zabron k
JF-Expert Member
- Nov 11, 2015
- 917
- 1,043
Shukran mkuuRIWAYA; MDUNGUAJI WA GOMA.
NA; BAHATI K MWAMBA.
SIMU; 0758573660.
SEHEMU YA TATU.
Wakati yeye akidhani ni yeye mwenye akili za kukagua mazingira kabla ya kazi, alijidanganya.
Kulikuwa na mtu mwingine nae alikuwa na kazi kama yake na, yeye alipenda kukagua mazingira kabla ya kazi na, jioni hiyo na yeye alikuwa anaenda kwenye jengo la mauzo kuweka mambo yake sawa.
Wote wawili walijikuta wakianza kazi kabla ya siku iliotakiwa. Walianza mtafutano kabla ya wakati.
Mtu huyo alikuwa ni mtaalamu wa mapigano na kuruka viunzi. Kujikunja na kujikunjua kwa kasi, kulifanya apachikwe jina la Kiuno cha nyoka, badala ya jina lake Said Magabe.
Jengo la mauzo lilijuta kuwafahamu viumbe wale kwa siku hiyo.
Moto ukawaka!
****
Jengo la mauzo lilikuwa katikati ya mji, ambapo kulikuwa na changanyikeni nyingi ya watu. Magari ya abiria na binafsi, yalipishana kwa mwendo was taratibu sana, kwa sababu ya wingi wa watu na shughuli zao.
Watu nao walikuwa wanapishana na magari hayo kwa umakini wa kawaida, kwa kuwa walijua wingi wao, uliwafanya madereva wawe makini kupita kiasi.
Miongoni mwa watu waliokuwa wakipishana na magari, alikuwa ni Miguu ya Kuku ambae macho yake yalikuwa makini kutazama lango la jengo alilokuwa anaelekea.
Alimtizama kila mtu aliyekuwa anaingia na kutoka kwenye jengo lile lenye urefu wa ghorofa nane. Miguu yake miembamba iliyofichwa na kanzu yake, ilizidi kulisogelea jengo lile bila kujali kuzongwazongwa na watu, waliokuwa na haraka zao.
Miguu yake ilimfikisha kwenye mlango wa vioo, ambao ulikuwa na kibao kilichoandikwa; ‘Push’.
Haraka haraka alitupia macho yake kila pande ya jengo lile na, alifanikiwa kuona njia upande wake wa mashariki. Njia ile ilikuwa inapitisha magari kuelekea mwenye maegesho, ambayo yalikuwa chini ya jengo lile. Kulikuwa na walinzi wawili wa kampuni fulani, ambao walilinda njia hiyo huku mmoja akiwa na kalamu na karatasi za risiti na, mwenzake akiwa na bunduki aina ya pumpaction 2p. Bunduki aina ya gobole, japo iliundwa kisasa zaidi na kupewa jina hilo.
Aliachana nao.
Mkono wake wa kulia ukataka kuusukuma mlango ule, lakini kuna mtu mwingine aliuvuta kwa ndani, ili apate nafasi ya kutoka ndani ya jengo lile lilosifika kwa uuzaji wa simu za aina zote; kwa bei ya jumla ama rejareja.
Alipishana na mtu yule ambae yalikuwa anatoka, na yeye akiingia.
Alipokelewa na hewa safi ilioletwa na viyoyozi, huku akishuhudia idadi kubwa ya watu ambao walikuwa wakichagua simu, kwenye maduka sita yaliokuwa pale ground.
Alivuta hatua zake taratibu akiwa kama ni mtu ambae anachagua duka la kufuata, lakini lengo lake lilikuwa ni kuona upande ambao ulikuwa na kambarau, ama mlango wa ngazi za kuelekea kwenye ghorofa za juu.
Macho yake yaliokuwa yanazurura mithili ya pimbi kwenye vilima vya mawe, yalifanikiwa kuona sehemu ya kambarau na sehemu ya ngazi za kawaida. Haraka haraka alipiga hatua na kuelekea ilipokuwa kambarau, alibonyeza kitufe cha kuruhusu kuingia, aliingia na kubonyeza kitufe namba nane.
Kambarau ilianza kupanda juu kuelekea mwisho wa jengo na muda wote Miguu ya kuku alikuwa makini na saa yake mkononi. Hadi anafika ghorofa ya mwisho, alikuwa amehesabu sekunde arobaini na tano tu na, hiyo ilikuwa ni kwa sababu haikusimama kuchukua ama kushusha mtu, alikuwa ni peke yake aliyeiongoza kuelekea mwisho wa jengo.
Alitoka na kuelekea upande wa ngazi, alichungulia chini na hakuona mtu, alichungulia upande wa juu na kuona ngazi zilikuwa zinaelekea juu, alizifuata.
Alitumia dakika moja kutokea juu ya jengo. Huko aliishia kuona mji wa Dar as laam kwa uzuri wake. Aliona majengo marefu yalivyolipendezesha jiji, aliona kwa mbali bahari ikiwa imebeba meli kubwa na ndogo, huku matanga ya mashua za wavuvi yakionekana kwa mbali, mithili ya nyota angani.
Miguu ya Kuku hakupanda huko juu kushangaa uzuri wa jiji la Dar es laam, bali alipanda huko juu kufanya vitu viwili.
Alitaka kujua ukubwa wa jengo lile kwa kusoma vipimo vya mzunguko wa huko juu na vipimo vile alivihesabu kwa hatua za miguu yake. Alipohakikisha amehesabu vema upana na urefu wa paa la jengo lile, alitulia na kuanza kupiga hesabu zake. Hesabu alizokuwa akipiga, ni upana wa kila ofisi ndani ya lile jengo na ilihitaji hatua zake ngapi,ili kuhama kibaraza kimoja kwenda kingine. Alipomaliza kukadiria, akabaki na kazi moja tu; kuhakikisha anatembelea moja ya ofisi zilizoko kwenye lile jengo na alichagua kutembelea ofisi itakayokuwa kwenye ghorofa ya nne, kwa kuwa alitakiwa kuchukua mzigo ghorofa ya tano.
Lakini kabla hajaenda kuitembelea ofisi hiyo, alitakiwa kumaliza jambo la pili ambalo lilikuwa limmfanya afike kule juu.
Kwa kuwa alijua lile jengo lilikuwa mtaa gani, alihitaji kuona mtaa wa pili ambao kulikuwa na makao makuu ya jeshi la polisi. Kupanda kule juu, kulimfanya autazame vema mtaa ule na aliangazia zaidi kwenye makao makuu ya jeshi la polisi.
Alitumia dakika tatu na sekunde kadhaa kutazama majengo ya makao makuu ya jeshi la polisi, kisha alitizama barabara zilizokuwa zinapitika kirahisi kutokea kwenye mtaa ule, kuelekea maeneo ya makao makuu ya jeshi. Wakati alipokuwa anatizama, bahati nzuri aliona kuna gari moja lilikuwa inatoka karibu na jengo la mauzo, kuelekea mtaa ambao kulikuwa na makao makuu ya jeshi. Alianza kuhesabu dakika za mwendo wa lile gari, hadi kufika mtaa uliokuwa na ofisi za jeshi la polisi.
Wakati macho yake yakiwa kwenye lile gari ambalo lilikuwa linatembea taratibu kwa sababu ya msongamano wa watu, huku akiwa amelikadiria mshale wa kasi wa lile gari, kuwa kwenye namba ishirini; Mara nyuma yake alisikia vishindo vya mtu, ambae ni kama alitua kutoka angani.
Masikio yake yanauwezo wa kutofautisha vishindo vya viumbe hai zaidi ya thelathini, hivyo hakupata shaka kujua vishindo vya kiumbe kilichodondoka nyuma yake.
Taratibu alielekeza macho yake juu, kuona kama kulikuwa na ndege ama helikopita yoyote iliyopita juu.
Ajabu hakuona wala kusikia kelele za miungurumo yoyote kutokea juu.
“Kiumbe gani anaepaa na kutua kwa vishindo vya binaadamu!” Aliwaza huku akianza kugeuka taratibu bila kuwa haraka yoyote.
Naam, macho yake yalikutana na binadamu akimtizama bila kupepesa macho. Binadamu ambae alikuwa ni mrefu na mpana wa mwili, huku akionekana kutozingatia mazoezi kwa sababu, nyama za mikono yake na kifua chake, havikuonekana kupitia kashkashi yoyote ya mazoezi.
Binadamu yule alikuwa ametota maji mwili mzima, huku mgongoni mwake akiwa amebeba kibegi, ambacho kilionekana kuwa na mzigo wa gram chini ya mia sita.
Macho ya Miguu ya Kuku yalimtizama mtu yule kwa umakini, kisha aliamua kutazama nyuma ya mtu yule na, hapo aliweza kuona tank la maji. Tank lile lilikuwa la Lita elfu moja.
“Ina maana mtu huyu katoka kwenye hilo simtank!?” Alijiuliza huku akishangaa peke yake.
Wakati akiendelea kumtazama, kwa haraka haraka alijaribu kupiga hesabu za dakika alizokaa kule juu, ambapo ilikuwa ni zaidi ya dakika saba na, muda wote huo ilimaanisha huyo mtu alikuwa ndani ya hilo tank.
“Inashangaza!” Alijisemea tena huku mara hii akigeuza shingo yake na kuitizama ile gari, ambayo ilikuwa inakaribia kufika usawa wa makao makuu ya jeshi la polisi. Aliondoa macho yake huko na kuitizama saa yake, ambapo aligundua imetumia dakika tano pekee, ikiwa kwenye mwendo wa kawaida sana.
Alirudi kumtizama yule bwana ambae muda wote alikuwa hajasema lolote zaidi ya kumwangalia tu.
“Pole na kazi fundi” Miguu ya Kuku alimwambia yule bwana.
“Wewe ni mhusika hapa?” aliuliza mtu yule kwa sauti ya kukwaruza.
“Napunga tu upepo bwana fundi” Miguu ya Kuku alijibu.
Bwana yule hakujibu kitu, alipiga hatua zake na kuelekea kwenye ngazi na kushuka chini.
Miondoko na macho ya yule mtu, yalimtisha Miguu ya Kuku, pia yalimpa tahadhari kubwa.
“Huyu sio mtu wa kawaida. Dakika saba ndani ya maji!” Alijiwazia huku akirudi kutazama kule kwenye ofisi za polisi.
Alianza kupiga hesabu zake kuhusu mwendo kasi wa magari ya jeshi la polisi, kuwahi kwenye jengo la mauzo baada ya tafrani kutokea.
“Kama mshale wa mwendo uko kwenye namba ishirini na, ametumia dakika tano, basi polisi kwenye mwendo wa dharura watatumia dakika moja na sekunde thelathini, wakiwa kwenye namba hamsini. Sekunde thelathini ni zile kona mbili tatu.” Aliwaza huku bado macho yake yakitizama barabara zilizotoka kwenye kituo cha polisi, kuelekea kwenye jengo la mauzo.
“Lakini polisi wetu huwa wanatumia dakika kumi hadi kumi na tano, kujiandaa kabla hawajaanza safari ya dharura. Dakika hizo hutumia kuitana, kubeba silaha na kupeana majukumu. Hivyo ili wafike kwenye hili jengo, inawahitaji watumie dakika ishirini pekee, japo hata kwa miguu wanaweza kufika ndani ya dakika nane na wakikimbia ni dakika tano. Lakini wakisikia risasi ni lazima waje na bunduki na magari.” Aliwaza tena huku alianza kuondoka na kuelekea chini, akiwa na nia ya kutumia ngazi kushuka chini.
Alitaka atumie ngazi ili ajue muda atakaotumia endapo itamlazimu kuzitumia.
Alipofika ghorofa ya saba, aligundua ofisi za kule juu wakati huo zilikuwa zimefungwa, hivyo kupelekea kuwe na ukimya wa kutisha.
Wakati anakaribia kufika ghorofa ya sita, masikio yake yalisikia vishindo vya mtu mwingine akipanda ngazi na, alipojaribu kusikiliza, aligundua mtu yule alikuwa anapanda ngazi kwa kasi kubwa na upandaji haukuwa wa kawaida.
Haraka na yeye aliziruka ngazi na kudondokea kwenye kibaraza cha ghorofa ya sita, kisha alichumpa na kwenda kujibanza kwenye korido ya moja ya ofisi zilizokuwa pale, kisha alitulia.
Vitendo vyake vilichukua sekunde mbili tu, kukamilisha mpango wake.
Sekunde tano baadae, alishuhudia mtu akipita kwa kasi kubwa, kuelekea ghorofa za juu. Mtu yule alikuwa ni yule aliemuona akiwa ametota maji.
“Baboon!” Alijisemea kivivu.
Akili yake ilimpa tahadhari, mwili wake nao ukakubali kuipokea tahadhari. Sekunde mbili baadae, kisu kilikuwa mkononi mwake na kwa kasi ya ajabu, aliichana kanzu yake katikati ya miguu, kisha akajifunga na kumfanya aonekane kama amevaa vazi la wahindi, jamii ya uddhu.
Lakini yeye pale alikuwa ametengeneza suruali kwa ajili ya dharura aliohitaji kukabiliana nayo.
Alirejesha kisu chake sehemu alipokitoa, kisha aliingiza mkono wa kushoto kwenye mfuko wa kanzu yake na alipoutoa, ilikuwa umeshika kifuko cha karanga kavu. Alikipasua kifuko kile, kisha alitoa karanga chache na kuzitupia mdomoni na, zilizosalia mkononi alizihesabu kwa idadi.
Zilikuwa karanga sita pekee, karanga zile alizitia kwenye mfuko wake wa kulia kisha akakitupa kifuko cha karanga, kikiwa na karanga zake, huku yeye akisalia na zile karanga sita mfukoni na zile za mdomoni akizimeza baada ya kuzitafuna.
Akapiga hatua ndefu kuelekea kwenye kibaraza cha ile ghorofa ya sita, ili apande ngazi kuelekea juu akutane na yule mbabe ambae alikuwa ameelekea huko.
Akili yake ilimwambia mbabe yule alikuwa amerudi kule juu kumuua, hilo hakutaka mbabe yule wa kukaa ndani ya maji, alifurahie.
Wakati mguu wake unakanyaga kwenye kibaraza, huku mkono wake ukijiandaa kudaka chuma cha kujishikiza ili kupanda ngazi, macho yake yalishuhudia kivulia kikija kwa kasi pale alipo.
Hakuzubaa.
Haraka nae alijivuta nyuma hatua moja, huku akimshuhudia yule jamaa akitua chini kama mzimu, baada ya kuruka kutokea kwenye kibaraza cha ghorofa ya saba, ikiwa na maana alitumia zile bomba kuserereka, kisha kujiachia na kutua ghorofa ya sita.
Macho ya Miguu ya Kuku yaliushuhudia mwili mkubwa, ukifanya maajabu.
Walitazamana bila kusemeshana.
Mchapo ukapangwa.
Wakati wao wakidhani walikuwa peke yao kwenye ofisi zilizokuwa ghorofa ya sita, walikosea. Kulikuwa na kiumbe mwingine ambae alikuwa kwenye lile jengo muda mrefu kabla yao, na alikuwa palepale kwenye ghorofa ya sita akiwa amejibanza akiwachora.
Huyu alikuwa ni Tembe za chai, mbabe wa babe.
Kumekuchwa jengo la Mauzo
.
.
.
.
Endelea kuwa nami
nyingine SAA ngapi??Kila siku