[h=1]Majangaaa Mbona Majangaaa! - 19-[/h]
ILIPOISHIA
Kwani ni lazima uingie? Eddy alihoji huku akimshangaa msichana huyo ambaye walishakubaliana uhusiano wao waufanye kuwa siri.
Hata hivyo, Eddy alikuwa anakijua kile ambacho Rehema angekutana nacho chumbani kwake, akamwachia ili aingie.
Alipoachiwa bila ya aibu, akazama chumbani huku shari ikiwa imemjaa, kwa kukidhamiria vibaya kile ambacho angekutana nacho chumbani humo.
POROMOKA NAYO
!
Moja kwa moja macho yake yakatua kitandani, akakikuta kitanda kikiwa cheupe, hakukuwa na mtu zaidi ya shuka zilizovurugika.
Watu waliokuwa ukumbini wakazidi kuchanganyikiwa na kujiuliza maswali kibao yaliyokosa majibu, kwani Rehema alikuwa amekumbwa na kitu gani mpaka avamie chumbani kwa watu.
Wengi walihisi kulikuwa na kitu kinachoendelea kati ya wawili hao, walimuonea huruma kaka wa watu ambaye ni mgeni ndani ya nyumba hiyo kwa kitendo cha kufanyiwa vurugu na msichana huyo.
Ni mtu mmoja tu aliyekuwepo katika ukumbi huo ambaye alikuwa akijua ni nini kilichokuwa kikiendelea.
Mtu huyo si mwingine bali ni mdogo wake na Queen, Pat ndiye aliyekuwa akiujua mchezo mzima.
Pat alikuwa akijua ni kwa nini Rehema alikuwa ameingia chumbani kwa Eddy, pia, alikuwa akijua kile ambacho msichana huyo angekutana nacho chumbani humo.
Kwa kuona hivyo, mama mwenye nyumba naye akapunguza mashambulizi yake kwa Rehema, hali kadhalika baba mwenye nyumba, wote wakabaki na mshangao na kujiuliza kulikoni!
Rehema hakuridhika na kile alichokutana nacho chumbani, akaangaza kila kona, akafungua kabati, akahamia uvunguni mwa kitanda, kote hakuambulia kitu.
Akabaki ameshangaa, hata hivyo hakutaka kuyaamini macho yake, akaendelea kufunua hata ndoo za maji, akili yake ilikuwa imempaa na aibu ilikuwa ikiutafuna uso wake.
Alitegemea angefumania, lakini sasa kibao kilikuwa kimemgeukia, hakujua cha kusema mbele ya kadamnasi akiamini kuwa amechezewa shere, uso wake ukawa mdogo kama kidonge cha piltoni.
***
Upande wa pili, Queen alifungua mlango wake na kutoka nje, akakutana na vicheko, watu wote walikuwa wakimcheka Rehema ambaye alikuwa kama mtu aliyekuwa amechanganyikiwa.
Rehema alishindwa hata kumuomba radhi Eddy, alikuwa amenyongonyea kama vile kunguru aliyekuwa amemwagiwa maji.
Shoga umelikoroga
utalinywa! alisema Mwamvita kisha akawahamasisha watu kwa kikolombwezo maarufu ambacho kimezoewa na wanawake wengi, akasema:
Halooo halooo
!
Halooo! wengine wakaitikia na kumfanya Rehema kuzidi kuchanganyikiwa na kujikongoja kwenda chumbani kwake akijihisi kama vile amejichafua kwa haja kubwa.
Kabla ya kuingia chumbani kwake, Queen akambetulia macho na kujishebedua mbele yake
kisha akamshusha na kumpandisha kiuchokozi kama vile kuku aliyekuwa akiangalia ndege ipitayo angani:
Shoga kimekusibu kipi? alimuuliza na kumfanya Rehema ashindwe kujibu.
Mbona miye sielewi? alihoji mama mwenye nyumba na kutaka kujua kwa nini Rehema alikuwa akifanya vituko siku ile.
Hata siye hatuelewi
msichana aitwaye Tabu naye alijibu kwa niaba ya wenzake. Kila mtu ndani ya nyumba hiyo akawa anataka kujua ni nini kilikuwa kimetokea siku hiyo hadi malkia wa nyumba hiyo akaikwaa aibu.
Queen aliachia kicheko baada ya kupitwa na Rehema, kisha akasema:
Mlaji ni mla leo mla jana kala nini? alisema na kumfanya Rehema kujua kuwa hicho kilikuwa kijembe chake. Akaamini kuwa Queen ndiye aliyekuwa chumbani kwa Eddy.
Ametokaje, akajiuliza na kukosa jibu.
Ukweli ni kwamba Queen alitoka chumbani humo wakati Rehema akiwa amelala amepitiwa na usingizi ukumbini, alipomuona alishangaa sana.
Queen alijua kuwa Rehema alihisi kuwa chumbani kwa Eddy kulikuwa na msichana hivyo akaamua kukaa ukumbini ili amshuhudie msichana huyo wakati akitoka.
Pia alijua kuwa mpaka wakati huo Rehema hakuwa akijua ni msichana gani aliyekuwa chumbani kwa mvulana huyo kwa kuwa wakati akitoka hakumuona.
Atakufa nacho kijiba cha roho, alisema Queen na kuahidi kuendeleza penzi lake na Eddy.
***
Moja kwa moja Rehema aliingia chumbani kwake na kujitupa kitandani, akaanza kulia kilio cha kwikwi, akajuta kumfahamu Eddy.
Yaani mwanaume nimempa raha zote lakini anakuja kunifanyia hivi, kweli wanaume hawaaminiki, aliwaza na kufikiria cha kufanya.
Bado katika nafsi yake alikuwa akitaka kujua nini kilichomfanya Eddy akamsaliti usiku mmoja tu baada ya kukutana naye.
Alikuwa chumbani kwake akifikiria hatua ya kufanya.
Hakutaka kumpoteza Eddy lakini bado alitaka kujua ni msichana gani aliyekuwa chumbani kwa mvulana huyo.
Mawazo yake yakaangukia kwa Queen, akahisi kwamba anahusika kwa njia moja ama nyingine.
Nini kiliendelea?