SoC02 Mazingira upataji elimu kwa Wanafunzi wa Kike shuleni yaboreshwe

Stories of Change - 2022 Competition
Jul 29, 2022
16
15

Mazingira ya upataji elimu kwa Wanafunzi wa Kike shuleni yaboreshwe​


Na wenu, Mtambo 1272019

Kwa miaka mingi, tumeshuhudia mtoto wa kike akiachwa nyuma katika suala la upataji wa elimu bora , jambo hili limechochea watoto wa kike kuwia ugumu kupata elimu bora bila vikwazo vingi. Pindi umuonapo mabinti (sio wote,bali wengi wao) wamefika chuo kikuu na kuendelea, elewa wamepitia mambo mengi ya kuwarudisha nyuma, lakini wakafanikiwa kwa mbinde. Kusema hivi simaanishi kuwa watoto wa kiume haujapitia au hatupitii mazingira magumu ya kupata elimu ,lakini ninachotaka kieleweke hapa ni kuwa kuna utofauti mkubwa cha changamoto nyingi au vikwazo kwa upataji wa elimu bora kwa mtoto wa kike.

Ingawaje kumekuwa na jitihada mbalimbali zimeendelea kufanywa na serikali na jamii kiujumla kumuwezesha mtoto wa kike kupata elimu bora na kusudiwa(kama ujengaji wa mabweni kwa baadhi ya shule,ugawaji wa taulo za kike kwa baadhi ya shule na utungwaji wa sheria kali kwa wakatishaji wa elimu kwa binti., lakini bado kuna changamoto nyimgi zipo;changamoto zinazokwamisha jitihada/juhudi husika. Changamoto hizo zimechagizwa na upuuzaji wa kuandaa na kuboresha mazingira bora kwa upatikanaji wa elimu kwa mtoto wa kike.. .

MIUNDO MBINU WEZESHI KWA ELIMU YA MTOTO WA KIKE IBORESHWE MASHULENI .

Ipo miundombinu mbalimbali ambayo ikiimarishwa na kuboreshwa mashuleni,ianaweza chochea kwa namna moja au nyingine katika maendeleo ya elimu ya mtoto wa kike nchini Tanzania na afrika kiujumla. Wacha tuyaangazie kwa pamoja hapa chini;

Vijengwe vyumba vya kubadilishia Nguo mashuleni . shule nyingi( mjini na vijini,za serikali na binafsi) zimekosa vyumba maalum kwaajili ya kumuwezesha motto wa kike kubadilishia nguo zake pale anapokuwa yupo mwezini. Hali hii imechochea wanafunzi wengi wa kike kukosa uhuru wawapo mashuleni kila waingiapo kwenye siku zao , na imepelekea wengine kushindwa kuhudhuria masomo mpaka pale damu zitakapo kata. Hivyo basi, kuna ulazima kwa serikali na taasisi binafsi kulitazama hili, na kuona haja ya kujenga vyumba maalum kwa mtoto wa kike;vyumba atakavyotumia mahsusi kwa kubadilishia nguo tu.

Vilevile, kuna haja ya kuhakikisha upatikaji wa maji safi na salama muda wote mashuleni. Shule nyingi hazina maji safi na salama,maji ambayo motto wa kike anaweza kuyatumia kujisafishia mwili wake(mahsusi, ukeni mwake). Baadhi ya shuleni hazina hata bomba za maji , hivyo wanafunzi hulazimika kwenda mtoni, kuteka maji kwaajili ya kujisafishia, na shughuli zinginezo za pale shuleni. Kuna haja kwa serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu, kuhakikisha kwa shule zote (mjini,vijini ) zinakuwa na mabomba ya maji, visima visivyo kauka na matenki ya kuhifadhia maji ,ili kumuwezesha motto wa kike kuwa na uhakika wa kujisafisha kila aingiapo kwenye siku zake na siku za kawaida. Naamini hili linawezekana kwa sababu sehemu nyingi za Tanzania zina vyanzo vingi vya maji.

Pia,Walezi wa wanafunzi(matrons)na walimu wa afya mashuleni, wapewe elimu na mafunzo toshelevu juu ya afya za wanafunzi(kike) husika. Walimu wengi wa afya na walezi mashuleni wamekuwa hawana elimu ya kutosha juu afya za watoto wakike, wakali,wasio na faragha na muda mwingine kuwa na lugha chafu kwa wanafunzi. Hali hii imechochea wanafunzi wengi wa kike kusita(kuogopa),kuona aibu na kukosa kujiamini kueleza shida zao za kiafya ikiwemo suala hedhi. Hivyo kuna haja.ya kuhakikisha kuwa walimu wanaoteuuliwa kusimamia na kuwa walezi wa afya ya watoto kike, lazima wawe na utu,kujali na huruma kwa wanafunzi. Lakini pia ,mafunzo ,semina na warsha mbalimbali zitolewe kwa walimu husika ili kuhakikisha kuwa ,mwalimu(mlezi) anayepatiwa majukumu husika,anakuwa na uwezo,maarifa na ujuzi wa kutosha juu ya afya ya mtoto wa kike .

Kampeni za ugawaji wa taulo za kike “pedi” mashuleni zipewe nguvu na kuwa sera kamili ya taifa. Kampeni za sasa zimekuwa zikifanyika sana maeneo ya mijini tu ,huku maeneo ya vijini yakiachwa nyuma. Watu kama flaviana matata,jokate mwegelo n.k wamekuwa kielelezo bora katika hili.Hili linafanyika kwa kuzingatia tafiti mbalimbali zilizofanywa na mashirika binafsi na shirika la afya la dunia (W.H.O),tafiti zinazo onesha kuwa kila mwezi, watoto wa kike wengi hukosa masomo kwa takribani siku 4-5 kwa sababu ya hedhi(kuwa mwezini).

Lakini vile vile , kampeni za ugawaji wa taulo za kike hazijapewa kipaumbele na serikali nyingi za kiafrika, mahsusi Tanzania,hata zile serikali,wizara za afya na elimu zinazoongozwa na wanawake,lakini bado suala hili limeachwa nyuma,na kuachiwa wana harakati,asasi za kiraia na mtu moja mmoja, ilhali imeonekana ukosefu wa “pedi” kwa wanafunzi wa kike mashuleni ni kikwazo kwa elimu ya mtoto wa kike.Hivyo, ningetoa ushauri kwa serikali na wizara zake husika kwa kuhakikisha ugawaji wa taulo za kike mashuleni, unakuwa ni mchakato endelevu kwa wasichana wote mashuleni. Pia, serikali ishiriki moja kwa moja katika kutengeneza sera rasmi za kuwezesha taulo za kike zikigawiwa bure nchi zima, ili kumuwezesha motto wa kike kupata elimu kusudiwa. Ikumbukwe kuwa taulo za kike zina uwezo wa kudumu au kutumika zaidi ya miezi sita, hivyo ni bora zaidi kiuchumi na kiafya pia.

RAI YANGU
Ningependa kumalizia, kutoa ushauri kwa wadau wa elimu,afya,wanaharakati na serikali kiujumla,kuhakikisha kuwa eimu juu ya afya(hedhi na balehe) zikitolewa kwa wanafunzi wote kwa uwazi, ili kuhakikisha kuwa kuna kuwa na uwelewa mpana juu ya mabadiliko yanayotokea kwa mwili na akili wa mtoto wa kike na kiume. Hii kwasababu , bado tafiti zinaonesha kuwa bado kuna uelewa duni miongoni mwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari juu ya mabadiliko ya kimwili na akili wanayokumbana nayo mapema baada ya balehe. Hivyo ili kuhakikisha miundombinu wezeshi inafanikiwa kwa elimu ya mtoto wa kike, lazima kuhakikisha elimu ya afya(balehe na hedhi ) inatolewa kwa uwazi kwa wanafunzi wote(kike na kiume)

“UKIMUELIMISHA MWANAMKE(MSICHANA),UMEELIMISHA JAMII NZIMA”
 
Back
Top Bottom