki utakuta viboksi viwili, ambavyo vyote vinauzito wa kilo tanotano, lakini viboksi vingine ambavyo unaweza kuvikuta, haviwezi kuwa na hizo kilo. Kikubwa hakikisha unachukua vyenye huo uzito na viko viwili tu!” Rich alitua.

Ukapita ukimya mfupi, kisha Miguu ya Kuku alipata sauti kwa mara ya kwanza tangu aingie pale ndani.
“Sasa hiyo ni nyongeza au ni kazi nyingine?” Aliuliza huku akiwa anamtizama Rich'one.

“Nayo ni kazi pia.” Rich alijibu.

“Kama ni kazi ina maana nayo itakuwa na malipo tofauti pia”

“Hilo la malipo tulishalijadili hapa na tayari tunajua namna ya kukulipa kwenye hizo kazi mbili.”

“Mimi huwa malipo yangu hayajadiliwi nikiwa sipo, malipo yanajadiliwa nikiwepo na lazima mlipe kiasi ninachohitaji” Alisema Miguu ya Kuku kwa kujiamini, huku akiwaacha Boys among men wakitazamana.

“Aah,nadhani hata majadiliano yetu hayakuwa mabaya bwana Zuki”Alfa aliingilia kwa utulivu, lakini Zuki alimkatisha.

“Huwa naishi kwa misingi na kanuni zangu ambazo, kamwe sijawahi kwenda tofauti na zinavotaka na moja ya kanuni inasema:- ‘Kamwe sitapokea malipo yaliojadiliwa bila kushirikishwa'. Hiyo ni kanuni namba kumi, kati ya kanuni kumi nambili za kazi yangu. Hivyo kifupi sitaki kusikia malipo mlioyajadili, tujadili upya” Zuki Gadu p.a.k Miguu ya Kuku alizidi kushikilia msimamo wake.

Boys among men walitazamana kwa mshangao. Walikuwa wamekutana na mtu mwenye msimamo wake ambao kamwe, hauyumbi.

“Ok! Tujadili malipo kama unavyohitaji” Rich'one aliamua kurahisisha ule ubishani uliotokea.

“Hapo kila kichwa kimoja ni milioni mia” Miguu ya Kuku alisema.
“Hahaa!” Omega alicheka kibabe, kisha aliendelea..

“…Ndiyo maana tulikwambia tumeshajadili malipo yako, si unaona bado unaingia kwenye hesabu zetu!”

“Hesabu zenu zilitaka nichukue milioni mia kwa kila kichwa, ikiwa na maana kuwa mlipanga kunipa milioni mia sita?” Miguu ya Kuku aliuliza kwa upole.

“Hakika kabisa. Milioni mia sita keshi bwana mdogo” Omega alizidi kusititiza.

“Hiyo si bei yangu ndugu zangu”

“Haaa!!” Wazee walishangaa kwa pamoja.

“Ndiyo, kila kichwa ni milioni mia, lakini hapo ni kabla sijaanza kazi. Nikianza kazi na kuifanikisha vema, kila kichwa kitaongezeka bonusi ya milioni ishirini hivyo kila kichwa mtanipa milioni mia moja na ishirini na, kwa ujumla milioni mia saba ishirini.” Miguu ya Kuku alitua maelezo yake.

“Aah wapi! Pesa nyingi sana hiyo, haiwezekani aisee” Rich'one alibwata kwa hasira, huku akisimama na kuilegeza tai yake.

“Milioni mia saba ishirini! Duh, pesa kubwa sana hiyo kijana” Alfa nae aliongeza kushangaa ukubwa wa dau lililotajwa.

“I'm not cheap guys, sifanyi kazi za mia mia kama muuza karanga, nafanya kazi ya pesa kubwa kubwa tu na kama hamuwezi kunipa hiyo pesa, tafuteni mwingine. Wapo wanafanya kazi ya hata milioni ishirini wazee” Miguu ya Kuku aliendelea kuwapa maelezo yenye kujipa uthamani wa kazi yake.
“Sasa wa milioni thelathini ataweza nini?” Omega alimuuliza.

“Sasa kama huhitaji kufanyiwa kazi na majambazi, kubali kulipa pesa ya kutosha ili mamluki kama mimi, wafanye kazi yako. Tofauti na hapo agiza majambazi ya kuiba bank, yakufanyie kazi yako huko Kongo.” Miguu ya Kuku aliendelea kuwapasha.

“Ni kanuni namba tano ya kazi yangu, ambayo inanitaka kila nikua mtu, ninunue gari la bei kubwa na nibaki na pesa ya kula maisha, sasa jiulize kwa hiyo pesa nitanunua gari na kubaki na kiasi gani. Naisimamia kanuni namba tano wakubwa” Aliongeza tena.

Wazee walichoka, kila mmoja alijikuna kichwa kwa utaratibu wake. Lakini kabla mafikirio yao hayajahitimishwa, waliongezwa moto mwingine ili wajikune vizuri mvi zao.

“Na mlisema kuna kuiba viboksi viwili.” Miguu ya Kuku alinyamaza kidogo na kuwatizama wale wazee, ambao walikaa kimya tena kumsikiliza anataka kuongeza jambo gani.

Akaendelea na alilokusudia kulisema..
“Hiyo nayo ni kazi kama kazi nyingine, inaweza kubeba uhai wa mtu asiyehusika, ili mradi nipate kinachotakiwa. Mtaweka mezani milioni mia mbili, jumla itakuwa milioni mia tisa ishirini” Alitua.

“Aaah wapi weweee!! Yaani billioni kasoro senti kadhaa! Aah wewee, si utatufilisi sasa.” Omega alikuja juu huku akiwa ametoa macho, mithili ya mzee aliyesikia, korona ipo kwenye mipapai yake.

“Huwa sifanyi kazi na wabishi na huwa silegezi kamba na sishushi wala kupandisha, maana siuzi nepi mimi” Miguu ya Kuku aliongea huku akisimama kwa nia ya kuondoka, kisha akawageukia…

“Mkumbuke bado nawadai milioni kadhaa za mkoba mweusi, malizieni hizo pesa leo hii. Sitaki ifike saa kumi sijanunua pikipiki na ikifika saa kumi hamjanilipa, nitakuja kuwadai gharama nyingine mlionitumia bila kunambia. Mlinifanya Jana nimuue Kiuno cha nyoka bila malipo. Mkichelewa, nitawadai pesa yake, pia nitawadai pesa ya kuwarahisishia kumuua Tembe za chai mbele yangu. Mi naondoka” Miguu ya kuku aliunguruma kizembe, huku akiweka sasa suti yake na kuanza kupiga hatua za kuiacha ofisi ile ya madini.

Miguu ya Kuku hufanya kazi kwa sheria zake, na hayumbi hata kidogo. Kujiamini ikiwa ni silaha yake kubwa, kufanikisha mambo yake.
.
.
.
.
.
Endelea kuwa nami
 
Dah!! Inaelekea pazuri sana... jamaa anataja pesa kama vile mbegu za karanga...


Cc: mahondaw
 
Dah! Salute Sana kiongozi, kumbe sisi wasomaji tunavyolalamika arosto kumbe Kudo umejipinda nyuma ya keyboard kutuletea burudani ya motomoto. Heshima kwako kiongozi.
 
RIWAYA; MDUNGUAJI WA GOMA.

NA; BAHATI K MWAMBA

SIMU; 0758573660.

SEHEMU YA TANO.



Yeye alitaka awe wa mwisho ili awasake mmoja mmoja kwa kadri alivyoweza.
Lakini kwa kuwa hakujua watu wa aina gani anaowafuata na laiti angelijua, hizo nguvu angelikwenda kuzitumia kujiandaa kwa ajili ya kuchukua mzigo, ghorofa ya tano.

Lakini kwa kuwa ninge huja baada ya kutokea, alijikuta akiunga mfukuzano wa wababe wale aliotoka kuwashuhudia muda mfupi uliopita.

Moto ukawaka kwenye mitaa ya Lumumba na Posta.

Vita ya watu watatu, ikawa zaidi ya vita vya Waryenchoka na waryenchali Tarime, Mara.

****

Wa kwanza kuudaka usafiri alikuwa ni kiuno cha nyoka, aliwahi kuingia kwenye gari ambayo alikuja nayo na kuiacha mita chache, kutoka kwenye jengo la mauzo.

Licha ya hali yake kuwa mbaya, lakini alijitahidi kuwahi kuingia ndani ya gari lake na kuliwasha, kisha kwa fujo aliingia barabarani huku akipiga honi hovyo. Kitendo cha yeye kupiga honi, kilizua taharauki kwa watembea kwa miguu na baadhi ya madereva waungwana. Lakini yeye hakujali, alichojali ni kuwahi kutoka katikati ya mji ili aende kupumzika, kwa kuwa alihisi hali yake ilikuwa inazidi kuwa mbaya. Mtikisiko aliopewa ulikuwa umemkolea kiasi chake.

“Pigo gani lile, sijawahi kuliona abadani!!” Alijisemea huku akilamba kona kwa kasi, kuingia mtaa wa Nkrumah kama anakifuata kituo cha polisi, lakini hakufika kituoni, badala yake alichukua uelekeo wa mtaa wa uhuru.
Njia nzima aliacha taharuki na ajali za hapa na pale, huku akiwa amegonga watu wawili na hakutaka kusimama.

Wakati akiwa anafikiria njia gani rahisi kuifuata, ili aepuke msongamano, macho yake yalitizama side mirror na hakuamini alichokiona.

Nyuma yake kulikuwa na pikipiki aina ya boxer na, juu yake kulikuwa na mtu aliyekuwa amevaa kanzu iliochanwa na baraghashia kichwani.

Mtu yule ndiye aliemfanya akimbie kama jogoo muoga, lakini kukimbiwa hakuridhika na badala yake, aliamua kumfuata nyuma na pikipiki ya kupora aina ya boxer.

Alipagawa na bila kutarajia alijikuta akitoa bomu lingine, kutoka kwenye begi lake huku gari lake likiyumba hovyo.

Hakutaka kupima madhara ya bomu lile, katikati ya msongamano wa watu, bali alitaka kuona maisha yake yanakuwa salama bila uwepo wa kiumbe wa ajabu nyuma yake yake.

Haraka alitoa kichwa chake nje na kurusha bomu lile dogo, kumuelekea hasimu wake ambae alikuwa umbali mfupi na gari lake.

Bomu likakutana na ardhi, mlipuko ukatokea na kufanya taharuki iongezeke zaidi, watu walikimbia bila mpango, huku mwenye nguvu ndiye anaefanikiwa kukimbia katikati ya msongamano, kwa sababu atawasukuma wenzake.

Kasi ya bomu haikuwa sawa na kasi ya pikipiki, hivyo wakati bomu linatua barabarani, tayari pikipiki ilikuwa imeshapita hivyo hakuna madhara yoyote yaliotokea kwa mwendesha pikipiki na ndo kwanza, mfukuzano uliendelea.

Safari yao yenye adha za hapa na pale, hatimae iliwafikisha mtaa wa msimbazi, huku risasi zikianza kurushwa baina ya dereva wa gari na yule wa pikipiki. Hakuna aliyejali uhai wa watu wasio na hatia, bali kila mmoja alitaka kumwangusha mwenzake.

Wa kwanza kugundua kuna kitu kingine cha ziada kwenye msafara wao, alikuwa ni Miguu ya Kuku. Aligeuka nyuma mara moja na kuona Difenda ya polisi ikiwa nyuma yao, huku maaskari wenye baleti nyekundu, wakiwa wameshika vema silaha zao.

“****…!” Lilimtoka tusi zito huku akila kona kuelekea kushoto kwake, kwenye njia ambayo aliamini gari lile la polisi lisingeweza kufika.

Kupotea kwa adui yake nyuma yake, kulimfanya Kiuno cha nyoka apumue kwa ahueni, japo aliamini asingeachwa na yule mtu kirahisi namna ile. Alipanga kubadili usafiri akiingia kwenye mtaa mwingine.
Mara akahisi muungurumo usio wa kawaida nyuma yake.

“Shiit! Pila hilo” Alijisemea kwa uchungu huku akiilani siku hiyo. Kwake ilikuwa bora kumimbizwa na Miguu ya Kuku, lakini si jeshi la polisi na haraka haraka aliwaza maafa walioyaacha mtaani kwa fujo zao.

Lakini ilikuwa ni yeye afe ama awakimbie polisi.

Wakati alipokuwa anaumaliza mtaa wa msimbazi ili aingie kwenye barabara ya mwendokasi, akiwa na nia ya kuvuka apite Regency Medical center, mbele yake mita kama hamsini hivi, kilisimama kiumbe kingine kikiwa kwenye pikipiki kubwa aina ya Baja. Kiumbe kile kilikuwa na bastola mkononi mwake na kilikuwa ni kiumbe kilekile alichopamiana nacho, kwenye jengo la mauzo ghorofa ya sita.

Kilikuwa ni kiumbe kilekile alichokichapa konde kifuani, kisha akazua kizaazaa kwenye lile jengo.

“Leo siku gani kwangu!!?” Aliropoka kwa sauti, huku akifungua mlango wa gari lake, kisha alijiachia na kuruka nje kwa ufundi mkubwa na kuliacha gari lake likichakaa risasi za Tembe za chai, ambae alishambulia akiwa hajaliona gari la polisi nyuma ya gari la kiuno cha nyoka.

Wakati akitaka kumlenga kiuno cha nyoka baada ya, kuona ametoka kwenye gari; ghafla alishangaa bega lake likikoswa kidogo na risasi za polisi na, hapo ndipo alipogundua kulikuwa na polisi walioingilia songombingo lile.

“Wapuuzi hawa!” Alijisemea huku akiondoa pikipiki yake kwa kasi. Lakini hakwenda mbali, bado alikuwa na jambo lake pale.

Polisi walisimamisha gari lao kwa kasi, macho yao yakilishuhudia gari la mtuhumiwa wao likila mweleka mzito, baada ya dereva wake kujitosa nje kama mpiga mbizi.

Haraka haraka walimfuata pale alipokuwa amedondokea na kujaribu kuona kama bado, anapumua.

Kiuno cha nyoka alikuwa mzima, japo alikuwa na majeraha ya hapa na pale.

Polisi na wao waliamua kuliweka eneo lile kwenye ulinzi mkali, huku bunduki zao zikiwa tayari kwa lolote.

Kiuno cha nyoka alikuwa amekamatika bila kupenda na, taratibu walimuinua huku tayari pingu zikiwa mikononi mwake na walianza kupiga nae hatua, kuelekea kwenye karandinga.

Licha ya ulinzi kuwa mkali na bunduki za maofisa zikiwa tayari kupururua kichwa cha mwendawazimu yeyote, lakikni watu wawili walikuwa wamesimama umbali wa mita mia moja, wakitizama namna Kiuno cha nyoka alivyokuwa akichukuliwa. Kila mmoja alikuwa akiwaza lake, huku maamuzi fulani yakiwapita kwa kasi.

Watu wale licha ya kuwa umbali sawa na wakiwaza sawa, lakini hawakuwa wakionana kwa maana kila mmoja alikuwa amesimama upande wake.

“Yule bwege anaweza kunichoma kwa polisi, ameniona sura yangu na polisi hawawezi kushindwa kunichora kama nilivyo.” Miguu ya Kuku aliwaza huku akiwasha pikipiki, aliokuwa amempora mpita njia maeneo ya jengo la mauzo.

Hesabu zake alizipiga akiwa tayari ameshaingia kwenye njia isioruhusiwa. Alikuwa ameingia kwenye njia ya magari ya mwendokasi.

Kitendo cha yeye kuingia kwenye njia isiyorasmi, kisha kuendesha kwa kasi kuwafuata maaskari ambao walikuwa na mtuhumiwa; kiliwashitua maafande, ambao bila kuuliza silaha zao zilianza kutema risasi kwa fujo.

Lakini hawakujua wanaemtupia risasi tayari alikuwa ameshawaona na kuwapigia hesabu, hivyo alijua mwendo wake wa pikipiki ulikuwa unawaomdoa kwenye shabaha bila kupenda na, tayari alishaona ni yupi ambae alikuwa na uwezo wa kumpiga risasi yenye madhara kwenye mwili wake.

Hesabu zake zilimwangukia dereva wa karandinga, ambae hata hivyo alikuwa na bastola ambayo alikuwa ameiweka kiunoni, hivyo ilihitaji sekunde thelathini kuitoa na kumchapa risasi, sekunde ambazo tayari yeye alikuwa ameshawakaribia maafande, kisha akatoa bastola yake kwa utaalamu wa hali ya juu na, kusimama juu ya pikipiki, kisha akaachia risasi mbili ambazo zilienda kutua kwenye kisogo cha kiuno cha nyoka, ambae maafande walishindwa kukinga vema baada ya kuanzisha varangati na mtu ambae alivaa baraghashia na kufunika uso wake kwa kitambaa, na kuacha sehemu ya macho tu.

Alipohakikisha risasi zake zimefanya kazi alioitarajia, haraka aliidaka pikipiki ambayo ilianza kupoteza mwelekeo, kisha kwa kitendo ambacho hakikutarajiwa, alienda kukunja kona mita sita kutoka ilipokuwa karandinga, kisha alitimka kama mwizi wa mafuta sheli.

Aliondoka na kuacha risasi nyuma zikimsindikiza, huku risasi moja ikifanikiwa kuingia kwenye nyama za mkono wake wa kushoto.

Kitu kimoja ambacho siku zote kilimpa ushindi Miguu ya Kuku ni, uwezo wake wa kupiga hesabu na kuutumia udhaifu wa wapinzani wake.

Alifanikiwa kuwatoka polisi bila majereha makubwa, kwa sababu alitumia kanuni yake ambayo aliipa namba; ‘kanuni namba sita'.

Kanuni hii ilisema;- “Tumia udhaifu wa hofu ya adui, kwa kuwa kila kiumbe mwenye damu, anayohofu. Hofu ya kifo”

Na kanuni hiyo ndiyo alioitumia kuwavamia polisi na kumuua mtuhumiwa wao, huku risasi zao zikikosa shabaha sahihi, kwa sababu ndani ya dakika moja, hofu ilitawala akili zao na wakati hofu inaondoka na akili ya kupambana inawaingia, tayari mvamizi alishatokomea huku akiua mtuhumiwa mikononi mwao.

Kitu kizuri ni kuwa, hakuna polisi aliyejeruhiwa wala kuawa, kwa sababu mvamizi hakuwa na lengo hilo.

Wakati Miguu ya kukua anafanya yaliondani ya uwezo wake, Tembe za chai alikuwa amepigwa na butwaa huku akiwa na pikipiki yake, akiwa hajui cha kufanya.

Ni kweli alikuwa na nia ya kumuua kiuno cha nyoka, lakini uwepo wa polisi ilikuwa kikwazo na, tena polisi walikuwa na silaha na yeye hakutaka kujeruhiwa kizembe.

Yeye akiwa anafikiria, ndipo alipomuana Miguu ya kuku akifanya vitu vyake kwa uwezo mkubwa, huku akitumia pikipiki aina ya boxer. Pikipiki ambayo haikuwa na uwezo mkubwa, kama aliokuwa nayo yeye.

Ilimshangaza. Tena ilimshangaza zaidi alipoona jamaa akiondoka, bila risasi za polisi kumwangusha bali, ni yeye ambae alimwacha kiuno cha nyoka akiwa hana uhai, kwenye mikono ya polisi.

“Duh!!” Alishangaa huku akiwasha pikipiki yake na kuanza kumfuatilia Miguu ya Kuku.

Tembe za chai aliamini siku zote ni yeye aliestahili kupambana na watu wa aina ile. Aliamua kumfuatilia Miguu ya Kuku.

Kitu ambacho hakujua ni kuwa, Miguu ya Kuku nyayo zake hazifuatwi abadani.

Aliufuata moto
.

.

.

.

ENDELEA KUWA NAMI
Moto umezid
 
Back
Top Bottom