Hongera na kila la heri Ndugu Mnyika!!
Another feather in your cap!
Mnyika Mwenyekiti IYDU
na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IYDU).
Taarifa hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Erasto Tumbo, kwenye tovuti ya chama hicho jana.
Tumbo amesema Mnyika amechaguliwa katika nafasi hiyo kwenye uchaguzi uliofanyika wakati wa mkutano wa baraza la umoja huo nchini Uingereza mwanzoni mwa mwezi Desemba, mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi huo, Mnyika alikuwa mgombea pekee kutoka Afrika, hivyo kuwa pia mwakilishi pekee wa Afrika katika Kamati Kuu ya IYDU.
Alisema kwenye taarifa hiyo kuwa mgombea wa nafasi hiyo anapendekezwa na chama chake na kuungwa mkono na nchi nyingine zaidi ya mbili.
Uteuzi wa jina la Mnyika kugombea nafasi hiyo uliungwa mkono na vyama vya kidemokasia Afrika pamoja na nchi kadhaa za Ulaya hususan Norway na Finland, alisema Tumbo.
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Bunge la Norway anayetoka Chama cha Hoyre, Peter Gitmark, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa IYDU.
Akizungumza baada ya kurejea nchini, akitoka kwenye uchaguzi huo, Mnyika alisema uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkubwa.
Alisema vigezo vilivyomfanya achaguliwe ni baada ya kuzunguzia suala la ongezeko la joto, UKIMWI na kukua kwa demokrasia ya vyama vingi.
Mkutano huo wa baraza la IYDU ulianza Novemba 29 na kumalizika Desemba 2006, na ulihudhuriwa na wajumbe 250, wengi wakiwa ni viongozi wa vijana na wabunge vijana kutoka nchi mbalimbali.
CHADEMA inaendelea kupata nafasi za juu kwenye umoja huo baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA).
Mbunge wa chama hicho, Zitto Kabwe wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, katikati ya mwaka huu, aliteuliwa na Rais wa Ujerumani Horst Kohler kuwa miongoni mwa timu ya vijana wanaomshauri rais huyo kuhusu masuala ya siasa, uchumi na ushirikiano wa kimataifa.
SOURCE: Tanzania Daima 28 Desemba 2006