Mdunguaji wa Goma

RIWAYA; MDUNGUAJI WA GOMA.

NA; BAHATI K MWAMBA

SIMU; 0758573660.

SEHEMU YA TANO.



Yeye alitaka awe wa mwisho ili awasake mmoja mmoja kwa kadri alivyoweza.
Lakini kwa kuwa hakujua watu wa aina gani anaowafuata na laiti angelijua, hizo nguvu angelikwenda kuzitumia kujiandaa kwa ajili ya kuchukua mzigo, ghorofa ya tano.

Lakini kwa kuwa ninge huja baada ya kutokea, alijikuta akiunga mfukuzano wa wababe wale aliotoka kuwashuhudia muda mfupi uliopita.

Moto ukawaka kwenye mitaa ya Lumumba na Posta.

Vita ya watu watatu, ikawa zaidi ya vita vya Waryenchoka na waryenchali Tarime, Mara.

****

Wa kwanza kuudaka usafiri alikuwa ni kiuno cha nyoka, aliwahi kuingia kwenye gari ambayo alikuja nayo na kuiacha mita chache, kutoka kwenye jengo la mauzo.

Licha ya hali yake kuwa mbaya, lakini alijitahidi kuwahi kuingia ndani ya gari lake na kuliwasha, kisha kwa fujo aliingia barabarani huku akipiga honi hovyo. Kitendo cha yeye kupiga honi, kilizua taharauki kwa watembea kwa miguu na baadhi ya madereva waungwana. Lakini yeye hakujali, alichojali ni kuwahi kutoka katikati ya mji ili aende kupumzika, kwa kuwa alihisi hali yake ilikuwa inazidi kuwa mbaya. Mtikisiko aliopewa ulikuwa umemkolea kiasi chake.

“Pigo gani lile, sijawahi kuliona abadani!!” Alijisemea huku akilamba kona kwa kasi, kuingia mtaa wa Nkrumah kama anakifuata kituo cha polisi, lakini hakufika kituoni, badala yake alichukua uelekeo wa mtaa wa uhuru.
Njia nzima aliacha taharuki na ajali za hapa na pale, huku akiwa amegonga watu wawili na hakutaka kusimama.

Wakati akiwa anafikiria njia gani rahisi kuifuata, ili aepuke msongamano, macho yake yalitizama side mirror na hakuamini alichokiona.

Nyuma yake kulikuwa na pikipiki aina ya boxer na, juu yake kulikuwa na mtu aliyekuwa amevaa kanzu iliochanwa na baraghashia kichwani.

Mtu yule ndiye aliemfanya akimbie kama jogoo muoga, lakini kukimbiwa hakuridhika na badala yake, aliamua kumfuata nyuma na pikipiki ya kupora aina ya boxer.

Alipagawa na bila kutarajia alijikuta akitoa bomu lingine, kutoka kwenye begi lake huku gari lake likiyumba hovyo.

Hakutaka kupima madhara ya bomu lile, katikati ya msongamano wa watu, bali alitaka kuona maisha yake yanakuwa salama bila uwepo wa kiumbe wa ajabu nyuma yake yake.

Haraka alitoa kichwa chake nje na kurusha bomu lile dogo, kumuelekea hasimu wake ambae alikuwa umbali mfupi na gari lake.

Bomu likakutana na ardhi, mlipuko ukatokea na kufanya taharuki iongezeke zaidi, watu walikimbia bila mpango, huku mwenye nguvu ndiye anaefanikiwa kukimbia katikati ya msongamano, kwa sababu atawasukuma wenzake.

Kasi ya bomu haikuwa sawa na kasi ya pikipiki, hivyo wakati bomu linatua barabarani, tayari pikipiki ilikuwa imeshapita hivyo hakuna madhara yoyote yaliotokea kwa mwendesha pikipiki na ndo kwanza, mfukuzano uliendelea.

Safari yao yenye adha za hapa na pale, hatimae iliwafikisha mtaa wa msimbazi, huku risasi zikianza kurushwa baina ya dereva wa gari na yule wa pikipiki. Hakuna aliyejali uhai wa watu wasio na hatia, bali kila mmoja alitaka kumwangusha mwenzake.

Wa kwanza kugundua kuna kitu kingine cha ziada kwenye msafara wao, alikuwa ni Miguu ya Kuku. Aligeuka nyuma mara moja na kuona Difenda ya polisi ikiwa nyuma yao, huku maaskari wenye baleti nyekundu, wakiwa wameshika vema silaha zao.

“https://jamii.app/JFUserGuide…!” Lilimtoka tusi zito huku akila kona kuelekea kushoto kwake, kwenye njia ambayo aliamini gari lile la polisi lisingeweza kufika.

Kupotea kwa adui yake nyuma yake, kulimfanya Kiuno cha nyoka apumue kwa ahueni, japo aliamini asingeachwa na yule mtu kirahisi namna ile. Alipanga kubadili usafiri akiingia kwenye mtaa mwingine.
Mara akahisi muungurumo usio wa kawaida nyuma yake.

“Shiit! Pila hilo” Alijisemea kwa uchungu huku akiilani siku hiyo. Kwake ilikuwa bora kumimbizwa na Miguu ya Kuku, lakini si jeshi la polisi na haraka haraka aliwaza maafa walioyaacha mtaani kwa fujo zao.

Lakini ilikuwa ni yeye afe ama awakimbie polisi.

Wakati alipokuwa anaumaliza mtaa wa msimbazi ili aingie kwenye barabara ya mwendokasi, akiwa na nia ya kuvuka apite Regency Medical center, mbele yake mita kama hamsini hivi, kilisimama kiumbe kingine kikiwa kwenye pikipiki kubwa aina ya Baja. Kiumbe kile kilikuwa na bastola mkononi mwake na kilikuwa ni kiumbe kilekile alichopamiana nacho, kwenye jengo la mauzo ghorofa ya sita.

Kilikuwa ni kiumbe kilekile alichokichapa konde kifuani, kisha akazua kizaazaa kwenye lile jengo.

“Leo siku gani kwangu!!?” Aliropoka kwa sauti, huku akifungua mlango wa gari lake, kisha alijiachia na kuruka nje kwa ufundi mkubwa na kuliacha gari lake likichakaa risasi za Tembe za chai, ambae alishambulia akiwa hajaliona gari la polisi nyuma ya gari la kiuno cha nyoka.

Wakati akitaka kumlenga kiuno cha nyoka baada ya, kuona ametoka kwenye gari; ghafla alishangaa bega lake likikoswa kidogo na risasi za polisi na, hapo ndipo alipogundua kulikuwa na polisi walioingilia songombingo lile.

“Wapuuzi hawa!” Alijisemea huku akiondoa pikipiki yake kwa kasi. Lakini hakwenda mbali, bado alikuwa na jambo lake pale.

Polisi walisimamisha gari lao kwa kasi, macho yao yakilishuhudia gari la mtuhumiwa wao likila mweleka mzito, baada ya dereva wake kujitosa nje kama mpiga mbizi.

Haraka haraka walimfuata pale alipokuwa amedondokea na kujaribu kuona kama bado, anapumua.

Kiuno cha nyoka alikuwa mzima, japo alikuwa na majeraha ya hapa na pale.

Polisi na wao waliamua kuliweka eneo lile kwenye ulinzi mkali, huku bunduki zao zikiwa tayari kwa lolote.

Kiuno cha nyoka alikuwa amekamatika bila kupenda na, taratibu walimuinua huku tayari pingu zikiwa mikononi mwake na walianza kupiga nae hatua, kuelekea kwenye karandinga.

Licha ya ulinzi kuwa mkali na bunduki za maofisa zikiwa tayari kupururua kichwa cha mwendawazimu yeyote, lakikni watu wawili walikuwa wamesimama umbali wa mita mia moja, wakitizama namna Kiuno cha nyoka alivyokuwa akichukuliwa. Kila mmoja alikuwa akiwaza lake, huku maamuzi fulani yakiwapita kwa kasi.

Watu wale licha ya kuwa umbali sawa na wakiwaza sawa, lakini hawakuwa wakionana kwa maana kila mmoja alikuwa amesimama upande wake.

“Yule bwege anaweza kunichoma kwa polisi, ameniona sura yangu na polisi hawawezi kushindwa kunichora kama nilivyo.” Miguu ya Kuku aliwaza huku akiwasha pikipiki, aliokuwa amempora mpita njia maeneo ya jengo la mauzo.

Hesabu zake alizipiga akiwa tayari ameshaingia kwenye njia isioruhusiwa. Alikuwa ameingia kwenye njia ya magari ya mwendokasi.

Kitendo cha yeye kuingia kwenye njia isiyorasmi, kisha kuendesha kwa kasi kuwafuata maaskari ambao walikuwa na mtuhumiwa; kiliwashitua maafande, ambao bila kuuliza silaha zao zilianza kutema risasi kwa fujo.

Lakini hawakujua wanaemtupia risasi tayari alikuwa ameshawaona na kuwapigia hesabu, hivyo alijua mwendo wake wa pikipiki ulikuwa unawaomdoa kwenye shabaha bila kupenda na, tayari alishaona ni yupi ambae alikuwa na uwezo wa kumpiga risasi yenye madhara kwenye mwili wake.

Hesabu zake zilimwangukia dereva wa karandinga, ambae hata hivyo alikuwa na bastola ambayo alikuwa ameiweka kiunoni, hivyo ilihitaji sekunde thelathini kuitoa na kumchapa risasi, sekunde ambazo tayari yeye alikuwa ameshawakaribia maafande, kisha akatoa bastola yake kwa utaalamu wa hali ya juu na, kusimama juu ya pikipiki, kisha akaachia risasi mbili ambazo zilienda kutua kwenye kisogo cha kiuno cha nyoka, ambae maafande walishindwa kukinga vema baada ya kuanzisha varangati na mtu ambae alivaa baraghashia na kufunika uso wake kwa kitambaa, na kuacha sehemu ya macho tu.

Alipohakikisha risasi zake zimefanya kazi alioitarajia, haraka aliidaka pikipiki ambayo ilianza kupoteza mwelekeo, kisha kwa kitendo ambacho hakikutarajiwa, alienda kukunja kona mita sita kutoka ilipokuwa karandinga, kisha alitimka kama mwizi wa mafuta sheli.

Aliondoka na kuacha risasi nyuma zikimsindikiza, huku risasi moja ikifanikiwa kuingia kwenye nyama za mkono wake wa kushoto.

Kitu kimoja ambacho siku zote kilimpa ushindi Miguu ya Kuku ni, uwezo wake wa kupiga hesabu na kuutumia udhaifu wa wapinzani wake.

Alifanikiwa kuwatoka polisi bila majereha makubwa, kwa sababu alitumia kanuni yake ambayo aliipa namba; ‘kanuni namba sita'.

Kanuni hii ilisema;- “Tumia udhaifu wa hofu ya adui, kwa kuwa kila kiumbe mwenye damu, anayohofu. Hofu ya kifo”

Na kanuni hiyo ndiyo alioitumia kuwavamia polisi na kumuua mtuhumiwa wao, huku risasi zao zikikosa shabaha sahihi, kwa sababu ndani ya dakika moja, hofu ilitawala akili zao na wakati hofu inaondoka na akili ya kupambana inawaingia, tayari mvamizi alishatokomea huku akiua mtuhumiwa mikononi mwao.

Kitu kizuri ni kuwa, hakuna polisi aliyejeruhiwa wala kuawa, kwa sababu mvamizi hakuwa na lengo hilo.

Wakati Miguu ya kukua anafanya yaliondani ya uwezo wake, Tembe za chai alikuwa amepigwa na butwaa huku akiwa na pikipiki yake, akiwa hajui cha kufanya.

Ni kweli alikuwa na nia ya kumuua kiuno cha nyoka, lakini uwepo wa polisi ilikuwa kikwazo na, tena polisi walikuwa na silaha na yeye hakutaka kujeruhiwa kizembe.

Yeye akiwa anafikiria, ndipo alipomuana Miguu ya kuku akifanya vitu vyake kwa uwezo mkubwa, huku akitumia pikipiki aina ya boxer. Pikipiki ambayo haikuwa na uwezo mkubwa, kama aliokuwa nayo yeye.

Ilimshangaza. Tena ilimshangaza zaidi alipoona jamaa akiondoka, bila risasi za polisi kumwangusha bali, ni yeye ambae alimwacha kiuno cha nyoka akiwa hana uhai, kwenye mikono ya polisi.

“Duh!!” Alishangaa huku akiwasha pikipiki yake na kuanza kumfuatilia Miguu ya Kuku.

Tembe za chai aliamini siku zote ni yeye aliestahili kupambana na watu wa aina ile. Aliamua kumfuatilia Miguu ya Kuku.

Kitu ambacho hakujua ni kuwa, Miguu ya Kuku nyayo zake hazifuatwi abadani.

Aliufuata moto
.

.

.

.

ENDELEA KUWA NAMI
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom