inaendelea....
Uongozi; Serikali, Utawala, Dola
Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) zimebahatika kuwa na awamu si chini ya nne za uongozi wa Serikali kuu, ingawa kwenye Bunge na Mahakama, watumishi wake wameendela kuwa ni wale wale kwa muda mrefu.
Tatizo kubwa tulilonalo kama Taifa ni ufinyu wa viongozi bora na utashi binafsi wa wachache walio katika nyanja za uongozi kwa kukosa sifa muhimu kwa viongozi. Mzee Mwinyi amesema majuzi kuwa Tanzania ina viongozi wasomi wasioelimika. Kauli hii ni ya kweli na ni ya msingi kutambua kuwa uongozi si lelemama, ni kipaji na ni kazi ngumu.
Uongozi ni kujitolea na kuweka matwakwa na maslahi ya wengine kuwa mstari wa mbele na si matakwa binafsi na kujinufaisha. Marehemu John Kennedy rais wa Marekani alitoa kauli moja maarufu iliyosema kuwa "kiongozi ajiulize ni vipi atalitumikia Taifa na si Taifa kumtumikia yeye Kiongozi" Umashuhuri na uzuri wa Kiongozi unatokana na hekima, busara, uchapakazi, ufanisi, ufuatiliaji, uimara, uungwana, uwajibikaji na unyenyekevu wake. Ama fikra endelevu na upeo wa kuongoza ni muhimu na si kauli tamu au uzuri wa sura.
Uwezo wa Tanzania kuwa na maendeleo ya kweli utaanza na Uongozi bora.
Uongozi bora ni ule;
· wenye mapenzi ya kweli na dhati na kujivunia Utaifa wake
· wenye kujali na kulinda maslahi ya Taifa lake na watu wake
· wenye uwezo wa kupanda mbegu imara ya Uzalendo kwa kila mwananchi bila kujali itikadi, rangi, kabila, dini, elimu, umri au jinsia
· wenye uwezo wa kuhamasisha na kuchochea juhudi za maendeleo ya jamii, umma na Taifa
· wenye nidhamu, watiifu, kuwajibika, tija, ufanisi, kujituma na ufuatiliaji wa hali ya juu
· wenye usikivu, uungwana na unyenyekevu kukiri makosa, kukubali kukosolewa na kupokea na kufanyia kazi maoni ya wengine
· wenye uwezo wa kufanya kazi, kufikiri, kuwa na upeo na wepesi wa kukabili na kufanya maamuzi magumu
· usiolea uzembe, ubaguzi, unyanyasaji, uhujumu, ubadhirifu, rushwa, kudharau, kudhalilisha, kujuana au kulinda maslahi ya wachache au kikundi Fulani
Wajibu wetu kama Taifa na haki yetu kama wapiga kura kuchagua viongozi kutuongoza unabidi uachane na mfumo duni tulioujenga wa kuangalia sura na chama na tuangalie wagombea wetu wa uongozi kwa vigezo hivyohapo juu ili kuunda tabaka jipya la viongozi ambao ni wachapakazi na watakuwa manahodha wazuri kutuongoza katika safari yetu ya kulijenga Taifa.
Tukilegalega katika hili na kupuuzia wajibu juu mkubwa na kuendelea kuchagua viongozi na wawakilishi wabovu, tutakuwa hatuna sababu yeyote kulia na kulalamika kuwa tu masikini au wanyonge kwa kuwa ni Ujinga na Upumbavu wetu kutumia akili na busara zetu tulizopewa Mungu tumekimbilia kurudia makosa ya kuwapa dhamana ya uongozi watu ambao hawafai kutuongoza.
Tuchague viongozi si kwa kuangalia vyama au sura, bali tuangalie uwezo wao wa kuongoza, kuhamasisha na kufanya kazi. Tupime kauli zao na matokeo ya kazi zao kama wanavyojinadi.
Serikali ni watu, inaundwa na watu tuliowachagua na tunawapa watu hawa na Serikali mamlaka makubwa ya kutuongoza, kupanga na kulinda Taifa na Katiba yetu. Dhamana hii imefanywa kwa kuaminiana kuwa Serikali itafanya kazi kwa manufaa ya Wananchi wake na kwa matakwa na utashi wa Wananchi wake.
Inapotokea kuwa Serikali inafanya kazi tofauti na dhamana iliyopewa, ni wajibu na haki ya kila Mwananchi kudai na kuhoji mapungufu yanayoonekana au kuzungumzwa. Ni wajibu wa Serikali na Uongozi kujibu na kuwajibika kwa Wananchi waliowapa dhamana ya kuongoza Taifa.
Ikiwa Serikali na watendaji wake na Viongozi wanashindwa kufanya kazi zao kama wanavyotegemewa kuzifanya na kushindwa kutimiza matarajio ya Wananchi na Taifa, ni wazi kuna umuhimu wa kupima uwezo wa viongozi na kuhoji Uzalendo wao na kama bado wanastahili kulitumikia Taifa.
Kuanzia Rais, Mawaziri, Majaji, Mahakimu, Wabunge, Wakuu wa Taasisi na Mashirika, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Polisi, Magereza,Jeshi na watendaji wengine wa Serikali, tumaini la Watanzania na Taifa ni kuwa watu hawa wamepewa nafasi hizo kwa kuwa wanauwezo wa kitaaluma na kiutendaji kuwa viongozi na walinzi wa nguzo za Taifa letu kupitia Katiba na Sheria zake.
Hivyo basi pamoja na kuwa ni jukumu la sisi kama Raia na Taifa kudai uwajibikaji, lakini uzito wa kuhakikisha ufanisi wa Uongozi na uwajibikaji wake utaanzia na Mkuu wa Nchi ambaye ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu.
Wasifu wa Uongozi bora nilioutaja hapo juu, si wa Rais pekee, ni wa kila mtu aliye kiongozi na ni shurti kila Mtanzania aishi kwa kuviangalia na kuvitumikia vipengele hivyo bila kujali yeye ni Kiongozi au la.
Serikali yetu ni kubwa sana na ina watendaji wengi ambao sitaficha kusema kuwa asilimia 55% hawastahili kuwa viongozi kutokana na kushindwa kuwa na sifa nilizozitaja hapo juu.
Hii ni hatari sana kwa Maendeleo na Usalama wa Taifa letu. Hatuwezi kuendelea kujiongoza kiholela huku zaidi ya nusu ya viongozi wetu hawana Uzalendo au uchungu na nchi yao. Swali kwako Mtanzania ni kwa nini basi ukubali kuendelea kujichagulia viongozi wabovu wasiofaa na kuwapa dhamana kubwa sawa na kumpa Simba jukumu la kulinda Mbuzi wako?
Kinachokosekana kutoka Uongozi Mkuu hasa Urais na hata Mawaziri ni uwezo wa kudai kwa nguvu uwajibikaji na uadilifu. Hadithi na tuhuma za ufisadi zilizotawala Taifa letu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 ni kutokana na kuwa na Uongozi dhaifu, usiojali maslahi ya Taifa, uongozi uliojaa woga na kulindana na kushindwa kusimama kidete kulinda rasilimali za Taifa letu.
Viongozi wakuu wa jamii kuanzia wakuu wa vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa hata Taifa, wameendelea kufanya kazi bila kupimwa na waajiri wao wawe Wananchi au Serikali kuu kuhusiana na ufanisi na uwezo wao katika safari ya kulijenga Taifa na kuleta maendeleo.
Mapendekezo yangu ambayo yataanzia na wewe Mtanzania ni kuwapima viongozi wako kwa kutumia vipimo vyepesi sana. Vipimo hivi ni kama ifuatavyo;
· kupitia ripoti za kila mwezi, robo, nusu na mwaka mzima za maendeleo na kupima mafanikio na matatizo ya shughuli za maendeleo
· kuhoji na kuhakiki viwango vya kuongezeka vita dhidi ya ujinga katika wilaya au mikoa kupitia shule za msingi, sekondari, vyuo na elimu ya watu wazima
· kuhoji maendeleo ya afya kupiga vita maradhi, kuangalia takwimu za kupungua vifo vya Uzazi, vifo vya watoto, kupungua kwa uadimu wa lishe na magunjwa kama Kwashiakor, Utapiamlo, kupungua kwa magonjwa na vifo vya Malaria na Ukimwi
· ongezeko la nyumba bora, maji safi, barabara nzuri, shule, hospitali na zahanati, vyanzo vya ajira, viwanda na shughuli za kilimo
· hifadhi za chakula kukabiliana na njaa, mauzo ya mazao ya biashara na chakula
· matumizi bora ya fedha za bajeti ikiwa pamoja na kubana matumizi yasiyo ya muhimu, kudhibiti matumizi na mahesabu ya fedha za bajeti za matumizi na maendeleo
· kukagua na kuhakiki shughuli za maendeleo kuwa ni endelevu na kuhakikisha hazizoroti
Kwa kifupi ni kuhoji na kutathmini, ni shule ngapi tulizonazo, ni ngapi zimeongezeka, ni wanafunzi wangapi wamehitimu shule, ni hospitali ngapi tulizonazo zina uwezo gani, msisitizo wa kinga ni mkubwa kiasi gani kulingana na tiba, kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji mali na hifadhi za mazao, kubana matumizi na matumizi mazuri ya fedha.
Nimeweka wajibu huu kwako wewe mwananchi kwanza na si ile kasumba ya kusubiri Kiongozi Mkuu-Rais au Waziri Mkuu ndio wawe wenye jukumu na uhalali wa kuhoji haya.
Vipimo hivi haviishii kwa Mbunge, Mkuu wa Wilaya au Mkoa ni mpaka kwenye Serikali kuu na hata vigezo hivi vinaweza tumika katika mashirika na taasisi za umma na zile binafsi.
Kama vigezo hivi vya uongozi bora na kupima uwajibikaji vingekuwa vikifuatwa kwa makini, tungeweza kuona uwiano wa maendeleo wa Taifa letu. Lakini ni mpaka pale tutakaboshinikiza na kudai kwa nguvu Utawala na uongozi bora, ndipo tutakapoona mafanikio na hivyo kuanza kupata tumaini la maendeleo ya Taifa zima.
Uongozi na Utawala bora huendana sambamba na dola. Katika Utawala bora, Serikali na Viongozi ni wabunifu wa mipango mizuri ya maendeleo, ni wapimaji wa kasi ya maendeleo na hufuata kanuni na sheria katika kufanya kazi zao.
Panapokuwa na Uongozi na Utawala mzuri, kero za wananchi hupungua na hata matumizi ya dola na vyombo vyake huheshimika na huwa ni kwa ajili ya manufaa ya Taifa.
Hali halisi ya Tanzania imejenga mfumo wa utawala unaolinda utashi na maslahi ya chama tawala au kikundi chenye nguvu za madaraka nja mali. Hali hii imefikia hatua ya kikundi hiki cha watawala kutumia nguvu za dola kutawala kwa mabavu, kukiuka sheria na kanuni alimradi wanatumia kinga ya uongozi.
Utawala wa namna hii si mzuri na hauna manufaa hata kidogo kwa nchi yetu au Taifa lolote. Tunapaswa kukemea na kuondokana na mfumo huu mbovu wa Utawala ambao unatumia dola na kuweka wajibu wa kwanza wa Uongozi ni kulinda matakwa ya Chama au kikundi maalum.
Aidha matumizi mabovu ya dola na vyombo vyake, Bunge, Mahakama, Polisi, Jeshi na Usalama wa Taifa yamesababisha kwa kiwango kikubwa kuzorota kwa Uongozi, kuweko kwa utawala mbovu ambao umeishia kuangamiza uchumi na juhudi za maendeleo ya Taifa.
Wajibu wa vyombo kama Bunge na Mahakama ni kuwa mihimili mingine ya Serikali. Bunge likitunga Sheria, Mahakama ikitoa tafsiri za sheria na Serikali kuu kufanyia kazi sheria. Badala ya vyombo hivi kuwa huru na hata kuhakiksha vyombo visaidizi kama Polisi, Jeshi, Mahakama, Magereza, Usalama wa Taifa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu vinabakia kuwa vyombu huru ndani ya mfumo wa kisiasa, vyombo hivi vimegeuzwa na kutumika kama silaha ya kulinda chama kinachotawala kwa kutoa vitisho kwa wananchi na vyama visivyo na madaraka.
Suluhisho la haya yote ni kuundwa kwa Katiba mpya na Sheria mpya ambazo zitalenga;
· kutoa haki sawa kwa kila mwananchi bila upendeleo
· kutofungamana na chama au kikundi cha siasa au watawala,
· kuwajibisha Watanzania wote bila kujali nafasi zao katika jamii na Taifa,
· kulinda maslahi, haki , uhuru na mali za Watanzania wote bila kujali itikadi, dini, elimu, jinsia, umri au kabila
· kutoa tafsiri na maelezo ya kisheria na kanuni ambayo hayana utata au kukosa nguvu kufanyiwa kazi na kufuatiliwa
· kumpa kila Mtanzania fursa na haki sawa katika kuchangia kwake ujenzi wa Taifa na hata kuongoza bila kuwa na vipingamizi vya kibaguzi ambavyo vimewekwa maksudi katika katiba ya sasa na Sheria kuzuia ushindani au kuwepo kwa uhuru kamili wa kujieleza na kufanya mambo ya siasa na uongozi
· kujenga miiko mikali na maadili kwa viongozi, utawala na wanachi kwa ujumla
· kuweka mfumo bora wa uteuzi au uchaguzi wa viongozi na wawakilishi
Penye nia pana njia, kama wote tutakaa mstari mmoja na kukubaliana kwa pamoja kuwa haya ndiyo tunayoyataka kutoka kwa viongozi wetu, mfumo wetu wa utawala na dola, nafasi ya kupata viongozi wazuri, kuwa na mipango mizuri itafanikiwa na hivyo kuruhusu wananchi na viongozi kuwajibika kwa dhati na kujituma ili kuhakikisha kuwa shughuli za Ujenzi wa Taifa kiuchumi unafanikiwa kukiwa na Amani, Mshikamano, Sheria na Uongozi Bora.
mwisho....