Kwanza niseme kuwa walimu wameghafilika kidogo na kupitiliza hivyo wanapaswa kujaribu kupunguza hasira. Ila pia inashangaza kuona watu humu wanaonekana kuwa na uchungu sana na wengine kutoa lugha za kejeli na kibabe kwa walimu. Hivi kwa ninyi mnaosema angakuwa mwanao huyo ungeishia jela kwa kufanya kitu kibaya, unadhani wewe utakuwa sahihi kufanya kitu kibaya kwa walimu lakini wao hawakuwa sahihi kufanya kitu kibaya kwa mwanafunzi aliyewaudhi? Na kama ndivyo tofauti yako wewe na wao ni ipi?
Pili, shuleni kuna changamoto nyingi sana kwa walimu. Kuna wanafunzi anakosea, unataka kumuadhibu anagoma, unampeleka ofisi bado anagoma, anashika fimbo anaivunja, ukimshika shati vizuri ili umuadhibu anakukwida shingoni, nauliza kwenye mazingira hayo unafanyaje?
Tatu, wale wanaofikiri ni rahisi kufukuza mwanafunzi shule wanakosea sana. Ni kazi ngumu mno kumfukuza mwanafunzi shule haswa kwa shule za serikali. Wanafunzi wengine kwakutambua hilo wanaweza amua kumuabisha tu mwalimu vile watakavo. Isitoshe kufukuza shule sio njia bora ya kumrekebisha tabia mwanafunzi. Shule watu haweindi tu kujifunza mambo ya darasani bali ni pamoja na kujifunza na kufundishwa tabia nzuri. Hivyo tusikimbilie kusema kazi ya mwalimu ni kufundisha tu maana huwezi mfundisha mtu amabaye hana nidhamu. Sote tunatambua kuwa elimu na nidhamu zinaendana. Shule zikijikita kwenye kufukuza fukuza tu ni kina nani watabaki huko? Kuna watu leo wamekuwa na maisha mazuri na mchango mkubwa kwa taaifa lakini wakati wanasoma walikuwa wakorofi sana kiasi kwamba wangepaswa kufukuzwa shule. Hata hivyo busara za walimu kwa kuamini katika kuwadhibu ndizo zilizosaidia mpaka leo hii wamefika walikofika, na pengine wengine wamo humu. Je wangefukuzwa shule wangekuwa wapi leo? Kwahiyo huwezi kuwa kila kosa au kila mwanafunzi anapogomea adhabu au vinginevyo wewe unafukuza shule, hakuna utaratibu wa dizaini hiyo.
Nne, wazazi wengi wameshindwa kutimiza majukumu ya kulea wanao. Kazi yote ya malezi ametupiwa mwalimu, unategemea nini. Mwanafunzi mkorofi kiasi cha kupigwa na walimu kadhaa hata nyumbani lazima anashida. Wanafunzi wanafanya makosa, mzazi anaitwa afike shuleni lakini anatoa jibu jepesi kabisa "Huyo mtoto mimi ameshanishinda, ninyi amueni tu mtakavoamua" kwenye hali kama hiyo unadhani tabia ya mtoto itakuwaje. Tukiwa huku kwenye mitandao tunataka tuonekane wazazi tunaojali lakini ukweli ni kuwa wazazi wengi siku hizi wamekuwa kero kwa walimu na malezi kwao sio ishu tena. Kila mmoja hapa ajiulize anashiriki vipi kuhakikisha mwanae anapata maadili mazuri akiwa shuleni na nyumbani? Ni mara ngapi unasikia mzazi akilalamika kumshindwa mtoto ambaye pengine hata msingi hajamaliza na wengine wakiwa kidato cha kwanza au cha pili? Ni kweli inauma lakini tujiulize kwanza juu ya uwajibikaji wetu kabla ya kuwahukumu wengine.
Tano; kuhusu kufuta taratibu za kuadhibu hilo ni jambo gumu kuliko uhalisia wake. Hakuna namna kila kosa likifanyika walimu wajipange kwa mkuu wa shule kuelezea kosa, wasubiri kibali cha kuadhibu viboko vitatu kwa mwanafunzi tena wamuandike kwenye daftari. Utaratibu huu ni mgumu sana na kwa wanafunzi wameaka hii tutazalisha vijana watukutu na masifuri mengi mno. Hivyo tujaribu kuangalia na uhalisia.
Mwisho, ni kweli kuwa kitendo kile kimevuka sifa za adhabu(characteristics of punishment) na hakipaswi kuungwa mkono. Kama binadamu walimu ni vizuri kujaribu kuhimili hasira na kutokuadhiba pale ambapo mtu amekasirika. Ni watie moyo kwa kazi ngumu na nzuri mnayoifanya sio tu ya kutoa maarifa bali pia ya kulea vijana. Tukumbuke kuwa jamii hii hii inayolalamika na kutaka sheria za adhabu kufutwa ndiyo hiyo hiyo itakayo lalamika kuwa malezi yamewashinda na ndio maana mtaani wanafunzi wamekuwa wakorofi. Narudia siungi mkono adhabu kupitiliza lakini natambua namna ambavyo vijana wa leo wamekuwa wakiwapa changamoto kubwa sana walimu.